Wednesday, August 14, 2013

MUGABE ALIPOMTUKANA BUSH NEW YOR



                                


                      


Miaka zaidi ta 10  iliyopita, ripoti ya Military Balance( ya harakati za Kijeshi Duniani) iliyochapishwa na Chuo Kikuu cha Oxford Uingereza, ilionyesha Korea Kaskazini na Iran zikiwa juu katika Orodha ya nchi 30 zenye vikosi vingi vya kijeshi Duniani.
     Hadi 1999, ripoti hiyo ya mwaka 2000 ilisema, Korea Kaskazini ilikuwa ya nne Duniani ikiwa na jumla ya vikosi 1,055.0 nyuma ya India yenye vikosi 1,173.0, Marekani (vikosi 1,371.5), na Uchina yenye vikosi 2,820.0.
   Hii maana yake ni kwamba, nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na vikosi vingi vya kijeshi ni Uchina, ikifuatiwa na Marekani, kisha India na Korea Kaskazini. Russia ilikuwa na vikosi 1,004.0, wakati Korea Kaskazini ilikuwa na majeshi ya Akiba 4,700.0 ikitumia Dola za Mrekani Bilioni 2.5 katika medani hiyo ya ulinzi.
   Marekani yenyewe ilikuwa ikitumia Dola zake Bilioni 283, Uchina(dola bilioni39.9), na India(dola bilioni 15, wakati Russia ilikuwa ikitumia dola bilioni56.8 katika ulinzi wakati raia wake wakifa njaa.
      Korea Kusini ilishika nafasi ya sita duniani kwa ukubwa wa majeshi, ikiwa na vikosi 672.0 na majeshi ya Akiba 4,500.0 ikitumia kiasi cha dola bilioni 12.1 za Marekani katika medani ya ulinzi.
    Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa ya nane ikiwa na vikosi 545.6; wakati ilikuwa na majeshi ya akiba 350.0; ikitumia dola za Marekani bilioni 5.7. Iran ilikuwa na vifaru vikubwa vya kivita(MBT) 1,135 na madege, nyambizi na zana nyingine hatari.
    India na Pakistan waliingia katika orodha ya Mataifa ya Nyuklia mwaka 1998. Wakati Iran wanazua mchecheto kwa Mpango wao wa Nyuklia, Korea Kaskazini wameshawishiwa kufunga kiny chao cha Yongbyon kwa mrabaha wa tani milioni za mafuta, au kitita chenye thamani sawa na mafuta hayo.
      Pakistan ilikuwa ya sita ikiwa na vikosi 587.0; vikosi vya akiba 513, vifaru vikubwa 2,285. Katika orodha hii, kutoka Afrika, nchi za Misri ni ya 11 nyuma ya Vietnam. Misri ina vikosi 450.0, vya akiba 254.0 na hutumia dola za Marekani bilioni tatu kwa gharama za kijeshi.

                          VITA VYA MISRI NA ISRAELI
    Umewahi kusikia vita vya Misri na Israeli mwaka 1973?
Tulikuwa  ukingali kinda.
 Lakini, Israeli iliingia vitani kupambana na Misri ikiwa na jumla ya vifaru, ndege na vikosi vichache sana kulinganisha na vile utitiri vya Waarabu. Waarabu walisaidiwa sana na Urusi.
    Israeli ilikwenda Sinai na vifaru 1,700 tu kulinganisha na 2,600 vya Misri na 2,000 vya Syria.
   Kwa siku tatu tu za vita, Israeli ilikwishapata hasara kubwa, ikabaki kufanya mashambulizi  ya kushtukiza(counter-attacks). Israeli  Iliishikilia Sinai wakati wa vita vya siku sita, mwaka 1967.
    Kuona hivyo, Rais Jimmy Carter wa Marekani akakimbia kumwita Waziri Mkuu wa Israeli, Menachem Begin na Rais wa Misri, Anwar al Sadat kule Camp David mwaka 1978.
  Henry Kissinger,yule Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, akakimbia kutafuta amani na suluhu, kwa sababu Israeli ilikuwa inamwagiwa maji ya moto na Waarabu katika vita. Wakati huo, Waisraeli walikuwa wakisherehekea Siku Kuu ya Kiyahudi, Yom Kippur; walisalimu amri na kuiachia Sinai, huku Mayahudi wakilalama.

                         ETHIOPIA MSHIRIKA WA MAREKANI
     Naam. Ethiopia ni ya 17 katika orodha ya nchi zenye majeshi makubwa duniani ikiwa na jumla ya vikosi 325.5; na hutumia dola bilioni 0.4 katika bajeti yake ya ulinzi. Utaona ni jinsi gani waweza kutuliza ghasia hata Somalia.
