JUMAPILI moja niliketi varandani mwa nyumba moja jirani na njia panda.
Nikaanza kupeleleza maisha ya wapita njia, ambao hata katika Daladala walikuwa hawaachi kumshutumu aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Zakia Hamdan Meghji, kwa bajeti yake.
Mkononi, nilikuwa na kitabu cha riwaya iliyotungwa zaidi ya miaka 50 iliyopita na mwandishi mahiri sana hapa Afrika.
Nilikuwa nikiisoma mara kwa mara riwaya ile.
Na nilikumbuka kukirejea kitabu kile, kwa kuwa niliamua kuitumia siku hii kupumzika.
Kila aliyekuwa akipita kutoka kona moja au nyingine, nilimwangalia. Wanaume, wanawake na watoto niliwaangalia.
Nilipokosa mahluki wa kuangalia, nikaendelea na ‘hamsini’ zangu; yaani kusoma riwaya yangu, iliyokuwa mkono wa shoto.
Kila kiumbe kilichopita hapo barabarani, mita chache tu kutoka upenuni mwa nyumba, ngazini mwa milango ya maduka nilipokuwa nimejiputika, nilikiangalia. Nilijikuta nikitoa hukumu yangu moyoni, kulingana na kile ambacho kwa takriban wiki mbili- tatu sasa, jamii ilikuwa ikimlaumu Waziri Meghji kwa bajeti kandamizi.
Hata sasa tunamlaumu Waziri Mustafa Mkullo kwa bajeti ya 2011/2012 ambayo twasema, kandamizi!
Mienendo ya wapiti njia niliyoiona hapo barabarani, ilitosha kuwa ushahidi wa kuwatoa au kuwatia hatiani, kwa kelele zile zile za Bajeti kandamizi inayofanya maisha kuwa magumu hata siku hizi.
Naam, Jumapili hiyo siku ya mapumziko, niliwaona vijana wengi wakiwa na rafiki zao wa kike, wakitembea kwa madaha.
Bila shaka, walikuwa wakienda katika starehe ama tuseme anasa, katika majumba ya starehe, au katika mahoteli ya fahari, ambako huwezi kukanyaga kama huna fedha.
Wasichana wengi niliowaona walikuwa wamenenepa; walikuwa waking’aa mithili ya mbalamwezi.
Wavulana walioandamana nao, wengi walikuwa wamepauka; nikajua bila shaka kutokana na kazi za harubu za wiki nzima juani.
Wengine wakata nyasi, wengine machinga, wasukuma mkokoteni, wengine wajasiliamali!
Unajua, mwanaume sharti kusaka noti juani, ili mkono uende kinywani.
Akina dada wale, wengi walivalia suruali ‘Jeans’ za kubana sana .
Wengine walivalia vivazi vyao vya siku hizi, vinavyoacha sehemu kubwa ya mwili wao kuwa nje; vilikuwa vya rangi anuwai, huku vikiandamana na vijishati- utadhani vya wadogo zao-kumbe vilikuwa vyao wenyewe.
Walipokuwa wakitembea, naam kupita njia ile nilipokuwa, walikuwa wakinesa mithili ya twiga wenye himila changa; huku minofu ya kiwiliwili, pengine sehemu za nyuma za makalio, zikitetema utadhani hatimaye zingedondoka!
Kitu cha ajabu nilichobaini katika upelelezi wangu, ni kwamba akina kaka wengi(kasoro wachache) walioandamana na akina dada wale Jumapili hiyo, mbali na kusinyaa kwa jua la hari, walivalia vibaya, masurupwenye makubwa yenye kuwapwaya.
Naam; kwa kifupi, ni kisa cha wavulana vibubutu ama malofa, waliojitia kutoa ‘ofa’ kwa mabinti warembo waliotingisha minofu makalioni, kwa mwendo wa madaha mithili ya twiga mwenye himila changa.
Nikatoa hukumu yangu kwamba, hawa walikuwa wavulana “Genetic Modified” kwa kifupi, GMO waliokuwa wameumbwa kuwastarehesha wengine, huku wao wakiungua mithili ya mshumaa!
Mshumaa una upendo wa kijinga (nitaeleza baadaye aina tatu za upendo) wa kuwaangaza wengine, wakati ukiteketea.
.Nikajiuliza: Kwanini wao wakonde na kuonekana mifupa mitupu kwenye masurupwenye,wakati wasichana wao wamenona kwa pesa zao walizotafuta mchana wa hari?
Wasichana wale walikuwa na simu za mkononi za gharama kubwa, huku wakinukia uturi wa thamani.
Kwa vyovyote, wavulana wao walinuka jasho kufuatia kazi za harubu za kuchumia juani!
Wengine hawakuwa na simu.Wamehonga fedha yoote!Watakuwaje na simu zao wenyewe? Ubwege tu!!
