Friday, July 8, 2011

Rais ajaye Tanzania anafaa mseja,yatima, ama mjane!





NILIMPIGIA kura mgombea mmoja..
  Lakini, nimepata mashaka kidogo moyoni mwangu!
  Siyo kwamba, Kikwete ni Rais mbaya; la hasha.
 Si kwamba amefanya kazi mbaya. Nafurahishwa na vitu vingi anavyofanya Rais wetu; lakini ningependa Tanzania iongozwe na Rais mwenye sifa mbadala, ambaye hajawahi kuwepo.

   Ningependa sasa Tanzania iongozwe na Rais mwenye sifa za pekee ili kuondokana na majanga kama haya ya viongozi kuendesha Biashara zao(japo halali) wakiwa Ikulu.
 Naam, namtaka Rais ambaye ana sifa ambazo Kikwete hana!

   Nimeorodhesha hapa baadhi ya sifa ninazotaka Rais mpya baada ya Kikwete awe nazo: Rais asiwe na mke, yaani awe mseja; na awe hivyo kipindi chote cha kuwa  kwake Ikulu yetu ya Magogoni, Dar es salaam !

   Pili, Rais atakayekuja baada yam hula wa Kikwete kumalizika mwaka 2015, awe yatima.
 Rais asiyekuwa na ndugu na jamaa wenye madhambi yanayoigubika nchi kwa kashfa; tena kashfa zenyewe kubwa zinazopamba kurasa za mbele za magazeti.

