Monday, November 5, 2012

UNALIJUA JIJI LA MWANZA?


                                      TAHADHARI!!
 *Mwanza kuendelea kubugia  kinyesi na kemikali za sumu wasipodhibitiwa kwa sheria kali
 
WAZIRI WA ARDHI,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Kajumlo Tibaijuka, aliwahi kusema kwamba, Mwanza ni miongoni mwa miji iliyojengwa pasipokuzingatia sheria za makazi na ulinzi wa mazingira.
Jiji hili lilijengwa na Mjerumani, Emin Pasha,mwaka 1892,ili kuwa kituo cha ununuzi wa mazao ya biashara kama pamba,katika ukanda wa ziwa.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Daniel Ole Njoolay, Machi 5,mwaka 2004 wakati akizindua Mradi wa   Majitaka jijini Mwanza,alisema Jiji hili linaongoza kuwa na watu wengi wanaoishi katika eneo  eneo dogo(high population density),kiasi cha kuchafua mazingira,hususan vyanzo vya maji.
Jiji la Mwanza sasa hukadiriwa kuwa na wakazi takriban milioni moja, ambao kwa siku hunywa maji safi kiasi cha mita za ujazo 70,000.Wakazi wa Mwanza,kwa siku huzalisha maji taka,zaidi kinyesi,kiasi cha lita milioni 38.Asilimia  90 ya maji taka hurejea Ziwa Victoria bila kutibiwa.
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Majisafi na Taka Mwanza(MWAUWASA),Robert Masunya,katika mahojiano na safu hii juzi, anasema wakazi wa Mwanza kwa siku hunywa maji yenye ujazo wa lita milioni 70.
Hii ni sawa na kusema,kwa siku wakazi wa Jiji hili,ambao wao wenyewe huita,” The Rock City” hunywa kiasi cha mapipa 350,000 ya maji safi ya MWAUWASA. Maji taka wanayozalisha(kinyesi,uchafu na kemikali za sumu) ni sawa na mapipa 200,000 ambayo humwagwa ziwani kila siku.
Afisa Uhusiano wa MWAUWASA,Robert Nasunya, ameiambia safi hii kwamba,ifikapo mwaka 2020,uwezo wao ni kuzalisha maji safi na salama yenye viwango vya ubora wa kimataifa kufikia mita za ujazo 108,000 ambazo ni sawa na lita milioni 108, ama mapipa 549,000 kila siku.
MWAUWASA wana matangi matano yenye uwezo wa kuhifadhi maji yenye ujazo wa mita 27,000,sawa na lita milioni 27.
 Kutokana na ujenzi holela usiozingatia sheria za makazi,MWAUWASA wanapozalisha maji mengi hata kiwango kisichotumika(Idle Capacity),yapo maeneo ambayo hayapati maji ya bomba yaliyotibiwa na kusafishwa.
Maeneo hayo hayafikiwi na maji ya bomba; mengi yako katika miinuko mikali,vilimani,kwa sababu maji ya bomba hutiririka kwa ‘gravity’,hayapandi mlima mpaka yasukumwe kwa mashine kama pampu.
Maeneo ya vilimani(Mwanza huzungukwa na vilima,miamba na mawe)yasiyopata maji ni pamoja na Kabuhoro, Ibanda,na Mji Mwema.Mengine ni Sangabuye,Kayenze na Bugogwa.
Afisa Uhusiano wa MWAUWASA,Masunya anasema, wakati wakazi wa Mwanza wanakunywa maji safi lita 70 milioni kwa siku moja, na wakati uwezo wa MWAUWASA ni kuzalisha lita milioni 108 kwa siku moja, lita 30 milioni hubaki-hushindwa kuwafikia watu.
Masunya anasema, wakazi hawa wa Mwanza huzalisha lita milioni 40 za taka zikiwemo kemikali za majumbani, hospitalini,viwandani,madukani na hata kinyesi cha binadamu na mifugo.
Serikali na Jumuiya ya Ulaya(EU) wamejenga mfumo wa kusukuma maji taka kutoka lita 35 hadi lita 170 kwa sekunde.Maji haya taka husukumwa hadi katika mabwawa 10 yaliyoko Butuja,Ilemela ambako hutibiwa kabla ya kurejeshwa Ziwani Victoria.
Mradi huu ulifadhhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani(KfW) na ukakamilika Oktoba mwaka 2010.Una uwezo wa kukusanya majitaka ya kiwango cha  asilimia 15 tu ya wakazi wa Jiji linalokuwa kila siku. Ukiamka asubuhi,unakuta vijumba vimeota milimani,pasi na ruhusa ya Mipango miji!
Asilimia 9 ya wakazi wa  Jiji hili la miamba,ndiyo waliounganisha maji yao katika mfumo huu wa maji taka,nao hawazidi wateja 2,000. Hawa ndiyo kinyesi chao na kemikali zao husafishwa na kurejeshwa ziwani.
Nimezungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA,Anthony Sanga, Alhamisi iliyopita, akasema mfumo wa MWAUWASA wa kutibu maji taka,hufanya kazi chini ya kiwango,kwa sababu wakazi wa jiji wameshindwa kuunganisha makaro yao ya maji machafu kwenye mfumo huo wa kutibu maji taka.
Sanga, ananiambia kwamba sasa wameanzisha mpango wa kuwakopesha wananchi ili waunganishe maji taka yao kwenye mfumo wa maji taka.Wanachotakiwa kufanya ni kulipa sh.5,000/ tu,halafu watakatwa pole pole baada ya kuingia mkataba.
Mfumo huu wa maji taka ulijengwa na Sirling International ya Italia. Na kulingana na MWAUWASA,Mwanza kuna vyanzo vya maji safi katika eneo la Capri Point,Chakula Barafu na Luchelele, ambavyo vyote hutoa maji Ziwa Victoria linalochafuliwa kwa kinyesi kisichorejezwa(recycled) kwa kutibiwa Butuja.
Kuna mpango wa kuongeza chanzo kingine cha maji chenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 50,000 kwa siku ili kuondoa shida ya maji Kabuhoro,Ibanda na maeneo mengine wanakolazimika kunywa maji ya ziwani yasiyotibiwa na kupimwa kitaalam,ili kudhibiti uchafu na kiwango cha kemikali.
Kemikali zinaweza kuleta madhara ya afya kwa binadamu na wanyama.Ziwa Victoria liko kandoni mwa migodi ya dhahabu ambayo hutumia zebaki(mercury)kusafishia dhahabu,na kasha mvua zinaponyesha husomba zebaki hiyo hadi ziwani na kuua samaki,wanyama,binadamu kasha kuharibu mazingira.
Hata hivyo,licha ya MWAUWASA kuzalisha maji kwa kiwango cha ziada,Mwanza ni jiji ambalo wakazi wake hunywa maji ya chupa ya Uhai kutoka Dar es salaam, Kilimanjaro, wakati mwingine wanakunywa Rwenzori,kutoka Milima ya Rwenzori huko Uganda!
Yaani, bei ya lita moja ya maji ya kunywa Mwanza haina tofauti kubwa na bei ya lita ya petrol kutoka Arabuni,wakazi Ziwa tunalo hapa,lakini maji yamechafuliwa kwa kinyesi! Fika Mwaloni Kirumba,utajionea kinyesi majini,Ziwani…hii ndiyo Mwanza!
Sasa,Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA,Anthony Sanga, ananiambia labda sheria zitumike sasa kuwabana watu wanaotiririsha maji taka Ziwani, wanaokataa kuunganisha majitaka yao katika mfumo wa MWAUWASA,ili yakatibiwe Butuja.
Wakati wa mvua,watu hutapisha vyoo vyao na hufungulia makaro ya maji taka ambayo huingia ziwani. Kutiririsha kinyesi mitaroni Mwanza ni kitu cha kawaida. Halafu eti Mwanza ndilo jiji safi kuliko yote Tanzania!!
Zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa Mwanza,ambao huishi vilimani katika makazi yasiyopimwa,hhutiririsha kinyesi na kemikali ziwani. Maji ya ziwa yanapotumiwa pasipo kuchemshwa ni hatari.
Novemba, 22 mwaka 2005,aliyekuwa Mkemia Mkuu wa Serikali,  Dk.Ernest  Mashimba, alisema jijini Mwanza kuwa Sheria namba 3 ya mwaka 2003 ya Udhibiti wa Kemikali Viwandani na Majumbani,haizingatiwi na wakazi wa jiji hili.
Hayati,Dk. Mashimba alisema,Mwanza ni miongoni mwa maeneo ambayo kuna uvuvi haramu kwa kutumia kemikali za sumu.Wakati wavuvi wanapovua kwa kutumia sumu,humwaga kemikali hizo ziwani na kuhatarisha maisha ya viumbe.
Makopo ya sumu Mwanza hutupwa mitaroni na kuachwa kuingia ziwa Victoria,wakati sheria hii inawataka kuzika makopo hayo au kuyarejesha viwandani,yaharibiwe.
Kulingana na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa(WHO)asilimia kubwa ya watu wanaodhuriwa na sumu ni kama hawa wakazi wa Mwanza,ambao huacha hata sumu za kuulia wadudu kuingia ziwani.
Maradhi yanayoongoza kuwaua watu wengi Mwanza ni minyoo,kichocho,kuhara damu,safura,homa za matumbo na hata kipindupindu-hii ni kutokana na kunywa kinyesi hiki wanachorudisha ziwani; kuliko na chanzo chao cha maji.
Mwanza,watu hubugia kinyesi chao kwa hiari!!
Ili kunusuru hali hii,Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Anthony Sanga, anasema sheria zitumike kuwafanya wakazi wa Mwanza kuunganisha maji taka yao na mfumo rasmi wa maji taka wa MWAUWASA.
0713 324 074
 