Nika waona pia, akina baba-watu wazima-bila shaka wenye familia zao na watoto wao, wakitoka mmoja baada ya mwingine katika makazi yao .
Jioni hakuna aliyeandamana na mke au watoto. Walikuwa peke yao , wakibofya-bofya simu zao za mikononi.
“Haloo? Sasa tuonane pale…tulipozungumza jana n’takusubiri…Ok? Tchao!!
”Nikajua walizungumza juu ya miadi yao , bila shaka na hawara zao wa nje. Mimi mwenyewe, siku moja tu kabla ya Jumapili hiyo, mama mmoja mtu wa makamo, aliniambia nimpigie simu, ili tukutane Hoteli yoyote ya fahari, ili tuzungumze!
Uso ukanisawajika.
Nikaghairi; na badala yake nikaja hapo ngazini, njia panda kufanya udakuzi huu. Nilijua akina dada na akina mama wa siku hizi makali ya Bajeti(ingawa imetolewa na mwanamke mwenzao) wao hawayajui
Nikaogopa kujitoa mhanga mithili ya mshumaa, badala yake nikaja kusoma kitabu changu hapa njia panda, na kuwapeleleza Watanzania hawa na ahadi yao ya Maisha bora!
Abadan sikuogopa kuitwa mtu mgumu, bahiri, mkono wa birika na akina dada hawa wenye hadaa mithili ya dagaa.
Simu bado zinazuzua watu. Badala ya kufanya shughuli za maendeleo, ni anasa.
Hawa, nikawaona wanaingiza vocha za maelfu na kuendelea kubofya-bofya, huku wakisema, “Wala haina shida, hata mkija watatu; wanne mtakunywa, mtakula, mtastarehe vya kutosha; wala hakuna wasiwasi!”
Nikajiuliza: Na familia tunazifanyia haya?
Hawaa akinaa "Mr. Bingo uchwara" akina Bill Gates wa kuchonga, wana ubavu?
Au, ni unafiki huu wa kujiteketeza mithili ya mishumaa?
Nikakumbuka maneno katika Biblia, kwamba, ‘ Kama kondoo waongozavyo machinjoni…”
Nikakumbuka miongo mitatu iliyopita, nilipokuwa nikichunga mifugo ya Babu yangu, wakati mwingine nililazimika kuwapeleka ng’ombe na mbuzi malishoni bila kutia chochote kinywani.
Matokeo yake, ng’ombe wakanenepa, mimi nikakonda!
Ilikuwa kabla ya kubaini kuwa ulikuwa utumwa…naam utumwa wa hiari.
Yaani, mtu huacha kununua chakula na mahitaji mengine ya lazima ili ajaze fedha kwenye simu, akawakoge wenzie baa!
Simu zimeingia nchini siku si nyingi.
Wengine ‘ndundundu’ ujira wa mtwangaji, ndio kwanza wamezinunua juzi, vidole vinawawasha kubofyabofya.
Mwaka 2005 Benki ya Dunia(WB) ilisema kulikuwa na simu nne tu kwa kila Watanzania 1,000.WB ikaongeza kwamba Watanzania watano tu kati ya 1,000 ndio waliomudu kununua magazeti yote ya kila siku ili kujisomea.
Watu 293 tu kati ya 1,000 ndio waliokuwa na redio, ambazo wengi waliishia kusikiliza ‘bongo flavour’ tu bila kusikiliza habari.
Wenye televisheni walikuwa 23 tu kati ya 1,000; nao waliishia kutazama ‘jumba la dhahabu’ kwa jirani, huku pesa zao wakiteketeza kunenepesha wengine mitaani
Waliokuwa na kompyuta zao walikuwa hawafiki wanne kwa kila Watanzania 1,000. Kati ya watu 10,000 waliokuwa na kopyuta zao zenye intanet walikuwa 0.3; wengine hawa hata leo hawajui internet ni mdudu gani?
Kati ya Watanzania milioni 35 wanaotumia internet ni 25,000 wengi wao vijana wanaotafuta kutazama ngono na mapaja ya machangudoa wa ughaibuni.
Swala la elimu na mawasiliano Tanzania, linawekwa kando; starehe na anasa hupewa kipaumbele.
Baadhi ya wanawake wa kileo akili zao ni ‘Genetic Modified’ (GMO) kwa ajili ya ofa za maraha,anasa na starehe,wanawalazimisha akina baba wa watu(wenye familia zao) kuwapa ‘offer’ katika mahoteli ya gharama, wakati uwezo na mishahara yao ni kibubutu, mkia wa pimbi!
Maskini hawa, wanajiingiza kichwangomba(kichwa chini miguu juu), matokeo ni kashfa za kuacha simu baa na kuchojolewa viatu au mashati!
Huku mitaani hawaachi kumlaumu Mama Meghji, kuwa bajeti yake ilikuwa ya kikatili! Je, walitaka bajeti hiyo iwe ‘rafiki’ hata kwa machakaramu wa vimwana katika kashfa zao za akina Monicagate?!
