Friday, June 24, 2011

Tanzania haimwitaji Kikwete, Dk. Slaa wala Prof.Lipumba,tunamhitaji rais mseja, tena mjane!



NILIMPIGIA kura Rais Jakaya Kikwete, lakini nimepata mashaka moyoni mwangu!
  Siyo kwamba, Kikwete ni Rais mbaya; la hasha.
Aweza kuzidiwa na Dk. Slaa au Lipumba.
. Nafurahishwa na vitu vingi anavyofanya Rais wetu; lakini ningependa Tanzania iongozwe na Rais mwenye sifa mbadala, ambaye hajawahi kuwepo.
Sifa mbadala hizi, hawezi kuwa nazo Kikwete, Mbowe, Slaa ama Lipumba.

   Ningependa sasa Tanzania iongozwe na Rais mwenye sifa za pekee ili kuondokana na majanga kama haya ya viongozi kuendesha Biashara zao wakiwa Ikulu. 
Naam, namtaka Rais ambaye ana sifa ambazo Kikwete hana! Lipumba na Mbowe,hawana! Slaa hana!

   Nimeorodhesha hapa baadhi ya sifa ninazotaka Rais mpya baada ya Kikwete awe nazo:
Rais asiwe na mke, yaani awe mseja; na awe hivyo kipindi chote cha kuwa  kwake Ikulu yetu ya Magogoni, Dar es salaam !

   Pili, Rais atakayekuja baada ya mhula wa Kikwete kumalizika mwaka 2015, awe yatima.
Rais asiyekuwa na ndugu na jamaa wenye madhambi yanayoigubika nchi kwa kashfa; tena kashfa zenyewe kubwa zinazopamba kurasa za mbele za magazeti.

