ARISTOTLE (384-322
BC) ni miongoni mwa wanafalsafa wa Ugiriki, ambaye wakati wa uahai wake aliwahi
kusema hivi:
“To say of what is not, or of what is
not that it is-is FALSE. While, to say what of what is that it is and of what
is not that is not, is TRUE!!”
Falsafa
ngumu hii ya Aristotle nimeitafsiri hivi:
“Kusema namna kitu ama jambo lisivyokuwa ni
UONGO,wakati kusema namna jambo au kitu kisivyokuwa wakati kweli hakiko
hivyo,huu ni UKWELI”.
Naam.Ukweli
unaweza kuongopa,pindi nusu ukweli unaposimuliwa au kuzungumzwa,kwa nia ya
kuongoza watu kwenye UONGO.
UKWELI ni
nini basi?
Kulingana na
wanafalsafa, Ukweli ni mwafaka baina ya matukio na uhalisia wa mambo(Truth is
Agreement with Facts and Reality).
Aghalabu,natamani
kuwa mkweli siku zote, ili nisimulie matukio yaliyowahi kutukia duniani kama
mifano hai ya uhalisia wa mambo,kwa lengo la kuwaongoza wasomaji wangu wote
katika ukweli.
Kwa mfano:
Nisemapo, “Amara Kanu Nwanko ni mke wa mwanandinga nguli wa Nigeria,Nwanko
Kanu”, nasema Ukweli.
Pia nikisema
Barack Obama wa Marekani, ni Rais wa
Marekani ambaye hana maslahi yake hapa Afrika, na Mwafrika kumshangilia sana na
kumtegemea ni kupoteza muda wake bure, nasema ukweli mchungu.
Tuukubali ukweli,ili utuweke huru-ukweli
huwaweka watu huru kweli kweli.
Sasa, niseme
kwamba Tanzania kuna magaidi wa mafanikio yao wenyewe. Kila mtu gaidi wa
mafanikio yake, aghalabu ni yeye mwenyewe na wanaomzunguka.
Nimekuwa
nikiandika harakati za magaidi,kwamba siyo majambazi wa kawaida ama
majangangili wanaofanya uhalifu kwa nia ya kujipatia chumo la faida.
Magaidi wa
sura ama mtazamo sawa na wanaharakati wa Haki(za Binadamu?)wanapopigania mambo
yao na maslahi yao.
Kama vile
magaidi wa kawaida, kupigania haki kwa njia hii,ni lazima kupora haki za
wengine. Kujitoa mhanga na kupoteza maisha maana yake ni kupoteza haki ya
kuishi kwa nia ya kuwaangaza wengine.
Neno ‘mhanga’ ama ‘wahanga’ halimaanishi watu
waliopatwa na ajali kama ya Mv.Skagit huko Zanzibar. Hakuna wahanga wa
Mv.Skagit hata kidogo, bali kuna waathirika wa ajali ya meli,basi ama ndege.
Kujitoa mhanga, ni kuwa hiari kufa kwa ajli ya
jambo Fulani(harakati) na wala hakuna watu wanaojitoa(wanaopenda) kufa ajalini.
Waandishi wa habari wameuwa wakiongea Kiswahili kibovu sana kwamba ‘wahanga’ wa
ajali!
Wanaharakati,hususan
magaidi hujitoa mhanga,huwa radhi kupoteza maisha yao na ya wengine ili kupigania maslahi Fulani.
Hii siyo
haki aslani. Ni nusu haki na nusu dhuluma. Nusu haki na nusu dhuluma haiwezi
kuwa haki, na haiwezi kuwa kweli. Twende na msingi huu.
Tanzania
kuna harakati za kigaidi zilizoanza zamani sana; kwa kile kiitwacho harakati za
UKOMBOZI dhidi ya UTUMWA Mamboleo,ukoloni ama mfumo kandamizi.
Kuna
ufisadi,ubwenyenye,ubeberu,pasipo uhuru ama usawa n.k
Feburuari
26, mwaka 1982,Ndege ya Boeing 737 ya Shirika la Ndege Tanzania, “Tango Charlie
207” iliyokuwa na Jina, ‘Kilimanjaro’ mbavuni, ilitekwa na magaidi wa
ki-Tanzania.
Waliilazimisha
kwenda London. Ilikuwa na abiria 74 na wafanyakazi watano,na ilitokea katika
Uwanja wa Ndege wa Mwanza na ilitaka kusafiri hadi Dar es salaam, magaidi hao
walipotokea na kuiteka nyara,wakailazimisha kwenda London!