    Eritrea ni ya 29, Morocco ya 30, Ujerumani ya 16, Myanmar (Burma) inayopigana na waasi sasa ya15, Ufaransa (ina Nyuklia) ya 18, Sysia ya 19, Japan ya 25, Uingereza(ina Nyuklia) ya 27 miongoni mwa nchi hizo 30.
     Mwaka 1999 Iran ilikuwa na vifaru 1,135 wakatI Uingereza wakiwa na 616 tu, Ufaransa walikuwa na vifaru 1,207, Ujerumani walikuwa na 2,815. Hali hii huonyesha ni jinsi gani Wakurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani(CIA) walikuwa makini sana kuchunguza harakati za kijeshi za Iran, Syria, Korea Kaskazini na Waarabu wengine wasioiunga mkono Marekani na washirika wake.
    Utaona wakurugenzi wa CIA, akina William E.Colby, George Bush(Baba), Stanfield Turner, William J. Casey, William Webster, Robert M. Gates(Waziri wa Ulinzi), R. James Woolsey, John M. Deutch na George J. Ternet, walivyokuwa makini siku zote kuzihujumu nchi hizo katika harakati zao za kijeshi.
     Hizi ni harakati za vichaa kujaribu kutafuta amani katika dunia majununi(Crazy People in Crazy World).Ndiyo maana kuna mikataba mingi sana ya kuzuia utengenezaji wa silaha hatari tangu mwaka 1963.
     Miongoni mwa hii ni Strategic Arms Reduction Treaty (START) wa kwanza na wa pili uliokuja kusainiwa Moscow, kati ya Urusi na Marekani.
   Upo pia uitwao, Comprehensive Test Ban Treaty(CTBT) uliozuia majaribio ya Nyuklia na milipuko wa Septemba 1996.
    Oktoba 2000 nchi 160 kati ya 196 zilitia saini Mkataba huo, pamoja na Marekani, Russia, Uchina, Uingereza na Ufaransa.
    Wakati huo wa vita baridi, Kambi mbili za Mashariki(za Mkataba wa Warsaw) na Magharibi, NATO(North Atlantic Treaty Organization), walishindana sana kutewngeneza silaha.
      Mkataba uitwao, SALT (Strategic Arms Limitation Treaty) wa kwanza na wa pili uliazimu kupunguza silaha za masafa marefu. Miongoni mwa makombora ya masafa marefu yaliyomilikiwa na kila upande ni ICBM(Intercontinental Ballistic Missile); misaili lenye kulenga shabaha zaidi ya kilomita 6,000; zaidi ya kutoka Moscow hadi Washington.
     Misaili nyingine ni SLBM (Submarine Launched Ballistic Missile), MIRV (Multiple Independently Targetable Re-entry Vehicle), gari linaloruhusu misaili kubeba zaidi ya kichwa kimoja cha silaha na kupiga shabaha tofauti bila kukosa.
     Baadhi ya watu wanahoji: Kama Marekani wana nia njema ya kuiokoa dunia na maangamizi; kwa nini wameshindwa kusaini mkataba wa Kyoto unaozuia uzalishaji wa gesi za sumu angani zinazoleta ongezeko la joto? Je, Ongezeko la gesi za sumu na joto duniani, si kitisho zaidi ya Nyuklia?
    Matukio ya Septemba 11 mwaka 2001 yameifanya Marekani kuchanganyikiwa na kuwa wababe zaidi ili kuyakandamiza mataifa ya Kiarabu, ili kujilinda zaidi dhidi.
    Jengo la WTC lilipobomolewa kwa mara nyingine mwaka 2001, liliwaonyesha Wamarekani jinsi ya kuwa makini zaidi na adui zao Waarabu.
Vifusi vya WTC ni mnara wa kumbukumbu ya kipigo cha magaidi. Ukiupima udongo wote wa kifusi cha WTC hutakosa tani milioni 1.2, na kifusi chote kimejaa eneo la ekari 10.
    Inakisiwa,  mpango wa mashambulizi ya Sepotemba 11 umegharimu kati ya Dola za Marekani 200,000 na 500,000; na kwamba uchumi wa New York uliathiriwa kwa zaidi ya Dola bilioni 100.
   Rais Robert Mugabe na Bush, mwaka 2007 walifafanua jinsi gani fujo za ‘vichaa’ kama akina Bush na Mugabe  wanapojaribu kutafuta amani ya dunia  kwa kupandisha mizuka!
    Alhamisi, Septemba 27 mwaka 2007, Mugabe alisema kitu kinachosaidia kujibu maswali ya wasomaji wengi wa Rai juu ya unafiki wa wakuu wa dunia hii.