   Naam. Rais asiye na mke anayepenyeza pua yake katika masuala ya uongozi wan chi, wakati hakuna aliyempigia kura kufanya hivyo!
Rais mwenye mke ambaye anafungua makampuni yanayoendesha biashara pengine bila kulipa kodi.
 Mke wa Rais(First Lady) ambaye atapewa leseni na kukopeshwa fedha na mabenki kwa kasi ili kufanya biashara kubwa kubwa, akijidai mjasiliamali.
    Lazima Tanzania yenye watu kama Milioni 38 iwe na Rais mwenye sifa za pekee, kuliko Benjamin William Mkapa, au Jakaya Kikwete.
 Mwenye hekima, mtu wa haki, mwenye akili, lakini hana familia, hana jamaa wa kumharibu akili awapo Ikulu pale.
   Nimewahi kusikia tetesi za wake za Marais wastaafu, jamaa zao na watoto wao kuitumia vibaya ikulu kufanya biashara.
Nakiri, sijawahi kusikia tetesi za Mjane wa Hayati Mwalimu, Mama Maria Nyerere kutumia Ikulu kufanya biashara.
    Tetesi kwamba Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa waliendesha kampuni yao , ANBEN wakiwa Ikulu, zinanivuruga akili.
Biashara hiyo ya Mkapa na Mama Anna, iwe halali au haramu, si hoja kwangu.
Lakini, napendekeza Tanzania isiwe na Marais wenye familia zinazowasukuma kufanya biashara mapema wakiwa Ikulu, ili kukimbia umasikini!
    Wapo marais waaminifu na ndugu zao na watoto wao ni waaminifu; hawaitumii vibaya Ikulu.
   Kadhalika, wapo wake wabaya wa marais  wenye wapambe, ndugu na jamaa wanaowashauri vibaya ili kujinufaisha na Ikulu.
Wake, jamaa, wapambe na ndugu hawa nao hujigeuza maofisa wa serikali.
   Nani aliyewachagua kufanya chochote? Nani aliwateua kuwa na sauti hadi kuwafokea mawaziri?
Kama ni hivyo, basi tungepewa nafasi ya kuwapigia kura hawa jamaa za marais kabla hawajaingia Ikulu.
   Au, kwa sababu ndugu yao anapoingia Ikulu, wao hujigeuza ‘Mabalozi’ ama ‘Wabunge’ Fulani, basi wangepelekwa kula kiapo mahakamani, kwamba hawataitumia Ikulu kwa maslahi binafsi kipindi chote cha Bwana, Bibi, Mjomba au Shemeji yao, anapokuwa Ikulu.
   Leo, tunashuhudia mbio kali za watoto wa vigogo kutaka kuwania madaraka. Sisemi kwamba watoto wa wakubwa hawana haki ya kuwania madaraka, la hasha! Wawe watoto wa wakubwa wenye Visheni; waachane na hadithi za kurithi damu za uchifu wenye falsafa ya kurithishana madaraka.
    Siasa si maneno matupu majukwaani.
Ni kuzifanya sera zizae maendeleo ya watu. Je, watoto wa vigogo wanaosaka madaraka kwa udi na uvumba, kupitia vyama Tawala, wanayo Visheni hii?
    Au,wanawania madaraka  ‘kutetea’ madhambi ya baba zao pindi wanapomaliza mhula wao, baada ya kushindwa kubadili Katiba ili kurefusha muda wa kusalia madarakani?
   Licha ya wake za marais kudaiwa kufanya biashara ama kufungua vikampuni visivyotozwa kodi wakiwa Ikulu, watoto wao wamekuwa wakiwasaidia baba  au mama zao kutawala kwa mabavu.
 Wamekuwa wakishiriki kuwatesa raia na kukiuka Haki za Binadamu.
    Rais wa zamani wa Liberia, Charles Ghankay Taylor ambaye juzi amesusia mashtaka ya Uhalifu wa kivita  huko The Hague, Uholanzi, mtoto wake, Charles Mc Arthur Emmanuel, au Charles Taylor Jr; ambaye Liberia alifahamika sana kama, Roy Belfast Jr, alitiwa mbaroni Desemba 15 mwaka 2005, akafunguliwa kesi mbili.
   Alitiwa mbaroni huko Miami , Marekani kwa kosa la kuwatesa kinyama waliompinga baba yake, na pia alikuwa na kesi ya kughushi Hati ya kusafiria.
   Ghankay Taylor, ambaye sasa anasusa mashitaka The Hague, alishirikiana na rafikiye, Foday Sankoh, wa kikundi cha RUF kufanya unyama Sierra Leone na kuwauzia waasi hao silaha kwa kubadilishana na almasi.
    Licha ya kuwepo kwa tetesi za wake za marais kuingilia mambo ya serikali, kuwafokea mawaziri na hata kuwatwanga makofi waandishi wa habari hapa Afrika, watoto wa Marais pia wanatuhumiwa kuhusika na kashfa nzito.
    Gideon Moi, mtoto wa Rais wa zamani wa Kenya , Mzee Moi, ana tuhuma za kuhusika katika kashfa anuai za ufisadi nchini humo.
Wengine, wakiwemo watoto wa wakubwa wa Dunia hii, wanatuhumiwa kubwia unga, kuuza ama kuvuta bangi na kuendesha biashara haramu hata katika Vyuo vikuu, lakini kwa sababu ya upendeleo, woga au kujikomba, vyombo vya Usalama hujikuta vikishindwa kuwachukulia hatua.
