Tuesday, June 7, 2011

Kobra wa CCM Musoma vijijini hawajivui gamba


wanaogopa kuwavua magamba “Black Mamba” wa Musoma vijijini wanaohujumu chakula cha njaa?

        SIKU HIZI kuna falsafa ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) kujivua magamba,mithili ya nyoka,vijoka na majoka.
      Hata hivyo, yako majoka ndani ya CCM na serikali yake, hayataki kujivua magamba.
 Magamba ya nyoka huwa katika ngozi yake.
Kwa sababu hiyo,nyoka anapojivua magamba ya ngozi yake,ni kurejesha upya wake,yaani kurejerea ujana wake,ama nguvu zake za awali na kasi zake katika harakati zake za mawindo katika maisha-struggle for existence.
   Kuna aina nyingi za nyoka na majoka,mengine ni ya kufikirika tu; ya hadithini.
   Ukiachana na majoka ya hatari, ya hadithini, nyoka halisi wanaishi porini,majini,mashimoni,mapangoni na hata jangwani kuna majoka.
 Siku hizi, kuna ‘majoka’ hata ndani ya CCM yamepewa sharti la kujivua magamba,kuachana na tabia zao mbaya.
   Miongoni mwa majoka hatari sana, marefu,yaendayo kasi mithili ya kupaa hewani,ni King Cobra.
King Kobra, ana urefu wa futi 16; na akikugonga unapoteza fahamu na moyo husimama mara kufuatia sumu yake kali.
 Kuna Taipan wenye urefu mpaka futi 11; na wapo Black Mamba, na majoka mengine hatari sana kwa maisha ya viumbe wengine.
 Black Mamba, ni joka hatari, ambalo nalo hujivua magamba. Urefu wake kutoka kichwani hadi mkiani ni futi 14.Linatimka mbio kali. Hata hapa Afrika kuna majoka haya ambayo yanapomgonga mtu, kupona ni asilimia chache.
 Hata Musoma vijijini,mkoani Mara, wapo ‘Black Mamba’ wa kufikirika ama kusadikika, na wamepewa madaraka kuusimamia umma!
 Black Mamba, hutimka mwendo kasi wa maili 20 hivi(kama kilomita 30) kwa saa.
Kila joka hujivua magamba ili kurejesha nguvu zake,kasi zake na uwezo wake wa awali.
 Kibaiolojia, magamba ya nyoka katika ngozi yake ni mithili ya nguo zake.
Magamba ni mavazi ya nyoka. Kila nyoka hutambulika kwa mavazi yake, yaani ngozi yake. Koboko hujulikana kwa ngozi yake na magamba yake.
 Kubadili magamba, ni kubadili mavazi.
 Mavazi, humfanya mvaaji ajulikane alivyo.Mavazi, ni kitambulisho maridhawa kwa mhusika. Daktari, Polisi wa Usalama Barabarani,Mkunga ama fundi Makanika, hata mwanafunzi,hutambulika kwa mavazi yao-naam sare zao.
   Kuna msemo wa Kiingereza, kwamba,
”Clothes Makes the Man” Ukiwa na maana kwamba, kile anachovaa mtu humtambulisha kazi yake,tabia yake,mienendo yake na hata mapendeleo yake(Hobbies) katika maisha.
   Kujivua magamba, maana yake ni ‘kubadili mavazi’ yaani kubadili tabia,kubadilisha nia na mienendo,malengo na mapendeleo ama mazoea,yakiwemo mabaya.
  Naam, wachezaji wa Yanga, Simba, Manchester United, Chelsea, Barcelona n.k hutambuliwa kwa mavazi yao.
 Mchezaji wa Yanga akivaa jezi nyekundu hata mitaani siku isiyo ya mechi,kuna hatari  manazi wa Yanga, kumhusisha na U-simba, samba hivi..
 Kubadili mavazi, hufananishwa pia na kubadili tabia na mienendo ama mapendeleo ya mtu. Unaweza kumbaini kibaka, ama mwizi kwa mavazi yake.
 Utamtambua mwanaume shoga kwa mavazi yake; na mavazi tu yatakwambia ni yupi changudoa, na ni nani  Msabato au Mlokole, na yupi Mwislam.
 Inaposemwa kwamba, mchezaji wa timu moja amevua jezi ama ‘katundika daruga’ lake, maana yake kaachana na kucheza dimbani,na hataingia kuisaidia timu yake abadan.
  Kulingana na falsafa hii ya CCM na serikali yake kujivua magamba; yaani kuachana na tabia yake na mienendo yake ya awali, tunapata sababu ya kuchunguza na kutazama kwa makini tabia za baadhi ya vigogo wa serikali hususan wakati huu wa kugawa chakula cha njaa huko Musoma vijijini mkoani Mara.
  