    ‘RG’ MUGABE AMEBAKI  ILI KUWATOA KAMASI MAREKANI
    Akihutubia kwa ukali Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa(UN), Mugabe alisema Bush ni ‘mnafiki mwandamizi’ anayejidai kuheshimu Haki za Binadamu, kumbe vitanga vya mikono yake vimelowa damu za watu, hususan katika viambaza vya Guantanamo Bay!
Na Abu Ghraib.
       “Vitanga vya mikono(ya Bush)  vilikuwa vinachuruzika damu ya wasio na hatia wa mataifa mengi”, Mugabe alisema katika hotuba kali katika mkutano huo wa 62 wa Umoja wa Mataifa,”Anajidai kuwa Mkuu wetu katika Haki za Binadamu?”
   Mugabe(89) ambaye amezeeka,nchi imemshinda lakini hadi sasa akina Tsivangirai si mbadala wake, alihoji siku hiyo hiyo Bush alipozizodoa Belarus, Syria, Iran na Korea Kaskazini kama ‘Mataifa katili zaidi’ duniani.
    Akiizungumzia Zimbabwe, Bush alisema inaongozwa na ‘JAHILI’ Mugabe, anayewararua watu wake mwenyewe.
                Zimbabwe leo inakumbwa na kimbunga kikali cha uchumi mbaya.
Mfumuko wa bei unafika asilimia 7,000 na utafika asilimia 10,000 kabla ya Krisimasi. Fedha zinafika mwisho wa matumizi(expiration) utadhani unga wa ngano ama dawa ya mswaki. Mugabe anawatupia lawama Wazungu kwa hujuma anuwai.
Hata hivyo Zimbabwe sasa hutumia dola za Marekani badala ya dola ya Zimbabwe!
     Lakini, mwaka 2007 akamchambua Bush (kama karanga) na kusema ni mnafiki wa hali ya juu!
    Mugabe, pia amewahi kuwatwanga virungu wapinzani wake, akiwamo Morgan Tsivangirai wa MDC.Tsivangirai sasa kashindwa, analalama kuwa kaibiwa kura!
   Lakini, alisema Bush anatesa watu Abu Ghraibu nchini Irak na katika jela za kijeshi  nchini Cuba, mahali walipowatuhumiwa wa al-Qaeda!
Ilikuwa safi hiyo?
    “Katika kambi hizo za mateso”, alisema Mugabe, “Hakuna sheria na hata zile za kimataifa hazina nguvu. Marekani wanawajibika kuandika upya Tangazo la Haki za Binadamu…hata Septemba 11(2001) Wamarekani ni wakosaji”, alisema Mugabe.
    Mugabe alimkosoa Bush kwa kuwakamata watuhumiwa na kuwafunga bila kuwafikisha mahakamani. Mugabe anamuunganisha Bush na rafikiye, Tony Blair(Waziri mkuu mstaafu wa Ui8ngereza) kama watu walioiburuza sana dunia, hususan Umoja wa Mataifa. Baada ya kuharibu Irak sasa wanaacha jukumu kwa Umoja wa Mataifa kulinda amani na kuponya kidonda!
   “Mwenyezi Bush(alimkejeli kujilinganisha na Mungu) sasa karejea Umoja wa Mataifa kusaka msaada wa wokovu…kwa sababu, pua  yake inavuja damu zisizo na hatia…bado anajitutumua kutuhadithia madhila ya ukatili”, Mugabe alisema.
     Naam, hivi ni vituko vya vichaa katika Ulimwengu majununi(Crazy People in a Crazy World), Mugabe na Bush kumwagiana shombo katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kusaka amani! Mkuki kwa nguruwe sijui nyani dume haoni kundule? Alamsiki.
   0713 324 074
                       



Monday, August 5, 2013

http://ts2.mm.bing.net/th?id=U.4930640688712695&pid=15.1

KIKOMBE CHA BABU WA LOLIONDO KIMEINYWESHA SUMU TZ




ZAIDI ya watu 10,260 waliacha kwenda kuchukua dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi Mkoani hapa,tangu 2004 hata sasa.
Serikali ya Tanzania leo,kwa kushirikiana na Tume ya Kikristo, The Christian Social Service Commission(CSSC) na serikali ya Marekani,siku hizi wanatumia mabilioni ya Dola za Marekani kuwarejesha wenye virusi vya Ukimwi hospitalini ili kupata tiba ya kisayansi.
Mkakati huo unaitwa, ‘Back to Treatment” na unalenga kuwarejesha watu 10,262 wa mkoa wa Mwanza tu hospitalini.
Baadhi yao waliacha tiba ya kisayansi, wakatimkia Samunge,Loliondo mwaka 2011 kwa Yule ‘Babu’ wa Kikombe cha Miujiza,kilichodaiwa kuponya magonjwa sugu,ukiwemo Ukimwi kwa majuma matatu tu!
