Aprili, mwaka 2009, ni mwezi
ambao kulitokea vitu vingi adhimu sana, na vya kukumbukwa sana hapa
nchini.
Safari ya mwana wa Dikteta wa zamani wa Uganda , Jaffar Amin(47)
aliyesafiri kutoka Uganda hadi Mwitongo, Butiama, mkoani Mara.
Idhaa ya
Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, iliratibu safari
hiyo ya Jaffar, ambaye ni mtoto wa nne, kati ya watoto takriban 60 wa
Amin.
Jaffar alikutana na mtoto wa Pili wa
Mwalimu, Madaraka Nyerere.
Ziara ya Jaffar
huko Mwitongo, Butiama katika mwezi huo wa Aprili, mwaka 2009,
inatukumbusha miaka 34 kamili baada ya kuanguka kwa utawala wa baba yake
huko Uganda , Aprili 11 mwaka 1979.
Amin Dada,
alitimuliwa na majeshi ya Tanzania mwishoni mwa vile vita vya Kagera;
akatimkia Sudan, Libya kisha Saudi Arabia, alikofariki dunia mnamo Agosti
16 mwaka 2003.
Naam. Ziara ya
Jaffar Amin huko Mwitongo, Butiama mkoani Mara, ilikuja wakati wa
Kumbukumbu ya 87 ya kuzaliwa kwa Mwalimu mahali hapo.
Nyerere alizaliwa Aprili 13 mwaka 1922.
Tena, Jaffar
amekuja Tanzania wakati hayati Mwalimu alipojadiliwa sana katika lile
Tamasha lake lililowaleta nchini wasomi na wanazuoni maarufu Afrika; kama
Prof. Wole Soyinka wa Nigeria .
Tumjadili kidiogo
Jaffar Amin, ambaye leo ni kiongozi wa familia ya Marehemu baba yake, Idi
Amin Dada, mtawala wa zamani wa Uganda (1971-79).
Mwaka 2005,
alikwenda Akokoro, ili kuhudhuria mazishi ya Dk. Apollo Milton Obote.
Amin ndiye aliyempindua Obote mwaka 1971 alipokuwa nchini Singapore
akihudhuria Mkutano wa Jumuiya ya Madola(Commonwealth); Obote akakimbilia
Tanzania .
Kitendo cha
Jaffar kuhudhuria mazishi ya Dk. Milton Obote, hasimu mkubwa wa baba
yake, kilivuta hisia za watu wengi, hata kuona msamaha na
maridhiano miongoni wa Waganda na Waafrika wengine wa zama zetu hizi.
Jaffar Amin, ni somo kwa
Waafrika wote zama hizi, kusameheana na kuacha chuki na vita visivyo na
sababu, wakatiti sisi Waafrika ni ndugu wamoja.
Jaffar, alipowapa pole
familia ya Obote katika msiba huo, akageuza upya historia na kuanza kumuumba
upya babaye, Dikteta wa zamani wa Uganda, aliyejibandika vyeo
lukuki kama, Field Marshal, Mshindi wa Dola ya Kiingereza,
Mwanamasumbwi Nguli Duniani, Bingwa wa Kuogelea na mwenye Medali za
kutukuka sana kama Victoria Cross n.k!
Jaffar, anapofika
Butiama kuzungumza na Madaraka Nyerere kwa msaada wa Mkuu wa Idhaa ya
Kiswahili ya BBC, Bwana Solomon Mugela, anawaondoa Watanzania katika
lindi la fikra hasi za kumtazama Amin kama ‘Joka Kuu’ la kale la Uganda,
Nduli, muuaji, mla nyama za watu, hususan adui zake wa kisiasa.
Nazungumza umuhimu wa
toba na msamaha kwa sisi Waafrika, yaani kuachana na uhasama ili kutafuta
umoja na mshikamano kisha maendeleo yetu na wanetu.
