*Kununua tiketi ya usafiri katika boti hizo, ni kununua tiketi
ya kuzimu!
Na Conges Mramba, Mwanza
NI SAA nane mchana, Alhamisi,Mei 24. Niko
Mwaloni,Kirumba,Jijini Mwanza,katika moja ya Bandari bubu zilizomea kama uyoga,
kandoni mwa Ziwa Victoria.
Mbele yangu kuna boti iliyojengwa kwa mbao na
mabati; imechakaa. Inapakia abiria na mizigo,tayari kung’oa nanga kuelekea
katika moja ya visiwa vingi vidogo vidogo vya Ziwa Victoria.
Nachungulia ndani ya boti hii, Mv. Maisha,
nabaini kuna maboya machache yameputikwa ndani ya gunia kuu kuu.Sioni vifaa vya
kuzimia moto(Fire Extinguishers), sioni kisanduku cha Msaada wa Kwanza(First
Aid).
Kama ada, makuli wanaendelea kupakia ndani ya
Mv.Maisha mizigo; viroba vya sukari,chumvi,maboksi ya sabuni. Pia wanapakia
magudulia ya mafuta ya taa na hata petrol! Wanachanganya abiria na mizigo?
Abiria na petroli?
Naam, hii ni boti iitwayo, Mv.Maisha inapakia
abiria na mafuta ya taa na petrol, abiria wameketi botini kimya,hakuna
anayeshangalia kitisho cha ajali ya moto, pindi petrol ikichokozwa kwa moto wa
injini ya boti, ama moshi wa sigara!
Abiria wanazidi kuingia na kuketi. Hawana
muda kuhoji ikiwa boti hii ina maboya ya kutosha? Ina Bima? Ina vifaa vya
kuzimia moto, au vile vya uokozi pindi ajali ikitokea?
Alfred Wariana, ni Afisa Mfawidhi wa Mamlaka
ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(SUMATRA), Mkoani Mwanza, ambaye
anasema Ajali ya Meli ya Mv.Bukoba,Mei 21,mwaka 1996,iliizindua serikali katika
usingizi wa pono,imetunga sheria za Usalama Majini!
“Kufuatia Ajali ile. Sheria ya Kuongozea
vyombo vya majini, The Merchant Shipping Act, imetungwa mwaka 2003,ikaanza
kutumika mwaka 2004 ili kudhibiti Ajali”,Wariana anasema katika Mahojiano
Maalum ofisini mwake.
Kulingana na Wariana, Ofisa huyu Mfawidhi wa SUMATRA, Mwanza kuna jumla ya
Meli 47 ambazo zote zimesajiliwa, zina BIMA kwa sababu mtu hawezi kuendesha
biashara ya huduma za Usafiri pasipo kuzingatia taratibu, sheria na kanuni.
“Changamoto ya SUMATRA,Mwanza kuna boti zaidi
ya 10,000 zinazosafirisha abiria na mizigo kwenda visiwani na Sengerema,Ukerewe
na Geita. Huwezi kusema, asilimia mia zote hufuata sheria, na kuzingatia
maelekezo.SUMATRA Mwanza, tuna wakaguzi watatu tu,lakini tunao
mtandao(usiotosha) wa kuwadhibiti wasafirishaji wasiopenda kutii sheria pasipo
shuruti. Kumbuka, Ziwa siyo barabarani ambako utaweza vizuizi njiani na kufanya
ukaguzi ili kuwabaini wakosaji”, anafafanua Wariana.
Polisi
na Watendaji wa vijiji wapo katika maeneo ya vituo vya kibiashara,ambako boti
hizi hutia nanga na kupeleka bidhaa,wanapaswa kuwatia mbaroni wasafirishaji
wasiozingatia sheria za Usafirishaji wa Majini.
Kulingana na
SUMATRA,Mwanza, ziko changamoto kuwafikia wamiliki wote wa vyombo vya majini,hususan
vidogo vidogo,na kuvikagua kila mara.
“Hata hivyo,mtandao wetu wapaswa kukagua na
kuhakikisha kila chombo ni salama kabla ya kuanza safari,na kila chombo cha
usafiri chapaswa kuwa na cheti cha kufaa-sea
worthiness.
Katika Ziwa Victoria,SUMATRA wana ofisi Mwanza, Bukoba
na Musoma. Ziwa Victoria kuna visiwa takriban 60, Ukerewe pekee kuna visiwa 38
vingine hukaliwa na wavuvi tu.
Mei 21,
mwaka 1996,Meli iliyomilikiwa na lililokuwa Sherika la Reli(TRC) ilizama umbali
wa mail inane(kilomita 12) za majini, jirani na Bandari ya Mwanza, uelekeo wa
Bwiru.
