Na Conges
Mramba, Nansio
MAMLAKA ya
Udhibiti Usafiri Nchi Kavu na Majini(SUMATRA) inadaiwa kushindwa kusimamia
ukaguzi wa vyombo vya majini Ziwa Victoria, hivyo kusababisha hofu ya kuweza
kutokea ajali.
“Maofisa wa SUMATRA wanapotoka Dar es salaam
kuja Ziwa Victoria kuendesha zoezi la ukaguzi,wanawashurutisha wamiliki wa
vyombo vya majini kuwalipia gharama za chakula na malazi hotelini”, Gazeti hili
limedokezwa.
Nahodha wa
Meli moja ya kampuni binafsi, ameliambia Gazeti hili kwamba,kitendo cha maofisa
wa SUMATRA kupewa hisani ya gharama za chakula,malazi na maburudisho wakati
wanapofanya ukaguzi wa vyombo vya usafiri majini Ziwa Victoria,huhafifisha
ubora wa vyombo husika,na changamoto kwa manahodha na mabaharia.
“SUMATRA,
wanapofika Mwanza,toka Dar es salaam, wanakula na kulala kwa gharama za
wamiliki wa meli na boti hapa Ziwa Victoria, sasa watakagua nini kama siyo
kulipa fadhila kwa yale waliyotendewa na wamiliki wa meli ama boti?” Amehoji
Nahodha wa Meli moja kwa masharti ya kutotajwa jina wakati wa mahojiano na
gazeti hili.
Tumemtafuta
Ofisa Uhusiano wa SUMATRA, David Mziray, kwa takriban juma zima,ili
kujibu tuhuma hizo, lakini simu yake ya mkononi ama iliita pasipo majibu, ama
ilikuwa imefungwa.
Hata hivyo, Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA,Mkoani
Mwanza, Alfred Wariana, amesema maofisa wa SUMATRA kutoka Dar es Salaam,hufika
Mwanza kufanya ukaguzi wa kila mwaka,na hulipiwa gharama za usafiri,malazi na
chakula na Mamlaka, na wala siyo wamiliki wa vyombo vya usafirishaji Ziwa
Victoria.
Jumapili, Mei 27 mwaka huu,mwandishi wa
makala haya alisafiri kutoka Jijini Mwanza,kwenda Nansio,Ukerewe kwa Meli ya
Mv. Samar II inayomilikiwa na Kampuni na Kampuni ya Samar Filling Station,ya
Mwanza.
Hii ni meli
iyojengwa mwaka 2009 na Kampuni ya Songoro Marine Transport pia Jijini Mwanza,kama
meli ya mizigo. Ilikuwa ikifanya safari zake kati ya Mwanza na Uganda.
Meli hiyo ilibadilishwa matumizi mwaka huu,
ikawekewa viti na kuanza kusafirisha abiria kutoka Mwanza hadi Nansio,Ukerewe.
Uwezo wake ni kuchukua abiria 248 na tani kati ya 101 na 138 za mizigo.
Nilimuuliza Nahodha wa meli hii,Kapteni Adam
Andrew Alex, “Meli ina vifaa vya uokozi kwa kiwango gani?”
“Ina
maboya(life rings) 60 na life jackets 350.Tuna mashua moja na vifaa 10 vya
kuzimia moto”, Kapteni Alex alisema.
Kutoka Jijini
Mwanza hadi Nansio, mji mkuu wa wilaya ya Ukerewe yenye visiwa 27 na vingine 11
visivyokaliwa na watu kuna umbali wa mali 29 za majini.
Kapt.Alex
anasema alihitimu katika Chuo cha Mabaharia, Dar es salaam Maritime Insitute,
na alikuwa na uzoefu wa mwaka mmoja kazini. Akasema meli yake ilikuwa na
mabaharia tisa wenye uzoefu wa kati ya miezi sita na mwaka mmoja kazini.
Akizungumzia mazingira ya kazi, amesema
mikataba ya ajira katika vyombo hivi vya binafsi haiendani na kazi, “Hakuna
hata malipo ya muda wa ziada wa kazi(over time),wala hakuna usafiri baada ya
kazi”, Kapt. Alex amedai.
Eferi Bulongo(75) ni miongoni mwa abiria
waliosafiri na meli hiyo, Samar II kwenda Nansio. Nilimuuliza, “Una maoni gani
kuhusu usafiri Ziwa Victoria?”
“Sipendi kusafiri kwa meli binafsi;zinasumbua,
ratiba ya safari haieleweki,ni namna wanavyojisikia wao, na melini hakuna
mahitaji ya lazima ya kuaminika kama chakula na vinywaji;kuna chai”, Bulongo
amedai.
Amesema, meli za Mashirika ya Umma,kama Marine
Services Company(MSC) ni bora kabisa, ratiba ya safari huzingatiwa.
