MWANAHALISI wa Afrika, “The Great
Son of Africa”, “Tata” Mandela, amepumzika kaburini baada ya kuwa mahututi
tangu Juni mwaka huu.
Ilikuwa vigumu Mandela kuishi katika hali ya
maradhi mabaya ya mapafu na kupumulia mashine tangu awe mahututi miezi sita
iliyopita.
Sasa,Mandela amefariki nyumbani
kwake Desemba 5, saa 2: 57 usiku huko Johennesburg.
Binafsi,nilikuwa nimepoteza
matumaini ya mtu huyu nimpendaye sana kuishi,japo afikishe miaka 100 kamili
ifikapo Julai 18,mwaka 2018.
Nelson Rolihlahla ‘Madiba’ Mandela,
alizaliwa Julai 18 mwaka 1918 katika kijiji cha Mvezo,katika Jimbo la Eastern
Cape,Afrika ya Kusini.
Alikuwa mwanaharakati mashuhuri sana
katika kupinga ubaguzi wa rangi wa Chama cha African National
Congress(ANC)kinachoongoza sasa Afrika ya Kusini.
Miaka 27 ya uhai wake aliitumia
akiwa jela,kufuatia harakati zake za kuwapinga Makaburu wa Afrika Kusini na
siasa zao za Kibaguzi zilizoungwa mkono na Mataifa makubwa ya Magharibi.
Muda mwingi akiwa jela, akawa
anaponda kokoto mchana wa hari akiwa hana viatu,hususan huko Kisiwa cha Robben,ambacho
sasa ni kituo cha utalii.
Watu huenda kuona chumba alicholala
shujaa huyu wa karne hapa Afrika na dunia nzima.
Namba yake ya jela, ‘46664’ itakaa
kama ALAMA ya harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika, na katika harakati za
uhuru hapa Barani.
Mtu huyu, ambaye sasa ni marehemu,aliachiwa
huru na Makaburu Feburuali 11 mwaka 1990, na akawasamehe waliomsweka jela kwa
jumla ya miaka 27.
Ni mzaliwa wa ukoo wa Thembu,katika
kijiji cha Mvezo,wilaya ya Umtata,mji mkuu wa Transkei.Anatokana na ukoo wa
Chifu Ngubenguka(alifariki 1832).
Babaye, Gadla Henry
Mphakanyiswa(1880-1928) aliwahi kuwa chifu wa Mvezo,akapokonywa uchifu na
wakoloni wa Kiingereza.
Mzee huyo alikuwa na wake
wanne,akazaa watoto 13,Mandela alikuwa mtoto wa mke wa tatu,NESEKENI
FANNY,Binfi wa Nkedama wa Mpemvu,wa kabila la XHOSA.
Jina la Rolihlahla maana yake ni
‘Kuvuta Tawi la Mti’ lenye kumaanisha ni mtu mwenye fujo!
Akiwa na umri wa miaka saba
alikwenda shule, mwalimu wake aliposhindwa kutamka jina la Rolihlahla, akampa
jina Nelson kwa heshima ya Mkoloni Mwingereza,Horatio Nelson.
Baba yake alifariki Mandela akiwa na
miaka tisa tu; ikabidi sasa alelewe na rafiki wa baba yake.Mandela alisoma
shule ya misheni ya Wesleyan.
Akaingia jandoni akiwa na umri wa
miaka 16,kabla ya kwenda kusoma Clarke bury Insitute,alikotunukiwa cheti.
Aliwahi kucheza ndondi na
riadha.Hapa namkumbuka mwanamasumbwi Nguli,Mweusi wa Marekani aliyetukanwa
udongo wa mfinyanzi kufuatia kuwa Mweusi,Mohammed Ali.(Clay).
Mandela, alisoma Shahada ya kwanza
katika Chuo Kikuu cha Port Hare, alipokutana na Mpigania uhuru mwenzake,Oliver
Tambo.
Tambo, alikuja kuwa kiongozi wa ANC
kabla ya kufariki dunia.Mandela aliwahi kuwa karani katika kampuni sheria mjini
Johannesburg; alisaidiwa kupata kazi na Walter Sisulu.
Baadaye, alisoma sheria
Witwatersand, ambako alikutana na wanaharakati wengine.Mandela na Oliver Tanbo
waliendesha kampuni ya uwakili ili kuwasaidia Weusi waliokuwa wakikumbana na
madhila ya kunyanyaswa na Makaburu.
Desemba 5, mwaka 1956 Mandela na
wenzake walitiwa mbaroni na wenzake 150 na kushitakiwa kwa makosa ya
uhaini-walishinda kesi hatimaye wakaachwa huru.
Johannesburg,ndiko aliswekwa rumande
baadaye,baada ya kutafutwa sana na Shirika la Ujasusi la Marekani,Central
Intelligence Agency(CIA).
Nataka msomaji,hasa vijana wa siku
hizi kujua kwamba Marekani na washirika wake,waliwasaidia Makaburu na wakoloni
wengine kuwahujumu Weusi wasije kujitawala siku moja katika nchi zao wenyewe.
Naam,leo hung’ata na kupuliza,na
wajinga wote wanaona Mataifa haya ndiyo ‘Masihi’ na mabingwa wa demokrasia na
Haki za Binadamu,kumbe ujinga mtupu!
Marekani na Shirika lake la CIA
ambao hupigiwa goti siku hizi,wakishirikiana na Makabuu wa Afrika ya Kusini na tawala
za Kiimla(Authoritarian) wakamshitaki Mandela kwamba alichochea mgomo wa
wafanyakazi na kutoroka nchini kinyume cha sheria.
Yawezekana,ni wakati huu Mandela na
wanaharakati wenzake walikuwa Mazimbu,Morogoro katika Makambi ya wapigania
uhuru-Tanzania.
Oktoba 25 mwaka 1962 Mandela
alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.Akiwa jela, huku nyuma polisi wa
Makaburu waliwasweka rumande wanaharakati wengine wa ANC, akina Walter
Sisulu,Govan Mbeki na wenzao.
Juni 12 mwaka 1964 wakahukumiwa
kifungo cha maisha jela.
Kati kesi hiyo MANDELA pia
aliunganishwa,wakapelekwa Kisiwa cha Robben mahali ambao Mandela akakaa miaka
18.
Kazi yao ilikuwa kugonga miamba na
kuipasua ili kupata kokoto za kujengea jela imara sana za Makaburu ili
wafungwa(WEUSI)wasitoroke.
Machi,1982 Mandela alihamishiwa
Polls moor, akiwa na wenzake wa ANC akina Walter Sisulu.
Feburuari,1985 P.W.Botha, alimpa
Mandela ‘Offer’ ya kuachiwa huru kwa masharti kwamba aachane na harakati za
uhuru wa Mtu Mweusi.
Mandela alikataa ‘offer’ hiyo akatoa
taarifa kupitia binti yake,Zindzi akisema:
“Uhuru gani ninaopewa wakati taasisi
ya watu inabaki imepigwa marufuku? Hata hivyo,mfungwa hawezi kuingia mikataba!”
Mandela aligoma kuachwa huru-uhuru bandia.
Wewe kijana wa sasa ulishaona wapi
msimamo mkali wa Mwanahalisi wa Afrika (The Great Son of Afrika) mithili ya MANDELA?
Makaburu WALIFANYA MKUTANO NA
Mandela mfungwa mwaka 1985 Novemba, katika hospitali ya Volks, Cape town
alipokuwa akitibiwa saratani-alikutana na waziri wa Makaburu,Kobic Coetsee.
Mwaka 1989,PW Botha aliugua
kiharusi,nafasi yake ikachukuliwa na Frederic Willem de Klerk,rais wa Kwanza
Kaburu Barani Afrika, wenzake walikuwa Mawaziri wakuu, akatangaza kuwa Mandela
angekuwa huru mwaka 1990.
Waafrika tukafurahi,mtu huyu kipenzi
cha watu kuwa huru
.Alipewa nishani ya Amani ya Nobel,yeye
na De Clerk mwaka 1993.
Baadaye Makaburu walimuua Chris
Hani,Aprili 1993.Mandela alikuwa rais Afrika ya Kusini akiwa na miaka 77 mwaka
1994, akaja kustaafu mwaka 1999.
Aliapishwa kuwa Rais wa kwanza Mweusi
wa Afrka ya Kusini Mei 10, mwaka 1994,de Clerk akawa Makamu wa Kwanza wa rais
na Thabo Mbeki akawa Makamu wa Pili katika serikali ya Umoja wa kitaifa kama ya
Zanzibar hivi.
Utawala wa
Makaburu(Boers)ulikumbatiwa na Uingereza na Marekani;wakati watu zaidi ya
14,000 (Weusi)walipouliwa huko Zulu,katika miaka ya 1980.
Tumeona Mobutu akisaidiwa na mataifa
haya ambayo siku hizi hujidai ‘Masihi’ hapa duniani,na huimba demokrasia na
Haki za Binadamu kwa midomo bila vitendo.
Mobutu,na hawa,waliwasaidia Waasi wa
Angola kukipinga Chama cha Ukombozi, Popular Movement for the Liberation of
Angola(MPLA),uhuru usipatikane kutoka kwa Wareno,hadi nchi ikabaki vitani kwa
muda mrefu.
Mobutu na hawa rafiki zake, Ungereza
na Marekani, walimsaidia Jonas Malheiro Savimbi na Chama chake cha Unita,
kilichopinga uhuru wa Angola.
Tumeona harakati za uhuru nchini
Afrika ya Kusini chini ya African National Congress (ANC) zikiwa zimeharamishwa
na utawala dhalimu sana wa Makaburu hadi Rais De Clerk alipokuja kuondoa
marufuku hiyo Feburuari 1990
“Tata”Mandela aliachiwa huru kutoka
Greza la Victor Verster, lililopo Paarl Feburuari 11 mwaka 1990. Ni tukio la
kihistoria kuachiwa kwa Mandela; ni kama Afrika ilipata uhuru mwaka 199
Mtu huyu, “Tata” Mandela,alitangaza
msamaha kwa Makaburu waliomtesa; ikaunfdwa Tume ya Ukweli na Maridhiano(THE
TRUTH COMMISSION) iliyoongozwa na Askofu Desmond Tutu.
Mandela alikiri chama chake (ANC)
kuunda tawi la jeshi(Umkontho we Sizwe) kwa nia ya kujilinda na kujihami dhidi
ya siasa za ubaguzi wa rangi; siasa zilizoandamana na dhuluma na mauaji ya
kinyama dhidi ya wazalendo na harakati za ukombozi.
Mandela na De Clerk walitunukiwa
baadaye tuzo ya Nobel ya Amani,mwaka 1993.Aprili mwaka huo 1993 ndipo Mpigania
uhuru Chris Hanni alipouliwa na utawala wa Makaburu,rafiki wa Uingereza na
Marekani.
Mandela, ameishi siku zote kama
Mwafrika halisi; akachaguliwa kuwa rais mwaka 1994 akiwa na umri wa
miaka 77-na alistaafu mwaka 1999 akamwachia kiti Thabo Mvuyelwa Mbeki,mmoja wa
wana wa mashujaa wa mapambano dhidi ya Kaburu jeuri.
ANC kilishinda uchaguzi wa 1994 kwa
asilimia 62 ya kura.Mandela aliapishwa kuwa rais wa Kwanza Mweusi Mei 10,mwaka
1994,wakati Kiongozi wa National Party, de Clerk akiambulia Umakamu wa Kwanza
wa rais;wakati Thabo Mbeki alipopewa Umakamu wa Pili katika serikali ya Umoja
wa Kitaifa.
Naam, tunamkumbuka ‘Tata’Mandela kwa
mashati yake ya Batiki.
