Thursday, April 25, 2013

USHIRIKI WA WANAUME KATIKA AFYA YA UZAZI




Na Clara Matimo, Mwanza
KAMPENI ya kupunguza Maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto, “Prevention of Mother to Child Transmission”(PMTCT), na Ushiriki wa Wanaume katika Uzazi wa Mpango,unakwamishwa  na  tabia ya mfumo dume ulioota mizizi Kanda ya Ziwa, imefahamika.
Mratibu Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mtoto Jijini Mwanza, Sarah Mahumbuga, amesema kwa miaka miwili ya 2011 na 2012, akina baba wachache walifika Kliniki na katika vituo vya Afya,ili kupima afya zao na kushiriki Uzazi wa Mpango.
Amesema,Shirika la Engender Health kupitia Mradi wa CHAMPION(Men Involvement), linalotoa huduma katika baadhi ya mikoa hapa nchini, Mkoa wa Mwanza ukiwemo,  wilaya za Ilemela na Nyamagana zinahusishwa na mradi huo.
Hospitali ya Nyamagana na Kliniki ya Makongoro  huhusishwa na mradi huo kwa nia ya kuwahamasisha  akina baba kushiriki Afya ya Uzazi na Maambukizi ya Ukimwi.
Sarah Mahumbuga amesema, katika kipindi cha mwaka 2011,wanaume walioshiriki kupima afya zao na Uzazi wa Mpango ni 3,370 sawa na asilimia 18  tu ya lengo lililokusudiwa, katika Jiji la Mwanza.

