Friday, June 17, 2011

'NO SEX STRIKE' NI HATARI

     



SITAKI kujiingiza katika upande wowote wa sakata la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(Utawala Bora)Sofia Simba,kudaiwa kuwataka wanawake wa Chama cha Mapinduzi(CCM),kuwashushua waume wao walioko upinzani,kwa kuwanyima unyumba!

Sofia Mnyambi Simba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi(UWT)Taifa,siyo mtu wa kwanza duniani kuhamasisha kampeni kali ya kuwanyima akina baba unyumba!

 Kampeni hiyo kali, “No Sex Campaign” ya akina mama dhidi ya akina baba walio katika ndoa,imepata kutumiwa mara nyingi,ili kufanya mashinikizo.

Huu ni mgomo tata ambao,wanawake wote(wakiwemo wasichana) wakiutekeleza kwa kauli kauli moja,hakuna wa kuuzima hata kwa kutumia virungu vya polisi  hata wa General Service Unit(GSU) huko Kenya na FFU hapa nyumbani.

  Ni aina ya migomo inayodaiwa salama(Nonviolence resistance) sawa sawa na ule wa Mahtama Gandhi,wa kugomea chakula huko India zama za kudai uhuru mikononi mwa wakiloni wa Kiingereza.

Hata hivyo, mgomo na maandamano ya kunyimana haki za ndoa,siyo salama kama watu wanavyodhani.

 Migomo ya kunyimana haki za ndoa haijawai kuleta suluhu katika vita na matatizo duniani, haijawai kuleta amani ya kweli. Migomo sampuli hii, haitanzui matatizo ya kijamii; bali huanzisha matatizo mapya na yaliyojisokota zaidi.

 Sipendi kabisa kuamini kuwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Utawala Bora,Sofia Simba eti amewahi wakati wowote na mahali popote kuwahamasisha akina mama wa Chama tawala(CCM)kuwanyima unyumba wanaume wao walioko kambi ya upinzani.

 Sipendi na sitaki kabisa,kukubali kwamba Sofia Simba na Chama chake cha Mapinduzi(CCM)wanaweza kutumia ‘silaha’hiyo ya “Sex Strike” kuwashinikiza waume wao walioko kambi ya upinzani,wasalimu amri na kukubali kuipigia kura CCM,Oktoba 31.

Siamini,kwamba Sofia Simba anaweza kutumia “bunduki kali’ namna hii ya wanawake wa CCM kuwanyima unyumba waume wao wa ndoa,kitu ambacho ni haki yao ya ndoa. Haki za msingi!!

Tendo la ndoa,.ni haki ya msingi ya wanandoa,kulingana na katiba ya nchi na sheria za nchi yetu.

 Kadhalika, ni haki ya msingi katka sheria za Mungu.Tazama Biblia takatifu katika kitabu cha 1Wakoritho 7:3-6.

 Vitabu vitakatifu vya dini, vinapiga marufuku wanandoa kunyimana unyumba, ama kufanyiana mgomo wowote hata kama ni mushinikiza waume wao waache vita na misimamo ya hatari.

 Isipokuwa, imeandikwa kama wote waume na wanawake, “wakikubaliana”. Yaani, kama watapatana-tena kwa maombi makali,ili Shetani asije akawajaribu.

 Ni kwa sababi hii tu, Biblia inasema, mke hana amri juu ya mwili wake(viungo vyake vya uzazi) isipokuwa mumewe, na mume hana amri juu ya mwili wake isipokuwa mkewe.

Kwa Bwana mkubwa,Mungu, “No Sex Campaign” IMEPIGWA MARUFUKU.

Vitabu vitakatifu vimepiga marufuku migomo sampuli hiyo yenye kuwatenganisha wanandoa japo kwa usiku mmoja. Sembuse kuanzia sasa hadi baada ya Oktoba 31?

 Amani gani, baba kukosa haki ya ndoa mwezi huu hadi Oktoba 31?

 Demokrasia na uhuru upi, baba kunyimwa unyumba na mkewe wa ndoa. Kisa…uanachama wa CUF,TLP,NCCR-Mageuzi,DP sijui CCJ n.k?

Huu,ndiyo mwanzo wa akina baba kuhamia kambi ya fisi kusaka ubembelezi wa vyangudoa!

 Hatimaye, ni kusomba Virusi vya Ukimwi(VVU) na kujileta majumbani pindi uchaguzi mkuu ukipita Oktoba na mgomo wa “No Sex” ukimalizika salama bila salama.

Nataka kusema kwamba, migomo kama hii ya kunyimana unyumba wenzi wa ndoa siyo salama na haiku katika Haki za Binadamu zilizohasisiwa Desemba 10, mwaka 1948.

