Thursday, August 18, 2011

pamba hujenga vitambi vya wakubwa


PAMBA, “Dahahabu Nyeupe” hulimwa katika mikoa 13 hapa nchini; ni katika wilaya 42; na huajiri wakulima kati ya 350,000 hadi 500,000 hivi.
 Mnyororo wa thamani ya pamba, unaajiri watu wapatao milioni 14.
 Hivyo,hili ni zao ambalo, kama lingeangaliwa vizuri,lingewatoa Watanzania katika lindi la umasikini wa kutupwa.
 Mikoa inayolima pamba hapa nchini, ni pamoja na Iringa,Tanga, Pwani,Kilimanjaro,Mbeya,Morogoro na Arusha,iliyo katika Kanda ya Uzalishaji wa zao hili ya Mashariki(Eastern Cotton Growing Area), ambalo pamba hulimwa,lakini haizalishwi sana.
   Hii ‘Dhahabu Nyeupe’ lakini wazalishaji wake ni masikini kupindukia,hulimwa sana hapa nchini katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza,Mara,Kagera,Tabora,Kigoma,Singida, na Rukwa, ambayo imewekwa katika Kanda ya Magharibi(Western Cotton Growing Area).
Mchango wa hii ‘Dhahabu Nyeupe’ wazalishaji wake fukara, mcango wake katika Pato la Taifa kwa msimu wa mwaka 2009/2010 ulikuwa asilimia 2.13; ni chini kabisa ya matazamio.
 Serikali, inajitetea kwamba, uzalishaji wa zao hili katika msimu wa 2010/2011 ulishuka kwa sababu ya ukame, na wakati mwingine mvua zilinyesha nyingi sana , hususan Musoma Mkoani Mara, mashamba yakatitia!
 Wakulima walishindwa kunyunyizia madawa ya kuulia wadudu mashambani mwao, kwa sababu eti ruzuku haikusimamiwa vizuri.
  Katika eneo hili hapa la madawa ya kuulia wadudu,mbolea na pembejeo nyingine,kuna uzembe na ufisadi wa hali ya juu unaowafanya wakulima walime,lakini pamba yao ikose viuwadudu, na hatimaye iliwe na wadudu, kwa sababu, waliopewa jukumu hili ama wamepora mbolea na kuiuza wanakojiua, au hata hayo madawa ya kuulia wadudu ni feki ama bandia, na hayafikishwi kwa wakulima kwa wakati.
  Kuna wakati, wakulima waliuziwa mbegu zilizochubuliwa kwa kemikali, wao wanaita ‘delinted seeds’ zikagoma kuota!
  Wakulima walilia; badala ya kulipwa fidia kwa utapeli huu,na kwa hasara waliyopata kutovuna msimu mzima, wakalipwa mbegu!!
  Kisheria,hii ni hujuma-ni kuhujumu uchumi wa nchi,kumuuzia mkulima mbegu mbovu zisizo na viwango vya ubora, counterfeit, ama double standard.
 Hili niliache kwanza.
   Msimu wa 2010/2011,(sasa huu ni msimu wa 2011/212) ulivunja rekodi, kufuatia mabadiliko makubwa ya bei katika sokola dunia.
  Bei ilipanda kutoka senti 86 za Dola ya Marekani,mwezi Agosti 2010 hadi Dola 2.44 kwa ratili moja mwezi Machi mwaka huu wa 2011.
  Rekodi iliyowahi kufikiwa ni senti 96 za dola ya Marekani, katika msimu wa 1994/95.
  Ratili mbili ni kilo moja, kwa sababu hiyo, katika msimu huu pamba iliuzwa hadi kwa dola 4.88 kwa kilo ambazo ni kama shilingi 7,320.
   Sasa, angalia.
Hata kama kuna kodi, kulipa riba mikopo ya benki(wanunuzi wa pamba hukopeshwa na mabenki,hususan CRDB),kulipa mishahara na tozo anuwai, ndiyo mkulima wa zao hili alipwe shilingi 600/= kwa kilo?
Katika msimu huu, Bodi ya Pamba nchini(Tanzania Cotton Board) imetangaza kwamba,bei ya kuanzia kununua pamba ni shilingi 1,100 kwa kilo.
Mwisho wa siku wakulima wamelipwa shilingi 800 kwa kilo, na wengine wamekopwa pamba yao huko mkoani Mara,na haijulikani watalipwa lini?
