Tuesday, September 3, 2013

ukweli ni nini?


      
Historia ndiyo Darubini kali iliyomwibua mmoja wa Wanafalsafa wakubwa Ugiriki, ambaye anaweza kutwambia nini maana ya Ukweli?
Aristotle wa Athens aliyeishi kati ya mwaka 384 hadi 322 BC. Alipata kusema:
“Truth is agreement with FACTS and REALITY” ,Tafsiri yangu ni kwamba,Ukweli ni mwafaka baina ya habari ya kilichotukia na usahihi ama uhalisia wa mambo.
Kulingana na Aristotle, ukweli huweza kuongopa ikiwa UKWELI nusu-nusu unapowaongoza watu kwenye UONGO.
Aristotle  alisema hivi:
“To say what is that is not or of what is not that is-is FALSE, while to say what of what is that it is, and what is not that is not-is TRUE!!
Tafsiri yangu isiyo rasmi ni kwamba Aristotle alisema kusema jambo kwa namna isivyokuwa namna kitu kilivyokuwa hakika,ni UONGO;wakati kusema kitu kilivyo hakika na ukasema kwamba hakiko hivyo wakati hakiko hivyo huo ni Ukweli.
Aristotle, hutwambia kuhusu UONGO WA UKWELI(The lie of Truth) ambao mfano wake ni kama kudondosha tone la ukweli katika pipa la Uongo.Ukweli hauchanganywi na uongo ukabaki ukweli.Sumu kidogo ya panya haichanganywi na unga au mkate,kikabaki kuwa chakula bali sumu!
Chakula jumlisha sumu ni sumu,basi.
Naam, ‘a little truth drop in the bucket’ matokeo yake ni jamii kuamini uongo na kuufanyia kazi, ndivyo ilivyo hata hapa Tanzania.Jamii hufanyia kazi umbeya,uongo na upumbavu tu!
Watu wengi hata hapa Tanzania hudanganywa kwa ukweli kidogo ndani ya uongo mwingi,na tayari wameathiriwa na sumu ya uongo na umbeya,mishipa yao ya fahamu imedhoofishwa na majungu na uvumi.
Nilishaandika kwamba, Daktari akisema ‘Unaumwa Ukimwi’ ni FACTS-ni ukweli dhahiri. Lakini mpigadebe akisema kwakuwa una kikohozi na kichomi na umekonda-ni ‘Opinion’ ni maoni tu-maoni siyo ukweli halisi,ni kukisia na umbeya tu.Angalia sasa nchi hii walivyo hawatofautishi Opinion na Facts!
Ukweli haufahamiki kwa kusemwa na watu wengi ama kwa njia ya sanduku la kura!
Mwandishi,Derek J.Morris aliandika katika Jarida la MINISTRY la Juni mwaka huu 2013, kama ifuatavyo:
“TRUTH is not determined by opinion poll or popular vote!”
Ukweli hauamuliwi kwa wingi wa kura za maoni za watu wengi vijiweni! UKWELI huweza kusemwa na mtu mmoja mwenye taaluma kama daktari kusema ‘una ukimwi’ ndugu zako na jamaa wote wakashikilia umerogwa!
Ukweli hauamuliwi kwa sauti kubwa na maandamano ya vibaka na wanasiasa wakasema ndiyo NGUVU YA UMMA!
Aristotle amesema watu wengi huchelea kusema ukweli wasije wakachukiwa na umma mkubwa, ‘PEOPLES POWER’.
Watu wengi siyo wa kuamini,na mawazo yao siyo ya kufanyia kazi mara zote,wapo wafuata mkumbo tu,mashabiki na mabingwa wa kuigiza kila jambo na kuangamiza jambii kama tunavyoona leo madawa ya kulevya,bangi na ndoa za jinsia moja!
Bendera kufuata upepo tu! Kizazi hiki kimepotoka mno,kwa kuiga ya Magharibi ya watu wengi, sasa wachache hawana cha kusema,wataalam kama madaktari, wahandisi,maprofesa n.k ushauri wao ulishakataliwa na public opinion.
