Monday, June 13, 2011

wakubwa wa IMF na Benki ya Dunia nao wanabaka!


IMF na WB wanakopesha  Dola, Euro na ngono  kwa akina mama
                                        *huko  kuna mapenzi kazini-‘kazi na dawa’
                                        *kuna rushwa ya ngono, wake za watu hutwangwa talaka
                                        *Tanzania kuna Maprofesa wanaotoa ‘digrii za chupi’
                                           Na Conges Mramba, Mwanza
   WATU WENGI hapa duniani, wanadhani    kazi ya Benki ya Dunia(WB) na Fuko la Fedha la Kimataifa(IMF) ni kupanga,kuratibu Programu za Fedha, Uchumi na Maendeleo ya watu ili kupunguza umasikini.
  Fuko la Fedha la Kimataifa(International Monetary Fund) hupanga mikakati ya Kupunguza Umasikini na Kuwezesha Ukuaji wa Uchumi,yaani wao wanaita, Poverty Reduction and Growth Facility,(PRCF).
   Umoja wa Mataifa(UN) kupitia taasisi anuwai,hususan mashirika haya na IMF na WB wanajidai kutoa misaada maridhawa kwa mataifa fukara sana duniani, Heavily Indebted Poor Countries(HIPC).
   Yumkini, IMF na IMF wanaongoza duniani katika harakati za kupambana na umasikini,kumbe wanaongoza kwa upendeleo katika ajira,udhaifu na rushwa ya ngono.Wamekuwa wakitumiwa na wakoloni wakongwe kuendelea kuzitawala nchi masikini hususan Afrika, Asia na Amerika Kusini.
  Wameendelea kututawala hata baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia,mwaka 1945 na hata baada ya Vita Baridi kumalizika,mwanzoni mwa miaka ya 90.
   Sasa ni dhahiri shahiri kwamba, IMF na Benki ya Dunia ni makao makuu ya tamaa za kingono,rushwa ya mapenzi na ubakaji kwa akina mama.
 Mkuu wa zamani wa IMF ,Dominique Strauss-Kahn, amepandishwa kizimbani kujibu mashitaka ya kujaribu kumbaka msichana ambaye ni mhudumu wa hoteli, jijini  New York,Mwezi Mei mwaka huu.
   Strauss-Kahn, alikana mashitaka ya kujaribu kubaka. Ushahidi umeonesha kwamba, kulikuwa na mazingira ya ngono kati ya Mkuu huyo wa zamani wa IMF na Mhudumu huyo wa Hoteli,jijini New York,Marekani.
   Mawakili wa upande wa utetezi, wanadai kwamba mteja wao, Dominique Strauss-Kahn(62) na kimwana huyo, walikuwa wamekubaliana kufanya ngono.
  Hiyo Mosi: Ubakaji IMF.Bila shaka, na uchumi wa dunia unabakwa!
   Pili:Rais wa zamani wa Benki ya Dunia(WB),Paul Walfowitz, aliachia ngazi Juni 30 mwaka 2007 baada ya kukutwa na kashfa ya rushwa ya ngono. Rushwa ya ngono hata ndani ya Benki ya Dunia(WB) vinara wa kukosoa nchi masikini kwa rushwa na kukosa uadilifu?
    Wolfowitz,Balozi wa zamani wa Marekani nchini Indonesia na Naibu Waziri wa Ulinzi,tamaa ya huba kwa kidosho,mfanyakazi wa Benki hiyo kuu duniani ilimgharibu  wadhifa wake,marupurupu maridhawa, mambo yakaenda harijojo.
    Alikuwa mpiganaji wa mstari wa mbele dhidi ya rushwa.
 Kumbe, alikuwa dhaifu sana katika huba kwa vimwana,hadi alipopewa penzi akatoa nyongeza ya mshahara na kumpandisha cheo mwanamama huyo,hadi alipokaliwa kikao na kamati ya maadili ya WB.
   Alipochaguliwa kushika wadhifa huo mtukufu, wa Rais wa Benki ya Dunia, akadhaniwa angekuwa shujaa wa kupambana na umasikini duniani, na daktari bingwa wa kuponya pengo kati ya fukara na matajiri.
 Kumbe, Wolfowitz alikuwa mwenye nguvu lakini dhaifu(strongest but weakest) kwa mahaba ya vimwana    katika ofisi ya umma.
  Marekani, ndiyo nchi yenye mamlaka ya peke yake katika kumteua Rais wa Benki ya Dunia.