  Nataka kusema kwamba, hata kama bei imepanda msimu huu,kutoka shilingi 600/= mpaka  800/=wakulima walizouzia pamba msimu uliopita, ndiyo kitu kani kulinganisha na wanachokipata wenye vinu vya kuchambulia pamba?
  Yaani, bei ipande katika soko la dunia hadi kufikia zaidi ya shilingi 7,000 za hapa, wao walipwe shilingi 600 hadi 1,000!!
Wakati mwingine wamekopwa ama kudhulumiwa kabisa.
  Sababu za kupanda bei ya pamba msimu huo zilikuwa ni kupungua kwa akiba ya pamba duniani, yaani uzalishaji wa zao hili duniani ulipungua,na kulikuwa na mahitaji makubwa ya pamba katika viwanda vya nguo duniani.
  Hii ni fursa kwa wakulima wetu,hasa wa Ukanda wa Ziwa Victoria na mikoa mingine iliyotajwa.
Lakini, wameishia kulia njaa; pamba wameuza,lakini hawana kitu wanakabiliwa na njaa,hadi serikali imeombwa kuwapelekea chakula cha njaa, na maofisa wa serikali wakapata mwanya kusafirisha chakula hicho hadi Sirari,na kukiingiza nchini Kenya !
   Mkurugenzi wa Pamba, KANDA YA MAGHARIBI, Jones Bwahama, ameniambia mwishoni mwa wiki, kwamba mabadiliko ya bei yanaweza kutokea mwezi Oktoba hivi,baada ya wazalishaji wakubwa wa pamba duniani: China , Pakistan , India , Marekani,Uturuki n.k kuingia sokoni.
 Ni kama Bwahama alikuwa akiniambia kwamba, bei ya pamba yetu katika sokola dunia,hutegemea sana hali ya hewa ya uchina,Marekani,Uturuki n.k
 Hata hivyo, Bwahama akaniambia kwamba, pamba ya Tanzania inaweza kupanda bei kwa sababu kuna wawekezaji toka Thailand na Uturuki wanaonesha nia ya kuwekeza katika viwanda vya kufuma nyuzi(spinning) ili kuzichakata nyuzi za pamba,kuziongezea thamani,kabla ya kuziuza.
Bwahama, pia ameniambia kuna makampuni yenye matatizo ya kifedha yameshindwa kuwalipa wakulima,hususan mkoani Mara,sasa bodi inahaha mnunuzi mwingine apatikane kuinunua pamba hiyo!
  Hata hivyo, hata pamba ipande maradufu,katika soko la dunia,mbona mkulima anabaki masikini yuleyule; habadiliki.
   Badala yake, wanakuja watu matapeli, wanavuna pamba mgongoni mwake,wanajenga rosheni mijini,wananunua magari ya fahari kwa pamba hii hii “Dhahabu Nyeupe” yeye akibaki fukara anayesubiri chakula cha msaada kutoka serikalini!
  Bwahama, amesema katika msimu huu pamba inayotazamiwa kuvunwa katika eneo la hekta 477,354 nchini ni kilo 247,247,860; ni kama kilo 250,000.
 Mkoa wa Mwanza pekee unatazamiwa kuvuna kilo 54,122,750,lakini wakulima wa pamba wa Mwanza wataambulia nini, kama siyo vipapatio vya pamba?
 Mkoa wa Mara,unatazamiwa kuuza kilo 11,033,610 na Shinyanga ambao ndiyo wazalishaji wakubwa wa pamba wanategemewa kuvuna pamba yenye uzani wa kilo 160,968,875.
   Wakulima wa pamba wanalima kwa taabu, wakati mwingine mazao yananyauka kwa kiangazi, wanapofanikiwa kuvuna na kuuza wanakutana na ujanja ujanja,wizi na utapeli.
   Angalia;Wizara ya Viwanda na Biashara ilishapiga marufuku matumizi ya mizani aina ya Kapani, kununulia pamba tangu mwaka 2009.
  Kapani zinawaibia wakulima; nyingi zinachezewa na wanunuzi wa pamba na mawakala wao, zinaweza kuwapora wakulima hata kilo 15 nakuendelea.
   Serikali,ikasema kapani zisitumike, ziletwe mizani aina ya Salter kutoka Uingereza, ambazo haziwezi kuchezewa kwa urahisi.
  Wanunuzi wa pamba, wakaanza, mara “ooh,tumetoka kwenye mtikisiko wa uchumi, hatuna uwezo wa kununua mizani mpya na  kuzitupa kapani za mabilioni ya shilingi ghafla!”
