Friday, December 6, 2013

NAMLILIA TATA MANDELA



NELSON MANDELA MNARA WA KUMBUKUMBU YA UHURU AFRIKA
Na Conges Mramba
Obama alipokuja Dar es salaam wakati hakuwahi kusahau hujuma kama hizi na zile za Kanisa la Anglican, za kuwaweka mhuri wa moto mgongoni Waafrika wenzetu waliofanywa watumwa-The Transafrica Slave Trade-waliobandika mihuri ya “society”, migongoni!

Napenda kumwambia Barak Hussein Onyango Obama,kwamba urais wake Marekani umekuja baada ya harakati za ukombozi za akina  Nelson Mandela, Malcolm X,Martin Luther King Jr, na wenzao ambao walijikuta wakiuliwa na Pentagon ama kufungwa  maisha kwa uhaini.

Mandela sasa atalala kaburini, lakini  jina lake litabaki kama mnara wa kumbukumbu ya mapambano ya Mtu Mweusi kutafuta Uhuru na Haki.
Wakati Obama anapojitia kushutumu tawala za kiimla, Authoritarian regimes, asisahau kwamba serikali ya nchi yake imekiuka haki za msingi za Weusi kwa kuwaunga mkono majambazi kama Savimbi,majeshi ya Makaburu,Wareno na makampuni ya kifisadi kuihujumu Afrika.
Wakati ule,Marekani iliungana na Makaburu wa Afrika Kusini kumsaka Tata Mandela kama gaidi,na ilihusika kuua na kuhujumu harakati za ukombozi kwa kushirikiana na Shirika lake la Ujasusi,CIA.
Nigeria kwa mfano, inasemwa Boko Haram wameua watu 1000 wakati ukweli ni kwamba hata makampuni ya mafuta ya Magharibi kama Elf,Agip, Royal/Dutch Shell,Chevron n.k wamehujumu raia wa Niger Delta,waliodai haki zao zama za utawala wa Dikteta Sani Abacha,ambaye wao walibeba sana kwenye mbeleko hadi akawaua akina Ken Saro-Wiwa.
Makampuni ya Marekani,Ufaransa na Uingereza yameua watu wangapi Kusini mwa Nigeria kulinganisha na Boko Haram?
Zaidi ya dola bilioni 400 za mafuta zimeporwa na makampuni hayo tangu zama za uhuru hata sasa huko kwa Waogoni,Igbo,(Biafra) na Yoruba.
Obama, anapozungumza utawala bora na demokrasia ana maana gani kama makampuni ya Magharibi yanashiriki unyonyaji, na dhuluma hapa Afrika.
Na yumkini Obama akaja Afrika wakati Mandela akiwa tayari katika kitanda cha mauti. Urais wa Obama,ni matokeo ya harakati za Mtu Mweusi kudai haki,vinginevyo asingekubaliwa kuwa Rais wa taifa hili beberu sana duniani
RAIS BARACK Hussein Onyango Obama, aliwasili katika miji ya Dakar,Johannesburg,Pretoria na Dar es salaam, mwezi Julai Mandela akiwa anashindana na kifo katika kitanda cha Mauti, MediClinic
Baadaye, akarejeshwa nyumbani mjini Johannesburg ambako Desemba 5 mwaka huu 2013, saa 2:57 hivi usiku akaaga Dunia huku familia yake ikimsindikiza kuzimu.
Afrika ilikuwa chini ya ulinzi wa makachero wa Marekani,Obama alipotua katika ardhi ya Afrika,Julai mwaka huu, Mandela alipolala usingizi usiojulikana mustakabali wake huko Mediclinic.
Hatimaye sasa amefariki dunia baada ya kuugua muda mrefu.
Ujio wa Obama,Afrika naam,Afrika Kusini, Senegal na Tanzania kitovu cha harakati za Ukombozi wa Mtu Mweusi, wakati huu wa mashaka ya kuishi au kufariki kwa Mandela, unatupa kurejea historia.
HISTORIA YA MAPAMBANO YA MTU MWEUSI imetamalaki tangu Bahari ya Hindi hadi Pwani ya Atlantiki.
Mzungu wa kwanza kufika Rasi ya Tumaini Jema(Cape of Good Hope),Afrika ya Kusini, Bartholomew Diaz,mwaka 1485 ilikuwa ni katika safari za kwenda India
Muongo mmoja na ushee hivi baadaye,(1497-98) alikuja Vasco Da Gama;hawa Wareno wakizunguka dunia ili kujua ilivyoumbwa-huu ulikuwa mwanzo wa Utandawazi.
Ni wakati huo, Amerigo Vespucci wa Italia alipofika Pwani ya Amerika Kusini mwaka 1497-99,Zama hizo(1492-1502) ndipo Christopher Columbus wa Italia alipofika hasa Marekani na kunakoitwa, West Indies.
Huu ndio wakati wageni kutoka Ulaya walipoanza safari za kwenda Afrika ya Kusini ambako walisimika tawala zao za kidhalimu kwa zaidi ya karne nne, hadi Mandela alipozaliwa Julai 18 mwaka 1918.
Nataka kueleza namna Wazungu walivyofika Afrika na kuanzisha tawala za kidhalimu,kisha wakachukua ndugu zetu kuwa watumwa Marekani, ambako pia walitawala kabla ya Marekani kupata uhuru Juni 4,mwaka 1776.