 Naam, tunawajadili viongozi wa Chama na serikali mkoani Mara.
Tunawapeleleza vigogo wa serikali hii ya CCM huko Musoma, wakati huu Chama hiki tawala kinaposema kimebadili ‘magamba’ na mienendo yake, kwamba CCM kimefanya ‘matengenezo’ wakati serikali inapogawa chakula cha njaa kwa wenye njaa kwa utapeli.
  Mara, ni miongoni mwa mikoa ya hapa nchini inayokumbwa na ukame,na serikali tayari imepeleka chakula cha bei nafuu na kile cha bure kwa waathirika. Rorya, Tarime, Serengeti,Musoma mjini na Vijijini kuna ukame mkali na kuna njaa ya kutisha mwaka huu.
   Safu hii ilikuwa Musoma vijijini,katika kata ya Nyambono, Tarafani Nyanja siku ya Ijumaa na Jumamosi, Mei 27 na 28 Mwaka huu, wakati chakula cha njaa kilipoletwa kwa wenye njaa.
  Hakika,chakula cha njaa hakiwafikii wenye njaa. Kinapelekwa kwa polisi, watumishi wa serikali na wenyeviti wa vijiji,vitongoji, watendaji wa vijiji na kata, hasa wenye uwezo wa kukinunua chakula hiki kwa bei ya kuruka!
 Watendaji wa kata na vijiji hukiuza chakula hiki kwa wenye pesa; na kingine hupeleka nyumbani kwao wakale na familia zao na nyumba ndogo zao.
  Safu hii ilimsaili ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyambono,Musoma vijijini, Rehema Lebayo, ni kwa sababu gain alifanua siri sirini idadi na takwimu halisi za magunia ya mahindi yaliyoletwa katani mwake ili awagawie wenye njaa?
  “Hata kama nimekabidhiwa tani hamsini za mahindi, zinakuhusu nini? Na nikiamua kuwagawia wananchi gunia moja(Lina uzani wa kati ya kilo 90-100 hivi) wewe utanifanya nini?”
 Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyambono, Rehema Lebayo, aliniambia huku akinitukana na kunibeza kupita kawaida.
 Niliamua ‘kujivua gamba’ la uandishi wa habari, nikajivika uana harakati ili kuwahamasisha wananchi wa kata hii wanaokabiliwa na njaa kali, kuhoji uhalali wa miungu watu wa kata hii, akiwemo ofisa mtendaji kata,na wenzake,kuacha kudhani kwamba, chakula cha msaada kilicholetwa na serikali hii ya CCM, ilikuwa mali yao binafsi!
   Serikali  ilileta katani humo chakula cha njaa ili kiuzwe kwa bei nafuu ya shilingi 50 kila kilo,na kingine wapewe bure wasiojiweza kabisa. Hakikuletwa ili kigawanywe holela kufuatia mapenzi ya ofisa mtendaji wa kata na vigogo wenzake; ili magunia 100 ama zaidi wakagawane wao ama kuuzwa kwa bei kubwa ili kujitajirisha!
 Nilihamasisha umma, kutaka kujua kwamba, serikali ilileta katani Nyambono magunia 533 ya mahindi na wala siyo 400 kama ilivyodaiwa awali.
Pia, nikahamasisha wananchi kujua kwamba chakula cha njaa ni kwa ajili ya wananchi masikini wenye njaa,na wala siyo mali ya Ofisa Mtendaji kata na wasaidizi wake, ama nyang’au wachache waliotumia madaraka na kiburi cha utajiri kupora magunia zaidi ya 130!
Nikamtaarifu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Musoma juu ya njama hizi za kutaka kuficha magunia zaidi ya 100, nikamtaarifu Kamanda wa Polisi wa wilaya(OCD)ambaye alitoa amri wahusika wakamatwe na kufunguliwa mashitaka,lakini hawakukamatwa,badala yake wakataka sisi tukamatwe na kuswekwa rumande,kwa uchochezi!
