AWAMU ya Pili ya kuratibu na kukusanya maoni ya
wananchi itafanywa kupitia Mabaraza ya Katiba.
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba itaratibu na kukusanya maoni ya wananchi kupitia Mabaraza
ya Katiba katika ngazi anuwai,kabla ya maoni hayo kuwasilishwa Makao Makuu,kwa
ajili ya tathmini na kuandaliwa Ripoti.
Mabaraza ya
Katiba yanatakiwa kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba na kujadili ili kutoa
maoni kwa kupitia mikutano itakayoitishwa na Tume ya Katiba,ili kushirikisha na
kukutanisha wawakilishi toka makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii.
Kufuatia
hali hiyo,uchaguzi wa wawakilishi ama wajumbe wa Mabaraza ya Katiba unafanywa.
Niseme wazi kuwa uchaguzi huo unatia kinyaa.
Napenda
kumhadharisha Mwenyekiti wa Tume hiyo,Jaji Msitaafu,Joseph Sinde Warioba na
wenzake kwamba, wajumbe wa Mabaraza ya Katiba hususan wale wa kata, wengi wao
ni kichekesho cha mwaka!
Wamechaguliwa
kwa kuhonga vijisenti,na wengine walichaguliwa kwa upendeleo wa udini na
ukoo,kiasi kwamba inatia shaka kama hata Katiba wanaijua na umuhimu wake!
Vijijini,rushwa
za kijinga zimetumika ili kuwapata wajumbe wa Mabaraza hayo ya Kata; kwani
mfumo mzima umeendeshwa kimbumbumbu,pasipo hata wasimamizi kujua ni aina gani
ya watu walihitajika kuchaguliwa ili wawawakilishe wenzao katika kupitia Rasimu
ya Katiba na kutoa maoni yao.
Jaji
Warioba, aamini ama asiamini,wajumbe wengi wa Mabaraza hayo ya Kata.hawaelekei
kufahamu chochote juu ya Katiba na umuhimu wake.
Bali,
wamechaguliwa kutokana na ujanja ujanja ili wajipatie posho,ambayo inasemekana
ni kubwa,ili kujiongezea kipato.Kilichowasukuma kuanza kuhonga wajumbe, si
weledi ama ujuzi na nia ya kutoa maoni,bali kusudi ni kujipatia posho
inayotolewa na Tume.
Kama
ingewezekana, wajumbe wote wangepewa mtihani ili kupima uelewa wao japo kidogo
tu kuhusiana na Katiba na Misingi yake kama Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Hatuwahitaji
watu waliouza mbuzi na kuku na kuhonga honga wananchi na wajumbe wa Mabaraza ya
Kata(WDC) mwisho wa siku,Tume ya Jaji Warioba itakumbana na kituko cha mikutano
ya watu wa ajabu wasio na ufahamu juu ya mahitaji ya msingi ya wananchi
wenzao,isipokuwa wamelipwa posho za mikutano na kujiondokea.
Kulingana na
Tangazo la Serikali Na 394 la mwaka 2011 Sheria Na 2 ya mwaka 2012 kifu.3,
Mabaraza haya yanayoundwa na raia wa Tanzania yangepaswa kuwa na mawazo ya
Watanzania,badala ya kuwakilisha kiu ya posho,njaa na uzalendo wa matumbo yao
badala ya uzalendo kwa taifa letu.
Kuhonga
wananchi vitu vidogo vidogo ili wachjaguliwe kushiriki Mabaraza hayo pasipo
wengine kujua na kusoma, ili wakapitia Rasimu ya Katiba,ni kichekesho cha
mwaka.
Nimezungumza
na wananchi wa Kata ya Nyambono,wilayani Butiama,mkoani Mara, wakasema uchaguzi
uliofanywa katani humo umeshinikizwa na viongozi ili wasikose kura kutoka kila
kijiji katika uchaguzi wa 2014 wa serikali za Mitaa.
Mahali
pengine uchaguzi wa Mabaraza ya Katiba ulifuata itikadi,dini na ukoo kiasi
kwamba watu makini walitupwa nje,wakachaguliwa watu ambao hata kujua kusoma ni
taabu. Sasa hawa watapitia vipi Rasimu ya Katiba,ikiwa hata kuzungumza
Kiswahili ni shida?
Ama Tume ya
Jaji Warioba inataka kushirikisha wananchi wengi mbumbumbu sana,mradi tuseme
Katiba Mpya ilitungwa na wananchi wa kawaida,hata kama hajui kusoma wala
kuandika?
