Tuesday, June 28, 2011

Mheshimiwa Spika, naomba kuondoa shilingi kwenye bajeti ya Waziri Ngeleja!

TANESCO wanataka serikali iwape takriban shilingi za TANZANIA trilioni moja ili mgawo huu wa umeme umalizike!
 Hili ni janga kubwa kwa wananchi wa Tanzania. Siku hizi tunalala gizani, wizi,vibaka, siyo jambo la kuepuka,kwa sababu ya giza.
 Tunavaa nguo zenye kukunjamana, sababu pasi bila umeme?
 Usafi... sasa ni jambo la kutazama kwa mbali.
 Ndiyo maana tunakuuliza, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, bora ungejiuzulu hata kabla ya Bajeti yako kusomwa bungeni
 Kwanini Ngeleja hujajiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini, wakati hatuna umeme? Maji nayo hayapandi katika vilima vya Mwanza pasipo umeme, televisheni hatuangalii, kazi hazifanyiki sasa maana kompyuta bila umeme,ni kama ugali bila mboga bwana!
 Ni kwa sababu hiyo, niombe muongozo wa spika,ili nimwondolee shilingi, Ngeleja kwenye bajeti yake hata kabla ya kusomwa bungeni!
 Kwa nini tulale njaa..kisa umeme umekosekana hata kusaga unga? Magazeti nayo hayachapwi sasa,kazi hakuna,barafu hazitengenezwi, kazi zifungwe tukale wapi Ngekeja?
 Wewe ni mtu mmoja,jiuzulu ili kunusuru maslahi ya Watanzania?
 Kwanini useme mgawo utakwisha,kumbe umegeuka mkali zaidi?
 Siku tatu bila umeme?
 Ngeleja ondoka bwana kazi imekushinda!

OBAMA, UNAKUJA DAR ES SALAAM? NJOO NA MAJAWABU YA MASWALI HAYA




  NIMESIKIA,kwamba Rais wa Marekani, Barack Hussein Obama, anaweza kufika Dar es salaam kabla ya mwaka huu kwisha.
   Hii itakuwa ziara ya kulipiza,kufuatia ziara aliyofanya Rais Jakaya Kikwete huko Washington,miaka michache iliyopita.
 Kwa sababu hiyo, nasmwambia Rais Obama akifika Dar es salaam, awe na majawabu yamaswali tuliyonayo sisi Waafrika wenzake,maana tunamwona yeye hana hata chembe ya huruma kwetu.
Kuna dalili kwamba, Afrika inaanza kupingana na Jumuiya za Wazungu, ama zile za kimataifa, ambazo kimsingi Bara letu  huburuzwa na matakwa ya Wazungu.
  Umoja wa Afrika unakaribia kung’amua kwamba mataifa makubwa ya Wazungu, huyaburuza sana mataifa ya Afrika, hadi kuwachagulia nini cha kufanya.
   Umoja wa Afrika, uliowahi kuongozwa na Kanali Muammar al-Gaddafi wa Libya,  anayepigwa na mabomu ya Umoja wa Kujihami wa Ulaya Magharibi(NATO), umeanza kupingana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita(ICC) iliyoko Hague, Uholanzi, juu ya suala la kumkamata Kiongozi wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir.
 Al Bashir, siku hizi ana urafiki na Uchina,maana Wamarekani wao ni vinyonga.
    Nilipokuwa  nikisoma gazeti la The East African,  Julai 20-26, mwaka 2009 nilikutana na katuni iliyosema, Umoja wa Afrika(AU) unataka sana kutuma ushahidi wa kumsaidia kiongozi wa zamani wa Liberia, Charles Taylor.
  Charles Taylor, yuko The Hague, akikabiliwa na kesi ya kuasaidia waasi wa Sierra Leone(RUF) kufanya unyama mkubwa, kuua watu wakiwemo watoto na pia kupora almasi za nchi hiyo.
    Taylor, anadaiwa kusaidiana sana na waasi hao wa United Revolutionary Front, walioongozwa na marehemu Foday(Poppay) Sankoh, kupora almasi za Sierra Leone, kufyeka watu mikono na miguu kwa mashoka na kisha kuwachukua watoto mateka na kuwatumikisha katika shughuli za kivita.
  Taylor, aliwahi kuwalaumu sana Marekani kuchochea kesi hiyo, akisema kana kwamba, kumbe alipomtumia sana, akatimiza matakwa yao, sasa wanamtupa kama ganda la muwa la juzi, na wanamshitaki The Hague, ili kujiosha katika macho ya Ulimwengu.
 Taylor, na Wazungu wakiwemo Wamarekani, walipigana vita Sierra Leone, wakaiba almasi huko na kuiuza Ulaya,kupitia Zimbabwe, Afrika Kusini n.k ili kukwepa sheria walizoweka, za kutonunua madini kutoka nchi za vita.
   Naam, filamu iitwayo, BLOOD DIAMOND inawaonyesha Wazungu wa Magharibi, wakiwemo Wamarekani, wakichochea vita mjini Freetown, miaka hiyo ya mwishoni mwa 90 na mwanzoni mwa 2000.
   Ni wazi, hao RUF walibadilishana almasi kwa bunduki na Wazungu wengine kutoka Afrika Kusini, Zimbabwe na Ulaya Magharibi.
  Sasa, katuni ya GADO katika The East African, ilileta kichekesho kwamba AU chini ya Kanali Muammar al-Gaddafi, ikiisha mtetea sana al-Bashir wa Sudan asikamatwe, na Robert Gabriel “R.G” Mugabe wa Zimbabwe asiondolewe madarakani kwa shinikizo la Wazungu, sasa ilikua na mkakati wa kutuma ushahidi mzito wa kumtetea Charles Taylor, asipatikane na hatia huko The Hague.
   Kuna maswali kutoka huku kwetu kmba, mbona mahakama hiyo(ICC) inawatia mbaroni Waafrika tu.
  Akina Louis-Moreno Ocampo, hawaoni makosa ya akina George W. Bush kuivamia Irak kinyume cha matakwa ya Umoja wa Mataifa?
 Je, ICC inawaona akina Kanali Muammar Qaddafi tu, na wale sita wa Ocampo, "The Ocampo Six" waliosababisha vifo vya watu 1,400 na wengine 600,000 kukosa makazi,baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya,mwaka 2007?
 Tena, wapo baadhi ya viongozi hapa Afrika, kutokana na uswahiba na Marekani, hawajakamatwa kuhusika na uhalifu wa kivita katika nchi zao, au nchi jirani.
Kwa nini? Nani anachochea vita Congo(DRC)?
 Nani anaiba madini ya Congo kwa kubadilishana madini kwa silaha na waasi?
  Kwa sababu AU inaanza kung’amua njama za Wazungu kuwatumia viongozi wa Bara hili kutumia vita na machafuko ili kupora rasilimali, basi katika katuni hiyo, Muammar al-Gaddafi anawaongoza viongozi wa AU kupiga simu(bila shaka mjini Hague) kusema kwamba, AU ilikuwa na nia ya kutuma ushahidi mpya kabisa wa utetezi kwa Bwana Charles Taylor!
  Nataka kusema kwamba, Rais Barack Obama wa Marekani, akiwa mjini Accra, Ghana Julai 11 alisema Afrika inakuwa duni sana kwa sababu ya rushwa, ufisadi, ukosefu wa demokrasia na utawala bora.
  Nampinga sana Obama kuwalaumu sana mafisadi na viongozi wa Afrika, kuhujumu maendeleo ya watu wao, kana kwamba akina marehemu Jean-Bedel Bokassa, Joseph Mobutu, Sani Abacha na wenzao, hawakusaidiwa sana na Mataifa makubwa ikiwemo Marekani.
   Mobutu, aliiba dola za Marekani milioni sita, akazificha Uswisi.
Fedha hizo zilikuwa nyingi sawa sawa na deni la nje la Zaire wakati huo, Marekani ilikuwepo, lakini haikusema kwamba zirejeshwe ili kusaidia maendeleo ya watu.
   Juzi, iliamuriwa Dola milioni sita za Marekani, ipewe familia ya marehemu Mobutu, kwa sababu serikali ya Joseph Kabila imegwaya kuzidai.
   Sasa, kama akina Abacha, akina Charles Taylor, Mobutu, Bokassa na madikteta wenzao waliitumikia Marekani, kwa mshahara wa mauti kwa watu wao, akina Gaddafi, Taylor,  Fodday Sankoh n.k wanakuaje wakosaji pekee katika kesi ambayo watuhumiwa ni wengi?
 Marekani na Uingereza, wanawatengeneza magaidi kama Osama bin Laden,kisha huwalaumu. Uingereza, ndiko tulikoibiwa dola milioni 40 za rada kanyabwoya, sasa mahakama ya bishara mjini London ikaamuru turejeshewe pesa za ziada, sasa Uingereza haitaki!
 Inataka kutufanyia 'janja ya nyani'.
  Obama, anapowalaumu viongozi wa Afrika kwa rushwa, utawala wa ovyo, ufisadi na ukosefu a demokrasia na maendeleo, anajifanya kiziwi na kipoofu kutoona na kusikia madhara ya ukoloni, na haja ya mataifa haya kushitakia na kutulipa fidia ya madhara ya ukoloni mkongwe na mamboleo.
  Rais Barack Obama, mkewe Michelle ni mzaliwa wa mabaki ya watumwa Waafrika waliopelekwa huko kulima mashamba ya miwa.
 Baba yake, Hussein Obama, alikwenda Marekani kutafuta elimu, kabla ya kukutana na mama wa Kimarekani aliyemzaa Obama.
  Babu yake, Mzee Obama, huko Kenya aliwahi kuwa ‘Boy’ wa Wazungu.
Na alikuwa mwanajeshi wa Jeshi la Kikoloni,la kumlinda Malkia, 'King's African Rifles' ama KAR.
Na hao mabinti  wawili WA Rais Obama, Sasha na Malia, kisha wakweze, Fraser na Marian Robinson, lazima  wanaakisi madhara ya utumwa wa Mtu Mweusi kwa hawa WAZUNGU, ambao hata sasa wana vibaraka Afrika, wanawapa silaha ili kupora maliasili na kugawana nao.
  Makampuni ya mafuta na madini, ndiyo huchangia rushwa na ufisadi kwa mikataba mibovu; na huwapa nguvu kubwa watawala wetu hata kuwarejesha mamlakani, kwa kutumia chaguzi zisizo huru na haki.
   Ken Saro-Wiwa, hakuuawa na Abacha pekee. Makampuni ya mafuta ya Wazungu kama Royal Dutch/Shell na mengine, yalikuwa yakimletea sialaha Abacha, ili akabiliane na wanaharakati.
 Vita vya rasilimali katika Niger Delta, ni ushahidi kwamba makampuni ya Magharibi hulalamikiwa kuondoa maendeleo na utawala wa haki wenye manufaa kwa Mtu Mweusi.
  Obama, alipohutubia bunge mjini Accra,  wakati wa Ziara ya kwanza Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, hakusema kitu kwa makampuni ya mafuta na madini, kukwepa kodi na kulipa mrabaha kidogo serikalini, kitu ambacho ni kuwanyima maendeleo Waafrika.
   Watawala wetu hawawajali wananchi, kwa sababu ni vibaraka wa Marekani, Uingereza, Canada n.k yaani wako radhi wanachi wafe kwa njaa ili madini na mafuta yaende.
   Sasa, lawama za Obama kwa viongozi wetu kwamba wanakatalia madarakani kwa muda mrefu na kuwanyima atu wao maendeleo mbona ni za upande mmoja?
   Tujiulize: Marekani wana makampuni yao ya mafuta Niger Delta, Chevron, Conocco Phillips n.k yanalipa kiasi gani serikalini,Nigeria?
Mbona bado Waogoni na Waijaw wa huko Niger Delta, wanalalamika?
 Au, hapa kwetu kampuni za uchimbaji madini na za utalii, haziogelei katika misamaha ya kodi na kuwahonga vigogo wetu, mafisadi?
   Mbona mikataba imesainiwa Paris?
Mbona Obama hakutangaza mkakati wa serikali yake kuwabana mafisadi wa rada  wa Uingereza, walioshirikiana na wa hapa kwetu?
  Mbona Obama, hajasema majambazi walioko Marekani na Ulaya, wanaowapa rushwa mafisadi wetu ili wapore huku na kuficha kwao dola zetu mabilioni, wakati tunapokufa njaa, na umasikini na kukosa elimu?
  Ni kwa sababu hii, tunadhani Afrika ina haja ya kutazama mipango yetu kwa maslahi yetu, siyo kuburuzwa na akina Obama, ambao kimsingi ni Weusi lakini siyo Waafrika wenzetu.
  Akina Obama wanayo maslahi yao Marekani, na kamwe siyo tena Kogelo, Kisumu, Kenya au popote Afrika.
Hawa, wanatekeleza sera za Marekani tu, na lawama na misaada yao kwetu ni ile ya kutudidimiza kwa riba nzito na wizi wa rasilimali unaofanywa na makampuni yao ya madini na uchimbaji mafuta, utalii n.k
  Kama Obama angekuwa mwenzetu, angetangaza huko Accra kwamba, Afrika iwe na nafasi sawa na mabara mengine, kwa sababu rasilimali zake ni nyingi na muhimu kabisa.
 Na kama Obama ni mwenzetu, ni mwathirika ya madhara ya utumwa na ukoloni mkongwe, lazima akifika Dar es salaam, atueleze, ana mpango gani wa kuondoa utapeli wa madola makubwa kwetu?
Na kwamba, kwanini bara hili tajiri la rasilimali, liwe duni kimaendeleo, kama siyo wizi, utapeli na ufisadi wa Mataifa yao dhidi yetu?
 Na viongozi wetu kwa nini wawe vikaragosi wa Marekani,Uingereza,Ufaransa na washirika wao, halafu wakiwepo akina Gaddafi,wakiwapinga wanapigwa mabomu na kupinduliwa?
   Hivi shina la ufisadi, mfano wa rada ya BAE Systems, au ukwepaji kodi wa makampuni ya madini, ni mafisadi wetu, au wao wenyewe?
 Fisadi anawezaje kuiba na kuficha fedha katika mabenki yao kwa miaka 40 kisha ndipo waseme, ‘ziko huku’ baada ya kufa?
 Hivi, mahakama kama Hague, haina meno kuwafunga jela wale waliowauzia bunduki Taylor na Foday Sankoh?
Je, nani waliwauzia silaha Revolutionary United Front, kama si Mzungu?
 Obama ana habari hata sangara wa Mwanza wanaleta faida maradufu kwa matapeli, wakati sisi ‘tumefulia’ ingawa tunavua na kukokora katika tufani na pepo kali kila siku?
   Nataka kusema kwamba, Obama anajua mizania halisi ya ufisadi, rushwa, utawala a ovyo na ukosefu wa demokrasia. Anajua nani mizizi, nani shina na sisi ni matawi.
 Kesi yangu dhidi yake ni kwamba hata yeye mmoja wa waathirika wa wizi, dhuluma na ukoloni mkongwe na mamboleo, mbona anawalaumu vikaragosi, huku akichelea kuwataja anaofanya Afrika iwe zii?
 Obama, ana kesi ya kujibu, asijitie kua mwendesha mashita dhidi ya mafisadi wetu, alioingia madarakani kwa utajiri haramu uliotokana na mgawo wa rasilimali zetu kati ya wawekezaji mafisadi wazungu na viongozi, kwa kutumia mikataba feki na hewa.
 Obama, ukija Dar wewe na mkeo Michelle, na mabinti zenu wawili, Malia na Sasha, usikose kuja na majawabu sahihi ya maswali niliyokuuliza hapo juu!
 Usijitie Mzungu, ukasahau kwamba Baba yako, Hussein Obama alikwenda Marekani kusoma, akakutana na mama yako, wakaoana, ukazaliwa wewe!
 Babu yako, Mzee Obama aliwahi kuwa 'Boy' wa Mzungu, na akatumikia jeshila Malkia, King's African Rifles(KAR) sasa wewe utasahauje uhalifu wa ukoloni?
 Hata huko Marekani kwenyewe, wamekubagua kwamba wewe Mkenya!
 Ukifika Dar es salaam, wewe,mkeo Michelle, ambaye pia ni Mwafrika wa Kimarekani na binti zako Malia na Sasha, usikose kuzungumza namna ya Mwafrika kuondokana na huu utapeli wa Kizungu,Ukoloni M kongwe na Mamboleo.
 Usijitie Bush,kupeleka vita Libya, wakati wabunge wa Congress wa Chama chako cha Democrat na wale wa Republican wanapinga sana, unyama wako wa kupeleka maangamizi ya raia Tripoli.
 Tafadhali Obama, ukifika Dar, tuzungumze mambo haya kwa kina.
    0786-324 074
  