Siku hizi ‘wengi wape’ japo wapumbavu sana!
Watu wengi, aghalabu mbumbumbu mzungu wa reli fuata mkumbo, propaganda za siasa huishia kuipotosha jamii na kizazi hiki kwamba ndiyo haki za Binadamu.Haki za Mashoga,haki za wasagaji,haki za watoto kutochapwa viboko n.k
Watu wachache wenye haki aghalabu hawana ubavu wa kutetea ukweli usiochanganywa na uongo,umbeya,hisia tu na majungu.
Wakristo wameonywa sana kuwa waangalifu katika kuamua kati ya UKWELI(Right) na uongo(Wrong) kwa kufuata kura za maoni za wajinga wengi(Opinion poll) ama kura za watu wengi wanaopenda uhalifu na uovu(popular vote).
Kuna watu hawataki hata sheria ziwepo ili waingie mitaani na kupora mali za wenzao kwa kisingizio, Maisha ni Magumu!
Wachache wenye hekima wanajua matokeo ya kukosekana kwa sheria,lakini wapumbavu wengi watalaani kuwepo sheria,mahakama,polisi,mgambo,mahakimu n.k hawa wote ni vibaka akilini.
Ukweli na uongo,sharti kuamuliwa kwa muktadha wa mafundisho sahihi ya Neno la Mungu(Biblia n.k)Kwa mfano Zaburi 119:105 HUSEMA Neno la Mungu ni Taa iongozayo miguu ya wenye haki.
Watu wanasema Mungu alishakufa,hayupo na neon lake ni batili,sasa hawa wanakwenda njia gani halafu uwafuate gizani?
Watu wanapotaka kwenda upande wa kweli wa Historia,wanapaswa kugeukia hekima ya Mungu tu basi. Hekima ya Mungu ni Ukweli,haki,amani,upendo n.k
Biblia,kwa mfano husema njia ni nyembamba sana iendayo kwenye ukweli nao wanaoona ukweli ni wachache tu.Wengi huenda kwenye uongo,maana njia ya uongo ni pana hata mbumbumbu huiona.
Njia ya haki huonwa na wenye hekima,ni nyembamba hutazamwa kwa hadubini kali.
Ni kwa sababu hii,watu shupavu wanaotetea ukweli(rejea tafsiri ya ukweli) hawapendwi na wengi;huishia kutengwa,kusulubiwa.
Kusema kwamba kitu hiki hakiko hivyo wakati kweli hakiko hivyo ni hatari,unafanywa kama Nabii Yeremia,Martin Luther King Jr,Martin Luther wa Ujerumani,Socrates,Yohana Mbatizaji,orodha ndefu.
Katika kitabu cha Luka Mtakatifu 3:11-14 Yohana Mbatizaji anapokemea rushwa,ufisadi miongoni mwa maofisa wa serikali fisadi, anapokataza masikini kuporwa wake na mali zao, anaishiwa kunyongwa kijinga.
Nani atatetea kichwa ili akatwe kichwa?
Marko Mtakatifu 6: 17 na 18 hutwambia kwamba ni mtu labda mmoja tu anayekubali ukweli usemwe potelea mbali apoteze maisha yake,kuliko kuacha wajinga wengi waseme uongo na kuufurahia.
Public Opinion, mara nyingi hukinzana na ukweli na uhalisia wa mambo-husema minyoo huletwa na wachawi,na wala siyo uchafu na kula bila kunawa ama kunywa maji yasiyo chemshwa!
Ukisema ukweli utaitwa msaliti! Kuna mifano tele katika Biblia,niiache wengine wananiambia hataki kusoma biblia.Biblia ni kitabu,hawapendi kusoma ila kucheza na kucheka-cheka tu.