   Hata kama waliua, au hata kama walijeruhi ama kutaharukisha umma, huachiwa mara moja, wasiyaone magereza!
   Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Bi Margaret Thatcher(81), Mark Thatcher(54)a lituhumiwa kuendesha biashara haramu na kufanya uhaini.
   Sir Mark Thatcher, mwenye vituko vya “Front Page” katika magazeti, aliwahi kupotea katika Jangwa la Sahara .
Alipotea kwa siku kadhaa, wakati akishiriki Mashindano ya Paris-Dakar( Senegal ) Rally, akasababisha Bi Thatcher kuangua kilio hadharani, wakati akiwa Waziri Mkuu!
    Margaret Thatcher, alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza tangu mwaka 1979 hadi 1990.
 Lakini, mtoto wake huyo aliwahi kutiwa mbaroni na polisi wa Afrika Kusini kwa tuhuma za kuongoza njama za kupindua serikali ya Guinea ya Ikweta.
    Ametiwa mbaroni na vikosi vya usalama mahali pengi Afrika; hata Zimbabwe .
Polisi wa Afrika Kusini walisema, walikuwa na ushahidi wa kutumainiwa, kwamba Mark Thatcher aliwapa fedha waasi wa Guinea ya Ikweta, ili wampindue Brigedia Jenerali Mstaafu, Teodoro Nguema Mbosongo, Rais wa Baraza la Kijeshi la nchi hiyo, aliyedaiwa kuvunja Haki za Binadamu.
   Guinea ya Ikweta ni ya tatu Afrika kwa kuzalisha mafuta kwa wingi. Pengine, Mark anayetuhumiwa hata kuhusika katika biashara haramu ya silaha, alitaka mafuta ya nchi hiyo
. Naam, hao ndiyo watoto wa wakubwa.
   Hata hivyo, wapo watoto wa viongozi waliopata kuwa viongozi wazuri. Waziri Mkuu wa zamani wa India , Indira Ghandhi, alikuwa Binti wa Waziri Mkuu wa Kwanza wa India , Jawaharlal Nehru. Baadaye, Sanjay na Marehemu Rajiv Ghandi nao wakafuata nyayo.
    John Quincy Adams aliyekuwa Rais wa Marekani 1825-1829, alikuwa mtoto wa Rais John Adams aliyetawala Marekani mwaka 1791 hadi 1801. Adams alikuwa Rais wa pili baada ya George Washington.
    Yupo George W.Bush ambaye baba yake George Walker Herbert Bush, alikuwa rais miaka ya 90. Nduguze, kama Jeb Bush ni viongozi; ni wanasiasa maarufu. Hata hivyo, katika orodha, wapo wengi viongozi watoto wa viongozi kama akina Sir Mark Thatcher wahaini, wezi, wauza unga na wahujumu uchumi, wao na wapambe wao, lakini hawakamatwi wala kuhojiwa!
    Wako akina Roy Belfast Jr. wanaoghushi hati mbalimbali na  kufanya biashara haramu na halali, wanaotesa wapinzani wa serikali za baba zao, ambao pia hugeuza Ikulu kuwa ‘mapango’ ya wanyang’anyi ama ‘Mungiki’ wanao ifanyia jamii ugaidi mkubwa.
   Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kuwaonya watu kuiogopa Ikulu. Ikulu ni mahali Patakatifu. Si mahali pa kufanyia biashara hata ziwe halali na nyeupe kama sufi.
Rais anapoboronga, ama mkewe, jamaa au shemeji zake wanapoendesha magendo ikulu(Doing Business from Ikulu), ndipo harakati za kutafuta warithi huanza!
    Akina Umaru Yar’ Adua wa Nigeria walitafutwa na akina Obasanjo mara nyingi sana kupitia kitu ambacho si Uchaguzi, bali unyafuzi na Uchafuzi Mkuu wa Haki, Demokrasia na Uhuru Afrika!
    Ni kwa sababu hii, ningependekeza wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu, angetazamwa Mgombea ambaye jamaa, wapambe, rafiki, mke na watoto wake hawataiabisha ikulu kwa magendo, vituko, skandali na biashara zisizolipiwa kodi.
     Kama watoto, wake na wapambe wa Rais wangepelekwa Bungeni kwanza kuthibitishwa na kula viapo mahakamani, basi hofu kama ya Rais Jakaya Kikwete ya kumchunguza mtangulizi wake, isingekuwepo.
Hofu ya kutafuta kubadili katiba isingekuwepo, kama wake, watoto na jamaa wa Rais wangedhibitiwa na Bunge au Mahakama.
    Lakini, pamoja na haya yote, ili kuepuka Marais kufanya Biashara Ikulu, napendekeza Tanzania ingekuwa na Rais Mseja, lakini asiye mzinzi wa kukwapua wake za raia wake; asiyekaribisha machangudoa Ikulu na kuitia unajisi nchi, rais mjane asiye na familia ya kumtia majaribuni; na yatima ambaye baba, mama na watoto wake ni raia wake.
 Kwa nini mke wa rais awe tajiri kwa siku mbili?
 Kwa nini mtoto wa rais awe bilionea kwa miaka michache tu?
 Tunamtaka rais mseja,mjane,mgane na asiye na ndugu na jamaa!
   0755 324 074
   0754  324 074
congesdaima@yahoo.com

