Wednesday, June 8, 2011

maafa ya NATO kwa ulimwengu


     

Umoja wa kujihami wa nchi za magharibi, NATO, ni umoja ulioundwa kwa madhumuni ya kujihami kijeshi.
Ni makubaliano ya kumhami kwa pamoja mwanachama wa umoja huo endapo atashambuliwa.

Ingawa lengo la NATO wakati wa kuundwa kwake lilikuwa kujihami dhidi ya mashambulizi yoyote, lakini mashambulizi yaliyokuwa yakiogopewa na kutarajiwa zaidi yalikuwa kutoka kwa iliyokuwa USSR. USSR ilikuwa muungano wa jamhuri mbali mbali jirani na Russia (Urusi), ikiwemo Russia yenyewe, zilizokuwa zikifuata siasa ya kikomunisti. Muungano huo ulisambaratika na kwa sasa haupo.

Kipindi cha kabla USSR haijasambaratika, kilikuwa cha vita baridi kati ya kambi mbili zilizokuwa na nguvu duniani. Kambi moja ya nchi za magharibi iliongozwa na Marekani na kambi nyingine ya nchi za mashariki iliongozwa na USSR. Ni katika kipindi hicho, nchi zilizokuwa katika kambi ya magharibi zilipounda umoja wao wa kujihami waliouita NATO.

Kwa mazingira ya wakati huo ya vita baridi, NATO ilikuwa muhimu kwa nchi za magharibi kiusalama; lakini kwa sasa ambapo hakuna tena hofu ya kushambuliwa, umuhimu uliosababisha kuundwa kwake haupo tena. Hata hivyo, idadi ya nchi wanachama wa NATO imekuwa ikiongezeka hata baada ya kusambaratika USSR. Nchi zilizojiunga baada ya kusambaratika USSR sio za magharibi tu bali pia zilizokuwa zikiunda USSR na zilizokuwa washirika wa karibu wa USSR. Hata Russia, iliyokuwa mdau mkubwa wa USSR na ambayo bado ina nguvu imewahi kuombwa kujiunga.

Baada ya kusambaratika kwa USSR, wengi wangetarajia umuhimu wa NATO kupungua. Hata hivyo, umuhimu wake unaonekana kuongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya wanachama wake.  La kushangaza ni kwamba, mataifa yanayoungana ni yale yenye nguvu zaidi duniani. Hapo ndipo tunapaswa kujiuliza: Yanaungana dhidi ya nani?

Kimantiki kitendo cha kuunganisha mataifa makubwa na kuacha madogo kunamaanisha kuwa, ama maslahi ya mataifa makubwa hayazihusu nchi ndogo, huathiriwa na nchi ndogo, au ni dhidi ya nchi ndogo. Hapa napo tunapaswa kujiuliza: Ni maslahi gani yanayozihusu nchi kubwa tu na kutozihusu nchi ndogo? Nchi ndogo zinawezaje kuathiri maslahi ya nchi kubwa? Je, Mataifa makubwa kuungana kuna athari gani kwa nchi ndogo na hasa zikiwa zimetengana?

Kwa muda mrefu, mataifa makubwa na hasa ya Ulaya yamekuwa na maslahi katika Afrika na nchi nyingine za dunia ya tatu. Mara kwa mara katika kutafuta maslahi hayo, mataifa haya yamekuwa yakikumbana na vikwazo mbali mbali vikiwemo viwili vikubwa. Kikwazo cha kwanza ni migongano ya maslahi miongoni mwao unaotishia hali ya usalama na upatikanaji wa maslahi yenyewe. Kikwazo cha pili ni upinzani kutoka kule maslahi hayo yanakopatikana.

Katika hali hiyo, mashikamano na maelewano miongoni mwao ni muhimu ili kusuluhisha tofauti zao na kuunganisha nguvu katika kukabiliana na kikwazo cha pili, hivyo kurahisisha upatikanaji wa maslahi kwa kila mmoja wao.

Umuhimu wa maelewano miongoni mwa mataifa makubwa unaonekana hata wakati mataifa hayo yalipokuwa yakigombania kuitawala Afrika. Badala ya kuvutana wao kwa wao na pengine kupigana katika kugombea maeneo, walikaa pamoja kwa maelewano mjini Berlin nchini Ujerumani na kuigawana Afrika.  

Bila maelewano ya wenyewe kwa wenyewe, ingekuwa kazi ngumu kuingia na kuitawala Afrika. Maelewano yao yaliwawezesha kila mmoja wao kuelekeza nguvu zake katika kupambana na upinzani kutoka nchi anayotaka kuitawala badala ya kuzielekeza pia kwa wenzake hali ambayo ingewapunguzia wote uwezo wa kupambana.

Kama ilivyokuwa wakati huo, hata sasa maelewano miongoni mwa mataifa makubwa yanahitajika ili iwe rahisi kwao kuchukua na kugawana rasilimali za dunia. Maelewano yao huwawezesha kuelekeza nguvu zao katika kuzima upinzani kutoka nchi raslimali hizo zinapopatikana badala ya kuzipoteza katika ugomvi wa wenyewe kwa wenyewe.

Maelewano yao pia huwawezesha kuunganisha nguvu pale ambapo inamwia vigumu mmoja wao kupambana akiwa peke yake. Nguvu hizo sio za silaha peke yake bali pia za propaganda ili kuhalalisha matendo yao na kuwashinda kisaikolojia wale wanaokwamisha upatikanaji wa maslahi yao.  