Nimesema kwamba ukweli huonwa na wachache tu na husimamiwa na watu shupavu wawili ama watatu tu-wengine bendera kufuata upepo unakoelekea, watu wengi wanafiki tu.
Wanaosema ukweli huitwa waongo na waongo huitwa wakweli.Mara nyingi waongo huenda kinyume cha Historia-The wrong side of History.
Historia inamsema Socrates(469-400 BC) ALIVYOULIWA na utawala wa Athens kwa kukataa umbeya kwamba kuna miungu 391 inatawala juu ya Mlima Olympus!
Walimpa sumu ainywe kwa kutetea kwamba kuna Mungu mmoja na huishi mbinguni tu. Yesu aligoma kufuata dini ya ukandamizi ya Kiyahudi, Martin Luther aligomea mafundisho ya Kipapa, Martin Luther King Jr. ambaye juzi Ndoto yake( (I have a Dream)ilisherehekewa miaka 50 na akina Obama, aliuliwa Aprili 1968 kwa kusisitiza ukweli kuhusu ubaguzi wa rangi Marekani, aliuliwa na Pentagon kwa kutetea ukweli.
Wapo akina Mandela wamesota rumande miaka 27, wapo wengine walifukuzwa kazi n.k
Katika mfululizo wa makala haya nitatilia shaka kila kinachoitwa UKWELI ili kutufanya kuchunguza mambo kwa akili tunduizi(critical mind) kuacha mikumbo na umbeya wa siasa za kipumbavu zinzoleta ugomvi katika jamii hii.
Tutajadili ‘fuata mkumbo’ iliyoleta shida hapa Tanzania, katika Nyanja tofauti siyo siasa tumhata dini zinazoshadidiwa na watu.
Nitakuwa nikitumia nukuu za wanafalsafa,wasomi,wataalam lengo ni kukiokoa kizazi hiki na kuiga na kufuata mkumbo wa kila kinachosemwa ili tuepuke propaganda,matangazo ya uongo redioni kwenye tv na maamuzi ya wengi katika kura za maoni(Opinion polls)
Nitatilia shaka hata katiba mpya itakayoamuliwa na wengi,lakini vipofu wakaacha maoni ya wachache ama mmoja mwenye hekima,mtu wa haki mnyoofu n.k
0786 324 074



Wednesday, August 14, 2013

MUGABE ALIPOMTUKANA BUSH NEW YOR



                                


                      


Miaka zaidi ta 10  iliyopita, ripoti ya Military Balance( ya harakati za Kijeshi Duniani) iliyochapishwa na Chuo Kikuu cha Oxford Uingereza, ilionyesha Korea Kaskazini na Iran zikiwa juu katika Orodha ya nchi 30 zenye vikosi vingi vya kijeshi Duniani.
     Hadi 1999, ripoti hiyo ya mwaka 2000 ilisema, Korea Kaskazini ilikuwa ya nne Duniani ikiwa na jumla ya vikosi 1,055.0 nyuma ya India yenye vikosi 1,173.0, Marekani (vikosi 1,371.5), na Uchina yenye vikosi 2,820.0.
   Hii maana yake ni kwamba, nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na vikosi vingi vya kijeshi ni Uchina, ikifuatiwa na Marekani, kisha India na Korea Kaskazini. Russia ilikuwa na vikosi 1,004.0, wakati Korea Kaskazini ilikuwa na majeshi ya Akiba 4,700.0 ikitumia Dola za Mrekani Bilioni 2.5 katika medani hiyo ya ulinzi.
   Marekani yenyewe ilikuwa ikitumia Dola zake Bilioni 283, Uchina(dola bilioni39.9), na India(dola bilioni 15, wakati Russia ilikuwa ikitumia dola bilioni56.8 katika ulinzi wakati raia wake wakifa njaa.
      Korea Kusini ilishika nafasi ya sita duniani kwa ukubwa wa majeshi, ikiwa na vikosi 672.0 na majeshi ya Akiba 4,500.0 ikitumia kiasi cha dola bilioni 12.1 za Marekani katika medani ya ulinzi.
    Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa ya nane ikiwa na vikosi 545.6; wakati ilikuwa na majeshi ya akiba 350.0; ikitumia dola za Marekani bilioni 5.7. Iran ilikuwa na vifaru vikubwa vya kivita(MBT) 1,135 na madege, nyambizi na zana nyingine hatari.
    India na Pakistan waliingia katika orodha ya Mataifa ya Nyuklia mwaka 1998. Wakati Iran wanazua mchecheto kwa Mpango wao wa Nyuklia, Korea Kaskazini wameshawishiwa kufunga kiny chao cha Yongbyon kwa mrabaha wa tani milioni za mafuta, au kitita chenye thamani sawa na mafuta hayo.
      Pakistan ilikuwa ya sita ikiwa na vikosi 587.0; vikosi vya akiba 513, vifaru vikubwa 2,285. Katika orodha hii, kutoka Afrika, nchi za Misri ni ya 11 nyuma ya Vietnam. Misri ina vikosi 450.0, vya akiba 254.0 na hutumia dola za Marekani bilioni tatu kwa gharama za kijeshi.

                          VITA VYA MISRI NA ISRAELI
    Umewahi kusikia vita vya Misri na Israeli mwaka 1973?
Tulikuwa  ukingali kinda.
 Lakini, Israeli iliingia vitani kupambana na Misri ikiwa na jumla ya vifaru, ndege na vikosi vichache sana kulinganisha na vile utitiri vya Waarabu. Waarabu walisaidiwa sana na Urusi.
    Israeli ilikwenda Sinai na vifaru 1,700 tu kulinganisha na 2,600 vya Misri na 2,000 vya Syria.
   Kwa siku tatu tu za vita, Israeli ilikwishapata hasara kubwa, ikabaki kufanya mashambulizi  ya kushtukiza(counter-attacks). Israeli  Iliishikilia Sinai wakati wa vita vya siku sita, mwaka 1967.
    Kuona hivyo, Rais Jimmy Carter wa Marekani akakimbia kumwita Waziri Mkuu wa Israeli, Menachem Begin na Rais wa Misri, Anwar al Sadat kule Camp David mwaka 1978.
  Henry Kissinger,yule Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, akakimbia kutafuta amani na suluhu, kwa sababu Israeli ilikuwa inamwagiwa maji ya moto na Waarabu katika vita. Wakati huo, Waisraeli walikuwa wakisherehekea Siku Kuu ya Kiyahudi, Yom Kippur; walisalimu amri na kuiachia Sinai, huku Mayahudi wakilalama.

                         ETHIOPIA MSHIRIKA WA MAREKANI
     Naam. Ethiopia ni ya 17 katika orodha ya nchi zenye majeshi makubwa duniani ikiwa na jumla ya vikosi 325.5; na hutumia dola bilioni 0.4 katika bajeti yake ya ulinzi. Utaona ni jinsi gani waweza kutuliza ghasia hata Somalia.
    Eritrea ni ya 29, Morocco ya 30, Ujerumani ya 16, Myanmar (Burma) inayopigana na waasi sasa ya15, Ufaransa (ina Nyuklia) ya 18, Sysia ya 19, Japan ya 25, Uingereza(ina Nyuklia) ya 27 miongoni mwa nchi hizo 30.
     Mwaka 1999 Iran ilikuwa na vifaru 1,135 wakatI Uingereza wakiwa na 616 tu, Ufaransa walikuwa na vifaru 1,207, Ujerumani walikuwa na 2,815. Hali hii huonyesha ni jinsi gani Wakurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani(CIA) walikuwa makini sana kuchunguza harakati za kijeshi za Iran, Syria, Korea Kaskazini na Waarabu wengine wasioiunga mkono Marekani na washirika wake.