  

Friday, June 24, 2011

Tanzania haimwitaji Kikwete, Dk. Slaa wala Prof.Lipumba,tunamhitaji rais mseja, tena mjane!



NILIMPIGIA kura Rais Jakaya Kikwete, lakini nimepata mashaka moyoni mwangu!
  Siyo kwamba, Kikwete ni Rais mbaya; la hasha.
Aweza kuzidiwa na Dk. Slaa au Lipumba.
. Nafurahishwa na vitu vingi anavyofanya Rais wetu; lakini ningependa Tanzania iongozwe na Rais mwenye sifa mbadala, ambaye hajawahi kuwepo.
Sifa mbadala hizi, hawezi kuwa nazo Kikwete, Mbowe, Slaa ama Lipumba.

   Ningependa sasa Tanzania iongozwe na Rais mwenye sifa za pekee ili kuondokana na majanga kama haya ya viongozi kuendesha Biashara zao wakiwa Ikulu. 
Naam, namtaka Rais ambaye ana sifa ambazo Kikwete hana! Lipumba na Mbowe,hawana! Slaa hana!

   Nimeorodhesha hapa baadhi ya sifa ninazotaka Rais mpya baada ya Kikwete awe nazo:
Rais asiwe na mke, yaani awe mseja; na awe hivyo kipindi chote cha kuwa  kwake Ikulu yetu ya Magogoni, Dar es salaam !

   Pili, Rais atakayekuja baada ya mhula wa Kikwete kumalizika mwaka 2015, awe yatima.
Rais asiyekuwa na ndugu na jamaa wenye madhambi yanayoigubika nchi kwa kashfa; tena kashfa zenyewe kubwa zinazopamba kurasa za mbele za magazeti.

