Monday, February 4, 2013

AFRIKA KIZMBANI 14

AFRIKA KIZIMBANI (14)
 
 
 CHARLES GHANKAY Taylor (62), Rais wa zamani wa Liberia aliyekuwa akikabiliwa na mashitaka  11 ya uhalifu wa kivita huko Sierra Leone,  na baadaye kufungwa miaka 50 jela,anatufundisha somo mahsusi.
 Kwamba,katika mahakama ya uhalifu wa kivita(ICC) mjini Hague, Uholanzi, Taylor amesemwa na mashahidi wa upande wa mashitaka kwamba alipokuwa Afrika Kusini wakati fulani, akatumia almasi alizokwiba  bega kwa bega na waasi wa RUF  huko Sierra Leone, kumhonga kidosho,mwanamitindo wa Kiingereza, Naomi Campbell.
 Unaona utajiri wa Afrika unavyotumika?
 Naam, Filamu iitwayo, ‘Blood diamond’ ya Jennifer Connelly, inatueleza kwamba, Charles Taylor, Marehemu Fodday ‘Poppay’ Sankoh na waasi wa Revolutionary United Front(RUF) waliiba almasi,wakabadilishana kwa silaha na Wazungu wa Ulaya na Afrika ya Kusini.
  Kumbuka msomaji, kulikuwa na mikataba ya Umoja wa Mataifa(UN) ya kutofanya biashara ya almasi za damu kutoka Sierra Leone.
 Hata hivyo, almasi hizi zilinunuliwa kwa magendo na kuingizwa Afrika ya Kusini, Zimbambwe kisha Ulaya na Mrekani.
 Kitendo hicho kilichochea sana vita hivi, wakati nia ya Mzungu ilikuwa kunufaika na utajiri wa Mafrika,potelea mbali Mwafrika huyu afe; aaangamie kwa risasi-The Shame of Poverty in Plentiful.
 Je, hujawahi kusikia kwamba hata Congo(DRC) vikosi vya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa(UN),wakati mwingine husahau jukumu la kulinda amani,na badala yake huanza kuiba madini,huku wakiacha kuwaokoa watu wanaouawa na wanawake kubakwa?
 Tangu kifo cha Laurent Desire Kabila katika Ikulu ya mjini Kinshasa, Januari 16,mwaka 2001,ukichungulia ndani ya uasi na uporaji wa rasilimali za ‘Bakongo’ kuna Mzungu.
 Hata ufisadi mithili ya ule wa kampuni ya Kiingereza, British Aerospace(BAE Systems) kutuuzia rada kanyaboya hapa,kwa Dola za Marekani milioni 40, kuna Mzungu anayeshiriki kutuumiza sisi tunapokosa shule, hospitali,maji, barabara na kwa ujumla maisha bora.
  Fedha za wizi: Hufichwa Jersey, Uingereza, Uswisi na katika mabenki ya Ulaya na Marekani, na hawasemi wizi huu.
 Joseph Mobutu aliiba dola za Marelani milioni sita akazificha Ulaya, hawakusema mpaka akatimkia uhamishoni, Morocco, kisha amefariki, wakazirejesha kwa familia yake.
 Mifano iko tele ya wizi. Uingereza iliwahi kutiliana saini mkataba na Misri mwaka 1929 eti sisi tusitumia maji ya Ziwa Nyanza linaoliwa Victoria kwa heshima ya Malkia wa Uingereza.
  Mkataba huu wa 1929 uliorejewa mwaka 1957 lengo lake lilikuwa kutuzuia kutumia maji ya Ziwa hili kwa miradi ya  kilimo cha umwagiliaji ili kujiokoa na kitisho cha njaa , kinachotukabili kila mwaka.
  Sasa tafakari: Kuna Ongezeko la Joto Duniani linalochangia mabadiliko ya  Tabianchi(Global Warming&Climate Change)ambalo chimbuko lake hasa ni Marekani,Ulaya,Uchina, Japan, Mashariki ya Kati n.k-nchi za viwanda.
  Wanamwaga sumu nyingi angani, sisi Afrika tunachangia ongezeko la joto kwa asilimia tatu tu,lakinimadhara makubwa, majanga ya asili tunapata sisi kuliko wao.
 Mifugo imekufa kwa ukame, mazao yamenyauka shambani, kwa kukosa mvua-hata zikinyesha ni mafuriko yanayozoa mazao,kubomoa nyumba na udongo kuporomoka kama huko Same.
  Umasikini wetu unachangiwa na harakati za Mzungu kutafuta utajiri.
 Sasa angalia, Uingereza kutiliana saini na Misri mkataba kwamba tusitumie maji ya Ziwa hilo kumwagilia mashamba yetu mwaka 1929 na 1957.
  Mwaka 1929 na 57 Tanzania,Kenya na Uganda tulikuwa bado kupata uhuru. Uingereza; hili ziwa Nyanza lilikuwa lao lini mpaka wawagawie Misri?
Mzungu anaona mali ya Mwafrika ni ya kugawa kama nyama mezani!
  Wakati mikataba hiyo inatupiga marufuku kumwagilia mashamba maji ya Ziwa Nyanza, ama kuyatumia maji hayo kama chanzo cha umeme(hydroelectric schemes), kama huko Owen Falls,Jinja,Uganda na miradi kama huo wa kupeleka maji Kahama, Shinyanga, hawa Misri wanamwagilia mashamba makubwa ya kama ekari 600,000 jangwani.
  Uhalali huo Uingereza iliutoa wapi?
   Kutoka mwaka 1929 hadi sasa-takriban karne nzima, Uingereza na Misri wametulipa Pauni bilioni ngapi kama gawio katika biashara hii, ili sisi tuache kumwagilia mashamba,tusivue samaki n.k tuwaachie wao maji yote?
 Kwanza,kuliita ziwa hili eti Victoria, ni kesi; ni wizi wa mchana,ni utapeli. Hizi ziwa linaitwa Nyanza, Inyanja, Nyanja, Lweru n.k kulingana na makabila yanayolizunguka.
 Huyo Victoria amekujaje hapa?
 Ziwa Nyanza lilianza lini kuwa mjukuu wa Malkia Victoria, hata alibandike jina la ukoo? Anayo hakimiliki? Waache ujanja.
  Mto Nile(mungu wa Wamisri, “Ra”) unaanzia mto Kagera,hukatisha ziwani humo na kutokea Owen Falls, ambako huanza safari ya kilomita takriban 7,000 hadi huko Bahari ya Mediterranean.
 Nchi za Bonde la Nile ni Uganda, Tanzania, Kenya, Congo,Rwanda,Burundi, Ethiopia,Eritrea na Sudan ,lakini nchi iliyowahi kusema maji ni mali yake!
  Sasa, Uingereza ilikuwa Mungu kumuuzia maji ya Ziwa letu “Faraoh” wa Misri mwaka 1929 na 1957?
  Bila maji haya,hakuna Misri-River Nile is the matter of life and death.
Maji ni yetu,mali yao (basi uwe) ni mto bila maji yatokayo nyumbani kwetu!
Hapo mpo? Bila sisi,hakuna Nile, hakuna Hosni Mubarak waka Wamisri; wajirekebishe!! Ebo! wanatukatazaje kumwagilia mpunga huko Shinyanga na Kahama ili kujinusuru na njaa, na kula mafuvu ya mbwa, wakati wao wanategemea mashamba yaliyomwagiliwa na maji ya mvua inayonyesha huku kwetu Aprili na  Mei na kufika kwao Julai na Agosti?
 Misri ji jangwa,hakina mvua. Sisi tunaambiwa tukome kumwagilia viazi huko Majita, Nassa na Bukoba eti maji yatiririke kwa usalama hadi Bwawa la Aswan, Bonde la Toska n.k
  Eti watu milioni 100 tunaozunguka Ziwa hili kubwa Afrika,tufe njaa,wao watu takriban 75 walime,wavune wapate kuishi.Wao watu,sisi tumbili?
 Misri, imekuwepo tangu mwaka 3,2000 BC ina kila kitu,ina mafuta,madini,samaki, mbona haijatugawia sehemu ya maji ya Suez Canal, tuvue samaki?
 Waache uchokozi kwa mikataba feki ya mwaka 1929 na 57 sisi hatukuwahi kuitwa kusaini mikataba hii ya kitapeli.
  Afrika inajua njama za Mzungu kutaka kupora rasilimali zetu. Ndiyo maana, siku za karibuni, tulimsikia aliyekuwa Mwenyekiti wa AU, Kanali Muammar AL- Qaddafi wa Libya, kabla ya mauti kumkumba, akitaka Waafrika tuungane na kuwa taifa moja, UNITED STATES OF AFRICA.
 Tatizo, naye Gaddafi kaona umuhimu wa Waarabu wa Kaskazini na Weusi wa Kusini mwa Jangwa la Sahara(Pan Afrcanism) baada ya kuwindwa na Wamarekani kwa madege ya kivita huko Benghazi na Tripoli Aprili 14 mwaka 1986.
 Shushushu wa Libya, Abdel Basseti Ali al- Meghri,akahukumiwa kifo Januari 31 mwaka 2001 kwa ugaidi.
 Gaddafi, alikuwa na ugomvi na Wazungu,Wamarekani, kwa sababu wanasema Desemba 21 mwaka 1988 ndege ya Marekani Pan American Airways(Pan Am) aina ya Boeing 747 ililipuliwa na kombora na magaidi wa Gaddafi huko katika anga ya Lockerbie, Scotland.
Huu ulikuwa uongo mkubwa,na waliokamatwa na kuhukumiwa kifo waliachwa huru,ikasemwa walionewa!
  Watu 270 walikufa,wakafa pia 11 waliokuwa ardhini-Gaddafi kakubali yaishe,akalipa fidia.
  Gaddafi  akataka kuwapendeza  na kuacha kuisema Marekani ama Ulaya vibaya. Waburgaria waliwachoma watoto mjini Cairo kwa sindano zenye UKIMWI,wakaachiwa,wakarejea mjini Sofia,Burgaria kama mashujaa. Nani wa kukemea wazungu?
 Mandela? Gaddafi?
Labda, ‘R.G’ Mugabe .Hata Dodoma tuna Uranium,lakini nani wa kuanzisha mradi wa nyuklia ili tupate umeme?
  Najadili sababu za Afrika kuwa bara tajiri lakini watu wake masikini-The shame of plenty in the midst of poverty!
  Waafrika bilioni moja katika ya  wakazi bilioni 6.9 wa dunia ndifo fukara zaidi wakati kuna kila kitu?
 Uchaguzi huru na haki kama huu wa kwetu ndiyo unailetea Afrika matatizo makubwa.
 Transparency International(TI) linasema Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ndiko kitovu cha ufisadi,wizi ndiko kuna nchi masikini zaidi, Highly or Heavily Indebted Poor Countries(HIPC) na sote tunafanya chaguzi za kidemokrasia!
 Huku twafa njaa,lakini akina Charles Taylor wanahonga almasi zetu kwa vimwana wa Uingereza, akina Naomi Campbell!!! Baadaye wanatiwa mbaroni na kufungwa ili kuwaziba midomo.
   0786 324 074
  
 
 
 
 
  
 
 
  
  
 
 

No comments:

Post a Comment