Friday, May 24, 2013

SAFARI ZA AKINA OBAMA AFRIKA HAZINA TIJA(50

Rais Barack Hussein Onyango Obama, anawasili Dar es salaam Jumamosi,Juni Mosi mwaka huu.
Obama,na mkewe Michelle wanakuja Afrika kwa ziara ya siku nane,na watakuwa Senegal,Tanzania na Afrika Kusini.
Hata hivyo,ziara za marais na viongozi wa Marekani hapa Afrika hazina tija...sasa endelea kusoma sehemu ya tano ya makala haya
SITAPENDA kuamini kirahisi, kwamba eti Marekani ni rafiki wema sana kwetu Tanzania,hadi viongoi wake huja hapa kila mara,hukaa siku nyingi na hutuletea hisani.
Na siamini kwamba, eti fadhila, hisani ama misaada ya Marekani kwetu hutoka katika kiini cha moyo wao na mapenzi ya dhati kwa Watanzania!
Kwa hulka yao,Marekani hawana rafiki wa kudumu.Maslahi yao ndiyo rafiki yao mkuu wa enzi zote.Kwa sababu hiyo,ukiona Marekani wanakupenda,kuna maslahi yao yaliyofichika sirini nyumbani kwako, Wamarekani wanapokuja kwako, wanafuata maslahi nyumbani kwako,kwa jirani yako ama kwa rafiki zako.
Naam. Marekani hawana rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu.Wana maslahi ya kudumu Taifa hili babe sana duniani, lililopata uhuru wake zaidi ya miaka 230 iliyopita, aslani halina urafiki wa kuaminika-lina maslahi ya kudumu.
Kwa sababu hiyo, leo nitajadili maslahi ya Marekani yanayoweza kuwa yamefichika ndani ya ngozi ya Watanzania, na hivyo ujio wa viongozi wa Marekani wa mara kwa mara ukawa na nia ya kutuchuna ngozi ili wachukue kile kilichofichika ndani yetu.
Ziara ya Waziri wa Mambo ya        Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton, inaweza kuwa na kitu ‘nyuma ya Pazia’.
  Jumamosi, hadi Jumatatu, Juni 11-13, MWAKA 2011, Hillary Clinton alikuja kwetu.
 Huyu Hillary Clinton(66) ni mwanamke wa kwanza, mke wa Rais Mstaafu(Bill Clinton) kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.
Pia, ni mwanamke wa tatu wa  nchi hiyo kushika wadhifa huu wa ‘kikachero’ katika siasa za Ulimwengu.
Wanawake wengine waliomtangulia kushika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje(The Secretary of State) wa Marekani, ni Madeleine K. Albright aliyeteuliwa kumrithi Warren Christopher mwaka 1997 zama za urais wa William(Bill) Jefferson Clinton.
 Mwingine, Dk. Condoleezza Rice, ama kama alivyoitwa na rafiki zake, “Condi” aliyemrithi Jenerali Colin Powel.
Dk. Rice, ‘rafiki’ wa familia ya akina Bush,alimaliza muda wake siku Rais Barack OBAMA ALIPOAPISHWA KUWA Rais wa 44 wa nchi hiyo, Januari 20 mwaka 2009.
Hillary, aliyekuwa seneta wa New York, alipewa wadhifa huu  mtukufu baada ya kushindwa kura zao maoni za urais ndani ya chama cheo cha Democrat na huyo huyo Rais Obama.
Wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani(secretary of state) ni nyeti sana; hupewa mtu muhimu sana Marekani kwa wakati huo, mwenye ujanja mwingi wa kughilibu na kushawishi mataifa kukubaliana na Marekani dhidi ya changamoto zake na vizingizi dhidi yao. Huyu hawezi kuwa waziri tu,bali pia shushushu ama kiongozi wa majasusi wa ghiliba ulimwenguni.
Dk. Henry Alfred Kissinger, yeye alichora ramani ya kukomesha ujamaa wa Ki-Marx duniani. Alimsaidia Rais Richard Milhous Nixon(Nixon ni maarufu kwa kashfa ya Watergate) kumpindua Rais Mjamaa wa Chile, Salvador Allende,kwa kutumia Shirika lao la Ujasusi, CIA.
