| IJUMAA, Januari 21 mwaka huu, Gazeti la KULIKONI liliandika makala isemayo, “Kwenye samaki wengi hakuna samaki tena” huku makala hiyo ya Mwandishi ,Hamisi Kibari, ikirejea Filamu ya ‘Mapanki’ iitwayo, The Darwin’s Nightmare. Nataka kuwakumbusha wasomaji wa gazeti kwamba,kitengo cha samaki cha Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO) kinachoitwa Globefish,kilishasema kwamba samaki wanakwisha Ziwa Victoria. Hata Rais Jakaya Kikwete aliyekerwa sana na ‘documentary’ hiyo, akakutana na mtunzi wake, Hubert Sauper huko Ulaya mwaka 2006,akaingia mitini, alishakiri kwamba Ziwa Victoria samaki wanakwisha. Samaki hawajaisha Mugango na Majita,Musoma mkoani Mara tu. Hata Mwanza hakuna samaki, Bukoba siku hizi wanakula ndizi pasipo samaki. Visingizio ni vingi,ukiwemo uvuvu haramu, lakini ukweli ni kwamba viwanda vya samaki vya Umoja wa Ulaya(EU) na washirika wao,Wahindi, wamekausha samaki Ziwa Victoria. Nina takwimu.Sibabaishi ninapoandika jambo! Globefish, walisema mwaka 2004 kwamba mauzo ya samaki, wa Tanzania,hususan sangara, yalishapungua katika masoko ya Ulaya kutoka tani 56,000 mwaka 2004 hadi tani 52,800 mwaka 2005. Basi, sangara wakaanza kupanda bei katika masoko hayo ya EU kutoka euro 192 milioni hadi euro milioni 210 kwa sababu sangara walipungua, mahitaji yakaongezeka, wakati huko Mugango, Musoma na Mwanza na Bukoba bei ikisalia ile ile. Kati ya mwaka 2004/2005 kilo moja ya sangara waliosindikwa viwandani iliuzwa kwa euro 3.43 hadi euro 5 ambazo zilikuwa kama shilingi za Tanzania kati ya 6,000 na 8,000 tu. Wakati huo,wavuvi wa Bukima na Bugunda,Majitta, Mugango,Mwanza hadi Bukoba walilipwa shilingi 1,200 hadi 2,000 tu kwa kilo moja ya sangara ghafi. Uporaji wa hali ya juu! Kulingana na Globefish,kilo moja ya ya fileti ya sangara huko Ulaya iliuzwa kwa wastani wa euro 60. Euro moja wakati huo ilikuwa sawa na shilingi 1,600 za Tanzania. Sasa angalia, Mzungu analala usingizi kisha anaamkia supermarket yake na kuuza kilo moja ya sangara kwa euro 60, wakati mvuvi alivua usiku mzima hapa,akapigwa dhoruba, akaishia kulipwa shilingi 1,200! Maudhui katika Filamu ya Darwin’s Nightmare,iliyotungwa na Hubert Sauper mwaka 2004, akatunukiwa tuzo anuwai duniani,ikiwemo tuzo ya Oscar, ni kwamba Tanzania ilikuwa ikidhulumiwa sana kupitia biashara hii ya sangara Ulaya. Tanzania,ilibweteka kwa sifa hewa kwamba inauza sana sangara,kumbe Wahindi na Wazungu walichuma sana migongoni mwa wavuvi(akina Mkono wa huko Bukoba na Musoma) ambao waliishia kulipwa kidogo, wakabaki kunywa gongo na kupukutika na Ukimwi katika makambi ya uvuvi. Mwandishi wa mwanzo kuwasha moto ,alikuwa Johnson Mbwambo, ambaye aliandika katika Gazeti la RAI Toleo Na 640 la Januari 12-18 mwaka 2006 kwamba documentary ya Darwin’s Nightmare ilituzindua usingizini! Serikali mkoani Mwanza, wakati huo Daniel Ole Njoolay, akiwa Mkuu wa mkoa, akatoa Tamko kali kulaani documentary hiyo kwamba ilikuwa ya kizandiki; na kwamba Tanzania ilifaidika mno na mauzo ya sangara Ulaya.Akapinga Watanzania kula vichwa na mifupa ya sangara waliotupwa viwandani baada ya kusindika minofu-maarufu sana kama mapanki. Nimesema wakati huo bei ya sangara ilikuwa shilingi 1,200 na viwanda vya mkoa wa Mwanza pekee vilikuwa vikisafirisha zaidi ya kilo 30,000 za sangara waliosindikwa,wakati Mwanza pekee kukiwa na wavuvi 39,370.Shilingi milioni 200 zilikuwa zikiingia katika mzunguko wa fedha kila siku. Njoolay,alisema pato lililotokana na sangara mwaka mmoja kabla ya filamu hiyo,lilikuwa shilingi bilioni 5.7 wakati shilingi milioni 200 zinazunguka katika mzunguko kila siku,wavuvi wakitembea na mifuko ya plastiki,’Rambo’ iliyojaa noti! Kwa ujumla, serikali iliibeza makala ya Johnson Mbwambo, ambaye wakati huo alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wandishi wa Habari za Mazingira(JET). Jumatatu,Julai 31 mwaka 2006,Rais Jakaya Kikwete, akafanya mkutano na wazee wa Mwanza kwenye ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu(BoT) Capri-Point,Mwanza na kuilaani vikali Filamu ya Mapanki, Darwin’s Nightmare. Vyombo takriban vyote vya habari vikahanikiza laana hizo za Rais Kikwete kwa Hubert Sauper,kwa sababu huko Ulaya na Marekani, Filamu hiyo “Mapanki’ iliichafua sana Tanzania huko Ughaibuni, hata Rais alipokwenda kujitambulisha huko baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2005, akakutana na habari za filamu hiyo. Rais Kikwete alikasirika; kwa sababu alidhalilishwa kusikia na kuiona hiyo filamu ikitubeza kwamba tuliuza Ulaya minofu ya sangara,sisi tukabaki kula vichwa na mifupa-mapanki-mithili ya vijibwa! Mapanki yenyewe ni yale yenye funza, tuliyinyang’anyana na mwewe na mbwa huko Kanyama na Nyamuhongolo,nje kidogo ya Jiji la Mwanza, barabara iendayo Sirari na Musoma. Naam, mimi na Richard Mugamba(sasa Mhariri wa The Guardian on Sunday)tukajitoa mhanga kuuzindua umma wa Kitanzania juu ya kile alichosema Hubert Sauper,katika filamu ile. Kwamba,wakati Mzungu anapopelekewa minofu huko, sisi tunakula mifupa na vichwa vya sangara vilivooza,ili kujikimu,kwababu nchi ilikuwa katika janga la njaa,kiasi cha kusaidiwa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa,FAO na WFP. Shirika la Utangazaji la Uingereza(BBC) likafika Mwanza na timu ya Watangazaji wengi, akiwemo Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili, Tido Mhando,nilipewa muda kuzungumza namna biashara hiyo ya sangara ilivyokuwa ikimaliza samaki Ziwa Victoria na kuwaacha wananchi na njaa na umasikini wao. Kutoka mwaka 2006 hadi 2011 Mhariri wa Gazeti hili, Hamisi Kibari anapofanya ziara Mugango,Musoma na kubaini kuwa hakuna samaki huko,kwa sababu zile alizosema Hubert Sauper katika Darwin’s Nightmare, serikali ikabisha,miaka mitano imekwishapita. Nataka niwaambie wasomaji kwamba serikali ilishakubali maoni ya filamu hiyo kimya kimya, na hapa nitaeleza kauli za Rais Kikwete na mawaziri wake. Jumanne, Mei 13 mwaka 2008, Rais Kikwete alipokuwa akifungua kiwanda cha kusindika samaki cha TFDC,Ilemela,Mwanza, akasema wananchi waanzishe mabwawa ya kufugia samaki,maana Ziwa Victoria ‘linakauka’. “Ndiyo njia pekee ya kuondokana na kitisho cha kupungua samaki katika Ziwa hili kubwa kuliko yote Afrika”, Rais alisema. Wavuvi, wakiwemo haramu wengine kutoka nchi jirani za Kenya na Congo DRC walishaongezeka sana kutoka 51,935 mwaka 2002 hadi 98,015 mwaka 2007. Zana za uvuvi zikiwemo haramu zilishaongezeka mno kutoka 15,434 hadi 29,730 katika kipindi hicho.Bila shaka Rais alishabaini ukweli wa mambo,kwamba kipindi kile wasaidizi wake walimpotosha kwamba hatuli ‘Mapanki’ kwa sababu walizojua wao! Na uzembe wao ndiyo ulimfanya Sauper kupiga picha za filamu ile(nilishaandika jambo hili katika gazeti hili). Mwaka 2004 samaki waliovuliwa Ziwa Victoria walikuwa wenye uzito wa tani 750,000. Lakini mwaka 2007 samaki waliovuliwa katika Ziwa hili walipungua hadi tani 375,400 tu. Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,wakati huo John Pombe Magufuli akachoma makokoro haramu,wakati maofisa uvuvi wakiwapora wavuvu sehemu moja na kuyauza kwingine-baadhi yao walikuwa na hayo makokoro haramu mengi tu. Samaki wa Musoma wakaendelea kutoroshwa hadi Nairobi na Ulaya kwa magendo. Takwimu zikawa zinapikwa tangu viwandani hadi Mamlaka ya Mapato(TRA) bila wasiwasi. Waziri wa MAALIASILI na Utalii,Prof Jumanne Maghembe, Juni 11 mwaka 2007 wakati akifungua semina kuhusu uvuvi endelevu hapo BoT,Mwanza akasema samaki wamekwisha,wakati bei imebeki ile ile tu. Prof. Maghembe akaagiza hadi Juni 11,mwaka 2008 samaki waliosalia angalau waachwe wazae uzazi mmoja tu! “Pasipo kufanya mkakati wa kuepusha samaki kutoweka Ziwa Victoria,Tanzania haitaepuka ‘HUKUMU YA ULIMWENGU’ kwa kuruhusu rasilimali zake wakiwemo sangara kutoweka,na hivyo maisha ya watu kuathiriwa vibaya”, alisema Prof. Maghembe hiyo Juni 11 mwaka 2007. Hiyo hukumu ya ulimwengu aliyosema Prof. Maghembe ni ipi kama siyo kilichosemwa na documentary hiyo ya Mapanki serikali ikabisha? Kwamba, sangara wa Ziwa Victoria waliliwa Ulaya, sisi tukabaki na njaa yetu na kuomba misaada, wakati wavuvi wakifa kwa ukimwi makambini,wakibugia gongo na dada zetu wakijiuza kwa marubani wa madege ya Kirusi-Ilyusin-kwa ujira wa dola 10 Niliitazama Filamu hiyo, DARWIN’S NIGHTMARE ofisini kwa Mkuu wa mkoa, Daniel Njoolay wakati huo kabla ya kuhamishiwa Rukwa. Niliitazama kwa mara ya pili ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Mwanza(MPC)nikaandika habari kadhaa na makala za kutosha. Habari iliyokaribia kunitia matatani,ni ile ya Alhamisi, Agosti 3,mwaka 2006 iliyotolewa katika Gazeti la Tanzania Daima,ikiwa na kichwa, “Mapanki yamgeuka J.K” Katibu wa CCM, mkoa wa Mwanza,wakati huo,Mujuni Kataraia,akaitisha maandamano ya kuipinga habari hiyo, halafu akaniambia, “Kwanini kila mara wewe uko against na(unaipinga) serikali?” Nadhani Rais Kikwete aliyapuuza maandamano yale. Ingawa alikuwa jijini Mwanza kwa mapumziko,hakujali maandamano yale ya kunipinga. Darwin’s Nightmare,imejengwa katika Falsafa za mwanabaiolojia wa Kiingereza, Charles Robert Darwin(1809-1882) ya viumbe vyenye nguvu kuvitafuna dhaifu, “Survival of The Fittest” katika Ulimwengu wa utandawazi. Wazungu wanapoacha akiba samaki wa maziwa yao na bahari, wanachuma hawa wa kwetu kwa bei chee,halafu wakiisha wanang’oa viwanda vyao na kutoweka huku wakituacha na njaa yetu-hii ndiyo Theory na ‘Darwinism’ na Survival of the Fittest. Wenye nguvu wanawala dhaifu ama masikini! Tanzania ilivikwa kilemba cha ukoka kwamba ilikuwa msafirishaji namba wani wa sangara duniani,kumbe samaki sasa hawapo baada ya madege ya Kirusi, Illyushin kusomba takriban tani 50 kila dege kwa siku. “Falsafa” hii ya Darwin haikutuzindua usingizini, waandishi kama Johnson Mbwambo wakaishia kubezwa na serikali,mwisho wa siku sasa kilio cha kutoweka kwa samaki kinasikika kila upande! Samaki ni fursa muhimu katika nchi.Lakini, wameporwa na wawekezaji kwa bei poa, na hata Wacongo wanavua huko visiwani,maofisa wa maliasili wapo tu,wanapewa rushwa ndogo ndogo na samaki wanazdi kutoweka! Kitengo cha Globefish cha FAO kilishasema mwaka 2006 kwamba samaki wanatoweka kwa kasi Ziwa Victoria na kuwaacha Watanzania na njaa,na umasikini na dhiki nyingi huku watoto wa mitaaani wakigombea ubwabwa katika sufuria la mpita njia,mama ntilie! Madege ya Kirusi yalisomba sangara hadi yakaanguka Ziwani kwa kuzidisha uzito ili kukwepa Mamlaka ya Mapato(TRA). Sauper, katika filamu hiyo ya mapanki alitukumbusha namna Yesu wa Nazareti alivyotumia visamaki viwili tu(Tanzania tulikuwa na masangara makubwa mengi tu)na mikate mitano kuwalisha zaidi ya watu 5,000 katika kijiji cha Bethsaida,wakasaza mabaki yaliyojaa vikapu 12! Katika filamu hii,Darwin’s Nightmare, muujiza wa Yesu wa kuwalisha watu hao( Injili ya Marko 6:34-44 na Luka 9:10,11) ili Tanzania tujifunze kutumia rasilimali zetu vizuri kuwalisha watu wenye njaa siku hizi tunapolia na ukame. Sauper, alimtangaza Yesu katika filamu hiyo kama kiongozi bora, anayejua kutumia rasilimali chache kwa maslahi ya wengi hadi kusaza vikapu 12! Laiti Yesu angekuwepo leo Tanzania,penye masangara makubwa haya, na jodari mithili ya wale wa Magufuli, dagaa, almasi, tanzanite,dhahabu,wanyamapori,misitu,matunda, mifugo,mito,bahari,milima mirefu na mabonde,bila kusahau madini mengi haya, watu milioni 43 wa Tanzania wasinge kula na kusaza vikapu bilioni nyingi? Tatizo, Watanzania siyo wazalendo, na siyo viongozi tu wasio wazalendo, hata wavuvi siyo wazalendo kama wale wanafunzi wa Yesu walioleta visamaki viwili na mikate yao mitano Yesu akaibariki na kuwalisha watu zaidi ya 5,000! Tanzania, tuna njaa katika utajiri wa rasilimali? Sababu,hakuna viongozi wazalendo kama Yesu wa Nazarethi, na kila mtu ni mchoyo asiyewajibika. Tuna rasilimali tele,fursa tele. Tuna ‘Jodari’ kama wale wa Magufuli na masangara makubwa, lakini yamekwisha na kutuacha masikini na wenye njaa-hatuna akili. 0786/0754-324 074 |
Wednesday, June 15, 2011
Ziwa Victoria samaki wamekwisha kabisa!!