 
 
 
 
 
 
 
 

BURIANI KAMANDA BARLOW 4




INSPEKTA JENERALI WA POLISI(IJP) Said  A.Mwema, akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza,Oktoba 25 mwa huu, akasema wajibu wa raia na polisi kwa taifa letu.
Aliwakariri wanafalsafa juu ya wajibu wa kila mtu kuweka mbele  maslahi ya Taifa.Alizungumza wajibu wa Jeshi la polisi kushirikiana na wananchi katika kulinda Amani ya nchi yetu.
Tuijadili kidogo kauli ya Mwema kuhusu Rais wa 35 wa Marekani,John Fitzgerald maarufu sana kama “Mr. J.F” Kennedy(Democratic) ambaye aliishi kati ya Mei 29 mwaka 1917-Novemba 22,mwaka 1963.Alifariki kwa kupigwa risasi katika msafara wake huko Dallas,hiyo Novemba 22 mwaka 1963.
Uzalendo wa wajibu wa kwanza wa kila raia(hata polisi,JWTZ,Uhamiaji,Usalama wa Taifa n.k).Hata hivyo, wananchi tunamshauri IJP Mwema,atazame ikiwa polisi wake,wakiwemo wenye vitambi, wanao uzalendo kwa taifa,ama kama wanaweka mbele maslahi ya Taifa,au maslahi binafsi ambayo ndiyo uzalendo wa matumbo yao wenyewe.
Ni wazi, Tanzania kuna kitisho cha amani ,kwa sababu maadili yamepotea,na uzalendo wan chi na maslahi ya Taifa kama alivyosema Mwema,akimkariri JF Kennedy na Abrahm Lincoln,leo vinatupiliwa mbali.
Turejee Mwanza,katika matukio ya uhalifu yaliyowahi kufanyika Mwanza,polisi wa IGP Mwema wakiwepo,wakashindwa kuwatia mbaroni wahusika.
Aliyekuwa Mbunge wa Mwanza Mjini(baadaye majimbo haya yaliitwa Ilemela na Nyamagana),Marehemu Ali Shomari, alimwagiwa tindikali na mtu ambaye hatimaye “aliyeyuka” mikononi mwa dola.
Pia,mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato(TRA)alimwagiwa tindikali(corrosive acid) iliyomuunguza vibaya,akalazwa hospitalini.Mwanza ni mahali ukicheza unamwagiwa tindikali.Polisi wa Mwema,wapo wanabarizi upepo!
Hata siku za karibuni,baada ya mauaji ya Kamanda Barlow,yupo mwanasheria aliyepigwa risasi pajani na kulazwa hoi hospitalini Bugando.
Matendo haya na mengine mengi,huripotiwa polisi. Tatizo,umma huwa haujui na haujulishwi hatma ya mambo haya, na mustakabali wa kesi hizo huwa haujulikani.
Tunazungumza juu ya uzalendo na wajibu wa raia kuona FAHARI kwa nchi yetu Tanzania. Mke wa Rais Obama(naamini anashinda mhula wa pili)Michelle Obama, aliwahi kusema hivi:
“For the first time in my adult life time, I am really proud of my country”  akimaanisha kuionea fahari nchi yake katika maisha yake ya sasa ya utu uzima.
Naam, kama kila raia wa Tanzania atatekeleza wajibu wake,huu uzembe,kukosa uzalendo na mauaji ya kinyama sampuli hii,vitaondoka.
Tuitembee Mwanza kidogo. Mei 20 mwaka 2010, aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, ambalo sasa linakuwa Manispaambili, Leonard Bihondo(64) alitiwa mbaroni na polisi kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya aliyekuwa Katibu Kata wa CCM,Isamilo,Bahati Stephano.
Bihondo, alikamatwa uwanja wa ndege wa Mwanza, akitokea Dar es salaam,ambako alihudhuria mkutano wa ALAT,alituhumiwa kushirikiana na Jumanne Oscar(30),Abdul Ausi na Baltazar Shushi, ambao wote pia walitiwa mbaroni,na kesi yao ingali inasubiri kusikilizwa.
Oktoba 15,kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Lucas Omahe Garani, alijipenyeza katika ‘msitu’ wa walinzi wakiwemo polisi, Green guard na Usalama wa taifa, akavamia jukwaa ambako    Rais Jakaya Kikwete alikuwa,wakati huo akiwa mgombea wa CCM.
Ilikuwa Jumamosi, Alasiri,safu hii ilikuwepo uwanjuani hapo ikifuatilia kwa makini. Huyu Omahe Garani, alinyatia jukwaa akamfumania Kikwete na kuanza kumnyuka mieleka ili ambwage chini!
Kilichomfanya Kikwete asianguke chini,ni medani ya kijeshi,Kikwete alimudu kujitetea,baadaye Green Guard na polisi wakamtia mbaroni Garani na mwenzake Mzaki JAMAL,wakasokomezwa ndani ya karandinga la polisi,baada ya kukong’otwa sana na virungu vya Green Guard na polisi.
Walipelekwa gerezani Butimba. Matimbiko yaliyofanywa ili kumtawaza Kikwete kuwa ‘Chifu’ wa Wasukuma, eti yaliwaalika Omahe Garani(Mkurya wa Mara) na Mzaki Jamal(Muha wa Kigoma!)sijui walitaka kufanya nini! Wee Mwanza uione hivyo tu.
Kamanda wa polisi mkoani Mwanza,zama hizo,Zelothe Stephen, alisema polisi hawakupaswa kulaumiwa kwa tukio hilo,kwa kuwa hawakuhusishwa katika tukio hilo la kumtawaza Kikwete kuwa Chifu wa Wasukuma.
Chama cha Mapinduzi, kililaumiwa kwa kukumbatia sana imani za kishirikiana, hadi mgombea wake wa Urais akafanyiwa huduma ya tambiko bila vikosi vya usalama kuhusishwa.
Lucas Omahe GARANI na mwenzake Mzaki Jamal walifikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi, Ilvin Mgetta,kwa makosa ya kula njama na kumfanyia fujo Kikwete,jukwaani.
Waendesha mashitaka, Wilson Frank na Muna Paschal waliiambia mahakama kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo katika mkutano wa kampeni,Oktoba 15 mwaka 2005.
Kwa kifupi, washitakiwa walipatikana na hatia wakafungwa jumla ya miaka 10 kufuatia tukio hilo la kumfanyia fujo Kikwete ambaye alishinda uchaguzi baadaye na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
