Tuesday, October 16, 2012

Siri za kifo cha Liberatus Barlow




IJUMAA,Oktoba 12 mwaka huu,yaani siku moja kabla ya mauaji ya kinyama dhidi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi, Liberatus Barlow(55), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi(SSP) Lily Matola, anawaambia waandishi wa Habari:
“Kesho Jumamosi(Oktoba 13) Kamanda,Liberatus Barlow) anataka kuzungumza nanyi kitu nyeti”, SSP Liliy Matola, anasema.
“Unajua, yeye anakawaida ya kushiriki Doria yeye binafsi bila kuhusisha askari; ana cha kuwaambia, baadhi yenu ana namba zenu za simu, atawajulisha muda wa kukutana naye,lakini ni kama saa tano hivi asubuhi”, anasema SSP Matola,Ofisa Mnadhimu wa Polisi(Staff One) Mwanza.
Asubuhi, siku ya Jumamosi, zikasikika habari kuwa Barlow alikuwa kauliwa na majambazi,katika eneo la jirani na Hoteli ya Tai Five, karibu na Kona ya Bwiru,Kitangiri,Jijini Mwanza.
Nilikutana na ACP Liberatus Barlow(55) mara ya mwisho Oktoba 19,siku ya Jumatano mwaka huu. Ilikuwa takriban saa 50 kabla ya mauti kumkumba.Alikuwa ndani ya sare zake za kipolisi na kofia kichwani.
Ilikuwa saa saba hivi mchana, akiwa nje ya jingo la ofisi yake.Alikuwa akiwaambia wanahabari juu ya tukio la kukamatwa vibaka watatu waliojaribu kupora maberamu ya mafuta katika matangi ya Kampuni ya ENGEN, Igogo,Jijini Mwanza.
Naam, Kamanda Barlow ameuawa na watu wanaosadikiwa majambazi,huko Kitangiri,jijini Mwanza,majira ya kati ya saa saba na saa nane za usiku, alipokuwa akitokea kumsindikiza Doroth Moses, ambaye ni Mwalimu katika shule ya Msingi ya Nyamagana B,mara baada ya kikao cha watu wa mkoa wa Kilimanjaro.
Baada ya kupata  habari za kifo cha Barlow, mara nakumbuka kauli ya SSP Lily Matola:
“Kesho, Jumamosi waandishi mje hapa ofisini Kamanda Barlow anawahitaji,atakuwa na jambo muhimu kuwapasheni habari wananchi”.SSP Lilian Matola, alikuwa akisema kwa utulivu mkubwa,kama ilivyo kawaida yake,huku akitoa tabasamu tamu la asali.
Sijui,Kamanda Barlow aliwaalika waandishi lufika ofisini kwake Jumamosi hiyo kufanya ‘coverage’ ya kitu gani? Labda, alitabiri kitakachomkuta?!
Sikufika ofisini kwa Kamanda asubuhi hiyo ya Jumamosi,kwa kuwa nilikuwa nikihudhuria Ibada, kanisani Kirumba.Napenda kumwabudu Mungu.
Mkurugenzi wa kituo cha televisheni cha Barmedas cha jijini Mwanza na Meneja wa Kituo, Charles Sokoro, walinigutua kusema kanisani hapo kwamba,Kamanda Barlow alikuwa kauliwa na majambazi usiku wa kuamkia hiyo Jumamosi!
Hili siyo tukio la kwanza la majambazi kuwaua maofisa wa ngazi za juu wa   Polisi jijini Mwanza. Jiji la Mwanza linao raia wema na pia wapo majambazi,mashetani hayawani na majahili waliozowea kupokonya maisha ya watu kwa kuwamwagia tindikali,kuwaua kwa risasi na sumu.
Julai 28,mwaka 2003, aliyekuwa Mkuu wa kituo kikuu cha Polisi Jijini Mwanza(OCD)Daniel Maburuki Mahende(45) alipigwa risasi kichwani na majambazi.
Ilikuwa majira ya saa 3 usiku, Mahende na askari wake wakijaribu kufuatilia majambazi waliotaka kupora huko Bugando, akajikuta katikati ya mvua ya risasi za rashasha za majahili hao,wakamuua.
Mrakibu Msaidizi wa Polisi(ASP) Mahende, alikuwa katika doria ya kuwakabili majahili hao wanaotishia amani ya raia na mali zao, ilisadikiwa walikuwa ageni kutoka Burundi,walitumia bunduki ya rashasha,SMG  kummaliza Mahende.