Mhudumu wa Afya wa Kliniki ya Makongoro akimhudumia mama mjamzito Aprili 25,mwaka huu
Mahumbuga afafanua kwamba, mwaka 2012  akina baba walioshiriki katika zoezi hilo muhimu ni 8,541 sawa na asilimia 43.
“Mwaka 2010 wanawake waliohudhuria Kliniki kwa mara ya kwanza walikuwa 18,952. Idadi ya waliopima virusi vya Ukimwi ni 12,057 sawa na silimia 63 ya akina mama wote waliohudhuria Kliniki kwa mara ya kwanza, na kati ya hao wanawake 756 sawa na asilimia 6.2 walikutwa na maambukizi ya Ukimwi”,Mahumbuga amesema.
Akilinganisha na akina baba waliopima virusi vya Ukimwi mwaka huo 2010 amesema walijitokeza akina baba 328 tu ambao ni sawa na asilimia 6.
Akaongeza kuwa mwaka 2011 wanawake waliofika kliniki kwa mara ya kwanza walikuwa 18,726; na kati yao waliopima Virusi vya Ukimwi ni 7,947 sawa na asilimia 42. Kati yao waliokutwa wakiwa na maambukizi ya virusi hivyo vya Ukimwi ni 506 idadi ambayo ni sawa na asilimia 6.3.
Mratibu huyo Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mtoto Jijini Mwanza, anasema katika mwaka huo 2011 wanaume waliofika Kliniki na wake zao na wakapima afya ni 374 sawa na asilimi 6.9.
Katika mwaka 2012,Mratibu huyo amebainisha kuwa wanawake waliohudhuria kliniki kwa mara ya mwanzo walikuwa 19,946; na kati yao waliopima afya zao ni 11,299 sawa na asilimia 57.Waliokutwa na maambukizi ya Ukimwi ni 523 sawa na asilimia 4.6.
Mratibu huyo amesema wanaume waliohudhuria kliniki mwaka 2012 walikuwa 596 ambao ni asilimia 2.1 tu
 Baba akiwa    akishiriki zoezi la upimaji katika Kliniki ya Makongoro,Mwanza
“Kama wanawake wanaohudhuria kliniki wangekuwa wanafika na wenzi wao na kupima, akina baba wangetambua umuhimu wa kushiriki zoezi hilo la kuokoa maambukizi kutoka kwa wazazi kwenda kwa mtoto”, amefafanua.
Akizungumzia changamoto zinazokabili Kampeni hiyo ya Afya ya Uzazi na Mtoto,   katika utendaji wa kazi wa kila siku, ameseka kuna uhaba wa vitendanishi( HIV TEST KITS) , akatoa mfano kwamba kwa mwaka huu 2013 Jiji la Mwanza limepata kit 69 tu wakati vipo vituo 24 vinavyotoa huduma hiyo.     Kit moja ina vifaa 100 vya kupima ukimwi.
“Kufuatia hali hiyo, mwaka 2011 wanawake waliofika kliniki mara ya kwanza walikuwa 18,726,lakini waliopima walikuwa 7,947; hali hiyo husababisha waliobaki kukosa huduma kufuatia vifaa hivyo vya kupimia Ukimwi kuwa vichache”, alisisitiza.
Amewataka wanaume kujitokeza kwa wingi bila woga katika zoezi hilo ambalo lazima lihusishe baba,mama na mtoto.
“Wanaume wote wanapaswa kufika kliniki pindi wake zao wanapopata ujauzito; kwa sababu kuna faida nyingi; kujua mama ana tatizo gani wakati wa ujauzito,dalili za hatari; na ikitokea shida baba ajue cha kufanya ili kumsaidia mama mja mzito kujifungua salama”,
Hatari za akina baba kutoshiriki zoezi la upimaji wa afya ya uzazi  humfanya mama mjamzito kuathiriwa kisaikolojia,hususan anapopimwa na kubainika kuwa ameambukizwa.
“Wakipimwa pamoja wakagundua tatizo ina kuwa rahisi wote kwa pamoja kujua namna ya kumkinga mtoto aliyeko tumboni asipate maambukizi; na pia hujua namna ifaayo kutumia dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto”, Mratibu huyo amesisitiza.
 Imeelezwa pia kwamba,wanaume wengi wa Tanzania hawapendi kupima Ukimwi ukilinganisha na wageni wanaofika nchini, ambao Mratibu huyo wa Afya ya Uzazi na Mtoto amesema hawajifichi;lakini wanaume wa hapa nchini hawapendi kujitokeza kuzungumzia hali zao za kiafya kwa wataalam wa afya.
Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dk.Kimaro Daniel amesema kuna wanaume wengi waliojitokeza kupima afya zao Mwanza ukilinganisha na wanaume wa wilaya za Sengerema na Ukerewe.
Akitoa taarifa kwa Naibu  Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Seif Rashid,Siku ya Utepe Mweupe,Machi 15 mwaka huu,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo amesema mkoa huu una jumla ya wakazi 2,571,402 kulingana na SENSA YA WATU NA MAKAZI ya 2012,ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 2.7.
Ndikilo amesema Mkoa wa Mwanza una watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja 106,360 na wenye umri wa chini ya miaka mitano 488,851; wakati akina mama wenye umri wa kuzaa ni 926,179.
Akizungumzia idadi ya hospitali na vituo vya afya vinavyotoa huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto,Dk.Ndikilo amesema kuna vituo 353; na kati ya hivi vipo katika hospitali 14(mbili za rufaa);hospitali za wilaya,za binafsi na za mashirikika ya dini.
Kati ya vituo hivyo 353,vituo 326 sawa na asilimia 92 hutoa huduma ya afya ya mama na mtoto;wakati vituo 239 sawa na asilimia 73.3 hutoa huduma ya kuzuia maambukizi ya Ukimwi toka kwa mama kwenda kwa mtoto.
          Mhudumu wa Afya akiwapa huduma  mama wajawazito
Miongoni mwa akina mama 926,179 wenye umri wa kuzaa, akina mama 121,530 walipata ujauzito na kati yao  82,214 walipata huduma ya uzazi wakati wa kujifungua sawa na asilimia 67.6
Mkuu wa Mkoa amesema kiwango cha maambukizi ya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kimeshuka kutoka asilimia 5.2 mwaka 2011 hadi asilimia 4.2 mwaka jana.
Amesema pia kwamba vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi vimepungua kutoka  217 kati ya 100,000 hadi 95 kati ya 100,000 mwaka jana.
Mkuu wa Mkoa amesema mkoani Mwanza sasa vifo vya watoto walio chini ya mwaka mmoja ni 11 kati ya watoto 1,000 waliozaliwa hai.Kiwango hiki ni cha asilimia 14.
Kulingana na Mratibu wa Taifa wa Afya na Mama na Mtoto katika Wizara ya Afya, Dk. Koheleth Winani,akina mama wa Tanzania wangali wanakabiliwa na hatari ya maradhi yanayoweza kuzuilika.
Kiwango cha akina mama  wajawazito wanaofariki nchini 454 kati ya 100,000.Na watoto wanaokufa ni 26 kwa kila watoto 1000 wakati wanapozaliwa.
Kufuatia halihiyo, Mkurugenzi wa Afya wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani(USAID),Alisa Cameron alisema siku ya uzinduzi wa Kampeni ya Uzazi salama Jijini Mwanza kwamba Kampeni ya ‘Wazazi Nipendeni’ inayotangazwa na vyombo vya habari nchini iwafanye akina baba kuacha mfumo dume na kushiriki ipasavyo katika zoezi la uzazi wa Mpango na kupima virusi vya Ukimwi,ili kuokoa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa  mtoto.
“WAZAZI NIPENDENI” inalenga kuwezesha akina mama wajawazito na wenzi wao kuchukua hatua thabiti za uzazi salama, na kuzua maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto(PMTCT).
Sekamponge  Makuki (24)mkazi wa jijini  Mwanza ambaye  ni mjamzito,anasema yeye anafaraja sana kwa kipindi hiki cha ujauzito kwa kuwa yeye na mumewe walipanga kupata mtoto,na pia wote wanahudhuria klinik jambo linalowafanya kupata elimu ya pamoja kutoka kwa wataalamu wa afya,na pia mumewe anafundishwa jinsi ya kuishi nae kwa kipindi cha ujauzito.
“Tangu tulipofunga ndoa na mume wangu,tumekuwa tukishirikiana nae katika masuala yote ya afya ya uzazi,hivyo na huu ujauzito nilionao tulipanga kwamba tazae,hata kabla ya kupata ujauzito tulipima afya zetu na baada ya ujauzito tulipima pia kwa pamoja,namshukuru MUNGU hatukupatikana na maambukizi ya ukimwi  anasema na kuongeza kuwa 
“lakini kwa kuwa tunashirikiana hata kama majibu yangekuwa mabaya tungeyapokea kwa pamoja,ni vizuri akisikia mwenywe  majibu kutoka kwa mtaalamu wa afya kuliko kumwambia mimi’’”anaeleza Makuki.