 Nakutembeza katika mitaa ya Mwanza,uone maajabu.Twende pamoja msomaji!
Desemba 4, mwaka 2009 saa 10  jioni.Edwin Miyaye(4) anatekwa nyara na Sospeter Nyanda(17) ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika sekondari ya Mnarani.Mwingine aliyeshirikiana na Sospeter kumteka mtoto huyu ni Daudi Madaraka(16) mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi,Bwiru. Mwanza kuna vituko!
Michael Joseph naye mwanafunzi wa shule ya msingi Bwiru naye alimteka mtoto huyo,walishirikiana na Getrude Rutabura(39).
Walimpomteka Edwin wakampigia simu babaye,Miyaye.Wakamwambia awalipe shilingi Milioni tano;la sivyo wangemuaa Edwin!Sospeter Nyanda, alijua namba ya simu ya Baba Edwin, alikuwa na nasaba naye.
Miyaye, alichelewa kuwapa wateka nyara hao sh. 5,000,000/= Alikwenda polisi ili wamsaidie kuokoa maisha ya mtoto, baada ya saa kupita, watekaji nyara wale walimfunga Edwin mawe makubwa shingoni na kiunoni,wakamtosa ndani ya vilindi vya maji ya Ziwa Victoria!!
Polisi waliwatia mbaroni Sospeter na wenzake kwa tuhuma za mauaji. Baada ya mahojiano na polisi(na virungu vya haja) walikubali kwenda kuonesha mahali walipomtosa Edwin.Micheal Joseph aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Bwiru ati alitoroka,hakukamatwa.
Edwin(4) alitoswa vilindini kwa sababu babaye,Miyaye alikosa sh.5,000,000 za kikombozi.Desemba 5,mwaka 20059 ndiyo siku maiti ya Edwin ilipoopolewa majini,Ziwa Victoria,ili kufanyiwa Postmortem na Daktari.Alikuwa kwa kuwa babaye alishindwa kulipa kikombozi-ransom!
Ilikuwa huzuni na majonzi. Edwin aliopolewa mbele za kamera za televisheni ya Star ya Jijini Mwanza.Maiti ya Edwin ilikuwa uchi wa mnyama! Naam,hii ndiyo Mwanza!
Desemba 6,mwaka huohuo wa 2009 Yohana Musa(25) muuza ndizi wa soko la Kirumba akiwa na mwenzake,Abuu walimteka nyara msichana,Judith John(29),Mhaya wa Bukoba,walimchinja mithili ya mbuzi.
Yohana na Judith walikuwa katika uhusiano wa kimahaba, sasa Judith akataka kumpiga chenga Yohana,ili achukuliwe na ‘mabuzi’ mengine yenye fedha. Unajua Krismasi ilikuwa ikijongea, na watu hutaka sana pesa wakati huo.
Sasa, Yohana akaazimu kulipa kisasi, yeye na wenzake wakazungumza na Abdallah Lucheme(70) aliyekuwa mganga wa kienyeji.Wakakubaliana kumchinja Judith na kumnyofoa viungo nyeti,kama shavu la kulia na nyeti zake ili wakafanyie matambiko ya pesa-ndagu!
Judith, alichinjwa majira ya saa sita usiku huko Songambele,Kirumba, walimchinja chumbani, wakatenganisha kichwa na kiwiliwili,chumbani kwa Yohana.
Kile kiwiliwili cha Judith kikafutikwa ndani ta gunia,wakakitelekeza kwenye pagala jirani na Mtaa wa Kiyungi.
Polisi walimtia mbaroni Yohana Musa(25) akiwa chumbani kwake akiuchapa usingizi.Walimtia pingu na baada ya dakika 40 hivi, akawaambia makachero wa polisi ni wapi kilipokuwa kichwa cha Judith.
Mganga wa kienyeji,Abdallah Lucheme(70) alitajwa na Yohana,akatiwa mbaroni na kufungwa pingu,akawapeleka korongoni ambamo kichwa cha Judith kilifichwa ndani ya mfuko mweusi wa Rambo, kichwa kilikuwa kimenyofolewa shavu la kulia. Jamani!
Walimchinja Judith baada ya kumfutika matambara kinywani,ili asiweze kupiga kelele humo chumbani kwa Yohana. Desemba 9,mwaka huo wa 2009 mwaka wa mauaji ya kishenzi-mwili wa Judith ukazikwa makaburini,Kitangiri.
Hii ndiyo Mwanza ambayo miaka mitatu baadaye,imechukua maisha ya Liberatus Lymo Barlow.
Hadi sasa watuhumiwa watano wa mauaji ya Kamanda Barlow wamepandishwa kizimbani, waliopandishwa kizimbani ni Muganyizi Michael Peter(36) Mhaya ambaye ni dereva,mkazi wa Nyakabungo,Mwanza,ambaye ndiye hasa anasadikiwa kumpiga risasi Barlow kwa bunduki, Shotgun-Greener.
Chacha Wekena Mwita(50)Mkurya ambaye ni mfanyabiashara wa Gongo la Mboto,Dar-Magige Mwita a.k.a ‘Tatoo’ yaani mzee ana umri wa miaka 48 naye ni Mkurya,mkulima eti wa mjini Bugarika,jijini Mwanza.
 Mwingine aliyepandishwa kizimbani  ni Bugazi Edward Buseta(22)Mhaya mfanyabiashara wa Tandika, Dar es salaam na Boke mwana wa Marwa Mwita(42) Mkurya na mfanyabiashara wa Mombasa-Ukonga,Dar.
Mbele ya Hakimu Mkazi,Angelo Lumisha, wakili wa serikali Castus Ndagambo, amesema washitakiwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji kinyume na sheria ya nchi kipengele cha 196 na 197 katika Penal Code Na 16.
Ndagambo, ameiambia mahakama kuwa washitakiwa hao watano kwa pamoja walimuua Kamanda Liberatus Lymo Barlow, Oktoba 13,mwaka huu  majira ya usiku huko Kitangiri,katika eneo la MINAZI MITATU,Wilaya ya Ilemela.
Washitakiwa wote watano kwa pamoja hawakutakiwa kusema lolote kufuatia mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.
Gwaride la utambulisho, IDENTIFICATION Parade lilifanywa, Dorothy,Yule mwanamama aliyekuwa na Barlow usiku wa mauti, akawatambua wote watano.
Walirejeshwa Butimba nyuma ya nondo hadi kesi yao hiyo JINAO NAMBA 30 ya mwaka 2012 itakapotajwa tena Novemba 15 mwaka huu.
Tukutane katika sehemu ya mwisho wa mkasa huu wa kusisimua

