Thursday, April 7, 2011

Kwa nini  uchaguzi wa 2010 Maalim  Seif hakusema kaibiwa kura, Zanzibar?

 KWANINI?!

   Na ni kwa sababu gani,Maalim Seif Sherrif Hamad, ambaye amekuwa akigombea Urais Zanzibar,kwa tiketi ya Chama cha Wananchi(CUF) tangu mwaka 1995 hadi  Oktoba 31 mwaka jana-akashindwa mara zote,  hakupinga matokeo?
    Kwanini,Maalim Seif amekubali kushindwa kirahisi mno mwaka 2010 wakati mwaka 1995, 2000 na 2005 alipinga kwa nguvu kubwa?
 Je, safari hii haukuwa ‘uchafuzi’ tupu na bahasha za khaki, bali ulikuwa uchaguzi huru na wa haki?
 Kwa sababu gani, Maalim Seif na Chama chake cha CUF,wamekubali matokeo upesi; kwamba mgombea wa Chama cha Mapinduzi(CCM),Dk. Ali Mohammed Shein aliibuka mshindi kwa asilimia 50.1 zilizopigwa, dhidi ya kura zao walizopata ambazo ni asilimia 49.1?
 Ni kwa misingi gani, CUF wamekubali kushindwa kirahisi, Zanzibar kisha Bara, hadi wakahudhuria sherehe zote mbili za kuapishwa  marais wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) na ile ya Jamhuri ya Muungano(SJMT), wakati wenzao wa Chama cha Demokrasia na Mendeleo(CHADEMA) wanapoweweseka na kumsusia Rais Jakaya Kikwete,huko Bungeni, Dodoma mwishoni mwa mwaka jana?
    Naam. Tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe hapa nchini mwaka 1992,CUF kimekuwa kikimteua Maalim Seif kugombea urais Zanzibar.
  Kwa sababu hiyo, Malim Seif amegombea urais Zanzibar mwaka 1995, 2000,2005 na mwaka  2010,mara zote bila mafanikio.Ameshindwa kwa asilimia 100.
  Katika chaguzi zote tatu zilizotangulia, 1995,2000 na 2005,Maalim Seif na chama chake cha CUF wamekuwa wakidai kuibiwa kura, ama kupokonywa usdhindi na Tume ya Uchaguzi, Zanzibar(ZEC).
 Katika uchaguzi mkuu wa 2000 kulitokea mtafaruku mkubwa uliosababisha umwagaji damu Januari 26 na 27,mwaka 2001.
 Kwa mara ya kwanza,baada ya ukimbizi wa akina Oscar Kambona, Tanzania iliingia katika ‘rekodi’ ya kuwa na wakimbizi huko Shimoni, Mombasa.Sababu za ukimbizi huu zilitokana na madai ya Maalim Seif kuibiwa kura ama kupokonywa ushindi dhahiri, Zanzibar.
  Nataka kusema kwamba, Chama cha CUF kimekuwa hakitambui matokeo na ushindi wa urais,wa CCM visiwani Zanzibar tangu mwaka 1995 zama za ‘Komandoo’ Salmini Amour na hata zama za Rais Mstaafu, Amani Abeid Karume,mwaka 2000 na 2005.
 Katika chaguzi hizo zote nne, wagombea wa CCM,  Dk.Salmin Amour, Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohammed Shein wamekuwa wakiibuka washindi kwa mbinde; kwa tofauti ya kura chache.
 Tumejadili kuwa urais wa “Komandoo” Salmin Amour na ule wa  Dk.Amani Abeid Karume,umekuwa hautambuliwi na CUF; hivyo kuzua sokomoko kubwa Visiwani.Watu wamepata kudundwa na polisi, wengine waliuliwa na akina mama kubakwa,hususan katika kijiji cha Piki, huko Pemba.
 Ni kwa sababu hii, Rais Mstaafu, Amani Abeid Karume wa CCM na Katibu M kuu wa CUF, Maalim Seif aliyegombea mara zote na kushindwa katika mpasuko mkubwa Zanzibar, walikutana na kufanya maridhiano.
 Hatua hiyo,ikapongezwa na Wazanzibari wote,ikafuatiwa na CUF kuutambua ushindi wa Karume,ingawa hatua hiyo ya kumtambua Karume ilikuja mwishoni mwa mhula wake wa pili.
 Ilikuwa mithili ya CUF ‘kukumbuka shuka asubuhi’. Ikaja hoja ya miamba hawa wa siasa kutaka Katiba ya Zanzibar irekebishwe ili Karume aongezewe muda wa kutawala Zanzibar japo kwa siku 720!