   Naam. Rais asiye na mke anayepenyeza pua yake katika masuala ya uongozi wa nchi, wakati hakuna aliyempigia kura kufanya hivyo! Nadhani wakumbuka vimbwanga vya Lucy Kibaki,huko Nyayo.
Rais mwenye mke ambaye anafungua makampuni yanayoendesha biashara pengine bila kulipa kodi. 
Mke wa Rais(First Lady) ambaye atapewa leseni na kukopeshwa fedha na mabenki kwa kasi ili kufanya biashara kubwa kubwa, akijidai mjasiliamali.
    Lazima Tanzania yenye watu kama Milioni 43 iwe na Rais mwenye sifa za pekee, kuliko Benjamin William Mkapa, au Jakaya Kikwete. Lipumba, Mbowe au Dk. Slaa.
Mwenye hekima, mtu wa haki, mwenye akili, lakini hana familia, hana jamaa wa kumharibu akili awapo Ikulu pale.Ikulu pasichafuliwe na jamaa na ndugu za rais au mkewe.
   Nimewahi kusikia tetesi za wake za Marais wastaafu, jamaa zao na watoto wao kuitumia vibaya ikulu kufanya biashara. Nakiri, sijawahi kusikia tetesi za Mjane wa Hayati Mwalimu, Mama Maria Nyerere kutumia Ikulu kufanya biashara.
    Tetesi kwamba Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa waliendesha kampuni yao , ANBEN wakiwa Ikulu, zinanivuruga akili. Akina Mama Salma Kikwete nao wana vikampuni vyao,kupitia Ikulu..havitozwi kodi.
Biashara hiyo ya Mkapa na Mama Anna, iwe halali au haramu, si hoja kwangu. 
Lakini, napendekeza Tanzania isiwe na Marais wenye familia zinazowasukuma kufanya biashara mapema wakiwa Ikulu, ili kukimbia umasikini!
    Wapo marais waaminifu na ndugu zao na watoto wao ni waaminifu; hawaitumii vibaya Ikulu.
   Kadhalika, wapo wake wabaya wa marais  wenye wapambe, ndugu na jamaa wanaowashauri vibaya ili kujinufaisha na Ikulu.
Wake, jamaa, wapambe na ndugu hawa nao hujigeuza maofisa wa serikali.
   Nani aliyewachagua kufanya chochote? Nani aliwateua kuwa na sauti hadi kuwafokea mawaziri? Kama ni hivyo, basi tungepewa nafasi ya kuwapigia kura hawa jamaa za marais kabla hawajaingia Ikulu.
   Au, kwa sababu ndugu yao anapoingia Ikulu, wao hujigeuza ‘Mabalozi’ ama ‘Wabunge’ Fulani, basi wangepelekwa kula kiapo mahakamani, kwamba hawataitumia Ikulu kwa maslahi binafsi kipindi chote cha Bwana, Bibi, Mjomba au Shemeji yao, anapokuwa Ikulu.
   Leo, tunashuhudia mbio kali za watoto wa vigogo kutaka kuwania madaraka. Sisemi kwamba watoto wa wakubwa hawana haki ya kuwania madaraka, la hasha! 
Wawe watoto wa wakubwa wenye Visheni; waachane na hadithi za kurithi damu za uchifu wenye falsafa ya kurithishana madaraka.
    Siasa si maneno matupu majukwaani. Ni kuzifanya sera zizae maendeleo ya watu. 
Je, watoto wa vigogo wanaosaka madaraka kwa udi na uvumba, kupitia vyama Tawala, wanayo Visheni hii?
 Wanamiliki mabilioni kwa muda mfupi, wanamiliki mahoteli makubwa ya fahari.
    Au,wanawania madaraka  ‘kutetea’ madhambi ya baba zao pindi wanapomaliza mhula wao, baada ya kushindwa kubadili Katiba ili kurefusha muda wa kusalia madarakani?
   Licha ya wake za marais kudaiwa kufanya biashara ama kufungua vikampuni visivyotozwa kodi wakiwa Ikulu, watoto wao wamekuwa wakiwasaidia baba  au mama zao kutawala kwa mabavu. 
Wamekuwa wakishiriki kuwatesa raia na kukiuka Haki za Binadamu.
    Rais wa zamani wa Liberia, Charles Ghankay Taylor ambaye juzi amesusia mashtaka ya Uhalifu wa kivita  huko The Hague, Uholanzi, mtoto wake, Charles Mc Arthur Emmanuel, au Charles Taylor Jr; ambaye Liberia alifahamika sana kama, Roy Belfast Jr, alitiwa mbaroni Desemba 15 mwaka 2005, akafunguliwa kesi mbili.
   Alitiwa mbaroni huko Miami , Marekani kwa kosa la kuwatesa kinyama waliompinga baba yake, na pia alikuwa na kesi ya kughushi Hati ya kusafiria.
   Ghankay Taylor, ambaye sasa anasusa mashitaka The Hague, alishirikiana na rafikiye, Foday Sankoh, wa kikundi cha RUF kufanya unyama Sierra Leone na kuwauzia waasi hao silaha kwa kubadilishana na almasi.
    Licha ya kuwepo kwa tetesi za wake za marais kuingilia mambo ya serikali, kuwafokea mawaziri na hata kuwatwanga makofi waandishi wa habari hapa Afrika, watoto wa Marais pia wanatuhumiwa kuhusika na kashfa nzito.
    Gideon Moi, mtoto wa Rais wa zamani wa Kenya , Mzee Moi, ana tuhuma za kuhusika katika kashfa anuai za ufisadi nchini humo. 
Wengine, wakiwemo watoto wa wakubwa wa Dunia hii, wanatuhumiwa kubwia unga, kuuza ama kuvuta bangi na kuendesha biashara haramu hata katika Vyuo vikuu, lakini kwa sababu ya upendeleo, woga au kujikomba, vyombo vya Usalama hujikuta vikishindwa kuwachukulia hatua.
Watoto wa akina Bush na Alfred Gore, wabwia unga!
   Hata kama waliua, au hata kama walijeruhi ama kutaharukisha umma, huachiwa mara moja, wasiyaone magereza!
   Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Bi Margaret Thatcher(81), Mark Thatcher(54) lituhumiwa kuendesha biashara haramu na kufanya uhaini.Baadaye alikwenda kupindua serikali ya Guinea ya Ikweta, akatiwa mbaroni huko Sauz.
   Sir Mark Thatcher, mwenye vituko vya “Front Page” katika magazeti, aliwahi kupotea katika Jangwa la Sahara . Alipotea kwa siku kadhaa, wakati akishiriki Mashindano ya Paris-Dakar( Senegal ) Rally, akasababisha Bi Thatcher kuangua kilio hadharani, wakati akiwa Waziri Mkuu!
    Margaret Thatcher, alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza tangu mwaka 1979 hadi 1990.
Lakini mtoto wake huyo aliwahi kutiwa mbaroni na polisi wa Afrika Kusini kwa tuhuma za kuongoza njama za kupindua serikali ya Guinea ya Ikweta.
    Ametiwa mbaroni na vikosi vya usalama mahali pengi Afrika; hata Zimbabwe .
Polisi wa Afrika Kusini walisema, walikuwa na ushahidi wa kutumainiwa, kwamba Mark Thatcher aliwapa fedha waasi wa Guinea ya Ikweta, ili wampindue Brigedia Jenerali Mstaafu, Teodoro Nguema Mbosongo, Rais wa Baraza la Kijeshi la nchi hiyo, aliyedaiwa kuvunja Haki za Binadamu.
   Guinea ya Ikweta ni ya tatu Afrika kwa kuzalisha mafuta kwa wingi.
Pengine, Mark anayetuhumiwa hata kuhusika katika biashara haramu ya silaha, alitaka mafuta ya nchi hiyo. Naam, hao ndiyo watoto wa wakubwa.
   Hata hivyo, wapo watoto wa viongozi waliopata kuwa viongozi wazuri. Waziri Mkuu wa zamani wa India , Indira Ghandhi, alikuwa Binti wa Waziri Mkuu wa Kwanza wa India , Jawaharlal Nehru. Baadaye, Sanjay na Marehemu Rajiv Ghandi nao wakafuata nyayo.
    John Quincy Adams aliyekuwa Rais wa Marekani 1825-1829, alikuwa mtoto wa Rais John Adams aliyetawala Marekani mwaka 1791 hadi 1801.
Adams alikuwa Rais wa pili baada ya George Washington.
    Yupo George W.Bush ambaye baba yake George Walker Albert Bush, alikuwa rais miaka ya 90. Nduguze, kama Jeb Bush ni viongozi; ni wanasiasa maarufu. Hata hivyo, katika orodha, wapo wengi viongozi watoto wa viongozi kama akina Sir Mark Thatcher wahaini, wezi, wauza unga na wahujumu uchumi, wao na wapambe wao, lakini hawakamatwi wala kuhojiwa!
    Wako akina Roy Belfast Jr. wanaoghushi hati mbalimbali na  kufanya biashara haramu na halali, wanaotesa wapinzani wa serikali za baba zao, ambao pia hugeuza Ikulu kuwa ‘mapango’ ya wanyang’anyi ama ‘Mungiki’ wanao ifanyia jamii ugaidi mkubwa.
   Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kuwaonya watu kuiogopa Ikulu.
Ikulu ni mahali Patakatifu. Si mahali pa kufanyia biashara hata ziwe halali na nyeupe kama sufi.
Rais anapoboronga, ama mkewe, jamaa au shemeji zake wanapoendesha magendo ikulu(Doing Business from Ikulu), ndipo harakati za kutafuta warithi huanza!
    Akina Umaru Yar’ Adua wa Nigeria wametafutwa na akina Obasanjo mara nyingi sana kupitia kitu ambacho si Uchaguzi, bali unyafuzi na Uchafuzi Mkuu wa Haki, Demokrasia na Uhuru Afrika!
    Ni kwa sababu hii, ningependekeza wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu, angetazamwa Mgombea ambaye jamaa, wapambe, rafiki, mke na watoto wake hawataiabisha ikulu kwa magendo, vituko, skandali na biashara zisizolipiwa kodi.
 Marehemu Frederick Chiluba alikosa kufungwa jela na Hayati Levy Patrick Mwanawasa, maradhi yalimwokoa kutiwa mangenge kwa kosa la kufanya deal ikulu ya LUSAKA,zambia.
     Kama watoto, wake na wapambe wa Rais wangepelekwa Bungeni kwanza kuthibitishwa na kula viapo mahakamani, basi hofu kama ya Rais Jakaya Kikwete ya kumchunguza mtangulizi wake, isingekuwepo.
Hofu ya kutafuta kubadili katiba isingekuwepo, kama wake, watoto na jamaa wa Rais wangedhibitiwa na Bunge au Mahakama.
    Lakini, pamoja na haya yote, ili kuepuka Marais kufanya Biashara Ikulu, napendekeza Tanzania ingekuwa na Rais Mseja,
lakini asiye mzinzi wa kukwapua wake za raia wake; asiyekaribisha machangudoa Ikulu na kuitia unajisi nchi, rais mjane asiye na familia ya kumtia majaribuni; na yatima ambaye baba, mama na watoto wake ni raia wake.
   0715 324 074
   0754  324 074
congesdaima@yahoo.com