0713 324 o74



www

Monday, October 29, 2012

AKINA NANI WALIMUUA BARLOW?



                 

JAMII ya Jijini Mwanza ilisema kuwa  “motive” ya mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi,ACP Liberatus Barlow,ni wivu wa kimapenzi.
Kikosi maalum cha upelelezi(TASK FORCE) kiliundwa ili kupeleleza mauaji haya ya tashtiti.Kilihusisha makachero wa kimataifa,”Interpol”, na miongoni mwao wataalam wa Kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,
Kabla ya majuma mawili kwisha, tangu mauaji ya Barlow, Oktoba 13 mwaka huu,tayari watu zaidi ya 10 walikuwa wamenaswa,wengine kwa mahojiano na wengine ndiyo hasa waliomuua Barlow jijini Mwanza,wakajakutimkia Dar es Salaam.
Dorothy Moses, ama Dorothy Lymo(42) ndiye mwanamama aliyekuwa na Kamanda Barlow(55) dakika chache kabla ya mauaji ya kinyama kumkumba.Alipigwa kwa risasi ya bunduki nzito, Shotgun, “Greener”shingoni,shingo likafumuliwa kabisa.
Felix Felician(50) ama maarufu Jijini kama ‘Pepe’ alitiwa mbaroni kwa tuhuma kuwa ndiye aliyekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Dorothy, ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi ya Nyamagana B,Jijini.
Ilihisiwa kuwa, pengine mwanamama huyu mfuauji, alikuwa akigawanya penzi la tashtiti kwa Marehemu Barlow na ‘Pepe’yumkini kiasi cha kuleta wivu na visasi.
Kufuatia tuhuma hizo ambazo polisi wangali wakifanyia kazi kwa umakini, alikamatwa pia Fumo Felician(46),mchezaji wa zamani na ‘striker’ mwenye mashuti makali katika timu ya Pamba ya Jijini Mwanza na Dar es salaam Young Africans. Pepe ni nduguye Fumo.
TASK FORCE ya makachero wa polisi iliongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini(DCI)Robert Manumba, iliwakamata pia Bahati Agostino na Waibe Maboto, kwa sababu Barlow alipouawa huko Kitangiri usiku wa kuamkia Oktoba 13, majahili wale walimpora redio ya upepo(Radio Call), na kasha walipora simu ya Dorothy.
Nataka kusema kuwa,bado watu hawajajifunza kwamba sasa kuiba simu ya mtu,hususan katika matukio ya ujambazi na mauaji namna hii ni kujiweka hatarini.
Nataka kuandika hapa kwamba, hisia za watu kwamba kundi hili la majambazi lilikuwa na watu werevu, ni uongo tu. Kama walitoweka na simu ya Dorothy wakaendelea kuitumia hata kama walishanyofoa laini, hawa walikuwa majambazi waliojua kufyatua risasi, na wala hawakujua chochote kuhusu teknolojia ya leo.
Hawa walivyo mazuzu, eti walitupa laini ya Dorothy, wakaendelea kuitumia simu ile wao wenyewe, ama mtu mwingine waliyemuuzia, huku wakijua simu ile ilisajiliwa na hata namba ya simu iitwayo ‘IMEI’ ilisajiliwa?
Kulingana na teknolojia ya siku hizi, ilikuwa rahisi kama nini kwa makachero wa ‘Interpol’ wenye utaalam wa hali ya juu katika ‘Information Technology’ kuiona simu hiyo na kujua mahali ilipokuwa ikiitia hata kama laini ya awali ilishanyofolewa na kutupwa.
Makachero waliifuatilia simu hiyo na kufanya mtego mdogo tu,tayari aliyekuwa nayo akatiwa mbaroni,ili akaeleze alikoipata na ilikuwa rahisi mno kuwasema waliompa au mahali wenzake walipokuwa.
Hivyo,tusiwape sifa majahili hawa kwamba walikuwa mauaji wa kimataifa, “Executioners’” kumbe majangili tu, wanaomea Tanzania kwa sababu ya uzembe wa polisi wetu na tabia ya jamii hii ya kufumbia macho watoto wao wahalifu.
Kwa kutumia IT makachero waliwanasa akina Bonge(30) na Amos Waibe Maboto; walikamatwa jijini Mwanza,kwa kutumia TEKNOHAMA.
Nataka kusema kwamba, umefika wakati sasa kutumia kompyuta kuwanasa wahalifu,badala ya kutumia mashushushu ambao wengine si waadilifu,nao hujiingiza katika usaliti na kuwaumiza raia.
ALHAMISI,Oktoba 25 mwaka huu,Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai,Kamishna Mwandamizi wa Polisi,Robert Manumba, akawaambia waandishi wa habari jijini Mwanza kwamba,kundi la watu waliokamatwa jijini Mwanza likihusishwa na mauaji ya Kamanda Barlow, hawa kuwa hasa wauaji.
Kwamba, walishikiliwa na jeshi hilo na kuhojiwa kwa sababu katika medani ya upelelezi,ni muhimu kama nini kuwahoji mashuhuda wengi,kama huyo Dorothy Lymo,ambaye alikuwa na marehemu wakati wa tukio la mauaji na hata hao ‘jamaa’ zake, akina Pepe na Fumo na wengine.
Wakikutwa hawana hatia,basi wataachwa huru.Ni muhimu polisi kuwahoji washukiwa wote na si mara moja au mbili,ili wakupe mwelekeo wa upelelezi nap engine sababu za kifo cha mtu kama huyo RPC Liberatus Barlow.
Kauli ya DCI Robert Manumba,kwamba hawa waliotajwa wangali wanapelelezwa,hata kama uchunguzi wa awali umebaini kuwa hawana uhusiano wa moja kwa maja na mauaji ya Kamanda,inaondoa tu ‘Motive’ kwamba aliuliwa kwa wivu wa kimapenzi, lakini bado tuhuma zingalipo dhidi yao.
Manumba, aliwaambia waandishi wa habari Alhamisi,Oktoba 25 kwamba waliomuua Barlow ni majambazi wazoefu(wa uhalifu,siyo weledi),na kwamba inawezekana lilikuwa tukio la ‘nasibu’ na bahati mbaya hivi.
Kundi la majahili saba, miongoni mwao watano: Muganyizi Michael Peter(36) mkazi wa Isamilo,Mwanza,Chacha Mwita(50),Edward Bugazi Kusuta,Bhoke Marwa Mwita(42)nz Magige Mwita Marwa, ambao wengine walikuwa wakazi wa Gongo la Mboto,Dar ndiyo hasa walioshiriki katika mauaji.
Watu hawa, majira ya saa nne hivi  usiku, siku ya tukio, walitangulia kupora mali za watu katika ‘grocery’ ya New Tuliza Inn,Pasiansi, waliwateka wanywaji na kuwapora vitu na simu ya mama mmoja.
Usiku huo wa Oktoba 12,Ijumaa saa sita hivi usiku walifika Kiseke katika baa iitwayo,Green Corner, waliwapora wateja,walipora hata Konyagi,wakabugia.
Sasa, wakati wanafika Kitangiri eneo lile la tukio,wakakutana na Barlow ambaye alikuwa akimsindikiza Dorothy nyumbani kwake, akawamulika kwa taa za gari.
Dorothy, anasema aliwaona wakiwa wamevalia vivazi vile vya Polisi Jamii ama Ulinzi Shirikishi, sasa Kamanda Barlow akidhani ni hao walinzi wa kijamii, akawamulika ili awaone vizuri.
Dorothy akamwambia Barlow, “Unawamulika unawajua?” Basi, kuona hivyo hgao jamaa wakamfuata Barlow haraka na kumzingira, wakaanza kufanya matata, Barlow akachukua ‘Radio Call’ ili awaite polisi.