 Maana yake ni kwamba,CUF walitaka uchaguzi usifanyike humo visiwani Oktoba 31 mwaka  wa 2010.Karume aendelee kutawala kwa miaka miwili;labda uchaguzi ungefanyika 2012!
 Hawakumtambua Karume kwa miaka 10.
Pia, hakuutambua urais wa Dk. Salimin Amour kuanzia 1995 hadi mwaka 2000.
Sasa, wanamtambua Karume kuanzia 2010 kwa sababu ya maridhiano waliyofanya; ili kuleta serikali ya Umoja wa Kitaifa,ili kuondoa Mpasuko, Zanzibar.
 Naam. Kufuatia kura za maoni,kukubali iundwe serikali ya Umoja wa Kitaifa, inayowashirikisha vigogo wa vyama vyote viwili katika utawala,CCM na CUF, wapinzani wengine nao wakaomba washirikishwe,bila mafanikio.
  Ni miezi mitatu hivi imepita,tangu kura ya maoni, na ni takriban miezi minne tangu tusikie mwangwi wa CUF kuanza kumpigia debe Karume kusalia madarakani, Zanzibar kwa siku 720!!
 Hata hivyo,uchaguzi wa Oktoba 31 mwaka jana  umekuja, mgombea wa CCM,Dk. Ali Mohammed Shein akaibuka mshindi  finyu kwa asilimia 50.1 dhidi ya 49.1 za CUF; hakuna kulalamika.
 Uchaguzi, ati ulikuwa, “Free and Fair” na hakuna mshindi na mshindwa,Zanzibar….wagombea wote wameshinda!
   ‘Ngangari kinoma’ sasa shwari,tangu bahari ya Hindi hadi Ziwa Tanganyika; naam tangu ziwa Victoria hadi Mto Ruvuma, hakuna mawimbi ya ‘Mapanga shaa’ Ngunguri zimekuwa Ngingiriii!
 Mwaka 2005Tume ya uchaguzi Zanzibar(ZEC)ilipomtangaza Karume kuwa mshindi kwa asilimia 53.2 ya kura zilizopigwa CUF walisusa kutambua matokeo; na hawakuhudhuria sherehe za kumwapisha.
 Balozi za nje hususan Marekani na Uingereza walisusa sherehe za kumwapisha Karume kwa madai kwamba uchaguzi ulighubikwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu.
 Nakumbuka, hata ubalozi wa Norway ukataka ufanyike uchunguzi huru kuhusu kilichotokea Zanzibar Oktoba 30 mwaka 2005,baada ya uchaguzi kuleta sokomoko kubwa.
 Bunge la Uingereza likaja juu sana juu ya kilichotokea Zanzibar. Ilikuwa kabla ya Maalim Seif na Dk. Juma Duni Hadji(maarufu Mjela-jela)kuteuliwa kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,kasha kushirikishwa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa, Zanzibar.
   Naam, ni kwa sababu hizi sasa naona hakuna ‘kimembe’ visiwani kama kile cha 1995,2000, na 2005.
 Badala yake, tunawaona sasa vigogo wa CCM na CUF wakishikana mikono na Karume na Dk. Shein na kuahidi kushirikiana na serikali ya CCM!
 Sipendi kuamini kwamba CUF  sasa ni ‘CCM-B’ Hayanihusu. Isipokuwa,tumewaona CUF wakisalim amri kwa Rais Jakaya Kikwetena kutambua ushindi wake wa asilimia 61. wakati wenzao wa Chadema wanalalama kuibiwa kura.
Siwabezi CUF, Na siyo nia yangu kuwapigia debe Chadema. Nawahadharisha wasomaji wangu,watafakari kwa makini,ni kitu gani kinawaongoza wapinzani kupinga matokeo,halafu wanapoitwa mezani na kupewa ‘vipapatio’ vya vyeo katika serikali waliyopinga, na kuomba Jumuiya za kimataifa kuwaunga mkono, wanaanza kuipigia debe kwamba isalie madarakani kwa siku 720!
   Chama tawala kinamshinikiza mtu wao kuheshimu katiba,wao wanasema katiba ivunjwe,yule adui yao sasa atawale kwa nyongeza ya miaka miwili! Kwa nini? 
Kwa sababu gani? Tunaambiwa ‘maslahi ya wananchi’.Sawa,
