Mwandishi wa kitabu maarufu, ‘SHAMBA LA WANYAMA’,George
Orwell,jina lake halisi ni Eric Blair.
Alizaliwa India mwaka 1903, ambako babaye alifanya kazi kama
Ofisa wa serikali huko Bengal.Akiwa mtoto,Eric Blair alipelekwa Uingereza,
akasoma shule binafsi ya Eton, ambayo ilikuwa bora sana zama hizo.
Wazazi wake walikuwa makabwela.Hivyo, Blair akaishi katika
madhila ya ufukara;maisha ambayo yalimfanya kudharauliwa na jamii ya Kiingereza
yenye ukwasi.
Mwaka 1922, akajiunga na jeshi la polisi Burma, siku hizi nchi
hii huitwa Myanmar.
Burma, ilitawaliwa na Uingereza kwa mkono wa chuma,kinyume
na matakwa ya raia.Siku hizi Uingereza inaimba wimbo wa ‘Demokrasia’ kumbe
kawimbo ‘demokrasia’ katamu,lakini waimbaji wake hunuka mithili ya kwapa la
Ibilisi! Unafiki tu!!
Eric, alipopata likizo akarejea Uingereza ambako alikaa muda
wa likizo ukapita-hakurejea Burma.Alijisikia vibaya sana kutumika katika jeshi
la Kiingereza kuwakandamiza raia wa nchi hiyo na matakwa yao.
Naaam, ilikuwa mwaka 1927.Eric Blair aliishi London,na
wakati mwingine mjini Paris,Ufaransa ambako aliishi katika lindi la ufukara wa
kupindukia.
Aliishi sanjari na watoto wa mitaani, ‘chokoraa’ na wasio na
ajira waliolala vibarazani katika mitaa ya kitajiri.Na wakati mwingine aliishi
na wasio na ajira, na waliolipwa kiduchu
mithili ya ujira wa mtwangaji.
Wakati mwingine, akaosha vyombo hotelini ili kujipatia mlo
wa usiku hususan huko mjini Paris,Ufaransa.
Ni hapa, Eric Blair alipoanza kuandika kuhusu maisha yake ya
kijungujiko.Kitabu chake cha awali kilichapwa kwa jina la GEORGE ORWELL,kwa
sababu alisema alionea aibu jina lake halisi,Eric Blair! Ufukara!
Amewahi kuwa mwalimu, akaacha.Alifanya kazi dula la
vitabu.Mwaka 1936 alimuoa Eileen Hertfordshire, wakaanzisha duka dogo la reja-reja.
Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Hispania,
alikwenda huko ili kupata cha kuandika kuhusu vita; akajikuta katika mapigano
makali.Alijikuta akipigana bega kwa began a Republican-akajeruhiwa vibaya,
akatimkia Ufaransa na mkewe ambaye waliandamana naye.
Mwaka 1938 George Orwell alikuwa mgonjwa sana, hata vita vya
Pili vya Dunia vilipozuka(1939-44) alitamani kujiunga jeshini,lakini hakufanya
hivyo.
Alifanya kazi kama Mwandishi wa habari.Mkewe alifariki
ghafla mwaka 1944;wakati mwandishi huyu mahiri alipokuwa yungali mwenye afya
mbovu.Wakati huo, alitumia muda mwingi katika korido za hospitalini ili
kutafuta tiba.
Mwaka 1949,Orwell alimuoa Sonia Brownwell.Walipanga kwenda
Switzerland, lakini Orwell akafariki dunia mwaka 1950.
Vitabu vingi vya mwandishi huyu mahiri duniani vinahusu
madhila yaliyompata katika taabu,dhiki,kudharauliwa sababu za ufukara.
Baadhi ya vitabu vyake ni Burmese
Days, Down and Out in Paris and
London vilivyohusu maisha ya ufukara katika miji mikuu ya Ulaya.
Homage to Catalonia,
kinahusu vita Hispania, A Clergyman’s
Daughter ni uzoefu wake katika kazi ya ualimu.
Aliandika Keep the
Aspidistra Flying kama uzoefu wake katika duka la vitabu.The Road to Wigan Pier ni stori zake
kuhusu maisha ya wasio na ajira Kaskazini mwa England, eneo la viwanda vikubwa.
Hata hivyo,George Orwell ni maarufu sana duniani kwa vitabu
vyake viwili alivyoandika mwishoni mwa uhai wake.
“1984” ni kitabu cha kuogofya kuhusu maisha ya
usoni(Future),wakati fikra za watu na maisha yao yatakapotawaliwa na serikali.
Kwamba mwaka huo 1984 watu wasingeamua hatma ya maisha yao wenyewe-Udikteta.