    Utaona wakurugenzi wa CIA, akina William E.Colby, George Bush(Baba), Stanfield Turner, William J. Casey, William Webster, Robert M. Gates(Waziri wa Ulinzi), R. James Woolsey, John M. Deutch na George J. Ternet, walivyokuwa makini siku zote kuzihujumu nchi hizo katika harakati zao za kijeshi.
     Hizi ni harakati za vichaa kujaribu kutafuta amani katika dunia majununi(Crazy People in Crazy World).Ndiyo maana kuna mikataba mingi sana ya kuzuia utengenezaji wa silaha hatari tangu mwaka 1963.
     Miongoni mwa hii ni Strategic Arms Reduction Treaty (START) wa kwanza na wa pili uliokuja kusainiwa Moscow, kati ya Urusi na Marekani.
   Upo pia uitwao, Comprehensive Test Ban Treaty(CTBT) uliozuia majaribio ya Nyuklia na milipuko wa Septemba 1996.
    Oktoba 2000 nchi 160 kati ya 196 zilitia saini Mkataba huo, pamoja na Marekani, Russia, Uchina, Uingereza na Ufaransa.
    Wakati huo wa vita baridi, Kambi mbili za Mashariki(za Mkataba wa Warsaw) na Magharibi, NATO(North Atlantic Treaty Organization), walishindana sana kutewngeneza silaha.
      Mkataba uitwao, SALT (Strategic Arms Limitation Treaty) wa kwanza na wa pili uliazimu kupunguza silaha za masafa marefu. Miongoni mwa makombora ya masafa marefu yaliyomilikiwa na kila upande ni ICBM(Intercontinental Ballistic Missile); misaili lenye kulenga shabaha zaidi ya kilomita 6,000; zaidi ya kutoka Moscow hadi Washington.
     Misaili nyingine ni SLBM (Submarine Launched Ballistic Missile), MIRV (Multiple Independently Targetable Re-entry Vehicle), gari linaloruhusu misaili kubeba zaidi ya kichwa kimoja cha silaha na kupiga shabaha tofauti bila kukosa.
     Baadhi ya watu wanahoji: Kama Marekani wana nia njema ya kuiokoa dunia na maangamizi; kwa nini wameshindwa kusaini mkataba wa Kyoto unaozuia uzalishaji wa gesi za sumu angani zinazoleta ongezeko la joto? Je, Ongezeko la gesi za sumu na joto duniani, si kitisho zaidi ya Nyuklia?
    Matukio ya Septemba 11 mwaka 2001 yameifanya Marekani kuchanganyikiwa na kuwa wababe zaidi ili kuyakandamiza mataifa ya Kiarabu, ili kujilinda zaidi dhidi.
    Jengo la WTC lilipobomolewa kwa mara nyingine mwaka 2001, liliwaonyesha Wamarekani jinsi ya kuwa makini zaidi na adui zao Waarabu.
Vifusi vya WTC ni mnara wa kumbukumbu ya kipigo cha magaidi. Ukiupima udongo wote wa kifusi cha WTC hutakosa tani milioni 1.2, na kifusi chote kimejaa eneo la ekari 10.
    Inakisiwa,  mpango wa mashambulizi ya Sepotemba 11 umegharimu kati ya Dola za Marekani 200,000 na 500,000; na kwamba uchumi wa New York uliathiriwa kwa zaidi ya Dola bilioni 100.
   Rais Robert Mugabe na Bush, mwaka 2007 walifafanua jinsi gani fujo za ‘vichaa’ kama akina Bush na Mugabe  wanapojaribu kutafuta amani ya dunia  kwa kupandisha mizuka!
    Alhamisi, Septemba 27 mwaka 2007, Mugabe alisema kitu kinachosaidia kujibu maswali ya wasomaji wengi wa Rai juu ya unafiki wa wakuu wa dunia hii.

    ‘RG’ MUGABE AMEBAKI  ILI KUWATOA KAMASI MAREKANI
    Akihutubia kwa ukali Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa(UN), Mugabe alisema Bush ni ‘mnafiki mwandamizi’ anayejidai kuheshimu Haki za Binadamu, kumbe vitanga vya mikono yake vimelowa damu za watu, hususan katika viambaza vya Guantanamo Bay!