LOVE IS A MODERN SLAVERY


 
JUMAPILI moja niliketi varandani mwa nyumba moja jirani na njia panda.
  Nikaanza kupeleleza maisha ya wapita njia, ambao  hata katika Daladala walikuwa hawaachi kumshutumu  aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Zakia Hamdan Meghji, kwa bajeti yake.
    Mkononi, nilikuwa na kitabu cha riwaya iliyotungwa zaidi ya miaka 50 iliyopita na mwandishi mahiri sana hapa Afrika.
 Nilikuwa nikiisoma mara kwa mara riwaya ile.
Na  nilikumbuka kukirejea kitabu kile, kwa kuwa niliamua kuitumia siku hii  kupumzika.
    Kila aliyekuwa akipita kutoka kona moja au nyingine, nilimwangalia. Wanaume, wanawake na watoto niliwaangalia.
Nilipokosa mahluki wa kuangalia, nikaendelea na ‘hamsini’ zangu; yaani kusoma riwaya yangu, iliyokuwa mkono wa shoto.
     Kila kiumbe kilichopita hapo barabarani, mita chache tu kutoka upenuni mwa nyumba, ngazini mwa milango ya maduka nilipokuwa nimejiputika, nilikiangalia. Nilijikuta nikitoa hukumu yangu moyoni, kulingana na kile ambacho kwa takriban wiki mbili- tatu sasa, jamii ilikuwa ikimlaumu Waziri Meghji  kwa bajeti kandamizi. 
Hata sasa tunamlaumu Waziri Mustafa Mkullo kwa bajeti ya 2011/2012 ambayo twasema, kandamizi!
      Mienendo ya wapiti njia niliyoiona hapo barabarani, ilitosha kuwa ushahidi wa  kuwatoa au kuwatia hatiani, kwa kelele zile zile za Bajeti kandamizi inayofanya maisha kuwa magumu hata siku hizi.
       Naam, Jumapili hiyo siku ya mapumziko, niliwaona vijana wengi wakiwa na rafiki zao wa kike, wakitembea kwa madaha. 
Bila shaka, walikuwa wakienda katika starehe ama tuseme anasa, katika majumba ya starehe, au katika mahoteli ya fahari, ambako huwezi kukanyaga kama huna fedha.
     Wasichana wengi niliowaona walikuwa wamenenepa; walikuwa waking’aa mithili ya mbalamwezi.
Wavulana walioandamana nao, wengi walikuwa wamepauka; nikajua bila shaka kutokana na kazi za harubu za wiki nzima juani.
 Wengine wakata nyasi, wengine machinga, wasukuma mkokoteni, wengine wajasiliamali!
       Unajua, mwanaume sharti kusaka noti juani, ili mkono uende kinywani.
    Akina dada wale, wengi walivalia suruali ‘Jeans’ za kubana sana .
 Wengine walivalia vivazi vyao vya siku hizi, vinavyoacha sehemu kubwa ya mwili wao kuwa nje; vilikuwa vya rangi anuwai, huku vikiandamana na vijishati- utadhani vya wadogo zao-kumbe vilikuwa vyao wenyewe.
    Walipokuwa wakitembea, naam  kupita njia ile nilipokuwa, walikuwa wakinesa mithili ya twiga wenye himila changa; huku minofu ya kiwiliwili,  pengine sehemu za nyuma za makalio, zikitetema utadhani hatimaye zingedondoka!
     Kitu cha ajabu nilichobaini katika upelelezi wangu, ni kwamba akina kaka wengi(kasoro wachache) walioandamana na akina dada wale Jumapili hiyo, mbali na kusinyaa kwa jua la hari, walivalia vibaya, masurupwenye makubwa yenye kuwapwaya.
   Naam; kwa kifupi, ni kisa cha wavulana vibubutu ama malofa, waliojitia kutoa ‘ofa’ kwa mabinti warembo waliotingisha minofu makalioni, kwa mwendo wa madaha mithili ya twiga mwenye himila changa.
   Nikatoa hukumu yangu kwamba, hawa walikuwa wavulana “Genetic Modified” kwa kifupi, GMO waliokuwa wameumbwa kuwastarehesha wengine, huku wao wakiungua mithili ya mshumaa!
     Mshumaa una upendo wa  kijinga (nitaeleza baadaye aina tatu za upendo) wa kuwaangaza wengine, wakati ukiteketea.
   .Nikajiuliza: Kwanini wao wakonde na kuonekana mifupa mitupu kwenye masurupwenye,wakati wasichana wao wamenona kwa pesa zao walizotafuta mchana wa hari?
   Wasichana wale walikuwa na simu za mkononi za gharama kubwa, huku wakinukia uturi wa thamani.
Kwa vyovyote, wavulana wao walinuka jasho kufuatia kazi za harubu za kuchumia juani!
Wengine hawakuwa na simu.Wamehonga fedha yoote!Watakuwaje na simu zao wenyewe? Ubwege tu!!
    Nika waona pia, akina baba-watu wazima-bila shaka wenye familia zao na watoto wao, wakitoka mmoja baada ya mwingine katika makazi yao .
 Jioni hakuna aliyeandamana na mke au watoto. Walikuwa peke yao , wakibofya-bofya simu zao za mikononi.
     “Haloo? Sasa tuonane pale…tulipozungumza jana n’takusubiri…Ok? Tchao!!
   ”Nikajua walizungumza juu ya miadi yao , bila shaka na hawara zao wa nje. Mimi mwenyewe, siku moja tu kabla ya Jumapili hiyo, mama mmoja mtu wa makamo, aliniambia nimpigie simu, ili tukutane Hoteli yoyote ya fahari, ili tuzungumze!
Uso ukanisawajika.
    Nikaghairi; na badala yake nikaja hapo ngazini, njia panda kufanya udakuzi huu. Nilijua akina dada na akina mama wa siku hizi makali ya Bajeti(ingawa imetolewa na mwanamke mwenzao) wao hawayajui
    Nikaogopa kujitoa mhanga mithili ya mshumaa, badala yake nikaja kusoma kitabu changu hapa njia panda, na kuwapeleleza Watanzania hawa na ahadi yao ya Maisha bora! 
Abadan sikuogopa kuitwa mtu mgumu, bahiri, mkono wa birika na akina dada hawa wenye hadaa mithili ya dagaa.
    Simu bado zinazuzua watu. Badala ya kufanya shughuli za maendeleo, ni anasa.
Hawa, nikawaona wanaingiza vocha za maelfu na kuendelea kubofya-bofya, huku wakisema, “Wala haina shida, hata mkija watatu; wanne mtakunywa, mtakula, mtastarehe vya kutosha; wala hakuna wasiwasi!”
    Nikajiuliza: Na familia tunazifanyia haya?
Hawaa akinaa "Mr. Bingo uchwara" akina Bill Gates wa kuchonga, wana ubavu?
Au, ni unafiki huu wa kujiteketeza mithili ya mishumaa?
Nikakumbuka maneno katika Biblia, kwamba, ‘ Kama kondoo waongozavyo machinjoni…”
    Nikakumbuka miongo mitatu iliyopita, nilipokuwa nikichunga mifugo ya Babu yangu, wakati mwingine nililazimika kuwapeleka ng’ombe na mbuzi malishoni bila kutia chochote kinywani.
 Matokeo yake, ng’ombe wakanenepa, mimi nikakonda!
 Ilikuwa kabla ya kubaini kuwa ulikuwa utumwa…naam utumwa wa hiari.
    Yaani, mtu huacha kununua chakula na mahitaji mengine ya lazima ili ajaze fedha kwenye simu, akawakoge wenzie baa!
Simu zimeingia nchini siku si nyingi.
 Wengine ‘ndundundu’ ujira wa mtwangaji, ndio kwanza wamezinunua juzi, vidole vinawawasha kubofyabofya.
    Mwaka 2005 Benki ya Dunia(WB) ilisema kulikuwa na simu nne tu kwa kila Watanzania 1,000.WB ikaongeza kwamba Watanzania watano tu kati ya 1,000 ndio waliomudu kununua magazeti yote ya kila siku ili kujisomea.
Watu 293 tu kati ya 1,000 ndio waliokuwa na redio, ambazo wengi waliishia kusikiliza ‘bongo flavour’ tu bila kusikiliza habari.
   Wenye televisheni walikuwa 23 tu kati ya 1,000; nao waliishia kutazama ‘jumba la dhahabu’ kwa jirani, huku pesa zao wakiteketeza kunenepesha wengine mitaani
   Waliokuwa na kompyuta zao walikuwa hawafiki wanne kwa kila Watanzania 1,000. Kati ya watu 10,000 waliokuwa na kopyuta zao zenye intanet walikuwa 0.3; wengine hawa hata leo hawajui internet ni mdudu gani?
    Kati ya Watanzania milioni 35 wanaotumia internet ni 25,000 wengi wao vijana wanaotafuta kutazama ngono na mapaja ya machangudoa wa ughaibuni.
 Swala la elimu na mawasiliano Tanzania, linawekwa kando; starehe na anasa hupewa kipaumbele.
    Baadhi ya wanawake wa kileo akili zao ni ‘Genetic Modified’ (GMO) kwa ajili ya ofa za maraha,anasa na starehe,wanawalazimisha akina baba wa watu(wenye familia zao) kuwapa ‘offer’ katika mahoteli ya gharama, wakati uwezo na mishahara yao ni kibubutu, mkia wa pimbi!
   Maskini hawa, wanajiingiza kichwangomba(kichwa chini miguu juu), matokeo ni kashfa za kuacha simu baa na kuchojolewa viatu au mashati!
 Huku mitaani hawaachi kumlaumu Mama Meghji, kuwa bajeti yake ilikuwa ya kikatili! Je, walitaka bajeti hiyo iwe ‘rafiki’ hata kwa machakaramu wa vimwana  katika kashfa zao za akina Monicagate?!
    Bajeti ngumu maana yake ni kujifunza kujitegemea na kutumia fedha kwa mambo ya maana, si starehe na anasa! Hapo mpo? Wewe mbango; pesa huna, mambo makubwa ya nini?
Angalia utajipeleka ‘machinjoni’mithili ya kondoo wa sadaka! Karo ya shule hujalipa, kodi ya nyumba hujalipa, maziwa ya mtoto,
     Ankara za maji, umeme, fedha za tuisheni n.k huwezi kulipa, badala yake unashughulikia ofa za akina mama shamla, mama uhondo, mama tabaradi, mama tambarare, huku huna kitu; maisha kichwangomba; halafu unahoji bajeti ya Zakia Meghji!
    Unahoji ahadi ya rais ya maisha bora kwa kila Mtanzania kwa stahili hii?
    Starehe kwako surupwenye; wavaao wana mwili, wewe ufyefye(dhaifu) mbavu tupu, utapwaya
!Usijifanye 'tupatupa', ukatapanya ulichovuna udobini kwa uroho na ujapongo kwa akina mama shamla(hawakauki ngomani, utaumia!
Maisha bora hayaji kwa kuvaa masurupwenye ya akina mama tamaa, mama anasa!
    Mshumaa hujiteteteza wenyewe kuwaangaza waungwana; wewe mshumaa? Mshumaa uliowashwa msituni(Candle in The Jungle) unawaka, kisha utazima kwa upepo wa kisulisuli, pasipokumwangaza mtu.
 Usijitie kuwasha mshumaa msituni; usijipendekeze.
   Mshumaa usijitie ukwasi. Usijidai kuwa na upendo wa Agape.
Kuna aina tatu za upendo:
 Eros ama Erao ni tamaa. Akina dada viduhushi, watajidai kukupenda ukiwa na chochote kitu; kikiisha hakuna tena mapenzi.
 Akina dada nao watapendwa kwa sababu ya makalio makubwa, hips, dodo mithili ya miba ya katani, vitovu mbonyeo n.k lakini vikitoweka, hakuna mapenzi- haya aslani si mahaba ni ashiki, tutumko, tamaa na hadaa tu.
   Kuna Philia. Baba atampenda mama kwa sababu anamhitaji kutunza familia. Na mama kadhalika anamhitaji baba kwa sababu zilezile za kibinadamu. Upendo huu pia hufika muda ukatoweka.
 Upo upendo wa mshumaa ‘agape’ ni upendo wa kujitoa mhanga.Wanaouweza ni ‘watumwa’ wa hiari.
   Miaka 2400 iliyopita Mgiriki mmoja aitwaye Euripides, aliandika kwamba, Admetus Mfalme wa Thessaly aliugua sana akakaribia kufa.
Miungu ilipoulizwa sababu ya maradhi ya Mfalme, ikasema, asipokufa mtu mwingine badala yake, Mfalme asingepona!
   Basi,baba yake akaulizwa kama angeweza kufa badala ya mwanae, akakataa. Mamaye akasema, ‘kweli Admetus ni Mfalme tena ni mzuri, lakini kamwe asingeweza kumfia. Wakaulizwa rafiki zake wote, hakuna aliyekubali kufa kwa ajili ya Admetus.
    Mwishoni, kidosho mmoja mpenzi wake aliyeitwa, Alcestis  akasema,  yeye alikuwa tayari kufa kwa ajili ya  Admetus!
 Alipokufa, Mfalme akapona maradhi yake, lakini hakurudi kuwathamini wazazi, rafiki wala ndugu kwa kuwa walikuwa na upendo wa maneno bila vitendo, isipokuwa marehemu mpenzi wake, Alcestis.
     Tena Biblia inaupinga upendo huu wa kidosho huyo Alcestis, kwa kusema ‘Yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki. Bali Kristo Yesu alitufia tulipokuwa tungali wenye dhambi.
Yesu aliwafia majambazi na magaidi; ndiyo agape!
 