Iliendeshwa
na Kapteni Deo Mazula,wakati huo wakati mimi nikiwa kijana mdgogo,nikipenda
sana kusoma hadithi za Upelelezi,hususan za wateka nyara wa Kipalestina,na
makomandoo wengine mahsusi.
Nimeandika
sana juu ya ndege ya Ufaransa, Air France Air Bus, iliyotekwa nyara na
kulazimishwa kuja kutoa Entebbe,Uganda,mwaka 1976. Zilikuwa harakati za kudai
haki,lakini haki hizi ziliondoka na maisha(haki ya kuishi) ya watu wengine
wasio na hatia-Hii aslani siyo haki na si KWELI. Tuendelee na msingi huu
kwamba,nusu haki na nusu ukweli siyo ukweli.
Turejee kwa
wateka nyara wa ki -Tanzania mwaka 1982.
Yassin
Membar(21),Mohammed Tahir(21),Abdallah Ali Abdallah(22),Mohammed Ally
Abdallah(26) na kiongozi wao Musa Membar(26) waliteka ndege hiyo ya ATC kwenye
uwanja wa ndege wa Mwanza, wakailazimisha kwenda London, Uingereza.
Lilikuwa
jambo la tashtiti.Walikuwa na silaha mwanasesere.Walikuwa magaidi wanagenzi.
Usalama
dhalili katika uwanja wa ndege wa Mwanza uliwawezesha kuingia ndegeni na midoli
ya bastola na kuwatisha abiria,rubani na wafanyakazi wa ndege hiyo.
Uwanja wa
ndege wa Mwanza, umeendelea kuwa dhaifu kiulinzi hadi miaka ya karibuni, mtunzi
wa Filamu ya Mapanki, The Darwin’s Night Mare, Hubert Sauper alipoingia na kamera katika chumba cha
kuongozea ndege na kuanza kupiga picha nyuki wakiranda katika vioo vya
dirisha,kisha alipiga picha maeneo ya kijeshi, jambo ambalo lilikuwa hatari mno
kwa usalama wa nchi.
Sauper,ni
raia wa Australia aishiye Ufaransa, na alisema mwenyewe kwamba alifanikiwa
kupiga picha hapa kwa sababu aliwapa wahusika rushwa ili afanikishe Documentary
yake iliyompa tuzo ya Oscar.
Naam. Wale
jamaa, akina Musa Membar, waliwateka nyara abiria,wakaikagua ndege na kupata
bastola halisi tena ‘revolver’ iliyokuwa katika chumba cha rubani.
Walipata
bastola nyingine yenye risasi baada ya kuwapekua abiria.
Tena,
walinyakua Shotgun mbili zilizokuwa na risasi ambazo zilikuwa mali ya abiria,
zilihifadhiwa kizembe-Hivyo safari ya London ikakolea bila wasiwasi.
Kwa kifupi,
ndege hiyo ilikwenda London,na ilikuja kurejeshwa na abiria wake 74 Machi 4,
mwaka huo wa 1982, wakapokelewa kishujaa sana Dar es salaam, nakumbuka Radio
Tanzania Dar es salaam ilitangaza ‘Live’ marejeo ya ndege hiyo.
‘Magaidi’
hao walifungwa London kati ya miaka mitatu na minne kwa makosa ya ugaidi,hata kama walikuwa na madai
mazuri nitakayoeleza punde. Ilikuwa
kumkimbia Shetani na kutafuta hifadhi ya ukimbizi kwa Ibilisi!
Sababu za
akina Membar kuteka nyara ndege,ni maisha magumu,ukosefu wa ajira hususan kwa
vijana kama wa zama hizi, umangimeza wa utawala wa Hayati Mwalimu Nyerere, na rushwa kama ufisadi wa siku hizi. Tabia ya mtu kuharibu hapa na
kuhamishiwa kwingine haikuanza leo.
Kumbuka, Mwalimu hakutawala kama zama hizi za ‘domo
kaya’ tunazoita za “Freedom of Expression” zama hizo Usalama wa Taifa
waliogopwa kama radi! Siku hizi mnawatukana hata baa,zamani walihesabu vizibo
vya bia!
Zama hizi
ndizo Marehemu Rammadhan Ongala ‘Remmy’ aliimba kwamba fundi viatu alipewa kuwa
Mkuu wa FAT unakumbuka, msomaji?
Nataka
kusema kwamba, hao akina Membar wangeteka nyara ndege leo na kwenda London
kusema maisha ni magumu sana na hali ni mbaya ndiyo maana wamechukua uamuzi
huo-WANGESHANGILIWA SANA!
Wangeonekana
wanaharakati,mashujaa,wanamapinduzi, walioandamana kueleza hisia zao!