Na Abu Ghraib.
       “Vitanga vya mikono(ya Bush)  vilikuwa vinachuruzika damu ya wasio na hatia wa mataifa mengi”, Mugabe alisema katika hotuba kali katika mkutano huo wa 62 wa Umoja wa Mataifa,”Anajidai kuwa Mkuu wetu katika Haki za Binadamu?”
   Mugabe(89) ambaye amezeeka,nchi imemshinda lakini hadi sasa akina Tsivangirai si mbadala wake, alihoji siku hiyo hiyo Bush alipozizodoa Belarus, Syria, Iran na Korea Kaskazini kama ‘Mataifa katili zaidi’ duniani.
    Akiizungumzia Zimbabwe, Bush alisema inaongozwa na ‘JAHILI’ Mugabe, anayewararua watu wake mwenyewe.
                Zimbabwe leo inakumbwa na kimbunga kikali cha uchumi mbaya.
Mfumuko wa bei unafika asilimia 7,000 na utafika asilimia 10,000 kabla ya Krisimasi. Fedha zinafika mwisho wa matumizi(expiration) utadhani unga wa ngano ama dawa ya mswaki. Mugabe anawatupia lawama Wazungu kwa hujuma anuwai.
Hata hivyo Zimbabwe sasa hutumia dola za Marekani badala ya dola ya Zimbabwe!
     Lakini, mwaka 2007 akamchambua Bush (kama karanga) na kusema ni mnafiki wa hali ya juu!
    Mugabe, pia amewahi kuwatwanga virungu wapinzani wake, akiwamo Morgan Tsivangirai wa MDC.Tsivangirai sasa kashindwa, analalama kuwa kaibiwa kura!
   Lakini, alisema Bush anatesa watu Abu Ghraibu nchini Irak na katika jela za kijeshi  nchini Cuba, mahali walipowatuhumiwa wa al-Qaeda!
Ilikuwa safi hiyo?
    “Katika kambi hizo za mateso”, alisema Mugabe, “Hakuna sheria na hata zile za kimataifa hazina nguvu. Marekani wanawajibika kuandika upya Tangazo la Haki za Binadamu…hata Septemba 11(2001) Wamarekani ni wakosaji”, alisema Mugabe.
    Mugabe alimkosoa Bush kwa kuwakamata watuhumiwa na kuwafunga bila kuwafikisha mahakamani. Mugabe anamuunganisha Bush na rafikiye, Tony Blair(Waziri mkuu mstaafu wa Ui8ngereza) kama watu walioiburuza sana dunia, hususan Umoja wa Mataifa. Baada ya kuharibu Irak sasa wanaacha jukumu kwa Umoja wa Mataifa kulinda amani na kuponya kidonda!
   “Mwenyezi Bush(alimkejeli kujilinganisha na Mungu) sasa karejea Umoja wa Mataifa kusaka msaada wa wokovu…kwa sababu, pua  yake inavuja damu zisizo na hatia…bado anajitutumua kutuhadithia madhila ya ukatili”, Mugabe alisema.
     Naam, hivi ni vituko vya vichaa katika Ulimwengu majununi(Crazy People in a Crazy World), Mugabe na Bush kumwagiana shombo katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kusaka amani! Mkuki kwa nguruwe sijui nyani dume haoni kundule? Alamsiki.
   0713 324 074
                       



Monday, August 5, 2013

http://ts2.mm.bing.net/th?id=U.4930640688712695&pid=15.1

KIKOMBE CHA BABU WA LOLIONDO KIMEINYWESHA SUMU TZ




ZAIDI ya watu 10,260 waliacha kwenda kuchukua dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi Mkoani hapa,tangu 2004 hata sasa.