Wakati huo, SMG na risasi zake vilibadilidhwa katika magulio ya mkoani Kigoma kwa debe la mahindi au mtama, amini usiamini.
Taarifa kutoka Kigoma zilisema kwamba vita huko Burundi vilifanya silaha na risasi kuuzwa magulioni,na wanunuzi wakubwa walitajwa kutokea Jijini Mwanza.Aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wakati huo, Adadi Rajabu, hakusadiki taarifa hizo zilizotolewa na watu wa mkoa wa Kigoma katika semina moja katika Hoteli ya New Mwanza.
Kulitokea majibizano ya risasi kati ya majahili hao kutoka Burundi(walikuwa Mwanza baada ya kukaribishwa na wenyeji)kati yao na polisi, ASP Mahende akapigwa risasi ya kichwa na kufariki.
Polisi waliandaa mtego wa kuwanasa majahili hao baada ya kupata taarifa kwa raia wema,kama majira ya saa tatu hivi usiku.Polisi walimuua jambazi moja na kumpora SMG iliyosheheni risasi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wakati huo Daniel Ole Njoolay akatangaza kiama cha majambazi, kama sasa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini(DCI) Robert Manumba, anavyotangaza kiama cha majahili hao.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Zelothe Stephen, akatangaza vita dhidi ya majambazi na wahamiaji haramu jijini Mwanza. Mwanza,kuna   wahamiaji haramu,wengine  Wabembe nao hujiita Waha kutoka Kigoma,kumbe hutoka Congo-DRC.Wengine ni    Warundi nao hujiita Waha wa Kigoma, si ulisikia baadhi yao wakitimkia porini, walipogomea sense ya watu na makazi?
Wengine Wasomali, wanahonga-honga maofisa wa uhamiaji na polisi, na kusalia mjini kuendesha ukiranga wao. Nataka kusema kwamba, Mwanza ilishaingiliwa!
Wakati huo,matukio ya uharamia yalikuwa mengi Ziwani Victoria, wizi wa shilingi milioni 90 katika Benki ya NBC,Misungwi, shilingi bilioni 2 zilizporwa wakati huo CRDB Dar es salaam, mamilioni ya fedha,kama milioni 200 ziliporwa katika kiwanda cha bia, Pasiansi Jijini Mwanza na   cashier akafumuliwa kichwa kwa risasi. Kesi yake,bila shaka iliharibiwa baada ya ushahidi kukosekana kuwatia hatiani waliotuhumiwa!
Jijini Mwanza pia ziliporwa milioni 12 katika kiwanda cha samaki cha Omega,Ilemela,Jijini Mwanza.Wakati huo migodi mingi ilivamiwa,Geita,Nyamongo,mabasi yalitekwa Ngara, Geita,Kahama,Kibondo,Sirari n.k
Siku moja kabla ya kifo cha Hayati Liberatus Barlow, ambaye alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP),nilimuuliza SSP Lily Matola,wakati wa mkutano wa kawaida na wanahabari:
“Umesema leo(Ijumaa 12)hakuna taarifa za uhalifu mkoani Mwanza. Jambo hili lina weza kuwa na maana mbili tofauti: Kwamba,Polisi wanafanya kazi zao vizuri sana,hadi uhalifu na wahalifu wametokomezwa? Au, raia wema wamekosa kuliamini jeshi la polisi,hata wameshindwa kulisaidia kuwabaini wahalifu,na sasa majahili hao wameachwa watambe?”
SSP Lily Matola, akitabasamu tabasamu tamu kama asali, akanijibu hivi:
“Swali ni zuri na muhimu, ila hatuwakatishi tamaa raia wema wanaotaka kutoa taarifa za wahalifu,tunategemea taarifa za raia wema ili tushirikiane kutokomeza majambazi na wahalifu”, SSP Matola alisema.
 Ni ukweli usiofichika kwamba, Hayati Liberatus Barlow alikuwa mwiba mchungu kwa wahalifu, baadhi yao waliuliwa kwa risasi na polisi,na wengine ni ndege wa jela.
Barlow, alifika Mwanza takriban mwaka mmoja unusu uliopita. Ilikuwa baada ya ACP  Simon Nyankoro Sirro kuhamishiwa Dar es salaam,Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, anakoshikilia wajibu mtukufu.