Wanamapinduzi
huwa na imani thabiti juu ya mabadiliko ya kisiasa,kijamii na kiuchumi; hudai
kufanya harakati kwa maslahi ya jamii nzima. Hawa wa kwetu hapa,ni domo kaya tu.
Siku hizi,huwa
nasikia watu wengi vijiweni wakisema Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa Rais mzuri
sana, kama malaika!
Huwa nacheka
sana!
Nakumbuka
akina Kapteni Tamimu, Uncle Tom, na wenzao waliposema walilazimika kutaka
kuipindua serikali,kwa sababu ya hali mbaya,upendeleo,rushwa,maisha
mabaya,magumu hata wanajeshi kuvaa viraka!!
Najua,baada ya vita vya Kagera(Novemba
1978-Aprili 1979) nchi ilitumia takriban Dola za Marekani milioni 500 kwa
gharama za kumtia adamu na kumpindua Nduli Idi Amin.
Askari wetu
620 walipoteza maisha katika vita hivyo, nchi ikafilisika,bidhaa madukani
zikapotea,watu tukavaa matairi ya magari miguuni!
Nataka
kusema kwamba, hali mbaya ya uchumi haikuanza jana hapa nchini.
Tumetumia
majani ya mipapai kufua nguo,tumewahi kuunga majivu badala ya chumvi sisi,
wakati huo vijana wadogo.Ingekuwa hivyo leo mngeandamana sana.
Kwa nini akina Membar na akina Uncle Thom
hawakushangiliwa kwa ‘ugaidi’ wao zama hizo?
Hazikuwa
zama za haya ya sasa, siyo kwamba watu walikuwa wajinga.Walikuwa
wastahimilivu,wazalendo tena wasikivu na wachapakazi.
Kwanini
wananchi walichanga ng’ombe,mbuzi na udaga wao kugharimia vita ya Kagera ? Hawa
wapenda raha na walalamikaji wangechanga nini? Hata kama wangechangia vita,
michango ingeporwa hata kabla ya kufika Mstari wa Mbele, hawa huibia hata
majeruhi na marehemu wa ajali hata ya Meli ya Mv. Bukoba! Utajiri wa Damu!
Hakika sisi
Watanzania hamnazo! Leo,tunasikia watu wakisema eti tupigane sisi kwa sisi
mafisadi wametamalaki! Uzuzu!
Eti tumekuwa
na amani saana, sasa yatoshaa!! Eti ili nchi iendelee lazima vije vita kwanza.
Kweli tumechoka na amani, ama utulivu tunataka vita? Vita mwavijua vizuri
nyie?.
Siyo kwamba
tunataka mapinduzi ya fikra na mitazamo ya wizi wizi tu na ‘shortcut’ na deal
ambazo ni za wizi?
Hata
hivyo,kila kiongozi huwa bora baada tu ya zama zake kupita.
Nyerere sasa
ni bora maana zama zake zimepita. Alipokuwepo nimesema watu walitaka kumuua
Jumapili moja Kanisani nadhani Mtakatifu Joseph,Dar. alipokwenda kuabudu, na
wengine ndiyo hao walioteka nyara ndege,ili watafute ukimbizi London, wakaishia
kolokoloni.
Walisema, Nyerere alitawala
kimabavu,kidikteta,kimangimeza n.k.Walitamani aondolewe, hakuondoka-siku hizi
anakaribia kuitwa Mtakatifu Nyerere! Watu Bwana!!
Walimbatiza
jina la ‘Nabii Musa’kwamba miezi ile baada ya vita ilifananishwa na safari ya
Waisraeli kutoka Misri kwenda Kanani.
Akina Membar
walipofika London walijidai kutumwa na Abdulrahman Mohamed Babu aliyekuwa
Mkimbizi wa kisiasa na alirejea nchini wakati wa vyama vingi,miaka ya 90.
Ukweli kwa
mujibu wa Aristotle, ni kwamba hata wakati wa Nyerere kulikuwa na shida kama
hii ya sasa.
Watu wajinga
walidhani mapinduzi ya umwagaji damu ama ugaidi ilikuwa ndiyo suluhu ya
matatizo,kumbe wapi bwana!
Leo,tunasikia
mambo ya kutisha,utadhani hakuna kinachoendelea. Tunaona watu
wanakasirika,migomo,maandamano,watu wanapigwa risasi na mabomu ya machozi.
Akina Dakta
Ulimboka sasa wanatekwa nyara kama zama zile za akina Membar kuteka nyara ndege
n.k Kuna machafuko na madai ya haki kama zama zile. Lakini namna ya kutafuta
suluhu ni tofauti sana ni ‘Violence’ badala ya kile alichosema Mpigania Haki za
Weusi Marekani, Martin Luther King Jr. “Nonviolence Resistance”.