 Kissinger, alishika wadhifa huu mwaka 1973 enzi za mwisho za Nixon na mwanzoni mwa Rais Gerald Rudolf Ford.
Nataka kusema kwamba, hawa mawaziri wa Mambo ya Nje huwa na kazi maalum iliyofichika katika nyayo za viatu vyao.
 Madeleine K. Albrigh, alipelekwa Korea Kaskazini kujaribu kwenda kuzungumza na viongozi wan chi hiyo,Kim Il Sung/Kim Jong Il waachane na mpango wao wa miradi ya nyuklia.
Hata siku za karibuni,walijaribu kuwashawishi waachane na miradi ya Nyuklia kwa ahadi kwamba wangepewa mafuta mengi na kitita cha dola za Marekani-rushwa.
Lengo lao lilikuwa Korea Kaskazini,moja ya nchi adui zao na nchi iliyokuwa katika Mhimili wa Uovu-The Axis of Evil- iachane na ukaidi kama Iran ya Mujahidin, Mahmoud Ahmadnejad.
Albright, alikwenda  Korea Kaskazini, kutuliza joto la uasi dhidi ya Marekani kwa mazungumzo na ghiliba ambazo hazijafua dafu hata siku hizi.
 Condoleezza Rice, “Condi” ambaye amepata kuwa Mshauri wa Mambo ya USALAMA WA TAIFA wa Rais Bush, Kafanya makubwa kufanikisha vita vya Ghuba,hasa mapinduzi ya serikali ya Wataliban wa Afghanistan na kuuondoa utawala wa Marehemu Saddam Hussein huko Irak.
Hawa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, wana mitego na ghiliba,na huwa na ‘Kazi Maalum’ ya kufanya katika ajenda za siri za Marekani, zinazofichwa nyuma ya pazia.
Kissinger, yeye alishughulikia sana migogoro ya Mashariki ya Kati hususan Vita vya Misri na wajomba zaWamarekani, Israeli. Hatimaye yalikuja mazungumzo ya amani huko Camp David, mwaka 1978 zama za Jimmy Carter.
Madeleine K. Albright,alitua Dar es salaam mwaka 1999. Ni siku ambayo mwili wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere uliagwa,katika uwanja wa Taifa,Dar, siku hizi Uwanja wa Uhuru ama Shamba la Bibi.
Rais Bill Clinton, alitua Tanzania, Agosti 27 mwaka 2000. Arusha-alialikwa na Msuluhishi wa Mgogoro wa Burundi,Nelson Rolihlahla ‘Madiba’ Mandela,wakati wa utiaji saini ule mkataba wa Amani ya Burundi. Hiyo haikuwa ziara ya kiserikali,bali ya kikazi tu.
Jumatano, Julai 13, mwaka 2005 mke wa Bush,Laura Welch Bush alitua Dar es salaam,kwa ziara ya siku mbili.
Mama huyu, alikuja Dar es salaam tena na mumewe. Kwake hiyo ilikuwa ziara ya tatu Afrika Mashariki, na ilikuwa mara ya tano kuja Afrika, Laura Bush ni mwenyeji Afrika.
Rais George Walker Bush, alikuja Dar es salaam Feburuari 2008. Ilikuwa ni miezi takriban kumi tu kabla ya Uchaguzi mkuu uliomweka madarakani Barack Obama.
 Nataka kusema kwamba, hawa vigogo wa MAREKANI wanapofika nchini mwetu kwa ziara zao, sisi Watanzania huwekwa “Chini ya Ulinzi” mkali wa makomando na majasusi wa Taifa hili babe sana.
Makachero wengi sana wenye suti nyeusi na miwani ya jua hutuzingira hata mifumo ya maisha ikiwemo ya mawasiliano hukamatwa-ndege haziwezi kuruka tena,kwa kuwa viwanja vyetu huwa chini ya ulinzi,”No Fly Zone” mithili ya ile amri ya ndege kutoruka huko Tripoli, Libya!!
 Uhuru wetu hutoweka kwa muda wote akina Hillary na Bush,Albright n.k wanapokuwa hapa kwetu.Bill Clinton alipotua uwanja wa Kimataifa Kilimanjaro,KIA huko Arusha, mijibwa ya Marekani ilinusa hata Mercedes Benz la mwenyeji wake.