Ni dhahiri kwamba, tofauti na wakati wa kuundwa kwake, lengo la NATO kwa sasa baada ya USSR kusambaratika haliwezi kuwa kujihami. Katika hali ya kawaida tungetarajia NATO ivunjike, lakini badala ya kuvunjika inazidi kuimarika. NATO inahitajika kwa walioiunda katika kujenga mshikamano na maelewano miongoni mwa wanachama na mataifa mengine makubwa ili iwe rahisi kwao kuchukua rasilimali za dunia ya tatu.

Historia inaonyesha kuwa, tangu zamani mataifa makubwa yamekuwa yakifaidika kutokana na rasilimali za mataifa madogo. Mifumo mbali mbali ya kisiasa, kiutawala na kiuchumi ilianzishwa au kusitishwa katika kufanikisha upatikanaji wa rasilimali hizo kutegemea mahitaji ya wakati, lakini mifumo yote ililenga upatikanaji wa rasilimali hizo.

Ingawa mifumo hiyo iko mingi kutegemea vigezo vitumikavyo kuiainisha, tunaweza kuiainisha kutegemea wakati ilipotumika katika historia ya dunia. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kuitaja mifumo hiyo kuwa ni utumwa, ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo. Kwa sasa tuko katika kipindi cha ukoloni mamboleo.

Kabla ya ukoloni (ukoloni mkongwe), mataifa ya Ulaya ambayo ndiyo yaliyokuwa na nguvu zaidi duniani, yalikuwa yakifaidika na biashara ya utumwa na watumwa kutoka Afrika. Biashara hiyo iliendelea hadi pale ilipokosa faida kiuchumi kwa mataifa hayo wakati wa mapinduzi ya viwanda barani Ulaya.

Wakati wa mapinduzi ya viwanda na baada ya hapo, mataifa yale yale ambayo kabla ya hapo yalikuwa yakifaidika na utumwa, yaliupiga vita kwa sababu uligeuka kuwa kikwazo kwa maendeleo ya uchumi uliotegemea viwanda. Katika hali hiyo, haikuwa bahati tu ya kihistoria Uingereza, nchi ambayo ndiyo iliyokuwa imeendelea zaidi kiviwanda na ambayo ingeathirika zaidi endapo biashara ya utumwa ingeendelea, kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utumwa.

Kwa kuwa propaganda ni mbinu mojawapo ya kivita, katika kupambana na utumwa mbinu hiyo ilitumika pia na bado inatumika kuwafanya watu waamini kuwa biashara ya utumwa ilikomeshwa kwa sababu za kibinadamu na walioikomesha ni watu wema sana waliojitolea kwa manufaa ya binadamu wenzao. Ukweli ni kwamba sababu za kiuchumi ndizo zilizokuwa muhimu. Ubinadamu ulitumiwa tu kama mbinu mojawapo ya kupambana na utumwa kwa maslahi ya kiuchumi.

Huko Marekani, vita ya wenyewe kwa wenyewe iliwahi kuzuka baada ya mgongano wa maslahi ya kiuchumi kati ya majimbo yaliyotaka utumwa uendelee na yale yaliyotaka ukomeshwe. Utumwa ulikuwa kikwazo kwa maendeleo ya viwanda katika majimbo ya kaskazini hivyo yakataka ukomeshwe, lakini utumwa huo huo ulikuwa neema kwa maendeleo ya kilimo katika majimbo ya kusini hivyo yakataka uendelee. Mgongano huo wa maslahi ulisababisha vita kati ya majimbo ya kaskazini na ya kusini.

Abraham Lincoln, aliyekuwa raisi wakati huo na mzaliwa wa moja kati ya majimbo ya kaskazini anasifika sana kwa juhudi zake za kupambana na utumwa. Hata hivyo, yeye mwenyewe aliwahi kunukuliwa wakati vita ikiendelea akisema: “Kikubwa ninachohitaji, ni kuona majimbo ya Amerika yakiwa yameungana. Ikiwa hilo litafanikiwa kwa kupiga vita utumwa, nitaupiga; na ikiwa litafanikiwa kwa kuupigania, nitapigania.” 

Ingawa kwa maslahi ya kaskazini anakotoka, Lincoln alikuwa akipiga vita utumwa, lakini kwa maneno yake hayo anaonyesha kuwa alifanya hivyo kwa kujali zaidi maslahi ya kiuchumi na kisiasa, ambayo yangeweza kuathirika endapo majimbo ya kaskazini na kusini yangetengana, kuliko alivyojali ubinadamu.   

Kama ilivyokuwa kwa utumwa kukomeshwa baada ya ukoloni kuonekana una maslahi zaidi kiuchumi, ukoloni mkongwe nao ulikomeshwa baada ya ukoloni mamboleo kuonekana una maslahi zaidi.

Ingawa wengi huamini kuwa tuna uhuru ambao tuliupata kwa kuupigania, tukiingalia vizuri historia ya Afrika tunaweza kubaini kama kweli harakati zetu za kudai uhuru ndizo zilizotuletea uhuru huo, na kama hicho tunachoita uhuru ni uhuru kweli.

Historia inaonyesha kuwa mapambano ya kuwaondoa wakoloni, kama kweli yanastahili kuitwa mapambano, hayakuwa makubwa kama yale ya kuwazuia kuingia. Kwa nini wakoloni walitumia nguvu kubwa kupambana na upinzani wakati wa kuingia ili watutawale, lakini hawakutumia nguvu kidogo iliyohitajika kuwafanya waendelee kutawala?

Iliwezekanaje washinde mapambano kwa wakati mmoja katika nchi zote miaka ya 1880 walipoingia na washindwe kwa wakati mmoja katika nchi zote miaka ya 1960 walipoondoka?