‘ANIMAL FARM’ ni riwaya kali ya kejeli(satire) kuhusu
wanyama-watu,akizungumza dhima ya Mapinduzi yaliyoshindwa ya Joseph Stalin huko
Urusi.Si Urusi tu,kitabu hiki Animal Farm huonesha yanayojiri hata sasa hapa
Tanzania.
Ujumbe mahsusi ni kwamba,tama ya madaraka ya viongozi
huwaingiza walalahoi katika matumaini makubwa,kisha hugeuka watumwa wa
kupindukia-hata humwaga damu yao ya thamani.
Baadhi ya “wanyama” katika riwaya hii kali huwakilisha watu
muhimu sana katika taifa(Public Figures) na ambao hupendwa sana na mashabiki
wao utadhani miungu-sacred cows ,kuwagusa
inakuwa laana na kifo!
Ni maisha halisi ya wanyama hawa hata hapa unapopenda sana
wewe bila akili tunduizi(critical mind).Nguruwe wajanja,wasomi waliojitia ku-“organize” wanyama wenzao ili kuondokana
na utumwa ulioendeshwa na BINADAMU-Madhila ya utumwa na ukandamizaji hata leo
tunao hapa hapa kijiweni petu-kila mtu na kijiwe chake.
Wanyama walikusudia kufanya MAPINDUZI uili kujenga JAMII
YENYE USAWA! Jamii yenye usawa katika dunia hii hii eeh??
Taifa jipya la Wanyama walilokusudia baada ya mapinduzi ni
lenye haki tupu,kweli,ubora na usawa, ambalo lingeleta Maisha Bora kwa Kila (Mtanzania)!
Hapana, maisha bora katika shamba la wanyama-ANIMA FARM.
Kufuatia mawazo haya ya kimapinduzi, zilitungwa sheria, ama
AMRI SABA(The seven commandments) ili kuwalinda wanyama.
Amri zote saba zilibeba maudhui na muktadha ya USAWA- “ALL
ANIMALS ARE EQUAL”.Naam, usawa,usawia.
Nadhani msomaji umepata kusikia au kuona, ama vyote
viwili-kuona na kusikia baadhi ya wanyama ambao ni ‘Public Figures’ katika
Tanzania hii hii wanapotokwa mapovu mdomoni kuhubiri juu ya Tanzania yenye
usawa,wakati ukweli halisi ni ubeberu na udikteta uliokamaa kuzidi wa mkoloni
katili!
Nianze kukutajia AMRI SABA za wanyama wa George Orwell.Shamba
la wanyama la Uingereza!
1.Kila aendaye kwa miguu miwili(binadamu) ni adui wa
wanyama.
2.Kila aendaye kwa miguu minne au mbawa ni rafiki
3.Ni marufuku mnyama kuvaa nguo!
4.Ni marufuku wanyama kulala kitandani
5.Hakuna mnyama kufakamia kilaji(pombe,masanga,ulabu n.k)
6.Marufuku mnyama kuua mnyama mwenzake
7.WANYAMA WOTE WAKO SAWA
Amri hizi zote zilitundikwa ukutani,ili wanyama wote katika
shamba hili la wanyama waishi na kuzifuata, na wanyama wote walisomewa kwa
sauti ili wazisikie.
Kusudi ni kila mnyama kuondokana na utumwa,udikteta,ufisadi
na matumizi mabaya ya madaraka katika jamii ya wanyama-haki stahiki.
Ni ufisadi wa kutisha kwa wanyama hao wa George Orwell
ulioendeshwa na binadamu.
Binadamu(binadamu mniwie radhi kusema haya) alikula bila
kuzalisha chochote!(MAN IS ONLY CREATURE THAT CONSUMES WITHOUT PRODUCING)!
Binadamu HAMKAMULIWI MAZIWA,wala hamtagi mayai;ninyi ni
dhaifu kupindukia hata hamwezi kukokota jembe linalokokotwa na wanyama
kazi(plough).
Binadamu wala hamwezi hata kufukuza kasungura,mpaka msaidiwe
na mbwa!
Mbwa akifukuza sungura,hutokwa jasho jingi na povu mdomoni;
lakini mara anapokamata ‘Apwoyo’ sungura, binadamu humpora kasha huchukua
minofu na kumtupia mbwa mifupa na matumbo! Mbwa hula makombo,pamoja na kulinda
mali ya binadamu utadhani yake, wakati wa hatari, wa baridi,mvua-jua lake mvua
yake!!
Eti huyu binadamu ndiye “Lord of all animals”,
KATILI,mbinafsi ndiye anayeamrisha wanyama wote kufanya kazi na kumpa yeye
chakula,kiburi na utajiri,anasa!