Hawa wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba, wengi wao hata Katiba hajui ni mnyama gani, na kwa
kuwashawishi wananchi wenzao ili wawachague wamedhihirisha hawafai,maana ni
wala rushwa ambao hawawezi kutuletea Katiba ya maana,isipokuwa mianya ya posho
na ulaji!
Nawashangaa
wananchi hasa wa vijijini na mitaa ya Mijini,kuhongwa chai,maharage na unga ili
wawachague watu vipofu ili wakapitie Rasimu ya Katiba! Ati hii ndiyo
Demokrasia(Participation of Majority?) ushirikishaji wa watu wengi mbumbumbu
ili kututungia Katiba Mpya!
Nawashangaa
wananchi,kuwachagua watu Mbumbumbu Mzungu wa Reli(si wote) ili kupitia Rasimu
ya Katiba,kwa sababu tu walituhonga,ama walikuwa wa dini yetu,jamaa zetu ama wa
chama chetu!
Nimewaona
wanachama wa chama Fulani cha siasa wakimsuta Diwani kutoka chama chao kwamba
walimsaidia kushinda sasa amewatupa kwenye ulaji wa Mabaraza ya Katiba ya Kata!
Nimewasikia
wanachama wa chama kimoja wakilalamika kuachwa katika mabaraza hayo kwa kuwa
walikuwa na itikadi tofauti!
Kwa nini
Rasimu ya Katiba Mpya kujadiliwa na wajumbe waliopatikana kwa mizengwe na
rushwa, wakati hata uelewa wao ni shida kubainika miongoni mwa jamii?
Eti jambo la
msingi kama Katiba linatawaliwa na tama ya posho,udini,udugu,kujuana na itikadi
za vyama-huu ni umajununi.
Bado hatujui
umuhimu wa Katiba, ingawa vijijini inasemwa kuwa wananchi hunyanyaswa sana na
polisi,watendaji wa vijiji na kata,hata Haki za Binadamu hukiukwa sana,badala
yake wamechaguliwa watu kwa rushwa ili wakatazame Rasimu ya Katiba!
Hawa wapenda
posho wataitazama Rasimu ya Katiba Mpya ili kutafuta Haki zao za Msingi kwenye
Katiba Mpya, ama ni kichekesho?
SHeria Na
1(5) inatoa Uhuru wa Maoni(Freedom of Expression) lakini uhuru gani ikiwa
wamechaguliwa mbumbumbu ili wakatetee raia wa vijijini kunyimwa malipo ya mazao
yao na kuswekwa rumande na polisi na watendaji wa kata hadi wahonge mbuzi,ndipo
wapewe dhamana?
Katiba ya
kuwatoa kamasi miungu watu wa vijijini itatungwa na watu wasiojua kusoma na kuandika?
Kuna
wasiwasi jumuiya za wakulima vijijini kuwakilishwa na watu wa ajabu sana,wakati
jumuiya zingine kama wafanyakazi wakiwemo walimu na wale wa migodini
wamewakilishwa vema na watu wenye weledi kuingiza mahitaji yao katika Katiba
Mpya.
Hapa,demokrasia
ambayo ni ushirikishwaji wa wengi imekosa shabaha kuwaleta watu wenye nia ya
kugombea posho kupitia Rasimu ya Katiba!
Posho na
Katiba ni vitu viwili tofauti,na namwomba Jaji Waryoba kuwahoji watu hawa
mlangoni kabla ya kushiriki mikutano hiyo kwa kulala usingizi na kusubiri
kusaini posho nono inayotegemewa kutoka Tume ya Katiba.
Nashauri
zoezi hili lisitishwe,ili wakulima wajipatie wawakilishi wenye weledi ili
kutetea Haki za Wakulima vijijini ambao ni wengi lakini hawana hospitali wala
barabara,licha ya Pato la Taifa kutokana na Kilimo wanaolima wameachwa nyuma
wakati miundo mbinu inapojengwa mijini.
Bei za mazao
zinaporomoka wakati wafanyakazi wa mijini wanapoongezewa mishahara mikubwa,
wanalalama sana wakati mkulima anapohongwa chai ili amchague mbumbumbu kwenda
kuandika Katiba!
Demokrasia
haina maana ikiwa itawashirikisha watu wa ajabu sana kupitia Rasimu ya
Katiba,utungwe mtihani watakaoshinda wapitishwe kwenda kupitia Rasimu hiyo ya
Katiba ambayo ni muhimu kwa Tanzania ya kesho,lengo ni kuwatimua wajumbe
wapenda posho katika mikutano hiyo.
0786 324 074
www.congesmrambatoday.blogspot.com
No comments:
Post a Comment