JULAI 28,mwaka 2003, aliyekuwa Mkuu wa kituo kikuu cha Polisi (OCS) Jijini Mwanza, Daniel Maburuki Mahende(45)
aliuawa kwa risasi na majambazi,katika
eneo la Bugando,jijini Mwanza.
Serikali iliahidi kuwatia mbaroni wauaji hao, waliohisiwa
majambazi kutoka Burundi. Haikujulikana baadaye kwamba wauaji hao walichukuliwa
hatua gani na mahakama.
Mwanza,kumetokea matukio ya mauaji ya kinyama sana.Lakini umma
haukujulishwa hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika ili liwe fundisho kwa
wengine wenye tabia kama zao.
Katika makala yaliyotangulia, nikaeleza kwamba, aliwahi
kupigwa risasi ya kichwa ‘cashier’ wa Tanzania Breweries Limited(TBL),Pasiansi,
Jijini,zikaporwa zaidi ya shilingi milioni 200.
Baadaye,nilipomuuliza aliyekuwa Wakili wa Serikali
Mfawidhi,katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP)Kanda ya Ziwa, Anselm
Mwampoma, akaniambia:
“Kesi hiyo ya mauaji ya ofisa wa TBL,huko Pasiansi,haikuwa
na ushahidi wa kutosha kuwatia watuhumiwa hatiani”, alisema Mwampoma.
Tuseme, kesi hiyo “Ilivurugwa” ama ilichakachuliwa,hata
ushahidi uliokuwepo haukutosha hata kuwafikisha mahakamani washitakiwa. Hili
Mosi.
Pili, aliyewahi kuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mwanza,(RCO)
Goodluck Mongi, aliwahi kusema katika semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) kwamba wapo maofisa wa Mahakama Mwanza,
waliwahi kumtorosha mtuhumiwa wa ujambazi ,gerezani Butimba,kwa ‘removal order’ akatoweka rumande, na siku ya kesi
mahakamani mshitakiwa hakuonekana!
Yaani, wakati maofisa
wa polisi wakihaha kumfikisha mtuhumiwa wa ujambazi mahakamani, alishayeyuka
rumande!
Sipendi kusema kilichotokea, lakini msomaji unaweza kujua
inakuwaje mtuhumiwa wa ujambazi anapewa dhamana, kwa “removal order” ya Mheshimiwa Hakimu, pasipo hata polisi kujua?
Kuna matukio lukuki
ya ujambazi Mwanza,wizi,uhalifu,mauaji ya kutatanisha n.k Hata hivyo,
umma haujui kwa nini wahusika hawajakamatwa na kufikishwa mahakamani ili sheria
ichukue mkondo wake.
Hii ni HATARI!! Matukio ya karibuni sana ambayo hata Marehemu
Kamanda Liberatus Barlow aliyashuhudia,ni ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Gazeti la
Kasi Mpya, Richard Masatu, ambayo licha ya ripori ya daktari kuoneshwa kuwa
aliuawa, polisi waliendelea kusema aligongwa gari!
Kuna mauaji ya mmiliki wa nyumba moja ya wageni Jijini
Mwanza anayejulikana kwa jina la Manumbu, aliuliwa kwa risasi,lakini umma
haujafahamu kilichotokea, na wala hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio
hilo.
Kuna kawaida ya matukio ya mauaji kutokea Mwanza,lakini
sijui polisi wanashindwa kuwabaini wauaji ili wafikishwe mahakamani?
Kuna watu wanakufa katika mazingira ya kutatanisha,lakini
mwisho wa siku hakuna mtu anayekamatwa na polisi ili ashitakiwe mahakamani.
Mwanza,kuna historia
ya Mbunge mmoja, kumwagiwa tindikali,lakini ‘kesi iliyeyuka’ kwa njia
zisizofahamika,kufuatia mtuhumiwa kuyeyuka,kama walivyoyeyuka mashahidi wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa huko Kenya,zama za
NYAYO,Dk.Robert Ouko.
Aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Leonard Bihondo, alituhumiwa
kumuua aliyekuwa Katibu wa CCM wa Kata ya Isamilo, Bahati, alitiwa mbaroni na
kesi yake ingali ikisubiri kuanza kusikilizwa.
Jumatano, Oktoba 17,mwaka huu,nikaazimu kumuuliza Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini(DCI)Robert Manumba,kama alijua mauaji ya
Kamanda Barlow yalifuatiwa na mauaji ya watu wengine hapo Mwanza,lakini
haikufahamika hatma ya mauaji hayo?
Na kwamba, Je, polisi wamefikia hatua ya ku “compromise” na hali hiyo? Nilimkuta Robert
Manumba,mbele ya jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mwanza,nikamsalimia kasha nilipomgusia
jambo hilo akaniambia:
“Rafiki yangu,mimi ni mgeni hapa! Wenyeji mbona wapo ofisini
unaweza kuwauliza hata wakasema kuhusu kilichopo?’ Manumba aliniambia.
Nilicheka,kasha nikamuaga,maadam alikwisha pangua ‘ngumi’ za uso nilizotaka
kumtupia!
Nilimpata Mkuu wa Upelelezi (RCO)Mkoani Mwanza,Mrakibu
Mwandamizi wa Polisi(SSP)Joseph Konyo(siyo Joseph Kony wa Lord’s Resistance Army wa Uganda).Siku hiyo,
Oktoba 17,nikamwambia Joseph Konyo, juu ya migogoro Rwanda,Burundi na Jamhuri
ya Congo(DRC) ilivyosababisha wakati Fulani huko mkoani Kigoma bunduk,SMG,i
kuuzwa kwa kubadilishana na DEBE LA
MAHINDI au MTAMA!
Nilimuuliza Konyo, kama hakujua kwamba wakati Fulani wananchi
kutoka Kigoma walihudhuria semina moja ya Upunguzaji silaha, wakasema Mwanza ndilo lilikuwa soko kuu la silaha?
Na kwamba, polisi waliposhindwa kuchukua hatua sasa silaha
haramu zinapatikana mikononi mwa wahalifu hata kuweza kuua raia na hata maofisa
wa polisi kama Kamanda Liberatus Barlow?
“Nilikuwa Kigoma, wakati huo mwaka 2004,iliposemwa kwamba
bunduki moja ya SMG ilibadilishwa kwa debe la mtama au mahindi katika magulio.Haikuwa
na ushahidi kwamba wanunuzi wa silaha hizo walitokea Mwanza, hata hivyo polisi
lazima washirikiane na raia ili kutokomeza uhalifu”, Joseph Konyo alisema.
“Nawashauri raia wema wa Mwanza,wasiache kushirikiana na
polisi ili kusaidia kuondoa kitisho cha amani. Bila amani,hakuna
kitakachofanyika. Wasikate tamaa,raia wanapaswa kutoa taarifa hata katika ngazi
za juu za polisi,wanapaswa kutuamini kama wanataka tupambane na uhalifu na
kuushinda”, Konyo alisema.
Akasisitiza kuwa, kumkamata mtuhumiwa ni jambo moja,lakini
kumfikisha mahakamani na kuthibitisha kosa, ni jambo la pili linalohitaji
ushiriki wa raia wema kutoa ushahid, ili kuthibitisha kosa pasipo shaka yoyote.
Nikamkumbusha RCO,Konyo madai ya wananchi wa Mwanza,kwamba
wakitoa taarifa za uhalifu,mara wahalifu hukamatwa kasha kuachwa huru ambapo
kitendo cha raia kuwajulisha polisi wahalifu hugeuka jambo hatari kwa maisha
yao?
Siku tano baadaye, RCO,Joseph Konyo akafanya mkutano na
maofisa wa Polisi na kuwataka kushirikiana ipasavyo na wananchi katika vita
dhidi ya uhalifu nchini.
“Polisi tunapofuatilia uhalifu,tunapowajibika ipasavyo
katika matukio ya uhalifu,tukishirikiana na raia wema tutatokomeza uhalifu”,
Konyo alisikika akiwaambia maofisa wa Polisi.
Mkutano huo,ulihusisha maofisa wakaguzi wa polisi, maofisa
wa idara ya upelelezi na maofisa wa kawaida.
Kauli hiyo ya Konyo
imekuja siku chache baada ya kifo ca Barlow, ambaye pia ameuliwa katika
mazingira ya kutatanisha, ambayo raia wanadhani kulikuwa na uzembe na tabia ya
kuwalea wahalifu iliyojengwa muda mrefu hata kusababisha mazingira ya ‘Mdharau
Mwiba Guu likaota tende!”
Kufuatia hali hiyo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai Nchini,Robert Manumba, anasaidiana na makachero wa Polisi wa Kimataifa,
Interpol, kuwawinda majahili hao waliomuua Barlow,na inshallah, baada ya
kitambo watakuwa wametiwa mbaroni na kufikishwa mbele ya sheria.
Hadi sasa watu takriban 15 wamehojiwa na polisi,na watu
kadhaa wanashikiliwa kufuatia mauaji hayo ya kuamkoa Jumamosi,Oktoba 13, majira
ya saa 7-8 huko Kitangiri.
Mwanza ni mahali ambapo motto aliwahi kutekwa nyara,
watekanyara wakaomba wapewe mamilioni ya fedha ili wamwachie mtoto huyo.
Uliwahi kusikia hadithi za utekaji nyara na watekaji kuomba fedha nyingi za ‘kikombozi’?
Haili liliwahi
kutokea huko Bwiru,mtoto akatekwa nyara, wateka nyara wakaomba pesa, polisi
walipojaribu kumwokoa wakishirikiana na babaye, mtoto alitoswa Ziwa Victoria na
kufa!
Haya mambo ya Palestina, Ulaya na Afghanistan,yaliwahi
kutokea bwiru,Mwanza. Mwanza watu waliwahi kuteka msichana wa baa,wakachinja,
wakachukua kichwa,shavu la kulia wakanyofoa sehemu zake za siri,kasha kiwiliwili
kikasokomezwa kwenye sandarusi na kuachwa penye pagala!
Wauaji wengine walitoroka,polisi hawakuwahi kuwakamata na
kuwasweka hata rumande. Hapa Mwanza, ndipo mahali ambapo mwanamke anachinjwa
chumbani, hata majirani wakashindwa kujua hadi walipoalikwa na mainzi ya kijani
asubuhi,maiti akiwa ndani ya kiroba,katika pagala la mitaa ya Kiyungi!
Hapa ndipo jamaa mmoja wa Kenya alitaka kumuuza albino kwa
shilingi milioni 400,ikawa bahati polisi wakamnasa na kumwokoa albino aliyekuwa
hatarini kuchinjwa ili viungo vyake vikauzwe kwa watu wanaotaka utajiri kwa
kutumia ‘ndaku’ au bahati Fulani za
utajiri.
Huku ndiko albino
huwindwa kama wanyama,hata sasa wapo wanaoishi katika kambi maalum wasije
kuuliwa. Hapa ndipo vikongwe wanauliwa kwa tuhuma za ushirikina.
Hapa ni mahali ambapo wahalifu wana ‘confidence’ hata
walipomaliza kumuaa Kamanda Barlow, walitoroka na Radio Call na bastola
yake.Walivalia majazi ya polis Jamii.Waliyatoa wapi?
Hata hivyo, katika medani ya upelelezi,ni mapema mno kusema
nani alimuua Kamanda Barlow ambaye tayari amezikwa kwao Kilimanjaro.
Katika medani ya ukachero,siyo kila anayekutwa na kamba
shingoni akiwa amekufa,basi kajinyonga! Polisi wana kazi ya kuchuja
habari,kuzikagua na kugundua wahalifu wapya,kasha kutafuta ushahidi na kuutetea
mahakamani,ili kuithibitishia mahakama
pasipo shaka yoyote(beyond reasonable doubt) kwamba muuaji ni Fulani.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment