Wednesday, June 8, 2011

MUAMMAR AL-QADDAFI ANAHUJUMIWA NA NATO KWA VISASI


     

UKITAZAMA, uzalishaji na matumizi ya rasilimali hususan nishati duniani(World Energy Consumption and Production Trends) kuanzia miaka ya 70, utamaizi hatari kubwa inayoziangukia nchi za Afrika zenye utajiri mkubwa sana wa rasilimali.
  Madini, mafuta, nishati, mazao ya misitu n.k vinazidi kutindika, wakati viwanda vya matajiri wa Ulaya na Marekani vinapozidi sana kuhitaji malighafi, tena kutaka kuweka akiba ya siku za usoni.
  Uchumi wa dunia unapoanguka, na uchafuzi wa mazingira ya anga, vyanzo vya maji na nchi kavu unapozidi kuathiri sana shughuli za uchumi wa watu masikini kama Waafrika, kunatakiwa mapambano ya kujiondoa katika kitisho.
  Afrika, iliyokuwa imelala usingizi wa pono, watu wake wameanza kuamka japo wana tongotongo.Wanaanza kuwapinga wageni wanaokuja kusomba kila rasilimali kwa kutumia mlango wazi wa uwekezaji.
 Kiongozi wa Libya, Kanali Muammar al-Qaddafi, na Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila wamewahi kuzipinga hila(Conspiracy Theories) za mataifa haya bepari, kutaka kutuangamiza kwa maradhi yatokanayo na sumu za kutengeneza kibaiolojia, ili tufe wao wabaki wakijitwalia rasilimali zetu kirahisi tu.
  Mataifa tajiri yalishaanza kutumia kila njama, pamoja na kutumia jeshi na silaha ili kuwaua watu kwa malengo ya kujichotea rasilimali(za chee) kwa ajili ya mahitaji yao ya sasa na kuweka akiba siku za baadaye.
 Katika Afrika, kuna vita vya watu masikini kutokana na kuanza kung’amua njama za wizi za makampuni makubwa ya Ulaya na Marekani.Makampuni yanahonga serikali zetu na kuingia mikataba ya ulaghai, wanatumia jeshi la ulinzi ama polisi kushiriki kuwanyonya raia, kuwakandamiza wakati rasilimali zinapohamishwa machoni pao.
  Niger Delta, ni jimbo tajiri lenye uoto mkubwa wa asili. 
Kuna miti mizuri iotayo majini, ni eneo lenye shughuli za uvuvi, kilimo na mafuta yanayobubujika chini ya ardhi.
  Niger Delta, jimbo lililoko Nigeria , ni mahali watu wake wangeweza kujipatia mahitaji na chakula chao pasipo shida.
 Hata hivyo, makampuni ya kigeni yanachimba mafuta huko na kuharibu sana mazingira.
Mabaki ya mafuta yanayochimbwa yanaua samaki na ustawi wa mazao ya chakula umeharibiwa kwa kemikali.
   Mazingira yanachafuliwa kwa kiwango kikubwa, watu wanaugua maradhi ya ngozi, hata maji salama ya kunywa hayapo.
Ardhi yenye rutuba imeharibiwa, na hakuna kulipwa fidia inayolingana na hiyo hasara.
Uhusiano kati ya makampuni ya mafuta Niger Delta na wananchi wazalendo ni hasi.
Kwa hiyo, kuna makabiliano na mapambano ya kudai mrahaba wa haki.
  Wananchi wanapinga makampuni hayo kuharibu mazingira yao ,wakati hawanufaiki kwa huo uchimbaji wa mafuta, hawana shule, hawana hospitali, vituo vya afya hata hayo mafuta yanayochumbwa hupatikana kwa bei za kupaa.
  Kwa sababu wananchi wameazimu kupambana na wawekezaji hao raiki wa serikali, kwamba liwalo na liwe, basi jeshi limeamua kuyalinda makampuni hayo kwa kudhibiti nguvu za umma.
 Kwa lugha ya Kiingereza, mbinu hizi za kutumia jeshi huitwa, ‘Militarization” ili kuyapa nafasi makampuni ya kigeni kuendelea kuchuma rasilimali ya mafuta, hata kama mazao ya wakulima yanaungua, na hata kama samaki wanapokula mabaki ya mafuta hayo hufa au kuangamia kwa mamilioni na kukwamisha kilimo na uvuvi ama kukosekana kwa chakula.
 Ni kwa sababu hii, mwaka 1995 serikali ya Jenerali Sani Abacha ilimuuua Ken Saro-Wiwa na wanaharakati wenzake wanane, kwa sababu walitaka kukomeshwa kwa biashara hiyo hatari.
 Jen. Sani Abacha, akishirikiana na kampuni kubwa linaloongoza uchimbaji wa mafuta mahali hapo, liitwalo Royal Dutch/Shell,walianza kukabiliana na upinzani uliotoka kwa wanaharakati wa kabila la Waogoni chini ya chama chao kilichoitwa, The Movement for the Survival of the Ogoni People(MOSOP).
  Saro-Wiwa na wenzake waliuliwa kwa kupigwa risasi za kichwa mchana kweupe Novemba 10 mwaka huo wa 1995 licha ya jumuia za kimataifa kupinga sana hukumu dhidi yao iliyotolewa na mahakama za kijeshi, wakati wao walikuwa raia.
  Saro- Wiwa, aliyapinga makampuni ya kikoloni kuwaacha wazalendo wenyeji wakiugua upele na kuishi katika mazingira yaliyonajisiwa,wakati shughuli zao za uchumi zikiwa haziendelei.