Muganyizi Peter akamfatulia risasi ya Shotgun shingoni, ikamfumua shingo kabisa, ilimvunjilia mbali shingo lake.
Walichukua hiyo Radio Call ya Barlow na simu ya Dorothy,wakajitoma gizani.Keshoye, wakajiondokea kwenda Dar es Salaam,bila shaka walishajua walimuua nani!
TASK FORCE ya makachero wa polisi ya KIKOSI  CHA KISASI DHIDI YA MAUAJI YA BARLOW kiliwasili jijini Mwanza jioni Oktoba 13. Hata Inspekta Jenerali wa Polisi, Said A. Mwema, mtikiso wa mauaji hayo ulimleta Mwanza siku hiyo.
Makachero wa polisi, wakiwamo hao wa kimataifa, Interpol waliwasili Mwanza, wakasambaa Mara,Shinyanga,Mwanza, Geita,Bukoba na Dar es salaam, ili kufanya mtandao mkubwa katika medani ya upelelezi.
IGP Mwema, amewaambia wanahabari kuwa,waliomuua Barlow walikuwa saba, hao watano wamekamatwa tayari na wengine wawili wananyatiwa bado, na kwamba hata kama waende Uingereza watatiwa mbaroni na Interpol na watashushwa hapa nchini ili wakabiliane na mashitaka,ili kuwa fundisho kwa wenzao. Hiki ndicho KISASI alichosema Mwema, dhidi ya mauaji ya Barlow.
Nataka kusema kwamba, kulingana na Mwema,makachero wa hiki KIKOSI MAALUM CHA KISASI, walifanya kazi yao kabla ya siku 12 kwisha na kuwatia mbaroni wahusika, kama wanavyofanya kazi Federal Bureau of Investigation, Scotland Yard   ama  Military Intelligence 5(MI5)!
Majambazi hao walikamatwa Dar,Gongo la Mboto,wakakutwa na silaha mbili,Shotgun hiyo waliyotumia kumuua Barlow,ilikatwa kiatako na nyingine ni ‘Pump Action’.
Hadi Oktoba 25 redio ya upepo ya Barlow waliyopora eneo la tukio,ilikuwa bado kukamatwa,ndiyo iliyochongea Barlow kuvunjwa shingo kwa Shotgun Greener iliyofyatuliwa na huyo Muganyizi Peter,Mhaya kutoka Kagera!
Walipomuua Barlow wakatorokea Dar es salaam ambako pia hawakulala,walipora mali za raia hadi siku walipokamatwa. Nakwambia Jasiri haachi asili.
Kufuatia maelezo ya IGP Mwema na DCI Manumba, nataka kutafakari mambo machache hapa. Sina ubishi na kauli kuwa Barlow hakuuliwa kwa wivu na  visasi vya kimapenzi.
Nataka msomaji ajiulize maswali yafuatayo:
Mwanza,kuna majambazi mwazoefu wenye bunduki kama Shotgun, wanatamba tangu saa nne tu za usiku kuanzia Pasiansi,Lumala hadi Kiseke?
Polisi wa doria wanakuwa wapi hadi baa ziporwe hata Konyagi na majambazi,hata waanze kujipongeza,Kazi na Dawa, utadhani nchi haina mwenyewe?
Akina Muganyizi, walipokamatwa eti walikutwa na simu nyingi walizopora wananchi, bila shaka mchana kweupe!
Polisi walikuwa wapi wakati vibaka, wezi na majambazi wanapotishia maisha ya watu na mali zao?
Hivi Mwanza nako kuna  ‘Security Service’? Mbona raia wanatishiwa na vibaka na majambazi ambao sasa hawana hofu tena na doria za polisi?
Niliandika katika sehemu iliyotangulia kwamba, hapa Mwanza ndipo hakimu mmoja aliwahi kumtorosha jambazi sugu kwa ‘removal order’, siku ya kesi RCO Goodluck Mongi, akaambiwa na askari wake kwamba,mshitakiwa hakuwepo rumande!
Hapa Mwanza,ndipo jamaa mmoja mwaka 2005, alijipenyeza katika msitu wa wana usalama pale CCM Kirumba, akampiga mweleka Jakaya Kikwete wakati huo akiwa mgombea mteule wa Chama cha Mapinduzi! Kesi hii ilifika mahakamani,jamaa akanyeshewa mvua ya miaka jela.
Aliyekuwa Mbunge wa Shinyanga Mjini, Leonard Derefa, aliwahi kusema Bungeni kwamba jeshi la polisi livunjiliwe mbali,kwa kuwa lilishashindwa kulinda raia na mali zao-limewaacha majambazi na vibaka kutamba!
Mimi sitaki jeshi hili livunjwe,ili kuwe na “Vacuum” ama Ombwe ambalo linaweza kuleta kiama zaidi ya hapa tulipo.
Nataka kumwambia rafiki yangu Mwema ajiulize kama raia tunavyojiuliza: Kwanini Barlow alikuwa peke yake usiku wa manane,bila ulinzi? Kwanini alitembelea gari la kiraia tena lenye stika bandia ya Bima?
RPC hakuwa na walinzi? Je,polisi wa Mwanza wanafanya nini kuwakamata vibaka hata wanamiliki silaha na kumuua RPC? Polisi wanakamata wahalifu au wanafanya biashara ya daladala mjini? Kwa nini polisi wawe na vitambi? Mbona hata Bill Gates, Carlos Slim, Warren Buffett na wenzao hawana vitambi? Eti Polisi wa Mwanza wana vitambi!!
Nataka kumwambia IGP Said Mwema akumbuke kwamba, nilimuuliza katika mkutano na waandishi wa habari kwamba, Barlow aliuawa Oktoba 13, ilipofika Oktoba 25 tayari majahili hao walikwishatiwa mbaroni-siku 12 tu  za Operesheni ‘LIPA KISASI DHIDI YA MAUAJI YA BARLOW’.
Nika mkazia macho ya kidadisi IGP Mwema na kumbandika swali,
“Kwanini kasi hiyo ya majuma mawili ya kuwakomesha majambazi waliomuua Barlow isitumike pia kuwakomesha majahili wanao ua raia na kuwapora mali zao?”
Kwa nini kasi hiyo, “Supersonic Speed” isitumike katika upelelezi wa kesi nyingine za raia wa kawaida, wanaohujumiwa na majahili hawa na kuporwa mali na maisha?
Kwa nini polisi wanashindwa kufikisha kesi hata ya vibaka mahakamani, eti upelelezi haujakamilika? Kwanini kesi ya Barlow upelelezi ufanywe kwa kasi za viwango kama zile za Samuel Sitta-Standard and Speed!
“Polisi na raia wema lazima kuunganisha nguvu na talanta zao ili kuongeza ‘speed’ ya kuwakomesha wahalifu,ili nchi iwe salama”, alinijibu IGP Mwema,pale ukumbi wa Jini,Mwanza.
Said Mwema, anatishwa na jamii kukosa uzalendo kwa Taifa letu, na kushindwa kutimiza wajibu wa kizalendo kwa Taifa.
Oktoba 25,ndiyo siku nilipobaini kuwa Said A.Mwema, ni mwanafalsafa wa kiwango cha juu sana.Alianza kueleza kauli za marais wa Marekani akina John Fitzgerald “J.F” Kennedy na Abraham Lincoln, juu ya maslahi ya nchi kuwa kipaumbele cha kwanza,na uzalendo kwanza kuliko matumbo. Siku hizi Tanzania raia na polisi ni wazalendo wa matumbo yao!
Naam, Mwema akauliza hivi, “Usiulize Tanzania itakufanyia nini,uliza utaifanyia nini Tanzania?” Mwema amesema uzalendo unatoweka katika nchi yetu na maslahi ya taifa yametupwa,ndiyo maana polisi na raia wameshindwa kuunganisha nguvu na vipaji vyao ili kuwatoa kamasi majambazi!
Nitaichambua hotuba ya IGP Mwema, juma lijalo , Itaendelea.










