JAMII ya Jijini Mwanza ilisema kuwa “motive” ya mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa
Polisi,ACP Liberatus Barlow,ni wivu wa kimapenzi.
Kikosi
maalum cha upelelezi(TASK FORCE) kiliundwa ili kupeleleza mauaji haya ya
tashtiti.Kilihusisha makachero wa kimataifa,”Interpol”, na miongoni mwao
wataalam wa Kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,
Kabla ya
majuma mawili kwisha, tangu mauaji ya Barlow, Oktoba 13 mwaka huu,tayari watu
zaidi ya 10 walikuwa wamenaswa,wengine kwa mahojiano na wengine ndiyo hasa
waliomuua Barlow jijini Mwanza,wakajakutimkia Dar es Salaam.
Dorothy
Moses, ama Dorothy Lymo(42) ndiye mwanamama aliyekuwa na Kamanda Barlow(55)
dakika chache kabla ya mauaji ya kinyama kumkumba.Alipigwa kwa risasi ya
bunduki nzito, Shotgun, “Greener”shingoni,shingo likafumuliwa kabisa.
Felix
Felician(50) ama maarufu Jijini kama ‘Pepe’ alitiwa mbaroni kwa tuhuma kuwa
ndiye aliyekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Dorothy, ambaye ni mwalimu wa shule
ya msingi ya Nyamagana B,Jijini.
Ilihisiwa
kuwa, pengine mwanamama huyu mfuauji, alikuwa akigawanya penzi la tashtiti kwa
Marehemu Barlow na ‘Pepe’yumkini kiasi cha kuleta wivu na visasi.
Kufuatia
tuhuma hizo ambazo polisi wangali wakifanyia kazi kwa umakini, alikamatwa pia
Fumo Felician(46),mchezaji wa zamani na ‘striker’ mwenye mashuti makali katika
timu ya Pamba ya Jijini Mwanza na Dar es salaam Young Africans. Pepe ni nduguye
Fumo.
TASK FORCE
ya makachero wa polisi iliongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
nchini(DCI)Robert Manumba, iliwakamata pia Bahati Agostino na Waibe Maboto, kwa
sababu Barlow alipouawa huko Kitangiri usiku wa kuamkia Oktoba 13, majahili
wale walimpora redio ya upepo(Radio Call), na kasha walipora simu ya Dorothy.
Nataka
kusema kuwa,bado watu hawajajifunza kwamba sasa kuiba simu ya mtu,hususan
katika matukio ya ujambazi na mauaji namna hii ni kujiweka hatarini.
Nataka
kuandika hapa kwamba, hisia za watu kwamba kundi hili la majambazi lilikuwa na
watu werevu, ni uongo tu. Kama walitoweka na simu ya Dorothy wakaendelea
kuitumia hata kama walishanyofoa laini, hawa walikuwa majambazi waliojua
kufyatua risasi, na wala hawakujua chochote kuhusu teknolojia ya leo.
Hawa walivyo
mazuzu, eti walitupa laini ya Dorothy, wakaendelea kuitumia simu ile wao
wenyewe, ama mtu mwingine waliyemuuzia, huku wakijua simu ile ilisajiliwa na
hata namba ya simu iitwayo ‘IMEI’ ilisajiliwa?
Kulingana na
teknolojia ya siku hizi, ilikuwa rahisi kama nini kwa makachero wa ‘Interpol’
wenye utaalam wa hali ya juu katika ‘Information
Technology’ kuiona simu hiyo na kujua mahali ilipokuwa ikiitia hata kama
laini ya awali ilishanyofolewa na kutupwa.
Makachero
waliifuatilia simu hiyo na kufanya mtego mdogo tu,tayari aliyekuwa nayo akatiwa
mbaroni,ili akaeleze alikoipata na ilikuwa rahisi mno kuwasema waliompa au
mahali wenzake walipokuwa.
Hivyo,tusiwape
sifa majahili hawa kwamba walikuwa mauaji wa kimataifa, “Executioners’” kumbe
majangili tu, wanaomea Tanzania kwa sababu ya uzembe wa polisi wetu na tabia ya
jamii hii ya kufumbia macho watoto wao wahalifu.