 Ulaya, wana haki ya  Peke yao kumteua Mkuu wa Fuko la Fedha la Kimataifa(IMF). Nchi nyingine kama Japan,Uchina na za Afrika na Marekani ya Kusini,huishia kulalamika kuburuzwa na Marekani na Ulaya,kuigeuaza IMF na WB mikono yao miwili ya kuiburuzia dunia wanakotaka.
    Taasisi hizi zina uwezo wa kuwawekea vikwazo vya uchumi wale wapinzani wao kama Muammar al-Qaddafi anayenyeshewa mvua ya mabomu na madege ya NATO, na ambaye tayari mji wake wa Benghazi umekuwa ngome ya Waasi wanaobebwa katika mbeleko na Marekani na washirika wake wa Ulaya.
 Wapinzani wengine wa Marekani, ni pamoja na Robert Gabriel(R.G)Mugabe wa Zimbabwe,Hugo Chavez wa Venezuela, Fidel Alejandro Castro Ruz,Rais Mstaafu wa Cuba.
Naam, Rais Mstaafu wa Marekani, George W.Bush alimteua Robert Zoellic kumrithi “Mzee wa Vimwana”Wolfewitz. Zoellic, ni mwakilishi wa zamani wa wafanya biashara wa Marekani,mabwenyenye na wahafidhina wa sera kandamizi za uchumi duniani.Bei ya mazao wanapanga wao, mazingira wanachafua wao na hakuna wa kuwagusa!
   Benki ya Dunia, hukopesha takriban dola za MarekaniBilioni 10 sawa na euro Bilioni 5 kwa mwaka; hukopesha mataifa masikini zaidi kupitia programu na mipango anuwai kama IDA.
 Shaha Ali Riza, ndiye kimwana aliyemzingua Rais huyo wa Benki Kuu Duniani,Dk.Wolfowitz,mwaka 2007 hadi alipokiuka maadili na kutopea katika utovu wa maadili.
   Shaha Ali Riza(57) ni kidosho aliyemgharimu Wolfowitz urais wa Benki ya Dunia.Walipokutana kwa nasibu mno,wakapendana penzi la tashtiti…wakati huo Wolfowitz akiwa Naibu Waziri wa Ulinzi,zama za Rais Ronald Reagan.Wakati huo, Donald H.Rumsfeld alikuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani.
    Kimwana huyu,Shaha Riza, alizaliwa Tripoli,Libya huko kunakopigwa mvua ya makombora kumwangamiza Kanali Muammar al-Qaddafi na milki take ya miaka 42. Alizaliwa mwaka 1954.
 Baba wa kidosho huyu,Riza aitwaye Khalid Alwalid na mamaye ambaye alikuwa chotara wa Syria na Saudi Arabia, walimpeleka Shaha Riza Uingereza.Akawana uraia wa Uingereza
 Baadaye, akahamia Marekani,ni baada ya kuolewa na Bulent Ali Riza ama kwa kifupi,Aliriza  (60)sasa.Kisura huyu aliyemzamisha Rais Wolfowitz  huko Benki ya Dunia alisoma London School of Economics, akatuzwa shahada ya Uzamili katika Uhusiano wa Kimataifa,huko Oxford mwaka 1983.
   Ana uwezo wa kuongea lugha tano, miongoni mwake,Kiingereza,Kiarabu,Kiitaliano na Kifaransa.
 Mumewe alimpa taraka,kwa sababu ya uhusiano wa kimapenzi ba Rais wa Benki ya Dunia.Benki ya Dunia inapochangia kuvunjika kwa ndoa na watoto wasio na wazazi wa pande mbili, nani awape msaada?
 Shaha, alijiunga na Benki ya Dunia mwaka 1997, akitokea Mashariki ya Kati. Huko, alitumiwa na Marekani kuipeleleza Afrika na Mashariki ya Kati,ili eti kusaka demokrasia katika ulimwengu wa Kiarabu.
 Kimwana huyu wa Kiarabu alikuwa kibaraka na shushushu wa Marekani aliyetumika kupandikiza chuki ili vita vianze Ghuba wao waibe mafuta!
   Machi, mwaka 2005,sakubimbi(jirani yao) aliviambia vyombo vya habari juu ya uhusiano wa kimahaba ya Wolfowitz. Huu ndiyo mwaka Wolfowitz alipothibitishwa katika wadhifa wa Rais wa Benki ya Dunia, akaanza kuutumia vibaya wadhifa huo ili kununua huba la ‘mtoto’ wa Kiarabu, Shaha Ali Riza, aliyekwishaachika.
    Alipagawa kwa penzi la tashtiti kwa huyu Shaha Riza,kazi zikaharibika,ukawa upendeleo tu-Bwana mkubwa haoni wala hasikii-Upofu wa Penzi Pevu kwa kimwana wa Kiarabu.Mzuri mithili ya Jini!