Baada ya uhuru, yaliyokuwa makoloni yameendelea kushikamana na mkoloni wao wa zamani. Waliotawaliwa na Uingereza walijiunga na Jumuia ya Madola na waliotawaliwa na Ufaransa wamebakia kuwa na uhusiano wa karibu na Ufaransa. Kwa nini nchi zilizokuwa makoloni zishikamane na wakoloni wao mara tu baada ya kupata uhuru hadi leo? Inawezekanaje waliokuwa wakipambana wawe marafiki, tena wa kuaminiana, mara tu baada ya mapambano? Inawezekanaje aliyeshinda vita ndiye amnyenyekee aliyashindwa?

Jumuia ya Madola huundwa na nchi zilizowahi kutawaliwa na Uingereza isipokuwa Marekani. Kwa nini Marekani haimo kwenye Jumuia ya Madola ingawa na yenyewe iliwahi kutawaliwa na Uingereza na lugha yake ni Kiingereza?

Kwa nini katika Jumuia ya Madola kiongozi lazima awe ni Muingereza mkoloni wao wa zamani? Kwa nini mara kwa mara Uingereza hutishia baadhi ya nchi kufukuzwa kwenye Jumuia ya Madola lakini hazifukuzwi? Kwa nini nchi zinazotishiwa hutishika?

Waingereza na Wafaransa wana nguvu kuliko Wareno. Kimantiki kama ni kuwatoa wakoloni kwa mapambano, ingekuwa rahisi kuwatoa Wareno kuliko Wafaransa na Waingereza. Kwa nini basi makoloni yaliyokuwa yakitawaliwa na Wareno ndiyo yaliyochelewa kupata uhuru kuliko yaliyotawaliwa na Waingereza na Wafaransa?

Ingawa kuna majibu mengi ya maswali haya, jibu moja la ujumla ni kwamba, bado tunatawaliwa. Waingereza na Wafaransa waliondoka lakini hawakuacha makoloni yao yakiwa huru, bali walibadili tu mfumo wa utawala kwa kuachana na ukoloni mkongwe na kutawala kimamboleo.

Mreno alichelewa kuondoka kwa sababu alikuwa hajawa tayari kukabiliana na mfumo mpya wa kutawala makoloni yake kimamboleo. Hata kuondoka kwake kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na shinikizo za kimataifa kuliko mapambano ya wapigania uhuru. Waingereza na Wafaransa walikuwa tayari. Katika hali hiyo, ni dhahiri kuwa wazungu waliondoka Afrika kwa uamuzi wao baada ya kuamua kubadili mfumo wa utawala kutoka ukoloni mkongwe kuwa ukoloni mamboleo.

Wazungu waliamua kuondoka baada ya kubaini kuwa ukoloni mkongwe una gharama kubwa kiuendeshaji kuliko ukoloni mamboleo. Dhana ya kupigania uhuru imeingizwa vichwani mwetu ili kutupumbaza na kutuaminisha kuwa tuna uhuru kamili, tena tulioupata kwa juhudi zetu. Licha ya kwamba, sio juhudi zetu zilizotuletea kile tunachoita uhuru, kupeperusha bendera zetu hakujatufanya tuwe huru.

Ukoloni mamboleo ni hali ya nchi moja kujenga ushawishi wake kwa nchi nyingine kiutawala, kisiasa, kiutamaduni, kiuchumi, kijeshi n.k ili nchi inayojenga ushawishi huo inufaike na iendelee kunufaika kutoka kwa nchi inayoshawishiwa bila kujali kama kuna manufaa au hakuna kwa nchi inayoshawishiwa.

Njia zinazotumiwa kuimarisha ushawishi huo ni pamoja na kueneza propaganda, kuweka viongozi vibaraka na hata kuingilia kati kijeshi inapokuwa lazima. Hivyo ndivyo NATO inavyofanya Libya kwa sasa, na Marekani ilivyofanya Iraq miaka michache iliyopita.

Propaganda ni habari za uwongo au zilizotiwa chumvi sana ili kuwashawishi watu wakubaliane nazo. Lengo la propaganda, ni kuwapumbaza watu ili waamini na kukubali kile mpiga propaganda anachotaka.

Katika mifumo yote ya kutawaliwa, mtawaliwa huaminishwa kuwa mtawala ni bora kwa kila hali na mtawaliwa ni duni katika kila hali. Tangu enzi za utumwa, ukoloni mkongwe na sasa ukoloni mamboleo, hali hiyo imekuwapo ili kumfanya mtawaliwa aendelee kuwa tegemezi kwa mtawala.

Kwa muda mrefu nchi za Afrika na dunia ya tatu, zimeaminishwa kuwa mambo ya kimagharibi ni bora na yenye manufaa kwao. Imani hiyo ndiyo inayotufanya tuwe tegemezi hivyo kuwarahisishia wakoloni (mamboleo) wetu kazi ya kututawala. Anayeonekana kuamini kinyume chake au tofauti na hivyo, hutazamwa kwa tahadhari na nchi hizo (za magharibi) na juhudi za makusudi huchukuliwa ili imani yake isienee kwa wengine.

Namna ya kuhakikisha kuwa imani yake haienei kwa wengine ni pamoja na kuondolewa madarakani kama ni kiongozi na hata kuuwawa. Sababu mojawapo ya NATO kuipiga Libya kwa Lengo la kupindua serikali ya Muamar Gaddafi ni kutokana na Muamar Gaddafi kujiamini na kujitegemea kimawazo na kiuchumi badala ya kutegemea nchi za magharibi.

Hali hiyo ya Gaddafi kujiamini na kujitegemea haitakiwi na nchi za magharibi kwa sababu licha ya kuzikosesha maslahi kutoka Libya, hushawishi nchi nyingine kujiamini na kujitegemea kimawazo pia, hali ambayo ni kikwazo kwa maslahi ya nchi za magharibi.