    Je,Vibubutu wenye ujira ndundundu, wanapojitia kuwastarehesha akina mama shangwe huku nyumbani kwao watoto wakikosa lepe kwa kung’atwa mbu, ndiyo agape yenyewe, au kichwangomba waliogeuzwa vichwa chini-miguu juu kwa huba la tashtiti; huba la kitapeli lililojaa ujapongo; yaani uroho na kigeugeu?!
   Naam, kama huu ndio upendo, basi ni utumwa kuliko wa mshumaa. Mbona hata Yesu aliwaasa wanafunzi wake kuanzia wokovu nyumbani kwao (Yerusalem)? Kwanini muwe mifupa mitupu kuwanenepesha wengine, wakati kwenu midabwada?
    Kumbe watumwa wangalipo?
  0754 324 074
   0786 324 074 
congesdaima@yahoo.com
   
    

Friday, June 17, 2011

'NO SEX STRIKE' NI HATARI

     



SITAKI kujiingiza katika upande wowote wa sakata la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(Utawala Bora)Sofia Simba,kudaiwa kuwataka wanawake wa Chama cha Mapinduzi(CCM),kuwashushua waume wao walioko upinzani,kwa kuwanyima unyumba!

Sofia Mnyambi Simba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi(UWT)Taifa,siyo mtu wa kwanza duniani kuhamasisha kampeni kali ya kuwanyima akina baba unyumba!

 Kampeni hiyo kali, “No Sex Campaign” ya akina mama dhidi ya akina baba walio katika ndoa,imepata kutumiwa mara nyingi,ili kufanya mashinikizo.

Huu ni mgomo tata ambao,wanawake wote(wakiwemo wasichana) wakiutekeleza kwa kauli kauli moja,hakuna wa kuuzima hata kwa kutumia virungu vya polisi  hata wa General Service Unit(GSU) huko Kenya na FFU hapa nyumbani.

  Ni aina ya migomo inayodaiwa salama(Nonviolence resistance) sawa sawa na ule wa Mahtama Gandhi,wa kugomea chakula huko India zama za kudai uhuru mikononi mwa wakiloni wa Kiingereza.

Hata hivyo, mgomo na maandamano ya kunyimana haki za ndoa,siyo salama kama watu wanavyodhani.

 Migomo ya kunyimana haki za ndoa haijawai kuleta suluhu katika vita na matatizo duniani, haijawai kuleta amani ya kweli. Migomo sampuli hii, haitanzui matatizo ya kijamii; bali huanzisha matatizo mapya na yaliyojisokota zaidi.

 Sipendi kabisa kuamini kuwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Utawala Bora,Sofia Simba eti amewahi wakati wowote na mahali popote kuwahamasisha akina mama wa Chama tawala(CCM)kuwanyima unyumba wanaume wao walioko kambi ya upinzani.

 Sipendi na sitaki kabisa,kukubali kwamba Sofia Simba na Chama chake cha Mapinduzi(CCM)wanaweza kutumia ‘silaha’hiyo ya “Sex Strike” kuwashinikiza waume wao walioko kambi ya upinzani,wasalimu amri na kukubali kuipigia kura CCM,Oktoba 31.

Siamini,kwamba Sofia Simba anaweza kutumia “bunduki kali’ namna hii ya wanawake wa CCM kuwanyima unyumba waume wao wa ndoa,kitu ambacho ni haki yao ya ndoa. Haki za msingi!!

Tendo la ndoa,.ni haki ya msingi ya wanandoa,kulingana na katiba ya nchi na sheria za nchi yetu.

 Kadhalika, ni haki ya msingi katka sheria za Mungu.Tazama Biblia takatifu katika kitabu cha 1Wakoritho 7:3-6.