Ziwa Victoria samaki wamekwisha kabisa!!
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema mwaka 2007 kwamba, sangara walioliingizia Taifa mabilioni ya fedha za kigeni, sasa wametoweka." Wanapungua kwa kasi sana . Kama hatua za dharura hazitachukuliwa, watakwisha; wananchi watateseka kwa kukosa kipato. Viwanda wa samaki vitafungwa na kuathiri mapato ya nchi na ajira muhimu." Alisema Prof Maghembe, mwaka huo 2007Prof. Magembe, ambaye alikuwa akifungua kikao-kazi kwa viongozi wa mikoa na wilaya kuhusu uvuvi endelevu Ziwa Victoria , Juni 11 mwaka 2007 katika Ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu Mwanza, ameonya kuwa maisha bora kwa Watanzania hawa yanaweza kuwa pwaji, ama porojo tupu.Lishe kwa wakazi milioni 30 wanaozunguka ziwa hili, wa Tanzania , Kenya na Uganda , itaporomoka; wakati fedha nyingi zikiwemo za kigeni, zitakosekana. Prof. Maghembe aliagiza, angalau ifikapo Juni mwaka 2007 ufanywe mkakati kuhakikisha sangara waliobaki wanazaa japo uzazi mmoja tu!Akasema, kitu kimoja muhimu sana , ambacho ni muktadha wa makala hii leo: Kwamba, bila kufanya mkakati wa kuepusha sangara ama samaki kutoweka Ziwa Victoria , Tanzania haitaepuka ‘Hukumu ya Ulimwengu’ kwa kuruhusu rasilimali zake wakiwemo sangara, kutoweka, na hivyo maisha ya watu wake kuathiriwa vibaya.“Hili, inabidi litimie. Vinginevyo, hatutaepuka hukumu ya Ulimwengu kwa kuruhusu rasilimali hii kutoweka, na hivyo watu wetu kuathirika vibaya”, alisema Profesa Maghembe.Aliweka kipindi cha nusu mwaka, kuhakikisha taarifa ya kazi inatolewa. Kwamba jambo hili si muhali; hivyo kushindwa kulitekeleza ili kuondoa kitisho hiki si chaguo la serikali yetu.Kwa upande mwingine, ‘Hukumu hii ya Ulimwengu’ aliyosema Prof. Maghembe, ilikwisha tolewa na Hubert Sauper, yule Mtunzi wa Filamu ya tashtiti, ya Mapanki(The Darwin’s Nightmare), serikali ikabisha!Kwamba, sangara wa Ziwa Victoria walikuwa wakiliwa Ulaya, wakati wazalendo wa nchi hii wakiambulia vijisenti kidogo vya kikunjajamvi, wakati wengine wakiambulia vichwa na mifupa-mapanki!Jinamizi la Darwin;Charles Robert Darwin (1809-1882) lililosimuliwa na Hubert Sauper, kwa njia ya kejeli, miaka michache iliyopita, kupitia filamu iliyomfedhehesha hata rais wetu, lilikuwa onyo tosha.Onyo kwa serikali yetu kuwamaizi Pwagu,(wezi na wadanganyifu), Pwaji(wapiga porojo) na Pwaguzi(wajanja zaidi kuliko Pwagu), waliokuwa wakikomba sangara wetu na kutuacha masikini.Filamu hii iliwataka Watanzania kuondoka usingizini mara moja na kuepuka kugombea ubwabwa kidogo katika sufuria chafu, kula mapanki yenye funza, na kunywa pombe haramu ili kupata tafaraji, baada ya kuvua sana na kuuza samaki wengi sana kwa Pwagu, yaani wakala wa Pwaguzi, bila faida!Watanzania tulionywa na filamu hiyo kuwa na akili; yaani kuvua kwa tija, badala ya kuvua sana tukiishi katika makambi mithili ya manamba, ambako wavuvi huishia kufa kwa Ukimwi, na dada zetu huishia kuwa machangudoa wanaopigwa ‘kipopo’ mithili ya wezi, na Wazungu kwa ujira wa dola dola 10 tu.Athari hasi za utandawazi, muktadha wake ni pamoja na kugombea maisha(struggle for existance); ni harakati zinazowafanya viumbe dhaifu kushindwa mapambano; na hivyo kuishia kuliwa mithili ya mchwa, panzi na kumbikumbi.Falsafa ya ya Charles Robert Darwin, mwanasayansi maarufu sana wa Kiingereza(alizaliwa Feburuali 12 mwaka 1802 na kufa Aprili 19, mwaka 1882) iitwayo Darwinism, huonya kwamba, katika maisha viumbe dhaifu ikiwemo mimea, abadan havishindani na vyenye nguvu.Katika zama hizi za utandawazi, mataifa dhaifu kama Tanzania , hujikuta yakinyang’anwa chakula, maji, hewa na mwanga wa jua, ili kuyapisha yenye nguvu kustawi.Tanzania kama mmea, itanyauka baada ya kuzongwa na magugu(Super powers), au baada ya kutafunwa kama sangara anavyowatafuna samaki wadogo, ama kama simba anavyowatafuna swala,pofu, nyumbu na palahala porini.Kitu hiki, ndicho Darwinism; yaani kwamba wenye kupona ni wenye nguvu tu(survival of the fittest).Kitendo cha sangara wetu kuuzwa Ughaibuni kwa vijisenti kidogo na kuwalisha Wazungu na Wahindi huku Watanzania wakihangaika kwa njaa kali, ni athari yakinifu za utandawazi unaoruhusu wakubwa kuwatafuna wadogo.Yesu wa Nazareti aliwalisha watu zaidi ya 5,000 