Juhudi za kujenga utegemezi zilifanyika hata wakati wa utumwa na wa ukoloni mkongwe.Watumwa waliaminishwa kuwa jambo muhimu na lenye manufaa kwao ni kutii amri za mmiliki wao. Hata dini zilitumika kufanya hivyo. Watumwa waliokaidi amri za wamiliki wao waliadhibiwa vikali sana na hata kuuwawa kikatili ili kufuta kabisa mawazo yao na ya watumwa wengine ya kukaidi amri za wamiliki wao, na kuondoa kabisa uwezekana wa watumwa kufikiria kukaidi.

Watumwa waliokuwa na nguvu au ushawishi kwa watumwa wenzao waliandamwa na kudhalilishwa hata kwa makosa ya kubambikizwa mradi tu kufanya hivyo kuondoe ushawishi wao na kuwaogopesha watumwa wanyonge. Mbinu mbali mbali zilitumika kuhakikisha kuwa matumaini yote ya mtumwa yapo kwenye kutekeleza amri za mmiliki wake na sio vinginevyo.

Hata sasa enzi za ukoloni mamboleo mbinu hizo hutumika. Mwenye nguvu na ushawishi anayeweza kuathiri imani ya watawaliwa kwa mtawala wao lazima adhalilishshwe ikiwa ni njia muhimu ya kuhakikisha kuwa wakati wote matumaini ya mtawaliwa yako kwa mtawala wake. Hivyo ndivyo alivyofanyiwa na Wamarekani Sadam Hussein wa Iraq, na kwa sasa anavyofanyiwa na NATO Muamar Gaddafi wa Libya.

Namna nyingine ya kurahisisha upatikanaji wa rasilimali kutoka mataifa madogo ni kuyafarakanisha yasiwe na umoja. Enzi za utumwa viongozi wa nchi zilizokuwa zikitoa watumwa walifarakanishwa na kila mmoja wao kuaminishwa kuwa mafarakano hayo yana manufaa kwake.

Viongozi hao walishawishiwa kwa njia mbalimbali kujihusisha na ukamataji wa watumwa, kuuza watumwa hao na kulinda misafara ya watumwa. Zawadi ndogo ndogo walizokuwa wakipewa zilitosha kuwashawishi kushambuliana katika jitihada za kila mmoja wao kupata watumwa wengi iwezekanavyo kutoka himaya ya mwingine. Kwa ujumla waliaminishwa kuwa biashara hiyo ni muhimu sana kwao kiuchumi na kiutawala kuliko biashara nyingine.

Hata sasa enzi hizi za ukoloni mamboleo, mbinu za kutufarakanisha au kuhakikisha kuwa hatuungani hutumiwa. Mbinu mojawapo ni kuwasakama wale wanaotaka kutuunganisha. Muamar Gaddafi ni mmoja kati ya watu wanaotaka kutuunganisha hivyo lazima asakamwe na wakoloni mamboleo. Hivyo ndivyo NATO inavyofanya kwa sasa nchini Libya.

Mbinu nyingine ni kuchochea hali ya kutoelewana kati ya makundi ndani ya nchi au wananchi na serikali yao kwa visingizio mbalimbali kama vile demokrasia na haki za binadamu. Demokrasia ya vyama vingi iliingizwa kwetu na wakoloni mamboleo bila ridhaa yetu ili kujenga mazingira rahisi ya kutufarakanisha endapo wataamua kufanya hivyo. Mazingira hayo pia huwarahisishia uwekaji wa viongozi vibaraka wao.

Mfumo huo pia umeambatana na urahisi wa kuanzisha vikundi mbali mbali vya kijamii ambavyo ingawa huonekana kuwa na malengo mazuri, lakini lengo la wanaoshinikiza uanzishwaji wake ni kujirahisishia njia ya kutufarakanisha endapo watahitaji kufanya hivyo, bila shaka kwa maslahi yao.

Kabla ya mwaka 1990, ilikuwa karibu sawa na uhaini kuzungumzia suala la vyama vingi nchini Tanzania. Ilihitaji ujasiri kulizungumza hata chumbani mkiwa wawili. Uhuru wa ghafla wa kuzungumzia suala hilo hadharani ulitoka wapi?

Mjadala kuhusu kuwa au kutokuwa na vyama vingi ulianzishwa na marehemu Mwalimu Nyerere mwaka 1990 na haikuwa rahisi kwa mtu mwingine kuanzisha mjadala huo. Kwa kauli yake, akianzisha mjadala huo alisema: “Kwa sasa sio dhambi kuzungumzia suala la vyama vingi vya siasa nchini Tanzania.” Kwa kauli hiyo tujiulize; kwa nini ilikuwa dhambi kabla ya mwaka huo, na isiwe dhambi baada ya hapo?”

Baada ya majadiliano kuhusu ama kuwa au kutokuwa na mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania, asilimia themanini (80%) walikataa mfumo huo. Hata hivyo, kinyume na matarajio ya mwanademokrasia yeyote, tulifuata mfumo wa siasa ya vyama vingi vya siasa. Kwa nini?

Mfumo huo uliingia kwa wakati mmoja barani Afrika miaka ya 1990. Iliwezekanaje uzuri wake uonekane kwa Waafrika wote kwa wakati mmoja?

Maswali yote haya yana jibu moja tu lililo wazi. Afrika ililazimishwa kufuata mfumo huo. Mjadala uliofanyika nchini Tanzania kuhusu ama kuwa au kutokuwa na vyama vingi haukuwa na maana yoyote isipokuwa tu labda kuwaandaa wananchi kisaikolojia kupokea mfumo mpya ambao hawakuuzoea.

Ndugu msomaji; ni muhimu kuzingatia kuwa sio lengo la mwandishi wa makala hii kujadili uzuri au ubaya wa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Lengo hapa ni kuwafanya wasomaji wajadili madhumuni ya walioshinikiza kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, na kama kweli tuliamua kuingia mfumo huo kwa hiari yetu.