Ambilikile Mwasapila,(78),Mchungaji Mstaafu wa KKKT, alikuwa ameota ndoto ikimwambia aondoke Babati na kuhamia porini huko Samunge, ambako alianza kunywesha maelfu ya watu kutoka Afrika Mashariki,Ulaya na Asia dawa ya miujiza kutoka kwenye mti uitwao,Carisa Spinarum, ama ttuuite     Mrigariga!
Serikali ikaanza kuishabikia dawa hiyo iliyouzwa kwa shilingi 500 tu kwa kikombe, maelfu ya watu wakanywa, wakiwemo wasomi,maprofesa,wafanyabiashara na hata wakulima wa kijijini.
Vigogo wa serikalini walikuwa mstari wa mbele kuishabikia na kuibugia ili wapate tiba ya kimiujiza-Cure in the Tanzanian Bush!
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Abbas Kandolo(yuko Mbeya siku hizi) alipoulizwa na Mwandishi huyu aliyefanya mkutano kamambe ofisini kwake kuratibu safari za kwa ‘Babu’ wa Loliondo,mwaka huo 2011, “Ni kwanini serikali inahaha kushiriki ushirikina na miujiza ya uponyaji huko kwa Babu,Loliondo, kabla ya dawa hiyo kuthibitishwana taasisi husika, Tropical Pesticides Research Institute, TFDA, labda na TBS, akaniambia kwa hamaki!
“Sasa wewe mtu layman (usiye na taaluma ya kitabibu) unawazidi maprofesa wanaoinywa dawa ya Babu wa Loliondo?” akamtaja mkubwa mmoja.
Katika mkutano huo wa Mkuu wa Mkoa na wafanyabiashara wenye mabasi ya kusafirisha watu kwenda Loliondo, walikaribia kunimeza,kuona nilikuwa nikitaka kuwaharibia biashara, wakati serikali ilishamkubali huyo ‘Babu wa Kikombe’ aliyeleta neema kwa wenye mabasi mwaka 2011.
Carisa tree, ni mti uliokuwa ukitajirisha si babu huyo tu, bali na wenye vyombo vya usafirishaji na hata mama ntilie wa Samunge.Wagonjwa wengine waliopelekwa wakiwa mahututi, walifariki dunia.
Leo,serikali inameza machungu, inashirikiana na serikali ya Marekani na taasisi za dini kufanya mkakati wa kuwarejesha wenye virusi vya Ukimwi kwenye tiba uitwao kwa Kimombo, “Back  To Treatment” kwa mabilioni ya dola.
Mkakati huu, BACK TO TREATMENT, ulizinduliwa rasmi jijini Mwanza Agosti Mosi mwaka huu kwa mbwembwe, na watu wakalipana posho!
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanywa katika Hospitali ya Sekou Toure, Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa wa Tume hiyo ya Kikristo ya Huduma za Jamii,Dk.Michelle Roland       akasema:
“Tangu 2003 serikali za Marekani na Jamhuri ya Muungano zimekuwa na ushirika kupambana na Ukimwi unaoathiri watu wote Duniani,hususan Watanzania”,Dk. Michelle Roland alisema.
Akabainisha kuwa ubia huu umewafanya wananchi wa Marekani kuchanga jumla ya Dola za Marekani bilioni 2.2 ambazo ni sawa na shilingi za Tanzania Trilioni 3.2.
Fedha hizi ni kwa ajili ya kupambana na magonjwa sugu,ukiwemo Ukimwi.
Mkuu wa Mkoa,Evarist Welle Ndikilo, akafungua mkakati huo, akisema Tanzania Bara sasa kuna zaidi ya watu 430,000 wanaopewa dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi kupitia Mpango huo wa Back to Treatment wa hao  Christian Social Service Commission(CSSC).
Ndikilo, akasema eti sasa Mkakati huo wa Back to Treatment utawarejesha wagonjwa kwenye tiba na utaifanya Tanzania mahali pasipo na maambukizi ya Ukimwi-AIDS-free Tanzania!
Labda, asitokee Babu mwingine kama wa Loliondo,bibi ama shangazi!
Asilimia 25 ya wenye kuishi na virusi vya Ukimwi walikimbia vituo vya kutolea dawa za Ukimwi, antiretroviral Therapy.
Wamekuwa hawapati dawa hizo ili kuwawezesha kuishi na afya njema na kushiriki ujenzi wa taifa.
Mama huyu wa Kimarekani,Michelle Roland, akaonya kuwa endapo wenye kuishi na virusi vya ukimwi hawatapata tiba sahihi,jamii nzima itaathiriwa vibaya,na maambukizi yataongezeka maradufu, na virusi vitajenga usugu-hizi ni athari za akina Abbas Kandoro kupigia debe Sangoma,kama Babu wa Loliondo!