 Bendera za rangi nyekundu na nyeupe,zenye jumla ya nyota 50 hupepea kila mahali na kuzifunuka za kwetu.
 Majibwa yanayodondoshwa madegeni,hunusa kila kitu,kila mahali, askari wetu na makachero wetu huonekana mithili ya askari mgambo tu-wasio na kazi!
 Mawasiliano hata ya simu hukatwa,magari hukaguliwa au huzuiwa kutembea utadhani ‘Check Pont’ za Baghdadi,huko Irak. Hata waandishi wa habari wa kwetu hukosa uhuru huwa kama wafungwa magaidi,huko Abu Ghraib na Guantanamo Bay,Cuba!
Magari ya Zimamoto;Fire huachana na kuzima moto na kwenda kupiga deki barabara,omba omba na walemavu huondolewa mitaani wanakoomba,na kwenda kuswekwa rumande, hadi Bwana Mkubwa aondoke mjini!
Na ndivyo inavyokuwa Obama na Michelle wanapowasili katika nchi za Afrika,mahoteli hujaa mashushushu,mfumo wa kawaida wa maisha ya watu husimama mwezi mmoja kabla ya Bwana mkubwa kufika!
 Wakati huo,usafi huwa wa hali ya juu sana, Manisaa au Jiji hawalali na Mkurugenzi wake hukesha akisimamia usafi wa Barabara,umeme haukatiki ng’oo! Mpaka Bwana mkubwa aondoke!
Anapokuja Bush au Hillary Clinton, ama Obama na kimwana wake,Michelle, pumzi huwakatika viongozi wa Tanzania,tangu Mizengo Pinda hadi wafagizi wa barabara.
Shughuli zote za uchumi za kawaida husimama, mfumo wetu wa maisha wa kawaida huugua kiharusi, wapelelezi wote huwa kazini na safari aghalabu huwa ya siri sana.
Nakumbuka, wakati Bush anatua Dar es salaam Mtangazaji wa TBC Taifa alisema MAKACHERO wa Marekani walimsimamia sana ni kama walimweka chini ya ulinzi wakati alipotangaza tukio hilo hapo uwanja wa ndege.Walimtazama hadi mdomoni alipotangaza waone kama kulikuwa na bomu likitaka kuripuka!
Waandishi wa Tanzania waliwekwa chini ya ulinzi,walipigwa mtama,walipojaribu kuwania picha bora.
Sasa, naachana na hayo. Hivi wewe msomaji,unadhani kiongozi Mkuu toka Washington atakuja Dar es salaam kukaa siku mbili,tatu nne au tano kufanya mambo madogo madogo kama kukagua mashamba,Kibaha nkoani Pwani,kukagua miradi ya Afya,sijui Lishe halafu aende Mlandizi na kuangalia miradi ya umeme ya Marekani huko Ubungo?
Bush,alipokanyaga Dar mgogoro wa Richmond ukatua,na akasema kaleta Symbion,hata akina Mbowe na Silaa hawakuhoji kitu tena!
 Tuchukulie kwamba ni kweli kwamba Hillary Clinton alikuja Dar es salaam kwa ziara ya siku tatu,pamoja na mambo mengine,kuzungumza na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Kikwete na maofisa wa serikali ya Tanzania, ya Marekani nay a Ireland.
 Je, walikuja mashushushu ama majasusi wangapi?Walidaka mambo mangapi? Walitupeleleza kiasi gani hadi siku moja waanze kutulipua kwenye mitandao yao ya kichizi,kama Wiki leaks?
Hidhuru,Bush kaja va vyandarua na miradi ya MCC na Global Fund.
 Hata hivyo, siwaamini makachero wa Marekani,hususan Central Intelligence Agency,ambao kuja kwa Hillary Clinton ama Obama hapa Bongo land kwa siku tatu hapa,ni kama kuwaleta majasusi wa kututazama hata utumbo!
 Eti Mkewe Bush, yeye mwenyewe na Hillary Clinton waje kwetu tena wakae hapa siku mbili, tatu nne,tano wakodishe hoteli la nyota sita au tano kwa mwezi mzima kabla ya ziara kuanza hadi baadaye, waishie kukagua Lishe na mashsmba Dar?
