Wednesday, May 4, 2011

Obama kamuua Osama, au geresha na janja ya Marekani?

                       
WAMAREKANI wanashangilia sana,Rais Barack Obama kafanikiwa kumuua Osama bin Laden.
Marekani sasa wameushinda Ulimwengu.
Mwanzoni, Osama alikuwa ‘rafiki’ yao na mshirika wao katika vita vya kuyapinga majeshi ya Urusi nchini Afghanistan.
Marekani, sasa wamewaua adui zao karibu wote katika vita vinavyoitwa vya ugaidi-WAR AGAINST TERRORISM- na wanakaribia kuwatia mbaroni wote wanaowapinga,walioko katika ‘Mhimili wa Uovu’ Duniani.
Saddam Hussein,mtawala wa nchi iliyo na mito miwili ya Tigris na Euphrates, nchi ya Irak, alinyongwa kwa kamba nene shingoni, katika jingo la Camp Justice, Alfajiri ya Jumamosi,Desemba 30 mwaka 2006,mjini Baghdad.
Awali, walitangulia kuwaua wanaye,Udday na Qussay,kwa mvua ya mabomu iliyomwagwa na madege ya kivita, na vikosi maalum kama Delta Force.
 Naam. Tunaweza kusema, ‘Mto Frati ulikauka’ hiyo Desemba 2006, pale sanamu ya Saddamu Hussein ilipoangushwa mjini Baghdad,kabla ya yeye kunyongwa.
 Sura ya Pili ya kitabu cha Danieli katika Biblia Takatifu,hutuambia kwamba Babeli ambayo sasa ni Irak ilikuwa nchi ya sanamu kubwa za madini yenye thamani kubwa,zilizoabudiwa.
Sanamu ya Saddam ilibomolewa na kushushwa mahali pake,kuonesha enzi ya Babeli ama Irak ya Saddam ilishakoma mwaka 2003, ili kutoa nafasi na njia kwa mataifa ya Mashariki yaliyowapinga Marekani na washirika wake wa NATO,kuvuka mto na kuungana na Ulaya Magharibi.
Mto mkubwa, Frati, ‘ulikaushwa’ kabisa mwaka 2006, wakati Dola kuu duniani, Marekani ilipojizatiti kuitawala dunia baada ya dola ya Urusi ya Kisovieti(USSR) kusambaratika mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Marekani sasa ni ‘baba’ wa Ulimwengu, na anayewapinga anaishia kukamatwa na kufungwa jela ama kuuawa kwa mabomu makali,kama siyo kutiwa kitanzi.
Mabaki ya Ukomunisti yangalipo,ndiyo Uislam wenye msimamo mkali; na ndiyo akina Kanali Muammar al-Gaddafi wa Libya, Hugo Chavez wa Venezuela,  Mugabe wa Zimbabwe, Fidel Alejandro Castro Ruz na nduguye Raul Castro Ruz wa Cuba na wenzao.
Siku zao zinahesabika,kwa sababu tayari mtoto wa Gaddafi,Saif al-Arab ameualiwa pamoja na wanaye watatu mjini Tripoli.
Mauti yanamkaribia Gaddafi,kama siyo kifungo jela,kasha kunyongwa kwa kamba hadi kufa kama Marehemu Saddam.
Basi, ulimwengu wa Kikomunisti umekoma,na Gaddafi anakaribia ukingoni,kwa kuwa madege ya vikosi vya majeshi ya Umoja wa Kujihami Ulaya Magharibi,NATO, wanamvizia kama walivyomwotea Osama bin Laden na kumlipua usiku wa kuamkia Mei Pili,jirani na Islamabad, Pakistan.
Osama bin Laden(54) ameuawa na vikosi maalum vya Marekani,vikishirikiana na majasusi wa Central Intelligence Agency(CIA). Ilikuwa siku chache tu, baada ya mtoto wa Gaddafi, Saif al- Arab kuuawa pamoja na wanaye watatu.
Naam.Kupitia kituo cha televisheni cha sky news,nimeuona uso unaodaiwa wa Osama bin Laden,ukiwa umefumuliwa,macho yamefumbwa,hana kilemba cheupe tena,madevu yamesawajika!
Hakika, alikuwa amekufa, na mtu Yule alifanana sana na Osama-Amekufa. Naam, Osama bin Laden amekufa,ingwa wengine bado wanasema ni Propaganda za Marekani tu,Osama yungali hai!