Ama ‘Mandela Shirts’ yanayovaliwa siku hizi
hata na akina Rais Jakaya Kikwete.
Uchaguzi wa kwanza huru Afrika ya
Kusini ulifanyika Aprili 26-29,mwaka 1994,ANC kikapata asilimia 62,National
Party cha Makaburu kikapata asilimia 20.4.Inkhata Freedom Party cha Chifu
Mangusuthu Butelezi kilipata asilimia 10.5.
‘Tata’ Mandela alipata kuoa mara
tatu; ni baba wa watoto sita,wajukuu 22 na vitukuu vingi. Mmoja wa wajukuu zake
ni Chifu Mandla Mandela.
Mzee huyu kipenzi cha Afrika
alifunga ndoa ya kwanza na Evelyn Ntoko Mase kutoka kwao Mandela huko
Transkei.Walikutana Johannesburg-walizaa wavulana wawili,Thembikile ama Thembi mwaka
1946,Magkatho alizaliwa 1950 na wasichana wawwili waliopewa jina moja,Makaziwe,
“Maki” mmoja alizaliwa 1947 na mwingine 1953.Mwingine alifariki dunia kabla ya
kufikisha umri wa mwaka mmoja.
Ndoa ya Mandela na Evelyn Mase
ilivunjika baada ya miaka 13(mwaka 1957),Mandela alikuwa haonekani nyumbani kwa
muda mrefu,akiwa ‘Msituni’katika harakati za Ukombozi,mama huyo na imani yake
ya kilokole ya Mashahidi wa Jehova, aliamua kwenda zake,akaachana na Mandela.
Thembi, alifariki katika ajali
ya gari mwaka 1969 akiwa na miaka 25 wakati huo Mandela alikuwa selo, Robben
Kisiwani.Hawa watoto walisoma shule moja,baadaye Evelyn alifariki dunia 2004.
Ndoa ya pili ya Mandela ni ya Winnie
Madikizela-Mandela, huyu ‘Iron Lady’ kutoka Transkei.Watoto wa Mandela na
Winnie ni wasichana wawili:
Zenani au Zeni(Feburuari 4,1958) na
Zindzishwa ama Zindzi aliyezaliwa 1960.
Walitengana Aprili 1992; mwaka 1996
waliachana kabisa.Juzi, Winnie alikwenda kumtembelea Mandela hospitalini
anakolazwa.
Kaka mkubwa wa Mfalme wa
Swaziland,Mswati III,Prince Thumbumuzi Dlamini alimuoan Zenani mwaka 1973,na
wanaisti Boston,Marekani.
Mwaka 1998,Mandela alimuoa Graca
Machel nee Simbine wakati alipokuwa akiadhimisha ‘Birth Day’ ya 80.
Mwaka 2003,Cable News Network(CNN)
walitangaza tanzia ya Mandela.Mwaka 2007 pia ‘wasela’walitangaza kifo cha
Mandela,wakiwataka Wazungu kwenda kwao,la sivyo wangechinjwa!
Mtu huyu, ‘Tata’ Nelson Mandela ni
kielelezo cha Mzalendo wa kweli,Mwanahalisi wa Afrika aliyeitwa ‘Gaidi’ na
utawala wa Makaburu wa Waziri Mkuu PW Botha, aliyejiuzulu Agosti 14, mwaka 1989
ndipo akaingia De Clerk aliyemwachia huru Mandela.
Utawala wa Makaburu uliua watu
wengi,si Afrika Kusini tu bali hata Msumbiji walifanya njama na kumuua Samora
Machel mwaka 1986.
Naam,namkumbuka ‘Tata’Mandela, ambaye
namba yake ya jela ilikuwa 46664. Tunawakumbuka wanamapinduzi wa Afrika ambao
wamemwaga damu wakipigania uhuru wa watu wao, si ulaji wa matumbo yao
kama watu wengine wanavyotaka kuitwa leo.
Namkumbuka Samora Moises Machel,John
Garang de Mabior ‘ Chris Hani na wenzao.
No comments:
Post a Comment