Bajeti ngumu maana yake ni kujifunza kujitegemea na kutumia fedha kwa mambo ya maana, si starehe na anasa! Hapo mpo? Wewe mbango; pesa huna, mambo makubwa ya nini?
Angalia utajipeleka ‘machinjoni’mithili ya kondoo wa sadaka! Karo ya shule hujalipa, kodi ya nyumba hujalipa, maziwa ya mtoto,
Ankara za maji, umeme, fedha za tuisheni n.k huwezi kulipa, badala yake unashughulikia ofa za akina mama shamla, mama uhondo, mama tabaradi, mama tambarare, huku huna kitu; maisha kichwangomba; halafu unahoji bajeti ya Zakia Meghji!
Unahoji ahadi ya rais ya maisha bora kwa kila Mtanzania kwa stahili hii?
Starehe kwako surupwenye; wavaao wana mwili, wewe ufyefye(dhaifu) mbavu tupu, utapwaya
!Usijifanye 'tupatupa', ukatapanya ulichovuna udobini kwa uroho na ujapongo kwa akina mama shamla(hawakauki ngomani, utaumia!
Maisha bora hayaji kwa kuvaa masurupwenye ya akina mama tamaa, mama anasa!
Mshumaa hujiteteteza wenyewe kuwaangaza waungwana; wewe mshumaa? Mshumaa uliowashwa msituni(Candle in The Jungle) unawaka, kisha utazima kwa upepo wa kisulisuli, pasipokumwangaza mtu.
Usijitie kuwasha mshumaa msituni; usijipendekeze.
Mshumaa usijitie ukwasi. Usijidai kuwa na upendo wa Agape.
Kuna aina tatu za upendo:
Eros ama Erao ni tamaa. Akina dada viduhushi, watajidai kukupenda ukiwa na chochote kitu; kikiisha hakuna tena mapenzi.
Akina dada nao watapendwa kwa sababu ya makalio makubwa, hips, dodo mithili ya miba ya katani, vitovu mbonyeo n.k lakini vikitoweka, hakuna mapenzi- haya aslani si mahaba ni ashiki, tutumko, tamaa na hadaa tu.
Kuna Philia. Baba atampenda mama kwa sababu anamhitaji kutunza familia. Na mama kadhalika anamhitaji baba kwa sababu zilezile za kibinadamu. Upendo huu pia hufika muda ukatoweka.
Upo upendo wa mshumaa ‘agape’ ni upendo wa kujitoa mhanga.Wanaouweza ni ‘watumwa’ wa hiari.
Miaka 2400 iliyopita Mgiriki mmoja aitwaye Euripides, aliandika kwamba, Admetus Mfalme wa Thessaly aliugua sana akakaribia kufa.
Miungu ilipoulizwa sababu ya maradhi ya Mfalme, ikasema, asipokufa mtu mwingine badala yake, Mfalme asingepona!
Basi,baba yake akaulizwa kama angeweza kufa badala ya mwanae, akakataa. Mamaye akasema, ‘kweli Admetus ni Mfalme tena ni mzuri, lakini kamwe asingeweza kumfia. Wakaulizwa rafiki zake wote, hakuna aliyekubali kufa kwa ajili ya Admetus.
Mwishoni, kidosho mmoja mpenzi wake aliyeitwa, Alcestis akasema, yeye alikuwa tayari kufa kwa ajili ya Admetus!
Alipokufa, Mfalme akapona maradhi yake, lakini hakurudi kuwathamini wazazi, rafiki wala ndugu kwa kuwa walikuwa na upendo wa maneno bila vitendo, isipokuwa marehemu mpenzi wake, Alcestis.
Tena Biblia inaupinga upendo huu wa kidosho huyo Alcestis, kwa kusema ‘Yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki. Bali Kristo Yesu alitufia tulipokuwa tungali wenye dhambi.
Yesu aliwafia majambazi na magaidi; ndiyo agape!
Je,Vibubutu wenye ujira ndundundu, wanapojitia kuwastarehesha akina mama shangwe huku nyumbani kwao watoto wakikosa lepe kwa kung’atwa mbu, ndiyo agape yenyewe, au kichwangomba waliogeuzwa vichwa chini-miguu juu kwa huba la tashtiti; huba la kitapeli lililojaa ujapongo; yaani uroho na kigeugeu?!
Naam, kama huu ndio upendo, basi ni utumwa kuliko wa mshumaa. Mbona hata Yesu aliwaasa wanafunzi wake kuanzia wokovu nyumbani kwao (Yerusalem)? Kwanini muwe mifupa mitupu kuwanenepesha wengine, wakati kwenu midabwada?
Kumbe watumwa wangalipo?
0754 324 074
0786 324 074
congesdaima@yahoo.com
No comments:
Post a Comment