  Mashabiki na wapigadebe wa vyama sasa wanivumilie ninapojadili ni kwa nini na kwa sababu gani CUF wamelalamika mihula mitatu kwamba waliporwa ushindi, Zanzibar?
 Idadi ya kura ni ile ile tangu 1995 hadi 2010, wapiga kura ni wale wale tu, matokeo ni yale yale tu ya ushindi mwembaba wa wagombea wa CCM.
 Mzingira ni yale yale tu, masheha ni wale wale, labda tofauti ni ‘Maridhiano’ na kuundwa serikali ya Umoja wa kitaifa, na tayari ubishi wa nani mshindi halali Zanzibar ama hapa Bara,hauna tija.
   Ni kwa msingi huu, nakuwa na tashtiti.Kama Chadema watashikilia uzi kwamba waliibiwa kura.
   Ikitokea,Rais Kikwete akawaita mezani ili wajadili kuundwa kwa serikali ya Mseto ama ile ya Umoja wa kitaifa ama mfano wa zile zifanyazo kazi huko Kenya na Zimbabwe, “The Joint Operations Command”(JOC), watakataa? Wanakubali na kumsifu,kumtaka aendelee kutawala kinyume na katiba!
  Tumewaona wapinzani ‘wakikomaa’ kudai waliibiwa kura.Kumbe, wakiitwa kugawana ulaji,chini ya usimamizi wa akina Kofi Annan, Ban Ki Moon, Hillary Rodham Clinton ama Obama-wanatulizana mithili ya maji mtungini!
  Wanamtambua rais aliyeapishwa,naam aliyetangazwa mshindi,halafu wanaanza kumwombea dua aendelee kutawala hata nje ya matakwa ya katiba.
 Aliyekuwa akiitwa shetani, anakuwa malaika.
  “Champagne’ zinafunguliwa pale, picha za pamoja zinapigwa kwa fujo, chama tawala na wapinzani waliokataa matokeo-wanapokubaliana kugawana uhondo; ‘Tik-tik! Tik!!”
 Nachelea kusema hapa kwamba, kama tuonavyo Zanzibar,Kenya na Zimbabwe au kama iitwavyo kwa utani,”Zim Country” hata hapa Bara wanaweza kuwepo wanasiasa wanaotaka ku, “manipulate a situation to benefit themselves at the expense of others”.
   Tafsiri yangu:Wanasiasa wa chama  ‘twawala’ wanaweza kushindwa uchaguzi,wakachakachua matokeo,ukaja mgogoro,wakalazimishwa na jumuia za kimataifa kugawana vyeo na wapinzani,kama ilivyotokea Kenya na Zimbabwe.
   Waaama, mtu anashindwa kihalali kabisa; anakomaa wee!
Anadundwa virungu mfano wa Morgan Richard Tsvangirai huko Zimbabwe, anaota manundu kwa virungu vya polisi,yumo tu!
 Raia wanaomuunga mkono wanaingia barabarabi na mawe na matofali ili kumsaidia(Nguvu ya Umma),wakadundwa hadi wakafa!
 Kisha Jumuia za kimataifa zikawaambia wakae meza moja wajadiliane kugawana ‘Ulaji’ Bahari ikatulia,kukawa shwari.
 Naam, huku ndiko ku-“benefit your self at the expense of others!” yaani kujinufaisha kwa gharama(damu) za wenzako!
  Yawezekana,nina macho yenye makengeza,lakini jiulizeni: Kwanini Malim Seif safari hii kawa wa kwanza kutambua ushindi wa Shein Zanzibar, ba Prof Lipumba akakiri kushindwa na Kikwete asubuhi tu?
  Kwa nini ilikichukua chama cha CUF miaka takriban 20 kugoma kutambua ushindi wa CCM Zanzibar hadi juzi walipoonjeshwa madaraka,wakatambua ushindi wa CCM Bara na Visiwani mara moja,wakati Chadema wanaposhindwa kuamini kilichotokea?
    CUF wana macho gani na Chadema ni vipofu wasioona ushindi wa CCM hadi waitwe mezani na kufunguliwa ‘Champagne’?
  Wabunge wa Chadema wanapomsusia Rais Kikwete bungeni,Dodoma, ni ‘geresha’ tupu,siasa, mtazamo makengeza, na kuhafifisha matumaini ya waliowapigia kura?
 Mimi sijui.
   Nikijuacho ni kwamba, hatupaswi kushikilia ukweli tu, bali pia tuuache huo ukweli utushikilie.

0786/0754-324 074

No comments:

Post a Comment