katika kijiji cha Bethsaida kama miaka 2010 iliyopita, kwa visamaki viwali vidogo, ukilinganisha na sangara wa Ziwa Victoria, na mikate mitano.Katika Darwin’s Nightmare, muujiza huu unaosimuliwa katika Injili ya Mtakatifu Luka 9:10-11 na Marko 6:34-44 umeonyeshwa.Bila shaka, muujiza uliwekwa ili kuwakumbusha Watanzania kwamba, kama Yesu aliwalisha watu hao(walihesabiwa wanaume pekee, bila wanawake na watoto) kwa visamaki viwili; wakala hadi wakasaza vikapu12, Watanzania hushindwaje kujilisha kwa mabilioni ya sangara, dhahabu, almasi, tanzanite, ruby, wanyamapori, misitu,shaba, pamba, kahawa, katani, korosho na rasilimali zingine anuwai?Kwa upande mwingine, hofu ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Maghembe, kwamba samaki wetu(si visamaki) watatoweka na kuwafanya wananchi kuathiriwa vibaya, ni sawa na kilio cha uchungu kuashiria maombolezo ya taifa.Sauper, alitaka kuwasagua Watanzania, tena kuwagutua kwamba umasikini na njaa yetu wakati sangara mabilioni wakitoroshwa Ulaya na akina Pwagu, bazazi, dumizi na pwaguzi kwa mrabaha kidogo, ulikuwa umbumbumbu.Hata rasilimazi nyingine kama madini, wanyamapori na mazao ya kilimo hutoroshwa hivihivi na ma-Pwagu, Pwajizi na mapwaguzi, pasipo sisi kunufaika na chochote. Sisi ni ng’ombe wa maziwa-watu wa kukamuliwa hadi tone la mwisho la damu.Pwagu, Bazazi na Pwaguzi wanavyowanyonya wavuvi. Wanasomba sangara kwa ujira kidogo.Hushirikiana na Maofisa uvuvi,polisi, maofisa wa Forodha, TRA, na hata baadhi ya Mawaziri husafirisha sangara kwa magendo!
Kama Profesa Maghembe na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uvuvi,Geoffrey Nanyaro walikuwa hawajui, shime wamaizi kuwa sangara wetu hukombwa na'pwaguzi’ kwa ujira kidogo wanaolipwa akina Pwagu!Katika biashara hii, wamo bazazi na dumizi wanaojipendekeza kwa Pwagu, ili kujipatia makombo!Naam. Hapa, Tanzania inaliwa na kubakizwa mifupa mitupu-mapanki. Mapanki nayo huuzwa nje yakaliwe na kuku, wakati Watanzania wakibaki kugombea fadhila na chakula cha wahisani.Masikini wavuvi wanapofikisha sangara kiwandani, huambiwa na Mapwaguzi kwamba ni ‘reject’ kisha huambulia kipeto na kuondoka na njaa yao.Kitengo cha samaki (Globefish)cha Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO), Agosti mwaka jana kilisema kwamba sangara walikuwa wakitoweka kwa kasi Ziwa Victoria.Ni taathira kwa Watanzania watakaobaki hawana chakula, wakiomba msaada Ulaya na Marekani, ili kujiepusha kupotea katika uso wa dunia. Tunaambiwa Watanzania huambulia milioni 500 kwa siku kutokana na biashara ya samaki kila sikuKwamba kila mwaka wavuvi na wachuuzi wa samaki hupata sh. Trilioni176.
Kwa mwaka Wazungu hutafuna minofu maelfu ya tani kutoka Tanzania , wakati samaki wao wakiachwa akiba.
Vya walevi huliwa na mgema.Wavuvi wadogo leo husukumiwa laana ya kusababisha sangara kutoweka; kwamba wanavua kwa kutumia nyavu haramu.
Hizi nyavu haramu hukamatwa hapa na maofisa uvuvi, kisha huuzwa pale, baada ya kuchoma moto chache tu, mbele ya polisi na waandishi wa habari!Nyavu au makokoro hayo ya polisi na maofisa uvuvi ndiyo yanayoharibu mazingira ya ziwa na mazalia ya samaki.
Leo,Maofisa wanadanganywa kwamba wavuvi haramu ni wananchi vijijini! Wakale wapi sasa?
Samaki wawili wa kitoweo wanapunguza samaki?Sangara wadogo wanaosafirishwa nje ya nchi, wanavuliwa na nani kama si na hao maofisa uvuvi na ndugu zao?Kwanini wasikamatwe?
Watanzania masikini wanaovua bila leseni, huvua tani ngapi kama si kitoweo? Wanayuga-yuga kuepuka mhali, ama njaa inayowakabili. Kwanini akina Pwagu na Pwaguzi wanaachwa kuvua na kusafirisha mamilioni ya sangara kwa magendo?Tatizo si wavuvi wadogo, ni mapwagu, mabazazi,dumizi na pwaguzi wanaokomba samaki Ziwa Victoria na kuwauza nje kwa magendo, lakini hawakamatwi.
Vigogo, wakiwemo hata baadhi ya Mawaziri wana vikampuni hewa, wanapewa mgawo wao na akina Pwagu na Pwaguzi.Waziri Maghembe anawataka wabadilike!
Waache kuimumucha Tanzania ? Hizi ni porojo, pwaji na soga!
Waondolewe katika madaraka, tena wafilisiwe. Je, viongozi watazinduka? Wataweza? Shime wawafunge mikatale ili kuinusuru Tanzania.Wanao ubavu wa kuwakomesha akina Bazazi, pwajizi, pwagu na pwaguzi wasilikaushe ziwa Viktoria?
Labda.0754 324 0740786 324 074.
