TUNAJADILI
ikiwa yupo kiongozi mahiri wa siasa hapa duniani, anayewapenda wananchi kiasi
cha kujitoa mhanga mithili ya mshumaa.
Mshumaa,huwaangaza wengine huku
ukijiteketeza wenyewe.
Mwandishi wa
Kigiriki, Euripides, aliandika takriban millennia tatu zilizopita kwamba,Mfalme
kijana mtanashati wa Thesaly aitwaye, Admetus aliugua.
Miungu ya
Ugiriki(Ugiriki ni nchi ya masanamu ya miungu wengi) ikawaambia nduguze kuwa
lazima Admetus afe, isipokuwa kama angepatikana mtu mwingine wa kufa badala
yake.
Kwa
Kiingereza mtu wa kufa badala ya mwingine ni “Substitute” ambaye kama
angepatikana kufa badala ya Mfalme Admetus, angeweza kupona maradhi yake na
kuendelea kuishi.
Wakaulizwa
baba na mama yake kama walikuwa radhi kufa badala ya Admetus,wakakataa. Ndugu
zake nao waliulizwa,wakakataa. Marafiki nao walisema, “Admetus, ni kijana
mzuri; ni mfalme mzuri,lakini hakuna wa kufa badala yake!”
Mwisho wa
siku, mkewe msichana mrembo sana aitwaye, Alcestis, akahiari kufa kwa niaba ya
Admetus,kwa sababu alimpenda na alikuwa mtu mwema.
Baada ya
kifo cha Alcestis, Mfalme Admetus alitambua ‘HASARA’ iliyomkuta ya kumkosa
kipenzi chake, Alcestis aliyekuwa na upendo wa dhati kwake.
Akamwombolezea ifuatavyo:
“Nitakulilia mpenzi wangu,siyo kwa
mwaka mmoja au miwili;bai katika siku zote za maisha yangu,mwanamke
uliyenipenda! Baba na mama walinichukia,walinipenda kwa maneno matupu,siyo kwa
vitendo”, Admetus aliomboleza.
Nataka
msomaji atambue kwamba, kumpenda mtu kwa maneno matupu siyo kumpenda-ni
kumchukia.Upendo wa dhati siyo wa maneno matupu; ni vitendo kama alivyofanya
Alcestis.
Naam, “Love in words, not deeds” ni unafiki
mtupu, siyo upendo,kama wanavyojidai siku hizi wanasiasa na wakoloni wetu wa
zamani.
Nakusudia
kuwaonya Waafrika wasiwe wepesi kulaghaiwa na wanasiasa na hata wakoloni wetu
wa Ulaya na Marekani, kwamba wana upendo kwa wananchi-si kweli ni unafiki na
ufalisayo mkubwa!
Hata
hivyo,Katika Warumi 5:7 Profesa Paulo
anasema, “Ni shida mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema,kama Admetus.
Biblia,
katika Warumi 5:8-10, inasema, “ Lakini,Yesu Kristo alikufa kwa ajili
yetu,tulipokuwa tungali “ADUI” zake.Alitupatanisha na Mungu tulipokuwa tungai
adui zake”(wenye dhambi ni adui wa Mungu).
Nataka
kujifunza hapa kwamba, Biblia inatwambia kwamba UPENDO ni dhidi ya adui, ambaye
kwa kawaida hawezi kuwa na faida yoyote-Upendo usio na faida!
Upendo wa
Alcestis kwa Admetus siyo huu usio na faida,bali ni upendo wa mke kwa mumewe,
“Philos’ au Philia-upendo wa familia,upendo wa kibinadamu wa kidugu-Brotherly
Love.
Baba
humpenda mama,mama humpenda baba, wazazi huwapenda watoto,hata mwingine hujitoa
mhanga kuwaopoa motoni.Ndugu hupendana wao kwa wao n.k
Upendo wa mtu kumpenda adui hata kuwa radhi
kufa kwa niaba yake ni Agape kwa Kigiriki, Prof. Ibrahim Lipumba, Dk.Wilbroad
Slaa au Rais Jakaya Kikwete, hawawezi kuwa na upendo wa jinsi hii, wala ule wa
Alcestis kwa raia.
Tuambizane
ukweli.Upendo wa kweli, “TRUE LOVE” Agape au Philos ni upendo wa mtu kuumia kwa
ajili ya kumpatia mema mtu mwingine. Upendo wa Agape hauna faida, “suffers long
and it thinks no evil”, hata kama unamwonyesha upendo huo jambazi au adui yako!
Tujiulize:Wanasiasa
wetu hawa, viongozi wa sasa wanaweza kujitoa mhanga wafe kwa ajili yetu
wananchi?
