Monday, November 5, 2012

BURIANI KAMANDA BARLOW 4




INSPEKTA JENERALI WA POLISI(IJP) Said  A.Mwema, akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza,Oktoba 25 mwa huu, akasema wajibu wa raia na polisi kwa taifa letu.
Aliwakariri wanafalsafa juu ya wajibu wa kila mtu kuweka mbele  maslahi ya Taifa.Alizungumza wajibu wa Jeshi la polisi kushirikiana na wananchi katika kulinda Amani ya nchi yetu.
Tuijadili kidogo kauli ya Mwema kuhusu Rais wa 35 wa Marekani,John Fitzgerald maarufu sana kama “Mr. J.F” Kennedy(Democratic) ambaye aliishi kati ya Mei 29 mwaka 1917-Novemba 22,mwaka 1963.Alifariki kwa kupigwa risasi katika msafara wake huko Dallas,hiyo Novemba 22 mwaka 1963.
Uzalendo wa wajibu wa kwanza wa kila raia(hata polisi,JWTZ,Uhamiaji,Usalama wa Taifa n.k).Hata hivyo, wananchi tunamshauri IJP Mwema,atazame ikiwa polisi wake,wakiwemo wenye vitambi, wanao uzalendo kwa taifa,ama kama wanaweka mbele maslahi ya Taifa,au maslahi binafsi ambayo ndiyo uzalendo wa matumbo yao wenyewe.
Ni wazi, Tanzania kuna kitisho cha amani ,kwa sababu maadili yamepotea,na uzalendo wan chi na maslahi ya Taifa kama alivyosema Mwema,akimkariri JF Kennedy na Abrahm Lincoln,leo vinatupiliwa mbali.
Turejee Mwanza,katika matukio ya uhalifu yaliyowahi kufanyika Mwanza,polisi wa IGP Mwema wakiwepo,wakashindwa kuwatia mbaroni wahusika.
Aliyekuwa Mbunge wa Mwanza Mjini(baadaye majimbo haya yaliitwa Ilemela na Nyamagana),Marehemu Ali Shomari, alimwagiwa tindikali na mtu ambaye hatimaye “aliyeyuka” mikononi mwa dola.
Pia,mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato(TRA)alimwagiwa tindikali(corrosive acid) iliyomuunguza vibaya,akalazwa hospitalini.Mwanza ni mahali ukicheza unamwagiwa tindikali.Polisi wa Mwema,wapo wanabarizi upepo!
Hata siku za karibuni,baada ya mauaji ya Kamanda Barlow,yupo mwanasheria aliyepigwa risasi pajani na kulazwa hoi hospitalini Bugando.
Matendo haya na mengine mengi,huripotiwa polisi. Tatizo,umma huwa haujui na haujulishwi hatma ya mambo haya, na mustakabali wa kesi hizo huwa haujulikani.
Tunazungumza juu ya uzalendo na wajibu wa raia kuona FAHARI kwa nchi yetu Tanzania. Mke wa Rais Obama(naamini anashinda mhula wa pili)Michelle Obama, aliwahi kusema hivi:
“For the first time in my adult life time, I am really proud of my country”  akimaanisha kuionea fahari nchi yake katika maisha yake ya sasa ya utu uzima.
Naam, kama kila raia wa Tanzania atatekeleza wajibu wake,huu uzembe,kukosa uzalendo na mauaji ya kinyama sampuli hii,vitaondoka.
Tuitembee Mwanza kidogo. Mei 20 mwaka 2010, aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, ambalo sasa linakuwa Manispaambili, Leonard Bihondo(64) alitiwa mbaroni na polisi kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya aliyekuwa Katibu Kata wa CCM,Isamilo,Bahati Stephano.
Bihondo, alikamatwa uwanja wa ndege wa Mwanza, akitokea Dar es salaam,ambako alihudhuria mkutano wa ALAT,alituhumiwa kushirikiana na Jumanne Oscar(30),Abdul Ausi na Baltazar Shushi, ambao wote pia walitiwa mbaroni,na kesi yao ingali inasubiri kusikilizwa.
Oktoba 15,kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Lucas Omahe Garani, alijipenyeza katika ‘msitu’ wa walinzi wakiwemo polisi, Green guard na Usalama wa taifa, akavamia jukwaa ambako    Rais Jakaya Kikwete alikuwa,wakati huo akiwa mgombea wa CCM.
Ilikuwa Jumamosi, Alasiri,safu hii ilikuwepo uwanjuani hapo ikifuatilia kwa makini. Huyu Omahe Garani, alinyatia jukwaa akamfumania Kikwete na kuanza kumnyuka mieleka ili ambwage chini!
Kilichomfanya Kikwete asianguke chini,ni medani ya kijeshi,Kikwete alimudu kujitetea,baadaye Green Guard na polisi wakamtia mbaroni Garani na mwenzake Mzaki JAMAL,wakasokomezwa ndani ya karandinga la polisi,baada ya kukong’otwa sana na virungu vya Green Guard na polisi.
Walipelekwa gerezani Butimba. Matimbiko yaliyofanywa ili kumtawaza Kikwete kuwa ‘Chifu’ wa Wasukuma, eti yaliwaalika Omahe Garani(Mkurya wa Mara) na Mzaki Jamal(Muha wa Kigoma!)sijui walitaka kufanya nini! Wee Mwanza uione hivyo tu.
Kamanda wa polisi mkoani Mwanza,zama hizo,Zelothe Stephen, alisema polisi hawakupaswa kulaumiwa kwa tukio hilo,kwa kuwa hawakuhusishwa katika tukio hilo la kumtawaza Kikwete kuwa Chifu wa Wasukuma.
Chama cha Mapinduzi, kililaumiwa kwa kukumbatia sana imani za kishirikiana, hadi mgombea wake wa Urais akafanyiwa huduma ya tambiko bila vikosi vya usalama kuhusishwa.
Lucas Omahe GARANI na mwenzake Mzaki Jamal walifikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi, Ilvin Mgetta,kwa makosa ya kula njama na kumfanyia fujo Kikwete,jukwaani.
Waendesha mashitaka, Wilson Frank na Muna Paschal waliiambia mahakama kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo katika mkutano wa kampeni,Oktoba 15 mwaka 2005.
Kwa kifupi, washitakiwa walipatikana na hatia wakafungwa jumla ya miaka 10 kufuatia tukio hilo la kumfanyia fujo Kikwete ambaye alishinda uchaguzi baadaye na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
 Nakutembeza katika mitaa ya Mwanza,uone maajabu.Twende pamoja msomaji!
Desemba 4, mwaka 2009 saa 10  jioni.Edwin Miyaye(4) anatekwa nyara na Sospeter Nyanda(17) ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika sekondari ya Mnarani.Mwingine aliyeshirikiana na Sospeter kumteka mtoto huyu ni Daudi Madaraka(16) mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi,Bwiru. Mwanza kuna vituko!
Michael Joseph naye mwanafunzi wa shule ya msingi Bwiru naye alimteka mtoto huyo,walishirikiana na Getrude Rutabura(39).
Walimpomteka Edwin wakampigia simu babaye,Miyaye.Wakamwambia awalipe shilingi Milioni tano;la sivyo wangemuaa Edwin!Sospeter Nyanda, alijua namba ya simu ya Baba Edwin, alikuwa na nasaba naye.
Miyaye, alichelewa kuwapa wateka nyara hao sh. 5,000,000/= Alikwenda polisi ili wamsaidie kuokoa maisha ya mtoto, baada ya saa kupita, watekaji nyara wale walimfunga Edwin mawe makubwa shingoni na kiunoni,wakamtosa ndani ya vilindi vya maji ya Ziwa Victoria!!
Polisi waliwatia mbaroni Sospeter na wenzake kwa tuhuma za mauaji. Baada ya mahojiano na polisi(na virungu vya haja) walikubali kwenda kuonesha mahali walipomtosa Edwin.Micheal Joseph aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Bwiru ati alitoroka,hakukamatwa.
Edwin(4) alitoswa vilindini kwa sababu babaye,Miyaye alikosa sh.5,000,000 za kikombozi.Desemba 5,mwaka 20059 ndiyo siku maiti ya Edwin ilipoopolewa majini,Ziwa Victoria,ili kufanyiwa Postmortem na Daktari.Alikuwa kwa kuwa babaye alishindwa kulipa kikombozi-ransom!
Ilikuwa huzuni na majonzi. Edwin aliopolewa mbele za kamera za televisheni ya Star ya Jijini Mwanza.Maiti ya Edwin ilikuwa uchi wa mnyama! Naam,hii ndiyo Mwanza!
Desemba 6,mwaka huohuo wa 2009 Yohana Musa(25) muuza ndizi wa soko la Kirumba akiwa na mwenzake,Abuu walimteka nyara msichana,Judith John(29),Mhaya wa Bukoba,walimchinja mithili ya mbuzi.
Yohana na Judith walikuwa katika uhusiano wa kimahaba, sasa Judith akataka kumpiga chenga Yohana,ili achukuliwe na ‘mabuzi’ mengine yenye fedha. Unajua Krismasi ilikuwa ikijongea, na watu hutaka sana pesa wakati huo.
Sasa, Yohana akaazimu kulipa kisasi, yeye na wenzake wakazungumza na Abdallah Lucheme(70) aliyekuwa mganga wa kienyeji.Wakakubaliana kumchinja Judith na kumnyofoa viungo nyeti,kama shavu la kulia na nyeti zake ili wakafanyie matambiko ya pesa-ndagu!
Judith, alichinjwa majira ya saa sita usiku huko Songambele,Kirumba, walimchinja chumbani, wakatenganisha kichwa na kiwiliwili,chumbani kwa Yohana.
Kile kiwiliwili cha Judith kikafutikwa ndani ta gunia,wakakitelekeza kwenye pagala jirani na Mtaa wa Kiyungi.
Polisi walimtia mbaroni Yohana Musa(25) akiwa chumbani kwake akiuchapa usingizi.Walimtia pingu na baada ya dakika 40 hivi, akawaambia makachero wa polisi ni wapi kilipokuwa kichwa cha Judith.
Mganga wa kienyeji,Abdallah Lucheme(70) alitajwa na Yohana,akatiwa mbaroni na kufungwa pingu,akawapeleka korongoni ambamo kichwa cha Judith kilifichwa ndani ya mfuko mweusi wa Rambo, kichwa kilikuwa kimenyofolewa shavu la kulia. Jamani!
Walimchinja Judith baada ya kumfutika matambara kinywani,ili asiweze kupiga kelele humo chumbani kwa Yohana. Desemba 9,mwaka huo wa 2009 mwaka wa mauaji ya kishenzi-mwili wa Judith ukazikwa makaburini,Kitangiri.
Hii ndiyo Mwanza ambayo miaka mitatu baadaye,imechukua maisha ya Liberatus Lymo Barlow.
Hadi sasa watuhumiwa watano wa mauaji ya Kamanda Barlow wamepandishwa kizimbani, waliopandishwa kizimbani ni Muganyizi Michael Peter(36) Mhaya ambaye ni dereva,mkazi wa Nyakabungo,Mwanza,ambaye ndiye hasa anasadikiwa kumpiga risasi Barlow kwa bunduki, Shotgun-Greener.
Chacha Wekena Mwita(50)Mkurya ambaye ni mfanyabiashara wa Gongo la Mboto,Dar-Magige Mwita a.k.a ‘Tatoo’ yaani mzee ana umri wa miaka 48 naye ni Mkurya,mkulima eti wa mjini Bugarika,jijini Mwanza.
 Mwingine aliyepandishwa kizimbani  ni Bugazi Edward Buseta(22)Mhaya mfanyabiashara wa Tandika, Dar es salaam na Boke mwana wa Marwa Mwita(42) Mkurya na mfanyabiashara wa Mombasa-Ukonga,Dar.
Mbele ya Hakimu Mkazi,Angelo Lumisha, wakili wa serikali Castus Ndagambo, amesema washitakiwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji kinyume na sheria ya nchi kipengele cha 196 na 197 katika Penal Code Na 16.
Ndagambo, ameiambia mahakama kuwa washitakiwa hao watano kwa pamoja walimuua Kamanda Liberatus Lymo Barlow, Oktoba 13,mwaka huu  majira ya usiku huko Kitangiri,katika eneo la MINAZI MITATU,Wilaya ya Ilemela.
Washitakiwa wote watano kwa pamoja hawakutakiwa kusema lolote kufuatia mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.
Gwaride la utambulisho, IDENTIFICATION Parade lilifanywa, Dorothy,Yule mwanamama aliyekuwa na Barlow usiku wa mauti, akawatambua wote watano.
Walirejeshwa Butimba nyuma ya nondo hadi kesi yao hiyo JINAO NAMBA 30 ya mwaka 2012 itakapotajwa tena Novemba 15 mwaka huu.
Tukutane katika sehemu ya mwisho wa mkasa huu wa kusisimua

0713 324 o74



www

No comments:

Post a Comment