Pia,Dk.Michelle Roland amewataka wenye virusi vya Ukimwi kwenda hospitalini kupata tiba sahihi,kando ya mfumuko wa vikombe vya babu na shangazi!
Akashauri udhaifu uliopo katika mfumo wa tiba(zikiwemo imani potofu za viongozi ba ushirikina) uepukwe,ili watu waishio na virusi vya Ukimwi warejeshwe kwenye huduma za tiba na ushauri sahihi.
Dk. Michelle akawataka watu kubadilika,na kuacha kushabikia uvumi na umizimu na masangoma.
Kampeni kama hii iliwahi kuzinduliwa Iringa na Balozi wa zamani wa Marekani nchini,Alfonso Lenhardt.Ilikuwa Septemba mwaka uliopita.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Evarist Ndikilo amesema Tanzania kuna watu 945,142 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.
Kati ya hawa 530,118 ndiyo walioanzishiwa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi, watu 129,372 hapa Tanzania wamekimbia matibabu,wengine walitupa vidonge walipokunywa Kikombe cha Babu!
Hadi Machi mwaka huu watu 85,320 Mkoani Mwanza waliandikishwa kupata huduma,lakini ni 46,622 tu walioanzishiwa tiba.
Watu zaidi ya 10,000 hawajulikani walikokwenda,hawa ni pamoja na watoto 1,600 hapa Mkoani Mwanza.
Sasa  tukiulize,hizo imani za kishirikina zinazoshabikiwa na serikali na maofisa wake hata kukiuka sheria ilizoweka yenyewe kuhusu tiba ndiyo nini,kama siyo kuitesa nchi?
Imani potofu,ushirikina hata wa kuua Albino ili kushinda kura,kupata utajiri n.k
Wengine,watu wakubwa walibugizwa dawa ya babu na kuwafanya maelfu kufuata mkumbo wakaacha tiba sahihi.
Ndiyo maana tukasema, Kikombe cha Babu kimeinywesha sumu Tanzania,sasa inatumia mabilioni ya dola kurejesha wenye VVU hospitalini.
Hawa ni wenye VVU tu, saratani,kisukari,magonjwa ya moyo n.k siku hizi hupelekwa kwa sangoma kwa Baraka za akina Abbas Kandoro na serikali nzima!
0786 324 074





nduli Amin Dada(4)



                                    
Na Conges Mramba
Baada ya Amin kuingia madarakani, watu wa kabila la Lango na Acholi la Milton Apollo Obote,waliuliwa kwa maelfu, na maiti zao zikaliwa na mamba wa Mto Nile huko Jinja.
Wahindi wakatimliwa mwaka 1972 maduka yao wakapewa rafiki za Amin mjini Kampala,ndiyo maana hata leo kuna watu wanampenda Amin kuliko Museveni.
Naam,tumejadili Operation Thunderbolt, iliyomtoa jasho Amin kushabikia wateka nyara wa Kipalestina,huku akakosana na Israeli na Magharibi.
Kile kikosi cha makomandoo wa Israeli kilienda zake salama,kikapokelewa kwa heshima kubwa.Yule Jonathan komandoo aliyeuliwa alizikwa kwa heshima kubwa kama shujaa wa taifa.
Utawala wa Amin wa miaka minane ukaandamwa na mikosi hadi raia wake wakaanza kumwasi nao ni akina Museveni,Tito Okello na wengine kama tulivyoona katika toleo lililopita.
Amin alikosana siyo na Nyerere tu,bali hata Rais Moi wa Kenya zama hizo,akitishia kwamba hata Maili 20 Nairobi ilikuwa sehemu ya Uganda tangu zama za ukoloni.
Tumeona Amin akitimliwa mamlakani na kufia huko Saudi Arabia,baada ya Museveni kukataa azikwe Uganda.
Hata hivyo,mwanaye Amin,Jaffar siku za karibuni alifanya jambo la kuondoa chuki na kudumisha urafiki.
  Aprili, mwaka 2009, ni mwezi ambao kulitokea vitu vingi adhimu sana, na vya kukumbukwa sana hapa nchini.
      Safari ya mwana wa Dikteta wa zamani wa Uganda , Jaffar Amin(47) aliyesafiri kutoka Uganda hadi Mwitongo, Butiama, mkoani Mara.
    Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, iliratibu safari hiyo ya Jaffar, ambaye ni mtoto wa nne, kati ya watoto takriban 60 wa Amin.
 Jaffar alikutana na mtoto wa Pili wa Mwalimu, Madaraka Nyerere.
   Ziara ya Jaffar huko Mwitongo, Butiama katika mwezi huo wa Aprili, mwaka 2009, inatukumbusha miaka 34 kamili baada ya kuanguka kwa utawala wa baba yake huko Uganda , Aprili 11 mwaka 1979.