Labda, msomaji ataniuliza:
Ni kwa sababu gani Nigeria , chini ya Abacha serikali ilishirikiana na makampuni ya mafuta kuwaua wananchi wake, kwa sababu walipinga uharibifu mkubwa wa mazingira uliofanywa na makampuni ya kigeni?
  Kwanza, kampuni kubwa kama Shell liliwapa wanajeshi wa Abacha mishahara na posho ili kutekeleza operesheni hiyo kali dhidi ya waandamanaji wapinzani-fedha.
  Pili, kampuni la Chevron, liliajiri na kusafirisha polisi ambao waliwapiga risasi na kuwaua raia walioandamana, kwa helkopta yao mwaka 1998 na 99-ajira.
 Mkuki kwa nguruwe-siku hizi maandamano ya raia yanatumiwa na Marekani,Uingereza na Ufaransa kuanguzha serikali za Hosni Mubarak,Misri, Ben Ali wa Tunisia na Kanali Gaddafi huko Libya, kisha Yemen na Syria.
  Makampuni haya ya uchimbaji mafuta na rasilimali nyingine kama gesi, madini, vito n.k yakifika mahali huanza kuwatumikisha raia kama watumwa, pasipo ujira kwa ruhusa ya serikali, kwa sababu yanalipa kodi, tozo anuwai na mrabaha-royalty.
  Katika nchi kama Burma (siku hizi ni Myanmar) kampuni la kuchimba gesi la Unocal kwa kushirikiana na jeshi la nchi hiyo, walipojenga bomba la kusafirisha nishati hiyo lenye urefu wa kilomita 62 huko Yadana, waliua raia,walibaka akina mama,waliwatesa wananchi,wakawatumikisha pasipo malipo utadhani watumwa, mwaka 1994.
 Makampuni ya wageni yanapofika Afrika kuchimba mafuta au madini na rasilimali nyingine, yana tabia ya kuendesha sana ukoloni na kuwageuza wananchi watumwa kwa sababu tu makampuni hayo yanasaidia serikali na kuzirejesha madarakani-rushwa na hongo.
  Kampuni hilo  la Unocal la Kimarekani lilishitakiwa huko Los Angeles, Marekani mwaka 2003 kwa kuharibu haki za Binadamu. Likakimbia kuomba kesi kuondolewa mahakamani ili walipe fidia nje ya mahakama.
 Nataka kusema kwamba, serikali zetu hugeuka vipofu, tena viziwi, wasione na kusikia mateso ya wazalendo wananchi wao, kwa sababu tu makampuni hayo ya kigeni yamewapa misaada vigogo wa serikali.
 Pengine watoto wao wanasomeshwa Ughaibuni kwa gharama za makapuni haya, na watoto wa vigogo wakati mwingine hupewa kazi zenye maslahi makubwa katika makampuni haya, kama siyo kupewa hisa.
  Makamuni haya nyakati za chaguzi za vyama vingi, yanatoa misaada ya fedha ili kuhakikisha serikali rafiki zao zinasalia madarakani milele na milele, ili nao waendelee kuchuma bila jasho.
 Naam. Kupitia uwekezaji unaoshabikiwa na viongozi wetu siku hizi, makampuni ya kigeni haya hasa kutoka Ulaya na Marekani, kwa kutumia mikataba ya hila kama ya Carl Peters na Mangungo wa Msovero, yanahakikisha wazalendo wanateswa, wazalendo wanaharakati wanauawa na kukomeshwa, ndiyo kufungwa jela au kupigwa risasi ya kichwa utadhani pusi, paka, nyau wakomba mboga!
 Kumbe, hawa ni wanaharakati waliong’amua wizi na uporaji wa rasilimali huku wageni hao wakiharibu mazingira na kusababisha mauti kwa wazalendo wasije kuamka na kudai haki zao..
Raia wanapoamka kupinga huo unyanyasaji na wizi wa mchana, ama wanapoazimu kupinga mustakabali wa kifo (the destiny of death)dhidi yao , wanauliwa kama Ken Saro-Wiwa alivyouliwa mwaka 1995.
Lakini, penye maslahi ya wakoloni huko Bahari ya Kati, maandamano huungwa mkono kwa madege na vifaru vya Marekani na washirika wake,bila ajizi.
 Katika mikatataba ya uvunaji wa rasilimali inayofanywa siku hizi baina ya serikali na makampuni ya wageni, demokrasia(ambayo ni ushirikishwaji wa wengi katika maamuzi) hutupwa mbali na makampuni hay o hayo ambayo nchini  kwao huimbwa wimbo huo wa demokrasia na utawala wa watu.
 Serikali za watu na watu kwa njia za watu kwa ajili ya watu hugeuka kuwa za watu wachache kwa ajili ya wachache-government of the few by the few for the few.
 Matokeo yake, makampuni haya makubwa kutoka Ulaya na Marekani, yatawaangamiza watu wazalendo ili kuvuna rasilimali zao bila upinzani kwa njia mbalimbali kama vile kusambaza virusi vya mafua makali ya nguruwe(swine flu), ukimwi na njama tele za maangamizi.
 Ni kwa sababu hii, serikali za nchi zetu zinaposhirikiana na makampuni haya kuwaua raia na kufumbia macho uvunjaji wa haki za binadamu, ni sawa kwamba, sisi sangara, tunajikaanga wenyewe kwa mafuta yetu wenyewe.
 0786-324 074


No comments:

Post a Comment