Wednesday, June 15, 2011

Ziwa Victoria samaki wamekwisha kabisa!!



  
IJUMAA, Januari 21 mwaka huu, Gazeti la KULIKONI  liliandika makala isemayo, “Kwenye samaki wengi hakuna samaki tena” huku makala hiyo ya Mwandishi ,Hamisi Kibari, ikirejea Filamu ya ‘Mapanki’ iitwayo, The Darwin’s Nightmare.
Nataka kuwakumbusha wasomaji wa gazeti  kwamba,kitengo cha samaki cha Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO) kinachoitwa Globefish,kilishasema kwamba samaki wanakwisha Ziwa Victoria.
Hata Rais Jakaya Kikwete aliyekerwa sana na ‘documentary’ hiyo, akakutana na mtunzi wake, Hubert Sauper huko Ulaya mwaka 2006,akaingia mitini, alishakiri kwamba Ziwa Victoria samaki wanakwisha.
Samaki hawajaisha Mugango na Majita,Musoma mkoani Mara tu. Hata Mwanza hakuna samaki, Bukoba siku hizi wanakula ndizi pasipo samaki. Visingizio ni vingi,ukiwemo uvuvu haramu, lakini ukweli ni kwamba viwanda vya samaki vya Umoja wa Ulaya(EU) na washirika wao,Wahindi, wamekausha samaki Ziwa Victoria.
Nina takwimu.Sibabaishi ninapoandika jambo!
Globefish, walisema mwaka 2004 kwamba mauzo ya samaki, wa Tanzania,hususan sangara, yalishapungua katika masoko ya Ulaya kutoka tani 56,000 mwaka 2004 hadi tani 52,800 mwaka 2005.
Basi, sangara wakaanza kupanda bei katika masoko hayo ya EU kutoka euro 192 milioni hadi euro milioni 210 kwa sababu sangara walipungua, mahitaji yakaongezeka, wakati huko Mugango, Musoma na Mwanza na Bukoba bei ikisalia ile ile.
Kati ya mwaka 2004/2005 kilo moja ya sangara waliosindikwa viwandani  iliuzwa kwa euro 3.43 hadi euro 5 ambazo zilikuwa kama shilingi za Tanzania kati ya 6,000 na 8,000 tu.
Wakati huo,wavuvi wa Bukima na Bugunda,Majitta, Mugango,Mwanza hadi Bukoba walilipwa shilingi 1,200 hadi 2,000 tu kwa kilo moja ya sangara ghafi. Uporaji wa hali ya juu!
Kulingana na Globefish,kilo moja ya ya fileti ya sangara huko Ulaya iliuzwa kwa wastani wa euro 60. Euro moja wakati huo ilikuwa sawa na shilingi 1,600 za Tanzania.
 Sasa angalia, Mzungu analala usingizi kisha anaamkia supermarket yake na kuuza kilo moja ya sangara kwa euro 60, wakati mvuvi alivua usiku mzima hapa,akapigwa dhoruba, akaishia kulipwa shilingi 1,200!
Maudhui katika Filamu ya Darwin’s Nightmare,iliyotungwa na Hubert Sauper mwaka 2004, akatunukiwa tuzo anuwai duniani,ikiwemo tuzo ya Oscar, ni kwamba Tanzania ilikuwa ikidhulumiwa sana kupitia biashara hii ya sangara Ulaya.
 Tanzania,ilibweteka kwa sifa hewa kwamba inauza sana sangara,kumbe Wahindi na Wazungu walichuma sana migongoni mwa wavuvi(akina Mkono wa huko Bukoba na Musoma) ambao waliishia kulipwa kidogo, wakabaki kunywa gongo na kupukutika na Ukimwi katika makambi ya uvuvi.
Mwandishi wa mwanzo kuwasha moto ,alikuwa Johnson Mbwambo, ambaye aliandika katika Gazeti la RAI Toleo Na 640 la Januari 12-18 mwaka 2006 kwamba documentary ya Darwin’s Nightmare ilituzindua usingizini!