Kwa kutumia
IT makachero waliwanasa akina Bonge(30) na Amos Waibe Maboto; walikamatwa
jijini Mwanza,kwa kutumia TEKNOHAMA.
Nataka kusema
kwamba, umefika wakati sasa kutumia kompyuta kuwanasa wahalifu,badala ya
kutumia mashushushu ambao wengine si waadilifu,nao hujiingiza katika usaliti na
kuwaumiza raia.
ALHAMISI,Oktoba
25 mwaka huu,Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai,Kamishna Mwandamizi wa
Polisi,Robert Manumba, akawaambia waandishi wa habari jijini Mwanza
kwamba,kundi la watu waliokamatwa jijini Mwanza likihusishwa na mauaji ya
Kamanda Barlow, hawa kuwa hasa wauaji.
Kwamba,
walishikiliwa na jeshi hilo na kuhojiwa kwa sababu katika medani ya
upelelezi,ni muhimu kama nini kuwahoji mashuhuda wengi,kama huyo Dorothy
Lymo,ambaye alikuwa na marehemu wakati wa tukio la mauaji na hata hao ‘jamaa’
zake, akina Pepe na Fumo na wengine.
Wakikutwa
hawana hatia,basi wataachwa huru.Ni muhimu polisi kuwahoji washukiwa wote na si
mara moja au mbili,ili wakupe mwelekeo wa upelelezi nap engine sababu za kifo
cha mtu kama huyo RPC Liberatus Barlow.
Kauli ya DCI
Robert Manumba,kwamba hawa waliotajwa wangali wanapelelezwa,hata kama uchunguzi
wa awali umebaini kuwa hawana uhusiano wa moja kwa maja na mauaji ya
Kamanda,inaondoa tu ‘Motive’ kwamba aliuliwa kwa wivu wa kimapenzi, lakini bado
tuhuma zingalipo dhidi yao.
Manumba,
aliwaambia waandishi wa habari Alhamisi,Oktoba 25 kwamba waliomuua Barlow ni
majambazi wazoefu(wa uhalifu,siyo weledi),na kwamba inawezekana lilikuwa tukio
la ‘nasibu’ na bahati mbaya hivi.
Kundi la
majahili saba, miongoni mwao watano: Muganyizi Michael Peter(36) mkazi wa
Isamilo,Mwanza,Chacha Mwita(50),Edward Bugazi Kusuta,Bhoke Marwa Mwita(42)nz
Magige Mwita Marwa, ambao wengine walikuwa wakazi wa Gongo la Mboto,Dar ndiyo
hasa walioshiriki katika mauaji.
Watu hawa,
majira ya saa nne hivi usiku, siku ya
tukio, walitangulia kupora mali za watu katika ‘grocery’ ya New Tuliza
Inn,Pasiansi, waliwateka wanywaji na kuwapora vitu na simu ya mama mmoja.
Usiku huo wa
Oktoba 12,Ijumaa saa sita hivi usiku walifika Kiseke katika baa iitwayo,Green
Corner, waliwapora wateja,walipora hata Konyagi,wakabugia.
Sasa, wakati
wanafika Kitangiri eneo lile la tukio,wakakutana na Barlow ambaye alikuwa
akimsindikiza Dorothy nyumbani kwake, akawamulika kwa taa za gari.
Dorothy,
anasema aliwaona wakiwa wamevalia vivazi vile vya Polisi Jamii ama Ulinzi
Shirikishi, sasa Kamanda Barlow akidhani ni hao walinzi wa kijamii, akawamulika
ili awaone vizuri.
Dorothy
akamwambia Barlow, “Unawamulika unawajua?” Basi, kuona hivyo hgao jamaa
wakamfuata Barlow haraka na kumzingira, wakaanza kufanya matata, Barlow
akachukua ‘Radio Call’ ili awaite polisi.
Muganyizi
Peter akamfatulia risasi ya Shotgun shingoni, ikamfumua shingo kabisa,
ilimvunjilia mbali shingo lake.