Vurugu zinazoitwa nguvu ya umma ziliwaondoa madarakani maraisi wa Tunisia na Misri na zinaendelea kutikisa serikali nyingine kama vile Syria naYemen. Ingawa kipropaganda vurugu hizo huitwa nguvu ya umma, lakini ni jambo lisiloingia akilini, umma wote kwa pamoja kumchoka ghafla kiongozi wao aliyekaa madarakani zaidi ya miaka 30 bila hata kumpa nafasi ya kukabidhi serikali kwa njia ya amani. Hilo haliwezekani isipokuwa tu kwa msukumo kutoka nje.

Hatari ya kubadili serikali kwa njia ya mapinduzi, yawe ya kijeshi au ya kile kiitwacho nguvu ya umma, ni kutokuwa na hakika ya mustakali wa nchi baada ya mapinduzi. Wale wanaoshika madaraka baada ya mapinduzi mara kwa mara hutokea kuwa wabaya kuliko hata wale walioondolewa. Katika hali hiyo, wanaoshinikiza mabadiliko ya serikali kwa njia ya mapinduzi ni wale ambao ama hawajui athari za mapinduzi au ni wale wanaotarajia kufaidika na serikali itakayoshika madaraka kwa hali yoyote itakavyokuwa.

Historia inatuonyesha kuwa mataifa makubwa hayajali sana kinachotokea katika nchi yoyote ndogo isipokuwa tu kama kinaathiri maslahi yao. Huko nyuma, mataifa haya haya yanayoshinikiza kile wanachoita nguvu ya umma kuondoa serikali madarakani, ndiyo yaliyokuwa yakifadhili na hata kushiriki mapinduzi ya kijeshi yaliyokuwa yakifanyika katika nchi za Afrika na kwingineko.

Lengo lao ni kuondoa viongozi wasiowataka na kuweka vibaraka wao kwa kutumia njia yoyote wanayoona inafaa. Muhimu kwao sio namna ya kuwaondoa bali urahisi na uhakika wa kuwaondoa. Kwa nyakati hizi, mapinduzi ya kijeshi yameonekana kutokidhi haja hiyo, ndio maana wameamua kutumia kile wanachoita mapinduzi ya umma kwa kuchochea fujo.

Nguvu ya umma ni maneno tu ya kipropaganda yanayotumiwa kuhalalisha uingiliaji kati wa wakoloni mamboleo katika masuala ya nchi nyingine. Matumizi ya propaganda ni ya kutoka enzi na enzi.  Propaganda zilitumika hata katika kukomesha utumwa pale ulipoanza kuwa kikwazo cha kukua kwa uchumi na maendeleo ya viwanda huko Ulaya wakati wa mapinduzi ya viwanda.

Ubinadamu uliwekwa mbele kama hoja ya kuonyesha ubaya wa utumwa. Dunia iliaminishwa kuwa utumwa unapigwa vita kwa sababu za kibinadamu. Dini pia zilitumika kukemea na kuupiga vita utumwa, ingawa kabla ya hapo hata asasi za kidini zilikuwa zikimiliki watumwa.  

Wakati dini zilipokuwa zikitumika kupiga vita utumwa, zilikuwa zikitumika pia kuandaa mazingira mazuri kwa ujio na ustawi wa ukoloni. Ukoloni ulikuja kwa visingizio vya kupiga vita utumwa, kuhubiri dini, kuwaendeleza na kuwastaarabisha Waafrika n.k.

Ilipofika wakati wa ukoloni mkongwe nao kukosa tija kwa wakoloni, wakoloni hao waliamua kuachana nao na kuanzisha ukoloni mambo leo. Kama kawaida, propaganda na hadaa zilitumika, na bado zinatumika, kutufanya tuamini kuwa tuko huru. Hadi leo wengi tunajiona tuko huru kwa sababu tu tunapeperusha bendera zetu, na viongozi wetu wanatoka miongoni mwetu.

Wazungu walileta utumwa Afrika walipotaka, na kuukomesha walipotaka. Waliingiza ukoloni mkongwe walipotaka na kuuondoa walipotaka. Baada ya uhuru wa bendera wanatutawala kwa njia mbalimbali kwa jinsi wanavyotaka huku wakituaminisha kuwa kufanya hivyo ni kujali maslahi yetu.

Baada ya uhuru, mataifa makubwa na hasa ya Ulaya yamekuwa yakitumia njia mbali mbali za ukoloni mambo leo ili kuhakikishwa kuwa zinaendelea kufaidika na rasilimali za Afrika na za mataifa mengine madogo kama zilivyokuwa zikifaidika na hata zaidi. Njia mojawapo ambayo wamekuwa wakiitumia ni kuhakikisha kuwa nchi hizi za dunia ya tatu zinaongozwa na vibaraka wao.

Mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi uliokuwa ukitokea katika nchi za Afrika baada ya nchi hizo kupata uhuru wa bendera na mauaji ya viongozi, kwa kiasi kikubwa yalikuwa matokeo ya harakati za mataifa makubwa kuhakikisha kuwa Afrika inaongozwa na vibaraka wao.

Wakati nchi za Afrika zinapata uhuru wa bendera, kulikuwa na kambi mbili mahasimu zilizokuwa na nguvu duniani. Kambi ya magharibi inayofuata siasa za kipepari ikiongozwa na Marekani na kambi ya mashariki inayofuata siasa za kijamaa na kikomonisti ikiongozwa na Urusi (USSR). Hapa kuna swali la kujiuliza: Ikiwa kila nchi hufuata siasa na itikadi yake inayoona inafaa, kwa nini tofauti ya mitazamo ya kisiasa na kiitikadi isababishe uhasama?

