Nitajadili aina nne za upendo
katika mwendelezo wa makala hizi. Kuna aina nne za upendo kama wasemavyo
wanafalsafa wa Kigiriki: Eros, Philia,
Storge na Agape.
Hata hivyo, katika hizi,
upendo halisi ni Agape ambao siyo upendo wa faida. Hili niliache kwanza.
Tuijadili kidogo demokrasia.
Hawa hawa wanafalsafa wa Kigiriki wanasema, demokrasia ni ushirikishwaji wa
umma katika kutoa maamuzi, “Participation of Majority”.
Demokrasia, wanasema ni utawala wa watu na
watu kwa ajili ya watu.
Siku hizi wanasema kuna
tawala za kikatili sana ambazo kwao kuna serikali za wachache kwa ajili ya
wachache-Government of the few by the few for the few.
Katika zama hizi, serikali ya
watu na watu kwa ajili ya watu,huwa na uhuru wa kusema (chochote?)
Ndiyo maana siku hizi duniani utaona migomo na
maandamano yasiyokwisha, ambao pengine utaona virungu vya polisi na mabomu ya
machozi,ili kuwatawanya waandamanaji.
Vibaka nao hutumia mwanya huo wakijidai
waandamanaji, hupora mali za raia wenzao wasio na hatia na kutokomea. Jambo
hili lilitokea Mwanza,mwaka jana.
Hakika, hakuna kiongozi au mtawala atakayekaa
salama siku hizi za migomo na maandamano, ama kukosolewa.
Na Mungu hajawahi na hata sasa haachwi bila
kukosolewa. Kama ofisi ya Mungu(Elohim, Elyon,Adonai, Elshaddai, Yahweh ama
Yehovah) ingejulikana ilipo, angekwisha kumbana na maandamano na watu kumgomea!
Kama Mungu nyumba yake
ingejulikana, na sanduku lake la posta ama namba yake ya simu, tayari
angekwisha buruzwa mahakamani kujibu mashitaka,
“Ya kwanini alimuumba Shetani? Kwanini Shetani
yupo,na anawashawishi waungwana kuzini na wake za watu,kupora mali za umma na
kuwafanya wengine tajiri, wengine masikini?”
Nchini Romania, kuna kituko
cha jamaa aliyemburuza Mungu mahakamani,kwa kosa la kushindwa kumlinda jamaa
mmoja ili asitende makosa!
Pavela Mircea, alimfungulia Mungu kesi hii kwa
sababu ya kumuumba Shetani, ambaye alimshawishi kufanya mauaji, na kasha akajikuta
nyuma ya nondo za magereza.
Jamaa, alisema si yeye aliyeua bali ni Shetani
aliyemshawishi; na wala si Shetani,bali ni Mungu aliyemuumba Shetani!
Basi, akijibu mashitaka,
Mircea alisema alitiliana saini mkataba na Mungu,siku alipobatizwa Mungu
amlinde hadi asifanye kosa lolote!
Mircea, akaiambia mahakama
kuwa kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili, haikuwa yake bali alistahili kuitwa
Mungu aseme kwanini hakumlinda asitende kosa hilo?
“Mungu alipaswa kuniepusha na maovu yote,na tamaa
za wizi,rushwa,ufisadi, chuki na mauaji,lakini kwa uzembe,au kwa kutaka, Mungu
amemruhusu Shetani ambaye amenisukuma kuua!” Mircea alisema mbele ya hakimu
huko Romania.
Pia, alidai Mungu amlipe
fidia ya mamilioni ya fedha kwa sababu alilipa sadaka, na alinunua mishumaa
kanisani kwa muda wote hadi siku alipopatikana na kesi hiyo ya mauaji.
Mircea, akaiambia mahakama kuwa,kwa sababu
sadaka zake na mishumaa aliyonunua kanisani kwa muda wote wa tangu ubatizo,
hazikumsaidia chochote ili aachane na tamaa mbaya,chuki hadi kupatwa kesi hii
ya mauaji. Kwamba Mungu alipaswa kuzirejesha fedha zake kasha amlipe fidia!
Upande wa mashitaka ukatupilia mbali madai ya
Mircea. Kwa sababu, “Mshitakiwa” Mungu alishindwa kufika mahakamani hapo kwa
muda mrefu sana,ili kujibu mashitaka haya ya Mircea.
Jaji aliyesikiliza kesi hiyo, akatoa maamuzi
ya madai hayo kwamba kwa kuwa iliipa taabu kumpata Mungu ili aje kujibu madai
ya Mircea. Na kwa sababu haikujulikana wapi Mungu anaishi,nyumba namba ngapi?
Mtaa gani,tena mji gani hapa duniani?
Jaji alisema: “Tumejaribu
kutafuta anuani ya makazi ya Mungu,ili aitwe mahakamani, imeshindikana!
Tumeshindwa kujua hata namba yake ya simu…wala hajulikani anaishi mji gani, au
anuani ya nyumbani kwake”, Jaji aliwaambia waandishi wa habari wa Romania mwaka
2005.
Mircea, alitiwa hatiani kwa kosa la mauaji,
akafungwa jumla ya miaka 20 kwa kosa la mauaji,kwa sababu Mungu alishindwa
kufika mahakamani,ili kubebeshwa kesi ya mauaji kwa kosa la kumuumba Shetani!
Shetani eti ndiye husababisha wizi, tamaa,chuki,mauaji,ufisadi,rushwa
n.k Kwa nini Mungu alimuumba Shetani? Ndilo suala wanalouliza watu kwa hasira
siku hizi.
Hakuna mtu anayekiri(anayekubali
kuungama)makosa yake siku hizi. Kila mkosaji hutafuta mbuzi wake wa
kafara(scapegoat) kufuatia makosa yake aliyotenda kwa hiari yake mwenyewe,au
kwa uzembe.
Mtu akibaka katoto kachanga,
au akizini na bintiye na kufumaniwa, atasema, “Ni Shetani tu!”
Shetani angeonekana
mahakamani naye angesema, ‘Ni Mungu, maana bila Mungu Shetani asingekuwepo!
Akina Mircea, wako wengi
Tanzania.Hawataki kukiri makosa.
Kukiri ni kutambua
kosa(Confession is acknowledging of guilty),hakuna anaye tambua uhalifu
wake-kila mtu humsukumia aliye karibu naye kwamba ndiye chanzo cha umasikini
wake,chanzo cha matatizo yake na kuzikosa raha za dunia na wanawake wazuri!
Sisi sote tunamkasirikia
Mungu,Shetani,Waziri Mkuu,Rais,Bunge,Mawaziri au wakubwa Fulani,kuwa ndiyo
chanzo cha maafa Fulani.
Katika siasa,tunadai kuwepo UHURU WA
KUCHAGUA(Freedom of Choice) na uhuru wa kujieleza,kuandamana,kugoma n.k
Linapokuja suala la mtu mmoja mmoja kufanya
makosa na kupatwa na mabaya(consequences)
Kufuatia mabaya yaliyotendwa
zamani, tunaruka kimanga na kumsingizia Mungu,Shetani,Rais,Waziri Mkuu,Bunge na
serikali!
Unawezaje wewe kulazimishwa na Shetani kwenda
kubaka binti yako wa miezi miwili? Unawezaje kulazimishwa na Shetani kwenda
kumzini kuku ama mbuzi,kuua albino na kunyofoa viungo, kupora mali za watu n.k
Wewe huna uhuru wa kuchagua?
Huna uwezo wa kukataa jambo baya na kuchagua jema?
Nimkariri Mhariri wangu wa zamani, Muhingo
Rweyemamu, ambaye sasa ni Mkuu wa wilaya moja huko mkoani Pwani.
Kwamba, katika nafsi ya kila
mmoja kuna Nguvu Mbili
zinazoshindana-nguvu ya wema na uovu-Hata Paulo katika kitabu cha Warumi sura
ya 7 husema haya haya. Kuna Mbweha wawili katika nafsi ya mtu, Mbweha Mweupe na
Mweusi.
Tuchukulie kwamba falsafa hii hutwambia kuna
mbweha wawili wanakushawishi nafsini mwako. Mweusi anakushawishi kutenda baya,
Mweupe anakushawishi kutenda jema. Kwanini usichague jema,midhali una “Power of
Choice na Freedom of Choice?”
Tunadai uhuru,ukiwemo wa uchaguzi,tunadai
uwezo wa kuchagua. Mbona tunautumia vibaya? Mbona hatuwezi kuchagua,ila kila
mara tunalazimishwa kuchagua uchaguzi wa ovyo?
Bila shaka, ni kwa misingi
hii,tunahongwa gongo, sabuni na unga,kofia na t-shirt tunawachagua viongozi
wetu,halafu wakianza kuiba,tunalalamika!
Kama ulichagua kupewa rushwa ili mtu aingie
madarakani na kuamua kurejesha gharama zake alizokuhonga wakati wa kampeni ama
wakati wa uchaguzi, kelele za nini sasa?
Hii ndiyo “Consequences” ya hayo uliyochagua
vibaya zamani.Sasa unataka kumtoa kafara nani?
Nani chanzo cha makosa
haya,kama si wewe na uchaguzi wako mbaya?
Meli ikizama na kuua watu,wanasema ni Mungu
ametaka! Ohh ni tufani ilivuma! Abiria wakiingia kwenye boti isiyo na boya hata
moja,wakiumia wengine wakifa, wanaanza kulalama, ilijaa sana! Ilibeba mizigo na
hata petrol!
Huu ni uzuzu-hamna macho, hamwoni? Hujui
ukimbaka mtoto chekechea utafungwa maisha, sasa eti unamwambia Hakimu kwamba ni
Shetani! Acheni utoto.
Haya ya kukataa kuwajibika
kwa makosa yetu wenyewe, yamekuwepo tangu Adamu na Hawa. Hawa alipomwasi Mungu,
akasingizia Nyoka(Shetani),na Adamu alipoulizwa kwa nini yeye kila alichosema
mkewe akafuata bila kuhoji, akamsingizia Mungu kwamba kwanini alimuumba Hawa,na
kwa nini alimuumba nyoka, yaani Shetani?
Kwa nini dhambi iliruhusiwa? Tunauliza hivi
wakati madai ya Ulimwengu sasa ni uhuru(demokrasia) ili kufanya kila
jambo,kuandamana,kugoma,kukosoa hata Mungu mwenyewe n.k
Sasa, mlitaka Mungu amuue Shetani ili aonekane
Dikteta?Serikali ikimkamata Prof Lipumba au Dk. Wilbroad Slaa, kwa
uchochezi,mtasema kaonewa tu.
Je, Mungu angemfunga jela Shetani au kama
angemnyonga, tungesemaje? Shetani yupo kwa misingi ya demokrasia ile ile,ili
kila mtu achague cha kufanya.
Ukichagua vibaya usilalame na
kusingizia watu-ebu badili mkao-Change Position- batili mtazamo,uone kwamba
umekosea na sasa unatambua ulipoangukia,sawa? Acha kulalama kama chizi!
Tunachagua vibaya.Uchaguzi wa
ovyo. Adamu na Hawa walichagua ovyo wakaanza kulalama(Mwanzo3:13,17 na Mwanzo
4:9). Binadamu hutenda mabaya na kukataa kuwajibika. Meli inazama kwa uzembe,
SUMATRA wapo, serikali ipo na wewe mwenyewe unachagua kupanda meli mbovu,haina
boya hata moja,ukifa kizembe,lawama zinaanza-kaa chonjo wewe,acheni uzembe na
kulalamika!
Umeuza ardhi kwa mwekezaji,
sasa huna chakula,unasema “Hii serikali,sijui ya CCM!” Hivi AKILI ZETU ZIKO
wapi?Tumboni!
Utawala mbovu na rushwa na
ufisadi,matokeo yake ni wewe na mimi. Mimi ni chanzo cha rushwa. Rushwa
inapompa ndugu yangu cheo,na madaraka na pesa,mimi hufurahi kwamba sasa neema
imekuja. Mwisho wa siku, nchi inafilisiwa tunaanza kulia.
Angalia, unamsaidia mwanao kuiba mtihani,
anafaulu na kupata kazi nzuri serikalini,analipwa mshahara mzuri. Hakika huyu
mwanao ni mzuzu,mjinga,mbinafsi,mpuuzi na mwizi tu. Umma unapolia kwa huduma
zake za ovyo nawe unalia! Unalia nini wewe uliyeshiriki kuwaweka madarakani
watu wezi?
Tukitaka kupambana na rushwa na wizi na
ufisadi,tusianzie serikalini ama kwenye chama Fulani!
Tuanzie Katina nafsi zetu, ambamo kuna nguvu
mbili-naam mbweha wawili, MWEUSI na MWEUPE,tubadili mtazamo,tumchague Mbweha
mweupe atutawale-UCHAGUZI.
Naam,tunachagua vibaya sisi wenyewe. Unachagua
mke mbaya,mume mlevi halafu unasumbua watu. Unachagua kunywa gongo
iliyochanganywa na spirit, ukipofuka macho,unaanza lawama dhidi ya serikali.
Kuna watu hawataki kazi halali. Ni short
cut,kila kitu, shule, short cut, utajiri short cut,kuoa au kuolewa,short cut,
taabu ikitokea serikali, Mungu, Shetani, sijui mafisadi n.k mradi ni lawama na
maandamano na ghasia na migomo kila mahali duniani-hakuna kuwajibika!