.

Monday, July 4, 2011

UMOJA WA AFRIKA UMEBINAFSISHA WAJIBU WAKE NATO?




   KULINGANA na Agano la kale, katika Bablia Takatifu, Amani ni baraka anazopewa mtu,baada ya kutii maagizo ya Mungu ama sheria zake(Kumukumbu la Torati sura nzima ya 28).
   Kwanza,tufahamu; Amani ni kitu gani?
Amani ni nini na hutoka wapi?
Chimbuko la Amani, ni wapi?
  Kwa Kigiriki, neno hili Amani ni ‘eirene’ maana yake, hali ya kumalizika kwa vita, ama hali ya kutokuwepo vita na uadui.
   Kwa Kiebrania, Amani ni ‘Shalom’ au hata waweza kuita Salem.Mji wa Yerusalem(Yeroo-shalayim) maana yake ni mji wa amani. Hata Dar es salaam, maana yake ni Bandari ya salama; ya amani.
   Amani, huanzia katika nafsi ya mtu mmoja mmoja, na inahusisha na uhusiano wa mtu na watu wanaomzunguka. Uhusiano huu ukiwa mzuri huiambukiza jamii na taifa zima, na hata mataifa mengine yote kwa pamoja hupata amani. Mtu mmoja anapokosa amani, matokeo yake ama athari zake huwapata hata wengine.
   Kukosekana amani Burundi, Congo(DRC),Somali,Libya ama Rwanda,kutayafanya mataifa mengi ya dunia kuathiriwa,ama na wakimbizi,kubanda kwa bei za mafuta,uchumi kuwa mgumu n.k
   Kwa sababu hiyo,kuna tafsiri(definition) nyingi za neno amani:
    Uzima,ukamilifu wa kimwili,kiroho,kiakili na ustawi na utangamano miongoni mwa jamii. Hii ni tafsiri ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa(WHO) ya mwaka 1947.
 Kulingana na Kumbukumbu la Torati,sura nzima ya 28,Amani ni kufanikiwa kimwili,kiroho,kiakili na kutokuwa dhaifu ama mhitaji katika neno lolote. Kwa Kiingereza,ukamilifu huu unaweza kuitwa “Completeness”, ama “Wholeness” au “Wholesomeness”.
    Kwa sababu hii, amani haiwezi kuwa hali ya kutokuwepo vita(absence of war) peke yake; ni pamoja na usalama wa chakula,uchumi mzuri, utangamano na uhusiano mzuri wa raia katika taifa lao na katika mataifa yote ya dunia,uchumi mzuri, mazingira yawe mazuri na rafiki,na kusiwepo na dhiki,shida na taabu kama mgawo wa siku hizi wa umeme.
   Amani ni mlango wa kuingilia katika mambo yote mema-fanaka. Hata watu wanaohitilafiana na matakwa ya Mungu:Usiue,usinyang’anye mke wa mwenzako, usiibe na usiwe fisadi,uwe mtiifu,mwadilifu na mzalendo kwa taifa lako na kwa wenzako n.k,hawana amani,na huwasababisha raia wenzao kukosa amani.
  Mungu, amejitaja kwamba yeye ni Upendo(Agape),Mtu asiye na upendo kwa jirani zake, ndiyo raia wenzake hata wanaomsema vibaya,hana amani moyoni mwake nakatika mazingira yake pia.
 Maishani, huwezi kuwa na furaha na usalama kama una njaa na maradhi-unakosa amani, utaona kwamba, dhana ya kutokuwepo vita(conflict) migawanyiko katika familia na hata mapigano, haiwezi kuwapo amani.
 Kusigana kwa mawazo, magomvi,maandamano,migomo ya wafanyakazi,uchumi mbaya,maisha magumu,njaa,kuvunjika kwa ndoa na watoto wa mitaani,ni dalili za wazi kwamba nchi ama dunia haina amani. Amani ni kinyume cha laana.MAMBO YOTE MABAYA kwa wanadamu.
 Mathayo 10:34 Yesu alisema kwamba, neno tu laweza kuleta vita,migawanyiko katika familia nahata mapigano ya silaha. Kusigana kwa mawazo,migomo na maandamano,kutokuelewana ama kukubaliana,huleta chanzo cha kukosekana amani.
  Mtu mmoja aliwahi kusema, “Amani huanzia kwako”.
   Mtazamo wako chanya(mzuri) kwa jirani zako,kwa taifa lako kwa raia wenzako, huleta amani. Mtazamo hasi(mbaya,masengenyo,chuki,uzushi,majungu,fitina n.k) huleta kinyume cha amani,yaani laana kwa taifa zima. Haya yote huanzisha vita vya silaha.
