NIMESIKIA,kwamba Rais wa Marekani, Barack Hussein Obama, anaweza kufika Dar es salaam kabla ya mwaka huu kwisha.
Hii itakuwa ziara ya kulipiza,kufuatia ziara aliyofanya Rais Jakaya Kikwete huko Washington,miaka michache iliyopita.
Kwa sababu hiyo, nasmwambia Rais Obama akifika Dar es salaam, awe na majawabu yamaswali tuliyonayo sisi Waafrika wenzake,maana tunamwona yeye hana hata chembe ya huruma kwetu.
Kuna dalili kwamba, Afrika inaanza kupingana na Jumuiya za Wazungu, ama zile za kimataifa, ambazo kimsingi Bara letu huburuzwa na matakwa ya Wazungu. Umoja wa Afrika unakaribia kung’amua kwamba mataifa makubwa ya Wazungu, huyaburuza sana mataifa ya Afrika, hadi kuwachagulia nini cha kufanya. Umoja wa Afrika, uliowahi kuongozwa na Kanali Muammar al-Gaddafi wa Libya, anayepigwa na mabomu ya Umoja wa Kujihami wa Ulaya Magharibi(NATO), umeanza kupingana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita(ICC) iliyoko Hague, Uholanzi, juu ya suala la kumkamata Kiongozi wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir. Al Bashir, siku hizi ana urafiki na Uchina,maana Wamarekani wao ni vinyonga. Nilipokuwa nikisoma gazeti la The East African, Julai 20-26, mwaka 2009 nilikutana na katuni iliyosema, Umoja wa Afrika(AU) unataka sana kutuma ushahidi wa kumsaidia kiongozi wa zamani wa Liberia, Charles Taylor. Charles Taylor, yuko The Hague, akikabiliwa na kesi ya kuasaidia waasi wa Sierra Leone(RUF) kufanya unyama mkubwa, kuua watu wakiwemo watoto na pia kupora almasi za nchi hiyo. Taylor, anadaiwa kusaidiana sana na waasi hao wa United Revolutionary Front, walioongozwa na marehemu Foday(Poppay) Sankoh, kupora almasi za Sierra Leone, kufyeka watu mikono na miguu kwa mashoka na kisha kuwachukua watoto mateka na kuwatumikisha katika shughuli za kivita. Taylor, aliwahi kuwalaumu sana Marekani kuchochea kesi hiyo, akisema kana kwamba, kumbe alipomtumia sana, akatimiza matakwa yao, sasa wanamtupa kama ganda la muwa la juzi, na wanamshitaki The Hague, ili kujiosha katika macho ya Ulimwengu. Taylor, na Wazungu wakiwemo Wamarekani, walipigana vita Sierra Leone, wakaiba almasi huko na kuiuza Ulaya,kupitia Zimbabwe, Afrika Kusini n.k ili kukwepa sheria walizoweka, za kutonunua madini kutoka nchi za vita. Naam, filamu iitwayo, BLOOD DIAMOND inawaonyesha Wazungu wa Magharibi, wakiwemo Wamarekani, wakichochea vita mjini Freetown, miaka hiyo ya mwishoni mwa 90 na mwanzoni mwa 2000. Ni wazi, hao RUF walibadilishana almasi kwa bunduki na Wazungu wengine kutoka Afrika Kusini, Zimbabwe na Ulaya Magharibi. Sasa, katuni ya GADO katika The East African, ilileta kichekesho kwamba AU chini ya Kanali Muammar al-Gaddafi, ikiisha mtetea sana al-Bashir wa Sudan asikamatwe, na Robert Gabriel “R.G” Mugabe wa Zimbabwe asiondolewe madarakani kwa shinikizo la Wazungu, sasa ilikua na mkakati wa kutuma ushahidi mzito wa kumtetea Charles Taylor, asipatikane na hatia huko The Hague. Kuna maswali kutoka huku kwetu kmba, mbona mahakama hiyo(ICC) inawatia mbaroni Waafrika tu. Akina Louis-Moreno Ocampo, hawaoni makosa ya akina George W. Bush kuivamia Irak kinyume cha matakwa ya Umoja wa Mataifa? Je, ICC inawaona akina Kanali Muammar Qaddafi tu, na wale sita wa Ocampo, "The Ocampo Six" waliosababisha vifo vya watu 1,400 na wengine 600,000 kukosa makazi,baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya,mwaka 2007? Tena, wapo baadhi ya viongozi hapa Afrika, kutokana na uswahiba na Marekani, hawajakamatwa kuhusika na uhalifu wa kivita katika nchi zao, au nchi jirani. Kwa nini? Nani anachochea vita Congo(DRC)? Nani anaiba madini ya Congo kwa kubadilishana madini kwa silaha na waasi? Kwa sababu AU inaanza kung’amua njama za Wazungu kuwatumia viongozi wa Bara hili kutumia vita na machafuko ili kupora rasilimali, basi katika