   Naam. Rais asiye na mke anayepenyeza pua yake katika masuala ya uongozi wa nchi, wakati hakuna aliyempigia kura kufanya hivyo! Nadhani wakumbuka vimbwanga vya Lucy Kibaki,huko Nyayo.
Rais mwenye mke ambaye anafungua makampuni yanayoendesha biashara pengine bila kulipa kodi. 
Mke wa Rais(First Lady) ambaye atapewa leseni na kukopeshwa fedha na mabenki kwa kasi ili kufanya biashara kubwa kubwa, akijidai mjasiliamali.
    Lazima Tanzania yenye watu kama Milioni 43 iwe na Rais mwenye sifa za pekee, kuliko Benjamin William Mkapa, au Jakaya Kikwete. Lipumba, Mbowe au Dk. Slaa.
Mwenye hekima, mtu wa haki, mwenye akili, lakini hana familia, hana jamaa wa kumharibu akili awapo Ikulu pale.Ikulu pasichafuliwe na jamaa na ndugu za rais au mkewe.
   Nimewahi kusikia tetesi za wake za Marais wastaafu, jamaa zao na watoto wao kuitumia vibaya ikulu kufanya biashara. Nakiri, sijawahi kusikia tetesi za Mjane wa Hayati Mwalimu, Mama Maria Nyerere kutumia Ikulu kufanya biashara.
    Tetesi kwamba Benjamin Mkapa na Mama Anna Mkapa waliendesha kampuni yao , ANBEN wakiwa Ikulu, zinanivuruga akili. Akina Mama Salma Kikwete nao wana vikampuni vyao,kupitia Ikulu..havitozwi kodi.
Biashara hiyo ya Mkapa na Mama Anna, iwe halali au haramu, si hoja kwangu. 
Lakini, napendekeza Tanzania isiwe na Marais wenye familia zinazowasukuma kufanya biashara mapema wakiwa Ikulu, ili kukimbia umasikini!
    Wapo marais waaminifu na ndugu zao na watoto wao ni waaminifu; hawaitumii vibaya Ikulu.
   Kadhalika, wapo wake wabaya wa marais  wenye wapambe, ndugu na jamaa wanaowashauri vibaya ili kujinufaisha na Ikulu.
Wake, jamaa, wapambe na ndugu hawa nao hujigeuza maofisa wa serikali.
   Nani aliyewachagua kufanya chochote? Nani aliwateua kuwa na sauti hadi kuwafokea mawaziri? Kama ni hivyo, basi tungepewa nafasi ya kuwapigia kura hawa jamaa za marais kabla hawajaingia Ikulu.
   Au, kwa sababu ndugu yao anapoingia Ikulu, wao hujigeuza ‘Mabalozi’ ama ‘Wabunge’ Fulani, basi wangepelekwa kula kiapo mahakamani, kwamba hawataitumia Ikulu kwa maslahi binafsi kipindi chote cha Bwana, Bibi, Mjomba au Shemeji yao, anapokuwa Ikulu.
   Leo, tunashuhudia mbio kali za watoto wa vigogo kutaka kuwania madaraka. Sisemi kwamba watoto wa wakubwa hawana haki ya kuwania madaraka, la hasha! 
Wawe watoto wa wakubwa wenye Visheni; waachane na hadithi za kurithi damu za uchifu wenye falsafa ya kurithishana madaraka.
    Siasa si maneno matupu majukwaani. Ni kuzifanya sera zizae maendeleo ya watu. 
Je, watoto wa vigogo wanaosaka madaraka kwa udi na uvumba, kupitia vyama Tawala, wanayo Visheni hii?
 Wanamiliki mabilioni kwa muda mfupi, wanamiliki mahoteli makubwa ya fahari.
    Au,wanawania madaraka  ‘kutetea’ madhambi ya baba zao pindi wanapomaliza mhula wao, baada ya kushindwa kubadili Katiba ili kurefusha muda wa kusalia madarakani?
   Licha ya wake za marais kudaiwa kufanya biashara ama kufungua vikampuni visivyotozwa kodi wakiwa Ikulu, watoto wao wamekuwa wakiwasaidia baba  au mama zao kutawala kwa mabavu. 
Wamekuwa wakishiriki kuwatesa raia na kukiuka Haki za Binadamu.
    Rais wa zamani wa Liberia, Charles Ghankay Taylor ambaye juzi amesusia mashtaka ya Uhalifu wa kivita  huko The Hague, Uholanzi, mtoto wake, Charles Mc Arthur Emmanuel, au Charles Taylor Jr; ambaye Liberia alifahamika sana kama, Roy Belfast Jr, alitiwa mbaroni Desemba 15 mwaka 2005, akafunguliwa kesi mbili.
   Alitiwa mbaroni huko Miami , Marekani kwa kosa la kuwatesa kinyama waliompinga baba yake, na pia alikuwa na kesi ya kughushi Hati ya kusafiria.
   Ghankay Taylor, ambaye sasa anasusa mashitaka The Hague, alishirikiana na rafikiye, Foday Sankoh, wa kikundi cha RUF kufanya unyama Sierra Leone na kuwauzia waasi hao silaha kwa kubadilishana na almasi.
    Licha ya kuwepo kwa tetesi za wake za marais kuingilia mambo ya serikali, kuwafokea mawaziri na hata kuwatwanga makofi waandishi wa habari hapa Afrika, watoto wa Marais pia wanatuhumiwa kuhusika na kashfa nzito.
    Gideon Moi, mtoto wa Rais wa zamani wa Kenya , Mzee Moi, ana tuhuma za kuhusika katika kashfa anuai za ufisadi nchini humo. 
Wengine, wakiwemo watoto wa wakubwa wa Dunia hii, wanatuhumiwa kubwia unga, kuuza ama kuvuta bangi na kuendesha biashara haramu hata katika Vyuo vikuu, lakini kwa sababu ya upendeleo, woga au kujikomba, vyombo vya Usalama hujikuta vikishindwa kuwachukulia hatua.