 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma akamtuma Katibu Tarafa wa Nyanja na Ofisa Usalama wa Taifa(DSO)wilaya ya Musoma kuja Nyambono ili kujionea malalamiko ya wenye njaa kunyimwa chakula cha njaa.
 Ni Jumamosi, Mei 28 Katibu Tarafa wa Nyanja na DSO walipofika katika shule ya msingi ya Nyambono na kubaini kuwa,takriban magunia 22 ya mahindi yalifichwa katika chumba kimoja cha darasa,baada ya wananchi kukesha pale wakidai kugawiwa mahindi yote, kwa kuwa yaliletwa kwa ajili yao na wala hakikuletwa kwa ajili ya watendaji wa kata,vijiji,wenyeviti wa vitongoji na wenye pesa.
   Kufika hapo, vigogo hawa wa kata,vijiji na vitongoji,jitihada zao za kupora chakula cha njaa zikagonga ukuta wa zege.
 Huko vijijini Musoma,kuna miungu watu.Mtu mmoja aliyehoji kwa nini alinyimwa mahindi haya yaliyoletwa na serikali, aliswekwa rumande, zaidi ya saa 27, akaachwa huru kwa masharti ya kuheshimu mamlaka!
 Hata hivyo,licha ya Katibu TARAFA wa Tarafa hii ya Nyanja na Ofisa Usalama wa Taifa wa wilaya ya Musoma,kubaini kuwa vigogo wa kata ya Nyambono walitaka kuhujumu chakula cha njaa, walikigawa holela tena kwa upendeleo wakawakosesha walengwa, hakuna hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya hawa vigogo ambao ni miungu watu.
 Bado wanazidisha vitisho kwa raia na kutaka kuwasweka rumande mjini Musoma kwa siku 14,kwa madai kuwa ni wachochezi.
  Sasa, ujiulize: Chakula cha njaa,ni kwa ajili ya wananchi wenye njaa, au kwa vigogo na wafanyabiashara wenye pesa nyingi?
 Chakula hiki,hutolewa na serikali katika maghala kwa nia ya kuokoa maisha ya wanaokufa njaa, ambao ni fukara,au kutengeneza vitambi vya hawa miungu watu wa vijijini-polisi, watendaji wa kata na vijiji, wenyeviti wa vitongoji na vijiji na maswahiba wao,wataalam walioko vijijini?
   Ndiyo maana tunajiuliza; kwa nini mwananchi wa kawaida anapohoji zoezi lolote likiwemo la kugawa chakula cha njaa huko Musoma, anageuka haini na mwasi na kuishia kuswekwa rumande?
  Ndiyo maana,tukahoji: ‘Majoka’ yaliyomo katika hii serikali ya CCM hayapaswi kujivua magamba?
Miungu watu wa serikali ya CCM Huko Nyambono,Musoma,mkoani Mara, hawapaswi kujivua magamba?
 Kwa nini CCM inapojivua magamba, imewasahau hawa watendaji wa kata wanaopora chakula cha njaa, na kuwafanya wananchi wafe njaa?
 Kwa nini vijoka na majoka ndani ya vijiji na kata huko Musoma na kwingineko nchini,huachwa kutamba na kuwang’ata raia wenye njaa kwa sumu kali,bila kukamatwa na kuvuliwa magamba?
 Au,tuseme Musoma vijijini, hususan katani Nyambono, kuna “Black Mamba” wa hatari ambao hata CCM yenyewe huwaogopa kuwavua magamba?
 Iwapi sasa falsafa ya CCM kUJIVUA MAGAMBA,Musoma, huko mkoani Mara?
     0786-324 074



 

No comments:

Post a Comment