WANAWAKE wengi(kasoro mke wangu , mkeo na wengine wachache)hutafuta mwanaume mwenye pesa ili waolewe naye. Lengo lao ni kufikia pesa. Wanakwenda hata kwa sangoma,ili awasaidie kupata mwanaume atakayewalipia Ankara zao za umeme,maji na kila starehe. Mwanaume atakayewanunulia vocha za simu, atakayewanunulia vivazi vya gharama kubwa, magari ya kutembelea kama BMW, Mercedes-Benz, n.k Akina dada wa kileo, wako mbioni kuwasaka mibuzi na marafiki wenye uwezo wa kifedha. Watakaowapeleka “Out” mahali pa starehe pa gharama, kisha kuwanunulia zawadi za thamani kubwa, mithili ya Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy kwa kidosho chake kipya, Carla Bruni. Naam, wasomi na warembo kumshinda Malkia Cleopatra wa Misri, wanawasaka kwa udi na uvumba, wachumba watakaomudu kuwanunulia kila wakitakacho, ili waonekane, “Material Girls” kama Naomi Campbell ama Madonna! Akina mama na wasichana wa siku hizi, huwapenda wanaume wenye fedha nyingi kama David Bekham, watakaomudu kuwalipia ‘Bill’ zao. Naam, watakaoonesha penzi kwa vitendo; na aslani siyo wenye mikono ya birika na pesa za mawazo. Hawa warembo wa siku hizi, hawapendi kupewa ahadi utadhani wagombea kwa wapigakura wao. Siku hizi, hapendwi mtu,bali pesa zake! Maadili huwaonya wasichana kuacha kuuza utu wao na miili yao kwa pesa, kwa mapenzi yanayodumu kitambo. Mahaba ya pesa huja upesi kama umande,leo na hutoweka mapema kesho(easy come,easy go) hata kama mtu anazo pesa,lakini kashindwa kuzimwaga. Akina ‘Chuma Ulete,hasara si ajabu’ndiyo wenye turufu ya ushindi katika mnada huu wa mahaba. Wale wanaoamini kwamba mapenzi ya dhati hayana mzizi kukesha baa au sehemu za starehe, hawana chao. Kila msichana siku hizi huwaza kuolewa na mwanamume mwenye ukwasi-mwenye pesa. Hata watoto wanawaza kuzaliwa na wenye pesa-kuangukia penye pesa. Kila mtu anawaza huba la fedha;naam huba la tashtiti. Akina dada wasomi wanafikiri kuolewa na wanaume matajiri,wenye pesa kama ‘Becks’ wanawaza kufikia pesa. Wanafikiri kufunga ndoa za gharama na matajiri wenye fedha chekwa chekwa,potelea mbali ndoa zenyewe ziwe “Ndoa ndoano” mradi wamefaidi kwa kitambo. Naam, ndao za fahari, maisha ya fahari,kula kunywa na kuvaa kwa fahari na utukufu wa utajiri. Kutohangaika-hangaika,kufua-fua manguo,kuosha vyombo kila mara,bali kujilaza-laza sofani muda wote huku ukitazama televisheni kubwa mbele zako, na jioni kujimwaga kula maraha katika kumbi za sterehe na burudani. Nani ataka kuolewa ili kupika-pika,kufua-fua,kupiga deki nyumba siku hizi utadhani ‘House Girl’? Badala ya kufaidi ndoa yenye amani na fedha chekwaa? Akina dada wanatamani sana maisha matamu,ambayo hukolezwa na kuedesha magari ya thamani kama Mercedes-Benz kama ile SL 65 AMG, inayotimka mwendo kasi zaidi ya kilomita 350 kwa saa, ili kuwahi ‘appointment’. He! Mwaya, wee kalaghabao na huyo mume suruwali wako.Wanawake(kasoro wachache) hutamani kuolewa ama kuvikwa pete ya uchumba na watu kama Carlos Slim ama Bill Gates. Wanapoolewa wanataka kuendesha BMWs, Audis ama Merces.Wewe una mkokoteni, wa nini katika gulio la huba la vimwana? Unajua? Carlos Slim wa Mexico anaongoza duniani kwa ukwasi wenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 53.5. Anafanya biashara za mawasiliano; atapendwa na kila mwanamke mrembo duniani. Anayemfuata, ni huyo Bill Gates wa Marekani, ambaye utajiri wake kabla ya mtikisko wa uchumi,ulikuwa Dola bilioni 53. Biashara zake ni program za kompyuta kama Microsoft. Akina dada wangependa kuvikwa naye pete ya uchumba. Kwa mujibu wa majarida ya Forbes, na Wall Street Journal, Carlos Slim, maarufu sana kama “Super Slim” anachuma utajiri wa Dola za Marekani milioni 30 takriban kila siku. Ana utajiri ambao ni dola milioni 500 zaidi ya Bill Gates. Changudoa gani atamgeuzia mgongo? Thubutu! Warren Buffet wa Marekani ana utajiri wa Dola bilioni 47; anawekeza katika biashara za Berkshire Hatthway. India pia kuna matajiri kama Mukesh Ambani(hana uhusiano na Ambani aliyekuwa Yanga),anayefanya biashara za mafuta na gesi. Ambani wa India ana utajiri usiopungua dola za Marekani bilioni 29. Kisura gani wa Dar es salaam atamkataa? Wee acha tu. Lakshmi Mittal, Muhindi, anauza bidhaa za chuma ama mavyuma huko India na kwingineko.Utajiri wake ni dola bilioni 28.7. Hata wake za watu hapa wako radhi kuwakimbia watoto na waume zao ili wakaolewe