Katika
Mwanzo 3:1-24 tunaona Adamu akiuza utawala wake kwa Shetani kwa hiari yake
mwenyewe maadam alichagua kufanya hivyo.
Matatizo yanapoanza, anayakataa. Jamii ndiyo
chanzo cha rushwa,wizi,mauaji,polisi wezi,waporaji,mawaziri mafisadi wanaolala
usingizi bungeni, marais na wafalme wakwapuzi n.k
Hawa wakubwa serikalini wanatokana na jamii.
Jamii bora huzaa Rais bora. Jamii safi huzaa wabunge wasafi ambao miongoni mwao
huwa mawaziri wasafi na wachapakazi.
Inawezekanaje Rais ndiye amwe mwizi eti jamii
iwe safi?
Rais safi huzaliwa na jamii
safi, siyo? Tuanzie wapi kufanya mapinduzi? Wajinga wanasema Rais ni tatizo,
hawajui sisi raia ni tatizo na chanzo cha haya yote.
Tunavuna tulichopanda. Tulipanda Upepo sasa
tunavuna Tufani. Sasa hawa walalamishi,kazi yao ni kuchungulia Rais anafanya
nini!
Iulize nafsi yako wewe
unafanya nini? Umekaa kijiweni kupiga politiki, sasa leo utakula hewa? Ukikosa
hela, badala ya kulaumu kwa kupoteza muda bure,unasema ni serikali hii ya
mafisadi! Acha uzoba!
Hawa unaowalalamikia nao wako kama wewe.Wewe
pia ukipewa madaraka,unapora kuliko!
TAKUKURU nao siku hizi
wanalalamika, polisi wanalalamika, mawaziri wanalalamika,wabunge
wanalalamika,Rais wan chi analalamika!
Tunalalamika. Nchi ya
walalamishi,vipofu walioshindwa kuwajibika!
Siku hizi wabunge wanalalamikia sheria ya
mafao ambao waliitunga wao! Sababu ni nini? Tumeacha maadili.
Maadili ni nini? Maadili ya mwafrika ni yapi?
Upendo! Tazama nyumbani kwako watoto unawafundisha nini?
Matusi, ulevi,uchafu nguo fupi,chafu,vitovu
nje, wakiwa Malaya na machangudoa mnasema, ‘watoto wa siku hizi’! Siku hizi
hajawahi kuzaa watoto! Watoto wenu mnawalea vibaya,wakiwa majambazi wezi na
waporaji mnalalama. Ukihonga pesa mwao awe polisi, anakwenda fanya nini kama siyo
kuhujumu raia na kushirikiana na majambazi na wezi? Sasa una lalama serikali
imeshindwa nini kulinda raia?
Haya yalianza zamani sana. Mtu anahonga,
anashinda mtihani, anapewa digrii hata ya chupi!
Matokeo yake ‘consequences’ yakifika.tunakataa
kuwajibika!
Mrisho Mpoto anasema, “Kila siku afadhali ya
jana” kweli maana kila siku kuna mbinu mpya za uporaji na uchakachuaji.
Afadhali ya jana kwa sababu
ile jamii ya jana ilikuwa afadhali. Raia wa Nyerere walikuwa waadilifu kama
Nyerere. Raia wa Kikwete wanafanana na Kikwete. Haiwezekani raia wawe wema eti
Rais awe tapeli. Tunafanana. Tuukubali ukweli, acheni kusingizia watu, sisi
tubadili tabia,tuwajibike nchi yetu itakwenda.
Shida ziko vizazi
vyote,tumeona ndege zikitekwa, watu akitaka kupindua serikali,malumbano,uhujumu
uchumi n.k
Kizazi hiki hakitaki kukubali kwamba sisi
ndiyo tatizo letu, wao ni chanzo cha shida zao wenyewe,mimi nina mchango mkubwa
wa umasikini wangu mwenyewe-uwajibikaji,ukweli nimeuacha,muda unapotea vijiweni
kujadili siasa wakati sina chakula. Mchawi wangu ni mimi,siyo Rais wala
mwingine yeyote.
Wanasiasa tuachane nao-wote
hufanana kama ndizi katika chale moja.
Wote ni rangi moja, wanakula
pamoja,mama yao ni mmoja, na wote wamepinda-hakuna mwanasiasa aliyenyooka.
Politicians are like a bunch
of bananas, they hang together; all are yellow, but there is no a straight one!”
Itaendelea
0786/0713-324 074
No comments:
Post a Comment