Monday, November 7, 2011

Akina David Cameron hawajaanza leo kuiburuza Tanzania


 
 KATIKA mkutano wa Jumuiya ya Madola,uliofanyika juzi  hapa, tumemsikia David Cameron,Waziri Mkuu wa Uingereza,ambayo ni koloni letu akitoa shuruti,ili tubadili katiba,na kukubali mashoga!
 Watanzania wengi wamepinga jambo hili,lakini nadhani hawaelewi kwamba nchi 54 za Commonwealth, haziko huru-huria,zingali zikiburuzwa na Uingereza na washirika wao,kwa sababu ya misaada yao kwetu!
Wanatutishia kama watoto,kwa kuwa tulishasahau kujitegemea. Akina Julius Nyerere na siasa ya UJAMAA NA KUJITEGEMEA, walipoondoka, basi tukarejea kuwategemea ‘wajomba’ wa Magharibi.
Sasa, tunapatwa na kile walichoonya akina Nyerere, tunaamrishwa kama watoto!

Mwanzoni  mwa karne ya 19, ulimwengu ulianza harakati za kupinga Ukoloni na utumwa ulioendekezwa na mataifa ya Kaskazini dhidi ya yale ya Kusini.
    Watumwa toka nchi duni hususan za Afrika, Asia na Amerika Kusini walitumika kuzalisha mali kama kilimo cha mazao ya biashara, yaliyokuwa yakihitajiwa sana na wakubwa wa Magharibi.
    Mazao hayo yalitumiwa kama mali ghafi katika viwanda vyao; wao wakanufaika sana kuliko sisi vibarua au tuseme watumwa wao, tuliosalia duni, na bila usawa katika mambo yote, ikiwemo Haki za Binadamu, na usawa katika sheria.
     Vita vya kupinga unyanyasaji  (Civil War) vilianza Marekani , Aprili 12,mwaka 1861.
Hadi karne moja baadaye nchi nyingi zikiwemo za Afrika zilikwishapata uhuru; na utumwa ulikwisha pigwa marufuku katika Ulimwengu wote.
   Raia wote wa ulimwengu walikwisha kuwa sawa katika sheria na mahitaji mengine yote ya Binadamu.
Kupitia makubaliano ya Umoja wa Mataifa, hakuna raia wa nchi moja aliyekuwa bora kuliko wenzake wa nchi zilizokuwa dhalili.
Wakoloni walianza kutuamrisha siku nyingi. Kumbuka suala la Middleton na Benjamin Mengi.
    Ni kwa misingi hii, suala la Mwekezaji wa Kiingereza, Stewart Middleton,aliyekorofishana na mwekazaji mwenzake wa Kitanzania, Benjamin Mengi,kushughulikiwa na vyombo vyetu vya dola , ni kama ada.
    Mengi na Middleton walikorofishana katika masuala ya kibiashara, kufuatia ubia wa makampuni yao ya kilimo, ya Silverdale Tanzania Limited na Mbono Farms, ya huko Hai mkoani Kilimanjaro.
    Kulingana na gazeti la Mwananchi la Jumapili, Septemba 3,mwaka 2006,Mbunge mmoja wa Uingereza wa chama cha Mahafidhina, chama cha akina Cameron, Conservative, Roger Gale,alisema Bungeni kwamba Tanzania inyimwe misaada tangu sasa kwa sababu ya Mwekezaji huyo kutiwa nguvuni, ka kutishiwa kutimuliwa nchini!
    Kwamba Tanzania itatakiwa kunyimwa misaada na Uingereza, hadi hapo itakapoonyesha mazingira bora ya uwekezaji; yasiyowanyanyasa wawekezaji, hususan Waingereza!
Misaada inatunyima uhuru jamani…misaada! Inatuweka mkao wa kuliwa na Waingereza!
   Kwa kuwa Uingereza, kupitia Shirika lake la Misaada la Kimataifa,(DFID) ndiyo inayoomgoza kutoa misaada kwetu kuliko nchi nyingine yoyote duniani, basi swala la Mzungu huyo Stewart Middleton, linaweza kututoa nyongo!

     Si kusudi la makala hii kutaka kuingilia mgogoro wa Mengi na mzungu huyo, ambao tayari vyombo vyetu vya Dola vimechukua hatua stahili. Wala si nia ya makala hii kumpendelea Mtanzania mwenzetu, Mengi, na kutaka kumuumiza Mzungu huyo toka nchi wakoloni wetu wa zamani.

     Hata hivyo, nijadili basi kwamba serikali kwa kutumia vyombo vyake ambavyo tunaamini hutenda haki kwa raia wote wa nchi hii, wakiwemo wageni kama Middleton, imetekeleza wajibu wake bila upendeleo.

    Nasema bila upendeleo kwa sababu polisi walimtia mbaroni mzungu huyo, bila shaka baada ya suala hilo kufikishwa mezani kwao.
Kitendo cha mzungu yeyote kukabiliwa na polisi wetu wakiwa na silaha si hoja; kwa kuwa hata wazalendo wa nchi hii kukamatwa na polisi wenye silaha hata kwa tuhuma ndogo tu, kama kukataa kulipa deni la shilingi 1000, au kukopa kuku na kushindwa kulipa.

 Uingereza kwenyewe, hali ni hiyohiyo, kwamba watuhumiwa (bado si washitakiwa) hukabiliwa na polisi au askari kanzu wenye silaha.
 Ulimwengu haujasahau risasi za moto za askari wa Kiingereza zilipomiminwa miilini mwa wasio na hatia, kwa sababu tu walikaidi kukamatwa!

  Uingereza ikaishia kuomba radhi kwa kitendo cha askari wake kuua raia wa kigeni, kwa kuwa tu eti alifanana na waliolipua mfumo wa reli nchini humo…naam, magaidi!
   Middleton, kama raia wengine wa hapa, aliswekwa rumande wiki mbili (siku 14) bila kupewa dhamana, ambayo ni haki ya kila raia. Hata hivyo, aliachiwa huru, baada ya  vyombo vyetu vya dola kumaizi kuwa  madai dhidi yake hayakuwa na msingi wowote.

   Yawezekana kulikuwa na makosa ya kiutendaji au kiutekelezaji; lakini angalau kilichotendeka kimeonyesha kuwa vyombo vyetu vilifanya kazi kwa usawa, bila upendeleo wowote.
     Vilimkamata Mwingereza huyo; vikachunguza madai dhidi yake, kisha vikamwachia huru baada ya kubaini kuwa hakuwa na kesi ya kujibu.
   Suala la kumnyima Mzungu huyo dhamana, kama wanyimwavyo raia wengine ni changamoto kwa vyombo vyetu, katika barabara ya kuelekea utawala bora wa haki na demokrasia; na wala si kasoro kwa Middleton kwa kuwa ni mweupe, tena kutoka kwa Mabwana wakubwa, Uingereza.
   Kulikuwa na sababu nyingi za kumnyima dhamana Middleton; kwa sababu za usalama wake au hata ili kuepuka uwezekano wa yeye kutoweka kabla ya suala lake kushughulikiwa kwa nja za haki.
   Hata hivyo, kwa kujali sana uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Uingereza, serikali yetu ikafanya mazungumzo na wafanyabiashara hao wanaozozana, kisha ikazungumza kidiplomasia na ubalozi wa Uingereza. Suala hilo tayari liko mahakamani; chombo pekee cha kutoa haki kinachotambuliwa hata na Bunge la Uingereza.
    Lakini kwa kuwa sisi ni nchi masikini; tunaendesha mambo yetu kwa ufadhili wa Mamwinyi kama Mbunge, Roger Gale, vyombo vyetu kushughulikia suala la Mwekezaji wa Kiingereza, ni tatizo kubwa, la kusababisha Waziri Mkuu, Tony Blair (wakati huo) kuombwa kukata misaada!
   Makala hii haishangai kauli za aina hiyo katika mabunge ya wakoloni wetu wa zamani, ambao hata sasa wanatutawala kwa kutumia misaada yao inayopitia katika makampuni anuai ambayo ni mawakala wao wa kutukoloni (colonize);kwa kuwa machoni pao, sisi si chochote, si lolote,isipokuwa watumwa !

   Zimbabwe, rais Robert Mugabe anaonekana dikteta wa hali ya juu sana, si na wananchi, bali anavyotazamwa na Bunge la Uingereza kwanza.
 Si Zimbabwe tu, bali popote Waigereza walipowahi kutawala, ama palipo na maslahi yao, yanayopingwa kwa nguvu na serikali husika
.Naam huu ni uchoyo wa uingereza, ubaguzi na dharau.
   Waama, kila maslahi ya Marekani au Uingereza yanapopingwa kwa nguvu, basi huonekana machoni pao kuwa ni haki za “Binadamu” zimevunjwa! Je, binadamu ni nani? Marekani na Uingereza peke yake, bila raia wa mataifa mengine?
Je, inapokuja daawa baina ya Muingereza na Mtanzania, dola ikunje mkia miguuni, mithili ya kijibwa? Iufyate!!
  Mwaka 2004, askari wawili wa nchi hiyo waliokuwa mapumzikoni nchini, wakitokea vitani  Iraki, Nigel David (23) na  Brett Richard (20), walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka kwa zamu hadi kumuua msichana wa Kitanzania, Conjesta Ulikaye, mnamo Novemba 10, 2004.
   Tukio hilo lilitokea katika  ufukwe wa hoteli ya Siliver Sands, Dar es salaam. Shauri hilo la kesi ya mauaji, likashughulikiwa kwa siku 36 tu; wakati kesi za mauaji zinazowahusu Watanzania huchukua miaka mingi tu.
   Nigel na Brett walifikishwa mahakamani Novemba 16; yaani siku sita tu baada ya tukio.Kesi hiyo ilifutwa Desemba 22 mwaka jana, ikiwaacha ndugu wa marehemu kulalamikia mazingira hayo ya kuharakishwa kesi ya tukio la kikatili, na watuhumiwa kufutiwa shitaka upesi, kwa mujibu wa kifungu namba 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985.
      Mwandishi wa makala hii, alimuuliza Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Geofrey Shaidi, Machi Mosi mwaka 2006 jijini Mwanza, alipokuwa  akihutubia Mkutano wa Pili wa mwaka wa wanasheria wa   serikali.
    Kwamba kitendo cha ofisi yake kukimbia kuwaacha huru askari hao wa Uingereza, ilikuwa kulinda maslahi ya Uingereza au Tanzania?!
    “ Hawakuachiwa kwa ajili ya kulinda maslahi ya Uingereza au ya Tanzania…ushahidi uliokuwepo haukutosha. Wasingeendelea kushikiliwa bila ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani”, DPP Shaidi alisema.

    “Kesi hazicheleweshwi na ofisi ya DPP; zinachelewa mahakamani,zinapokuwa zikisubiri kupangiwa tarehe ya kusikilizwa. Hivyo faili la Wazungu hao lilipofika kwetu tukalishughulikia kama kawaida”, Shaidi aliendelea kufafanua.

   Akasema pia kwamba wanajeshi hao waliokuwa mapumzikoni wakitokea Iraki, vitani, hawakuachiwa huru kwa sababu ya serikali ya Tanzania kuchelea kunyimwa misaada na Uingereza, iwapo wangetiwa hatiani na mahakama na kupewa adhabu ya kunyongwa.

   Naam: Leo, baada ya kauli ya Mkurugenzi huyo wa Mashitaka nchini,Bunge la Uingereza limeombwa kuinyima misaada Tanzania kwa Muingereza  mwingine kutiwa mbaroni (kukamatwa tu) kwa shauri la kibiashara tu; si la mauaji. Na wala hajahukumiwa kifungo!
    Kwa jamaa na ndugu wa Marehemu Conjesta Ulikaye, wanaweza kupata jawabu la malalamiko yao dhidi ya vyombo vyetu vya dola. Pengine wangedhani wahusika walihongwa na wazungu hao wanajeshi, au ulikuwa woga wa bure kwa ngozi nyeupe katika kutekeleza haki.
   Kumbe picha inayoonekana leo katika nchi zetu tegemezi, ni kuingiliwa hata kuziondolea mahakama zetu uhuru wake.
 Ni hapa, kauli ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Geofrey Shaidi, inapoweza kutiliwa shaka na umma wa Watanzania leo, kwamba kesi za Wazungu, hususan Waingereza, haziishiki pabaya serikali!
     Kulingana na gazeti la Mwananchi la Jumapili, Septemba 3, mwaka 2006, misaada tunayopata toka Uingereza, imeongezeka kutoka Pauni milioni 80 (sh.Bilioni 208)mwaka 2003/2004 hadi pauni milioni 110 (sh.bilioni 286) mwaka 2006 na mwaka 2007.; huku asilimia 70 ikienda katika Bajeti.

   Naam, haya ndiyo madhara ya misaada toka kwa matajiri…kuingiliwa hadi uvunguni, chumbani na hata shukani! Uhuru wetu tuliopata Desemba 9, 1961 toka kwa Malkia wa Uingereza uko wapi?
Ati tunaadhimisha miaka 50 ya uhuru!
     Kama  Uhuru upo, kwa nini akina Roger Gale, washinikize vyombo vyetu kuchelea kuwachukulia hatua wawekezaji kama  Stewart Middleton, kama wana makosa?
Kwanini David Cameroon atuamrishe kukubali ushoga? Kwa nini tulazimishwe kwa kiwango hiki kama tuko huru?
Au wazungu hawakosei, kama si kuwa juu ya sheria za nchi walizowahi kutawala; ama wanaendelea kuzitawala kwa “remote control” kupitia mashirika ya misaada?
    Lini Waafrika tutakuwa huru dhidi ya ubeberu wa kimagharibi?
Kwa kuwa Tanzania ni nchi huru, na wala si Iraki, Afghanstan au Somalia ambako hakuna mfumo wa utawala unaoeleweka, ndiko ambako Uingereza ingetilia mashaka mfumo wa sheria na maamuzi ya haki, na kamwe si Tanzania.
    Uingereza itambue kuwa uhusiano uliopo kati yetu ni wa usawa, na wala si wa nchi moja kujiona iko juu kuliko nyingine katika jambo lolote, likiwemo la kisheria. Kama Mtanzania anavyoweza kufungwa kwa kuingia nchini humo bila kufuata taratibu, ndivyo Muingereza anavyoweza kujikuta Segerea au Butimba, kwa kukutwa na bangi.
   Kamwe, nchi yoyote isilalamike hatua za haki zinapochukuliwa dhidi ya mshukiwa au mshitakiwa.
Tumefika hapa kwa sababu ya kujikomba, laity Nyerere,Kaunda,Kenyatta,Nkrumah na wenzao wangekuwa hai leo!
Kwa kuwa hatuko huru,ndiyo maana tunaswagwa…
0786 324 074