Mandela, ameishi kwa taabu na wapigania uhuru wenzake wakijificha-ficha wasiuliwe ama kukumbana na kifungo cha maisha jela.
Rais wa kwanza Mzungu katika Bara la Afrika, FW De Clerk ,alizaliwa Machi 18,mwaka 1936 mjini Johannesburg,wakati tayari Mandela akiwa katika madhila ya ukoloni,Afrika ya Kusini.Huyu De Clerk, ndiye aliyekuja kumwacha huru Mandela Feburuari 11,mwaka 1990.
Mandela ameachwa na mkewe kufuatia harakati za kujificha-ficha asikamatwe,hakufika nyumbani muda mrefu, na laifukuzwa Chuo Kikuu cha Port Hare kwa kosa la kujihusisha na migomo huko Transkei.
Alijisomea nyumbani akatunukiwa shahada ya kwanza,BA.
Alitiwa mbaroni 1952,1956,1962 na 1964 akafungwa kifungo cha maisha gerezani.
Wakati Mandela anafungwa huko Afrika Kusini,Mtu Mweusi(Negros) hakuwa na ruhusa kuoa Mzungu katika majimbo 19 ya Marekani,na Afrika Kusini ilikuwa Mzungu akikukuta ndani ya basi umeketi,unampisha kiti!
Naam, ni wakati huu kulikuwa na Mitaa na mahoteli Mweusi huwezi kukanyaga,inaandikwa mlangoni, ‘For Whites Only’!
Marekani na Afrika ya Kusini zilifikiwa na wapelelezi(explorers) wakati mmoja,zikajikuta makoloni ya wageni,wakati Marekani inapata Uhuru mwaka 1776 kutoka Uingereza Afrika Kusini ilibaki chini ya makucha ya Waingereza, na baadaye Makaburu wabaguzi wa rangi.
Rais Barack Hussein Onyango Obama, anatua Afrika Kusini wakati Mandela roho yake inapokuwa ikishindana na malaika wa kifo huko MediClinic; akiwa anapumulia mashine.
Obama, amezaliwa Agosti 4, mwaka 1961 wakati harakati za Uhuru zikiwa zimepamba moto duniani.
Ubaguzi wa rangi ukiwa umepamba moto hata Marekani kwenyewe, ni wakati huu huu mamaye Obama,Ann alipokuja kutengana na Hussein Onyango Obama,akaolewa Indonesia akaishi Jakarta.
Nataka kusema kwamba, huyu mamaye Obama, alipata msuko-suko kuolewa na ‘Mjaluo’ wa Kenya-Afrika, akaondolewa chuoni alipopata ujauzito wa Obama, mama huyo akiwa na umri wa miaka 18!Alionja madhila ya ubaguzi wanaoshuhudia akina Eto'o siku hizi!
Hizi ndizo zama akina Martin Luther King Jr, walipowindwa mithili ya nguruwe pori, walipinga ubaguzi wa rangi kabla ya kuuliwa na Pentagon mwaka 1968.
Obama,huyu aliyeko Dar es salaam sasa, alizaliwa Honolulu huko Hawaii na mama Ann Dunham,mzaliwa wa Wichita, Kansas.
Kwa mara ya mwisho Obama alikutana na Mandela mwaka 2005 alipokuwa angali Seneta; na safari hii alitarajia kukutana na Mandela akiwa Rais wa Taifa baguzi la rangi…
Bahati mbaya,Mandela yu kimya kitanda cha mauti; kauli haitokei tena kumwambia Obama, “The change has Come to America! The change must come  to Africa!!” Hata kama Obama atahudhuria mazishi.
Hussein Onyango Obama, aliachana na Ann, Barack akiwa na miaka miwili,sababu ni mbinyo na ubaguzi wa rangi,wakati huo akina Martin Luther King Jr,Malcom X na wenzao sheria ziliwapiga marufuku kumuoa Mzungu.
Naam, Obama na bintize,Malia na Sasha, ni Weusi wenye damu halisi ya Afrika,wakati huu wanapokuwa nyumbani Afrika.
Obama, kasoma Indonesia,kasha Honolulu kabla ya kusoma vyuo vikuu vya Columbia na Harvard,chini ya usaidizi wa mamaye na nyanyaye, Madelyn Dunham.
Huyu nyanya alikufa wakati Obama akifanya kampeni mwaka 2008.Ilikuwa Novemba 3,mwaka 2008.
Mkewe Obama, Michelle, ni binti wa Fraser na Mariam Robinson,mabaki ya watumwa ndugu zetu waliopelekwa Marekani kulima miwa katika mashamba ya Mzungu.
Hawa ndugu zetu-Obama na Michele-wametua Dakar,Johannesburg,Pretoria na Dar ili kukumbuka nyumbani takriban miezi sita iliyopita.
Obama alikusudia kuzulu kisiwa cha Robben alikofungwa Mandela kwa miaka 18, alizaliwa Julai 18 mwaka 1918, akafungwa Robben kwa miaka 18, na De Clerk aliyemwachia huru alizaliwa Machi 18,mwaka 1936.
Obama alifika Robben.Naam mahali ambako patabaki kama kumbukumbu ya utumwa na ukoloni Afrika.
Mandela, amefungwa jumla ya miaka 27;zamani kisiwa cha Robben kilitengwa kwa sababu ilikuwa ni koloni la wakoma-Leper colony.
Kwa takriban miaka 30,utawala wa Makaburu uliwafunga maelfu ya Waafrika Weusi waliopinga ubaguzi wa rangi mahali hapa.
Mwaka 1987(miaka mitano baada ya Mandela kuhamishwa kutoka kisiwani hapo kwenda Bara) eneo hilo liligeuzwa Kivutio kikuu cha utalii.
Mandela alifungwa Robben miaka 18; eneo ambalo Obama huenda amefika,ili kukagua mateso ya Mtu Mweusi-Mandela na wenzake- ndiyo akina Walter Sisulu, Goven Mbeki, na viongozi wengine wa African National Congress(ANC) na Robert Sobukwe wa Pan Africanist Congress.
Wafungwa hawa,Mandela,Mbeki,Sisulu na wenzao waliponda kokoto bila viatu mchana wa hari-vumbi liliishia kifuani Mandela akaugua kifua.Asskari walinzi wa gereza waliwakojolea puani,wakati mwingine walilazimishwa kuoga maji ya baridi.
Jela ya Robben ilikuwa na vitanda 600;mahali ambapo hata baada ya mauti kumkumba ‘TATA’Mandela,itabaki kumbukumbu ya mateso ya mtu Mweusi wakati wa madhila ya ukoloni na ubaguzi wa rangi.
Waziri wa Sheria wa Makaburu, Cobie Coetsee, akahamuru akaina Mandela wahamishwe,wawachie ndege makazi.Kumbuka lilikuwa eneo la kutupwa wakoma,hakuna aliyeishi maeneo haya.
Siku hizi,kunajengwa mahoteli ya fahari na ni kituo cha utalii-a world class attraction! Obama,Michelle,Malian na Sasha, wanafurahi kukanyaga alipofungwa ‘Tata’Mandela.
Lilikuwa eneo la kuzika wakoma,katika selo nambari 30 B katika chumba kidogo cha mita 2 kwa 2 ndipo alipolala mtu huyu mwenye urefu wa mita 2.
Alijifunika shuka la kijivu na blanketila sufu rangi ya kahawia, taulo la samawati.
Gazeti la TIME la Julai 1991,LILIMKARIRI Brigedia Erika Van Zyl, Ofisa Uhusiano wa gereza hilo akiwakaribisha watalii mahali hapo na kusema mahali hapo ni ‘A world class attraction!
Zama za utawala wa Makaburu,hapa palikuwa The Worst Part of Imprisonment!
Hata hivyo, Mwandishi, Scot Mac Leod, aliandika katika gazeti hilo la TIME,Julai 22 mwaka 1991,mwaka mmoja baada ya Mandela kuachiwa huru na de Clerk,kwamba Brigedia Erika van Zyl,aliwakaribisha mahali hapo Robben, alikofungwa Mandela.
Bila shaka,hata kaburi la Mandela litageuka ‘Tourist Site’ maarufu hapa Afrika na dunia nzima.
Hakika,Mandela ameishi duniani bila raha na amani,sasa akifariki atazikwa katika kisiwa cha amani ya milele.
Kwa Obama, kitabu cha ‘Dream from my Father’ kilichoandikwa na  wakati babaye anarejea Kenya, ni kumbukumbu tosha Obama kutomsahau Mandela,Nyerere,Samora Machel,Kwame Nkrumah na wenzao, zama za harakati za Mtu Mweusi, akina Martin Luther King Jr, naam akina Malcolm X.
Obama, amekuwa rais wa taifa beberu lililounga mkono ubaguzi wa rangi akiwa na umri wa miaka 47, na sasa anapokuwa Dar atambue msingi wa Urais wake ni Mandela,Nyerere,Kwame Nkrumah,Patrice Emery Lumumba,Martin  Luther King Jr, mama Coletha King na wenzao mashujaa wa kupinga ubeberu na ubaguzi wa rangi.
“The change has come to America; and it must come to Africa too!
Buriani tata MANDELA,Mfungwa maarufu kuliko wote duniani aliyegeuka Shujaa kuliko wote duniani, amelala kitanda cha mauti,lakini atakuwa hai milele kwa   ‘legacy’ yake
0786 324 074/0713 324  074









Buriani Mandela!
0713 324 074







  •  

MANDELA BADO YU HAI HATA MILELE

MWANAHALISI wa Afrika, “The Great Son of Africa”, “Tata” Mandela, amepumzika kaburini baada ya kuwa mahututi tangu Juni mwaka huu.
 Ilikuwa vigumu Mandela kuishi katika hali ya maradhi mabaya ya mapafu na kupumulia mashine tangu awe mahututi miezi sita iliyopita.
Sasa,Mandela amefariki nyumbani kwake Desemba 5, saa 2: 57 usiku huko Johennesburg.
Binafsi,nilikuwa nimepoteza matumaini ya mtu huyu nimpendaye sana kuishi,japo afikishe miaka 100 kamili ifikapo Julai 18,mwaka 2018.
Nelson Rolihlahla ‘Madiba’ Mandela, alizaliwa Julai 18 mwaka 1918 katika kijiji cha Mvezo,katika Jimbo la Eastern Cape,Afrika ya Kusini.
Alikuwa mwanaharakati mashuhuri sana katika kupinga ubaguzi wa rangi wa Chama cha African National Congress(ANC)kinachoongoza sasa Afrika ya Kusini.