“Hata kinyesi cha wanyama ni mbolea.Kazi ya binadamu ni
kulewa pombe na machangudoa,kulewa sifa na mafanikio hewa.”
Hizi kauli za wanyama zilitia simanzi.
Kwamba, ingawa wanyama ni chanzo cha mapato na kiburi cha
mwanadamu katili, bado wanyama hawamiliki chochote wanachozalisha kasoro ngozi
zao tu!
Ng’ombe hawamiliki hata galoni moja ya maziwa,miongoni mwa
mabilioni ya papipa ya maziwa yanayokamuliwa kila mwaka na kuuzwa ama kunywewa
kila siku!Kuku hawakuwa na haki hata ya kula yai moja.
Vyote,binadamu akafakamia.Kuku akila yai hata moja alilotaga,
ni kosa. Mwisho wa siku hakuna mnyama anayenusurika kwa makali ya jisu!
Kuchinjwa!!
Hata mbwa aliyejitia ‘rafiki’ wa binadamu,pindi anapozeeka
na kuishiwa meno mdomoni, anaposhindwa kubwekea adui kwa maradhi na kuachwa nje
kila siku, hufungwa kamba nene shingoni na kutupwa katika shimo refu, asiweze
kuokoka!
Wenye masikio na wasikie.
Naam, kwa kifupi, sera za shamba la wanyama zilikuwa na
mashiko,ili kuuelekeza umma wa SHAMBA LA WANYAMA kufanya mapinduzi=mabadiliko.
Maslahi ya wanyama hayakuwepo isipokuwa
dhuluma,kudharauliwa,utumwa na unyang’au wa binadamu.
Binadamu walijiona “Aloof” walijiona wako juu kuliko
wanyama,walijiona “Better than Animals”.
UNAFIKI WA
KUTISHA
Hata hivyo,licha ya sera za wanyama kuitikisa nchi,mapinduzi
yalipokuja(mabadiliko) viongozi wa shamba la wanyama wakayateka
nyara.Wakabadili amri muhimu za usawa,amri zikaanza kusomeka hivi:
“ALL ANIMALS ARE EQUAL,
BUT SOME ANIMALS ARE MORE EQUAL THAN OTHERS!”
Kwamba, ingawa wanyama wote ni sawa, baadhi yao(viongozi
wateule wa mungu) walikuwa na usawa zaidi kuliko wenzao!
Nguruwe walipofanikiwa kuongoza mapinduzi ya kumtimua
binadamu kwa mapinduzi makali, walianza kulewa pombe, afadhali ulevi wa pombe
kuliko kulewa madaraka!
WALIVAA SUTI za binadamu!Mnyama kuvaa suti ya binadamu mkia
nje!!Kanuni za usawa zikatupwa chini,wanyama wakakosa haki na usawa
waliotegemea wakati wakifanya uasi dhidi ya mwanadamu.
Ndoto ya ukombozi ikaanza kupotea,demokrasia ikatupwa
shimoni, wanyama wakaanza kusema, “Heri utumwa wa kwanza kuliko wa sasa!”Wenye
masikio na wasikie.
Nguruwe, walioongoza mapinduzi,wakidai usawa na
demokrasia,wakaanza kukataa kuulizwa ‘Mapato na Matumizi’ ya Shamba la Wanyama!
Kuhoji hesebu za shamba la wanyama ikawa kujitafutia kifo ama kuchapwa
mijeledi!
Ukihoji kwanini hata
uchaguzi wa viongozi ndani ya shamba la wanyama, hakuna? Unaambiwa msaliti!
Umetumwa na binadamu kuvuruga shamba la wanyama!
Unatimliwa kinyama,unavuliwa hata ngozi yako uliyopewa na
Mungu! Unachapwa bakora!Wenye masikio na wasikie.
Uhaini! Eti kuhoji hesabu za shamba la wanyama ni
uhaini,usaliti! Ufisadi? Hamtaki kuulizwa Mapato na Matumizi ya SHAMBA LA
WANYAMA?
Nguruwe, hamtaki uchaguzi huru wa uhuru na haki? Hamtaki
kuulizwa mhula wenu wa uongozi utakoma lini? Mnaanza kusingizia wanyama wenzenu
kusaliti SHAMBA LA WANYAMA? Mizengwe,kuvuliwa ngozi yako uliyopewa na
Mungu-This is abuse of political power.
For this reason animals have even less freedom than before.
Wenye masikio na wasikie kilio cha shamba la wanyama Tanzania hii!
Itaendelea
0713 324 074