Tuesday, June 14, 2011
Monday, June 13, 2011
wakubwa wa IMF na Benki ya Dunia nao wanabaka!
| IMF na WB wanakopesha Dola, Euro na ngono kwa akina mama *huko kuna mapenzi kazini-‘kazi na dawa’ *kuna rushwa ya ngono, wake za watu hutwangwa talaka *Tanzania kuna Maprofesa wanaotoa ‘digrii za chupi’ Na Conges Mramba, Mwanza WATU WENGI hapa duniani, wanadhani kazi ya Benki ya Dunia(WB) na Fuko la Fedha la Kimataifa(IMF) ni kupanga,kuratibu Programu za Fedha, Uchumi na Maendeleo ya watu ili kupunguza umasikini. Fuko la Fedha la Kimataifa(International Monetary Fund) hupanga mikakati ya Kupunguza Umasikini na Kuwezesha Ukuaji wa Uchumi,yaani wao wanaita, Poverty Reduction and Growth Facility,(PRCF). Umoja wa Mataifa(UN) kupitia taasisi anuwai,hususan mashirika haya na IMF na WB wanajidai kutoa misaada maridhawa kwa mataifa fukara sana duniani, Heavily Indebted Poor Countries(HIPC). Yumkini, IMF na IMF wanaongoza duniani katika harakati za kupambana na umasikini,kumbe wanaongoza kwa upendeleo katika ajira,udhaifu na rushwa ya ngono.Wamekuwa wakitumiwa na wakoloni wakongwe kuendelea kuzitawala nchi masikini hususan Afrika, Asia na Amerika Kusini. Wameendelea kututawala hata baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia,mwaka 1945 na hata baada ya Vita Baridi kumalizika,mwanzoni mwa miaka ya 90. Sasa ni dhahiri shahiri kwamba, IMF na Benki ya Dunia ni makao makuu ya tamaa za kingono,rushwa ya mapenzi na ubakaji kwa akina mama. Mkuu wa zamani wa IMF ,Dominique Strauss-Kahn, amepandishwa kizimbani kujibu mashitaka ya kujaribu kumbaka msichana ambaye ni mhudumu wa hoteli, jijini New York,Mwezi Mei mwaka huu. Strauss-Kahn, alikana mashitaka ya kujaribu kubaka. Ushahidi umeonesha kwamba, kulikuwa na mazingira ya ngono kati ya Mkuu huyo wa zamani wa IMF na Mhudumu huyo wa Hoteli,jijini New York,Marekani. Mawakili wa upande wa utetezi, wanadai kwamba mteja wao, Dominique Strauss-Kahn(62) na kimwana huyo, walikuwa wamekubaliana kufanya ngono. Hiyo Mosi: Ubakaji IMF.Bila shaka, na uchumi wa dunia unabakwa! Pili:Rais wa zamani wa Benki ya Dunia(WB),Paul Walfowitz, aliachia ngazi Juni 30 mwaka 2007 baada ya kukutwa na kashfa ya rushwa ya ngono. Rushwa ya ngono hata ndani ya Benki ya Dunia(WB) vinara wa kukosoa nchi masikini kwa rushwa na kukosa uadilifu? Wolfowitz,Balozi wa zamani wa Marekani nchini Indonesia na Naibu Waziri wa Ulinzi,tamaa ya huba kwa kidosho,mfanyakazi wa Benki hiyo kuu duniani ilimgharibu wadhifa wake,marupurupu maridhawa, mambo yakaenda harijojo. Alikuwa mpiganaji wa mstari wa mbele dhidi ya rushwa. Kumbe, alikuwa dhaifu sana katika huba kwa vimwana,hadi alipopewa penzi akatoa nyongeza ya mshahara na kumpandisha cheo mwanamama huyo,hadi alipokaliwa kikao na kamati ya maadili ya WB. Alipochaguliwa kushika wadhifa huo mtukufu, wa Rais wa Benki ya Dunia, akadhaniwa angekuwa shujaa wa kupambana na umasikini duniani, na daktari bingwa wa kuponya pengo kati ya fukara na matajiri. Kumbe, Wolfowitz alikuwa mwenye nguvu lakini dhaifu(strongest but weakest) kwa mahaba ya vimwana katika ofisi ya umma. Marekani, ndiyo nchi yenye mamlaka ya peke yake katika kumteua Rais wa Benki ya Dunia. Ulaya, wana haki ya Peke yao kumteua Mkuu wa Fuko la Fedha la Kimataifa(IMF). Nchi nyingine kama Japan,Uchina na za Afrika na Marekani ya Kusini,huishia kulalamika kuburuzwa na Marekani na Ulaya,kuigeuaza IMF na WB mikono yao miwili ya kuiburuzia dunia wanakotaka. Taasisi hizi zina uwezo wa kuwawekea vikwazo vya uchumi wale wapinzani wao kama Muammar al-Qaddafi anayenyeshewa mvua ya mabomu na madege ya NATO, na ambaye tayari mji wake wa Benghazi umekuwa ngome ya Waasi wanaobebwa katika mbeleko na Marekani na washirika wake wa Ulaya. Wapinzani wengine wa Marekani, ni pamoja na Robert Gabriel(R.G)Mugabe wa Zimbabwe,Hugo Chavez wa Venezuela, Fidel Alejandro Castro Ruz,Rais Mstaafu wa Cuba. Naam, Rais Mstaafu wa Marekani, George W.Bush alimteua Robert Zoellic kumrithi “Mzee wa Vimwana”Wolfewitz. Zoellic, ni mwakilishi wa zamani wa wafanya biashara wa Marekani,mabwenyenye na wahafidhina wa sera kandamizi za uchumi duniani.Bei ya mazao wanapanga wao, mazingira wanachafua wao na hakuna wa kuwagusa! Benki ya Dunia, hukopesha takriban dola za MarekaniBilioni 10 sawa na euro Bilioni 5 kwa mwaka; hukopesha mataifa masikini zaidi kupitia programu na mipango anuwai kama IDA. Shaha Ali Riza, ndiye kimwana aliyemzingua Rais huyo wa Benki Kuu Duniani,Dk.Wolfowitz,mwaka 2007 hadi alipokiuka maadili na kutopea katika utovu wa maadili. Shaha Ali Riza(57) ni kidosho aliyemgharimu Wolfowitz urais wa Benki ya Dunia.Walipokutana kwa nasibu mno,wakapendana penzi la tashtiti…wakati huo Wolfowitz akiwa Naibu Waziri wa Ulinzi,zama za Rais Ronald Reagan.Wakati huo, Donald H.Rumsfeld alikuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani. Kimwana huyu,Shaha Riza, alizaliwa Tripoli,Libya huko kunakopigwa mvua ya makombora kumwangamiza Kanali Muammar al-Qaddafi na milki take ya miaka 42. Alizaliwa mwaka 1954. Baba wa kidosho huyu,Riza aitwaye Khalid Alwalid na mamaye ambaye alikuwa chotara wa Syria na Saudi Arabia, walimpeleka Shaha Riza Uingereza.Akawana uraia wa Uingereza Baadaye, akahamia Marekani,ni baada ya kuolewa na Bulent Ali Riza ama kwa kifupi,Aliriza (60)sasa.Kisura huyu aliyemzamisha Rais Wolfowitz huko Benki