BERNARD MEMBE HUNA UBAVU KUZUIA USHOGA TANZANIA!!






KATI ya mambo yanayochekesha sana ni “AMRI” ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron,kuziamrisha nchi za Jumuiya ya Madola(Commonwealth) kufanya Mabadiliko ya Katiba,  ili waweke kipengele cha kuruhusu ushoga!
Watanzania, wameonekana kumpinga sana David Cameron,kuhusu ushoga,  wanasahau kwamba nchi yetu haiko huru kabisa, na wala haijawahi kupata uhuru kutoka Uingereza!
Hili ni jambo linalouma sana; na wengi hawataki kuamini kwamba hatujawahi kupata uhuru,kama inavyodaiwa. Hii ni miaka 50 ya uhuru wa bendera.
Hata hivyo, nitapata fursa kujadili jambo hili kwa kina, siku nyingine.
Mimi najua Tanzania haijawahi kuwa huru,na nchi nyingi za Jumuiya na Madola hazijawahi kuwa huru,ndiyo maana tunaburuzwa na Malkia, wanaye akina Prince Charles, wajukuu akina Prince Harry na William na akina Tony Blair, Gordon Brown,David Cameron na wenzao.
 RAIS Barack Hussein Obama, yeye anawaunga mkono mashoga wazi wazi, na nchi za Afrika zinaona mashoga ni uchuro.
Kwa sababu, siku hizi ndiyo uhuru,usawa na demokrasia na Haki za Binadamu zinavyotaka-mashoga nao ni watu.
 Obama, amewateua mashoga na wasagaji kama 150 hivi,katika nafasi za juu serikalini mwake,kwa sababu Marekani yapo majimbo lukuki yaliyohalalisha mashoga na wasagaji kufunga ndoa.
 Afrika, viongozi wanapinga ushoga na usagaji. Sam Nujoma wa Namibia aliwahi kutoa amri,mashoga na wasagaji watiwe mbaroni na kufungwa jela.
   Rais wa Zimbabwe, Robert Gabriel Mugabe, kawafananisha mashoga kama mbwa koko na nguruwe hivi.
Naam, hizi ndizo kauli zinazolalamikiwa sana na mashoga. Na David Cameron, Malkia Elizabeth II na wenzao,wanawaona hawa viongozi wanawapinga mashoga,kwamba ni Madikteta!
 Uganda, kulikuwa na muswada wa kuwasweka rumande mashoga na wasagaji ama wanaojihusisha na ndoa za jinsia moja.
 Na kwamba,mtu akishindwa kutoa taarifa juu ya haya anafungwa jela miaka mitano au saba!
Hapa kwetu, ndiyo tumeamrishwa kubadili Katiba na kuwaruhusu mashoga waoane kwa uhuru pasipo ngebe!!
Askofu Desmund Tutu wa Afrika ya Kusini, alisema ushoga ni kinyume cha ubinadamu,ni tabia mbaya kabisa kuliko ubaguzi wa rangi. Ni kweli kabisa,lakini Kanisa la Anglikana la Malkia na David Cameron, linaona ushoga, ni bomba tu!!
Shirika la kutetea Haki za wafungwa duniani, Amnesty International, lenyewe hupinga ubaguzi,unyanyapaa dhidi  ya mashoga na wasagaji ama wenzi wa jinsia moja.
   Hata hivyo, wanaharakati wa Haki za Binadamu wameiona Afrika imeshindwa kufuatilia watoto wa mitaani na wagonjwa kulazwa wawili wawili vitandaji hospitalini, waafrika wanafuatilia vyombani na vitandani wanakolala mashoga!
 Desemba 23 mwaka jana,nyumbani kwao Luis Moreno Ocampo,( anayewatoa kamasi akina Uhuru Kenyatta siku hizi),huko kwao Argenjina, Jose Maria Di Bello na Alex Freyre,walikuwa wa kwanza kuoana huko Amerika Kusini.