 Vitabu vitakatifu vya dini, vinapiga marufuku wanandoa kunyimana unyumba, ama kufanyiana mgomo wowote hata kama ni mushinikiza waume wao waache vita na misimamo ya hatari.

 Isipokuwa, imeandikwa kama wote waume na wanawake, “wakikubaliana”. Yaani, kama watapatana-tena kwa maombi makali,ili Shetani asije akawajaribu.

 Ni kwa sababi hii tu, Biblia inasema, mke hana amri juu ya mwili wake(viungo vyake vya uzazi) isipokuwa mumewe, na mume hana amri juu ya mwili wake isipokuwa mkewe.

Kwa Bwana mkubwa,Mungu, “No Sex Campaign” IMEPIGWA MARUFUKU.

Vitabu vitakatifu vimepiga marufuku migomo sampuli hiyo yenye kuwatenganisha wanandoa japo kwa usiku mmoja. Sembuse kuanzia sasa hadi baada ya Oktoba 31?

 Amani gani, baba kukosa haki ya ndoa mwezi huu hadi Oktoba 31?

 Demokrasia na uhuru upi, baba kunyimwa unyumba na mkewe wa ndoa. Kisa…uanachama wa CUF,TLP,NCCR-Mageuzi,DP sijui CCJ n.k?

Huu,ndiyo mwanzo wa akina baba kuhamia kambi ya fisi kusaka ubembelezi wa vyangudoa!

 Hatimaye, ni kusomba Virusi vya Ukimwi(VVU) na kujileta majumbani pindi uchaguzi mkuu ukipita Oktoba na mgomo wa “No Sex” ukimalizika salama bila salama.

Nataka kusema kwamba, migomo kama hii ya kunyimana unyumba wenzi wa ndoa siyo salama na haiku katika Haki za Binadamu zilizohasisiwa Desemba 10, mwaka 1948.

 “Sex Strike” huzua migogoro,fujo na vita kali vyumbani hasa nyakati za usiku.

 Kunapopambazuka, ndoa hua zimesambaratika, na ni mwanzo wa mwisho wa taifa kuyumba na kufa, kwa sababu familia nyingi huwa zimevunjika.

Ni mwanzo wa watoto kuishi maisha hatarishi bila malezi,bila wazazi walioungana katika ndoa.

Ni mwanzo wa watoto wanaoishi maisha hatarishi zaidi mitaani,ni janga lisilosemeka, kwa sababu pia akina mama wengi watapatwa majanga.

  Sipendi mimi kuamini umbeya wa watu kwamba Sofia Simba, Waziri wa serikali na Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake wa CCM, anaweza kuhamasisha “Vita kali” miongoni mwa wanaume na wanawake kunyimana unyumba,hadi ndoa nyingi zivunjike vipande, na akina baba wenye misuli wawavunje bure wake zao wazuri mataya,kwa sababu ya kutekeleza mgomo wa kunyimana unyumba!

Mwezi juni mwaka jana,vikundi10 vya wanawake wa Kenya katika mashirika ya hiari,maarufu kama G-10 vilitangaza mgomo kama huo wa kuwanyima akina baba unyumba.

Gender 10,walitangaza mgomo huo wa ‘No Sex’ kwa akina baba katika ndoa zao,kama mgogoro wa kisiasa Kenya ungeendelea kati ya Rais Emilio Mwai Kibaki na Waziri Mkuu, Raila Odinga.

Mgogoro huo,ulizuka baada ya uchaguzi mkuu wa Desemba 2007, watu1.400 wakafa vitani,mali zikaharibiwa,akina mama wakabakwa, na watu 650,000 wakakosa makazi, wengine wakakimbilia uhamishoni.

Kufuatia hali hiyo, akina mama wa Kenya(G-10) wakatangaza mgomo mkali wa ‘No Sex’ kwa akina baba, hadi watakapoacha ubabe wao na kusitisha mapigano.

Nakwambia,mgomo huo uliungwa mkono na mke wa Rais,Lucy Kibaki na Yule wa Waziri Mkuu,mama Ida Odinga.

 Sijaelewa sakata hilo la ‘No Sex’ nchini Kenya liliishaje na kama hakuna watu walioumizana vyumbani.

Sijafahamu kwa yakini, kama ile serikali ya Joint Operations Command(JOC) ya Rais Kibaki na Waziri Mkuu,Raila Odinga kama ilikuja kufuatia shinikizo la ‘No Sex Campaign’ kwa kutumia mgomo huo,, Sex Strike.

 Wanawake wote na wasichana kuwanyima wanaume tendo la ndoa(mpaka kieleweke) uliwahi kutangazwa zamani,katika karne ya 5BC na mwanamke wa Kigiriki.

Lysistrasta, aliwahamasisha akina mama wa Uyunani(Ugiriki ya wakati huo) kuwanyima waume wao unyumba hadi watakapokubali kusalim amri na kukaa pamoja katika meza ili kuacha vita-cease fire. Ilikuwa katika karne ya 5 BC, Mwanamke huyo, Lysistrasta, akahamasisha wanawake wa Ugiriki,naam Uyunani ya zama hizo, waache vita ili kuleta amani katika nchi.

 Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31 hapa Tanzania siyo vita na vurugu kama zilizotokea Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa Desemba 2007.

 Na siyo kama vita baina ya Wayunani katika miaka ya 450 BC. Uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 watu wanatakiwa kupiga kura bila kushinikizwa na mtu ama kikundi cha wanaume na wanawake.

 Mtu anaposhinikizwa kukichagua chama ama mgombea Fulani kwa kampeni kama ,’No Sex’ siyo demokrasia, na ni mwanzo wa mwisho wa kukosekana kaya na familia.

Watu wakianza kunyimana unyumba katika ndoa ndiyo mwanzo wa kuuana vyumbani.

 Kama wadhani mchezo, wewe tangaza kwamba sasa Baba Rhobi na Mama Rhobi sasa wataanza kunyimana unyumba,ili wote wampigie kura mgombea wa chama kimoja!

Andaeni hospitali nyingi za kuokoa majeruhi katika hii vita mpya ya kimya vyumba vya kulala!

 Kwa sababu hiyo, “No Sex Campaign” Ni mgomo wa kimya kimya vyumbani,lakini madhara yake yatafika nje ya mipaka ya nchi; ni hatari na ni baa na balaa!

 Mwandishi wa safu hii anapatkana kwa barua pepe

:congesdaima@yahoo.COM
  0754 324074

WELCOME IN MWANZA,THE ROCKY CITY

LANGO Kuu la kuingilia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, iko takriban kilomita 100 tu kutoka hapa jijini Mwanza.

Watalii kutoka mataifa mbalimbali wanaotaka kutembelea Mbuga hizo zilizo miongoni mwa maajabu ya Dunia,yawapasa kutafuta lilipo jiji la Mwanza, ili wapate mahali pa kuanzaia.
Licha ya kuwa kitovu cha nchi nyingi za Maziwa Makuu:Rwanda,Burundi,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Kenya na Uganda, Mwanza jiji lililopo  kandoni mwa Ziwa Victoria,lina vyanzo tele vinavyoweza kuwaongezea wananchi kipato pamoja na serikali.

Jiji hili liko Kusini mwa fukwe za Ziwa hili kuu kuliko yote Afrika; ziwa ambalo ni miongoni mwa maziwa machache sana Ulimwenguni lenye maji baridi; na linalotoa sangara wanaouzwa katika masoko takriban yote ya Umoja wa Ulaya.

Mwaka 1892 ndipo Mwanza ulipoanzishwa na Mjerumani, EAMIN PASHA ili kuwa Makao Makuu ya kiutawala, ya maeneo yote ya Ukanda wa Ziwa, pia kuwa kituo kikuu cha Biashara kilichotumika kusafirisha nchi za nje zao la pamba.

Mwaka 1978 Mwanza ikawa na hadhi ya Manispaa; kabla ya kuwa Jiji kamili mwaka 2000. Lilikuwa jiji la pili nyuma ya Dar es salaam.

Asilimia 32 ya wakazi takriban milioni moja wa jiji hili wameajiriwa, wakati 27 hawana ajira. Wengi wameajiriwaq sekta binafsi, waliobaki hujishighulisha katika kilimo, biashara ndogo ukiwemo umachinga, na uvuvi mdogo unaowaingizia kipato cha wastani wa Dola za Marekani 21(shilingi takriban 30,000 tu kwa mwezi.

Mwanza kuna viwanda nane vinavyosindika sangara wanaouzwa sana Ulaya na kuliingizia Taifa mabilioni ya fedha. Pia kuna kuna viwanda sita vya kusindika pamba na kuzalisha mafuta ya kupikia. Kuna kiwanda cha Bia(Tanzania Breweris Limited), kiwanda cha vinywaji baridi cha Coca Cola, bekari takriban 100 za mikate, mashine za kusagia nafaka, viwanda vya mbao, kiwanda cha nguo cha Mwatex, magereji, viwanda vya bidhaa za plastiki, magodoro,sabuni vya chakula cha mifugo n.k.

Kuna mahoteli na vitega uchumi vingi. Miongoni mwa vitega uchumi vipya katika jiji hili, ni pamoja na Nyumba 280 za Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma, PPF, zilizokwisha jengwa katika eneo la Kiseke, ambazo zinapangishwa kwa wakazi wa jiji ili kuwapunguzia adha ya makazi.

Nyumba hizo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa nyumba 1,149 katika maeneo anuai ya jiji, ili kuliingizia Shirika hilo mabilioni ya fedha, licha ya kuwaondolea wananchi adha ya upungufu wa makazi.