     Mhudumu wa Afya aki wahudumia watoto katika Kliniki ya Makongoro

Mwanaume anayeshiriki katiaka suala zima la Uzazi wa Mpango katika kliniki ya makongoro iliyopo jijini Mwanza,Abel Luzibila (30)mkazi wa Bwiru jijini Mwanza anasema amekuwa akienda kliniki na mke wake tangu mwanzo wa ujauzito ili kufahamu maendeleo ya afya ya mke wake, kama wataalamu wa afya watabaini tatizo lolote kutoka kwa mke wake wajue watajipanga vipi kiuchumi katika kulitatua.
Luzibila, amesema kwamba mara ya kwanza alipofika Kliniki na mkewe ambaye ni mjamzito, alisema alivutiwa na somo la namna  inavyopasa kumsaidia mama mjamzito.
“Kwa mfano,leo(Aprili 25 mwaka,2013) tumejifunza somo la unyonyeshaji;tumefundishwa lishe bora wakati mama anaponyonyesha na sitabishia Bajeti inayotukabili kwa sababu tayari nimeshiriki mafunzo hayo na najua umuhimu  na athari za kukosa lishe bora”, Luzibila amesema.
Ofisa Mawasiliano wa Mradi  wa CHAMPION unaoshughulikia Ushiriki chanya wa Wanaume katika Mkakati wa kitaifa wa kupambana na Maambukizi ya  Virusi vya Ukimwi na Ukimwi (Engender Health),Muganyizi Mutta, anasema akina baba wanaposhiriki kikamilifu katika Uzazi wa Mpango watawezeshwa kupanga idadi ya watoto wanaowataka.
Mutta pia amesema baba na mama wakishiriki kwa pamoja katika zoezi hilo watapata njia za uzazi wa Mpango zinazofaa, na kuwa na familia zilizo bora.
“Shirika la Engender Health,kupitia Mradi wa CHAMPION(Men Involvement) limetenga Dola za Kimarekani milioni 16 kwa ajili ya kuhamasisha akina baba kushiriki kikamilifu katika mkakati huu kitaifa wa kupambana na virusi vya Ukimwi kutoka ,mradi ni wa miaka  mitano unaomalizika Septemba mwaka huu”, Mutta amesema




No comments:

Post a Comment