Serikali ya Tanzania leo,kwa kushirikiana na Tume ya Kikristo, The Christian Social Service Commission(CSSC) na serikali ya Marekani,siku hizi wanatumia mabilioni ya Dola za Marekani kuwarejesha wenye virusi vya Ukimwi hospitalini ili kupata tiba ya kisayansi.
Mkakati huo unaitwa, ‘Back to Treatment” na unalenga kuwarejesha watu 10,262 wa mkoa wa Mwanza tu hospitalini.
Baadhi yao waliacha tiba ya kisayansi, wakatimkia Samunge,Loliondo mwaka 2011 kwa Yule ‘Babu’ wa Kikombe cha Miujiza,kilichodaiwa kuponya magonjwa sugu,ukiwemo Ukimwi kwa majuma matatu tu!
Ambilikile Mwasapila,(78),Mchungaji Mstaafu wa KKKT, alikuwa ameota ndoto ikimwambia aondoke Babati na kuhamia porini huko Samunge, ambako alianza kunywesha maelfu ya watu kutoka Afrika Mashariki,Ulaya na Asia dawa ya miujiza kutoka kwenye mti uitwao,Carisa Spinarum, ama ttuuite     Mrigariga!
Serikali ikaanza kuishabikia dawa hiyo iliyouzwa kwa shilingi 500 tu kwa kikombe, maelfu ya watu wakanywa, wakiwemo wasomi,maprofesa,wafanyabiashara na hata wakulima wa kijijini.
Vigogo wa serikalini walikuwa mstari wa mbele kuishabikia na kuibugia ili wapate tiba ya kimiujiza-Cure in the Tanzanian Bush!
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Abbas Kandolo(yuko Mbeya siku hizi) alipoulizwa na Mwandishi huyu aliyefanya mkutano kamambe ofisini kwake kuratibu safari za kwa ‘Babu’ wa Loliondo,mwaka huo 2011, “Ni kwanini serikali inahaha kushiriki ushirikina na miujiza ya uponyaji huko kwa Babu,Loliondo, kabla ya dawa hiyo kuthibitishwana taasisi husika, Tropical Pesticides Research Institute, TFDA, labda na TBS, akaniambia kwa hamaki!
“Sasa wewe mtu layman (usiye na taaluma ya kitabibu) unawazidi maprofesa wanaoinywa dawa ya Babu wa Loliondo?” akamtaja mkubwa mmoja.
Katika mkutano huo wa Mkuu wa Mkoa na wafanyabiashara wenye mabasi ya kusafirisha watu kwenda Loliondo, walikaribia kunimeza,kuona nilikuwa nikitaka kuwaharibia biashara, wakati serikali ilishamkubali huyo ‘Babu wa Kikombe’ aliyeleta neema kwa wenye mabasi mwaka 2011.
Carisa tree, ni mti uliokuwa ukitajirisha si babu huyo tu, bali na wenye vyombo vya usafirishaji na hata mama ntilie wa Samunge.Wagonjwa wengine waliopelekwa wakiwa mahututi, walifariki dunia.
Leo,serikali inameza machungu, inashirikiana na serikali ya Marekani na taasisi za dini kufanya mkakati wa kuwarejesha wenye virusi vya Ukimwi kwenye tiba uitwao kwa Kimombo, “Back  To Treatment” kwa mabilioni ya dola.
Mkakati huu, BACK TO TREATMENT, ulizinduliwa rasmi jijini Mwanza Agosti Mosi mwaka huu kwa mbwembwe, na watu wakalipana posho!
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanywa katika Hospitali ya Sekou Toure, Mkurugenzi Mkazi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa wa Tume hiyo ya Kikristo ya Huduma za Jamii,Dk.Michelle Roland       akasema:
“Tangu 2003 serikali za Marekani na Jamhuri ya Muungano zimekuwa na ushirika kupambana na Ukimwi unaoathiri watu wote Duniani,hususan Watanzania”,Dk. Michelle Roland alisema.