Miaka 27 ya uhai wake aliitumia akiwa jela,kufuatia harakati zake za kuwapinga Makaburu wa Afrika Kusini na siasa zao za Kibaguzi zilizoungwa mkono na Mataifa makubwa ya Magharibi.
Muda mwingi akiwa jela, akawa anaponda kokoto mchana wa hari akiwa hana viatu,hususan huko Kisiwa cha Robben,ambacho sasa ni kituo cha utalii.
Watu huenda kuona chumba alicholala shujaa huyu wa karne hapa Afrika na dunia nzima.
Namba yake ya jela, ‘46664’ itakaa kama ALAMA ya harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika, na katika harakati za uhuru hapa Barani.
Mtu huyu, ambaye sasa ni marehemu,aliachiwa huru na Makaburu Feburuali 11 mwaka 1990, na akawasamehe waliomsweka jela kwa jumla ya miaka 27.
Ni mzaliwa wa ukoo wa Thembu,katika kijiji cha Mvezo,wilaya ya Umtata,mji mkuu wa Transkei.Anatokana na ukoo wa Chifu Ngubenguka(alifariki 1832).
Babaye, Gadla Henry Mphakanyiswa(1880-1928) aliwahi kuwa chifu wa Mvezo,akapokonywa uchifu na wakoloni wa Kiingereza.
Mzee huyo alikuwa na wake wanne,akazaa watoto 13,Mandela alikuwa mtoto wa mke wa tatu,NESEKENI FANNY,Binfi wa Nkedama wa Mpemvu,wa kabila la XHOSA.
Jina la Rolihlahla maana yake ni ‘Kuvuta Tawi la Mti’ lenye kumaanisha ni mtu mwenye fujo!
Akiwa na umri wa miaka saba alikwenda shule, mwalimu wake aliposhindwa kutamka jina la Rolihlahla, akampa jina Nelson kwa heshima ya Mkoloni Mwingereza,Horatio Nelson.
Baba yake alifariki Mandela akiwa na miaka tisa tu; ikabidi sasa alelewe na rafiki wa baba yake.Mandela alisoma shule ya misheni ya Wesleyan.
Akaingia jandoni akiwa na umri wa miaka 16,kabla ya kwenda kusoma Clarke bury Insitute,alikotunukiwa cheti.
Aliwahi kucheza ndondi na riadha.Hapa namkumbuka mwanamasumbwi Nguli,Mweusi wa Marekani aliyetukanwa udongo wa mfinyanzi kufuatia kuwa Mweusi,Mohammed Ali.(Clay).
Mandela, alisoma Shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Port Hare, alipokutana na Mpigania uhuru mwenzake,Oliver Tambo.
Tambo, alikuja kuwa kiongozi wa ANC kabla ya kufariki dunia.Mandela aliwahi kuwa karani katika kampuni sheria mjini Johannesburg; alisaidiwa kupata kazi na Walter Sisulu.
Baadaye, alisoma sheria Witwatersand, ambako alikutana na wanaharakati wengine.Mandela na Oliver Tanbo waliendesha kampuni ya uwakili ili kuwasaidia Weusi waliokuwa wakikumbana na madhila ya kunyanyaswa na Makaburu.
Desemba 5, mwaka 1956 Mandela na wenzake walitiwa mbaroni na wenzake 150 na kushitakiwa kwa makosa ya uhaini-walishinda kesi hatimaye wakaachwa huru.
Johannesburg,ndiko aliswekwa rumande baadaye,baada ya kutafutwa sana na Shirika la Ujasusi la Marekani,Central Intelligence Agency(CIA).
Nataka msomaji,hasa vijana wa siku hizi kujua kwamba Marekani na washirika wake,waliwasaidia Makaburu na wakoloni wengine kuwahujumu Weusi wasije kujitawala siku moja katika nchi zao wenyewe.
Naam,leo hung’ata na kupuliza,na wajinga wote wanaona Mataifa haya ndiyo ‘Masihi’ na mabingwa wa demokrasia na Haki za Binadamu,kumbe ujinga mtupu!
Marekani na Shirika lake la CIA ambao hupigiwa goti siku hizi,wakishirikiana na Makabuu wa Afrika ya Kusini na tawala za Kiimla(Authoritarian) wakamshitaki Mandela kwamba alichochea mgomo wa wafanyakazi na kutoroka nchini kinyume cha sheria.
Yawezekana,ni wakati huu Mandela na wanaharakati wenzake walikuwa Mazimbu,Morogoro katika Makambi ya wapigania uhuru-Tanzania.
Oktoba 25 mwaka 1962 Mandela alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.Akiwa jela, huku nyuma polisi wa Makaburu waliwasweka rumande wanaharakati wengine wa ANC, akina Walter Sisulu,Govan Mbeki na wenzao.
Juni 12 mwaka 1964 wakahukumiwa kifungo cha maisha jela.
Kati kesi hiyo MANDELA pia aliunganishwa,wakapelekwa Kisiwa cha Robben mahali ambao Mandela akakaa miaka 18.
Kazi yao ilikuwa kugonga miamba na kuipasua ili kupata kokoto za kujengea jela imara sana za Makaburu ili wafungwa(WEUSI)wasitoroke.
Machi,1982 Mandela alihamishiwa Polls moor, akiwa na wenzake wa ANC akina Walter Sisulu.
Feburuari,1985 P.W.Botha, alimpa Mandela ‘Offer’ ya kuachiwa huru kwa masharti kwamba aachane na harakati za uhuru wa Mtu Mweusi.