Monday, October 22, 2012

MAUAJI YA KAMANDA BARLOW-FULL STORY 2



                       
JULAI 28,mwaka 2003, aliyekuwa Mkuu wa kituo  kikuu cha Polisi  (OCS) Jijini  Mwanza, Daniel Maburuki Mahende(45) aliuawa  kwa risasi na majambazi,katika eneo la Bugando,jijini Mwanza.
Serikali iliahidi kuwatia mbaroni wauaji hao, waliohisiwa majambazi kutoka Burundi. Haikujulikana baadaye kwamba wauaji hao walichukuliwa hatua gani na mahakama.
Mwanza,kumetokea matukio ya mauaji ya kinyama sana.Lakini umma haukujulishwa hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama zao.
Katika makala yaliyotangulia, nikaeleza kwamba, aliwahi kupigwa risasi ya kichwa ‘cashier’ wa Tanzania Breweries Limited(TBL),Pasiansi, Jijini,zikaporwa zaidi ya shilingi milioni 200.
Baadaye,nilipomuuliza aliyekuwa Wakili wa Serikali Mfawidhi,katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP)Kanda ya Ziwa, Anselm Mwampoma, akaniambia:
“Kesi hiyo ya mauaji ya ofisa wa TBL,huko Pasiansi,haikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia watuhumiwa hatiani”, alisema Mwampoma.
Tuseme, kesi hiyo “Ilivurugwa” ama ilichakachuliwa,hata ushahidi uliokuwepo haukutosha hata kuwafikisha mahakamani washitakiwa. Hili Mosi.
Pili, aliyewahi kuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mwanza,(RCO) Goodluck Mongi, aliwahi kusema katika semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) kwamba wapo maofisa wa Mahakama Mwanza, waliwahi kumtorosha mtuhumiwa wa ujambazi ,gerezani Butimba,kwa ‘removal  order’ akatoweka rumande, na siku ya kesi mahakamani mshitakiwa  hakuonekana!
 Yaani, wakati maofisa wa polisi wakihaha kumfikisha mtuhumiwa wa ujambazi mahakamani, alishayeyuka rumande!
Sipendi kusema kilichotokea, lakini msomaji unaweza kujua inakuwaje mtuhumiwa wa ujambazi anapewa dhamana, kwa “removal order” ya   Mheshimiwa Hakimu, pasipo hata polisi kujua?
Kuna matukio lukuki  ya ujambazi Mwanza,wizi,uhalifu,mauaji ya kutatanisha n.k Hata hivyo, umma haujui kwa nini wahusika hawajakamatwa na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Hii ni HATARI!! Matukio ya karibuni sana ambayo hata Marehemu Kamanda Liberatus Barlow aliyashuhudia,ni ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Gazeti la Kasi Mpya, Richard Masatu, ambayo licha ya ripori ya daktari kuoneshwa kuwa aliuawa, polisi waliendelea kusema aligongwa gari!
Kuna mauaji ya mmiliki wa nyumba moja ya wageni Jijini Mwanza anayejulikana kwa jina la Manumbu, aliuliwa kwa risasi,lakini umma haujafahamu kilichotokea, na wala hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kuna kawaida ya matukio ya mauaji kutokea Mwanza,lakini sijui polisi wanashindwa kuwabaini wauaji ili wafikishwe mahakamani?
Kuna watu wanakufa katika mazingira ya kutatanisha,lakini mwisho wa siku hakuna mtu anayekamatwa na polisi ili ashitakiwe mahakamani.
 Mwanza,kuna historia ya Mbunge mmoja, kumwagiwa tindikali,lakini ‘kesi iliyeyuka’ kwa njia zisizofahamika,kufuatia mtuhumiwa kuyeyuka,kama walivyoyeyuka  mashahidi wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa huko Kenya,zama za NYAYO,Dk.Robert Ouko.
Aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Leonard Bihondo, alituhumiwa kumuua aliyekuwa Katibu wa CCM wa Kata ya Isamilo, Bahati, alitiwa mbaroni na kesi yake ingali ikisubiri kuanza kusikilizwa.
Jumatano, Oktoba 17,mwaka huu,nikaazimu kumuuliza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini(DCI)Robert Manumba,kama alijua mauaji ya Kamanda Barlow yalifuatiwa na mauaji ya watu wengine hapo Mwanza,lakini haikufahamika hatma ya mauaji hayo?
Na kwamba, Je, polisi wamefikia hatua ya ku  “compromise” na hali hiyo? Nilimkuta Robert Manumba,mbele ya jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mwanza,nikamsalimia kasha nilipomgusia jambo hilo akaniambia:
“Rafiki yangu,mimi ni mgeni hapa! Wenyeji mbona wapo ofisini unaweza kuwauliza hata wakasema kuhusu kilichopo?’ Manumba aliniambia. Nilicheka,kasha nikamuaga,maadam alikwisha pangua ‘ngumi’ za uso nilizotaka kumtupia!
Nilimpata Mkuu wa Upelelezi (RCO)Mkoani Mwanza,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi(SSP)Joseph Konyo(siyo Joseph Kony wa  Lord’s Resistance Army wa Uganda).Siku hiyo, Oktoba 17,nikamwambia Joseph Konyo, juu ya migogoro Rwanda,Burundi na Jamhuri ya Congo(DRC) ilivyosababisha wakati Fulani huko mkoani Kigoma bunduk,SMG,i kuuzwa kwa kubadilishana na  DEBE LA MAHINDI au MTAMA!
