Polisi wanapowasaka
wauaji wa Musoma kwa bunduki,virungu na pingu,wanaharakati wafungue darasa la
uwajibibikaji na Haki za Binadamu
TOLEO nambari 852 la gazeti hili la Rai(Januari 21-27 mwaka
huu), niliandika katika Mraba huu kwamba, iko haja ya wanaharakati wa Haki za
Binadamu kwenda Musoma, kufundisha Haki za Binadamu.
Niliandika kwamba,
ukitembea Musoma na kusikiliza maoni ya baadhi ya watu, hutakosa kurejesha
fikra zako katika zama za mauaji ya kuangamiza(genocide)huko Rwanda , mwaka
1994.
Katika makala yenye
kichwa, “Musoma vijijini uzee ni baraka au laana?” nilifananisha uwezo wa
kufikiri wa baadhi ya wakazi wa huko na wauaji wa Jimbo la Darfur( Sudan ) ama huko Chad , Congo Mashariki, Somali n.k
Nilisema hapa
mrabani, kwamba maeneo niliyotaja yamesababisha vikao vingi mjini Geneva , Uswisi, kujadili
namna ya kuwaokoa watu katika maangamizi.
Geneva , ni makao makuu ya Mashirika ya
kutetea wakimbizi nay ale yanayoshughulikia Haki za Binadamu. Geneva ni kitovu cha kamati ya kimataifa ya
Shirika la Msalaba Mwekundu(ICRC).
Msalaba Mwekundu kazi yao ni kulinda na kuokoa maisha ya watu.
Kwamba, Tanzania
ni miongoni mwa nchi zilizoridhia Tangazo la Umoja wa Mataifa la Haki za
Binadamu, lililotolewa Desemba 10, mwaka 1948.
Kwamba, mikataba
ya Haki za Binadamu na ile ya Geneva (The Geneva
Conventions), kama ule wa mwaka 1949; hukataza
mauaji.
Hata mateka wa vita
wanalindwa na mikataba hii wasiuliwe kasha wapewe matibabu na huduma za kiafya
hata wawapo na majeraha ya risasi, wanapokuwa mikononi mwa adui zao vitani.
Kinyume cha harakati
zza mashirika ya Haki za Binadamu na Msalaba Mwekundu, katika kulinda na kuokoa
maisha ya watu, Musoma kuja ‘Janjaweed’ mithili ya wale wanamgambo wa Kiarabu
wa huko Sudan , wanaofyeka
watu kwa majambia makali sana .
Musoma kuna kila dalili za watu kuanza kulipizana visasi.
Sababu za watu kuwa
na majambia au mapanga, ni visasi kufuatia tuhuma za kijinga-jinga, kama uchawi, ulozi, usihiri, wizi wa mifugo na hata chuki
za kikabila. Ukitazama kwa maikini, utaona mfumo wa kutoa haki Musoma, mkoani
Mara, unaugua kiharusi.
Katika makala yangu
katika mraba huu, Januari 21 mwaka huu, nilitaraji serikali ingechukua hatua
haraka kupeleleza na kuyasaka makundi ya wauaji wenye mapanga(Jajaweed) ambao
hukodishwa na watu kwenda kutekeleza mauaji ya kinyama; naam mauaji ya kisasi.
Walemavu wa
ngozi(albino) pia huuawa na hawa hawa Janjaweed, wanapotumwa na wenye fedha,
kutaka kufanya matambiko yao
anuwai.
Mauaji ya kishenzi kama hayo ya Buhare, nje kidogo ya Manispaa ya Musoma, siku
chache zilizopita, bila shaka yamefanywa na Janjaweed.
Nataka nikwamnie
msomaji. Zamani kidogo, walilipwa fedha wauaji wenye pindi na mishale ya sumu.
Kwenda kuua mtu yeyote aliyetuhumiwa kuwa mchawi ama mwizi kwa minajiri ya
kulipa kisasi, mradi kulikuwa na aliyetangaza ‘zabuni’ hiyo kwa ujira wa pesa.
Musoma, kuna
‘Janjaweed’ wanaoendesha maisha yao
kwa kuua. Musoma kuna vikundi vya siri vya wauaji wa kukodishwa.Wamefuzu medani
za kuua na hata kuangamiza kizazi na koo(genocide) kwa mapanga makali na pinde
zenye mishale ya sumu kali.
Akina mama na kina
baba vikongwe wanaotuhumiwa kwa uchawi, wameuliwa wengi bila serikali kuchukua
hatua. Ulegevu wa serikali-polisi na mahakama- umewapa Janjaweed kupenya mkondo
wa sheria.