Mapema  mwaka 2007, umefanyika Dar es salaam mkutano wa Kimataifa wa Kanisa la Anglikana, ili kujadili kama ndoa za jinsia moja na ushoga zihalalishwe. Tanzania ilikuwa ‘Pepo ya Mashoga’ siku nyingi!
    Naam, Tanzania ambako  kwa mujibu wa Katiba ya sasa, inasemwa vitendo hivi vya usagaji na ushoga ni kinyume cha sheria, iliridhia Mkutano huo ufanyike Whitesands,  mwaka 2007  kujadili haki za wasagaji na mashoga, ama usawa wa watu wa jinsia zote katika muungano wa hiari(Civil Partnership)  uitwao ndoa.
    Hapa nchini, sheria  inayoitwa ‘kandamizi’  (na mashoga) inaruhusu tu watu wa jinsia tofauti(heterosexual couples) kuoana.
   Katika Ulimwengu ulioendelea, sheria inaondoa kizingiti; inatoa “haki” kwa kila mtu kuoa ama kuolewa anavyotaka na anayemtaka, mradi tu anao umri wa miaka 18; umri wa mtu mzima kikatiba.
    Watu wakubwa sana wameolewa wanavyotaka katika Dunia hii.
  Naam, watu wenye kuheshimika sana: matajiri, wanaoketi meza moja na wafalme wa Dunia.
    Sir Elton John(60) alifunga pingu za maisha na mchumba wake wa siku nyingi, David Furnish(45) Mei mwaka 2005.
Siku hizi, wame 'adopt' mtoto, eti wameasili mtoto, wanalea!
    Alikuwa miongoni mwa watu 700 waliofunga ndoa  za namna  hiyo, mwaka huo. Hatua hiyo ilifikiwa baada ya England na Wales kupitisha sheria ya Ndoa za Jinsia Moja.
     Basi, baada ya  ndoa ya Sir Elton John, kulikuwa na hafla ‘kali’ katika Jumba la kifahari sana.
   Walitumia ukumbi wa karne ya 17 ambao pia aliutumia Prince Charles, wakati anamuoa mpenzi wake wa siku nyingi, Camilla Parker Bowles.
   Camilla na Prince Charles walifunga ndoa Apirili mwaka huo wa 2005.
    Siku ya harusi, Sir Elton John alivalia suti safi, tai nyeupe na miwani  myeusi, akashangiliwa kwa ushindi.
      Ndoa kama hizo zilishafungwa Ireland na Scotland.
  Waziri Mkuu, Tony Blair (wakati huo) aliwapongeza maharusi kwa kufuata sheria zilizowekwa…sheria za ndoa za mashoga.Haki za Binadamu!! Mimi simshangai David Cameron.
    Huo ulikuwa uhuru wa kikatiba wa mataifa ya Ulaya, Marekani, na Afrika Kusini.
 Sasa uhuru huu-Equal Marriage for All- unainyatia Tanzania, maadam Kanisa la Anglikana limeruhusiwa kujadili kitu hiki katika ardhi yetu.Katika mchakato wa Katiba Mpya,lipo wimbi la mashoga na wasagaji,kutaka haki zao.
   Kwa mara ya kwanza, Dar es salaam inakuwa pepo ya mashoga na wasagaji;wakati ulipofanyika mkutano wa Anglican, jijini Dar.
   naam watu maarufu sana katika jamii. Tazama ndoa ya Sir Elton John na David Furnish.
    David Furnish ni mtengeneza Filamu, raia wa Canada, ambaye amekuwa katika lindi la huba na Sir Elton kwa miaka 12 kabla ya ndoa hiyo. Mwaka huo 2005 ‘walifanyika mwili’ mmoja.Walifunga pingu za maisha.
   Waliiunga mkono sheria hiyo ya Ndoa za Jinsia moja kwa vitendo.
     Miongoni mwa waliohudhuria harusi hii ya kukata na shoka ni mamaye Sir Elton John, Sheila, na Babaye wa kambo Fred.
    Wazazi wa Furnish, Gladys na Jack, pia walikuwepo katika tukio hilo. Ndoa ilifungwa kwa kipindi cha saa moja; iliendeshwa na Msajili maarufu sana, Clair Williams, ambaye pia aliifungisha ndoa kati ya Prince Charles na Camilla.
            Miongoni mwa wageni waalikwa, alikuwepo pia Victoria Posh Adam, mkewe mwanasoka nguri wa Uingereza, David Beckham.
            Wengine walikuwa Jay Jopling. Sir Elton alivalia pete ya ndoa ya almasi; halafu wakaingia katika gari la kifahari, Rolls Royce jeusi; wakashusha vioo vya madirisha na kuendelea kupigana mabusu ya tashtiti!
     Sherehe ya harusi hiyo iligharimu takriban Pauni milioni mbili za Uingereza, yaani zaidi ya shilingi bilioni tano  za hapa.
   Walihudhuria wageni 700, wakastarehe ndani ya mahema. Sir Elton John alikuwa rafiki wa karibu wa Hayati Princess Diana Frances Spencer. Aliimba  Candle in The Wind katika mazishi yake mwaka 1997.