Mandela alikataa ‘offer’ hiyo akatoa taarifa kupitia binti yake,Zindzi akisema:
“Uhuru gani ninaopewa wakati taasisi ya watu inabaki imepigwa marufuku? Hata hivyo,mfungwa hawezi kuingia mikataba!” Mandela aligoma kuachwa huru-uhuru bandia.
Wewe kijana wa sasa ulishaona wapi msimamo mkali wa Mwanahalisi wa Afrika (The Great Son of Afrika)  mithili ya MANDELA?
Makaburu WALIFANYA MKUTANO NA Mandela mfungwa mwaka 1985 Novemba, katika hospitali ya Volks, Cape town alipokuwa akitibiwa saratani-alikutana na waziri wa Makaburu,Kobic Coetsee.
Mwaka 1989,PW Botha aliugua kiharusi,nafasi yake ikachukuliwa na Frederic Willem de Klerk,rais wa Kwanza Kaburu Barani Afrika, wenzake walikuwa Mawaziri wakuu, akatangaza kuwa Mandela angekuwa huru mwaka 1990.
Waafrika tukafurahi,mtu huyu kipenzi cha watu kuwa huru
.Alipewa nishani ya Amani ya Nobel,yeye na De Clerk mwaka 1993.
Baadaye Makaburu walimuua Chris Hani,Aprili 1993.Mandela alikuwa rais Afrika ya Kusini akiwa na miaka 77 mwaka 1994, akaja kustaafu mwaka 1999.
Aliapishwa kuwa Rais wa kwanza Mweusi wa Afrka ya Kusini Mei 10, mwaka 1994,de Clerk akawa Makamu wa Kwanza wa rais na Thabo Mbeki akawa Makamu wa Pili katika serikali ya Umoja wa kitaifa kama ya Zanzibar hivi.
Utawala wa Makaburu(Boers)ulikumbatiwa na Uingereza na Marekani;wakati watu zaidi ya 14,000 (Weusi)walipouliwa huko Zulu,katika miaka ya 1980.
Tumeona Mobutu akisaidiwa na mataifa haya ambayo siku hizi hujidai ‘Masihi’ hapa duniani,na huimba demokrasia na Haki za Binadamu kwa midomo bila vitendo.
Mobutu,na hawa,waliwasaidia Waasi wa Angola kukipinga Chama cha Ukombozi, Popular Movement for the Liberation of Angola(MPLA),uhuru usipatikane kutoka kwa Wareno,hadi nchi ikabaki vitani kwa muda mrefu.
Mobutu na hawa rafiki zake, Ungereza na Marekani, walimsaidia Jonas Malheiro Savimbi na Chama chake cha Unita, kilichopinga uhuru wa Angola.
Tumeona harakati za uhuru nchini Afrika ya Kusini chini ya African National Congress (ANC) zikiwa zimeharamishwa na utawala dhalimu sana wa Makaburu hadi Rais De Clerk alipokuja kuondoa marufuku hiyo Feburuari 1990
“Tata”Mandela aliachiwa huru kutoka Greza la Victor Verster, lililopo Paarl Feburuari 11 mwaka 1990. Ni tukio la kihistoria kuachiwa kwa Mandela; ni kama Afrika ilipata uhuru mwaka 199
Mtu huyu, “Tata” Mandela,alitangaza msamaha kwa Makaburu waliomtesa; ikaunfdwa Tume ya Ukweli na Maridhiano(THE TRUTH COMMISSION) iliyoongozwa na Askofu Desmond Tutu.
Mandela alikiri chama chake (ANC) kuunda tawi la jeshi(Umkontho we Sizwe) kwa nia ya kujilinda na kujihami dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi; siasa zilizoandamana na dhuluma na mauaji ya kinyama dhidi ya wazalendo na harakati za ukombozi.
Mandela na De Clerk walitunukiwa baadaye tuzo ya Nobel ya Amani,mwaka 1993.Aprili mwaka huo 1993 ndipo Mpigania uhuru Chris Hanni alipouliwa na utawala wa Makaburu,rafiki wa Uingereza na Marekani.
Mandela, ameishi siku zote kama Mwafrika halisi; akachaguliwa kuwa rais mwaka 1994   akiwa na umri wa miaka 77-na alistaafu mwaka 1999 akamwachia kiti Thabo Mvuyelwa Mbeki,mmoja wa wana wa mashujaa wa mapambano dhidi ya Kaburu jeuri.
ANC kilishinda uchaguzi wa 1994 kwa asilimia 62 ya kura.Mandela aliapishwa kuwa rais wa Kwanza Mweusi Mei 10,mwaka 1994,wakati Kiongozi wa National Party, de Clerk akiambulia Umakamu wa Kwanza wa rais;wakati Thabo Mbeki alipopewa Umakamu wa Pili katika serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Naam, tunamkumbuka ‘Tata’Mandela kwa mashati yake ya Batiki.
 Ama ‘Mandela Shirts’ yanayovaliwa siku hizi hata na akina Rais Jakaya Kikwete.
Uchaguzi wa kwanza huru Afrika ya Kusini ulifanyika Aprili 26-29,mwaka 1994,ANC kikapata asilimia 62,National Party cha Makaburu kikapata asilimia 20.4.Inkhata Freedom Party cha Chifu Mangusuthu Butelezi kilipata asilimia 10.5.