katuni hiyo, Muammar al-Gaddafi anawaongoza viongozi wa AU kupiga simu(bila shaka mjini Hague) kusema kwamba, AU ilikuwa na nia ya kutuma ushahidi mpya kabisa wa utetezi kwa Bwana Charles Taylor! Nataka kusema kwamba, Rais Barack Obama wa Marekani, akiwa mjini Accra, Ghana Julai 11 alisema Afrika inakuwa duni sana kwa sababu ya rushwa, ufisadi, ukosefu wa demokrasia na utawala bora. Nampinga sana Obama kuwalaumu sana mafisadi na viongozi wa Afrika, kuhujumu maendeleo ya watu wao, kana kwamba akina marehemu Jean-Bedel Bokassa, Joseph Mobutu, Sani Abacha na wenzao, hawakusaidiwa sana na Mataifa makubwa ikiwemo Marekani. Mobutu, aliiba dola za Marekani milioni sita, akazificha Uswisi. Fedha hizo zilikuwa nyingi sawa sawa na deni la nje la Zaire wakati huo, Marekani ilikuwepo, lakini haikusema kwamba zirejeshwe ili kusaidia maendeleo ya watu. Juzi, iliamuriwa Dola milioni sita za Marekani, ipewe familia ya marehemu Mobutu, kwa sababu serikali ya Joseph Kabila imegwaya kuzidai. Sasa, kama akina Abacha, akina Charles Taylor, Mobutu, Bokassa na madikteta wenzao waliitumikia Marekani, kwa mshahara wa mauti kwa watu wao, akina Gaddafi, Taylor, Fodday Sankoh n.k wanakuaje wakosaji pekee katika kesi ambayo watuhumiwa ni wengi? Marekani na Uingereza, wanawatengeneza magaidi kama Osama bin Laden,kisha huwalaumu. Uingereza, ndiko tulikoibiwa dola milioni 40 za rada kanyabwoya, sasa mahakama ya bishara mjini London ikaamuru turejeshewe pesa za ziada, sasa Uingereza haitaki! Inataka kutufanyia 'janja ya nyani'. Obama, anapowalaumu viongozi wa Afrika kwa rushwa, utawala wa ovyo, ufisadi na ukosefu a demokrasia na maendeleo, anajifanya kiziwi na kipoofu kutoona na kusikia madhara ya ukoloni, na haja ya mataifa haya kushitakia na kutulipa fidia ya madhara ya ukoloni mkongwe na mamboleo. Rais Barack Obama, mkewe Michelle ni mzaliwa wa mabaki ya watumwa Waafrika waliopelekwa huko kulima mashamba ya miwa. Baba yake, Hussein Obama, alikwenda Marekani kutafuta elimu, kabla ya kukutana na mama wa Kimarekani aliyemzaa Obama. Babu yake, Mzee Obama, huko Kenya aliwahi kuwa ‘Boy’ wa Wazungu. Na alikuwa mwanajeshi wa Jeshi la Kikoloni,la kumlinda Malkia, 'King's African Rifles' ama KAR. Na hao mabinti wawili WA Rais Obama, Sasha na Malia, kisha wakweze, Fraser na Marian Robinson, lazima wanaakisi madhara ya utumwa wa Mtu Mweusi kwa hawa WAZUNGU, ambao hata sasa wana vibaraka Afrika, wanawapa silaha ili kupora maliasili na kugawana nao. Makampuni ya mafuta na madini, ndiyo huchangia rushwa na ufisadi kwa mikataba mibovu; na huwapa nguvu kubwa watawala wetu hata kuwarejesha mamlakani, kwa kutumia chaguzi zisizo huru na haki. Ken Saro-Wiwa, hakuuawa na Abacha pekee. Makampuni ya mafuta ya Wazungu kama Royal Dutch/Shell na mengine, yalikuwa yakimletea sialaha Abacha, ili akabiliane na wanaharakati. Vita vya rasilimali katika Niger Delta, ni ushahidi kwamba makampuni ya Magharibi hulalamikiwa kuondoa maendeleo na utawala wa haki wenye manufaa kwa Mtu Mweusi. Obama, alipohutubia bunge mjini Accra, wakati wa Ziara ya kwanza Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, hakusema kitu kwa makampuni ya mafuta na madini, kukwepa kodi na kulipa mrabaha kidogo serikalini, kitu ambacho ni kuwanyima maendeleo Waafrika. Watawala wetu hawawajali wananchi, kwa sababu ni vibaraka wa Marekani, Uingereza, Canada n.k yaani wako radhi wanachi wafe kwa njaa ili madini na mafuta yaende. Sasa, lawama za Obama kwa viongozi wetu kwamba wanakatalia madarakani kwa muda mrefu na kuwanyima atu wao maendeleo mbona ni za upande mmoja? Tujiulize: Marekani wana makampuni yao ya mafuta Niger Delta, Chevron, Conocco Phillips n.k yanalipa kiasi gani serikalini,Nigeria? Mbona bado Waogoni na Waijaw wa huko Niger Delta, wanalalamika? Au, hapa kwetu kampuni za uchimbaji madini na za utalii, haziogelei katika misamaha ya kodi na kuwahonga vigogo wetu, mafisadi? Mbona mikataba imesainiwa Paris? Mbona Obama hakutangaza mkakati wa serikali yake kuwabana mafisadi wa rada wa Uingereza, walioshirikiana na wa hapa kwetu? Mbona Obama, hajasema majambazi walioko Marekani na Ulaya, wanaowapa rushwa mafisadi wetu ili wapore huku na kuficha kwao dola zetu mabilioni, wakati tunapokufa njaa, na umasikini na kukosa elimu? Ni kwa sababu hii, tunadhani Afrika ina haja ya kutazama mipango yetu kwa maslahi yetu, siyo kuburuzwa na akina Obama, ambao kimsingi ni Weusi lakini siyo Waafrika wenzetu. Akina Obama wanayo maslahi yao Marekani, na kamwe siyo tena Kogelo, Kisumu, Kenya au popote Afrika. Hawa, wanatekeleza sera za Marekani tu, na lawama na misaada yao kwetu ni ile ya kutudidimiza kwa riba nzito na wizi wa rasilimali unaofanywa na makampuni yao ya madini na uchimbaji mafuta, utalii n.k Kama Obama angekuwa mwenzetu, angetangaza huko Accra kwamba, Afrika iwe na nafasi sawa na mabara mengine, kwa sababu rasilimali zake ni nyingi na muhimu kabisa. Na kama Obama ni mwenzetu, ni mwathirika ya madhara ya utumwa na ukoloni mkongwe, lazima akifika Dar es salaam, atueleze, ana mpango gani wa kuondoa utapeli wa madola makubwa kwetu? Na kwamba, kwanini bara hili tajiri la rasilimali, liwe duni kimaendeleo, kama siyo wizi, utapeli na ufisadi wa Mataifa yao dhidi yetu? Na viongozi wetu kwa nini wawe vikaragosi wa Marekani,Uingereza,Ufaransa na washirika wao, halafu wakiwepo akina Gaddafi,wakiwapinga wanapigwa mabomu na kupinduliwa? Hivi shina la ufisadi, mfano wa rada ya BAE Systems, au ukwepaji kodi wa makampuni ya madini, ni mafisadi wetu, au wao wenyewe? Fisadi anawezaje kuiba na kuficha fedha katika mabenki yao kwa miaka 40 kisha ndipo waseme, ‘ziko huku’ baada ya kufa? Hivi, mahakama kama Hague, haina meno kuwafunga jela wale waliowauzia bunduki Taylor na Foday Sankoh? Je, nani waliwauzia silaha Revolutionary United Front, kama si Mzungu? Obama ana habari hata sangara wa Mwanza wanaleta faida maradufu kwa matapeli, wakati sisi ‘tumefulia’ ingawa tunavua na kukokora katika tufani na pepo kali kila siku? Nataka kusema kwamba, Obama anajua mizania halisi ya ufisadi, rushwa, utawala a ovyo na ukosefu wa demokrasia. Anajua nani mizizi, nani shina na sisi ni matawi. Kesi yangu dhidi yake ni kwamba hata yeye mmoja wa waathirika wa wizi, dhuluma na ukoloni mkongwe na mamboleo, mbona anawalaumu vikaragosi, huku akichelea kuwataja anaofanya Afrika iwe zii? Obama, ana kesi ya kujibu, asijitie kua mwendesha mashita dhidi ya mafisadi wetu, alioingia madarakani kwa utajiri haramu uliotokana na mgawo wa rasilimali zetu kati ya wawekezaji mafisadi wazungu na viongozi, kwa kutumia mikataba feki na hewa. Obama, ukija Dar wewe na mkeo Michelle, na mabinti zenu wawili, Malia na Sasha, usikose kuja na majawabu sahihi ya maswali niliyokuuliza hapo juu! Usijitie Mzungu, ukasahau kwamba Baba yako, Hussein Obama alikwenda Marekani kusoma, akakutana na mama yako, wakaoana, ukazaliwa wewe! Babu yako, Mzee Obama aliwahi kuwa 'Boy' wa Mzungu, na akatumikia jeshila Malkia, King's African Rifles(KAR) sasa wewe utasahauje uhalifu wa ukoloni? Hata huko Marekani kwenyewe, wamekubagua kwamba wewe Mkenya! Ukifika Dar es salaam, wewe,mkeo Michelle, ambaye pia ni Mwafrika wa Kimarekani na binti zako Malia na Sasha, usikose kuzungumza namna ya Mwafrika kuondokana na huu utapeli wa Kizungu,Ukoloni M kongwe na Mamboleo. Usijitie Bush,kupeleka vita Libya, wakati wabunge wa Congress wa Chama chako cha Democrat na wale wa Republican wanapinga sana, unyama wako wa kupeleka maangamizi ya raia Tripoli. Tafadhali Obama, ukifika Dar, tuzungumze mambo haya kwa kina. 0786-324 074 |
No comments:
Post a Comment