Mv. Bukoba, ilipinduka kasha kuzama,ikasababisha
vifo vya zaidi ya watu 800.Wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa,wakipoteza mali
nyingi za mamilioni ya shilingi,hususan mikungu mingi ya ndizi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Jaji Robert
Kissanga, iliyochunguza chanzo cha Ajali hiyo,usiku wa kuamkia siku ya ajali,Mv.Bukoba
ilipakia abiria kati ya 750 na 800 pamoja na wafanyakazi 37 wa Meli hii.
Kati ya
hao, 114 waliokolewa wakiwa hai, wakati 391 waliopolewa wakiwa wamefariki wakazikwa katika Makaburi ya
Igoma,nje kidogo ya Jiji la Mwanza. Miili mingine ilichukuliwa na jamaa zao
kwenda kuzikwa kwao. Jumla ya miili 332 haikupatikana.
Kila mwaka, ifikapo Mei 21, serikali
inayosema Haina Dini, huongozana na viongozi wa madhehebu ya dini na waganga
kwenda eneo la ajali,kufanya ‘matambiko’ na kumwaga mchanga eneo majini!
Serikali iliwashitaki katika Mahakama Kuu aliyekuwa Nahodha wa Mv.Bukoba, Jumanne
Rume-Mwiru, (ambaye sasa ni Marehemu),Mkaguzi wa Mamlaka ya Bandari(wakati huo
THA),Gilbert Mokiwa, aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Bukoba, Alphonce Sambo, na
aliyekuwa Maneja wa Bandari ya Kemondo, Prosper Lugumila.
Kesi
hiyo Nambari 22 ya mwaka 1998, ilianza kusikilizwa Mei 14 mwaka 2001. Miongoni
mwa waendesha mashitaka katika kesi hiyo ni Eliezer Feleshi, ambaye sasa ni
Mkurugenzi wa Mashitaka nchini(DPP).
Hukumu ya kesi hii ilitolewa Ijumaa, Novemba
29 mwaka 2002,majira ya saa sita mchana hadi saa 9 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu, Juxton Mlay(amestaafu).
Washitakiwa wote walishinda kesi hiyo,kufuatia
Hukumu yenye kurasa 118 iliyosomwa kwa dakika 160 na Jaji Mlay,kusema Mv.Bukoba
ilizama kwa sababu haikuwa na uwiano wa majini, na siyo uzembe wa washitakiwa.
Serikali ikakata rufaa, hadi leo majaliwa na
rufaa hiyo hayajulikani,na baadhi ya washitakiwa wamefariki dunia,bila kujua
hatma ya kesi hiyo na stahili zao.
Mv.Bukoba ilikuwa ‘Kaburi’ lenye kuelea Ziwa
Victoria. Ilikwishapigwa marufuku,kwa kuwa haikuwa na viwango vya ubora-sea worthiness.
Ilijengwa na Kampuni ya
Kibelgiji,ikazinduliwa Julai 27 mwaka 1979.Siku
ya uzinduzi, ilibainika haikuwa thabiti,na ilikosa uwiano,ilitaka kumtosa Baba
wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa Rais wan chi wakati huo.
Miaka michace
iliyopita, meli nyingine ya MSC, Mv. Butiama, ilizimika injini zake jirani tu
na Bandari ya Mwanza, lakini ikaelea kwa zaidi ya saa mbili,huku abiria
wakihaha bila msaada. Ilikuja kufahamika kwamba, meli hiyo haikuwa na
mawasiliano!
Meli nyingine ya mizigo, Mv.Nyamageni,ilizama
ziwa Victoria ikiwa na abiria zaidi ya 20 waliosafirishwa pamoja na masanduku
ya soda kwenda visiwani.
Feburuari mwaka huu, Mv. Pacific iliyokuwa ikisafiri kati ya Mwanza
na kisiwa cha Ghana ilizama, ilikuwa na abiria 17, mmoja alifariki wengine
wakaokolewa.
Kwa mujibu wa SUMATRA, Boti nyingine iliyokuwa
na abiria 31 ilizama huko Musoma,mkoani Mara,abiria wote wakaokolewa kwa kytumia zana za uokozi.
Kwa mujibu wa Alfred Wariana, Ofisa Mwandamizi
wa SUMATRA, katika ajali tatu za karibuni, kati ya watu 81 waliokuwemo katika
boti hizo,ni mmoja tu aliyefariki dunia,na anasema hii huonesha kwamba sheria
zimeanza kufuatwa.
Kabla
ya vyombo vya majini kuanza safari ni sharti kukaguliwa ili kuthibitishwa
usalama wake.
Hata hivyo, Wariana
anasema bado usafiri wa majini Ziwa Victoria ni salama zaidi kuliko barabarani.