 Alipandishwa vyeo,akapandishwa mshahara, alilipwa dola za Marekani 180,000 kwa mwaka,hazikukatwa kodi.
 Naam, mwenye mapenzi haoni,Riza alipandishwa mshahara kwa asilimia nane kila mwaka,kwa sababu,”MKUBWA ANATAKA!”
  Mwaka 2007, gazeti la Washington Post likafichua mshahara wa kimwana huyo kwamba uliongezwa kinyemela kutoka dola 132,660 hadi 193,590 kwa mwaka; tena pasipo kodi.
 Mwanamke huyo akajitetea na kujifaragua hivi na vile, katika Kamati ya Maadili ya Benki hiyo.Wafanyakazi wenzake wakalalamika kwamba, “Boss” alikuwa akiwashusha moyo kumpandisha cheo kimwana wa Kiarabu,Shaha Riza,wakati wao mshahara haupandi na cheo hawapandishwi.
 Huyu mama, aliwahi kufanya kazi Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani(The Pentagon) wakati ule Wolfowitz akiwa Naibu Waziri wa Ulinzi.
 Kwa hiyo,utaona huko Pentagon ndiko walikokutana,penzi likamea na kukua,jamaa alipoufuma u-‘Boss’ W.B akamwita mshushu wake huyu na kumpandisha vyeo na mshahara mkubwa! Hata Pentagon na Benki ya Dunia kuna Mapenzi kazini-‘Kazi na Dawa’ ama siyo msomaji wangu?
 Kumbe, makelele yao ya uzembe na kutowajibika kazini kwa nchi masikini ni domo kaya tu.
 Shaha Riza,ndiye aliyetumiwa kuipeleleza Irak na kuchochea vita vilivyomwondosha madarakani, Saddam Hussein mwaka 2003, na hatimaye akatiwa mbaroni na kunyongwa,Camp Justice,Desemba 2006.
  Mkewe Wolfiwitz,Clare Selgin alishamwonya mapema Rais Bush asiitumbukize Marekani katikavita vya Ghuba kwa kuwasikiliza akina Shaha Riza.
Aprili 12 mwaka 2007 Bwana Mkubwa huyo wa WB akajitetea kutumia cheo vibaya na kuitumia ofisi kufaidi penzi la kimwana wa Kiarabu; alisita kuachia ngazi kwa kashfa ile.
 Nakumbuka kashfa nyingine ya ngono baina ya Rais Bill Clinton na Monica Lewinsky-The Monicagate.
 Magavana wa Benki hii walikaa Aprili 15 mwaka 2007 ili kujadili uchafu huo na kutumia mali na madaraka kufaidi mapenzi ya kimwana wa Kiarabu katika ofisi nyeti ya umma.
  Magazeti yalimlima sana Wolfowitz kwa mapenzi katika ofisi ya umma-akaachia ngazi. Mail on Sunday, Jewcy, Wall Street Journal,Washington P ost, The New York Times, Los Angeles kwa kuyataja macache, ndiyo yaliyoongoza kumlima huyu kigogo.
 Kimwana wa Kiarabu toka Libya, mwenye mchanganyiko wa damu toka Syria na Saudia alipandishwa vyeo,licha kuajiriwa kwa mizengwe,akapandishwa mshahara, kupalilia penzi la kigogo!
 Mmewe aliitwa Cypriot Bulent Ali Riza,Mturuki na walishatengana. Wolfowitz yeye alimwoa Clare Selgin mwaka 1968 wakapeana talaka 2001.
  Rushwa ya ngono ambayo hata hapa Tanzania ipo, imeanzia huko Benki ya Dunia,na kupeana vyeo na kazi kulianzia huko kwa akina Wolfowitz, Bush na Obama.
 Hata hapa Bongo, maprofesa hupewa rushwa ya ngono,na ndiyo chimbuko la ‘digrii za chupi’ na taifa huenda mrama kwa wasomi feki waliojazana katika ofisi nyeti za umma!
    Itaendelea juma lijalo
    0786-324 074



                                                                                                                                                                ;                                                                                                                                                                                   ;                      

 

No comments:

Post a Comment