Nilimuuliza Konyo, kama hakujua kwamba wakati Fulani wananchi kutoka Kigoma walihudhuria semina moja ya Upunguzaji silaha, wakasema  Mwanza ndilo lilikuwa soko kuu la silaha?
Na kwamba, polisi waliposhindwa kuchukua hatua sasa silaha haramu zinapatikana mikononi mwa wahalifu hata kuweza kuua raia na hata maofisa wa polisi kama Kamanda Liberatus Barlow?
“Nilikuwa Kigoma, wakati huo mwaka 2004,iliposemwa kwamba bunduki moja ya SMG ilibadilishwa kwa debe la mtama au mahindi katika magulio.Haikuwa na ushahidi kwamba wanunuzi wa silaha hizo walitokea Mwanza, hata hivyo polisi lazima washirikiane na raia ili kutokomeza uhalifu”, Joseph Konyo alisema.
“Nawashauri raia wema wa Mwanza,wasiache kushirikiana na polisi ili kusaidia kuondoa kitisho cha amani. Bila amani,hakuna kitakachofanyika. Wasikate tamaa,raia wanapaswa kutoa taarifa hata katika ngazi za juu za polisi,wanapaswa kutuamini kama wanataka tupambane na uhalifu na kuushinda”, Konyo alisema.
Akasisitiza kuwa, kumkamata mtuhumiwa ni jambo moja,lakini kumfikisha mahakamani na kuthibitisha kosa, ni jambo la pili linalohitaji ushiriki wa raia wema kutoa ushahid, ili kuthibitisha kosa pasipo shaka yoyote.
Nikamkumbusha RCO,Konyo madai ya wananchi wa Mwanza,kwamba wakitoa taarifa za uhalifu,mara wahalifu hukamatwa kasha kuachwa huru ambapo kitendo cha raia kuwajulisha polisi wahalifu hugeuka jambo hatari kwa maisha yao?
Siku tano baadaye, RCO,Joseph Konyo akafanya mkutano na maofisa wa Polisi na kuwataka kushirikiana ipasavyo na wananchi katika vita dhidi ya uhalifu nchini.
“Polisi tunapofuatilia uhalifu,tunapowajibika ipasavyo katika matukio ya uhalifu,tukishirikiana na raia wema tutatokomeza uhalifu”, Konyo alisikika akiwaambia maofisa wa Polisi.
Mkutano huo,ulihusisha maofisa wakaguzi wa polisi, maofisa wa idara ya upelelezi na maofisa wa kawaida.
 Kauli hiyo ya Konyo imekuja siku chache baada ya kifo ca Barlow, ambaye pia ameuliwa katika mazingira ya kutatanisha, ambayo raia wanadhani kulikuwa na uzembe na tabia ya kuwalea wahalifu iliyojengwa muda mrefu hata kusababisha mazingira ya ‘Mdharau Mwiba Guu likaota tende!”
Kufuatia hali hiyo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini,Robert Manumba, anasaidiana na makachero wa Polisi wa Kimataifa, Interpol, kuwawinda majahili hao waliomuua Barlow,na inshallah, baada ya kitambo watakuwa wametiwa mbaroni na kufikishwa mbele ya sheria.
Hadi sasa watu takriban 15 wamehojiwa na polisi,na watu kadhaa wanashikiliwa kufuatia mauaji hayo ya kuamkoa Jumamosi,Oktoba 13, majira ya saa 7-8 huko Kitangiri.
Mwanza ni mahali ambapo motto aliwahi kutekwa nyara, watekanyara wakaomba wapewe mamilioni ya fedha ili wamwachie mtoto huyo. Uliwahi kusikia hadithi za utekaji nyara na watekaji kuomba fedha nyingi za ‘kikombozi’?
     Haili liliwahi kutokea huko Bwiru,mtoto akatekwa nyara, wateka nyara wakaomba pesa, polisi walipojaribu kumwokoa wakishirikiana na babaye, mtoto alitoswa Ziwa Victoria na kufa!
Haya mambo ya Palestina, Ulaya na Afghanistan,yaliwahi kutokea bwiru,Mwanza. Mwanza watu waliwahi kuteka msichana wa baa,wakachinja, wakachukua kichwa,shavu la kulia wakanyofoa sehemu zake za siri,kasha kiwiliwili kikasokomezwa kwenye sandarusi na kuachwa penye pagala!
Wauaji wengine walitoroka,polisi hawakuwahi kuwakamata na kuwasweka hata rumande. Hapa Mwanza, ndipo mahali ambapo mwanamke anachinjwa chumbani, hata majirani wakashindwa kujua hadi walipoalikwa na mainzi ya kijani asubuhi,maiti akiwa ndani ya kiroba,katika pagala la mitaa ya Kiyungi!
Hapa ndipo jamaa mmoja wa Kenya alitaka kumuuza albino kwa shilingi milioni 400,ikawa bahati polisi wakamnasa na kumwokoa albino aliyekuwa hatarini kuchinjwa ili viungo vyake vikauzwe kwa watu wanaotaka utajiri kwa kutumia  ‘ndaku’ au bahati Fulani za utajiri.
 Huku ndiko albino huwindwa kama wanyama,hata sasa wapo wanaoishi katika kambi maalum wasije kuuliwa. Hapa ndipo vikongwe wanauliwa kwa tuhuma za ushirikina.
Hapa ni mahali ambapo wahalifu wana ‘confidence’ hata walipomaliza kumuaa Kamanda Barlow, walitoroka na Radio Call na bastola yake.Walivalia majazi ya polis Jamii.Waliyatoa wapi?
Hata hivyo, katika medani ya upelelezi,ni mapema mno kusema nani alimuua Kamanda Barlow ambaye tayari amezikwa kwao Kilimanjaro.
Katika medani ya ukachero,siyo kila anayekutwa na kamba shingoni akiwa amekufa,basi kajinyonga! Polisi wana kazi ya kuchuja habari,kuzikagua na kugundua wahalifu wapya,kasha kutafuta ushahidi na kuutetea mahakamani,ili  kuithibitishia mahakama pasipo shaka yoyote(beyond reasonable doubt) kwamba muuaji ni Fulani.
Itaendelea