Wako tayari
sisi raia tuishi maisha bora kuliko wao?Wako tayari kuuza mashangingi,suti zao,
briefcase zao na rasilimali zao
nyingine, ili sisi wapigakura wao tuishi maisha bora?
Mtu
mbumbumbu anaweza kusema kwamba jibu la maswali haya ni Ndiyo! Haidhuru.
Tumjadili Mpigania Haki za Weusi wa Marekani, Martin Luther King Junior.
Kabla ya
kwenda kwa mtu huyu,tujisaili: Kwanini sisi masikini hatuna shule bora kwa
ajili ya elimu ya watoto wetu? Kwanini hatuna zahanati,dawa,vifaa na hatuna
hospitali?
Kwanini sisi vijijini hatuna barabara wala huduma
za jamii kama umeme,maji safi na salama n.k wakati wanasiasa hawa wao wana kila
kitu?Wanatembeleaje magari ya Milioni 60 wakati sisi hatuna zahanati wala dawa?
Viongozi wa
dini nao siku hizi wanatembelea magari ya fahari ya zaidi ya Bilioni 2, huku waumini
wao wakiwa hawana hata makubazi miguuni! Wanaimba Upendo! Mungu ni Upendoo,
aaameeen! Aibu tupu!!
Yawezekana
mtu “kuthubutu” kufa kwa ajili ya mtu mwema kama Admetus-huu upendo huitwa,Philosterges, kwa Kigiriki.
Lakini, kama
huna nasaba na mtu,humjui, naye ni adui yako na ukahiari kufa badala yake,
ndiyo AGAPE.
Wapo watu
wanakesha redioni na kwenye runinga wakiimba, “Nakupenda kama nyamachoma!” Huu siyo upendo, ni tamaa za
ngono(sexual drive, sexual affections, sexual love)ambazo mwisho wa ngono,hakuna
chochote,bali uchungu na majuto kwa aliyedanganyika.
Kumpenda mtu
usiyemjua,usiyewahi kukutana naye na hana faida kwako,ni “Impartiality Love”
upendo unaoitwa Agape ama Agapao kwa Kigiriki. Huu ndiyo upendo anaopaswa kuwa
nao kiongozi wa siasa-kuwapenda wananchi asiojua hata majina yao,na wanaishi
pembezoni kule,Masasi ama Saragana,Masinono na Bugwema,Musoma!
Siku hizi,
tunasikia kwamba kiongozi Fulani anawapenda wananchi, hadi wananchi wanakubali
kupigwa virungu,kupigwa machozi ama kupigwa risasi na polisi,kwa kutii shuruti
zake hata kuwapiga mawe polisi wenye SMG!
Polisi
wakizuia maandamano, kiongozi wa siasa akasema, Andamaneni, watu wanatii na
kupoteza maisha! Hii ndiyo Agape, watu kumfia kiongozi, siyo?
Agape, siyo
watu wafe kwa ajili yako ili uende Ikulu au uukwae ubunge ama madaraka Fulani.
Agape ni wewe kiongozi ufe kwa ajili ya masikini usio na nasaba nao,ili kwa
kifo chako wapate faida ya kukombolewa.
Tofautisha
upendo wa Alcestis,Martin Luther King Junior, Yesu na hawa jamaa. Tafakarini.
Tunajadili
upendo wa dhati.Viongozi wa siasa wanaonesha upendo huu kwa wananchi? Viongozi
wa kidini wanawapenda kwa dhati waumini wao? Mbona wao wanakula na kushiba,
wafuasi wao ni fukara?
Kwa nini
rushwa na ufisadi kama kuna upendo katika mtego uitwao siasa? Kwanini mishahara
ya wabunge na wafanyakazi iongezwe maradufu,halafu mazao ya wakulima yashuke
bei kwa visingizio vya kushuka kwa thamani ya shilingi au mtikisiko wa uchumi
duniani?
Kwa nini
hawa ambao hawajulikani kwa wanasiasa na viongozi wetu(wakulima),mazao yao
yanaposhuka bei,maisha yanapokuwa duni na hawana huduma za jamii,halafu
tunawachochea wafanye vurugu,wafe kwenye maandamano yaliyopigwa marufuku na
polisi,badaya ya kuwasaidia waishi,wanusurike kufa?
Tuambizane ukweli.Wanasiasa wote ni ndizi-ni
rangi moja na wamepinda! Msikubali wawatumie kama ngazi, wao wanaingia kula
maisha,nyie mwabaki kupigwa jua na mvua.
