Wednesday, August 14, 2013

MUGABE ALIPOMTUKANA BUSH NEW YOR



                                


                      


Miaka zaidi ta 10  iliyopita, ripoti ya Military Balance( ya harakati za Kijeshi Duniani) iliyochapishwa na Chuo Kikuu cha Oxford Uingereza, ilionyesha Korea Kaskazini na Iran zikiwa juu katika Orodha ya nchi 30 zenye vikosi vingi vya kijeshi Duniani.
     Hadi 1999, ripoti hiyo ya mwaka 2000 ilisema, Korea Kaskazini ilikuwa ya nne Duniani ikiwa na jumla ya vikosi 1,055.0 nyuma ya India yenye vikosi 1,173.0, Marekani (vikosi 1,371.5), na Uchina yenye vikosi 2,820.0.
   Hii maana yake ni kwamba, nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na vikosi vingi vya kijeshi ni Uchina, ikifuatiwa na Marekani, kisha India na Korea Kaskazini. Russia ilikuwa na vikosi 1,004.0, wakati Korea Kaskazini ilikuwa na majeshi ya Akiba 4,700.0 ikitumia Dola za Mrekani Bilioni 2.5 katika medani hiyo ya ulinzi.
   Marekani yenyewe ilikuwa ikitumia Dola zake Bilioni 283, Uchina(dola bilioni39.9), na India(dola bilioni 15, wakati Russia ilikuwa ikitumia dola bilioni56.8 katika ulinzi wakati raia wake wakifa njaa.
      Korea Kusini ilishika nafasi ya sita duniani kwa ukubwa wa majeshi, ikiwa na vikosi 672.0 na majeshi ya Akiba 4,500.0 ikitumia kiasi cha dola bilioni 12.1 za Marekani katika medani ya ulinzi.
    Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa ya nane ikiwa na vikosi 545.6; wakati ilikuwa na majeshi ya akiba 350.0; ikitumia dola za Marekani bilioni 5.7. Iran ilikuwa na vifaru vikubwa vya kivita(MBT) 1,135 na madege, nyambizi na zana nyingine hatari.
    India na Pakistan waliingia katika orodha ya Mataifa ya Nyuklia mwaka 1998. Wakati Iran wanazua mchecheto kwa Mpango wao wa Nyuklia, Korea Kaskazini wameshawishiwa kufunga kiny chao cha Yongbyon kwa mrabaha wa tani milioni za mafuta, au kitita chenye thamani sawa na mafuta hayo.
      Pakistan ilikuwa ya sita ikiwa na vikosi 587.0; vikosi vya akiba 513, vifaru vikubwa 2,285. Katika orodha hii, kutoka Afrika, nchi za Misri ni ya 11 nyuma ya Vietnam. Misri ina vikosi 450.0, vya akiba 254.0 na hutumia dola za Marekani bilioni tatu kwa gharama za kijeshi.

                          VITA VYA MISRI NA ISRAELI
    Umewahi kusikia vita vya Misri na Israeli mwaka 1973?
Tulikuwa  ukingali kinda.
 Lakini, Israeli iliingia vitani kupambana na Misri ikiwa na jumla ya vifaru, ndege na vikosi vichache sana kulinganisha na vile utitiri vya Waarabu. Waarabu walisaidiwa sana na Urusi.
    Israeli ilikwenda Sinai na vifaru 1,700 tu kulinganisha na 2,600 vya Misri na 2,000 vya Syria.
   Kwa siku tatu tu za vita, Israeli ilikwishapata hasara kubwa, ikabaki kufanya mashambulizi  ya kushtukiza(counter-attacks). Israeli  Iliishikilia Sinai wakati wa vita vya siku sita, mwaka 1967.
    Kuona hivyo, Rais Jimmy Carter wa Marekani akakimbia kumwita Waziri Mkuu wa Israeli, Menachem Begin na Rais wa Misri, Anwar al Sadat kule Camp David mwaka 1978.
  Henry Kissinger,yule Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, akakimbia kutafuta amani na suluhu, kwa sababu Israeli ilikuwa inamwagiwa maji ya moto na Waarabu katika vita. Wakati huo, Waisraeli walikuwa wakisherehekea Siku Kuu ya Kiyahudi, Yom Kippur; walisalimu amri na kuiachia Sinai, huku Mayahudi wakilalama.

                         ETHIOPIA MSHIRIKA WA MAREKANI
     Naam. Ethiopia ni ya 17 katika orodha ya nchi zenye majeshi makubwa duniani ikiwa na jumla ya vikosi 325.5; na hutumia dola bilioni 0.4 katika bajeti yake ya ulinzi. Utaona ni jinsi gani waweza kutuliza ghasia hata Somalia.
    Eritrea ni ya 29, Morocco ya 30, Ujerumani ya 16, Myanmar (Burma) inayopigana na waasi sasa ya15, Ufaransa (ina Nyuklia) ya 18, Sysia ya 19, Japan ya 25, Uingereza(ina Nyuklia) ya 27 miongoni mwa nchi hizo 30.
     Mwaka 1999 Iran ilikuwa na vifaru 1,135 wakatI Uingereza wakiwa na 616 tu, Ufaransa walikuwa na vifaru 1,207, Ujerumani walikuwa na 2,815. Hali hii huonyesha ni jinsi gani Wakurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani(CIA) walikuwa makini sana kuchunguza harakati za kijeshi za Iran, Syria, Korea Kaskazini na Waarabu wengine wasioiunga mkono Marekani na washirika wake.
    Utaona wakurugenzi wa CIA, akina William E.Colby, George Bush(Baba), Stanfield Turner, William J. Casey, William Webster, Robert M. Gates(Waziri wa Ulinzi), R. James Woolsey, John M. Deutch na George J. Ternet, walivyokuwa makini siku zote kuzihujumu nchi hizo katika harakati zao za kijeshi.
     Hizi ni harakati za vichaa kujaribu kutafuta amani katika dunia majununi(Crazy People in Crazy World).Ndiyo maana kuna mikataba mingi sana ya kuzuia utengenezaji wa silaha hatari tangu mwaka 1963.
     Miongoni mwa hii ni Strategic Arms Reduction Treaty (START) wa kwanza na wa pili uliokuja kusainiwa Moscow, kati ya Urusi na Marekani.
   Upo pia uitwao, Comprehensive Test Ban Treaty(CTBT) uliozuia majaribio ya Nyuklia na milipuko wa Septemba 1996.
    Oktoba 2000 nchi 160 kati ya 196 zilitia saini Mkataba huo, pamoja na Marekani, Russia, Uchina, Uingereza na Ufaransa.
    Wakati huo wa vita baridi, Kambi mbili za Mashariki(za Mkataba wa Warsaw) na Magharibi, NATO(North Atlantic Treaty Organization), walishindana sana kutewngeneza silaha.
      Mkataba uitwao, SALT (Strategic Arms Limitation Treaty) wa kwanza na wa pili uliazimu kupunguza silaha za masafa marefu. Miongoni mwa makombora ya masafa marefu yaliyomilikiwa na kila upande ni ICBM(Intercontinental Ballistic Missile); misaili lenye kulenga shabaha zaidi ya kilomita 6,000; zaidi ya kutoka Moscow hadi Washington.
     Misaili nyingine ni SLBM (Submarine Launched Ballistic Missile), MIRV (Multiple Independently Targetable Re-entry Vehicle), gari linaloruhusu misaili kubeba zaidi ya kichwa kimoja cha silaha na kupiga shabaha tofauti bila kukosa.
     Baadhi ya watu wanahoji: Kama Marekani wana nia njema ya kuiokoa dunia na maangamizi; kwa nini wameshindwa kusaini mkataba wa Kyoto unaozuia uzalishaji wa gesi za sumu angani zinazoleta ongezeko la joto? Je, Ongezeko la gesi za sumu na joto duniani, si kitisho zaidi ya Nyuklia?
    Matukio ya Septemba 11 mwaka 2001 yameifanya Marekani kuchanganyikiwa na kuwa wababe zaidi ili kuyakandamiza mataifa ya Kiarabu, ili kujilinda zaidi dhidi.
    Jengo la WTC lilipobomolewa kwa mara nyingine mwaka 2001, liliwaonyesha Wamarekani jinsi ya kuwa makini zaidi na adui zao Waarabu.
Vifusi vya WTC ni mnara wa kumbukumbu ya kipigo cha magaidi. Ukiupima udongo wote wa kifusi cha WTC hutakosa tani milioni 1.2, na kifusi chote kimejaa eneo la ekari 10.
    Inakisiwa,  mpango wa mashambulizi ya Sepotemba 11 umegharimu kati ya Dola za Marekani 200,000 na 500,000; na kwamba uchumi wa New York uliathiriwa kwa zaidi ya Dola bilioni 100.
   Rais Robert Mugabe na Bush, mwaka 2007 walifafanua jinsi gani fujo za ‘vichaa’ kama akina Bush na Mugabe  wanapojaribu kutafuta amani ya dunia  kwa kupandisha mizuka!
    Alhamisi, Septemba 27 mwaka 2007, Mugabe alisema kitu kinachosaidia kujibu maswali ya wasomaji wengi wa Rai juu ya unafiki wa wakuu wa dunia hii.