Walichukua
hiyo Radio Call ya Barlow na simu ya Dorothy,wakajitoma gizani.Keshoye,
wakajiondokea kwenda Dar es Salaam,bila shaka walishajua walimuua nani!
TASK FORCE ya
makachero wa polisi ya KIKOSI CHA KISASI
DHIDI YA MAUAJI YA BARLOW kiliwasili jijini Mwanza jioni Oktoba 13. Hata Inspekta
Jenerali wa Polisi, Said A. Mwema, mtikiso wa mauaji hayo ulimleta Mwanza siku
hiyo.
Makachero wa
polisi, wakiwamo hao wa kimataifa, Interpol waliwasili Mwanza, wakasambaa
Mara,Shinyanga,Mwanza, Geita,Bukoba na Dar es salaam, ili kufanya mtandao mkubwa
katika medani ya upelelezi.
IGP Mwema,
amewaambia wanahabari kuwa,waliomuua Barlow walikuwa saba, hao watano
wamekamatwa tayari na wengine wawili wananyatiwa bado, na kwamba hata kama
waende Uingereza watatiwa mbaroni na Interpol na watashushwa hapa nchini ili
wakabiliane na mashitaka,ili kuwa fundisho kwa wenzao. Hiki ndicho KISASI
alichosema Mwema, dhidi ya mauaji ya Barlow.
Nataka
kusema kwamba, kulingana na Mwema,makachero wa hiki KIKOSI MAALUM CHA KISASI,
walifanya kazi yao kabla ya siku 12 kwisha na kuwatia mbaroni wahusika, kama
wanavyofanya kazi Federal Bureau of
Investigation, Scotland Yard ama Military Intelligence 5(MI5)!
Majambazi hao
walikamatwa Dar,Gongo la Mboto,wakakutwa na silaha mbili,Shotgun hiyo
waliyotumia kumuua Barlow,ilikatwa kiatako na nyingine ni ‘Pump Action’.
Hadi Oktoba
25 redio ya upepo ya Barlow waliyopora eneo la tukio,ilikuwa bado
kukamatwa,ndiyo iliyochongea Barlow kuvunjwa shingo kwa Shotgun Greener
iliyofyatuliwa na huyo Muganyizi Peter,Mhaya kutoka Kagera!
Walipomuua
Barlow wakatorokea Dar es salaam ambako pia hawakulala,walipora mali za raia
hadi siku walipokamatwa. Nakwambia Jasiri haachi asili.
Kufuatia
maelezo ya IGP Mwema na DCI Manumba, nataka kutafakari mambo machache hapa.
Sina ubishi na kauli kuwa Barlow hakuuliwa kwa wivu na visasi vya kimapenzi.
Nataka
msomaji ajiulize maswali yafuatayo:
Mwanza,kuna
majambazi mwazoefu wenye bunduki kama Shotgun, wanatamba tangu saa nne tu za
usiku kuanzia Pasiansi,Lumala hadi Kiseke?
Polisi wa
doria wanakuwa wapi hadi baa ziporwe hata Konyagi na majambazi,hata waanze
kujipongeza,Kazi na Dawa, utadhani nchi haina mwenyewe?
Akina
Muganyizi, walipokamatwa eti walikutwa na simu nyingi walizopora wananchi, bila
shaka mchana kweupe!
Polisi
walikuwa wapi wakati vibaka, wezi na majambazi wanapotishia maisha ya watu na
mali zao?
Hivi Mwanza
nako kuna ‘Security Service’? Mbona raia wanatishiwa na vibaka na majambazi
ambao sasa hawana hofu tena na doria za polisi?
Niliandika
katika sehemu iliyotangulia kwamba, hapa Mwanza ndipo hakimu mmoja aliwahi
kumtorosha jambazi sugu kwa ‘removal order’, siku ya kesi RCO Goodluck Mongi,
akaambiwa na askari wake kwamba,mshitakiwa hakuwepo rumande!