Sirro, aliwahi kujipenyeza katika biashara haramu ya viungo vya binadamu,hususan walemavu wa ngozi, Albino, raia mmoja wa Kenya,Nathan Mtei(28) akajikuta akiishia mikononi mwa polisi,katika nyumba ya kulala wageni.
 Ilikuwa Agosti 15 mwaka 2010, Nathan Mtei alimhadaa Robinson Mkwana mlemavu wa ngozi naye raia wa Kenya,kuja jijini Mwanza,kwamba angemtafutia kazi ya utingo katika malori,kumbe kuuza viungo vyake.
Polisi walinasa mazunguzo yao na wafanyabiashara hao haramu, wakamhadaa Mtei ili amlete Mkwana akiwa mzima,ili wao ‘washughulike naye’. Walikubaliana kwamba Mtei angelipwa milioni 400. Basi Polisi wa Kamanda Sirro, wakamfuata Mkwana katika nyumba moja ya wageni, Nyakato,Jijini Mwanza walikofikia.
Nathan Mtei alipofungua mlango wa chumba walimofikia na albino Robinson Mkwana, polisi walijitoma ndani wakiwa na silaha mkononi!
Mtei alitekewa, akafungwa pingu.Albino, Robinson Mkwana akashangaa, polisi wakamwambia kwamba huyo Mtei hakuwa rafiki bali jambazi aliyetaka kumuua ili wamnyofoe viungo kwa milioni 400 ambazo polisi walifika nazo mahali hapo.
“Aliniambia tujenaye TZ angenitafutia kazi kwa Truck…”Robinson Mkwana alisema,wakati polisi walipowatia mbaroni.
Mauaji ya RPC,Barlow hapa jijini Mwanza ni kitisho kwa wananchi wa kawaida. “Sasa, kama RPC anauliwa namna hii, sisi raia wa kawaida tutapona?” mama mmoja anasikika akisema.
Mwanza ni miongoni mwa maeneo yenye kuwavutia wahalifu,ni mkoa ambao una rekodi ya juu ya kumiliki silaha kinyume cha sheria. Mikoa mingine ni Kigoma,Kagera,Geita,Arusha,Dar es salaam,Rukwa,Iringa na Mbeya.
Mwaka 2000 debe moja la mahindi ama mtama liliweza kubadilishwa kwa SMG ama debe la risasi katika magulio ama minada ya wananchi huko Kigoma.Wakati huo Tanzania ilikuwa na wakimbizi 500,000 ambao sasa wamerejeshwa kwao.Walikuja na bunduki.
Ukiacha Mwanza kuwa na watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, na wauaji wa albino na wafanya biashara hiyo haramu kutoka hata Kenya,Mwanza hamkani si shwari.
Niliwahi kumuuliza ACP  Simon Sirro, “Kwanini Mwanza,silaha zinazofanya uhalifu hazikamatwi?”
“Wanaficha hata Sirari au Nzega. Huwezi kuamini,tulimfuatilia jambazi mmoja tukamkamata akatupeleka Nzega ambako walikuwa wameficha SMG ardhini. Hiyo SMG ilikuwa ikitumika kufanya uhalifu Kanda nzima ya Ziwa”, alisema Simon Sirro Nyankoro.
Majangili wa Kisomali waliwahi kumuua OCD huko Ngorongoro, eneo ambalo sasa lipo mkoa wa Manyara.
 Mauaji ya Barlow, Mwanza yanazungumzwa kuhusishwa pengine na wivu wa kimapenzi,lakini walimu wa shule ya Nyamagana B wanakanusha Barlow kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwalimu mwenzao, Doroth Moses.
Doroth Moses, anashikiliwa na polisi kwa mahojiano, kwa kuwa ndiye mwanamke aliyekuwa akisindikizwa nyumbani kwake, usiku huo na Barlow. Doroth anaishi huko Kitangiri ambako ni eneo tukio la kumuua Kamanda Barlow lilitokea.
Mwili wa Barlow, uliagwa katika uwanja wa Nyamagana, Jumatatu iliyopita, ukasafirishwa kwa ndege hadi Dar es salaam ilikokuwa familia yake.
Tayari ACP Barlow amezikwa kwao mkoani Kilimanjaro, wakati Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(DCI)Robert Manumba, angali anaongoza Kikosi cha    makachero wa polisi,ili kuwabaini wahusika wa tukio hili la kinyama.
Makala hii itaendelea


No comments:

Post a Comment