Jibu ni kwamba, mataifa makubwa yaliyokuwa na itikadi tofauti za kisiasa yalikuwa na migongano ya kimaslahi kutoka mataifa madogo. Kila upande ulikuwa ukijitahidi kuingiza itikadi yake katika nchi ndogo kama mkakati wa kupata maslahi zaidi kutoka nchi hizo.

Kikubwa kilichokuwa kikishindaniwa, sio itikadi bali maslahi. Itikadi ilipigwa vita na upande wowote kwa sababu tu ilihatarisha, au kudhaniwa kuhatarisha maslahi ya upande huo, na iliungwa mkono kwa sababu tu ilirahisisha upatikanaji wa maslahi ya upande huo.

Ni dhahiri kuwa mivutano hiyo kati ya mataifa makubwa iliyafanya yapate maslahi yao kwa kutumia juhudi kubwa bila hata kuwa na uhakika wa kuyapata kuliko ambavyo ingekuwa kama mivutano hiyo isingekuwapo.  Katika hali hiyo NATO iliundwa ili kuondoa migongano miongoni mwa nchi za magharibi zenye itikadi moja na kuunganisha nguvu ili kujijengea uwezo wa kupambana na adui yao wa pamoja yaani nchi za mashariki na hasa USSR.

Hata baada ya kusambaratika kambi ya mashariki, ni dhahiri kuwa bado mataifa makubwa ya pande zote yana maslahi kwa Afrika na kwa nchi nyingine za dunia ya tatu wanayotaka kuyalinda. Ili kulinda vizuri maslahi yao, mataifa hayo bila kujali itikadi zao hujitahidi kadiri yawezavyo kuzuia migongano ya wenyewe kwa wenyewe. Kwa sasa NATO ina jukumu la kuwavuta hata maadui zake wa zamani na kujenga maelewano nao ili kuepuka vikwazo, na kurahisisha upatikanaji wa maslahi kuliko ilivyokuwa wakati wa vita baridi.

Ili kulinda maslahi yao, mataifa makubwa hujitahidi pia kuhakikisha kuwa mataifa madogo hayawezi kujisimamia na kujilinda kimaslahi dhidi yao. Yeyote anayeonyesha ishara ya kujisimamia na kujilinda kimaslahi au kwa namna yoyote kuwa, au kudhaniwa kuwa kikwazo kwa upatikanaji wa maslahi ya mataifa makubwa, lazima apigwe vita kwa njia yoyote iwezekanayo. Vita hiyo inaweza kuwa ya silaha au  ya maneno, yaani propaganda.

Jemadari mmoja aliwahi kuielezea vita kuwa ni utaalamu wa kuhadaa. Harakati nyingi katika kupigana vita ni kumhadaa adui. Ukiwa mbali unamfanya aone kuwa uko karibu, na ukiwa karibu aone kuwa uko mbali. Ukiwa unajiandaa kwa vita, unamfanya aamini kuwa hutaki wala kutarajia vita, na ukiwa hutaki vita unamfanya aamini kuwa umejiandaa kikamilifu kwa vita.

Kwa mujibu wa maelezo ya jemadari huyo, propaganda sio mbinu ya mapambano tu, bali pia uwanja kamili wa mapambano. Ili kuihadaa dunia, mataifa haya na hasa Marekani yamekuwa yakitumia sana propaganda na visingizio mbalimbali vya kupindua serikali za nchi ndogo, au kubadili mitazamo yao ya kisiasa na kiitikadi kutegemea maslahi ya mataifa hayo makubwa.

Visingizio hivyo ni kama vile kulinda demokrasia, kutetea haki za binadamu na kupambana na ugaidi. Ili kuhalalisha visingizio hivyo, mataifa haya huamua kuvibuni na kuvitetea kwa pamoja ili vikubalike na hatimaye kutumika kama sababu za kujiingiza katika nchi wanazotaka. Hata hivyo, la muhimu kwa mataifa hayo ni kukubaliana wao kwa wao ili kuepuka mivutano miongoni mwao.
Ingawa mataifa haya huishawishi dunia kukubaliana nao katika harakati zao, hufanya hivyo kama namna tu ya kurahisisha mapambano na kamwe sio kuomba ridhaa. Iwe kwa ridhaa au bila ridhaa, kwa amani au kwa vita; kwa haki au kwa dhuluma, lazima watekeleze wanalotaka. Mmarekani aliipiga Iraq bila ridhaa ya Umoja wa Mataifa, na kwa sasa NATO inaishambulia Libya ingawa ilipewa jukumu la kuzuia tu ndege za nchi hiyo zisiruke, ingawa hata hilo sio halali.

Visingizio vyao havitofautiani na vya hadithi moja ya mbwa mwitu aliyetaka kumla mwanakondoo. Kwa kuwa mwanakondoo ni chakula cha mbwa mwitu, ilikuwa lazima aliwe, lakini mbwa mwitu aliamua kutafuta visingizio mbali mbali vya kumla, huenda kwa lengo la kuwapumbaza wanyama wengine ambao pia ni chakula cha mbwa mwitu wanaoweza kuliwa wakati wowote.

Mbwa mwitu alianza kwa kumsingizia mwanakondoo kuwa anamchafulia maji ya kunywa, hivyo anastahili adhabu. Hata hivyo, kama suala lingekuwa maji kuchafuliwa, mbwa mwitu ndiye aliyekuwa katika nafasi ya kumchafulia mwanakondoo kwa sababu yeye (mbwa mwitu) ndiye aliyekuwa upande wa juu wa mto maji yanapotoka na kutiririkia chini alipokuwa mwanakondoo.