 Vita vya kugombea madaraka(strife for supremacy),kulipa visasi na ubeberu dhidi ya raia,huipeleka nchi pasipo na amani,yaani vitani. Vita ni chimbuko la maradhi,njaa, wakimbizi,umasikini,vifo,mambo yote mabaya hupingana na amani ya kweli.
 Amani ndiyo chimbuko la maendeleo ya watu,wanyama, wadudu ,ndege na viumbe wengine,na mazingira huwa bora sana.
 Chama cha Mapinduzi(CCM)husema Tanzania kuna utulivu(Tranquility) yaani kuna ukimya, ama kutokuwepo na makelele,fujo,magomvi n.k Utulivu siyo amani kamili. Na kutokuwepo na vita,hakuwezi kuitwa amani,ikiwa myoyo ya watu ina uchungu,majuto,masikitiko,dhiki,taabu na wana maradhi yasiyotibiwa,na hawana matumaini-hii siyo amani, japo kuwa wanagugumia kwa maumivu makali,bila kupigana-utulivu!
  Amani,ni hali ya kutokuwa na fikra hasi,ni uhuru kutoka hali ya vita,ni uhusiano mzuri katika jamii,miongoni mwa mataifa, uhusiano mwema baina ya mataifa ya dunia,na hali ya kutokuwepo kitisho cha vita,njaa,magombano na maradhi ya kufisha.Maendeleo huletwa na amani.
  Amani na afya njema ni hazina nahitaji la msingi kulinganisha na mahitaji yote.Watu huogopa sana vita na kukosekana usalama,lakini hata maradhi mabaya na afya mbaya,ni kukosekana kwa amani.
  Kisiasa, amani eti inaweza kuletwa kwa mtutu wa bunduki! Ndivyo tuonavyo siku hizi,Ufaransa na Marekani chini ya mwavuli wao NATO wanashiriki kuleta amani Libya kwa njia yam tutu wa bunduki, ili kumwondosha Kanali Muammar a- Gaddafi!
  Umoja wa Mataifa,kuna Baraza linaloitwa la Usalama(UN security Council) lenye kuundwa na mataifa 15.
   Mataifa matano:Uingereza, Ufaransa, Uchina, Urusi na Marekani ni wanachama wa kudumu wa Baraza hili lenye jukumu la kuleya amani duniani.
 Hata hivyo, nchi tano pekee hata ziwe na maguvu ya kijeshi kiasi gani aslani,haziwezi kuleta amani duniani. Hizi ndizo nchi zinazoongoza kuvuruga amani ya dunia.
 Ufaransa na Marekani,ndiyo wanaowapa WAASI wa Benghazi, Libya silaha ili kumpindua Kanali Muammar al-Gaddafi,eti kwa sababu utawala wake wa tangu mwaka 1969 umeondoa AMANI katika nchi hiyo, na hakuna demokrasia,haki za binadamu!
  Sijui,kwa Waingereza, Wafaransa na Wamarekani na washirika wao wa NATO, NENO AMANI TAFSIRI YAKE NI VISASI NA VITA DHIDI YA VITA?
 Pasipo shaka, kwa hawa mataifa babe duniani, amani maana yake ni vita, ni kugawa silaha kwa raia wa Libya ili wapigane wa kwa wao eti ili kumwondoa Gaddafi na kutatua matatizo yao!!
 Naam, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, huundwa pia na mataifa 10 yanayochaguliwa kila baada ya muda Fulani, na muda huo ukiisha,mataifa hayo 10 “ya kuja” huondoka kuyapisha mengine,tena na tena.
 Kwa sababu hiyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina wanachama wan chi 15;kati yao Urusi,Uingereza, China, Marekani na Ufaransa ni wanachama wa kudumu, wana maamuzi mazito-wanafanya kadiri wapendavyo,wanatumia silaha kuzishambulia nchi nyingine kijeshi,kwa madai kuwa hakuna amani,demokrasia na haki za binadamu huko.
 Je, vita vya silaha vinaweza kuleta amani kusiko na amani,uhuru na demokrasia?Hakuna majadiliano halafu vikwazo vya kiuchumi ama kizuizi cha kufanya biashara na kunyimwa misaada na mengine yanayopunguza vifo na uharibifu huletwao na vita vya silaha?
  Sheria za Umoja wa Mataifa(UN) zinataka,kabla mwanachama mmoja hajashambuliwa kijeshi,lazima kujadiliana naye,halafu asiposikia atengwe kisiasa na kiuchumi.
 Lakini, utaona Marekani na nchi za Ulaya, zilizowahi kutugeuza sisi watumwa wao, wanatoka kuishambulia nchi yoyote adui yao,bila kibali la Umoja wa Mataifa(UN).