   Amin Dada, alitimuliwa na majeshi ya Tanzania mwishoni mwa vile vita vya Kagera; akatimkia Sudan, Libya kisha Saudi Arabia, alikofariki dunia mnamo Agosti 16 mwaka 2003.
   Naam. Ziara ya Jaffar Amin huko Mwitongo, Butiama mkoani Mara, ilikuja wakati wa Kumbukumbu ya 87 ya kuzaliwa kwa Mwalimu mahali hapo.
 Nyerere alizaliwa Aprili 13 mwaka 1922.
   Tena, Jaffar amekuja Tanzania wakati hayati Mwalimu alipojadiliwa sana katika lile Tamasha lake lililowaleta nchini wasomi na wanazuoni maarufu Afrika; kama Prof. Wole Soyinka wa Nigeria .
   Tumjadili kidiogo Jaffar Amin, ambaye leo ni kiongozi wa familia ya Marehemu baba yake, Idi Amin Dada, mtawala wa zamani wa Uganda (1971-79).
   Mwaka 2005, alikwenda Akokoro, ili kuhudhuria mazishi ya Dk. Apollo Milton Obote. Amin ndiye aliyempindua Obote mwaka 1971 alipokuwa nchini Singapore akihudhuria Mkutano wa Jumuiya ya Madola(Commonwealth); Obote akakimbilia Tanzania .
   Kitendo cha Jaffar kuhudhuria mazishi ya Dk. Milton Obote, hasimu mkubwa wa baba yake, kilivuta hisia za watu  wengi, hata kuona msamaha na maridhiano miongoni wa Waganda na Waafrika wengine wa zama zetu hizi.
 Jaffar Amin, ni somo kwa Waafrika wote zama hizi, kusameheana na kuacha chuki na vita visivyo na sababu, wakatiti sisi Waafrika ni ndugu wamoja.
  Jaffar, alipowapa pole familia ya Obote katika msiba huo, akageuza upya historia na kuanza kumuumba upya babaye, Dikteta wa zamani wa Uganda, aliyejibandika vyeo lukuki  kama, Field Marshal, Mshindi wa Dola ya Kiingereza, Mwanamasumbwi Nguli Duniani, Bingwa wa Kuogelea na mwenye Medali za kutukuka sana kama Victoria Cross n.k!
   Jaffar, anapofika Butiama kuzungumza na Madaraka Nyerere kwa msaada wa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Bwana Solomon Mugela, anawaondoa Watanzania katika lindi la fikra hasi za kumtazama Amin kama ‘Joka Kuu’ la kale la Uganda, Nduli, muuaji, mla nyama za watu, hususan adui zake wa kisiasa.
 Nazungumza umuhimu wa toba na msamaha kwa sisi Waafrika, yaani kuachana na uhasama ili kutafuta umoja na mshikamano kisha maendeleo yetu na wanetu.
  Amin, alishatengenezewa filamu tatu zenye kuonyesha enzi ama zama za utawala wake wa kikatili na kimabavu sana kulinganisha na ugaidi wa siku hizi.
    Sauti ya Nyikani  hupenda sana kuzitazama zifuatazo:
The Rise and Fall of Idi Amin Dada, na ile ya Forest Whitaker, iitwayo, The Last King of Scotland.
  Katika sinema hizo, Amin huonyeshwa kama mtawala katili sana , pumbavu, zuzu, mpenda anasa na  mpenda wanawake, anayetawala nchi kwa hofu na vitisho karibia kumuua kila anayemuota ndotoni, akimpinga, akimsaliti hata kumchukulia mmoja wa wakeze.
   Filamu nyingine iitwayo, 90 Minutes at Entebbe au The Entebbe Raid, inatukumbusha Uganda ilivyoanza kuvunjika vipande, baada ya Bwanamkubwa Amin kuvuruga uhusiano wa kidiplomasia na Wazungu.
   Amin, alijiweka upande wa Waarabu hususan Wapalestina, magwiji wa medani za ugaidi wa kuteka  nyara ndege, kama hiyo ya Air France Air Bus, iliyokuwa safarini kutoka Paris,Ufaransa, kwenda Israeli, ikatekwa na kupelekwa Entebbe.
  Naam, tunamjadili kidogo Marehemu Idi Amin Dada na mwanaye, Jaffar Amin aliyefika Mwitongo, Butiama mwaka jana, kuja kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu, miaka 30 baada ya Vita vya Kagera, vilivyomwondoa madarakani, Uganda, Marehemu babaye, 'Joka Kuu' Nduli Amin, aliyelala mauti kaburini Saudi Arabia.
    Nataka kusema kwamba, namkumbuka Amin kwa ‘kuwachachafya’ vilivyo Wazunguna magabacholi.