‘Tata’ Mandela alipata kuoa mara tatu; ni baba wa watoto sita,wajukuu 22 na vitukuu vingi. Mmoja wa wajukuu zake ni Chifu Mandla Mandela.
Mzee huyu kipenzi cha Afrika alifunga ndoa ya kwanza na Evelyn Ntoko Mase kutoka kwao Mandela huko Transkei.Walikutana Johannesburg-walizaa wavulana wawili,Thembikile ama Thembi mwaka 1946,Magkatho alizaliwa 1950 na wasichana wawwili waliopewa jina moja,Makaziwe, “Maki” mmoja alizaliwa 1947 na mwingine 1953.Mwingine alifariki dunia kabla ya kufikisha umri wa mwaka mmoja.
Ndoa ya Mandela na Evelyn Mase ilivunjika baada ya miaka 13(mwaka 1957),Mandela alikuwa haonekani nyumbani kwa muda mrefu,akiwa ‘Msituni’katika harakati za Ukombozi,mama huyo na imani yake ya kilokole ya Mashahidi wa Jehova, aliamua kwenda zake,akaachana na Mandela.
Thembi, alifariki katika ajali  ya gari mwaka 1969 akiwa na miaka 25 wakati huo Mandela alikuwa selo, Robben Kisiwani.Hawa watoto walisoma shule moja,baadaye Evelyn alifariki dunia 2004.
Ndoa ya pili ya Mandela ni ya Winnie Madikizela-Mandela, huyu ‘Iron Lady’ kutoka Transkei.Watoto wa Mandela na Winnie ni wasichana wawili:
Zenani au Zeni(Feburuari 4,1958) na Zindzishwa ama Zindzi aliyezaliwa 1960.
Walitengana Aprili 1992; mwaka 1996 waliachana kabisa.Juzi, Winnie alikwenda kumtembelea  Mandela hospitalini anakolazwa.
Kaka mkubwa wa Mfalme wa Swaziland,Mswati III,Prince Thumbumuzi Dlamini alimuoan Zenani mwaka 1973,na wanaisti Boston,Marekani.
Mwaka 1998,Mandela alimuoa Graca Machel nee Simbine wakati alipokuwa akiadhimisha ‘Birth Day’ ya 80.
Mwaka 2003,Cable News Network(CNN) walitangaza tanzia ya Mandela.Mwaka 2007 pia ‘wasela’walitangaza kifo cha Mandela,wakiwataka Wazungu kwenda kwao,la sivyo wangechinjwa!
Mtu huyu, ‘Tata’ Nelson Mandela ni kielelezo cha Mzalendo wa kweli,Mwanahalisi wa Afrika aliyeitwa ‘Gaidi’ na utawala wa Makaburu wa Waziri Mkuu PW Botha, aliyejiuzulu Agosti 14, mwaka 1989 ndipo akaingia De Clerk aliyemwachia huru Mandela.
 Utawala wa Makaburu uliua watu wengi,si Afrika Kusini tu bali hata Msumbiji walifanya njama na kumuua Samora Machel mwaka 1986.
Naam,namkumbuka ‘Tata’Mandela, ambaye namba yake ya jela ilikuwa 46664. Tunawakumbuka wanamapinduzi wa Afrika ambao wamemwaga damu wakipigania uhuru wa watu wao, si ulaji wa matumbo  yao kama watu wengine wanavyotaka kuitwa leo.
Namkumbuka Samora Moises Machel,John Garang de Mabior ‘ Chris Hani na wenzao.


Monday, December 2, 2013

SHAMBA LA WANYAMA(2)



      
BINADAMU dhaifu hawawezi kufanya chochote cha mafanikio yake bila msaada wa wanyama?
Hatavikosi vya usalama katika tawala zilizofanikiwa sana za wanadamu, haviwzi kubaini hatari za milipuko ya mabomu pasipo kushirikisha mbwa,panya n.k ili kudhibiti hatari za magaidi kama al-Qaeda, al-Shabaab n.k
Novemba 29 mwaka huu huu, pal kwenye Uwanja wa CCM Kirumba,Mwanza wakati wa ujio wa Kombe la Dunia(Fifa World Cup Trophy) na Rais Jakaya Kikwete, nikaona polisi na Usalama wa Taifa,wakiwatumia mbwa kunusa kila kiti,kila meza,kila chumba na hata magari yalinuswa na mbwa zaidi ya mmoja,ili kubaini hatari!
Mbwa mdogo wa Usalama, mwnye madoa meusi na meupe,na mkanda shingoni, akang’ang’ania chupa tupu ya Coca-Cola mdomoni mwake!
Alikuwa ndiyo kwanza katoka kunusa jukwaa na vifaa vilivyokuwa jirani,njiani akakutana na hizo chupa tupu zilizokuwa chini, akachukua moja mdomoni mwake na kuanza kuondoka nayo,utadhani alibaini bomu ndani mwake!
Alipomaizi kuwa mbwa Yule alikuwa akifanya mzaha, askari Yule alimpokonya mbwa huyo mwenye cheo hiyo chupa tupu na kuitupa.Mbwa Yule alitaka kuirudia kisha akaendelea na hamsini zake.
Naam, katika sehemu iliyotangulia ya makala haya,tuliona haja na MAPINDUZI katika kizazi cha wanyama(pamoja na jamii ya wanadamu),kwamba mabadiliko katika maisha ni hitaji la msingi wakati wote ili kuboresha maisha.