Nimetumia
‘Facts’ ili kusema ukweli kwamba hakuna wakati watu walipokuwa hawalalamiki
hapa duniani,siyo hapa nchini tu. Hata Marekani, Wall Street ,kuna maandamano, Uingereza kuna migomo hata sasa
wakati wa Olimpiki. Mbinguni,kuliwahi kuwa na maandamano na mgomo,Lusifa
akamgoma Mungu,muumbaji wake, Soma Ufunuo 12.
Nataka
niwaambie Watanzania, hali mbaya na wakati mgumu wa uchumi vipo mara zote tangu
zamani,na tuendako mbali na kuvumbua mafuta,gesi na robot,hali itakuwa mbaya
sana.
Mara zote,
wanaharakati huamka kudai hali bora zaidi na maandamano hufanywa ili kudai haki
zaidi,maendeleo zaidi-maendeleo hayana mwisho.Hii ni dhana ya mapinduzi watu
kutafuta hali bora zaidi.
Sasa,
tutafute hali hii bora kwa akili. Tusianze kupigana na kuuana kwa kisingizio
cha uchumi mbaya na rushwa miongozi mwetu.
Juzi,
nilikwenda kwa Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Jijini Mwanza,MWAUWASA,Robert
Masunya, nikamwambia,
“Sisi hatuna
maji ya bomba sasa ni karibu siku nne,watu wanatumia maji machafu,kwa nini?”
“Mimi
nakwenda msibani, hilo gari hapo linaningoja mimi”, alisema huku akinionesha
hilo gari linalomngoja.
“Hiyo habari
ya msiba unaokwenda ndiyo jibu la matatizo yetu ya kukosa maji Mwanza,hadi
akina mama wanaamka saa 9 usiku kwa mwezi mzima?” nilimuuliza.
“Sasa wewe
unanilazimisha niseme nini? Una kitu (mali)gani wewe?” alisema.
Looh,nilishangaa.
Yaani huyu
ananiuliza mimi nina nini,yaani masikini kwa kuwa nimeuliza ukosefu wa maji kwa
siku nne mfululizo?” Nilijihoji. Hayo ya mali yalikujaje?
Huyu, siyo
serikali. Ni miongoni mwa jamii yetu hii isiyojali shida za wananchi. Kaajiriwa
katika taasisi ya umma, lakini wajibu wake hajui. Hajui kuwa hajui.
Anaona mambo
binafsi{kafa mtu mmoja) ni bora hata wafe milioni kwa kipindupindu kutokana na
kunywa maji ya vinyesi huko visimani!
Sasa,
tukipigana vita ndiyo tutawaondoa akina Masunya? La hasha.
Vita havijapata kuleta haki. Dawa ya moto si
moto,ni maji. Inawezekana bomu la Atomiki huko Nagasaki na Hiroshima lilimaliza
vita vya Pili mwaka 1945. Lakini, risasi moja hutosha kuifanya nchi Jehanam.
Irak kuna
vita tangu mwaka 2003, matatizo yao yameondoka? Kawaulizeni Somalia ama Libya.
Nataka
kusema kwamba, nusu ukweli siyo ukweli,tujifunze kutokana na historia, ili
kujua ukweli na kinachoujia ulimwengu,kufuatia kulipa visasi.
Nawashauri
watu kusema,kupinga dhulula mioyoni mwetu kwanza na katika familia zetu
kwanza,kabla ya kunyoosha vidole kwa wenzetu. Karibu watu wengi ni mafisadi
watarajiwa.wakipewa vyeo ni uporaji tu wa mali ya umma! Hao wapiga kelele wa Bungeni,Dodoma wawasikia?
Niliwahi
kuandika katika gazeti la Rai kwamba, “Kawimbo “Mafisadi” katamu,lakini waimbaji wake
hunuka mithili ya kwapa la Ibilisi!
Wabunge
karibu wote wanatuhumiwa kuwa mafisadi,mara TANESCO,IPTL,RICHMOND sijui EPA.
Shime tuanzie
myoyoni mwetu wenyewe kupigana vita vya kupinga dhuluma. Vita hivi tuvipige kwa
wema myoyoni mwetu, si baya kwa baya dhidi ya wenzetu. Tutafute haki kamili na
si nusu haki,kwa maslahi ya taifa letu. Tumepungukiwa Upendo wa Agape. Agape ni
nini?
Itaendelea
0786 324 074
www.congesdaima@yahoo.com
nimejifunza kitu hapa, thanks
ReplyDelete