Akabainisha kuwa ubia huu umewafanya wananchi wa Marekani kuchanga jumla ya Dola za Marekani bilioni 2.2 ambazo ni sawa na shilingi za Tanzania Trilioni 3.2.
Fedha hizi ni kwa ajili ya kupambana na magonjwa sugu,ukiwemo Ukimwi.
Mkuu wa Mkoa,Evarist Welle Ndikilo, akafungua mkakati huo, akisema Tanzania Bara sasa kuna zaidi ya watu 430,000 wanaopewa dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi kupitia Mpango huo wa Back to Treatment wa hao  Christian Social Service Commission(CSSC).
Ndikilo, akasema eti sasa Mkakati huo wa Back to Treatment utawarejesha wagonjwa kwenye tiba na utaifanya Tanzania mahali pasipo na maambukizi ya Ukimwi-AIDS-free Tanzania!
Labda, asitokee Babu mwingine kama wa Loliondo,bibi ama shangazi!
Asilimia 25 ya wenye kuishi na virusi vya Ukimwi walikimbia vituo vya kutolea dawa za Ukimwi, antiretroviral Therapy.
Wamekuwa hawapati dawa hizo ili kuwawezesha kuishi na afya njema na kushiriki ujenzi wa taifa.
Mama huyu wa Kimarekani,Michelle Roland, akaonya kuwa endapo wenye kuishi na virusi vya ukimwi hawatapata tiba sahihi,jamii nzima itaathiriwa vibaya,na maambukizi yataongezeka maradufu, na virusi vitajenga usugu-hizi ni athari za akina Abbas Kandoro kupigia debe Sangoma,kama Babu wa Loliondo!
Pia,Dk.Michelle Roland amewataka wenye virusi vya Ukimwi kwenda hospitalini kupata tiba sahihi,kando ya mfumuko wa vikombe vya babu na shangazi!
Akashauri udhaifu uliopo katika mfumo wa tiba(zikiwemo imani potofu za viongozi ba ushirikina) uepukwe,ili watu waishio na virusi vya Ukimwi warejeshwe kwenye huduma za tiba na ushauri sahihi.
Dk. Michelle akawataka watu kubadilika,na kuacha kushabikia uvumi na umizimu na masangoma.
Kampeni kama hii iliwahi kuzinduliwa Iringa na Balozi wa zamani wa Marekani nchini,Alfonso Lenhardt.Ilikuwa Septemba mwaka uliopita.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Evarist Ndikilo amesema Tanzania kuna watu 945,142 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.
Kati ya hawa 530,118 ndiyo walioanzishiwa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi, watu 129,372 hapa Tanzania wamekimbia matibabu,wengine walitupa vidonge walipokunywa Kikombe cha Babu!
Hadi Machi mwaka huu watu 85,320 Mkoani Mwanza waliandikishwa kupata huduma,lakini ni 46,622 tu walioanzishiwa tiba.
Watu zaidi ya 10,000 hawajulikani walikokwenda,hawa ni pamoja na watoto 1,600 hapa Mkoani Mwanza.
Sasa  tukiulize,hizo imani za kishirikina zinazoshabikiwa na serikali na maofisa wake hata kukiuka sheria ilizoweka yenyewe kuhusu tiba ndiyo nini,kama siyo kuitesa nchi?
Imani potofu,ushirikina hata wa kuua Albino ili kushinda kura,kupata utajiri n.k
Wengine,watu wakubwa walibugizwa dawa ya babu na kuwafanya maelfu kufuata mkumbo wakaacha tiba sahihi.
Ndiyo maana tukasema, Kikombe cha Babu kimeinywesha sumu Tanzania,sasa inatumia mabilioni ya dola kurejesha wenye VVU hospitalini.
Hawa ni wenye VVU tu, saratani,kisukari,magonjwa ya moyo n.k siku hizi hupelekwa kwa sangoma kwa Baraka za akina Abbas Kandoro na serikali nzima!
0786 324 074