Acha upambe,
angalia maisha yako ni ya thamani kubwa. Kwanini umpige polisi kwa mawe wakati
yeye ana SMG yenye risasi 30?
Nahimiza
watu kuheshimu maisha yao,nahimiza watu kuheshimu mamlaka, nahimiza usamaria
wema,nahimiza utii wa sheria bila shuruti na kuheshimiana sisi kwa sisi.
Tusikubali viongozi wa siasa kutugawa kwa
misingi Fulani ili tuanze kupigana.Tukipigana wao wana mbawa,sisi tunakufa na
wake na watoto wetu wanateketea wakati wao huruka kwa ndege na kwenda zao!
Vita vya
wenyewe kwa wenyewe Kenya,ni mfano mzuri kwetu.Waliokufa walikuwemo watoto wa
Kibaki? Hapana. Walikuwemo wa William Rutto, ama wa Raila Amolo Odinga?
Watakuwemo
wa Dk.Slaa au Kikwete na wenzake? Anzisha amani, acha ujinga.
ZBIGNIEW
BZEZINSKI, alikuwa Mshauri wa Usalama wa Taifa, enzi za Rais Jimmy Carter wa
Marekani.
Huyu,mtu
mkubwa, wa Taifa babe sana hapa duniani ambalo husemwa lina demokrasia
iliyopevuka,ndiye hasa anayetuhumiwa kusimamia mradi wa kutengeneza virusi vya
Ukimwi,katika maabara za kijeshi huko kilomita 75 kutoka New York, mwaka 1975.
Naam,viongozi
wakubwa ni wenye ‘madudu nakubwa’.Wenye mamlaka makubwa wana madhambi makubwa
sana, kinachowaokoa ni uzuzu wa wafuasi wao kueneza propaganda kwamba hao
viongozi wao siyo binadamu wa kawaida,bali malaika au miungu.
Watu wadogo,
hasa viongozi wa Waafrika utaona wanasemwa walifanya upumbavu huu na ule!
Utaona unyama unafanywa Afrika,utadhani Ulaya na Marekani ni mbinguni!
Martin Luther King Junior, alitiliana saini
muswada wa Uhuru kwa Weusi wa Marekani,Julai 3,mwaka 1964.Mkataba huo ulikuwa
kati ya Dk. Luther King na Rais Lyndon Johnson, Martin Luther aliuawa na
Pentagon,Makao Makuu ya Jeshi la Marekani mwaka 1968.
Huyu, alitoa
maisha yake akipigania haki za watu wake, WEUSI wa Marekani, dhidi ya ubaguzi
wa rangi.
Tabia hii
ingalipo Marekani, na Ulaya. Namwonya
Rais Jakaya Kikwete awe macho na Uingereza, Marekani na Ufaransa.
Siku hizi
wameanza kumtumia Joyce Banda,kutaka kuleta chokochoko Maziwa Makuu,vita
vinapofumuka sisi kwa sisi,wao wachote rasilimali zetu na kuondoka. Nyuma ya
Joyce Banda lazima wapo hawa wameona kunaweza kuwepo mafuta ama gesi, ili
tuking’amua tuache kuwategemea!
Kama
alivyosema manafalsafa wa Ugiriki, Salon, sheria zilizowekwa ni ‘utando wa
Buibui’. Marekani hukiuka sheria na kwenda zao pasipo kunaswa na sheria hizo.
Wewe ‘mdudu’ mdogo ukicheza unanaswa.
Angalia
baadhi ya wadudu wadogo walionaswa katika “Spider’s Web” ni pamoja na akina
Muammar al- Qaddafi,Saddam,Osama,Charles Taylor,Laurent Gbagbo n.k
Tumjadili
kidogo Charles Ghankay Taylor.Ametumwa na Marekani kufanya unyama Sierra Leone
wakaja kumwacha penye mataa.
Walimtorosha
wenyewe gerezani huko Boston, akakimbilia Libya, akajifunza mbinu za medani za
kijeshi, akasaidiwa kupindua serikali Liberia, akaanza ‘biashara’ ya kusaidiana
na Revulutionary United Front(RUF) huko Sierra Leone, wakachukua almasi na
kumpa Marekani, wakapewa bunduki!
Mwisho wa siku, Taylor amekamatwa,
amefunguliwa kesi akashinda makosa yote 11, Marekani wakalazimishwa afungwe
miaka 50,tena Uingereza,ili abaki kimya gerezani maishani mwake, asipate kusema
siri!