   Walikutana na   Furnish kwenye sherehe mwaka 1993 wakapendana. Miongoni mwa kazi zake ni ‘It’s a Boy Girl thing’.
    Nchi zilizokwisha kubali Ndoa za Mashoga ni pamoja na Afrika Kusini, Novemba mwaka 2006, kupitia Muswada wa Muungano wa Kiraia.
     Mchungaji V. Gene Robinson wa Kanisa la Angikana la New Hampshire, alifunga pingu za maisha na Mark Andrew, akawa Askofu wa kwanza shoga katika Ulimwengu.  Angikana ni ‘pepo ya Mashoga’ ingawa Afrika bado wanajidai shingo ngumu.
 Hiki ni kitendo kilichoigawa dunia katika mihimili miwili. Sasa, amri inatolewa watu wote kusalimu amri.
  Kwa sababu  ‘ubishi’ huu wa uhalali ama uharamu wa ndoa za Jinsia moja umefanyika Dar es salaam, na kualika mashoga wa kimataifa kujadiliana juu ya kuhalalisha ndoa hizi, ni wazi Tanzania tayari imevamiwa!
    Ndoa hizi zilihalalishwa Ulaya Kaskazini tangu mwaka 1990, kisha zikavuka Bahari ya Atlantic. Marekani, majimbo mengi yamebadili sheria kuridhia ndoa hizo. Limo Jimbo la Vermont, Connecticut. Majimbo mengine kama San Francisco na Massachusetts hutoa leseni kwa mashoga na wasagaji kuoana.
      Ndoa hizi zimeruhusiwa pia Canada, New Zealand, Ujerumani, Denmark, Norway, Sweden, Finland, Uhispiania Ubelgiji na Uholanzi.
    Katika Afrika, mwaka 2006 Mahakama Kuu ya Afrika Kusini ilisema Katiba ya nchi hiyo ilikuwa haiwazuii watu wa Jinsia moja kuoana.
   Basi, Waziri wa Mambo ya Ndani, wakati huo, Nosiviwe Mapisa-Nqakula, kufika mwaka 2007 awe amepitia sheria na kuifanyia mabadiliko ili kuruhusu kila mtu kuoa au kuolewa!
 Hata hapa, katiba mya ikikamilika,kutakuwa na huru mtu yeyote kuoa na kuolewa.Tunajidai kukataa,lakini kimsingi tutakubaliana na sera za Sodoma na Gomora,midhali tulishamwasi Bwana Mungu na kukataa amri zake.
  Sheria za Ndoa za kawaida hutoa ruhusa kwa watu wa Jinsia tofauti kuoana.
   Lakini, mashoga na wasagaji wa Afrika Kusini walikuja juu kutaka “usawa” katikama husiano ya kijamii.
  Usawa huu ukiridhiwa basi utatambua muungano wa mashoga na wasagaji; nao watafunga ndoa kisheria makanisani na popote sheria inakoruhusu.
    Kila mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na mwenzake wa jinsia yoyote mwenye umri wowote kuanzia miaka hiyo, ataruhusiwa kufunga ndoa, chini ya sheria hiyo.
   Hata wawe wa jinsia moja, mmoja atachagua kuwa mke, mwingine mume; kwa kadiri ya uamuzi wao.
  Mtu mmoaja hataruhusiwa kuwa katika ndoa zaidi ya moja.
            Makanisa yamepewa utaratibu wa kufunga ndoa hizi, na waliooa au kuolewa kabla ya sheria hizi Afrika Kusini, wametakiwa kufuata utaratibu; kukubali ndoa yake au kuomba talaka.
  Ndoa zitafungwa popote, hata kanisani kwa mujibu wa sheria.
    Ndoa itakubaliwa si kwa kubadilishana pete za harusi, bali kwa mtu kumshika mwenzake mkono na kukubali katika kiapo kwamba anakubali kuoana na kuchukuana na mwenzake!
     Hiki ndicho kitu walichokuwa wakijadili wachungaji wa Anglikana, Whitesands, Dar es salaam, mapema mwaka 2007.
Na hivyo ndivyo David Cameron na Ulaya wanavyotaka Afrika ifanye! Mpende,msipende Tanzania itakuwa Sodoma na Gomora! Kwa sababu dunia nzima wanaitawala wao na sasa wanataka iwe Sodoma, sasa mnapinga nini?
Kwa kuwa hata Tanzania tayari wapo wanaume na wanaume waliokwishawekana kinyumba, ni wazi Muswada wa Sheria ya Ndoa ya Jinsia Moja(Civil Union Bill) uko mbioni kufikishwa Bungeni mjini Dodoma,  mwaka na siku itakapofika,siku katiba mpya itakapowapa uhuru mashoga na wasagaji kuoana. Na Uingereza, wanaochangia takriban asilimia 40 ya Bajeti yetu, wanataka  hiyo Civil Union Bill, sasa wanaopinga watachangia kiasi gani kwenye bajeti?