Waishie kukagua ngoma za Wamasai na kwenda Mlandizi? Haiwezekani Bwana!
Kwanza, Marekani hutumia pesa nyingi mno kumweka mtu wao hapa kwetu-nchi masikini isiyo na usalama wa kutosha.Kumhifadhi Rais wa Marekani au huyo ‘Secretary of State’ katika nchi iliyowahi kupigwa mabomu na Al-Qaeda siyo jambo kidogo,kama unavyodhani.
Kumweka mtu wa Wamarekani hapa karibu na Somalia na al-Shabab,tena Dar karibu na Nairobi na Kampala ambako kote magaidi wa al-Qaeda na al-Shabab walishapiga mabomu, siyo kitu rahisi mno.
Ni suala la p esa na miundombinu ya ulinzi uliotukuka.Kuishi kwa mtu mkubwa wa Marekani katika nchi legelege kiulinzi halafu wao wakaondoka bila faida? Hapana kuna chumo Fulani wanalotafuta nyuma ya pazia.
Mtu akiniambia, Clinto alitumwa na Obama kuja Dar kuweka mipango thabiti ya kuwaangamiza al-Qaeda na al-Shabab,nitakubali kiasi. Akisema, Clinton kaja kulazimisha nchi za Mashariki mwa Afrika kuacha kumuunga mkono Gaddafi na magaidi wa Al Qaeda na al-Shabab kwa siri,tena kwa kusainishwa mikataba ya hila na ahadi ya misaada ya ghiliba,nitakubali!
Sasa, Marekani inahaha kuwatokomeza magaidi . Si unajua baada ya kumuua OSAMA Bin Laden Mei Pili mwaka 2011 huko Pakistan, al-Qaeda wameapa kulipa kisasi?
Sasa, ujio wa Mama Clinton Dar es salaam iliyowahi kupigwa mabomu na magaidi Agosti 7 mwaka 1998 ni kukagua mashamba na vinu vuya kufua umeme na kukagua MIRADI YA Lishe?
Bila shaka, Marekani wamekuja Dar es salaam na ‘AJENDA YA SIRI’ bila shaka kuwaburuza viongozi wetu wakubali matakwa yao kwa mikataba ya hila nay a siri sana.
Nimecheka kwamba hata wapinzani kama Prof.Lipumba walifyata mkia wakati Mama Clinton anatua,wasionekane ni watoto watukutu! Si unajua hata Kiiza Besigye wa Uganda kaenda Washington na New York kumshitaki, Museveni? Wapinzani hapa wana ubavu kwa mama Clinton? Thubutu!
Sasa, tunasubiri ziara hii ya Mama Clinton kama haina madhara kwetu-hata dawa ya babu wa Loliondo ina ‘side effect’.
 Pengine, Mama Clinton alikuja Dar kumfanyia kampeni Ban Ki Moon arejeshewe ukatibu Mkuu wa UN. Hata huyu Ki Moon aliwahi kuja Dar Jumatano, Feburuari 26 mwaka 2007. Siku iliyofuata Ban Ki Moon alikwenda Arusha kukagua Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya Uhalifu wa Kivita Rwanda kuhusu mauaji ya mwaka 1994, ICTR.
Juzi, alikwenda Goma,Congo kwa kitisho cha M 23.
Labda, Clinton amekuja kutaka Mahakama ya ICTR,Arusha ikimaliza kesi za Rwanda isifungwe,bali itumike kuwafunga jela magaidi wa al-Qaeda na al-Shabab wanaoleta kitisho kwa maslahi ya Mrekani huku.
 Waama, nikiachana na mashaka yangu,nampongeza Hillary Rodham Clinton kuja kukaa kwetu siku tatu, pasipo bomu kulipuka.
 Kumbe Marekani wajue hata huku kwetu kuna maisha,kuna watu tunaishi,tofauti na wanavyodhani kwamba huku kwetu ni njaa ni vita na mabomu hulipuka-kuna amani na ustaarabu pia bwana!
 Sasa,Obama anatua Dar labda kutazama uwezekano wa makampuni yao kupata kandarasi za kuchimba Uranium ama gesi ya Mtwara! Itaendelea
   0786-324 074


No comments:

Post a Comment



welcome to Mwanza The Rocky City

No comments:

Post a Comment