BAFFOR
ANKOMAH,Mhariri wa jarida mahsusi la New African la Julai mwaka huu, katika
safu yake ya “Baffour’s Beefs” amesema uovu wa Marekani na mataifa babe
haya(Metropolitan Powers) ambao waliwashinikiza akina Louis Moreno Ocampo na
Fatou Bensouda, kumkomesha kicha maji kama Charles Taylor.
Nataka
kuwaonya viongozi wa Afrika,wanaotumiwa na Marekani,Ufaransa na Uingereza,kukoma
kuihujumu Afrika,la sivyo wanaelekea mahali walipo Taylor,Gbagbo, Osama,
Gaddafi n.k
Marekani
hawana rafiki,rafiki ni rasilimali kwa maslahi ya Marekani, siyo Afrika!
Nawaonya pia viongozi wa vyama vya siasa hapa
Afrika.Wanapewa vijisenti na silaha ili wafanye vurugu,nchi zetu
zisitawalike,mwisho wa siku ni hawa Marekani,Uingereza na Ufaransa
watakaofaidika na vita vya Kunguru!
Wametoka
Libya,Misri,Irak,Yemen na sasa wako mbioni kuiteka Syria,wakimaliza watakwenda
Iran. Qatar,Kuwait,UAE,Lebanon,Bahrain kumetulia kwa kwa sababu wamekubali
‘unono’ uende Ulaya na Marekani! Ukipinga tu,unaoneshwa mtutu wa bunduki na
unapelekwa kwenye utando wa bui bui utakaokunasa.
Sisi ni
wadudu wadogo,nzi-kwenye ‘spider’s web’ hatuwezi kuvuka.Tando zote za buibui
kama ICC huko Hague,ni mali yao.
Sasa
jidanganye kwamba Marekani na Ulaya kuna demokrasia au haki za binadamu. Wewe
naye binadamu,mtu mweusi?
Kamuulize
Caster Semenya, au Samuel Eto’o.
Angalia
madudu ya akina Nicolas Sarkozy huko Ufaransa, amefanya ufuska,uchafu akiwa
rais. Angekuwa RG Mugabe au mwingine,ungesikia maneno.Raia wangeshawishiwa
kuingia barabarani na kuchoma moto magari ya serikali,majengo na matairi
barabarani,kwamba ndiyo, “PEOPLES POWER”!!
Ufaransa,
‘scandal’ za akina Sarkozy za kufanyisha watoto ngono, huko Thailand na
Ufaransa eti ni ‘minor thing’, lakini viongozi kama Luiz Inancio da Silva wa
Barazil watasemwa hawana elimu,ni washona viatu! Hawaongei kuwa uchumi wa
Brazil ulipaa wakati wa Da Silva!
Wanaona sana
akina Jacob Zuma Mushorozi na Mfalme Muswati III wa Swaziland kuona vimwana
kila mwaka!
Lakini, ufuska wa akina Silvio Berlusconi huko
Italia ni ‘Minor thing’! Raia hawashawishiwi kuingia barabarani na mawe na
hawalipwi mishahara huko kushika bunduki,kama Syria.
Sisi
‘Madodoki’tunalishwa kila pumba na kuanza kupigana sisi kwa sisi. Hatujui
mwisho wake utakuwaje? Hatutazami kesho kwa kuchungulia historia ya hawa akina
Charles Taylor,Jonas Savimbi,Mobutu, Hosni Mubarak na vibaraka wengine walivyofanyiwa.
Nataka
kusema kwamba,tujiepushe na Marekani na wanasiasa wa Afrika ambao leo Marekani
na washirika wake wanawalipa posho kuja kufanya vurugu Afrika,ili tupigane sisi
kwa sisi,wao wachukue rasilimali.
Kumbe hata
mgogoro kati yetu na Malawi haufai kuishia kuwa vita vuya silaha,tunawanufaisha
hawa majahili walioanza kuchochea vita kwa kujua Ziwa Nyasa kuna mafuta au
gesi!
Nawashauri
Waafrika kuachana na kulishwa ‘kasumba’ ya kikoloni. Tuanze kupendana sisi kwa
sisi na kutatua matatizo yetu kwa amani,bila kuwaalika majahili hawa.
Nawaonya viongozi wa siasa hapa Afrika na
wapambe wao wanaopokea posho toka Ulaya na Marekani ili wawachochee vijana
kufanya vurugu kwa kisingizio cha ufisadi, na kukosa ajira!
Fikirini vizuri. Vita vikifumuka ndiyo
mtaajiriwa kwa risasi na mizinga?Ndugu zenu wakifa ama mama zenu na wadogo zenu
wakiwa wakimbizi,ndiyo mtapata ajira?
Itaendelea
0786 324 074,0754 324 074
No comments:
Post a Comment