Wednesday, May 4, 2011

Nyoka yupi wa CCM aliyejivua magamba?


    
FALSAFA ya Chama cha MapinduziI(CCM)kufanya matengenezo(reform) kwa mfano wa nyoka anayejivua magamba, imetupa Watanzania agenda na tafakuri tunduizi.
Nyoka, ametumiwa mahali pengi(hata katika Biblia) kama mifano ya Shetani, au mashetani na wafuasi wao. Nyoka hutumika kama alama ya kuwatambulisha Freemason.
Biblia hiyo hiyo, inamtumia nyoka kama aishara ya Ukombozi wa Waisraeli wa kale,kutoka Utumwani Misri walikokuwa kwa miaka 400,kwenda nchi ya Ahadi, Kaanani, ambayo leo ni Palestina.
Awali, katika kitabu cha Mwanzo 3:1-5 Biblia imesema nyoka alikuwa mnyama mwerevu(mjanja na laghai) kuliko wanyama wote aliowaumba Bwana Mungu.
 Nyoka huyu, wa kitabu cha Mwanzo, alishirikiana na Ibilisi au shetani kuwalaghai Adamu na Hawa kumwasi Bwana Mungu na kusababisha maangamizi,ufisadi na dhiki, majanga ya asili na mabaya yote yameletwa na uasi wa Adamu na Hawa na ulaghai wa Shetani.
Tena, katika kitabu cha KUTOKA 4:1-4 NA KADHALIKA Kutoka 7:9-12,Nyoka alitumiwa na Musa na Haruni kama ishara ya Mamlaka ya ukombozi kutoka kwa Mungu dhidi ya Mtawala wa Misri, Farao.
Nataka kusema kwamba, nyoka siyo tu ni alama ya kumtambulisha Shetani na malaika zake,majini na mizimu,na Freemasons.
Nyoka, ni sihara ya ukombozi kutoka utumwa kama huo wa Misri zama zile za Nabii Musa na Waisraeli wenzake huko Misri.
 Pia, nyoka ni alama ya ukombozi kutoka utumwa wa dhambi; ni alama ya tiba na ondoleo la maradhi ya kufisha kama sumu.
 Biblia, katika kitabu cha HESABU 21:5-9, hutufundisha falsafa ya NYOKA WA SHABA, aliyeinuliwa Jangwani, aliyewaokoa wana wa Israeli wasife kwa sumu kali ya nyoka wakali wenye sumu,pindi Waisraeli walipokuwa safarini kutoka Misri, wakadharau Ulinzi wa Mungu.
 Kila nyoka hujivua magamba.Konokono anapojivua magamba, hufa. Lakini,nyoka anapojivua magamba, huwa kijana zaidi mwenye kasi zaidi.
 Yohana, katika kitabu cha Injili ya Yohana Mtakatifu 3:14,15 hutufundisha kwamba,Yule NYOKA WA SHABA kule Jangwani,zama za ukombozi wa Nabii Musa, alimwakilisha Bwana Yesu Kristo.
 Nyoka,siyo ishara ya Shetani tu, pia ni ishara ya ondoleo la dhambi na mauti. Hata hivyo,kila nyoka hujivua magamba. Kuna nyoka wenye sumu na wasio na sumu;na wote hujivua magamba!
 Kwa sababu hiyo, tunapata fursa ya kujisaili: Nyoka wa CCM aliyejivua magamba, ni Yule aliyewadanganya Adamu na Hawa, sasa karejea kwa sura ya Chama cha Siasa,ili kuja kuwadanganya watu waangamie?
Au, huyu ni nyoka anayesemwa kujivua magamba ni Yule wa SHABAaliyeinuliwa Jangwani ili kuwakomboa watu wenye kukaribia kukata roho kwa sumu za maisha magumu,kukata tama na mauti yanayowakabili?
Labda,huyu nyoka wa CCM aliyejivua gamba ni Yule ambaye Bwana Mungu aliwaamuru Musa na Haruni wamtupe mbele ya kasri la Farao wa Misri?
 Basi, Farao naye akawaita wachawi wa Misri,wakatengeneza nyoka bandia lakini wadogo wadogo, wakamezwa na Yule nyoka wa Musa na Haruni!
Hakika, huyu nyoka wa Musa na Haruni,hakuwa nyoka halisi. Ilikuwa fimbo ambayo ni alama ya utawala,”Sceptre” ama alama ya Mamlaka ya ufalme wa Mungu, ambao hauna mipaka katika jambo lolote.
 Je, nyoka wa CCM,aliyejivua gamba,ndiye huyo ambaye ni fimbo yenye mamlaka ya ufalme, “a rod symbolizes Royal Power” ndiyo inayojigeuza sasa ama kujivua gamba ili kujiondoa katika hali yake ya uzee?
 Tujadili kidogo falsafa ya nyoka kujivua magamba.
Mungu wa dawa wa Kigiriki, AESCULSPIUS, ama kwa Kilatini, Asclepius, huwa anaonekana ameshika fimbo,halafu nyoka anaonekana akiwa amejizinga kwenye fimbo hiyo. Naam, hapa pia kuna Fimbo ya nyoka.