naye. Lawrence Ellison wa Marekani, anauza teknolojia za kompyuta na ametajirika kwa dola bilioni28. Nakamilisha idadi ya matajiri 10 zaidi duniani(Top 10 Richest men in The World) kwa kuandika majina na utajiri wao kwenye mabano. Bernard Amault wa Ufaransa(dola bilioni 27.5), Eike Batista wa Brazil(dola bilioni 27), Amarcio Ortega wa Hispania(Dola bilioni 27)na Karl Albrecht wa Ujerumani(dola bilioni 23.5) kutokana na supermarkets. Nachelea kusema anuani zao na nambari zao za simu hapa gazetini,kwa sababu machangudoa watawasumbua sana kuwa ‘beep-beep’. Penzi la tashtiti? Mapenzi ya kweli hayana thamani, hayajali tajiri na fukara, hayalinganishwi na thamani za almasi na dhahabu na lulu. Kwa mujibu wa magazeti ya The Guardian, The Independent, Observer na Daily Telegraph, hawa matajiri hawana shida na vimwana wa Dar es salaam, Mwanza, Arusha n.k Wasinisumbue kwa meseji uchwara. Mapenzi ya kweli hayana thamani katika sarafu bali damu. Nataka kuuliza kwamba, kwa nini wanawake wa siku hizi wanataka kufikia pesa pindi wakifunga pingu za maisha? Kwa nini wanataka kuolewa na ‘tycoons’ wenye kumudu anasa potelea mbali wawe na vimada lukuki? Mapenzi hayanunuliwi na matajiri kama hawa katika vibanda vya masangoma. Mapenzi hayaletwi na hirizi ama talasimu na waonaji wa nyota. Mapenzi hayana anwani. Kuna aina nne za upendo duniani. Philia, Eros,Storge na Agape. Utajifunza hapa kwamba mapenzi ama upendo wa dhati haununuliwi kwa pesa za matajiri hata hao wote wakubwa duniani. Storge, ni ile hali ya vitoto vidogo kuwahitaji wazazi wao. Eros ni hashiki, tamaa za mwili na mahaba ya ghiliba,ama tamaa za kingono-ngono tu.Philia ni upendo wa kidugu (Brotherly love). Eros au tuite Erao na Storge ni upendo wenye makusudi ya kutimiza matakwa ya kibinafsi zaidi,ni tamaa za kimwili, wakati Philia ni upendo uletwao na kuhudumiwa wakati wa shida;ni kupenda pesa tu, ni mapenzi ya pesa. Philia hutokana na kufikiri ama kuwaza pamoja na kuwaza pesa tu. Agape ni neon la Kigiriki maana yake upendo usioegemea pesa,faida,tamaa,huduma n.k. Upendo wa Agape hauna chumo la faida. Huaegemei mahali penye urafiki ama udugu. Kwa Kiingereza, “Impartiality Love” ni upendo kama alionao Mungu au Yesu kwa kuwafia watu wote pamoja na majambazi, mafukara, magaidi na mafataki. Mapenzi huru huria hujitenga na chumo la faida. Miaka 2,400 iliyopita, mwandishi wa Kigiriki, Euripides, akaandika habari za kimwana mrembo sana aitwaye Alcestis, kwamba mfalme wa Thessaly aliyeitwa Admetus aliugua akataka kufa,lakini yeye akajitoa mhanga kufa badala yake. Miungu ya Ugiriki ilifuatwa kuulizwa sababu za ugonjwa wa Mfalme Admetus;ikasema asingeokoka,isipokuwa kama atapatikana mtu mwingine ambaye angekufa badala yake. Wakaulizwa wazazi wake kama wangekubali kufa badala ya mwana wao mfalme, wakakataa. Wakafuatwa ndugu na jamaa kama wangekuwa radhi kufa ili huyu Admetus abaki akitawala, kwa sababu alikuwa kijana mzuri, wakagoma. Wakaulizwa marafiki ili mmoja wao akubali kujitoa mhanga kufa mahali pake ili abaki akiwatumikia wananchi, wakakataa. Mwishowe, Alcestis, mwanamke mrembo sana, aliyekuwa mpenzi wa Admetus akakubali kufa badala ya Admetus. Baada ya Alcestis kufa, mfalme akaomboleza sana kwa miaka mingi,kwa sababu Alcestis alimpenda siyo kwa maneno matupu na kupenda raha, bali upendo wadhati, wa kuwa tayari kufa. Kisa hiki cha Admetus na Alcestis hutufundisha mapenzi ya kujitoa mhanga. Hata hivyo, huu upendo siyo Agape. Agape siyo kufa kwa ajili ya mtu mwema umpendaye. Yesu alitufia tulipokuwa tungali adui zake,na ndiyo Agape(soma Warumi 5:6-10) Yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema kama Admetus,lakini Kristo Yesu alitufia tulipokuwa tungali maaduzi zake, anatufundisha kuwapenda sana maadui zetu na wale ambao hawana faida kwetu kama hao matajiri. Tazama Mathayo 5:43-48. Sihubiri dini, bali nasema mapenzi ya kweli hayatazami faida na huduma, hayatazami fedha na utajiri wa mtu, hayaangalii urembo. Mapenzi hayana rangi,hayajali faida. Mapenzi hayaangalii zawadi na ng’ombe na farasi zizini. Mapenzi ya dhati huuzwa duka gani wewe tapeli? Mapenzi ya dhati huletwa na Mungu, kama hewa. Thamani yake halisi hakuna awezaye kuilipa. 0786-324 074 0754-324 074 |
Wednesday, June 15, 2011
I don't love u but your money first!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment