ZAIDI ya
watu 10,260 waliacha kwenda kuchukua dawa za kufubaza makali ya Virusi vya
Ukimwi Mkoani hapa,tangu 2004 hata sasa.
Serikali ya
Tanzania leo,kwa kushirikiana na Tume ya Kikristo, The Christian Social Service
Commission(CSSC) na serikali ya Marekani,siku hizi wanatumia mabilioni ya Dola
za Marekani kuwarejesha wenye virusi vya Ukimwi hospitalini ili kupata tiba ya
kisayansi.
Mkakati huo
unaitwa, ‘Back to Treatment” na unalenga kuwarejesha watu 10,262 wa mkoa wa
Mwanza tu hospitalini.
Baadhi yao
waliacha tiba ya kisayansi, wakatimkia Samunge,Loliondo mwaka 2011 kwa Yule
‘Babu’ wa Kikombe cha Miujiza,kilichodaiwa kuponya magonjwa sugu,ukiwemo Ukimwi
kwa majuma matatu tu!
Ambilikile
Mwasapila,(78),Mchungaji Mstaafu wa KKKT, alikuwa ameota ndoto ikimwambia
aondoke Babati na kuhamia porini huko Samunge, ambako alianza kunywesha maelfu
ya watu kutoka Afrika Mashariki,Ulaya na Asia dawa ya miujiza kutoka kwenye mti
uitwao,Carisa Spinarum, ama ttuuite
Mrigariga!
Serikali
ikaanza kuishabikia dawa hiyo iliyouzwa kwa shilingi 500 tu kwa kikombe, maelfu
ya watu wakanywa, wakiwemo wasomi,maprofesa,wafanyabiashara na hata wakulima wa
kijijini.
Vigogo wa
serikalini walikuwa mstari wa mbele kuishabikia na kuibugia ili wapate tiba ya
kimiujiza-Cure in the Tanzanian Bush!
Aliyekuwa
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Abbas Kandolo(yuko Mbeya siku hizi) alipoulizwa na
Mwandishi huyu aliyefanya mkutano kamambe ofisini kwake kuratibu safari za kwa
‘Babu’ wa Loliondo,mwaka huo 2011, “Ni kwanini serikali inahaha kushiriki
ushirikina na miujiza ya uponyaji huko kwa Babu,Loliondo, kabla ya dawa hiyo
kuthibitishwana taasisi husika, Tropical Pesticides Research Institute, TFDA,
labda na TBS, akaniambia kwa hamaki!
“Sasa wewe
mtu layman (usiye na taaluma ya kitabibu) unawazidi maprofesa wanaoinywa dawa
ya Babu wa Loliondo?” akamtaja mkubwa mmoja.
Katika
mkutano huo wa Mkuu wa Mkoa na wafanyabiashara wenye mabasi ya kusafirisha watu
kwenda Loliondo, walikaribia kunimeza,kuona nilikuwa nikitaka kuwaharibia
biashara, wakati serikali ilishamkubali huyo ‘Babu wa Kikombe’ aliyeleta neema
kwa wenye mabasi mwaka 2011.
Carisa tree,
ni mti uliokuwa ukitajirisha si babu huyo tu, bali na wenye vyombo vya
usafirishaji na hata mama ntilie wa Samunge.Wagonjwa wengine waliopelekwa
wakiwa mahututi, walifariki dunia.
Leo,serikali
inameza machungu, inashirikiana na serikali ya Marekani na taasisi za dini
kufanya mkakati wa kuwarejesha wenye virusi vya Ukimwi kwenye tiba uitwao kwa
Kimombo, “Back To Treatment” kwa
mabilioni ya dola.
Mkakati huu,
BACK TO TREATMENT, ulizinduliwa rasmi jijini Mwanza Agosti Mosi mwaka huu kwa
mbwembwe, na watu wakalipana posho!
Akizungumza
katika uzinduzi huo uliofanywa katika Hospitali ya Sekou Toure, Mkurugenzi
Mkazi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa wa Tume hiyo ya Kikristo ya
Huduma za Jamii,Dk.Michelle Roland
akasema:
“Tangu 2003
serikali za Marekani na Jamhuri ya Muungano zimekuwa na ushirika kupambana na
Ukimwi unaoathiri watu wote Duniani,hususan Watanzania”,Dk. Michelle Roland
alisema.
Akabainisha
kuwa ubia huu umewafanya wananchi wa Marekani kuchanga jumla ya Dola za
Marekani bilioni 2.2 ambazo ni sawa na shilingi za Tanzania Trilioni 3.2.
Fedha hizi
ni kwa ajili ya kupambana na magonjwa sugu,ukiwemo Ukimwi.
Mkuu wa
Mkoa,Evarist Welle Ndikilo, akafungua mkakati huo, akisema Tanzania Bara sasa
kuna zaidi ya watu 430,000 wanaopewa dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi kupitia
Mpango huo wa Back to Treatment wa
hao Christian Social Service
Commission(CSSC).
Ndikilo,
akasema eti sasa Mkakati huo wa Back to Treatment utawarejesha wagonjwa kwenye
tiba na utaifanya Tanzania mahali pasipo na maambukizi ya Ukimwi-AIDS-free
Tanzania!
Labda,
asitokee Babu mwingine kama wa Loliondo,bibi ama shangazi!
Asilimia 25
ya wenye kuishi na virusi vya Ukimwi walikimbia vituo vya kutolea dawa za
Ukimwi, antiretroviral Therapy.
Wamekuwa
hawapati dawa hizo ili kuwawezesha kuishi na afya njema na kushiriki ujenzi wa
taifa.
Mama huyu wa
Kimarekani,Michelle Roland, akaonya kuwa endapo wenye kuishi na virusi vya
ukimwi hawatapata tiba sahihi,jamii nzima itaathiriwa vibaya,na maambukizi
yataongezeka maradufu, na virusi vitajenga usugu-hizi ni athari za akina Abbas
Kandoro kupigia debe Sangoma,kama Babu wa Loliondo!
Pia,Dk.Michelle
Roland amewataka wenye virusi vya Ukimwi kwenda hospitalini kupata tiba
sahihi,kando ya mfumuko wa vikombe vya babu na shangazi!
Akashauri
udhaifu uliopo katika mfumo wa tiba(zikiwemo imani potofu za viongozi ba
ushirikina) uepukwe,ili watu waishio na virusi vya Ukimwi warejeshwe kwenye
huduma za tiba na ushauri sahihi.
Dk. Michelle
akawataka watu kubadilika,na kuacha kushabikia uvumi na umizimu na masangoma.
Kampeni kama
hii iliwahi kuzinduliwa Iringa na Balozi wa zamani wa Marekani nchini,Alfonso
Lenhardt.Ilikuwa Septemba mwaka uliopita.
Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza,Evarist Ndikilo amesema Tanzania kuna watu 945,142 wanaoishi na
Virusi vya Ukimwi.
Kati ya hawa
530,118 ndiyo walioanzishiwa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi, watu 129,372
hapa Tanzania wamekimbia matibabu,wengine walitupa vidonge walipokunywa Kikombe
cha Babu!
Hadi Machi
mwaka huu watu 85,320 Mkoani Mwanza waliandikishwa kupata huduma,lakini ni
46,622 tu walioanzishiwa tiba.
Watu zaidi
ya 10,000 hawajulikani walikokwenda,hawa ni pamoja na watoto 1,600 hapa Mkoani
Mwanza.
Sasa tukiulize,hizo imani za kishirikina
zinazoshabikiwa na serikali na maofisa wake hata kukiuka sheria ilizoweka
yenyewe kuhusu tiba ndiyo nini,kama siyo kuitesa nchi?
Imani
potofu,ushirikina hata wa kuua Albino ili kushinda kura,kupata utajiri n.k
Wengine,watu
wakubwa walibugizwa dawa ya babu na kuwafanya maelfu kufuata mkumbo wakaacha
tiba sahihi.
Ndiyo maana
tukasema, Kikombe cha Babu kimeinywesha sumu Tanzania,sasa inatumia mabilioni
ya dola kurejesha wenye VVU hospitalini.
Hawa ni
wenye VVU tu, saratani,kisukari,magonjwa ya moyo n.k siku hizi hupelekwa kwa
sangoma kwa Baraka za akina Abbas Kandoro na serikali nzima!
0786 324 074
No comments:
Post a Comment