“Hizi meli
za MSC zinahujumiwa na baadhi ya wafanyakazi wake.Labda wanapewa rushwa na wamiliki
wa meli za binafsi ili meli za MSC ziache kufanya huduma ili wafanye biashara, abiria wengi hawazipendi
hizi meli binafsi”, Bulongo amesisitiza, huku akihoji, “Kwanini Meli za MSC
ndizo ziharibike kila kunapokucha? Mv.Clarias haijafanya kazi kwa zaidi ya
miezi minne; sasa wamesikia Bunge la Bajeti karibu kuanza, ndiyo tunasikia
itaanza kati ya kesho(Mei 27) na kesho”, anasema Bulongo.
Nikampigia simu Kaimu Meneja Mkuu wa
MSC,Projest Kaija kujibu tuhuma hizo.
“Leo,
Jumapili Mei 27, tunaifanyia majaribio Mv.Clarias. Baada ya siku chache itaanza
safari zake kwenda Ukerewe”, Kaija anasema.
Anakanusha kuwepo kwa tuhuma zenye lengo la
kuhujumu Kampuni ya umma kwa nia ya kuwanufaisha wenye meli binafsi.
“Wafanyakazi
wa MSC wanawezaje kuhujumu kampuni inayowapa mshahara?” Anahoji,huku
akisisitiza kuwa tuhuma hizo zitachunguzwa,kwa kuwa uongozi wa kampuni hiyo ya
umma umebadilishwa siku chache zilizopita; kampuni inafanya matengenezo(reform)
anuwai.
Nikampigia simu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Everest
Ndikilo,ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa, kumsaili:
“Kwanini
abiria wanapopanda katika vyombo vya majini Ziwa Victoria hawakaguliwi, ili
kubaini uwezekano wa kuwepo kwa magaidi kama Al-Qaeda na Al-Shabaab, wanaotishia maisha ya
watu nchi jirani ya Kenya?”
Magaidi
waliwahi kuteka nyara ndege ya Air Tanzania(ATC)mwaka 1988 , yenye maandishi
ubavuni, ‘Tango Charlie” wakati ikipaa kutoka uwanja wa ndege wa
Mwanza,ikalazimishwa kwenda Jijini London ambako hatimaye jumla ya wateka nyara
watano raia wa Tanzania walihukumiwa kifungo cha kati ya miaka mitatu na mitano
jela,Jijini London.
“Ulinzi na Usalama ni Ajenda ya kudumu na siyo majini tu, hata kwenye
majengo,mahoteli na makazi ya raia”, Mkuu wa Mkoa Ndikilo anasema.
Kuhusu
maofisa wa SUMATRA,kutoka Dar es Salaam kulazimisha kulipiwa gharama za ukaguzi
na wamiliki wa vyombo ziwa Victoria, Ndikilo akasema, “Kama jambo hilo
lipo,basi ni tatizo kubwa,nitafuatilia ili hili likemewe”, Ndikilo akasema.
Gazeti moja litolewalo kila siku hapa nchini
kwa lugha ya Kiingereza, katika toleo lake la Mei 23 mwaka huu lilisema
kwamba,mwaka 1996 Mv.Bukoba ilipozama na kupoteza maisha ya abiria wake
takriban 1,000; miongoni mwao alikuwemo Abu Ubaidah al-Banshiri, ambeye alikuwa
nambari mbili wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda.
Naam, kundi
hili la AlQaeda, lilianzishwa na Osama bin Muhammad bin Awad bin
Laden,Feburuari mwaka 1998 kwa jina la WORLD ISLAMIC FRONT,ili kuhujumu maslahi
ya Marekani na washirika wake mahali popote duniani,hata kama ni Ziwa Victoria,
Osama
alikuwa mshirika wa Marekani na shirika lao la Ujasusi(CIA) mwaka 1979 wakati
majeshi ya Warusi walipovamia Afghanistan.CIA walimfadhili mabilioni ya Dola za
Marekani kuanzisha kambi ya mafunzo ya Makhtab al-Khidamat(MAK).
Lakini,baada
ya Urusi kuondoka Kabul mwaka 1989, Osama akageuka kuwa adui wa MAREKANI na
washirika wao, akaungana na Taliban na Mullah Muhammad Omar kuendesha ‘Jihad’
dhidi ya Marekani na washirika.
Nataka
kusema kwamba,mwaka 1996 wakati Mv.Bukoba inazama ziwa Victoria, al-Qaeda
tayari walikuwepo,na wangeweza kufanya madhara hapa nchini kwa mashambulizi
yenye kulenga shabaha Wamarekani ama maslahi yao hapa Tanzania.
Hata hivyo,
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Everest Ndikilo, amesema serikali imeimarisha ulinzi
katika Ziwa Victoria,kwa kuwa zipo boti za doria zinazozunguka ziwani, na raia
wanapaswa kutoa taarifa pindi wanapoona mienendo yenye mashaka ama kitisho cha
magaidi wa al-Qaeda ama al-Shabaab!
0786 324 074
No comments:
Post a Comment