 “Sex Strike” huzua migogoro,fujo na vita kali vyumbani hasa nyakati za usiku.

 Kunapopambazuka, ndoa hua zimesambaratika, na ni mwanzo wa mwisho wa taifa kuyumba na kufa, kwa sababu familia nyingi huwa zimevunjika.

Ni mwanzo wa watoto kuishi maisha hatarishi bila malezi,bila wazazi walioungana katika ndoa.

Ni mwanzo wa watoto wanaoishi maisha hatarishi zaidi mitaani,ni janga lisilosemeka, kwa sababu pia akina mama wengi watapatwa majanga.

  Sipendi mimi kuamini umbeya wa watu kwamba Sofia Simba, Waziri wa serikali na Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake wa CCM, anaweza kuhamasisha “Vita kali” miongoni mwa wanaume na wanawake kunyimana unyumba,hadi ndoa nyingi zivunjike vipande, na akina baba wenye misuli wawavunje bure wake zao wazuri mataya,kwa sababu ya kutekeleza mgomo wa kunyimana unyumba!

Mwezi juni mwaka jana,vikundi10 vya wanawake wa Kenya katika mashirika ya hiari,maarufu kama G-10 vilitangaza mgomo kama huo wa kuwanyima akina baba unyumba.

Gender 10,walitangaza mgomo huo wa ‘No Sex’ kwa akina baba katika ndoa zao,kama mgogoro wa kisiasa Kenya ungeendelea kati ya Rais Emilio Mwai Kibaki na Waziri Mkuu, Raila Odinga.

Mgogoro huo,ulizuka baada ya uchaguzi mkuu wa Desemba 2007, watu1.400 wakafa vitani,mali zikaharibiwa,akina mama wakabakwa, na watu 650,000 wakakosa makazi, wengine wakakimbilia uhamishoni.

Kufuatia hali hiyo, akina mama wa Kenya(G-10) wakatangaza mgomo mkali wa ‘No Sex’ kwa akina baba, hadi watakapoacha ubabe wao na kusitisha mapigano.

Nakwambia,mgomo huo uliungwa mkono na mke wa Rais,Lucy Kibaki na Yule wa Waziri Mkuu,mama Ida Odinga.

 Sijaelewa sakata hilo la ‘No Sex’ nchini Kenya liliishaje na kama hakuna watu walioumizana vyumbani.

Sijafahamu kwa yakini, kama ile serikali ya Joint Operations Command(JOC) ya Rais Kibaki na Waziri Mkuu,Raila Odinga kama ilikuja kufuatia shinikizo la ‘No Sex Campaign’ kwa kutumia mgomo huo,, Sex Strike.

 Wanawake wote na wasichana kuwanyima wanaume tendo la ndoa(mpaka kieleweke) uliwahi kutangazwa zamani,katika karne ya 5BC na mwanamke wa Kigiriki.

Lysistrasta, aliwahamasisha akina mama wa Uyunani(Ugiriki ya wakati huo) kuwanyima waume wao unyumba hadi watakapokubali kusalim amri na kukaa pamoja katika meza ili kuacha vita-cease fire. Ilikuwa katika karne ya 5 BC, Mwanamke huyo, Lysistrasta, akahamasisha wanawake wa Ugiriki,naam Uyunani ya zama hizo, waache vita ili kuleta amani katika nchi.

 Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31 hapa Tanzania siyo vita na vurugu kama zilizotokea Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa Desemba 2007.

 Na siyo kama vita baina ya Wayunani katika miaka ya 450 BC. Uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 watu wanatakiwa kupiga kura bila kushinikizwa na mtu ama kikundi cha wanaume na wanawake.

 Mtu anaposhinikizwa kukichagua chama ama mgombea Fulani kwa kampeni kama ,’No Sex’ siyo demokrasia, na ni mwanzo wa mwisho wa kukosekana kaya na familia.

Watu wakianza kunyimana unyumba katika ndoa ndiyo mwanzo wa kuuana vyumbani.

 Kama wadhani mchezo, wewe tangaza kwamba sasa Baba Rhobi na Mama Rhobi sasa wataanza kunyimana unyumba,ili wote wampigie kura mgombea wa chama kimoja!

Andaeni hospitali nyingi za kuokoa majeruhi katika hii vita mpya ya kimya vyumba vya kulala!

 Kwa sababu hiyo, “No Sex Campaign” Ni mgomo wa kimya kimya vyumbani,lakini madhara yake yatafika nje ya mipaka ya nchi; ni hatari na ni baa na balaa!

 Mwandishi wa safu hii anapatkana kwa barua pepe

:congesdaima@yahoo.COM
  0754 324074

No comments:

Post a Comment