  Kuna nchi 192 wanachama wa Umoja wa Mataifa. Kuna harakati za UN Kutuliza vita mahali pengi duniani. Kuna mashirika tele na vikosi tele vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani duniani, UNIKOM, unmibh,minurso,unifil,unmik,monuc,unmogip,unomig,unamsil n.k
 Kuna mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia uhalifu wa kivita. Mahakama hii ina mwanachama mmoja tu-Uholanzi, mjini The Hague.
 Kuna majaji 15 huko mjini The Hague wanaoshughulikia kesi za uhalifu na tumeona juzi hapa Mwendesha Mashitaka wa           Mahakama hii,Louis Mareno-Ocampo wa Buenos Aires, Argentina, akiwaita watuhumiwa sita wa mapigano ya Kenya ya Desemba, 2007, “The Ocampo Six” wakiitwa kujibu mashitaka mjini Hague.
 Tumesikia hata akina Charles Taylor,Slobodan Milosevic na wengine wakiwa wamekamatwa na kushikiliwa Hague. Tumesikia   Kanali Gaddafi tayari imetolewa waranti ya kumkamata yeye,mwanaye na mkuu wake wa ujasusi wakamatwe.
 Ilishatolewa waranti Omar Hassan Al Bashir wa Sudan ya Kaskazini naye akamatwe. Fodday,Sankoh, Joseph Kony,Hitler na watu wa kariba hii ni wakushitakiwa,kwa sababu wanakiuka haki za binadamu-wanaua watu,kuua ni kumnyima mtu haki ya kuishi,kila mtu ana haki ya kuishi.
  Sasa,msomaji, jiulize. Huko Libya,NATO inafanya nini? Ufaransa,inapogawa silaha kwa waasi wa Libya wanataka kufanyike nini kama siyo mauaji makubwa?
 Je, kwa kugawa silaha kwa waasi wa Libya, NATO,Marekani na Ufaransa hawaoni kwamba wanashiriki kupora maisha hata ya raia wasio na hatia Libya?
  Wao tayari ni Mahakama? Tayari wamefungua mashitaka Hague dhidi ya Gaddafi,lakini wanatafuta kumuua-wameshamhukumu kifo hata kabla ya kujitetea!
 Wao ni polisi,mahakama,mgambo na wanyongaji kwa wakati mmoja, hii ndiyo amani?
  Marekani, Benge la Congress limeshituka,Rais Obama kupeleka jeshi Libya bila idhini ya bunge,huu ungekuwa ushahidi kwa UN kumtia mbaroni Rais Barack Obama kwa kukiuka sheria za Umoja wa Mataifa na kuiingilia Libya kijeshi.
 Lakini,nani amfunge paka kengele?Waranti zinasainiwa wakamatwe akina Gaddafi, Al Bashir, Paul Kagame, The Ocampo Six, Fodday ‘Poppay’ Sankoh,Tayloy n.k
 Hakuna wa kunyooshea kidole Ufaransa,Uingereza na Marekani wala NATO! Kuivamia Libya ni sawa tu eti ni kulinda amani. Huu ndiyo Umoja wa Mataifa; na huku eti ni kulinda amani!
 Marekani kuwaunga mkono waasi wa Libya kuna tofauti gani na kumpa silaha Joseph Kony au Fodday Sankoh, Jonas Savimbi, Hitler, Idi Amin n.k kuua watu?
  Eti, Fodday Sankoh akakamatwa na kupelekwa mjini Hague kujibu mashitaka yak u ‘abuse human rights’ huko Sierra leone 1999-2000 Marekani na Ufaransa wakabaki.
 Marekani wanapomshitaki Charles Taylor kuwaunga mkono waasi wa RUF huko Sierra LEONE, wao wanawaunga mkono waasi wa Benghazi,Libya wanawapa silaha,wanawalea,Ufaransa inawaletea kila kitu,NATO wanawasaidia kupiga mabomu kwa ndege-mkuki wa nguruwe?
  Hii ni ‘double standadrs’ mwingine akifanya kosa lile anafungwa,wao wakifanya ni kosa takatifu!
  Afrika, haina veto power katika Umoja wa Mataifa wala katika Baraza la Usalama. Afrika kuna watu bilioni moja,lakini ulaya yenye watu wachache tu wana veto, wana ‘gutsy’ uwezo mtukufu wa kuingilia masuala ya Afrika,kupigana vita huku,kuua raia kwa makombora ya madege,na kuingilia masuala ya Afrika,bila Umoja wa Afrika(AU) kusema!
  Itaendelea
   congesdaima@yahoo.com
 0786 324 074
  