Serikali mkoani Mwanza, wakati huo Daniel Ole Njoolay, akiwa Mkuu wa mkoa, akatoa Tamko kali kulaani documentary hiyo kwamba ilikuwa ya kizandiki; na kwamba Tanzania ilifaidika mno na mauzo ya sangara Ulaya.Akapinga Watanzania kula vichwa na mifupa ya sangara waliotupwa viwandani baada ya kusindika minofu-maarufu sana kama mapanki.
Nimesema wakati huo bei ya sangara ilikuwa shilingi 1,200 na viwanda vya mkoa wa Mwanza pekee vilikuwa vikisafirisha zaidi ya kilo 30,000 za sangara waliosindikwa,wakati Mwanza pekee kukiwa na wavuvi 39,370.Shilingi milioni 200 zilikuwa zikiingia katika mzunguko wa fedha kila siku.
Njoolay,alisema pato lililotokana na sangara mwaka mmoja kabla ya filamu hiyo,lilikuwa shilingi bilioni 5.7 wakati shilingi milioni 200 zinazunguka katika mzunguko kila siku,wavuvi wakitembea na mifuko ya plastiki,’Rambo’ iliyojaa noti!
Kwa ujumla, serikali iliibeza makala ya Johnson Mbwambo, ambaye wakati huo alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wandishi wa Habari za Mazingira(JET).
 Jumatatu,Julai 31 mwaka 2006,Rais Jakaya Kikwete, akafanya mkutano na wazee wa Mwanza kwenye ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu(BoT) Capri-Point,Mwanza na kuilaani vikali Filamu ya Mapanki, Darwin’s Nightmare.
Vyombo takriban vyote vya habari vikahanikiza laana hizo za Rais Kikwete kwa Hubert Sauper,kwa sababu huko Ulaya na Marekani, Filamu hiyo “Mapanki’ iliichafua sana Tanzania huko Ughaibuni, hata Rais alipokwenda kujitambulisha huko baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2005, akakutana na habari za filamu hiyo.
Rais Kikwete alikasirika; kwa sababu alidhalilishwa kusikia na kuiona hiyo filamu ikitubeza kwamba tuliuza Ulaya minofu ya sangara,sisi tukabaki kula vichwa na mifupa-mapanki-mithili ya vijibwa! Mapanki yenyewe ni yale yenye funza, tuliyinyang’anyana na mwewe na mbwa huko Kanyama na Nyamuhongolo,nje kidogo ya Jiji la Mwanza, barabara iendayo Sirari na Musoma.
 Naam, mimi na Richard Mugamba(sasa Mhariri wa The Guardian on Sunday)tukajitoa mhanga kuuzindua umma wa Kitanzania juu ya kile alichosema Hubert Sauper,katika filamu ile.
Kwamba,wakati Mzungu anapopelekewa minofu huko, sisi tunakula mifupa na vichwa vya sangara vilivooza,ili kujikimu,kwababu nchi ilikuwa katika janga la njaa,kiasi cha kusaidiwa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa,FAO na WFP.
Shirika la Utangazaji la Uingereza(BBC) likafika Mwanza na timu ya Watangazaji wengi, akiwemo Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili, Tido Mhando,nilipewa muda kuzungumza namna biashara hiyo ya sangara ilivyokuwa ikimaliza samaki Ziwa Victoria na kuwaacha wananchi na njaa na umasikini wao.
Kutoka mwaka 2006 hadi 2011 Mhariri wa Gazeti hili, Hamisi Kibari anapofanya ziara Mugango,Musoma na kubaini kuwa hakuna samaki huko,kwa sababu zile alizosema Hubert Sauper katika Darwin’s Nightmare, serikali ikabisha,miaka mitano imekwishapita.
Nataka niwaambie wasomaji kwamba serikali ilishakubali maoni ya filamu hiyo kimya kimya, na hapa nitaeleza kauli za Rais Kikwete na mawaziri wake.
Jumanne, Mei 13 mwaka 2008, Rais Kikwete alipokuwa akifungua kiwanda cha kusindika samaki cha TFDC,Ilemela,Mwanza, akasema wananchi waanzishe mabwawa ya kufugia samaki,maana Ziwa Victoria ‘linakauka’.