 Naam, wakoloni ambao leo hutetemekewa sana kwa kicho utadhani miungu; hupigiwa goti na kulambwa dole gumba na watawala wetu waliojigeuza manyampala wa Wazungu.
   Watawala wa Afrika waliojaribu kuwapinga Wazungu ni Nelson Rolihlahla Mandela tu; labda na “R.G” Mugabe  na Kanali Muammar al-Qaddafi, tena kwa sababu zao!
 Nani leo atathubutu kuwapinga wazungu?
     Waama, filamu iitwayo, The Rise and Fall of Idi Amin Dada, inatukumbusha  baadhi ya vituko vya Amin ambavyo kwa kiasi kikubwa sana hushadidia ukombozi wa mtu Mweusi dhidi ya Weupe.
    Siku ile Mkutano wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika(OAU kabla ya kuwa AU), ulipofanyika mjini Kampala , Amin alibebwa na Wazungu katika machela, alipokuwa akiingia kufungua mkutano!
   Viongozi wenzake waliokuwa tayari katika chumba cha mkutano wakashangaa kuona Amin anaingia kwa staili ya kubebwa na Wazungu katika machela.
  Kumbuka msomaji wa safu hii, zama za Ukoloni ni Waafrika waliowabeba wakoloni wa Kizungu katika machela.
 Mwandishi, rafiki yangu, Prudence Karugendo, aliyekuwa Kampala zama hizo, ananiambia kitendo hiki hakijawahi kufanywa,bali propaganda za Magaharibi tu.
   Pia, wakati fulani, Amin alimhukumu kifo Mhadhiri wa Kiingereza, Dennis Hills , kwa makosa ya kuwasumbua na kuwanyang’anya ardhi wanakijiji.
 Jumuiya ya Kimataifa ilipomzonga sana Amin ili kumwacha huru Bwana Hills, akasema kwamba  hadi kama  Waziri Mkuu wa Uingereza, James Callaghan, angeruka kutoka London hadi Kampala, kuja kupiga goti na kumwombea msamaha Hills, ndipo angeondolewa kitanzi kilichomkabili!
 Siku hizi, hapa Afrika  iko mahakama yenye uwezo wa kumuhukumu Mzungu hata mwizi,gaidi, na mbakaji, bila kuuliza alikotoka,kama wamfunge jela au wamwachilie 'Fasta'?
 Hapa Tanzania, kasisi mmoja wa Katoliki,toka Italia alibaka wanafunzi wa kidato cha tatu jijini Mwanza, akafikishwa mahakamani na kuamuriwa kuondoka nchini, asije akaswekwa  'mangenge' hapa,akanyea mtondoo wa Butimba!
   Hiki ndicho kilikuwa ‘kidume’ cha Bwana Mkubwa Amin dhidi ya Wazungu.Aliwatoa kamasi Wazungu na Wahindi,bila kicho,kwa maslahi ya Waganda!
 Amin, alikuwa na ubavu wa kuwatoa kamasi Wazungu, bila kuwaogopa Malkia Elizabeth II, Waziri Mkuu wa Uingereza,wala nani!
Aliwatimua Waasia 100,000 mwaka 1972, biashara zao walizoacha nyuma akawapa Waganda wa kawaida sana , ili nao wapate kukabiliana na machungu ya maisha!
Walikuwa na hati za kusafiria za Uingereza,wakati wanafanya biashara Kampala! Walihamisha utajiri wa Uganda hadi Ulaya kwa utulivu mno, hadi Amin alipokuja kuwatolea uvivu.
    Leo, hata hapa Tanzania kuna Waasia wenye uraia na Hati za Kusafiria za Uingereza , Canada na Marekani, wanaofanya biashara za magendo, ya fedha chafu, utapeli,ufisadi na wizi na uhujumu uchumi, bila kusahau ufisadi wa EPA,rada kanyaboya ya BAE Systems, lakini viongozi wetu huwakodolea macho pasipo kuwachukulia hatua kali,  kama  Bwana Mkubwa, Amin!
 Namkumbuka Mhindi, Shailesh Vithlani alivyoiingiza 'mjini' Tanzania kwa rada kanyaboya kutoka BAE systems!
 Rada ya fedha ndogo, wao wakala 'cha juu' hadi zikafika Dola za Marekani 40,000!!
    Nikipembua uhalifu na unyama wa Amin, hasa aliofanya dhidi ya raia kwa kutumia polisi wa siri waitwao, The State Research Bureau, nasisitiza wasomaji wa safu hii  adhimu na viongozi wazalendo wasiache kumuiga Amin kwa vitendo vya kimapinduzi alivyofanya (hata kwa bahati) ili kuwakomboa wanyonge.
   Nazungumzia vitendo vya kihalifu alivyokataa Amin, hata kama walifanya Waingereza.