ya Dunia alisoma London School of Economics, akatuzwa shahada ya Uzamili katika Uhusiano wa Kimataifa,huko Oxford mwaka 1983. Ana uwezo wa kuongea lugha tano, miongoni mwake,Kiingereza,Kiarabu,Kiitaliano na Kifaransa. Mumewe alimpa taraka,kwa sababu ya uhusiano wa kimapenzi ba Rais wa Benki ya Dunia.Benki ya Dunia inapochangia kuvunjika kwa ndoa na watoto wasio na wazazi wa pande mbili, nani awape msaada? Shaha, alijiunga na Benki ya Dunia mwaka 1997, akitokea Mashariki ya Kati. Huko, alitumiwa na Marekani kuipeleleza Afrika na Mashariki ya Kati,ili eti kusaka demokrasia katika ulimwengu wa Kiarabu. Kimwana huyu wa Kiarabu alikuwa kibaraka na shushushu wa Marekani aliyetumika kupandikiza chuki ili vita vianze Ghuba wao waibe mafuta! Machi, mwaka 2005,sakubimbi(jirani yao) aliviambia vyombo vya habari juu ya uhusiano wa kimahaba ya Wolfowitz. Huu ndiyo mwaka Wolfowitz alipothibitishwa katika wadhifa wa Rais wa Benki ya Dunia, akaanza kuutumia vibaya wadhifa huo ili kununua huba la ‘mtoto’ wa Kiarabu, Shaha Ali Riza, aliyekwishaachika. Alipagawa kwa penzi la tashtiti kwa huyu Shaha Riza,kazi zikaharibika,ukawa upendeleo tu-Bwana mkubwa haoni wala hasikii-Upofu wa Penzi Pevu kwa kimwana wa Kiarabu.Mzuri mithili ya Jini! Alipandishwa vyeo,akapandishwa mshahara, alilipwa dola za Marekani 180,000 kwa mwaka,hazikukatwa kodi. Naam, mwenye mapenzi haoni,Riza alipandishwa mshahara kwa asilimia nane kila mwaka,kwa sababu,”MKUBWA ANATAKA!” Mwaka 2007, gazeti la Washington Post likafichua mshahara wa kimwana huyo kwamba uliongezwa kinyemela kutoka dola 132,660 hadi 193,590 kwa mwaka; tena pasipo kodi. Mwanamke huyo akajitetea na kujifaragua hivi na vile, katika Kamati ya Maadili ya Benki hiyo.Wafanyakazi wenzake wakalalamika kwamba, “Boss” alikuwa akiwashusha moyo kumpandisha cheo kimwana wa Kiarabu,Shaha Riza,wakati wao mshahara haupandi na cheo hawapandishwi. Huyu mama, aliwahi kufanya kazi Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani(The Pentagon) wakati ule Wolfowitz akiwa Naibu Waziri wa Ulinzi. Kwa hiyo,utaona huko Pentagon ndiko walikokutana,penzi likamea na kukua,jamaa alipoufuma u-‘Boss’ W.B akamwita mshushu wake huyu na kumpandisha vyeo na mshahara mkubwa! Hata Pentagon na Benki ya Dunia kuna Mapenzi kazini-‘Kazi na Dawa’ ama siyo msomaji wangu? Kumbe, makelele yao ya uzembe na kutowajibika kazini kwa nchi masikini ni domo kaya tu. Shaha Riza,ndiye aliyetumiwa kuipeleleza Irak na kuchochea vita vilivyomwondosha madarakani, Saddam Hussein mwaka 2003, na hatimaye akatiwa mbaroni na kunyongwa,Camp Justice,Desemba 2006. Mkewe Wolfiwitz,Clare Selgin alishamwonya mapema Rais Bush asiitumbukize Marekani katikavita vya Ghuba kwa kuwasikiliza akina Shaha Riza. Aprili 12 mwaka 2007 Bwana Mkubwa huyo wa WB akajitetea kutumia cheo vibaya na kuitumia ofisi kufaidi penzi la kimwana wa Kiarabu; alisita kuachia ngazi kwa kashfa ile. Nakumbuka kashfa nyingine ya ngono baina ya Rais Bill Clinton na Monica Lewinsky-The Monicagate. Magavana wa Benki hii walikaa Aprili 15 mwaka 2007 ili kujadili uchafu huo na kutumia mali na madaraka kufaidi mapenzi ya kimwana wa Kiarabu katika ofisi nyeti ya umma. Magazeti yalimlima sana Wolfowitz kwa mapenzi katika ofisi ya umma-akaachia ngazi. Mail on Sunday, Jewcy, Wall Street Journal,Washington P ost, The New York Times, Los Angeles kwa kuyataja macache, ndiyo yaliyoongoza kumlima huyu kigogo. Kimwana wa Kiarabu toka Libya, mwenye mchanganyiko wa damu toka Syria na Saudia alipandishwa vyeo,licha kuajiriwa kwa mizengwe,akapandishwa mshahara, kupalilia penzi la kigogo! Mmewe aliitwa Cypriot Bulent Ali Riza,Mturuki na walishatengana. Wolfowitz yeye alimwoa Clare Selgin mwaka 1968 wakapeana talaka 2001. Rushwa ya ngono ambayo hata hapa Tanzania ipo, imeanzia huko Benki ya Dunia,na kupeana vyeo na kazi kulianzia huko kwa akina Wolfowitz, Bush na Obama. Hata hapa Bongo, maprofesa hupewa rushwa ya ngono,na ndiyo chimbuko la ‘digrii za chupi’ na taifa huenda mrama kwa wasomi feki waliojazana katika ofisi nyeti za umma! Itaendelea juma lijalo 0786-324 074 ; ; |
SIYO BURE Safari za akina Hillary Clinton Bongo, zina kitu
SITAPENDA kuamini kirahisi, kwamba eti Marekani ni rafiki wema sana kwetu Tanzania,hadi viongoi wake huja hapa kila mara,hukaa siku nyingi na hutuletea hisani.
Na siamini kwamba, eti fadhila, hisani ama misaada ya Marekani kwetu hutoka katika kiini cha moyo wao na mapenzi ya dhati kwa Watanzania!
Kwa hulka yao,Marekani hawana rafiki wa kudumu.Maslahi yao ndiyo rafiki yao mkuu wa enzi zote.Kwa sababu hiyo,ukiona Marekani wanakupenda,kuna maslahi yao yaliyofichika sirini nyumbani kwako, Wamarekani wanapokuja kwako, wanafuata maslahi nyumbani kwako,kwa jirani yako ama kwa rafiki zako.
Naam. Marekani hawana rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu.Wana maslahi ya kudumu Taifa hili babe sana duniani, lililopata uhuru wake zaidi ya miaka 230 iliyopita, aslani halina urafiki wa kuaminika-lina maslahi ya kudumu.
Kwa sababu hiyo, leo nitajadili maslahi ya Marekani yanayoweza kuwa yamefichika ndani ya ngozi ya Watanzania, na hivyo ujio wa viongozi wa Marekani wa mara kwa mara ukawa na nia ya kutuchuna ngozi ili wachukue kile kilichofichika ndani yetu.
Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton, inaweza kuwa na kitu ‘nyuma ya Pazia’.
