Mwangwi wa A-Shabaab Nairobi, watikisa wasafiri Ziwa Victoria
*Mabadiliko
ya Tabianchi yatishia meli kuparamia miamba na kuzama
Na Conges Mramba, Mwanza
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari(TPA),
imewapandisha kizimbani wamiliki wa meli binafsi, kwani wanazuia Mamlaka hiyo
kusimamia usalama wa abiria na mizigo, hata wakati huu wa kitisho cha magaidi
wa Al-Shabaab,Afrika Mashariki.
Mkuu wa Bandari(Port Master)Mwanza, John
Mutalemwa, katika mahojiano maalum na gazeti hili juzi, alisema wamiliki hao wa
Bandari binafsi wanashindana na Sheria Na. 17(Tanzania Port Act) ya mwaka 2004.
Sheria hiyo
inaipa TPA nguvu ya kusimamia bandari
zote, zikiwemo za watu binafsi,ili kukagua usalama wa abiria na mizigo,kabla na
baada ya safari.
“Sheria inatupa Mamlaka ya kusimamia bandari
zote zikiwemo bubu, tukague na kujua
mizigo kiasi gani inasafirishwa; tunatakiwa kutazama abiria ikiwa wanalingana
na uwezo wa meli au boti,kulinganisha na uwezo wa chombo chenyewe, halafu tunatoa, “Port Clearance”
kabla ya meli kuanza safari”, Mutalemwa alisema.
Kwa mujibu
wa Mutalemwa, vipo vyombo vya usafiri majini,huchukua abiria na mizigo kuoita
uwezo. Hii ni kazi ya TPA kufanya ukaguzi makini,ili kuondokana na Ajali Ziwa
Victoria.
“Bandari ni mpaka wa nchi. Lazima tusimamie
hali ya usalama, meli inaweza kuleta Al-Qaeda ama Al-Shabaab, nap engine inaweza
kuingiza nchini silaha kutoka nchi za vita na migogoro. Eti wanakataa
tusiwasimamie…tumewafungulia kesi mahakamani”,Mutalemwa ameliambia gazeti hili
katika mahojiano Maalum ofisini kwake juzi.
Meli za mizigo za Jijini Mwanza, hufanya
safari zake hadi Port Bell, Uganda,na Kisumu nchini Kenya, ambako sasa magaidi
wa Al-Shabaab wanasaidia kuzimu kupanua kinywa chake.
Aidha, Mkuu huyo wa Bandari Mwanza amesema
nchi za Maziwa Makuu kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na Burundi hazina
amani, na Kenya hamkani si shwari,kufuatia kitisho cha Al-Shabaab, wanaopinga
majeshi ya nchi hiyo kuingia Somalia kuwafulusha magaidi hao.
Kufuatia
hali tete ya usalama nchi jirani, Mutalemwa amesema lazima Mamlaka yake kuwa
macho na usalama wa abiria na mali zao dhidi ya hujuma za magaidi, wanaoweza
kupata upenyo wakaingiza silaha nchini kupitia Ziwa Victoria.
Mamlaka ya Bandari humiliki bandari za Mwanza
Kaskazini na Kusini,Nansio Ukerewe,Kemondo Bay na Musoma.
Vituo
vingine vidogo vinavyomilikiwa na TPA ni Maisome,Nkome,Bukondo,Kahunda,Miharaba,Kome,Buchosa,Solima,Karumo,Chato
na Nyamirembe(Kagera) na Kinesi mkoani Mara.
Bandari ya Mwanza ni kiungo muhimu kwa nchi za
Maziwa Makuu,hususan Uganda na Kenya,na
huchangia kwa kiwango kikubwa kukua kwa shughuli za uchumi,hata katika nchi
wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki(EAC).
Ripoti ya Malka hii iliyotolewa kwa Kamati ya
Bunge ya Miundombinu(nakala tunayo), inasema bandari ya Mwanza ingeweza
kusafirisha abiria milioni moja kwa mwaka.
Ingeweza kusafirisha tani mamilioni za moja za mizigo,kama Reli ya Kati ingekuwa
inafanya kazi kwa ufanisi. Hili ni eneo muhimu kwa ukuaji wa uchumi wan chi,lakini
kinyume chake ni hasara kila upande.
“Huduma hafifu za Reli zimesababisha shehena
ya kahawa kutoka Uganda na hata Bukoba,kubadili njia(route) na kupitia Bandari
ya Mombasa,Kenya “, Ripoti hii inasema.
Kufuatia huduma duni za Shirika la Reli,
Bandari za Mwanza ziko taaban,kwa sababu ya kupungukiwa mapato, zinaendeshwa
bila faida.
Kulingana na Ripoti hii kwa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu,katika kipindi cha miaka mitano,kuanzia 2006/2007 hadi 2010/2011,
mizigo imepungua katika Bandari za Mwanza kutoka tani 480,568 hadi 248,860
mwaka 2011.
Utendaji
mbovu wa lililokuwa Shirika la Reli(TRL) ulisababisha treni iliyokuwa
ikisafirisha abiria na mizigo kati ya Mwanza na Bandari ya Dar es salaam
kusimamishwa.Hali hii husababishwa abiria na mizigo kubadili njia na kukosesha
mapato bandari za Mwanza.
Wafanyabiashara wa Uganda wanasafirisha bidhaa
zao kupitia bandari ya Mombasa,nchini Kenya.Shehena ya kahawa kutoka Uganda
iliyokuwa ikipitia bandari za Mwanza, inapitia Mombasa na hivyo kupunguza
kiwango cha mizigo kutoka tani 250,000 mwaka 2007 hadi tani 100,000 mwaka
2009/2010.