Pia PPF wamejenga jengo la kitega uchumi, maarufu kama PPF Plaza, katika Barabara ya Kenyatta, kwa gharama ya sh. Bilioni 10.6; .Jengo hilo la ghorofa tisa limekamilika,  li na maofisi,maegesho ya magari, migahawa mikubwa yenye hadhi ya Kimataifa, kumbi za mikutano ya Kimataifa, maduka makubwa; na linakadiriwa kuingiza shilingi Trilioni 1.1 kila  mwaka.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, NSSF, nao wamejenga jengo la kitega Uchumi katika barabara hiyo ya Kenyatta, na tayari wamepewa viwanja 1000 ili kujenga nyumba za makazi, katika eneo la Nyamuhongolo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro, anasema lengo ni kulifanya jiji hili kuwa kitovu cha biashara na utalii katika nchi za Maziwa makuu. Rais Jakaya Kikwete, alisema alipokuwa akizindua akifungua nyumba za makazi za Kiseke, kwamba katika kipindi cha utawala wake ataiacha Mwanza ikiwa California ya Tanzania katika sekta ya uwekezaji.

Hadi mwishoni mwa mwaka 2000 pato la mkoa mzima lilikuwa Shilingi Bilioni
643.595.
.Ongezeko la kipato katika eneo zima hili hutokana na ongezeko la vitega uchumi vilivyokwisha tajwa, vinavyotokana na sekta za samaki na madini.

Kilimo kimegawanyika katika mafungu mawili:
Kilimo cha mazao ya Biashara na chakula. Pamba ndilo zao linaloongoza kwa kuingiza kipato. Mwaka 2000 mkoa mzima wa Mwanza, kilimo peke yake kilichangia sh.308.925 Bilioni katika pato la mkoa. Hii ni sawa na asilimia 48 ya pato lote kwa mwaka.

Misitu,samaki, madini na Utalii kwa pamoja viliiuingizia mkoa wa Mwanza sh.199.515 Bilioni mwaka huo wa 2000
.Pato hilo ni sawa na asilimia31 ya pato lote la mkoa. Madini na samaki ndizo sekta zinazokua haraka na kuungizia mkoa kipato kikubwa sana. Mgodi wa Dhahabu wa Geita uko maili chache toka Mwanza mjini.

Sekta ya Biashara na Viwanda, kwa pamoja mwaka 2003 zilichangia sh. Bilioni 115.847 katika pato la mkoa.
Hili pato la sekta za Viwanda na Biashara lilikuwa sawa na asilimia 18 katika pato zima kwa mwaka katika mkoa wa Mwanza.

Sekta zingine zinazojumuisha na Utalii, ziliuingizia mkoa huu sh. Bilioni 19.308 katika mwaka huo, sawa na asilimia 3 ya pato lote la mkoa mwaka 2003.

Tangu mwaka 1995 pato la mkoa mzima wa Mwanza lilikuwa likiongezeka kwa asilimia 215. Yaani kutoka sh. Bilioni 203.939 mwaka huo wa 1995 hadi kufika sh. Bilioni 643.595 mwaka 2000.

Mbali na kipato hicho, bado wakazi wa eneo zima hili wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa miundombinu, hospitali,chakula, shule,ili kuwaongezea wananchi mahitaji ya lazima, huduma za jamii,ajira na maisha bora aliyoahidi Rais Jakaya Kikwete.

Mbali na kipato hiki, Mwanza ingali "Imelala" kufuatia kuwa na fursa tele na vivutio vingi vya utalii.Utalii katika Tanzania ni sekta ya pili kuliingizia Taifa kipato, nyuma ya kilimo. Huchangia asilimia 16.5 ya Pato la Jumla la Taifa(GDP); lakini Mwanza haijavuna vya kutosha kutokana na utalii.
 Ni kwa sababu hii jiji hili lingali linahitaji uwekezaji katika fursa tele katika nyanja tofauti za madini,utalii na kilimo.

Mwanza kuna visiwa vya Rubondo,maarufu kwa sokwe na jamii za jani,kuna Kisiwa cha Saa Nane,, eneo la Kijereshi ambalo ni lango kuu la kuingilia Serengeti.
 Kuna Makumbusho ya Bujora,mahali watumwa walipohifadhiwa kabla ya kusafirishwa hadi Bandari ya Zanzibar, tayari kuuzwa Ulaya na Arabuni.

Kuna miamba yam awe ya Bismark, mapango ya Hendbezyo, katika kisiwa cha Ukerewe, ambayo wenyeji walijificha wakati wa vita vya kikabila. Kuna milima ya Isamilo, ambako John Speke alisimama, alipokuwa akikagua Ziwa Nyanza(kabla ya kuitwa Victoria), kwa heshima ya Malkia wa Uingereza.

Hili ziwa ndilo chanzo cha Mto Nile unaosafiri kilomita zaidi ya 6,000 hadi Misri. Kuna mawe yanayocheza dansi, katika kisiwa cha Ukara, kuna mti wa ajabu uliokatwa, kesho yake ukaota! Upo mti mwingine, ukidondosha majani katika maji ya ziwa Victoria, basi majani hayo hugeuka mamba!

Magu kuna kaburi la Mpelelezi, Henry Stanley, Igoma kuna makaburi ya M.V. Bukoba.
Upo mti uliotumiwa na Wajerumani kunyongea Wazalendo, katika makutano ya Barabara za Makongoro, Kenyatta na Nyerere, jirani na jengo la CCM,Mkoa.
 Mti huu siku hizi umekatwa,lakini kisiki kingalipo.
 Hivi vyote ni vivutio vya utalii vinavyoweza kuingiza kipato kwa watu na kodi serikalini.

Mwanza ikitumia fursa zote kama mahoteli ya kisasa(yatakapojengwa kwa ubia na wawekezaji)uwanja mpya wa ndege wa kimataifa,maduka, kumbi za starehe n.k zitapunguza Umasikini na Kuongeza Kipatp(MKUKUTA).

Kwa kuwa mji huu unafikiwa na reli, kuna barabara nzuri ya rami kati yake na Nairobi,Arusha hadi Dar es salaam. Kuna uwanja wa ndege unaopaswa kupanuliwa hadi kuwa na hadhi ya kimataifa,kwa kuwa unatumiwa hata na ndege za mashirika ya njemkama Kenya Airways.
Miaka michache ijayo barabara iendayo Kampala, Uganda, Rwanda na DR-Congo itajengwa, bandari yake inayotumiwa na meli za abiria na mizigo hadi Kisumu na Jinja, itapanuliwa, na Mwanza utakuwa kituo kikuu cha Biashara katika nchi zote za Kenya,Uganda,Tanzania, Burundi, Rwanda na Congo.

Hadi sasa uwanja wake wa ndege ndio unasafirisha madini kama dhahabu, na pia sangara hadi Ulaya na Marekani.Samaki wa Mwanza husafirishwa kwa barabara hadi Congo, Afrika Kusini, Musumbiji, Kenya na Malawi.

Mpaka mwaka 2003 Uwanja wa ndege wa Mwanza, ulisafirisha wageni wa Kimataifa 5,344; wasafiri wa ndani 125,499 na jumla ya tani za mizigo 13,426.Hiki ni kiwango kidogo kulingana na hali halisi ya uwanja huo ulioko kandoni mwa sangara migodi ya dhahabu na almasi, pamba na kahawa.
mtanzania
Huu ni uwanja wa kwanza nchini ndege ilipotekwa na watu walioitwa wahuni miaka ya 80 hadi ulaya! Ni uwanja unaotarajiwa kubadili maisha ya wakazi wa eneo zima hili katika enzi hizi za utandawazi.

 0786 324 074

Wednesday, June 15, 2011

I don't love u but your money first!