  Waingereza wanatupa sisi Tanzania misaada.
Kila mwaka hiyo misaada huongezeka.
Mwaka 2003/2004 iliongezeka kutoka pauni milioni 80(sh. Bilioni 208) hadi pauni milioni 110(sh. Bilioni286) mwaka 2006 na 2007.Asilimia 70 ya misaada ya Uingereza huingia katika Bajeti ya serikali.
   Ni kwa sababu hii, mashirika ya misaada ya Uingereza na Bunge huwa na sauti kubwa sana hapa kwetu hadi kuingilia ‘mambo ya jikoni’ kwa maslahi ya Uingereza.
Haya ndiyo Amin aliyokataa enzi zake.Hata leo viongozi wetu wakimuiga Amin, kuna ubaya gani,na kwa maslahi ya umma?
 Nahitimisha safu hii  leo, kwa kuwakumbuka Waingereza vijana wawili:
 Nigel David(23) na Brett Richard(20) waliotiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka kisha kumuua msichana kigori wa Kitanzania, Conjesta Ulikaye, mnamo Novemba 10, mwaka 2004.
   Tukio hilo lilitokea katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, katika hoteli ya Silver Sands, Dar es salaam .
   Shauri la kesi ya mauaji likashughulikiwa kwa siku 36 tu, Nigel na Brett wakafikishwa mahakamani ‘Fasta’ Novemba 16; yaani siku sita tu baada ya tukio.
  Vibaka wa hapa wanasota rumande hata miezi sita bila upelelezi kukamilika!
Ndiyo maana kila siku hugoma kushuka kwenye karandinga na kujipaka kinyesi, hadi serikali iwajali kama inavyowanyenyekea Wazungu, naam na wenye cheo.
   Kesi hiyo ilifutwa Desemba 22 mwaka huohuo kwa mujibu wa kifungu 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985.
   Safu hii, iliwahi kumuuliza Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Geofrey Shaidi wakati huo(sasa Jaji), Machi Mosi mwaka 2005 alipokuwa jijini Mwanza:
    Hao Waingereza wawili(walikuwa wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwa mapumzikoni Dar, wakitokea vitani (Irak) waliachwa huru kwa maslahi ya umma wa Tanzania, au maslahi ya Uingereza?
    “Hawakuachwa huru kwa maslahi ya Uingereza au ya Tanzania …ushahidi uliokuwepo haukutosha!
Wasingeendelea kung’ang’aniwa bila ushahidi,” DPP Shaidi alisema.
   “Hata hivyo, kesi(dhidi ya raia) hazicheleweshwi na ofisi ya DPP, zinacheleweshwa mahakamani, zinaposubiri kupangiwa tarehe ya kusikilizwa.
Hivyo, faili la Wazungu lilipofika kwetu, tukalishughulikia(fasta?) kama kawaida”,
  alifafanua DPP Shaidi wakati huo, huku akikanusha madai kwamba Waingereza hao hawakuachwa huru kwa sababu ya kuchelea kunyimwa misaada na Uingereza endapo wangehukumiwa kutiwa kitanzi.
    Laiti Nigel David na Brett Richard wangefanya unyama wao huo wa kumbaka msichana kwa zamu na kumsababishia kifo huko Uganda , enzi za Amin, bila shaka wasingeepuka kitanzi!
   Hata kama Mawaziri Wakuu kama Margaret Thatcher, James Callaghan, Edward Health, John Major, Tony Blair na Gordon Brown, na David Cameron  kwa pamoja wangemkoromea Amin, bila shaka Nigel na Brett wangenyongwa tu hapa hapa Dar es salaam!
  Unacheza na Amin?
    Hata hivyo, hongera BBC  mwaka 2009, kutukumbusha mikasa ya lile Joka Kuu, “shujaa” Nduli Idi Amin Dada!!
   Ziara ya Jaffar imetukumbusha kuyasema pia mazuri ya marehemu, wakati huu tunapoingia mwaka mpya,ili tujirekebishe.
Tulizowea kumsema Amin kwa mabaya tu.Kwa heshima ya Jaffar, shime tutazame upande wa pili wa shilingi.
 Baniani mbaya,kiatu chake dawa, nikitazama viongozi wetu siku hizi wanavyowanyekea Wazungu na kuingia mikataba mibovu na wageni, wakiwemo matapeli wa Kihindi, kama Vithlani, nikikumbuka EPA,Dowans, Richmond na uchafu mwingi...namkumbuka Nduli Idi Amin, kwamba ingekuwa zama zake, lazima angewatoa kamasi hawa    magabacholi.
 Naam,  kwa sababu hiyo tu....nampenda 'Joka Kuu' Nduli Idi Amin Dada!!
     Congesdaima@yahoo.com
      0786/0754-324 074