Kufuatia madudu ya TRL, hata abiria wamepungua
katika bandari za Mwanza kutoka abiria 891,634 mwaka 2007 hadi abiria
593,342.Huu ni upungufu wa asilimia 6.3 unaoikosesha nchi mapato na fursa za
ajira kwa watu wake.
Ripoti hiyo ya TPA, imebaini kwamba, wasafiri
wa vyombo vya majini Ziwa Victoria wamepungua kufuatia ushindani uliopo wa
barabara,hususan baada ya mtandao wa barabara kukamika ujenzi kwa kiwango cha
lami.
Kati ya Mwanza na Bukoba kuna usafiri wa ndege
ambao huchangia pia abiria wasisafiri kwa meli.
Kufuatia
hali hiyo,ripoti hiyo imebaini kuwa Kampuni ya Huduma za Meli,Marine Services
Company(MSC) iko hatarini kufilisika,kufuatia meli zake kuharibika mara kwa
mara,kitu kinachodaiwa na baadhi ya abiria kuwa ni hujuma za baadhi ya
wafanyakazo wa MSC ili kuwanufaisha wenye meli binafsi.
Kaimu Meneja Mkuu wa MSC, Projest Kaija,
ameliambia Mwanahalisi kwamba madai
hayo hayana ukweli, kwa kuwa kuhujumu kampuni unayofanyia kazi maana yake ni
kuhujumu mshahara na mapato yako.
“Je,
unahujumu Kampuni namna hiyo ili kampuni ikifa wewe utoe wapi mshahara?’ Kaija
alihoji.
Siku za karibuni MSC imewaondoa viongozi wa
Kampuni hiyo na kuwaweka wapya ili kuboresha ufanisi na kupunguza nakisi.
Kwa kipindi cha miaka mitano, idadi ya meli
zilizohudumiwa na Bandari za Mwanza, imepungua kutoka 2,684 hadi meli 1,900
mwaka jana.
Bandari ya
Mwanza pia huendeshwa kwa hasara ya mamilioni ya shilingi kila mwaka,nakisi ni
takriban shilingi bilioni 4.5
Mabadiliko
ya Tabianchi na Ongezeko la Joto Duniani,pia hutishia USALAMA wa usafiri Ziwani
Victoria.
Kwa kipindi
cha kati ya mwaka 1998 hadi 2006,maji ya Ziwa Victoria yamepungua kutoka mita
1,141.24 juu ya usawa wa bahari hadi mita 1,139.20. Upungufu ni wastani wa mita
2.04.
Kulingana na
Ripoti hiyo, meli nyingi zimekuwa zikishindwa kufungwa katika bandari za Mwanza
na Nansio,Ukerewe. Kupungua kwa kina cha maji ya Ziwa hili pia huweza
kusababisha kuzuka kwa miamba ambayo huhatarisha usalama wa meli na boti na
usalama wa abiria,hasa wanaposafiri nyakati za usiku.
Meli
zinapoparamia miamba hutoboka na kujaa maji,ama kuwa katika hatari ya kuzama.
Ziwa Victoria ni chanzo cha Mto Nile, ambao
huanzia katika Maporomoko ya Owen,Uganda; maji husafiri umbali wa zaidi ya
kilomita 6,900 hadi Misri. Mvua za masika zinaponyesha Afrika ya Mashariki
hubeba rutuba mezi ya Aprili na Mei na rutuba hiyo hufika Misri kati ya Agosti
na Septemba na kuwawezesha Wamisri kupata rutuba jangwani.
Mto Nile ni mungu wa Wamisri. Miungu ya Misri
ina ‘mama’ yao Ziwa Victoria. Ni kwa sababu hii, mwaka 1929 na 1957 Misri
walitiliana saini mkataba na Wakiloni wa Kiingereza kuzuia matumizi ya maji ya
Ziwa Victoria kwa shughuli za kilimo na hata vyanzo vya umeme kama kilichopo
Jinja.
Aidha,kupungua kwa kina cha maji ya Ziwa hili
hufanya meli kutia nanga katika maji ya kina kirefu,na huku ni kuhatarisha
maisha ya abiria,hasa katika maeneo ya visiwa.
Mkuu wa Bandari ya Mwanza, John Mutalemwa
anasema Mamlaka yake imelazimika kuchimba mchanga katika bandari za Mwanza ili
kuongeza kina cha futi tatu ili kuwezesha meli kufunga gatini.
Mradi kama huu unafanyiwa upembuzi yakinifu
katika bandari ya Nansio,Ukerewe,lengo likiwa kujenga gati imara na salama.
Mpango wa
serikali wa kuunganisha Reli kutoka Tanga hadi Musoma kupitia Arusha, utaweza
kurejesha wingi wa abiria na mizigo katika Bandari za Mwanza, au abiria na
mizigo ya Uganda,Rwanda,Burundi na Congo wanaweza kutozifikia kabisa bandari za
Mwanza,na hivyo kuleta kifo cha mende kwa TPA na Meli za MSC.
Ziwa Victoria
ni fursa muhimu kwa Tanzania katika Soko la Pamoja la EAC,lakini fursa hii
inaachwa kwa wageni kupitia hujuma na ufisadi unaofanywa na maofisa wa
mashirika ya umma kama TRL na MSC.
www.congesmrambatoday.blogspot.com
0786 324 074
No comments:
Post a Comment