Bila shaka, msomaji umepata kuona alama ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa(WHO) kuna nyoka aliyejizinga kwenye fimbo, ama kijiti. Ni huyu, Asclepius-mungu wa dawa na uponyaji wa Kigiriki na Kirumi.
Alama hii,pia inaonekana kwenye noti ya shilingi 500/= hapa kwetu,na watu wengine husema hizi noti zina alama ya Freemasons!
Je, CCM wanapojivua magamba, ni nyoka Aesculapius ama Asclepius? Ni Freemasons? Ni nyoka wa Bustanini Edeni?
Hata hivyo, nyoka ni alama ya UPYA unaoleta UJANA. Kwa Sababu hiyo, nyoka ana uwezo wake wa kujivua magamba. Nyoka hutoa ngozi yake ya kale, analeta ngozi mpya.
 Wajitta wa Musoma vijijini,mkoani Mara wanaita, “Okwinyubhula”! Nyoka aliyejizinga katika kijiti,ni ishara ya uponyaji kutoka katika miungu ya dawa-aesculapius, aliyesadikiwa alikuwa na uwezo wa kuponya. Tazama kitabu kiitwacho, Compton’s A Britannica Publications Vol.1 ukurasa 87.
Hii miungu ya Kigiriki,ilisadikiwa kuishi katika kilele cha Mlima Olympus. Ilisemekana kwamba miungu hiyo 391 iliishi kama jamii moja kileleni mwa Mlima Olympus,pamoja na viumbe waliokufa(wanga na mizimu) na baadhi ya hiyo miungu ni Zeus, Titan, Poseidon(mungu wa maji), Hades au Pluto ambaye ni mungu wa wafu, Hestia, Hera,mungu wa vita-orodha ni ndefu.
Sina shaka,ulipata kusikia kwamba, Mwanafalsafa wa kale sana Ugiriki, Socrates au Sokrati, aliwafundisha wanafunzi wake, Aristotle, Plato na wenzake,kwamba kulikuwa na Mungu mmoja tu,naye aliishi mbinguni,wakampa sumu anywe ili afe.
Kwa sababu hiyo, Chama cha Mapinduzi hawakubahatisha kujifananisha na nyoka anayefanya, “Okwiyubula” yaani kujivua magamba.
 Tumeona Falsafa ya Kigiriki na Kirumi kwamba nyoka ni alama ya upya; ni ishara ya ujana. Kwa kuwa Katibu Mkuu Mpya wa CCM,Willson Mkama ni Mjitta awaeleze Watanzania, CCM imeji ‘nyubhula’ ili iwe mpya,ili kung’ata kwa sumu ya kuangamiza au kuponya?
CCM kujivua magamba mithili ya nyoka,ni kujifanya upya yaani CCM Mpya yenye ari zaidi,nguvu zaidi na kasi zaidi katika kuangamiza,au kuponya Watanzania sumu zilizomo miilini na akilini?
 Baadhi ya wasomaji wangu, wamenipigia simu kuniuliza: Je, CCM wanapojivua magamba mithili ya nyoka hutapika pia sumu?
 Na ndiyo kurejesha upya na ujana wao tayari kuleta madhara kwa kasi zaidi,ari zaidi na nguvu zaidi, au kuleta uponyaji na tiba na ondoleo la utumwa kwa ari,nguvu na kasi zaidi?
Niseme kwamba, falsafa ya CCM kujivua magamba ni kurejesha upya na ujana, sawa. Sijui kama CCM ni wale nyoka wa sumu kali waliowashambulia Waisraeli,Jangwani wakati wa safari yao ya kutoka Utumwani,Misri?
Labda, CCM ni Yule nyoka wa shaba ambaye alikuwa alama ya ukombozi kimwili na kiroho pia? CCM ni alama ya ukamilifu wa kimwili,kiroho na kiakili na hali bora kijamii?
 Sijafahamu,kama CCM ni nyoka waliojivua magamba kama ishara ya uponyaji mithili ya Aesculapius ama Asclepius, anayetumiwa na Freemnasons, WHO na mashirika ya madawa na uponyaji duniani.
Sijafahamu kama kikombe cha Babu wa Loliondo,kina alama gani ya uponyaji? Sitambui,kama nyoka wa CCM aliyejivua gamba ana sumu au hana.
Wapo nyoka wengi hawana sumu,chatu hana sumu lakini humeza watu!
Nikijuacho ni kwamba, nyoka akitumiwa vibaya ni alama ya laana na kifo. Nyoka aliyewadanganya Adamu na Hawa ni hatari.
 Alama ya nyoka ikitumiwa vizuri ni ishara ya ukombozi na tiba kwa matatizo sugu na kukata tama.
Labda, sasa CCM watwambie wenyewe, wao ni nyoka yupi aliyejivua gamba?
Nyoka mdanganyifu aliyeleta mauti na sumu kwa Watanzania, au nyoka wa Shaba, alama ya ukombozi wa kiroho na kimwili?
 0786-324 074

No comments:

Post a Comment