“Ndiyo njia pekee ya kuondokana na kitisho cha kupungua samaki katika Ziwa hili kubwa kuliko yote Afrika”, Rais alisema.
Wavuvi, wakiwemo haramu wengine kutoka nchi jirani za Kenya na Congo DRC walishaongezeka sana kutoka 51,935 mwaka 2002 hadi 98,015 mwaka 2007.
Zana za uvuvi zikiwemo haramu zilishaongezeka mno kutoka 15,434 hadi 29,730 katika kipindi hicho.Bila shaka Rais alishabaini ukweli wa mambo,kwamba kipindi kile wasaidizi wake walimpotosha kwamba hatuli ‘Mapanki’ kwa sababu walizojua wao!
Na uzembe wao ndiyo ulimfanya Sauper kupiga picha za filamu ile(nilishaandika jambo hili katika gazeti hili). Mwaka 2004 samaki waliovuliwa Ziwa Victoria walikuwa wenye uzito wa tani 750,000. Lakini mwaka 2007 samaki waliovuliwa katika Ziwa hili walipungua hadi tani 375,400 tu.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,wakati huo John Pombe Magufuli akachoma makokoro haramu,wakati maofisa uvuvi wakiwapora wavuvu sehemu moja na kuyauza kwingine-baadhi yao walikuwa na hayo makokoro haramu mengi tu. Samaki wa Musoma wakaendelea kutoroshwa hadi Nairobi na Ulaya kwa magendo.
 Takwimu zikawa zinapikwa tangu viwandani hadi Mamlaka ya Mapato(TRA) bila wasiwasi.
Waziri wa MAALIASILI na Utalii,Prof Jumanne Maghembe, Juni 11 mwaka 2007 wakati akifungua semina kuhusu uvuvi endelevu  hapo BoT,Mwanza akasema samaki wamekwisha,wakati bei imebeki ile ile tu.
 Prof. Maghembe akaagiza hadi Juni 11,mwaka 2008 samaki waliosalia angalau waachwe wazae uzazi mmoja tu!
“Pasipo kufanya mkakati wa kuepusha samaki kutoweka Ziwa Victoria,Tanzania haitaepuka ‘HUKUMU YA ULIMWENGU’ kwa kuruhusu rasilimali zake wakiwemo sangara kutoweka,na hivyo maisha ya watu kuathiriwa vibaya”, alisema Prof. Maghembe hiyo Juni 11 mwaka 2007.
 Hiyo hukumu ya ulimwengu aliyosema Prof. Maghembe ni  ipi kama siyo kilichosemwa na documentary hiyo ya Mapanki serikali ikabisha?
 Kwamba, sangara wa Ziwa Victoria waliliwa Ulaya, sisi tukabaki na njaa yetu na kuomba misaada, wakati wavuvi wakifa kwa ukimwi makambini,wakibugia gongo na dada zetu wakijiuza kwa marubani wa madege ya Kirusi-Ilyusin-kwa ujira wa dola 10
Niliitazama Filamu hiyo, DARWIN’S NIGHTMARE ofisini kwa Mkuu wa mkoa, Daniel Njoolay wakati huo kabla ya kuhamishiwa Rukwa.
 Niliitazama kwa mara ya pili ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Mwanza(MPC)nikaandika habari kadhaa na makala za kutosha. Habari iliyokaribia kunitia matatani,ni ile ya Alhamisi, Agosti 3,mwaka 2006 iliyotolewa katika Gazeti la Tanzania Daima,ikiwa na kichwa, “Mapanki yamgeuka J.K”
Katibu wa CCM, mkoa wa Mwanza,wakati huo,Mujuni Kataraia,akaitisha maandamano ya kuipinga habari hiyo, halafu akaniambia, “Kwanini kila mara wewe uko against na(unaipinga) serikali?”
Nadhani Rais Kikwete aliyapuuza maandamano yale. Ingawa alikuwa jijini Mwanza kwa mapumziko,hakujali maandamano yale ya kunipinga.