     Na kwa kuwa tunaiga kila jambo kutoka ‘majuu’ au ‘Sauz’ kama tunavyosema, Tanzania iko mbioni kuridhia Ndoa za Wasenge na Wasagaji, maadam hata sasa tayari wameoana kimya-kimya! Hata wanafunzi wa vyuo vikuu hapa…wamewekana kinyumba!
Kenya.viongozi wa madhehebu ya dini wanaipinga katiba mpya kwa kipengele hiki tu cha kila mtu kuwa huru kuoa na kuolewa!
     Ni kwa sababu hii hapa Tanzania, leo kusikia mwanaume akiitwa ‘Anti’ ni kitu cha kawaida sana!
Zamani, hawa walikataliwa na Kanisa la Mitume wa Yesu Kristo, wakaitwa mbwa!
 Kwa Uislam, ushoga ni dhambi ya mauti.Haki za Binadamu zinatambua pia haki za mashoga na wasagaji.
    Leo, Maaskofu(Waangalizi wa Kanisa) ndio wanaoolewa na wanaume wenzao; na mjadala wa Dunia nzima unaletwa Dar es salaam  kutafuta suluhu ama kutowaonea haya mashoga  hawa hata wanapohudumu madhabahuni.
     Kwa kuwa Haki za Binadamu zinawatambua mashoga kuwa ni binadamu wa kawaida wanaostahili haki zao, basi wanastahili watu hata wa Jinsia moja kuoana kama wale wa Jinsia tofauti wanavyooana, bila ubaguzi.
   Ni kwa sababu hii, wanaume wanaofanya vitendo vya kuingiliwa kimwili na wanaume wenzao, wanapata nguvu kubwa za kudai haki hiyo, hata kama baadhi ya watu bado wanawashangaa ama kuwaonea kinyaa!
    Tayari tunao hapa Tanzania wanaume mashoga wanaofanya biashara ya ngono.
Hawa wanaitwa ‘Kaka poa’ na hushindana vilivyo na ‘madada poa’ katika biashara hii haramu.
   Aliyekuwa   Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Simon Sirro, kabla ya kuhamishiwa Dar, alipoulizwa na Safu hii kwamba anawezaje kupambana na wimbi hili akasema,
 “Tunapowakamata, tunawafungulia mashitaka ya uzembe na uzururaji…sheria zetu ni dhaifu sana kuwashitaki hawa  makahaba na mashoga, kuhusiana na makosa yao halisi”, alisema. Naam sheria za sasa ni dhaifu kuwatoa kamasi mashoga!
    Naam, ‘kaka poa’ wapo katika miji mingi hapa nchini,  kasi ya kuwatia mbaroni ili wafunguliwe mashitaka, ama ni ndogo sana, au haipo kabisa. Ukikutana nao hawa, utadhani akinamama…wamebadili tangu mavazi hadi sauti!
    Kidogo kidogo  jamii imeanza kuwazoea hawa na baada ya muda Bunge linaweza kuridhia ushoga na usagaji! Alichosema Cameron ni hakika na kitakuja kutokea, ingawa tunabisha.
Kwa sababu gani serikali iliridhia ushoga kujadiliwa Dar es salaam, kama si kuanza kuukaribisha? Katiba mpya itaacha kuwapa kibali mashoga kufunga ndoa?
     Kwa tabia ya nchi yetu kushabikia kila ‘uchafu’ unaoletwa nchini, wimbi la ushoga na usagaji limeanza kushabikiwa na vijana, wakiwemo wa vyuo vikuu, ambao tayari wamewekana kinyumba ili kuridhisha nafsi zao, ama ili kuwa huru zaidi.
     Kwa sababu tayari watu maarufu sana kama Sir Elton John wamefunga ndoa za fahari sana; tena wamepongezwa na watu ‘wazito’ sana kama Tony Blair, Tanzania ya wapenda kuiga kila kitu  cha ‘majuu’ iko hatarini sasa kumezwa na gharika la ushoga kuliko nchi yoyote ya Afrika Mashariki.
   Na akina dada warembo wataanza kukataa kuolewa ili wapate muda wa kuwaoa wanawake wenzao, ili kusagana.
            Kwa kuwa ushoga na usagaji ‘hupigiwa debe’ na wanaharakati wa Haki za Binadamu wakiwemo wasomi hata wa Vyuo Vikuu; na kwa kuwa Makanisa yameanza kuruhusu mashoga kuhubiri madhabahuni, kumbe dhambi hii ya zamani “Soddomite” imetakaswa kwa damu ya wanaharakati hawa wa Haki za Binadamu!
     Kwa kuwa Tanzania suala la maadili liliachwa kuwa ajenda za kidini; kwa kuwa dini hususan hizi za wageni zimehalalisha usagaji na ushoga, basi vijana wengi wako hatarini kugharikishwa na tamaduni hizi za kishenzi sana kuliko wakati wowote.
    Kwa kuwa ungalipo muda kitambo, kabla ya Muswada wa Ushoga kupelekwa Bungeni, ni wakati mwafaka sasa jamii kutilia mashaka uovu unaokuja kama moja ya haki za Binadamu.

    Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe yeye ametangaza kuwapiga makonde mashoga watakaoleta ‘domo-kaya’ kudai haki zao nchini mwake!
  Mugabe atazamwe kama mpigania haki au Dikteta anayekandamiza uhuru wa watu?
Mimi ni Mwa-Adventista wa Sabato,namwona Mugabe kama shujaa. Lakini wangapi wanamwona Dikteta,kuwaita mashoga nguruwe? Yawezekana hata wewe,sasa wampinga nini Cameron juu ya Tanzania kuwa na mashoga?
    Lakini,  Mugabe anatazamwa kama Mhafidhina na dikteta zaidi kuliko kuwa mtu wa kisasa zaidi anayekwenda na wakati…yaani kwenda na wakati ni kuruhusu ushoga au kuwa shoga, midhali unafurahi na unaridhika kuwa hivyo nafsini mwako!
    Dalili ya mvua ni mawingu.
Kwa kuwa jamii iko katika kipindi cha mpito cha kuwazoea mashoga na wasagaji, basi Tanzania inaanza kuwa ‘pepo’ ya mashoga na wasagaji, siku katiba mpya ikianza kutumika,na mashoga waweza kupata haki na uhuru.
    Mkutano wa Waanglikana uliojadili ushoga, ni dalili kwamba jamii inaanza kushindwa kukememea vitendo hivyo.
 Madhehebu kadhaa ya Kikristo yamegawanyika sana juu ya ushoga na usagaji.
    Leo, viongozi wa kidini waliodhaniwa kuwa watu wa maadili,  ndio wanaoongoza kulawiti. Maadili ya kidini yalidhaniwa yangeiokoa jamii katika maangamizi, kumbe jamii inaanza kutumbukia shimoni.
     Hata Tanzania tunao akina Elton John, David Furnish na   V. Gene Robinson; watu wenye mvuto katika jamii, ambao tayari wameanza kuwavuta vijana wetu katika pepo za ushoga na usagaji.
    Kama hazitachukuliwa hatua za haraka za kukemea hali hii, wakati wowote na siku yoyote, si Dar es salaam tu, bali hata vijijini, tutashuhudia ( hata kwa njia ya televisheni) harusi za fahari sana za mashoga na wasagaji(watu maarufu sana; tena matajiri) zikifanywa kwa mbwembwe ili kuikoga jamii inayopinga  dhambi hii ya miji ya uwanda wa Sodoma na Gomora.
   Kwa kuwa tunao wawekezaji kutoka Ulaya, Marekani na Afrika Kusini, ambako ndoa za Mashoga na wasagaji ni halali, basi tusubiri kuona vijana wetu wakija na wachumba wao kutujulisha kuwa siku ya siku watafunga ndoa na wanaume wenzao!
 Sijui utamaduni wa mahari utaendelea?  
Kama sivyo, tunajiandaaje kupambana na Haki za aina hii za ‘Ndoa za Jinsia zote’ zikiwemo za mashoga na wasagaji?
 Je, Katiba Mpya itaepukaje kuwapa uhuru watu wa jinsia moja kuoana?
Tumewasikia maaskofu nao wakisema wanataka katiba mpya, sasa wasije kesho wakaipinga-wajiandae kufunga ndoa za mashoga makanisani!
Hii ni Sodoma na Gomorah, na kila mmoja anapaswa kujua kwamba hizi ni SIKU ZA MWISHO, huu ni MWANZO WA MWISHO-DUNIA INAKWISHA!!
    0754/0786- 324 074