Nataka kusema kwamba,
polisi mkoani Mara ni wazembe; tena wazembe kuliko. Nachelea kusema ni wala
rushwa, wanaoharibu upelelezi wa kesi za namna hii, wanapokuwa wamepewa
chochote kitu, ama kama wamelipwa ng’ombe, kondoo, kuku, bata kama
siyo fedha taslim.
Amini usiamini,
vyombo vya kutoa haki(polisi na mahakama) mkoani Mara havitendi kazi yake sawa
sawa. Kwa sababu, wezi na wahalifu wengine hata wa mauaji, hukamatwa leo, kasha
wakaachwa huru kesho asubuhi.
Kisingizio, ni
kukosekana kwa ushahidi ama kushinda rufaa. Rufaa za Musoma husikilizwa wapi
usiku wa manane, kama siyo upenuni mwa vilabu
vya pombe za kienyeji, ama baa?
Mahakama gani hukaa
usiku, siku za siku kuu na mapumziko?
Musoma, mhalifu
akifungwa jela na mahakama ya Mwanzo Ijumaa jioni, keshoye Jumamosi ama
keshokutwa Jumapili, anarejea nyumbani,
kwamba kashinda rufaa!
Hayo ndiyo ya
Musoma, sasa wana ula wa chuya! Wahalifu
wanapoachiwa huru hurejea vijijini kwenda kutishia raia wema waliowasema polisi
au kutoa ushahidi mahakamani.
Musoma, ukatoe
ushahidi mahakamani, mhalifu afungwe
jela siku mbili, na kurejea nyumbani baada ya juma moja; hujipendi?! Utakatwa koromeo mchana kweupe.
Raia wema na waadilifu wamekatishwa tamaa na utendaji wa
vyombo vya dola.
Siku hizi watuhumiwa huuawa na wananchi wenye hasira kali. Hufuatwa hata makwao na kuuliwa
kinyama, wao, wake na ndugu na jamaa zao, nyumba huchomwa moto hata mchana
kweupe.
Hakuna kuwapeleka
watuhumiwa polisi au mahakamani, kwa madai kwamba watarejea kesho! Mahakama
zinaugua kiharusi;polisi wana mafua!
Kuna mahakama 15
tu za Mwanzo mkoani Mara. Mkoa mzima wa Mwanza una mahakama za Mwanzo
20.Mahakimu ni wachache, tunaambiwa kuna upungufu wa mahakimu wa mahakama za
Mwanzo 500 nchi nzima!
Hizi mahakama ambazo
ndizo huwahudumia wananchi wengi wa vijijini, zina mahakimu wachache sana . Hawana vitendea
kazi, kesi zimefurika.
Hakimu mmoja husafiri kutoka mahakama moja
kwenda nyingine; na huko kuna msongamano wa kesi nyingi tena za miaka mingi.
Nataka kusema kwamba,
ni nadra kupata haki vijijini kupitia mahakama za Mwanzo. Hata mahakama za
wilaya ndizo huwaachia wezi na wahalifu kwa rufaa zilizosikilizwa baa au
klabuni, siku zisizo za kazi.
Mfumo wa utoaji haki
mkoani Mara, una walakini.
Kama hauugui
kifaduro, una kiharusi kikali.Hakimu mmoja husafiri kutoka mahakama moja kwenda
nyingine, anaposhindwa, watendaji wa vijiji na kata ndiyo wanaowasomea
mashitaka washitakiwa.
Hawa, hawana hata
‘ABC’ ya sheria. Matokeo yake, dhamana huandamana na kitita cha noti. Bila
fedha hakuna dhamana hata kama ni haki ya
mshitakiwa kikatiba na kisheria.
Vituo vya polisi
vya vijijini mkoani Mara, vimegeuka kuwa mahakama, kwa sababu polisi hutoa
hukumu;hutoza faini vituoni.
Wauza gongo na bangi, wezi wa bata, kuku,ng’ombe
n.k huachiliwa vituo vya polisi mradi wawe na pesa za hongo na rushwa!
Kama
hujawahi kuona mtu akikaa mahabusu mwaka mzima, nenda katika mahabusu za Musoma
vijijini, ufanye kosa dogo kasha usiwape rushwa polisi, watendaji wa kata na
vijiji.
Hiki ni kichocheo
cha watu kuchukua sheria mkononi, ama kukodisha ‘Janjaweed’ ili wakawalipie
visasi, kwa kuwa polisi na mahakama walishashindwa kuwafunga jela wauaji, wezi,
majambazi, kwa kuwa wana pesa za rushwa.
Huko Musoma, ile
dhana ya Robert Darwin ya “Survival of The Fittest”(ya mwenye nguvu kuua
wanyonge bila kufanywa kitu) hutenda kazi. Huna kitu Musoma huna haki polisi,
ofisini kwa Mtendaji wa kijiji, wa kata hata mahakamani!
Musoma vijijini, kama huna fedha za kujaza mafuta katika pikipiki ama gari
la polisi, hakuna mtuhumiwa wako kukamatwa. Hata akikamatwa na kufikishwa
kituoni, huna fedha za kumlisha chakula au kumlipia nauli kwenda rumande mjini
Musoma, hawezi kupelekwa!
Mkoani Mara, ndipo
hakimu mmoja wa mahakama ya mwazo hukabiliwa na kesi nyingi, kwa sababu tarafa
nzima huwa na mahakama moja ama mbili. Tarafa inakuwa na takriban watu 600,000.
Kuna kesi ngapi? Kesi nyingi hazitolewi maamuzi kwa wakati; na wanasheria
wanamsemo kwamba, “Justice delayed is Justice denied”(haki iliyocheleweshwa ni
haki iliyopotea).
Kwa hiyo, Musoma
hakuna haki? Kwa sababu haki hucheleweshwa, haki imepotea. Katika mazingira
haya, wananchi wamekata tamaa, wanaamua kuwalipa ujira ‘Janjaweed’ ili
wakawalipie kisasi dhidi ya wahalifu,watuhumiwa wao ama wabaya wao hata kama ni
tuhuma za kijinga kama za kishirikina.
Mfumo wa kutoa haki
unaugua kiharusi mkoani Mara.Wizi wa mifugo unaendelea kwa sababu ukiwa na
fedha utakamatwa leo, kesho utaachwa huru, au utafungwa leo na mahakama ya
chini na kushinda rufaa usiku wa manane!
Wapo watu,
wanaposikia Musoma kuna mauaji ya kutisha, wanadhani kuna watu wakatili sana . Hapana! Haya ni
mauaji ya visasi kwa sababu mfumo wa sheria umeshindwa.
Si kila raia mwema huuliwa, ila ukituhumiwa.Mauaji
ya kinyama huandamana na visasi kwa sababu mfumo wa sheria unaugua kiharusi
kikali.
Mauaji ya juzi huko
Buhare, Musoma, ambako watu 17 wa ukoo mzima walifyekwa mapanga na kuchinjwa
mithili ya njiwa, ni matokeo ya kulipizana visasi, kwa sababu vyombo vya
dola(polisi, mahakama, mageteza na watendaji) walishashindwa kufanya kazi yao barabara.
Nazungumzia
uwajibikaji wa vyombo vya dola, na umuhimu wa viongozi wa vyama na serikali
kuhimiza watu kuishi kwa kufuata sheria za nchi-uadilifu.
Mauaji ya kulipa
visasi; naam kulipa baya kwa baya(tit-for-tat) hudhihirisha kwamba mfumo wa
kutoa haki Musoma unaugua kiharusi cha ubongo na kiwili wili.
Mahali haki inapopatikana
mahakamani, watu huridhika, amani hushamiri, maendeleo huja na kuna demokrasia.
Tabia ya kuchukua sheria mkononi(Mob justice) iliyoenea Musoma, ni kielelezo
kwamba raia hawataki tena kupeleka kesi zao mahakamani ama polisi, kwa sababu
wanadhani hakuna haki.
Siku hizi watuhumiwa
huuawa hata mbele ya polisi.Polisi wanapoaachia huru watuhumiwa, waelewe
wanasababisha mauaji ya visasi namna hii.
Niliandika mrabani
hapa Januari 21 mwaka huu kwamba, Musoma ndiko wanakofanya mikutano ya hadhara
kutafuta namna ya kuwadhibiti wachawi kwa kuwakata mapanga!
Ujinga umejaa
vichwani mwa viongozi wa vijiji, vitongoji, kata n.k hadi sheria na haki za
binadamu ni kitenda wili.
Haki za binadamu ni
lugha ya kawaida ya ubinadamu.Haki ingalipo Musoma lakini hutindika.
Nataka kusema
kwamba, Musoma hakuna ubinadamu, kwa sababu watu huongea lugha ya kuua kwa
kulipa visasi-ni kuwaondolea watuhumiwa haki ya kuishi, hata kabla ya
mahakama(chombo pekee cha kutoa haki nchini)kutoa hukumu.
Narejea wito wangu
kuwataka wanaharakati wa haki za binadamu kwenda Musoma mkoani Mara, kufundisha
haki za binadamu, haki za raia, itifaki ya Geneva , uwajibikaji serikalini na vyombo vya
dola, ili kukinusuru kizazi hicho na maangamizi!
Narejea kauli yangu
kusema kwamba, unahitajika mkakati mzito wa kuwanusuru watu hawa katika kitisho
cha uvuli wa mauti ya kuchunjana kama ng’ombe kwa mapanga utadhani Bosnia , Darfur , Rwanda ya mwaka 1994, Somalia
au Congo na Chad !!
0715-324 074
No comments:
Post a Comment