Amin, alishatengenezewa
filamu tatu zenye kuonyesha enzi ama zama za utawala wake wa kikatili na
kimabavu sana kulinganisha na ugaidi wa siku hizi.
Sauti ya
Nyikani hupenda sana kuzitazama zifuatazo:
The Rise and Fall of Idi Amin
Dada, na ile ya Forest Whitaker, iitwayo, The Last King of Scotland.
Katika sinema hizo,
Amin huonyeshwa kama mtawala katili sana , pumbavu, zuzu, mpenda anasa
na mpenda wanawake, anayetawala nchi kwa hofu na vitisho karibia
kumuua kila anayemuota ndotoni, akimpinga, akimsaliti hata kumchukulia
mmoja wa wakeze.
Filamu nyingine
iitwayo, 90 Minutes at Entebbe au The Entebbe Raid, inatukumbusha Uganda
ilivyoanza kuvunjika vipande, baada ya Bwanamkubwa Amin kuvuruga uhusiano
wa kidiplomasia na Wazungu.
Amin, alijiweka
upande wa Waarabu hususan Wapalestina, magwiji wa medani za ugaidi wa
kuteka nyara ndege, kama hiyo ya Air France Air Bus, iliyokuwa
safarini kutoka Paris,Ufaransa, kwenda Israeli, ikatekwa na kupelekwa
Entebbe.
Naam, tunamjadili
kidogo Marehemu Idi Amin Dada na mwanaye, Jaffar Amin aliyefika Mwitongo,
Butiama mwaka jana, kuja kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu, miaka 30
baada ya Vita vya Kagera, vilivyomwondoa madarakani, Uganda, Marehemu
babaye, 'Joka Kuu' Nduli Amin, aliyelala mauti kaburini Saudi Arabia.
Nataka
kusema kwamba, namkumbuka Amin kwa ‘kuwachachafya’ vilivyo Wazunguna
magabacholi.
Naam, wakoloni ambao leo
hutetemekewa sana kwa kicho utadhani miungu; hupigiwa goti na kulambwa
dole gumba na watawala wetu waliojigeuza manyampala wa Wazungu.
Watawala wa
Afrika waliojaribu kuwapinga Wazungu ni Nelson Rolihlahla Mandela tu;
labda na “R.G” Mugabe na Kanali Muammar al-Qaddafi, tena kwa sababu
zao!
Nani leo atathubutu
kuwapinga wazungu?
Waama, filamu iitwayo, The Rise and Fall of Idi Amin Dada, inatukumbusha
baadhi ya vituko vya Amin ambavyo kwa kiasi kikubwa sana hushadidia
ukombozi wa mtu Mweusi dhidi ya Weupe.
Siku ile
Mkutano wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika(OAU kabla ya kuwa AU),
ulipofanyika mjini Kampala , Amin alibebwa na Wazungu katika machela,
alipokuwa akiingia kufungua mkutano!
Viongozi wenzake
waliokuwa tayari katika chumba cha mkutano wakashangaa kuona Amin
anaingia kwa staili ya kubebwa na Wazungu katika machela.
Kumbuka msomaji wa safu
hii, zama za Ukoloni ni Waafrika waliowabeba wakoloni wa Kizungu katika
machela.
Mwandishi, rafiki yangu,
Prudence Karugendo, aliyekuwa Kampala zama hizo, ananiambia kitendo hiki
hakijawahi kufanywa,bali propaganda za Magaharibi tu.
Pia, wakati
fulani, Amin alimhukumu kifo Mhadhiri wa Kiingereza, Dennis Hills , kwa
makosa ya kuwasumbua na kuwanyang’anya ardhi wanakijiji.
Jumuiya ya Kimataifa
ilipomzonga sana Amin ili kumwacha huru Bwana Hills, akasema kwamba
hadi kama Waziri Mkuu wa Uingereza, James Callaghan, angeruka
kutoka London hadi Kampala, kuja kupiga goti na kumwombea msamaha Hills,
ndipo angeondolewa kitanzi kilichomkabili!
Siku hizi, hapa
Afrika iko mahakama yenye uwezo wa kumuhukumu Mzungu hata
mwizi,gaidi, na mbakaji, bila kuuliza alikotoka,kama wamfunge jela au
wamwachilie 'Fasta'?
Hapa Tanzania, kasisi
mmoja wa Katoliki,toka Italia alibaka wanafunzi wa kidato cha tatu jijini
Mwanza, akafikishwa mahakamani na kuamuriwa kuondoka nchini, asije
akaswekwa 'mangenge' hapa,akanyea mtondoo wa Butimba!
Hiki ndicho
kilikuwa ‘kidume’ cha Bwana Mkubwa Amin dhidi ya Wazungu.Aliwatoa kamasi
Wazungu na Wahindi,bila kicho,kwa maslahi ya Waganda!
Amin, alikuwa na ubavu
wa kuwatoa kamasi Wazungu, bila kuwaogopa Malkia Elizabeth II, Waziri
Mkuu wa Uingereza,wala nani!
Aliwatimua Waasia 100,000
mwaka 1972, biashara zao walizoacha nyuma akawapa Waganda wa kawaida sana
, ili nao wapate kukabiliana na machungu ya maisha!
Walikuwa na hati za kusafiria
za Uingereza,wakati wanafanya biashara Kampala! Walihamisha utajiri wa
Uganda hadi Ulaya kwa utulivu mno, hadi Amin alipokuja kuwatolea uvivu.
Leo, hata
hapa Tanzania kuna Waasia wenye uraia na Hati za Kusafiria za Uingereza ,
Canada na Marekani, wanaofanya biashara za magendo, ya fedha chafu,
utapeli,ufisadi na wizi na uhujumu uchumi, bila kusahau ufisadi wa
EPA,rada kanyaboya ya BAE Systems, lakini viongozi wetu huwakodolea macho
pasipo kuwachukulia hatua kali, kama Bwana Mkubwa, Amin!
Namkumbuka Mhindi,
Shailesh Vithlani alivyoiingiza 'mjini' Tanzania kwa rada kanyaboya
kutoka BAE systems!
Rada ya fedha ndogo, wao
wakala 'cha juu' hadi zikafika Dola za Marekani 40,000!!
Nikipembua
uhalifu na unyama wa Amin, hasa aliofanya dhidi ya raia kwa kutumia
polisi wa siri waitwao, The State Research Bureau, nasisitiza wasomaji wa
safu hii adhimu na viongozi wazalendo wasiache kumuiga Amin kwa
vitendo vya kimapinduzi alivyofanya (hata kwa bahati) ili kuwakomboa
wanyonge.
Nazungumzia
vitendo vya kihalifu alivyokataa Amin, hata kama walifanya Waingereza.
Waingereza wanatupa
sisi Tanzania misaada.
Kila mwaka hiyo misaada
huongezeka.
Mwaka 2003/2004 iliongezeka
kutoka pauni milioni 80(sh. Bilioni 208) hadi pauni milioni 110(sh.
Bilioni286) mwaka 2006 na 2007.Asilimia 70 ya misaada ya Uingereza
huingia katika Bajeti ya serikali.
Ni kwa sababu
hii, mashirika ya misaada ya Uingereza na Bunge huwa na sauti kubwa sana
hapa kwetu hadi kuingilia ‘mambo ya jikoni’ kwa maslahi ya Uingereza.
Haya ndiyo Amin aliyokataa
enzi zake.Hata leo viongozi wetu wakimuiga Amin, kuna ubaya gani,na kwa
maslahi ya umma?
Nahitimisha safu
hii leo, kwa kuwakumbuka Waingereza vijana wawili:
Nigel David(23) na Brett
Richard(20) waliotiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka kisha kumuua msichana
kigori wa Kitanzania, Conjesta Ulikaye, mnamo Novemba 10, mwaka 2004.
Tukio hilo
lilitokea katika ufukwe wa Bahari ya Hindi, katika hoteli ya Silver
Sands, Dar es salaam .
Shauri la kesi ya
mauaji likashughulikiwa kwa siku 36 tu, Nigel na Brett wakafikishwa
mahakamani ‘Fasta’ Novemba 16; yaani siku sita tu baada ya tukio.
Vibaka wa hapa wanasota
rumande hata miezi sita bila upelelezi kukamilika!
Ndiyo maana kila siku hugoma
kushuka kwenye karandinga na kujipaka kinyesi, hadi serikali iwajali kama
inavyowanyenyekea Wazungu, naam na wenye cheo.
Kesi hiyo
ilifutwa Desemba 22 mwaka huohuo kwa mujibu wa kifungu 91(1) cha Sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985.
Safu hii, iliwahi
kumuuliza Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Geofrey Shaidi wakati huo(sasa
Jaji), Machi Mosi mwaka 2005 alipokuwa jijini Mwanza:
Hao
Waingereza wawili(walikuwa wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwa mapumzikoni
Dar, wakitokea vitani (Irak) waliachwa huru kwa maslahi ya umma wa
Tanzania, au maslahi ya Uingereza?
“Hawakuachwa huru kwa maslahi ya Uingereza au ya Tanzania …ushahidi uliokuwepo
haukutosha!
Wasingeendelea kung’ang’aniwa
bila ushahidi,” DPP Shaidi alisema.
“Hata hivyo,
kesi(dhidi ya raia) hazicheleweshwi na ofisi ya DPP, zinacheleweshwa
mahakamani, zinaposubiri kupangiwa tarehe ya kusikilizwa.
Hivyo, faili la Wazungu lilipofika
kwetu, tukalishughulikia(fasta?) kama kawaida”,
alifafanua DPP Shaidi
wakati huo, huku akikanusha madai kwamba Waingereza hao hawakuachwa huru
kwa sababu ya kuchelea kunyimwa misaada na Uingereza endapo wangehukumiwa
kutiwa kitanzi.
Laiti Nigel
David na Brett Richard wangefanya unyama wao huo wa kumbaka msichana kwa
zamu na kumsababishia kifo huko Uganda , enzi za Amin, bila shaka
wasingeepuka kitanzi!
Hata kama
Mawaziri Wakuu kama Margaret Thatcher, James Callaghan, Edward Health,
John Major, Tony Blair na Gordon Brown, na David Cameron kwa pamoja
wangemkoromea Amin, bila shaka Nigel na Brett wangenyongwa tu hapa hapa
Dar es salaam!
Unacheza na Amin?
Hata hivyo,
hongera BBC mwaka 2009, kutukumbusha mikasa ya lile Joka Kuu, “shujaa”
Nduli Idi Amin Dada!!
Ziara ya Jaffar
imetukumbusha kuyasema pia mazuri ya marehemu, wakati huu tunapoingia
mwaka mpya,ili tujirekebishe.
Tulizowea kumsema Amin kwa
mabaya tu.Kwa heshima ya Jaffar, shime tutazame upande wa pili wa
shilingi.
Baniani mbaya,kiatu
chake dawa, nikitazama viongozi wetu siku hizi wanavyowanyekea Wazungu na
kuingia mikataba mibovu na wageni, wakiwemo matapeli wa Kihindi, kama
Vithlani, nikikumbuka EPA,Dowans, Richmond na uchafu mwingi...namkumbuka
Nduli Idi Amin, kwamba ingekuwa zama zake, lazima angewatoa kamasi
hawa magabacholi.
Naam, kwa sababu
hiyo tu....nampenda 'Joka Kuu' Nduli Idi Amin Dada!!
Congesdaima@yahoo.com
0786/0754-324 074
|
No comments:
Post a Comment