Hapa
Mwanza,ndipo jamaa mmoja mwaka 2005, alijipenyeza katika msitu wa wana usalama
pale CCM Kirumba, akampiga mweleka Jakaya Kikwete wakati huo akiwa mgombea
mteule wa Chama cha Mapinduzi! Kesi hii ilifika mahakamani,jamaa akanyeshewa
mvua ya miaka jela.
Aliyekuwa
Mbunge wa Shinyanga Mjini, Leonard Derefa, aliwahi kusema Bungeni kwamba jeshi
la polisi livunjiliwe mbali,kwa kuwa lilishashindwa kulinda raia na mali
zao-limewaacha majambazi na vibaka kutamba!
Mimi sitaki
jeshi hili livunjwe,ili kuwe na “Vacuum” ama Ombwe ambalo linaweza kuleta kiama
zaidi ya hapa tulipo.
Nataka
kumwambia rafiki yangu Mwema ajiulize kama raia tunavyojiuliza: Kwanini Barlow
alikuwa peke yake usiku wa manane,bila ulinzi? Kwanini alitembelea gari la
kiraia tena lenye stika bandia ya Bima?
RPC hakuwa
na walinzi? Je,polisi wa Mwanza wanafanya nini kuwakamata vibaka hata
wanamiliki silaha na kumuua RPC? Polisi wanakamata wahalifu au wanafanya
biashara ya daladala mjini? Kwa nini polisi wawe na vitambi? Mbona hata Bill
Gates, Carlos Slim, Warren Buffett na wenzao hawana vitambi? Eti Polisi wa
Mwanza wana vitambi!!
Nataka
kumwambia IGP Said Mwema akumbuke kwamba, nilimuuliza katika mkutano na
waandishi wa habari kwamba, Barlow aliuawa Oktoba 13, ilipofika Oktoba 25
tayari majahili hao walikwishatiwa mbaroni-siku 12 tu za Operesheni ‘LIPA KISASI DHIDI YA MAUAJI YA
BARLOW’.
Nika mkazia
macho ya kidadisi IGP Mwema na kumbandika swali,
“Kwanini
kasi hiyo ya majuma mawili ya kuwakomesha majambazi waliomuua Barlow isitumike
pia kuwakomesha majahili wanao ua raia na kuwapora mali zao?”
Kwa nini
kasi hiyo, “Supersonic Speed” isitumike katika upelelezi wa kesi nyingine za
raia wa kawaida, wanaohujumiwa na majahili hawa na kuporwa mali na maisha?
Kwa nini
polisi wanashindwa kufikisha kesi hata ya vibaka mahakamani, eti upelelezi
haujakamilika? Kwanini kesi ya Barlow upelelezi ufanywe kwa kasi za viwango
kama zile za Samuel Sitta-Standard and Speed!
“Polisi na
raia wema lazima kuunganisha nguvu na talanta zao ili kuongeza ‘speed’ ya
kuwakomesha wahalifu,ili nchi iwe salama”, alinijibu IGP Mwema,pale ukumbi wa
Jini,Mwanza.
Said Mwema,
anatishwa na jamii kukosa uzalendo kwa Taifa letu, na kushindwa kutimiza wajibu
wa kizalendo kwa Taifa.
Oktoba
25,ndiyo siku nilipobaini kuwa Said A.Mwema, ni mwanafalsafa wa kiwango cha juu
sana.Alianza kueleza kauli za marais wa Marekani akina John Fitzgerald “J.F” Kennedy
na Abraham Lincoln, juu ya maslahi ya nchi kuwa kipaumbele cha kwanza,na
uzalendo kwanza kuliko matumbo. Siku hizi Tanzania raia na polisi ni wazalendo
wa matumbo yao!
Naam, Mwema
akauliza hivi, “Usiulize Tanzania itakufanyia nini,uliza utaifanyia nini
Tanzania?” Mwema amesema uzalendo unatoweka katika nchi yetu na maslahi ya
taifa yametupwa,ndiyo maana polisi na raia wameshindwa kuunganisha nguvu na
vipaji vyao ili kuwatoa kamasi majambazi!
Nitaichambua
hotuba ya IGP Mwema, juma lijalo , Itaendelea.
No comments:
Post a Comment