Mapinduzi yanapaswa kufanywa kwa makini ili kuleta mabadiliko chanya na aslani siyo mabadiliko hasi yatakayoleta majuto baadaye.
Ustawi wa kundi moja la wanyama,wakati mwingine hugeuka janga la kutisha kwa kundi linguine.Ustawi wa samba na mbwa mwitu huleta mauti kwa jamii ya wanyama walao nyasi. Ustawi wa tembo na hata nyati hulta kilio kwa mashamba ya mwanadamu.
Ustawi wa binadamu husababisha karamu kila siku na hivyo wanyama hujikuta wakichinjwa kila asubuhi na jioni.
Hata hivyo, binadamu ni mnyama mharibifu zaidi kuliko wanyama wote(man is only creature that consumes without producing).Binadamu hazalishi chochote yeye mwenyewe, hawezi hata kukokota jembe la kukokotwa na wanyama kazi(plough),hatagi hata yai moja,wala hawezi kurutubisha ardhi anayoiharibu kila siku.
Hii ni kazi ya wanyama ambao hata kinyesi chao ni mbolea safi. Kitu kinachozalishwa na wanyama huishia katika koromeo la binadamu huyu Dikteta na fisadi!
Naam, huu ndiyo uliokuwa mwito wa wanyama kutaka MAPINDUZI dhidi ya udikteta wa mwanadamu. Bahati mbaya mwito wa mapinduzi uligeuka UASI(rebellion) ulioishia kuleta majuto kwamba, “Heri utumwa wa mwanzo kuliko wa sasa!”
Kwa akili za wanyama, walidhani uasi dhidi ya binadamu,haki(justice) ingekuja yenyewe,na maslahi ya wanyama yangepatikana midhali binadamu fisadi alikwisha timuliwa katika umiliki wa SHAMBA LA WANYAMA.
Dhima ya wanyama ilikuwa, “PERFECT UNITY and PERFECT COMRADESHIP IN THE STRUGGLE”katika harakati za kuondokana na minyororo ya utumwa dhidi ya mwanadamu, wanyama waliona binadamu pekee alikuwa adui yao.
Na kwamba wanyama wote walikuwa ndugu na washirika wa kwale katika harakati za kutafuta ukombozi wa kweli(comrades),kumbe walisahau kwamba hata baadhi ya wanyama walitamani kuishi na kunyonya wqanyama wenzao mithili ya binadamu!
Kulikuwa na akina mbwa,hawakuwa tayari kuishi na sungura pasipo kuwakamata na kuwaua ili kupata kitoweo. Paka hawakuwa tayari kuishi bila kuwafukuza panya,mwewe hakutaka kuacha kuwapora vifaranga n.k
Nataka kusema kwamba,ilikuwa kazi ngumu jamii ya wanyama kujenga upendo wa kweli, uhuru wa kweli,haki na demokrasia halisi kulingana na sheria saba(amri)walizojiwekea zenye maudhui kwamba, “ALL ANIMALS ARE EQUAL”
Njozi yao ilikuwa
, “Golden future time… .Tyrant man to be overthrown and the fruitful fields of Tanzania to be trod by beasts- alone!
Wanyama waliota, siku za usoni utawala katili wa mwanadamu upinduliwe na kutimuliwa daima ili ardhi yenye rutuba inayozalisha maziwa na asali ibaki mikononi mwa jamii ya wanyama pekee!
Wanyama wanapotamani kuvunja minyororo ya utumwa ya jamii ya mwanadamu ili kujipatia uhuru kamili, walisahau kwamba miongoni mwao baadhi yao hawakuwa na nia dhati ya uhuru.
Baadhi yao walijiona bora kuliko wenzao, walikumbatia ubaguzi wa nasaba zao, majimbo yao ama mikoa yao,jamii zao na hata koo na makabila yao-ndiyo akina nyau dhidi ya panya,mbwa dhidi yap aka n.k
Walipigia kelele dhuluma ya mwanadamu dhidi ya wanyama,wakasahau MAPINDUZI sharti yaanzie katika fikra na mitazamo yao kwanza,yaani wote wakubali kuthamini usawa na uhuru wa kila mnyama.
Maslahi binafsi ya baadhi ya wanyama kama akina Nguruwe waliokuwa viongozi, ndiyo kilikuwa chanzo cha majuto makubwa,na ubaguzi wa kinasaba,kijimbo na kikabila hata wanyama wakalia kwamba, ‘Heri utumwa wa zamani kuliko wa sasa!
Miongoni mwa wanaharakati katika SHAMBA LA WANYAMA,kulikuwa na “Spies” na ‘Tale-Bearers” wachuuzi wa wenzao,waongo na wanafiki wakubwa,wasemaji wazuri,waliopigiwa makofi na kupata wafuasi wengi wa makundi ya wanyama,hususan wale wanyama wadogo.
Wapiga debe wengi walioitwa ‘Wapiganaji’ ama ‘wapambanaji’ wakatabiri “The existence of mysterious country called, SUCARCANDY MOUNTAIN”.
Nchi ya maziwa na asali ambayo baada tu ya binadamu kupinduliwa,jamii ya wanyama ingekwenda kuimiliki,nayo ni chi ya utamu mithili ya asali. SUGARCANDY MOUNTAIN eti ni Mlima wa vinono, ambako wanyama wangefanikiwa kuishi tu baada ya kufa!!