“Usafiri wa barabarani
hata wa ndege hapa Afrika ndiyo ‘Moving Coffins’ (majeneza yanayotembea),Barabarani
kuna magari kuna pikipiki zinazochinja watu kila siku”, anasema Wariana.
moja ya
meli za MSC ziwani Victoria
Akizungumza kuhusu
ushindani wa kibiashara, Ofisa huyu wa SUMATRA amesema, kuimarishwa kwa
miundombinu ya barabara, hususan kutoka
Mwanza hadi Musoma, Tarime na hata Kenya,kumesababisha abiria wengi
kususia usafiri wa meli.
Tangu barabara ya lami ya Mwanza hadi Musoma
ikamilike mwaka 1985, hakuna tena abiria wanaosafiri kwa meli kwenda
Musoma,Shirati au hata Kisumu,Kenya.
Upungufu huu ni wa abiria wa meli ni wa takriban asilimia 50.
Kaimu Meneja Masoko na Biashara wa Kampuni ya
Meli(MSC)Kapt. Obedi Nkongoki, anasema mwaka jana Kampuni hii ilisafirisha
jumla ya abiria 235,794 tu ambao ni chini ya uwezo wake. Mizigo iliyosafirishwa
ni tani 54,212.
Kulingana na Kapt. Nkongoki, MSC ina jumla ya
meli 15 zinazosafirisha abiria na mizigo kati ya Mwanza na Musoma,Bukoba,Kemondo,Jinja(Uganda),Kisumu(Kenya),Port
Bell Uganda, na Ukerewe.
Mv.Victoria ndiyo meli kongwe kuliko zote;
ilijengwa mwaka 1960. Imekuwa ikifanyiwa matengenezo na ukarabati mkubwa na
mdogo.
Kaimu Meneja Mkuu wa Marine Services
Company(MSC)Projest Kaija, anasema Mv..Victoria ina umri wa miaka 52, lakini
imefanyiwa ukarabati mkubwa na mdogo mara nyingi. Mara ya mwisho ilifanyiwa
ukarabati mkubwa(Major Rehabilitation) mwaka 2008 ambako ilikaa miezi sita
katika Bandari ya Mwanza South Port bila kufanya huduma.
Ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani
200 za mizigo;lakini kufuatia abiria kupungua siku hizi inachukua abiria
500-800,chini ya uwezo wake. Inafanya safari zake kati ya
Mwanza-Kemondo-Bukoba-Mwanza.
Kwa mujibu wa Kaija, meli nyingine za MSC
zinazofanya huduma Ziwa Victoria, ni Mv. Butiama,Serengeti,Clarias ambazo
hubeba abiria na mizigo kati ya Mwanza,Bukoba na hata Nansio-Ukerewe.
Meli za mizigo ni pamoja na Mv. Umoja, Mt.
Nyangumi ambayo husafirisha mafuta kutoka Mwanza hadi Kisumu,Kenya na Jinja na
Port Bell huko Uganda.
Mv.Ukerewe, MI wimbi na Malindi husafirisha
mizigo,wakati Tanganyika Sea Warrior ni
boti mpya ya kusafirisha watalii wapatao 15 kwa wakati mmoja.
Mt(Motor Tug) HUVUTA MATISHARI.
Ziwa Victoria lina eneo la kilomita za mraba
68,800. Ni ziwa la pili kubwa duniani lenye maji baridi na ni nyumba ya sangara
ambao sasa wamekaribia kwisha. Ni ziwa kubwa kuliko yote Afrika, Tanzania
inamiliki asilimia 49 ya ziwa hili, Kenya asilimia 6 na Uganda inamiliki
asilimia 45.
Kulingana na Wariana, Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA,Mwanza,
mabaharia wote wa meli wanapaswa kuwa na viwango na wawe wamehitimu katika Chuo
cha Mabaharia, Dar es salaam Maritime Institute,(DMI) ambacho hutambuliwa
kimataifa.
“Hakuna meli inayoendeshwa na Nahodha asiye na
sifa”, anasema Wariana wa SUMATRA.Vyo mbo vyote vinapaswa kuwa na BIMA na vifaa
vya uokozi,lakini boti chache na mitumbwi midogo na majahazi husafirisha abiria
pasipo mamlaka kubaini,na ni changamoto zilizopo, wanapaswa kufuata sheria”,
anasema Wariana wa SUMATRA.
Vyombo hivi vispofuata
sheria,kanuni na taratibu za usafirishaji salama majini, Wariana anasema ndiyo
hufanya kununua tiketi za usafiri katika vyombo hivi kuwa tiketi za kuendea
KUZIMU!
“Kwa bahati, shughuli za uvuvi ziwa Victoria
zimepungua sana katika visiwa hakuna tena watu wengi wanaoenda huku na huko,kwa
sababu samaki wamepungua sana ziwani,na ajali za majini zimepungua”, anasema
Alfred Wariana, Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA,Mkoani Mwanza.
No comments:
Post a Comment