Darwin’s Nightmare,imejengwa katika Falsafa za mwanabaiolojia wa Kiingereza, Charles Robert Darwin(1809-1882) ya viumbe vyenye nguvu kuvitafuna dhaifu, “Survival of The Fittest” katika Ulimwengu wa utandawazi.
Wazungu wanapoacha akiba samaki wa maziwa yao na bahari, wanachuma hawa wa kwetu kwa bei chee,halafu wakiisha wanang’oa viwanda vyao na kutoweka huku wakituacha na njaa yetu-hii ndiyo Theory na ‘Darwinism’ na Survival of the Fittest. Wenye nguvu wanawala dhaifu ama masikini!
Tanzania ilivikwa kilemba cha ukoka kwamba ilikuwa msafirishaji namba wani wa sangara duniani,kumbe samaki sasa hawapo baada ya madege ya Kirusi, Illyushin kusomba takriban tani 50 kila dege kwa siku.
“Falsafa” hii ya Darwin haikutuzindua usingizini, waandishi kama Johnson Mbwambo wakaishia kubezwa na serikali,mwisho wa siku sasa kilio cha kutoweka kwa samaki kinasikika kila upande!
Samaki ni fursa muhimu katika nchi.Lakini, wameporwa na wawekezaji kwa bei poa, na hata Wacongo wanavua huko visiwani,maofisa wa maliasili wapo tu,wanapewa rushwa ndogo ndogo na samaki wanazdi kutoweka!
 Kitengo cha Globefish cha FAO kilishasema mwaka 2006 kwamba samaki wanatoweka kwa kasi Ziwa Victoria na kuwaacha Watanzania na njaa,na umasikini na dhiki nyingi huku watoto wa mitaaani wakigombea ubwabwa katika sufuria la mpita njia,mama ntilie!
 Madege ya Kirusi yalisomba sangara hadi yakaanguka Ziwani kwa kuzidisha uzito ili kukwepa Mamlaka ya Mapato(TRA).
Sauper, katika filamu hiyo ya mapanki alitukumbusha namna Yesu wa Nazareti alivyotumia visamaki viwili tu(Tanzania tulikuwa na masangara makubwa mengi tu)na mikate mitano kuwalisha zaidi ya watu 5,000 katika kijiji cha Bethsaida,wakasaza mabaki yaliyojaa vikapu 12!
Katika filamu hii,Darwin’s Nightmare, muujiza wa Yesu wa kuwalisha watu hao( Injili ya Marko 6:34-44 na Luka 9:10,11) ili Tanzania tujifunze kutumia rasilimali zetu vizuri kuwalisha watu wenye njaa siku hizi tunapolia na ukame.
Sauper, alimtangaza Yesu katika filamu hiyo kama kiongozi bora, anayejua kutumia rasilimali chache kwa maslahi ya wengi hadi kusaza vikapu 12!
 Laiti Yesu angekuwepo leo Tanzania,penye masangara makubwa haya, na jodari mithili ya wale wa Magufuli, dagaa, almasi, tanzanite,dhahabu,wanyamapori,misitu,matunda, mifugo,mito,bahari,milima mirefu na mabonde,bila kusahau madini mengi haya, watu milioni 43 wa Tanzania wasinge kula na kusaza vikapu bilioni nyingi?
Tatizo, Watanzania siyo wazalendo, na siyo viongozi tu wasio wazalendo, hata wavuvi siyo wazalendo kama wale wanafunzi wa Yesu walioleta visamaki viwili na mikate yao mitano Yesu akaibariki na kuwalisha watu zaidi ya 5,000!
 Tanzania, tuna njaa katika utajiri wa rasilimali? Sababu,hakuna viongozi wazalendo kama Yesu wa Nazarethi, na kila mtu ni mchoyo asiyewajibika.
 Tuna rasilimali tele,fursa tele.
Tuna ‘Jodari’ kama wale wa Magufuli na masangara makubwa, lakini yamekwisha na kutuacha masikini na wenye njaa-hatuna akili.
0786/0754-324 074









No comments:

Post a Comment