Eti hii nchi ilikues angani, ikiwa imejaa meza za vinono(sweets) juu kuvuka mawingu!!
Moses, alikuwa mpigadebe wa siasa za uchochezi kuwafanya wanyama wenzake wavunje sheria ili wafe ili rahisi kuifikia ile nchi ya siri katika Mlima wa sukari-SUGARCANDY MOUNTAIN!!
Yeye, Moses hakufanya kazi yoyote zaidi ya kupiga ‘politiki’(Tazama Animal Farm uk 10)licha ya kuleta uongo kwa wanyama, aliwahimiza kumwaga damu ili kufikia ile  sugar candy mountain.
Wakati akifanya haya,yeye Moses alikuwa akivunja sheria walizojiwekea.Alikula akiguguna kwa wizi mkate uliokuwa umechovywa ndani ya pombe(Kumbuka Amri ya 5 ilisema ilikuwa Marufuku wanyama kunywa pombe)huko katika shamba la wanyama la Uingereza!
Ilipotokea wanyama wakapata uhuru,kufuatia utawala wa binadamu kutimuliwa, viongozi hawa wanafiki wa shamba la wanyama walianza kujifanya nao ni binadamu,wakageuza sheria ambazo zilianza kusomeka hivi:
ALL ANIMALS ARE EQUAL, BUT SOME ANIMALS ARE MORE EQUAL THAN OTHERS!”
Wanyama viongozi-akina nguruwe-walikwenda mbali wakaanza kulewa pombe,kuvuta sigara,mtemba, kusoma magazeti ya binadamu kama Daily Mirror n.k
Wanyama viongozi walianza kuvaa suti,hususan za binadamu kinyume cha sheria(Rejea Amri saba za wanyama katika sehemu iliyotangulia)wakafanya vikao ku-compromise na binadamu katika vikao vilivyoandamana na ulevi na ulaji wa nyama za wanyama wenzao!!
Matokeo, wanyama viongozi-nguruwe- waliafiki wanyama wadogo wafanyishwe kazi nyingi za kuvuja jasho,kazi za harubu,halafu ujira ni chakula kidogo-DHULUMA.
Wanyama walioitana,comrades,rafiki,mwanachama ama ndugu,sasa baadhi yao wakataka waabudiwe utadhani miungu.
Jina SHAMBA LA WANYAMA(ANIMAL FARM) wakataka libadilishwe na kuitwa, ‘Manor Farm’ yaani shamba ndani ya jumba kubwa la zamani lenye shamba lililomilikiwa na kigogo “VIP”.
Wenye masikio na wasikie! Inakuwaje wanyama wenye usawa miongoni mwao wawemo ‘VIP(VERY IMPORTANT PERSONS)?
Mwisho wa siku,jamii hi ya wanyama ikaishia kwenye ugomvi mkubwa sna kufuatia tuhuma dhidi yao,wanadamu na wanyama wakarudi kukubaliana kudhulumu wanyama haki zao na demokrasia.
Kitabu hiki SHAMBA LA WANYAMA kiliandikwa Novemba mwaka 1943 hadi Feburuari 1944,ni somo kwetu kwamba harakati za kutafuta haki,demokrasia na usawa hazifanywi kwa kukurupuka kwa kujumuisha nguruwe,mbwa,mbwa mwitu n.k
Wanyama wadogo wanapaswa kuwa na akili kutambua kuwa wanadanganywa sana na kutumiwa. Ukitaka kujua,ni kwamba ukihoji maslahi(mapato na matumizi ya shamba la wanyama) utaitwa, “Traitor” someone who helps an enemy against his own people.
Wanyama wengine wakubwa wanajiona “Aloof” bora wako juu sana na wanajiona better than others, hakuna kuhoji usawa katika kugawana keki ya shamba hili la wanyama,kufanya hivyo ni kujitakia kifo na kufukuzwa!
Unaweza hata kunyweshwa sumu au kuuliwa kwa namna yoyote. Kupinga vitendo vya akina Nguruwe ilikuwa kuleta eti ‘bewilderment’ machafuko kwenye shamba la wanyama,ninyi ni mashahidi wa haya!
Sasa kumwondoa binadamu ‘tyrant’ na kumwacha nguruwe kukalia kiti na kufanya unyama kuliko binadamu,ndiyo mapinduzi gani haya? Demokrasia gani;usawa upi huu?
Faida yake nini? Kama wapiga debe hawa siyo ‘cunning’ ni nani hawa wanaoongoza kizazi cha shamba la wanyama katika maangamizi kuliko ilivyokuwa kwanza?
SUGARCANDY MOUNTAIN iko wapi watu kukaa vijiweni na kupiga politiki huku wakihamasisha wenzao kufanya machafuko ili eti kufika huko  sugar candy mountain?
Jamhuri ya wanyama,ANIMAL REPUBLIC huru nayenye usawa inakujaje ikiwa akina nguruwe walishaanza ufisadi wa kuvaa suti za akina binadamu? Suti,ni tabia ile ya murder of some animals, wakati nguruwe wanaanza kutembelea miguu miwili(rejea Amri za wanyama) “The Pigs star walking on their two legs” wakajigeuza wakoloni,sheria zinakiukwa makusudi, wanajiona wao wako juu ya sheria,ila binadamu ndiye fisadi tu
Kawimbo, “mafisadi” katamu, lakini waimbaji wake hunuka mithili ya kwapa la ibilisi!
Itaendelea juma lijalo
0713 324 074