 
   WANAWAKE wengi(kasoro mke wangu , mkeo na wengine wachache)hutafuta mwanaume mwenye pesa ili waolewe naye.
Lengo lao ni kufikia pesa.
Wanakwenda hata kwa sangoma,ili awasaidie kupata mwanaume atakayewalipia Ankara zao za umeme,maji na kila starehe.
Mwanaume atakayewanunulia vocha za simu, atakayewanunulia vivazi vya gharama kubwa, magari ya kutembelea kama BMW, Mercedes-Benz, n.k
 Akina dada wa kileo, wako mbioni kuwasaka mibuzi na marafiki wenye uwezo wa kifedha. Watakaowapeleka “Out” mahali pa starehe pa gharama, kisha kuwanunulia zawadi za thamani kubwa, mithili ya Rais  wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy kwa kidosho chake kipya, Carla Bruni.
Naam, wasomi na warembo kumshinda Malkia Cleopatra wa Misri, wanawasaka kwa udi na uvumba, wachumba watakaomudu kuwanunulia kila wakitakacho, ili waonekane, “Material Girls” kama Naomi Campbell  ama Madonna!
Akina mama na wasichana wa siku hizi, huwapenda wanaume wenye fedha nyingi kama David Bekham, watakaomudu kuwalipia ‘Bill’ zao.
 Naam, watakaoonesha penzi  kwa vitendo; na aslani siyo wenye mikono ya birika na pesa za mawazo.
Hawa warembo wa siku hizi, hawapendi kupewa ahadi utadhani wagombea kwa wapigakura wao. Siku hizi, hapendwi mtu,bali pesa zake!
Maadili huwaonya wasichana kuacha kuuza utu wao na miili yao kwa pesa, kwa mapenzi yanayodumu kitambo.
 Mahaba ya pesa huja upesi kama umande,leo na hutoweka mapema kesho(easy come,easy go) hata kama mtu anazo pesa,lakini kashindwa kuzimwaga.
Akina ‘Chuma Ulete,hasara si ajabu’ndiyo wenye turufu ya ushindi katika mnada huu wa mahaba. Wale wanaoamini kwamba mapenzi ya dhati hayana mzizi kukesha baa au sehemu za starehe, hawana chao.
Kila msichana siku hizi huwaza kuolewa na mwanamume mwenye ukwasi-mwenye pesa. Hata watoto wanawaza kuzaliwa na wenye pesa-kuangukia penye pesa.
Kila mtu anawaza huba la fedha;naam huba la tashtiti.
Akina dada wasomi wanafikiri kuolewa na wanaume matajiri,wenye pesa kama ‘Becks’ wanawaza kufikia pesa.
Wanafikiri kufunga ndoa za gharama na matajiri wenye fedha chekwa chekwa,potelea mbali ndoa zenyewe ziwe “Ndoa ndoano” mradi wamefaidi kwa kitambo.
 Naam, ndao za fahari, maisha ya fahari,kula kunywa na kuvaa kwa fahari na utukufu wa utajiri.
Kutohangaika-hangaika,kufua-fua manguo,kuosha vyombo kila mara,bali kujilaza-laza sofani muda wote huku ukitazama televisheni kubwa mbele zako, na jioni kujimwaga kula maraha katika kumbi za sterehe na burudani.
 Nani ataka kuolewa ili kupika-pika,kufua-fua,kupiga deki nyumba siku hizi utadhani ‘House Girl’?
Badala ya kufaidi ndoa yenye amani na fedha chekwaa?
 Akina dada wanatamani sana maisha matamu,ambayo hukolezwa na kuedesha magari ya thamani kama Mercedes-Benz kama ile SL 65 AMG, inayotimka mwendo kasi zaidi ya kilomita 350 kwa saa, ili kuwahi ‘appointment’.
 He! Mwaya, wee kalaghabao na huyo mume suruwali wako.Wanawake(kasoro wachache) hutamani kuolewa ama kuvikwa pete ya uchumba na watu kama Carlos Slim ama Bill Gates.
Wanapoolewa wanataka kuendesha BMWs, Audis ama Merces.Wewe una mkokoteni, wa nini katika gulio la huba la vimwana?
Unajua? Carlos Slim wa Mexico anaongoza duniani kwa ukwasi wenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 53.5.
Anafanya biashara za mawasiliano; atapendwa na kila mwanamke mrembo duniani.
Anayemfuata, ni huyo Bill Gates wa Marekani, ambaye utajiri wake kabla ya mtikisko wa uchumi,ulikuwa Dola bilioni 53. Biashara zake ni program za kompyuta kama Microsoft. Akina dada wangependa kuvikwa naye pete ya uchumba.
Kwa mujibu wa majarida ya Forbes, na Wall Street Journal, Carlos Slim, maarufu sana kama “Super Slim” anachuma utajiri wa Dola za Marekani milioni 30 takriban kila siku.
                Ana utajiri ambao ni dola milioni 500 zaidi ya Bill Gates. Changudoa gani atamgeuzia mgongo?
 Thubutu!
Warren Buffet wa Marekani ana utajiri wa Dola bilioni 47; anawekeza katika biashara za Berkshire Hatthway.
 India pia kuna matajiri kama Mukesh Ambani(hana uhusiano na Ambani aliyekuwa Yanga),anayefanya biashara za mafuta na gesi. Ambani wa India ana utajiri usiopungua dola za Marekani bilioni 29. Kisura gani wa Dar es salaam atamkataa? Wee acha tu.
Lakshmi Mittal, Muhindi, anauza bidhaa za chuma ama mavyuma huko India na kwingineko.Utajiri wake ni dola bilioni 28.7.
Hata wake za watu hapa wako radhi kuwakimbia watoto na waume zao ili wakaolewe naye.
 Lawrence Ellison wa Marekani, anauza teknolojia za kompyuta na ametajirika kwa dola bilioni28. Nakamilisha idadi ya matajiri 10 zaidi duniani(Top 10 Richest men in The World) kwa kuandika majina na utajiri wao kwenye mabano.
Bernard Amault wa Ufaransa(dola bilioni 27.5), Eike Batista wa Brazil(dola bilioni 27), Amarcio Ortega wa Hispania(Dola bilioni 27)na Karl Albrecht wa Ujerumani(dola bilioni 23.5) kutokana na supermarkets.
 Nachelea kusema anuani zao na nambari zao za simu hapa gazetini,kwa sababu machangudoa watawasumbua sana kuwa ‘beep-beep’.
 Penzi la tashtiti? Mapenzi ya kweli hayana thamani, hayajali tajiri na fukara, hayalinganishwi na thamani za almasi na dhahabu na lulu.
Kwa mujibu wa magazeti ya The Guardian, The Independent, Observer na Daily Telegraph, hawa matajiri hawana shida na vimwana wa Dar es salaam, Mwanza, Arusha n.k Wasinisumbue kwa meseji uchwara.
Mapenzi ya kweli hayana thamani katika sarafu bali damu.
Nataka kuuliza kwamba, kwa nini wanawake wa siku hizi wanataka kufikia pesa pindi wakifunga pingu za maisha?
 Kwa nini wanataka kuolewa na ‘tycoons’ wenye kumudu anasa potelea mbali wawe na vimada lukuki?
Mapenzi hayanunuliwi na matajiri kama hawa katika vibanda vya masangoma. Mapenzi hayaletwi na hirizi ama talasimu na waonaji wa nyota. Mapenzi hayana anwani.
Kuna aina nne za upendo duniani. Philia, Eros,Storge na Agape. Utajifunza hapa kwamba mapenzi ama upendo wa dhati haununuliwi kwa pesa za matajiri hata hao wote wakubwa duniani.
Storge, ni ile hali ya vitoto vidogo kuwahitaji wazazi wao. Eros ni hashiki, tamaa za mwili na mahaba ya ghiliba,ama tamaa za kingono-ngono tu.Philia ni upendo wa kidugu (Brotherly love).
 Eros au tuite Erao na Storge ni upendo wenye makusudi ya kutimiza matakwa ya kibinafsi zaidi,ni tamaa za kimwili, wakati Philia ni upendo uletwao na kuhudumiwa wakati wa shida;ni kupenda pesa tu, ni mapenzi ya pesa.
 Philia hutokana na kufikiri ama kuwaza pamoja na kuwaza pesa tu. Agape ni neon la Kigiriki maana yake upendo usioegemea pesa,faida,tamaa,huduma n.k. Upendo wa Agape hauna chumo la faida. Huaegemei mahali penye urafiki ama udugu.
 Kwa Kiingereza, “Impartiality Love” ni  upendo kama alionao Mungu au Yesu kwa kuwafia watu wote pamoja na majambazi, mafukara, magaidi na mafataki. Mapenzi huru huria hujitenga na chumo la faida.
 Miaka 2,400 iliyopita, mwandishi wa Kigiriki, Euripides, akaandika habari za kimwana mrembo sana aitwaye Alcestis, kwamba mfalme wa Thessaly aliyeitwa Admetus aliugua akataka kufa,lakini yeye akajitoa mhanga kufa badala yake.
Miungu ya Ugiriki ilifuatwa kuulizwa sababu za ugonjwa wa Mfalme Admetus;ikasema asingeokoka,isipokuwa kama atapatikana mtu mwingine ambaye angekufa badala yake.
Wakaulizwa wazazi wake kama wangekubali kufa badala ya mwana wao mfalme, wakakataa. Wakafuatwa ndugu na jamaa kama wangekuwa radhi kufa ili huyu Admetus abaki akitawala, kwa sababu alikuwa kijana mzuri, wakagoma.
 Wakaulizwa marafiki ili mmoja wao akubali kujitoa mhanga kufa mahali pake ili abaki akiwatumikia wananchi, wakakataa. Mwishowe, Alcestis, mwanamke mrembo sana, aliyekuwa mpenzi wa Admetus akakubali kufa badala ya Admetus.
 Baada ya Alcestis kufa, mfalme akaomboleza sana kwa miaka mingi,kwa sababu Alcestis alimpenda siyo kwa maneno matupu na kupenda raha, bali upendo wadhati, wa kuwa tayari kufa.
 Kisa hiki cha Admetus na Alcestis hutufundisha mapenzi ya kujitoa mhanga. Hata hivyo, huu upendo siyo Agape. Agape siyo kufa kwa ajili ya mtu mwema umpendaye. Yesu alitufia tulipokuwa tungali adui zake,na ndiyo Agape(soma Warumi 5:6-10)
 Yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema kama Admetus,lakini Kristo Yesu alitufia tulipokuwa tungali maaduzi zake, anatufundisha kuwapenda sana maadui zetu na wale ambao hawana faida kwetu kama hao matajiri. Tazama Mathayo 5:43-48.
Sihubiri dini, bali nasema mapenzi ya kweli hayatazami faida na huduma, hayatazami fedha na utajiri wa mtu, hayaangalii urembo. Mapenzi hayana rangi,hayajali faida.
 Mapenzi hayaangalii zawadi na ng’ombe na farasi zizini. Mapenzi ya dhati huuzwa duka gani wewe tapeli?
 Mapenzi ya dhati huletwa na Mungu, kama hewa. Thamani yake halisi hakuna awezaye kuilipa.
 0786-324 074
0754-324 074