  
 

 

Friday, July 1, 2011

TANZANIA TUJIFUNZE KUTUMIA RASILIMALI KWA YESU WA NAZARETI

Nani wanajenga vitambi kwa pamba ya wakulima Kanda ya Ziwa?

       
PAMBA, “Dahahabu Nyeupe” hulimwa katika mikoa 13 hapa nchini; ni katika wilaya 42; na huajiri wakulima kati ya 350,000 hadi 500,000 hivi.
 Mnyororo wa thamani ya pamba, unaajiri watu wapatao milioni 14.
 Hivyo,hili ni zao ambalo,kama lingeangaliwa vizuri,lingewatoa Watanzania katika lindi la umasikini wa kutupwa.
 Mikoa inayolima pamba hapa nchini, ni pamoja na Iringa,Tanga, Pwani,Kilimanjaro,Mbeya,Morogoro na Arusha,iliyo katika Kanda ya Uzalishaji wa zao hili ya Mashariki(Eastern Cotton Growing Area), ambalo pamba hulimwa,lakini haizalishwi sana.
   Hii ‘Dhahabu Nyeupe’ lakini wazalishaji wake ni masikini kupindukia,hulimwa sana hapa nchini katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza,Mara,Kagera,Tabora,Kigoma,Singida, na Rukwa, ambayo imewekwa katika Kanda ya Magharibi(Western Cotton Growing Area).
Mchango wa hii ‘Dhahabu Nyeupe’ wazalishaji wake fukara, mcango wake katika Pato la Taifa kwa msimu wa mwaka 2009/2010 ulikuwa asilimia 2.13; ni chini kabisa ya matazamio.
 Serikali, inajitetea kwamba, uzalishaji wa zao hili katika msimu wa 2010/2011 ulishuka kwa sababu ya ukame, na wakati mwingine mvua zilinyesha nyingi sana, hususan Musoma Mkoani Mara, mashamba yakatitia!
 Wakulima walishindwa kunyunyizia madawa ya kuulia wadudu mashambani mwao, kwa sababu eti ruzuku haikusimamiwa vizuri.
  Katika eneo hili hapa la madawa ya kuulia wadudu,mbolea na pembejeo nyingine,kuna uzembe na ufisadi wa hali ya juu unaowafanya wakulima walime,lakini pamba yao ikose viuwadudu, na hatimaye iliwe na wadudu, kwa sababu, waliopewa jukumu hili ama wamepora mbolea na kuiuza wanakojiua, au hata hayo madawa ya kuulia wadudu ni feki ama bandia, na hayafikishwi kwa wakulima kwa wakati.
  Kuna wakati, wakulima waliuziwa mbegu zilizochubuliwa kwa kemikali, wao wanaita ‘delinted seeds’ zikagoma kuota!
  Wakulima walilia; badala ya kulipwa fidia kwa utapeli huu,na kwa hasara waliyopata kutovuna msimu mzima, wakalipwa mbegu!!
  Kisheria,hii ni hujuma-ni kuhujumu uchumi wa nchi,kumuuzia mkulima mbegu mbovu zisizo na viwango vya ubora, counterfeit, ama double standard. Hili niliache kwanza.
   Msimu wa 2010/2011,(sasa huu ni msimu wa 2011/212) ulivunja rekodi, kufuatia mabadiliko makubwa ya bei katika sokola dunia.
  Bei ilipanda kutoka senti 86 za Dola ya Marekani,mwezi Agosti 2010 hadi Dola 2.44 kwa ratili moja mwezi Machi mwaka huu wa 2011.
  Rekodi iliyowahi kufikiwa ni senti 96 za dola ya Marekani, katika msimu wa 1994/95.
  Ratili mbili ni kilo moja, kwa sababu hiyo, katika msimu huu pamba iliuzwa hadi kwa dola 4.88 kwa kilo ambazo ni kama shilingi 7,320.
   Sasa, angalia. Hata kama kuna kodi, kulipa riba mikopo ya benki(wanunuzi wa pamba hukopeshwa na mabenki,hususan CRDB),kulipa mishahara na tozo anuwai, ndiyo mkulima wa zao hili alipwe shilingi 600/= kwa kilo?
Katika msimu huu, Bodi ya Pamba nchini(Tanzania Cotton Board) imetangaza kwamba,bei ya kuanzia kununua pamba ni shilingi 1,100 kwa kilo.
  Nataka kusema kwamba, hata kama bei imepanda msimu huu,kutoka shilingi 600/= ama 700/=wakulima walizouzia pamba msimu uliopita, ndiyo kitu gain?
  Yaani, bei ipande katika soko la dunia hadi kufikia zaidi ya shilingi 7,000 za hapa, wao walipwe shilingi 600 hadi 1,000!!
  Sababu za kupanda bei ya pamba msimu huo zilikuwa ni kupungua kwa akiba ya pamba duniani, yaani uzalishaji wa zao hili duniani ulipungua,na kulikuwa na mahitaji makubwa ya pamba katika viwanda vya nguo duniani.
  Hii ni fursa kwa wakulima wetu,hasa wa Ukanda wa Ziwa Victoria na mikoa mingine iliyotajwa.
Lakini, wameishia kulia njaa; pamba wameuza,lakini hawana kitu wanakabiliwa na njaa,hadi serikali imeombwa kuwapelekea chakula cha njaa, na maofisa wa serikali wakapata mwanya kusafirisha chakula hicho hadi Sirari,na kukiingiza nchini Kenya!
   Mkurugenzi wa Pamba, KANDA YA MAGHARIBI, Jones Bwahama, ameniambia mwishoni mwa wiki, kwamba mabadiliko ya bei yanaweza kutokea mwezi Oktoba hivi,baada ya wazalishaji wakubwa wa pamba duniani: China,Pakistan,India, Marekani,Uturuki n.k kuingia sokoni.
 Ni kama Bwahama alikuwa akiniambia kwamba, bei ya pamba yetu katika sokola dunia,hutegemea sana hali ya hewa ya uchina,Marekani,Uturuki n.k
 Hata hivyo, Bwahama akaniambia kwamba, pamba ya Tanzania inaweza kupanda bei kwa sababu kuna wawekezaji toka Thailand na Uturuki wanaonesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya kufuma nyuzi(spinning) ili kuzichakata nyuzi za pamba,kuziongezea thamani,kabla ya kuziuza.
  Hata hivyo, hata pamba ipande maradufu,katika soko la dunia,mbona mkulima anabaki masikini yuleyule; habadiliki.