Watoto wa akina Bush na Alfred Gore, wabwia unga!
   Hata kama waliua, au hata kama walijeruhi ama kutaharukisha umma, huachiwa mara moja, wasiyaone magereza!
   Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Bi Margaret Thatcher(81), Mark Thatcher(54) lituhumiwa kuendesha biashara haramu na kufanya uhaini.Baadaye alikwenda kupindua serikali ya Guinea ya Ikweta, akatiwa mbaroni huko Sauz.
   Sir Mark Thatcher, mwenye vituko vya “Front Page” katika magazeti, aliwahi kupotea katika Jangwa la Sahara . Alipotea kwa siku kadhaa, wakati akishiriki Mashindano ya Paris-Dakar( Senegal ) Rally, akasababisha Bi Thatcher kuangua kilio hadharani, wakati akiwa Waziri Mkuu!
    Margaret Thatcher, alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza tangu mwaka 1979 hadi 1990.
Lakini mtoto wake huyo aliwahi kutiwa mbaroni na polisi wa Afrika Kusini kwa tuhuma za kuongoza njama za kupindua serikali ya Guinea ya Ikweta.
    Ametiwa mbaroni na vikosi vya usalama mahali pengi Afrika; hata Zimbabwe .
Polisi wa Afrika Kusini walisema, walikuwa na ushahidi wa kutumainiwa, kwamba Mark Thatcher aliwapa fedha waasi wa Guinea ya Ikweta, ili wampindue Brigedia Jenerali Mstaafu, Teodoro Nguema Mbosongo, Rais wa Baraza la Kijeshi la nchi hiyo, aliyedaiwa kuvunja Haki za Binadamu.
   Guinea ya Ikweta ni ya tatu Afrika kwa kuzalisha mafuta kwa wingi.
Pengine, Mark anayetuhumiwa hata kuhusika katika biashara haramu ya silaha, alitaka mafuta ya nchi hiyo. Naam, hao ndiyo watoto wa wakubwa.
   Hata hivyo, wapo watoto wa viongozi waliopata kuwa viongozi wazuri. Waziri Mkuu wa zamani wa India , Indira Ghandhi, alikuwa Binti wa Waziri Mkuu wa Kwanza wa India , Jawaharlal Nehru. Baadaye, Sanjay na Marehemu Rajiv Ghandi nao wakafuata nyayo.
    John Quincy Adams aliyekuwa Rais wa Marekani 1825-1829, alikuwa mtoto wa Rais John Adams aliyetawala Marekani mwaka 1791 hadi 1801.
Adams alikuwa Rais wa pili baada ya George Washington.
    Yupo George W.Bush ambaye baba yake George Walker Albert Bush, alikuwa rais miaka ya 90. Nduguze, kama Jeb Bush ni viongozi; ni wanasiasa maarufu. Hata hivyo, katika orodha, wapo wengi viongozi watoto wa viongozi kama akina Sir Mark Thatcher wahaini, wezi, wauza unga na wahujumu uchumi, wao na wapambe wao, lakini hawakamatwi wala kuhojiwa!
    Wako akina Roy Belfast Jr. wanaoghushi hati mbalimbali na  kufanya biashara haramu na halali, wanaotesa wapinzani wa serikali za baba zao, ambao pia hugeuza Ikulu kuwa ‘mapango’ ya wanyang’anyi ama ‘Mungiki’ wanao ifanyia jamii ugaidi mkubwa.
   Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kuwaonya watu kuiogopa Ikulu.
Ikulu ni mahali Patakatifu. Si mahali pa kufanyia biashara hata ziwe halali na nyeupe kama sufi.
Rais anapoboronga, ama mkewe, jamaa au shemeji zake wanapoendesha magendo ikulu(Doing Business from Ikulu), ndipo harakati za kutafuta warithi huanza!
    Akina Umaru Yar’ Adua wa Nigeria wametafutwa na akina Obasanjo mara nyingi sana kupitia kitu ambacho si Uchaguzi, bali unyafuzi na Uchafuzi Mkuu wa Haki, Demokrasia na Uhuru Afrika!
    Ni kwa sababu hii, ningependekeza wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu, angetazamwa Mgombea ambaye jamaa, wapambe, rafiki, mke na watoto wake hawataiabisha ikulu kwa magendo, vituko, skandali na biashara zisizolipiwa kodi.
 Marehemu Frederick Chiluba alikosa kufungwa jela na Hayati Levy Patrick Mwanawasa, maradhi yalimwokoa kutiwa mangenge kwa kosa la kufanya deal ikulu ya LUSAKA,zambia.
     Kama watoto, wake na wapambe wa Rais wangepelekwa Bungeni kwanza kuthibitishwa na kula viapo mahakamani, basi hofu kama ya Rais Jakaya Kikwete ya kumchunguza mtangulizi wake, isingekuwepo.
Hofu ya kutafuta kubadili katiba isingekuwepo, kama wake, watoto na jamaa wa Rais wangedhibitiwa na Bunge au Mahakama.
    Lakini, pamoja na haya yote, ili kuepuka Marais kufanya Biashara Ikulu, napendekeza Tanzania ingekuwa na Rais Mseja,
lakini asiye mzinzi wa kukwapua wake za raia wake; asiyekaribisha machangudoa Ikulu na kuitia unajisi nchi, rais mjane asiye na familia ya kumtia majaribuni; na yatima ambaye baba, mama na watoto wake ni raia wake.
   0715 324 074
   0754  324 074
congesdaima@yahoo.com

No comments:

Post a Comment