    ‘RG’ MUGABE AMEBAKI  ILI KUWATOA KAMASI MAREKANI
    Akihutubia kwa ukali Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa(UN), Mugabe alisema Bush ni ‘mnafiki mwandamizi’ anayejidai kuheshimu Haki za Binadamu, kumbe vitanga vya mikono yake vimelowa damu za watu, hususan katika viambaza vya Guantanamo Bay!
Na Abu Ghraib.
       “Vitanga vya mikono(ya Bush)  vilikuwa vinachuruzika damu ya wasio na hatia wa mataifa mengi”, Mugabe alisema katika hotuba kali katika mkutano huo wa 62 wa Umoja wa Mataifa,”Anajidai kuwa Mkuu wetu katika Haki za Binadamu?”
   Mugabe(89) ambaye amezeeka,nchi imemshinda lakini hadi sasa akina Tsivangirai si mbadala wake, alihoji siku hiyo hiyo Bush alipozizodoa Belarus, Syria, Iran na Korea Kaskazini kama ‘Mataifa katili zaidi’ duniani.
    Akiizungumzia Zimbabwe, Bush alisema inaongozwa na ‘JAHILI’ Mugabe, anayewararua watu wake mwenyewe.
                Zimbabwe leo inakumbwa na kimbunga kikali cha uchumi mbaya.
Mfumuko wa bei unafika asilimia 7,000 na utafika asilimia 10,000 kabla ya Krisimasi. Fedha zinafika mwisho wa matumizi(expiration) utadhani unga wa ngano ama dawa ya mswaki. Mugabe anawatupia lawama Wazungu kwa hujuma anuwai.
Hata hivyo Zimbabwe sasa hutumia dola za Marekani badala ya dola ya Zimbabwe!
     Lakini, mwaka 2007 akamchambua Bush (kama karanga) na kusema ni mnafiki wa hali ya juu!
    Mugabe, pia amewahi kuwatwanga virungu wapinzani wake, akiwamo Morgan Tsivangirai wa MDC.Tsivangirai sasa kashindwa, analalama kuwa kaibiwa kura!
   Lakini, alisema Bush anatesa watu Abu Ghraibu nchini Irak na katika jela za kijeshi  nchini Cuba, mahali walipowatuhumiwa wa al-Qaeda!
Ilikuwa safi hiyo?
    “Katika kambi hizo za mateso”, alisema Mugabe, “Hakuna sheria na hata zile za kimataifa hazina nguvu. Marekani wanawajibika kuandika upya Tangazo la Haki za Binadamu…hata Septemba 11(2001) Wamarekani ni wakosaji”, alisema Mugabe.
    Mugabe alimkosoa Bush kwa kuwakamata watuhumiwa na kuwafunga bila kuwafikisha mahakamani. Mugabe anamuunganisha Bush na rafikiye, Tony Blair(Waziri mkuu mstaafu wa Ui8ngereza) kama watu walioiburuza sana dunia, hususan Umoja wa Mataifa. Baada ya kuharibu Irak sasa wanaacha jukumu kwa Umoja wa Mataifa kulinda amani na kuponya kidonda!
   “Mwenyezi Bush(alimkejeli kujilinganisha na Mungu) sasa karejea Umoja wa Mataifa kusaka msaada wa wokovu…kwa sababu, pua  yake inavuja damu zisizo na hatia…bado anajitutumua kutuhadithia madhila ya ukatili”, Mugabe alisema.
     Naam, hivi ni vituko vya vichaa katika Ulimwengu majununi(Crazy People in a Crazy World), Mugabe na Bush kumwagiana shombo katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kusaka amani! Mkuki kwa nguruwe sijui nyani dume haoni kundule? Alamsiki.
   0713 324 074
                       



No comments:

Post a Comment