   Badala yake, wanakuja watu matapeli, wanavuna pamba mgongoni mwake,wanajenga rosheni mijini,wananunua magari ya fahari kwa pamba hii hii “Dhahabu Nyeupe” yeye akibaki fukara anayesubiri chakula cha msaada kutoka serikalini!
  Bwahama, amesema katika msimu huu pamba inayotazamiwa kuvunwa katika eneo la hekta 477,354 nchini ni kilo 247,247,860; ni kama kilo 250,000.
 Mkoa wa Mwanza pekee unatazamiwa kuvuna kilo 54,122,750,lakini wakulima wa pamba wa Mwanza wataambulia nini,kama siyo vipapatio vya pamba?
 Mkoa wa Mara,unatazamiwa kuuza kilo 11,033,610 na Shinyanga ambao ndiyo wazalishaji wakubwa wa pamba wanategemewa kuvuna pamba yenye uzani wa kilo 160,968,875.
   Wakulima wa pamba wanalima kwa taabu, wakati mwingine mazao yananyauka kwa kiangazi, wanapofanikiwa kuvuna na kuuza wanakutana na ujanja ujanja,wizi na utapeli.
   Angalia;Wizara ya Viwanda na Biashara ilishapiga marufuku matumizi ya mizani aina ya Kapani, kununulia pamba tangu mwaka 2009.
  Kapani zinawaibia wakulima; nyingi zinachezewa na wanunuzi wa pamba na mawakala wao, zinaweza kuwapora wakulima hata kilo 15 nakuendelea.
   Serikali,ikasema kapani zisitumike, ziletwe mizani aina ya Salter kutoka Uingereza, ambazo haziwezi kuchezewa kwa urahisi.
  Wanunuzi wa pamba, wakaanza, mara “ooh,tumetoka kwenye mtikisiko wa uchumi, hatuna uwezo wa kununua mizani mpya na  kuzitupa kapani za mabilioni ya shilingi ghafla!”
 Mpango huo ukanywea,kwa sababu pia ilisemekana aina hiyo ya mizani mpya ilikuwa biashara ya wakubwa!
 Yaani, matatizo na changamoto za mkulima wa pamba,hugeuka ‘deal’ kwa maofisa wa serikali na matapeli,naam mafisadi!
   Nilizungumza na Ofisa Mkaguzi wa Pamba, Kanda ya Magharibi(WCGA),Buluma Kalibushi, juu ya mpango huo wa serikali kuondoa kapani zinazowaibia wakulima katika manunuzi ya pamba msimu huu.
  “Kapani zitaendelea kutumiwa,kwa sababu kuziondoa na kuleta mizani mpya ni suala linalohitaji maandalizi. Kuna vituo kama 9,000 vya kununua pamba. Ukibadili mizani,unazungumza biashara ya shilingi takriban bilini tisa”.
   Kalibushi, aliniambia kwamba wanunuzi wa pamba wamezikataa mizani hizo kutoka Uingereza, kwanza walisema ilikuwa ‘biashara ya watu fulani’ kwamba zinatafutwa mizani bora zaidi.
 “Wanunuzi wa pamba wameleta sample(za mfano) ambazo ni za digitali,lakini haziku qualify(hazikukidhi viwango vya ubora)”
 Hizo kapani, zimewaibia wakulima na kuwaneemesha sana wanunuzi ambao katika pamba, wanauza pamba yenyewe, mbegu nazo mkulima anauziwa tena!
 Halafu, wanauza mafuta ya pamba yanayotumiwa kupikia chakula, na mashudu ambayo ni chakula cha mifugo.
  Wakati pamba ni dhahabu nyeupe, wakulima wa pamba hawana chakula,hawana nyumba wala maisha bora.
Mafuta yanaitwa “Black Gold” kwamba ni dhahabu nyeusi. Je, hatuwaoni wenye visima vya mafuta huko Arabuni, wakiwa matajiri?
 Iweje pamba iwe dhahabu nyeupe, lakini wakulima wa pamba hawana hata uwezo wa kupeleka watoto wao katika shule za kueleweka?
 Na shule wanazosoma watoto wao ni zile za kata,zisizo na waalimu na miundo mbinu?
 Nataka kusema kwamba, Bodi ya Pamba, haina wafanyakazi wa kutosha ili kuwabaini wanunuzi wa zao hili huko vijijini.
 Hawa wanunuzi na mawakala wao,kazi yao ni kuiba uzani wa pamba ya mkulima-ndiyo maana naye akaamua kuweka mawe,mchanga na maji katika pamba ili kuongeza uzito,maana naye anaporwa!
  Hata hivyo, kuna msemo wa Kiingereza, “Two wrongs can’t make a One Right” Kwamba kosa moja lisihalalishe kosa lingine.
  Huku ni kushusha thamani ya pamba katika masoko ya kimataifa, na mwisho wa siku atakayeumia ni mkulima wakati pamba yake inapokosa soko.
   Tunazungumza suala la ukosefu wa ajira,wakati pamba ingeweza kuwalipa wakulima 500,000 wakawa na maisha mazuri na wengine milioni 14 wangeajiriwa na pamba, ukosefu wa ajira ungetoka wapi?
   Tatizo,ni kukosa watu wenye utashi wa kisiasa na wazalendo wa kutaka kuendeleza nchi na fursa zake.
 Inapotokea, kuna wizi huu na uporaji katika sekta ya pamba, hakuna anayewajibika isipokuwa mkulima anawajibika mwenyewe kwa umasikini kuongezeka.
 Sasa, kuna wanunuzi binafsi wa pamba,na kilimo cha mkataba,ni yaleyale.
Nilidhani, KILIMO  KWANZA, ingekuwa kampeni kali ya kuondoa mianya ya rushwa,wizi na utapeli katika sekta ya kilimo hasa katika mazao ya biashara.
Lakini, bado wezi wanaachwa,wanabebwa pasipo kufungwa jela,halafu wakulima wanabaki masikini-tunaimba kwamba eti hatujui kwa nini wananchi ni masikini katika wingi wa fursa hizi!
  Nadhani, tumeona ni akina nani hasa wanaojenga vitambi kwa pamba ya mkulima.Serikali inajua,na inayasema haya kila mara,utekelezaji haupo!!
 Juma lijalo nitatazama uvuvi wa samaki,hussan sangara,ziwani Victoria
     0786 324 074
     0754 324 074