 Mpango huo ukanywea,kwa sababu pia ilisemekana aina hiyo ya mizani mpya ilikuwa biashara ya wakubwa!
 Yaani, matatizo na changamoto za mkulima wa pamba,hugeuka ‘deal’ kwa maofisa wa serikali na matapeli,naam mafisadi!
   Nilizungumza na Ofisa Mkaguzi wa Pamba, Kanda ya Magharibi(WCGA),Buluma Kalibushi, juu ya mpango huo wa serikali kuondoa kapani zinazowaibia wakulima katika manunuzi ya pamba msimu huu.
  “Kapani zitaendelea kutumiwa,kwa sababu kuziondoa na kuleta mizani mpya ni suala linalohitaji maandalizi.
Kuna vituo kama 9,000 vya kununua pamba. Ukibadili mizani,unazungumza biashara ya shilingi takriban bilini tisa”.
   Kalibushi, aliniambia kwamba wanunuzi wa pamba wamezikataa mizani hizo kutoka Uingereza, kwanza walisema ilikuwa ‘biashara ya watu fulani’ kwamba zinatafutwa mizani bora zaidi.
 “Wanunuzi wa pamba wameleta sample(za mfano) ambazo ni za digitali,lakini haziku qualify(hazikukidhi viwango vya ubora)”
 Hizo kapani, zimewaibia wakulima na kuwaneemesha sana wanunuzi ambao katika pamba, wanauza pamba yenyewe, mbegu nazo mkulima anauziwa tena!
 Halafu, wanauza mafuta ya pamba yanayotumiwa kupikia chakula, na mashudu ambayo ni chakula cha mifugo.
  Wakati pamba ni dhahabu nyeupe, wakulima wa pamba hawana chakula,hawana nyumba wala maisha bora.
Mafuta yanaitwa “Black Gold” kwamba ni dhahabu nyeusi. Je, hatuwaoni wenye visima vya mafuta huko Arabuni, wakiwa matajiri?
 Iweje pamba iwe dhahabu nyeupe, lakini wakulima wa pamba hawana hata uwezo wa kupeleka watoto wao katika shule za kueleweka?
 Na shule wanazosoma watoto wao ni zile za kata,zisizo na waalimu na miundo mbinu?
 Nataka kusema kwamba, Bodi ya Pamba, haina wafanyakazi wa kutosha ili kuwabaini wanunuzi wa zao hili huko vijijini.
 Hawa wanunuzi na mawakala wao,kazi yao ni kuiba uzani wa pamba ya mkulima-ndiyo maana naye akaamua kuweka mawe,mchanga na maji katika pamba ili kuongeza uzito,maana naye anaporwa!
  Hata hivyo, kuna msemo wa Kiingereza, “Two wrongs can’t make a One Right” Kwamba kosa moja lisihalalishe kosa lingine.
  Huku ni kushusha thamani ya pamba katika masoko ya kimataifa, na mwisho wa siku atakayeumia ni mkulima wakati pamba yake inapokosa soko.
   Tunazungumza suala la ukosefu wa ajira,wakati pamba ingeweza kuwalipa wakulima 500,000 wakawa na maisha mazuri na wengine milioni 14 wangeajiriwa na pamba, ukosefu wa ajira ungetoka wapi?
   Tatizo,ni kukosa watu wenye utashi wa kisiasa na wazalendo wa kutaka kuendeleza nchi na fursa zake.
 Inapotokea, kuna wizi huu na uporaji katika sekta ya pamba, hakuna anayewajibika isipokuwa mkulima anawajibika mwenyewe kwa umasikini kuongezeka.
 Sasa, kuna wanunuzi binafsi wa pamba,na kilimo cha mkataba,ni yaleyale.
Nilidhani, KILIMO  KWANZA , ingekuwa kampeni kali ya kuondoa mianya ya rushwa,wizi na utapeli katika sekta ya kilimo hasa katika mazao ya biashara.
Lakini, bado wezi wanaachwa,wanabebwa pasipo kufungwa jela,halafu wakulima wanabaki masikini-tunaimba kwamba eti hatujui kwa nini wananchi ni masikini katika wingi wa fursa hizi!
  Nadhani, tumeona ni akina nani hasa wanaojenga vitambi kwa pamba ya mkulima.Serikali inajua,na inayasema haya kila mara,utekelezaji haupo!!
 Juma lijalo nitatazama uvuvi wa samaki,hussan sangara,ziwani Victoria
     0786 324 074

No comments:

Post a Comment