Juzi Jumamosi, hadi Jumatatu, Juni 11-13 Hillary Clinton alikuja kwetu. Huyu Hillary Clinton(64) ni mwanamke wa kwanza, mke wa Rais Mstaafu(Bill Clinton) kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.
Pia, ni mwanamke wa tatu wa nchi hiyo kushika wadhifa huu wa ‘kikachero’ katika siasa za Ulimwengu.
Wanawake wengine waliomtangulia kushika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje(The Secretary of State) wa Marekani, ni Madeleine K. Albright aliyeteuliwa kumrithi Warren Christopher mwaka 1997 zama za urais wa William(Bill) Jefferson Clinton.
Mwingine, Dk. Condoleezza Rice, ama kama alivyoitwa na rafiki zake, “Condi” aliyemrithi Jenerali Colin Powel.
Dk. Rice, ‘rafiki’ wa familia ya akina Bush,alimaliza muda wake siku Rais Barack OBAMA ALIPOAPISHWA KUWA Rais wa 44 wa nchi hiyo, Januari 20 mwaka 2009.
Hillary, aliyekuwa seneta wa New York, alipewa wadhifa huu mtukufu baada ya kushindwa kura zao maoni za urais ndani ya chama cheo cha Democrat na huyo huyo Rais Obama.
Wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani(secretary of state) ni nyeti sana; hupewa mtu muhimu sana Marekani kwa wakati huo, mwenye ujanja mwingi wa kughilibu na kushawishi mataifa kukubaliana na Marekani dhidi ya changamoto zake na vizingizi dhidi yao. Huyu hawezi kuwa waziri tu,bali pia shushushu ama kiongozi wa majasusi wa ghiliba ulimwenguni.
Dk. Henry Alfred Kissinger, yeye alichora ramani ya kukomesha ujamaa wa Ki-Marx duniani. Alimsaidia Rais Richard Milhous Nixon(Nixon ni maarufu kwa kashfa ya Watergate) kumpindua Rais Mjamaa wa Chile, Salvador Allende,kwa kutumia Shirika lao la Ujasusi, CIA.
Kissinger, alishika wadhifa huu mwaka 1973 enzi za mwisho za Nixon na mwanzoni mwa Rais Gerald Rudolf Ford.
Nataka kusema kwamba, hawa mawaziri wa Mambo ya Nje huwa na kazi maalum iliyofichika katika nyayo za viatu vyao.
Madeleine K. Albrigh, alipelekwa Korea Kaskazini kujaribu kwenda kuzungumza na viongozi wan chi hiyo,Kim Il Sung/Kim Jong Il waachane na mpango wao wa miradi ya nyuklia.
Hata siku za karibuni,walijaribu kuwashawishi waachane na miradi ya Nyuklia kwa ahadi kwamba wangepewa mafuta mengi na kitita cha dola za Marekani-rushwa.
Lengo lao lilikuwa Korea Kaskazini,moja ya nchi adui zao na nchi iliyokuwa katika Mhimili wa Uovu-The Axis of Evil- iachane na ukaidi kama Iran ya Mujahidin, Mahmoud Ahmadnejad.
Albright, alikwenda Korea Kaskazini, kutuliza joto la uasi dhidi ya Marekani kwa mazungumzo na ghiliba ambazo hazijafua dafu hata siku hizi.
Condoleezza Rice, “Condi” ambaye amepata kuwa Mshauri wa Mambo ya USALAMA WA TAIFA wa Rais Bush, Kafanya makubwa kufanikisha vita vya Ghuba,hasa mapinduzi ya serikali ya Wataliban wa Afghanistan na kuuondoa utawala wa Marehemu Saddam Hussein huko Irak.
Hawa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, wana mitego na ghiliba,na huwa na ‘Kazi Maalum’ ya kufanya katika ajenda za siri za Marekani, zinazofichwa nyuma ya pazia.
Kissinger, yeye alishughulikia sana migogoro ya Mashariki ya Kati hususan Vita vya Misri na wajomba zaWamarekani, Israeli. Hatimaye yalikuja mazungumzo ya amani huko Camp David, mwaka 1978 zama za Jimmy Carter.
Madeleine K. Albright,alitua Dar es salaam mwaka 1999. Ni siku ambayo mwili wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere uliagwa,katika uwanja wa Taifa,Dar, siku hizi Uwanja wa Uhuru ama Shamba la Bibi.
Rais Bill Clinton, alitua Tanzania, Agosti 27 mwaka 2000. Arusha-alialikwa na Msuluhishi wa Mgogoro wa Burundi,Nelson Rolihlahla ‘Madiba’ Mandela,wakati wa utiaji saini ule mkataba wa Amani ya Burundi. Hiyo haikuwa ziara ya kiserikali,bali ya kikazi tu.
Jumatano, Julai 13, mwaka 2005 mke wa Bush,Laura Welch Bush alitua Dar es salaam,kwa ziara ya siku mbili.
Mama huyu, alikuja Dar es salaam tena na mumewe. Kwake hiyo ilikuwa ziara ya tatu Afrika Mashariki, na ilikuwa mara ya tano kuja Afrika, Laura Bush ni mwenyeji Afrika.
Rais George Walker Bush, alikuja Dar es salaam Feburuari 2008. Ilikuwa ni miezi takriban kumi tu kabla ya Uchaguzi mkuu uliomweka madarakani Barack Obama.
Nataka kusema kwamba, hawa vigogo wa MAREKANI wanapofika nchini mwetu kwa ziara zao, sisi Watanzania huwekwa “Chini ya Ulinzi” mkali wa makomando na majasusi wa Taifa hili babe sana.
Makachero wengi sana wenye suti nyeusi na miwani ya jua hutuzingira hata mifumo ya maisha ikiwemo ya mawasiliano hukamatwa-ndege haziwezi kuruka tena,kwa kuwa viwanja vyetu huwa chini ya ulinzi,”No Fly Zone” mithili ya ile amri ya ndege kutoruka huko Tripoli, Libya!!
Uhuru wetu hutoweka kwa muda wote akina Hillary na Bush,Albright n.k wanapokuwa hapa kwetu.Bill Clinton alipotua uwanja wa Kimataifa Kilimanjaro,KIA huko Arusha, mijibwa ya Marekani ilinusa hata Mercedes Benz la mwenyeji wake.
Bendera za rangi nyekundu na nyeupe,zenye jumla ya nyota 50 hupepea kila mahali na kuzifunuka za kwetu.
Majibwa yanayodondoshwa madegeni,hunusa kila kitu,kila mahali, askari wetu na makachero wetu huonekana mithili ya askari mgambo tu-wasio na kazi!
Mawasiliano hata ya simu hukatwa,magari hukaguliwa au huzuiwa kutembea utadhani ‘Check Pont’ za Baghdadi,huko Irak. Hata waandishi wa habari wa kwetu hukosa uhuru huwa kama wafungwa magaidi,huko Abu Ghraib na Guantanamo Bay,Cuba!