Mwanakondoo alipombainishia mbwa mwitu hilo, mbwa mwitu akatoa kisingizio kingine cha kuvunjiwa heshima na mwanakondoo kwa mwanakondoo kumtangulia mbwa mwitu kunywa maji. Mwanakondoo alipodhihirisha kuwa yeye hanywi maji wala chochote isipokuwa kunyonya maziwa ya mama yake, mbwa mwitu akasingizia kuwa mwanakondoo huyo aliwahi kumtukana. Hata hivyo, ikabainika kuwa wakati mbwa mwitu anaodai kutukanwa, mwanakondoo alikuwa hajazaliwa.

Visingizio vilipokwisha, mbwa mwitu akahalalisha tu kitendo cha kumla mwanakondoo eti kwa sababu aliyemtukana anafanana sana na mwanakondoo huyo kiasi ambacho yeye hawezi kuwatofautisha. Isitoshe, kama aliyemtukana sio yeye, basi ni ndugu yake hivyo tabia zao zinafanana ikiwa ni pamoja na tabia ya kutukana. Hatimaya mbwa mwitu akamla mwanakondoo ambaye hata hivyo ilikuwa lazima aliwe.

Sadam Hussein, aliyekuwa raisi wa Iraq, alikuwa rafiki wa Marekani utawala wake ulipokuwa na maslahi kwa Wamarekani. Utawala huo ulipokuwa kikwazo kwa maslahi ya Marekani, ikawa lazima aondolewe kwenye utawala, awe na hatia asiwe na hatia.

Kwanza alisingiziwa kumiliki silaha za niuklia. Cha kushangaza ni kwamba, dunia nzima ilionekana kukubaliana na suala la kuandamwa kwa mtuhumiwa wa kumiliki silaha hizo, lakini kutosema lolote kuhusu wale ambao ni dhahiri kabisa kuwa wanazimiliki. Cha kushangaza zaidi ni kwamba mmiliki mkubwa kuliko wote wa silaha hizo ambaye dunia nzima inamfahamu, ndiye aliyekuwa msitari wa mbele kabisa kumwandama mtuhumiwa.

Ilipodhihirika kuwa Sadam Hussein hakuwa na silaha hizo, akasingiziwa kumiliki silaha za maangamizi na za biolojia. Wanaozimiliki wapo na wanajulikana lakini licha ya kutoandamwa, hata kulaumiwa hawalaumiwi na yeyote. Bila aibu, wamiliki wa silaha hizo anazotuhumiwa mwingine kuzimiliki, ndio walijipa kazi ya kumwandama mtuhumiwa.

Ilipodhihirika pia kuwa mtuhumiwa hana kilichoitwa hatia ya kumiliki silaha hizo, ikabuniwa sababu nyingine ya kuwa ni mshirika wa Al-qaeda, mtandao wa magaidi. Hilo nalo lilipodhihirika kuwa sio kweli, akaitwa dikteta anayenyanyasa raia wake, hivyo lazima aondolewe madarakani.

Hata baada ya utawala wake kuangushwa, aliendelea kutafutwa hadi alipopatikana. Kitendo cha kumkamata kilishangiliwa kama vile ndio lililokuwa lengo la vita vya kuishambulia Iraq. Chama alichokuwa akiongoza kilipigwa marufuku, bila shaka katika jitihada za kuficha kila linaloweza kuonekana jema kwa jamii alilowahi kutenda.

Kuna sababu gani ya kupiga marufuku chama kwa sababu tu aliyewahi kuwa kiongozi wake alikuwa mbaya au dikteta? Je, wanachama wote huwa wabaya kwa sababu tu kiongozi wao ni mbaya? Kupiga marufuku chama cha siasa kwa sababu ya aliyewahi kuwa kiongozi wake ni kitendo kisichokubalika kwa mstaarabu yeyote licha ya mwanademokrasia na hasa anayedai kuwa mlinzi wa demokarasia kama Mmarekani.

Pamoja na hayo yote, dunia haikuthubutu japo kuilaumu Marekani ambayo iliishambulia Iraq bila idhini ya Umoja wa Mataifa. Mataifa madogo yaliogopa na makubwa yaliheshimu ushirikiano wao, au angalao kuvumilia ili kuepuka mivutano miongoni wao.

Mabutu naye alikuwa rafiki mkubwa wa nchi za magharibi alipokuwa na maslahi kwao. Maslahi yalipokwisha ndipo akaitwa dikteta na mwizi wa mali za umma ingawa mali hizo walimhifadhia kwa miaka mingi aliyokuwa madarakani. Mataifa makubwa na hasa ya magharibi yana tabia ya kuwashawishi viongozi wa nchi ndogo kuwa mafisadi ili kujijengea mazingira mazuri ya kuwatumia. Wanapowahitaji, huwatumia kupora mali za nchi zao, lakini ikifika wakati hawawahitaji tena huwageuka na kuwaita mafisadi ili iwe sababu nzuri ya kuwaondoa.

Viongozi wa Tunisia, Misri na mataifa mengine ya Kiarabu, wameitwa madikteta na wezi wa mali za umma, hivyo kustahili kuondolewa madarakani kwa kile kinachoitwa nguvu ya umma kinachochochewa na mataifa hayo makubwa ya magharibi. Viongozi hao wametawala kwa miaka mingi, na kwa muda wote huo walikuwa wakihifadhi mali wanazodaiwa kuiba katika nchi hizo hizo zinazowaita mafisadi. Kwa wakati wote huo, tawala za viongozi hao zilikuwa na maslahi kwa mataifa hayo yanayowaita mafisadi kwa sasa.

Maslahi hayo yalipokwisha, ndipo wakaitwa wezi na madikteta. Je, wizi na udikteta huo umebainika sasa? Ni dhahiri kuwa udikteta ni kisingizio tu cha kuwaondoa na kisingizio hicho kisingetosha, kingetafutwa kingine mradi tu waondolewe madarakani.

Joseph Stalin, aliyewahi kuongoza taifa kubwa laUrusi aliwahi kunukuliwa akiwaambia Warusi kama ifuatavyo: “Urusi imekuwa na historia ya kupigwa. Ni wengi waliowahi kuipiga Urusi wakati fulani katika historia. Urusi imekuwa ikipigwa na wengi kwa miaka mingi.Yote hayo yamefanyika kwa sababu kuipiga kulikuwa na manufaa kwa wapigaji; na wapigaji hawakupata na wala wasingepata adhabu kwa matendo yao, na hilo walilijua vizuri.”

Hata sasa wanaopigwa hupigwa kwa sababu kuwapiga kuna manufaa kwa wapigaji na wapigaji hawataadhibiwa kwa vitendo vyao hivyo. NATO inaipiga Libya kwa kisingizio cha Gaddafi kuwa dikteta, anashambulia raia wake na anang’ang’ania madaraka. Kwa NATO kutawala muda mrefu ni kung’ang’ania madaraka. Je, jukumu la NATO kwa sasa ni kuondoa madikteta duniani na waliotawala kwa muda mrefu? Je, Gaddafi ni dikteta namba moja duniani kwa sasa? Majibu ya maswali haya hayana maana kwa NATO. Mradi kumpiga Gaddafi kuna manufaa kwa wapigaji, na wapigaji hao hawawezi kuadhibiwa na yeyote, Gaddafi lazima apigwe.

Kwa NATO, waasi wenye silaha wanaopigana na serikali ya Gaddafi ndio wanaostahili kulindwa, na hakuna namna ya kuwalinda isipokuwa kupiga majeshi ya serikali ya Gaddfi, lakini raia wasio na silaha walipouwawa huko Rwanda na Burundi mwaka 1994 hawakustahili kulindwa. Cha ajabu ni kwamba waasi wa Gaddafi lazima walindwe hata kama kufanya hivyo, ni kuua raia wasio na hatia.

Mfaransa anayeongoza mapigano ya kile kinachoitwa kuwalinda raia wa Libya alikuwa na askari nchini Rwanda wakati wa mauaji. Askari hao walishuhudia kilichokuwa kikifanyika, lakini badala ya kuingilia kati, walifanya kazi ya kuhakikisha tu kuwa raia wa Ufaransa na wazungu wengine wanaondoka nchini humo salama. Walipoondoka wote, askari hao nao wakaondoka na kuacha mauaji yakiendelea.

Kuzuia mauaji Rwanda hakukuwa na manufaa kwa wafaransa na kufa kwa Wanyarwanda hakukuwa na hasara kwao, lakini kupiga serikali ya Gaddafi kuna manufaa kwao, na hawawezi kuadhibiwa popote na yeyote.

Historia inatuonyesha kuwa uhusiano wetu na Wazungu wakati wote umekuwa wenye maslahi kwao. Hawajali kama uhusiano huo una maslahi kwetu pia au hauna. La muhimu uwe na maslahi kwao. Ikiwa maslahi yao wanayapata kwa kutupiga watatupiga. Ikiwa wanayapata kwa kutuhadaa watatuhadaa.

Wanaopigwa, hawapigwi kwa sababu wana makosa makubwa zaidi bali kwa sababu ndiyo njia ya wapigaji kupata maslahi yao. Kama wana makosa, makosa yao ni sawa na kosa la tembo kuwa na pembe za thamani hivyo kustahili kuuwawa. Kosa la nguruwe na ngedere ni kuharibu mashamba, lakini nguruwe ana kosa lingine la nyama yake kuliwa na baadhi ya watu. Asiye na chochote chenye thamani wala kuathiri chochote chenye thamani hana hatia.

Kosa la tembo ni kubwa zaidi. Lazima asakwe popote alipo na kuuwawa. Kosa la nguruwe linaweza kuwa kubwa au dogo kutegemea anamkosea nani. Kwa kosa la kuharibu mashamba, adhabu yake inaweza kuwa kufukuzwa tu, au kujenga uzio kumzuia asiweze kuingia shambani. Kwa kosa la nyama yake kuliwa na binadamu, lazima asakwe popote alipo na kuuwawa. Kosa la ngedere ni dogo. Inatosha kumfukuza au kumzuia tu asifike shambani.

Wakati wa utumwa, mtu kuingizwa utumwani kulitegemea sana uwezo wake wa kufanya kazi. Wahindi wekundu huko Marekani walikuwa dhaifu na walishambuliwa na magonjwa mara kwa mara. Waafrika walikuwa na uwezo wa kufanya kazi ngumu na miili yao kutoshambuliwa sana na magonjwa. Hilo ndilo kosa lililowafanya wapelekwe utumwani.

Pamoja na sababu zote tunazoweza kutaja za baadhi ya nchi kushambuliwa na mataifa makubwa, Stalin anatukumbusha sababu mbili miongoni mwa hizo. Kwanza kupigwa kuna manufaa kwa mpigaji, na pili mpigaji hatarajii adhabu kwa kitendo chake cha kupiga. Badala ya kuwatia hatiani wanaopigwa, ni muhimu kujiuliza kama kweli wanastahili kupigwa na kama sisi tunaweza kuepuka vipigo vyao.

Swali moja kubwa la kujiuliza: Nini hatima ya mataifa makubwa kuungana na madogo kusambaratika?    


                                           Halifa Shabani
                                           0754 810541 
                                          HUYU NI SHABIKI WA BLOGU HII
                                            by conges













 

No comments:

Post a Comment