Magari ya Zimamoto;Fire huachana na kuzima moto na kwenda kupiga deki barabara,omba omba na walemavu huondolewa mitaani wanakoomba,na kwenda kuswekwa rumande, hadi Bwana Mkubwa aondoke mjini!
Wakati huo,usafi huwa wa hali ya juu sana, Manisaa au Jiji hawalali na Mkurugenzi wake hukesha akisimamia usafi wa Barabara,umeme haukatiki ng’oo! Mpaka Bwana mkubwa aondoke!
Anapokuja Bush au Hillary Clinton, pumzi huwakatika viongozi wa Tanzania,tangu Mizengo Pinda hadi wafagizi wa barabara.
Shughuli zote za uchumi za kawaida husimama, mfumo wetu wa maisha wa kawaida huugua kiharusi, wapelelezi wote huwa kazini na safari aghalabu huwa ya siri sana.
Nakumbuka, wakati Bush anatua Dar es salaam Mtangazaji wa TBC Taifa alisema MAKACHERO wa Marekani walimsimamia sana ni kama walimweka chini ya ulinzi wakati alipotangaza tukio hilo hapo uwanja wa ndege.Walimtazama hadi mdomoni alipotangaza waone kama kulikuwa na bomu likitaka kuripuka!
Waandishi wa Tanzania waliwekwa chini ya ulinzi,walipigwa mtama,walipojaribu kuwania picha bora.
Sasa, naachana na hayo. Hivi wewe msomaji,unadhani kiongozi Mkuu toka Washington atakuja Dar es salaam kukaa siku mbili,tatu nne au tano kufanya mambo madogo madogo kama kukagua mashamba,Kibaha nkoani Pwani,kukagua miradi ya Afya,sijui Lishe halafu aende Mlandizi na kuangalia miradi ya umeme ya Marekani huko Ubungo?
Tuchukulie kwamba ni kweli kwamba Hillary Clinton alikuja Dar es salaam kwa ziara ya siku tatu,pamoja na mambo mengine,kuzungumza na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Kikwete na maofisa wa serikali ya Tanzania, ya Marekani nay a Ireland.
Je, walikuja mashushushu ama majasusi wangapi?Walidaka mambo mangapi? Walitupeleleza kiasi gani hadi siku moja waanze kutulipua kwenye mitandao yao ya kichizi,kama Wiki leaks?
Hidhuru,Bush kaja va vyandarua na miradi ya MCC na Global Fund.
Hata hivyo, siwaamini makachero wa Marekani,hususan Central Intelligence Agency,ambao kuja kwa Hillary Clinton hapa Bongo land kwa siku tatu hapa,ni kama kuwaleta majasusi wa kututazama hata utumbo!
Eti Mkewe Bush, yeye mwenyewe na Hillary Clinton waje kwetu tena wakae hapa siku mbili, tatu nne,tano wakodishe hoteli la nyota sita au tano kwa mwezi mzima kabla ya ziara kuanza hadi baadaye, waishie kukagua Lishe na mashsmba Dar?
Waishie kukagua ngoma za Wamasai na kwenda Mlandizi? Haiwezekani Bwana!
Kwanza, Marekani hutumia pesa nyingi mno kumweka mtu wao hapa kwetu-nchi masikini isiyo na usalama wa kutosha.Kumhifadhi Rais wa Marekani au huyo ‘Secretary of State’ katika nchi iliyowahi kupigwa mabomu na Al-Qaeda siyo jambo kidogo,kama unavyodhani.
Kumweka mtu wa Wamarekani hapa karibu na Somalia na al-Shabab,tena Dar karibu na Nairobi na Kampala ambako kote magaidi wa al-Qaeda na al-Shabab walishapiga mabomu, siyo kitu rahisi mno.
Ni suala la p esa na miundombinu ya ulinzi uliotukuka.Kuishi kwa mtu mkubwa wa Marekani katika nchi legelege kiulinzi halafu wao wakaondoka bila faida? Hapana kuna chumo Fulani wanalotafuta nyuma ya pazia.
Mtu akiniambia, Clinto alitumwa na Obama kuja Dar kuweka mipango thabiti ya kuwaangamiza al-Qaeda na al-Shabab,nitakubali kiasi. Akisema, Clinton kaja kulazimisha nchi za Mashariki mwa Afrika kuacha kumuunga mkono Gaddafi na magaidi wa Al Qaeda na al-Shabab kwa siri,tena kwa kusainishwa mikataba ya hila na ahadi ya misaada ya ghiliba,nitakubali!
Sasa, Marekani inahaha kuwatokomeza magaidi . Si unajua baada ya kumuua OSAMA Bin Laden Mei Pili mwaka huu huko Pakistan, al-Qaeda wameapa kulipa kisasi?
Sasa, ujio wa Mama Clinton Dar es salaam iliyowahi kupigwa mabomu na magaidi Agosti 7 mwaka 1998 ni kukagua mashamba na vinu vuya kufua umeme na kukagua MIRADI YA Lishe?
Bila shaka, Marekani wamekuja Dar es salaam na ‘AJENDA YA SIRI’ bila shaka kuwaburuza viongozi wetu wakubali matakwa yao kwa mikataba ya hila nay a siri sana.
Nimecheka kwamba hata wapinzani kama Prof.Lipumba walifyata mkia wakati Mama Clinton anatua,wasionekane ni watoto watukutu! Si unajua hata Kiiza Besigye wa Uganda kaenda Washington na New York kumshitaki, Museveni? Wapinzani hapa wana ubavu kwa mama Clinton? Thubutu!
Sasa, tunasubiri ziara hii ya Mama Clinton kama haina madhara kwetu-hata dawa ya babu wa Loliondo ina ‘side effect’.
Pengine, Mama Clinton kaja Dar kumfanyia kampeni Ban Ki Moon arejeshewe ukatibu Mkuu wa UN. Hata huyu Ki Moon aliwahi kuja Dar Jumatano, Feburuari 26 mwaka 2007. Siku iliyofuata Ban Ki Moon alikwenda Arusha kukagua Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya Uhalifu wa Kivita Rwanda kuhusu mauaji ya mwaka 1994, ICTR.
Labda, Clinton amekuja kutaka Mahakama ya ICTR,Arusha ikimaliza kesi za Rwanda isifungwe,bali itumike kuwafunga jela magaidi wa al-Qaeda na al-Shabab wanaoleta kitisho kwa maslahi ya Mrekani huku.
Waama, nikiachana na mashaka yangu,nampongeza Hillary Rodham Clinton kuja kukaa kwetu siku tatu, pasipo bomu kulipuka.
Kumbe Marekani wajue hata huku kwetu kuna maisha,kuna watu tunaishi,tofauti na wanavyodhani kwamba huku kwetu ni njaa ni vita na mabomu hulipuka-kuna amani na ustaarabu pia bwana!
Nakutakia safari njema mama Clinton!!
0786-324 074
Subscribe to:
Posts (Atom)