Rais  wa Marekani, Barack Obama, amaeutangazia ulimwengu kwamba, Osama ameuawa na mwili wake ulikuwa chini ya ulinzi wa vikosi maalum vya Marekani.
 Kichwa chake kiliwekewa dhamana ya dola za Marekani milioni 50; na inawezekana Wapakistan wamemsaliti kwa majeshi ya Marekani au majasusi wa CIA.
Vita vya Marekani dhidi ya Ugaidi, viko ukingoni; na upinzani wa kweli dhidi ya Marekani na washirika wake unakoma, kwa hiyo nchi za Mashariki mwa Mto Frati, zinakwenda kuungana na Magharibi yaani NATO na soko la pamoja Common Market, matarijio ni nchi nyingi duniani kama siyo zote kuanza kutumia pesa moja iitwayo Euro,ambayo ina picha ya Askofu Mkuu wa Rumi,Baba Mtakatifu au Papa.
Osama bin Muhammad bin Awad bin Laden, alikuwa mshirika wa zamani wa Marekani wakati wakiyapiga majeshi ya Urusi(USSR) ya Kisovieti,yalipoivamia Afghanistan.
 Alizaliwa mwaka 1957,na alikuwa mtoto wa 17 kati ya watoto 50 wa Muhammad bin Laden,kibarua wa Yemen aliyekwenda Saudi Arabia akawa tajiri mno kupitia miradi ya ukandarasi.
 Huyu, babaye Osama alikufa kwa ajali ya ndege mwaka 1968, Osama akarithi kitita cha dola za Marekani kati ya milioni 50 hadi 300 hivi.
Ilikuwa Desemba, 1979 Osama alipoungana na Mujahedin wa Afghanistan kuipinga Urusi kuivamia Afghanistan.
Wakati ule wa VITA BARIDI,Marekani walipigana bega kwa began a Osama dhidi ya majeshi ya Muungano wa Kisovieti wa Urusi(USSR).
Shirika la Ujasusi la Marekani(CIA) lilimfadhili Osama mabilioni ya dola ili kuwashirikisha Waafaghan kuwapinga Warusi kuingia kijeshi mjini Kabul na kufanya uvamizi.
Osama, akawa na fedha,akaanzisha kambi ya mafunzo ya Mukhtab al-Khidemat(MAK), AKAFUNDISHA maelfu ya vijana kutoka nchi dazeni kupigana vita dhidi ya uvamizi wa Kirusi huko Afghanistan.
Fedha, alipewa na Marekani. Hivyo kambi ya MAK ndiyo chimbuko hasa la al-Qaeda miaka ile ya 1980.Osama alirejea Saudi Arabia baada ya majeshi ya Urusi kuondoka Afghanistan mwaka 1989.
Msomaji,unajua sababu za Osama kukosana na Marekani na kuanza kumpinga Mfalme wa Saudi Arabia?
Saudi Arabia,iliungana na majeshi ya washirika wa Marekani katika Vita vya Ghuba ya Uajemi,dhidi ya Irak,mwanzoni mwa miaka ile ya 1990.
 Yaani,Mfalme wa Saudi Arabia aliungana na Marekani kupigana vita dhidi ya Marehemu Saddam Hussein,katika vita vya kwanza vya Ghuba, Irak ilioishambulia Kuwait,wakati wa George Herbert   Walker Bush(Bush Baba)wakati ule akipigana na Saddam.
Osama ali ‘waasi’ Marekani wakati wa vita vya kwanza vya Ghuba,vilivyopiganwa kwa sababu ya mafuta. Chimbuko la uasi wa Osama dhidi ya Marekani ni maslahi ya mafuta ya Waarabu wa Irak,dhidi ya vibaraka wa Marekani wa Kuwait-zote hizi ni nchi zinazozalisha sana mafuta,naam Mafuta!
Vita vya kwanza vya Ghuba vilipokwisha,Bin Laden alitimkia Sudan.
Nataka nikwambie msomaji,Sudan ni nchi kimbilio la magaidi ambao wakati mwingine tuwatazame kama wanaharakati!
Namkumbuka Ilich Ramirez Sanchez, maarufu kama Carlos The Jackal wa Venezuela, aliyehitimu Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba,mjini Moscow, akapinga sera za Marekani za kibabe juu ya Palestina inayopambana siku nyingi na Israeli.
Carlos The Jackal alikimbilia Sudan kujificha, akajakukamatwa na majasusi wa Kifaransa mjini Khartoum,wakampeleka Paris alikofungwa kifungo cha maisha.
Carlos, alipinga ubeberu wa Kimarekani na Uzayuni wa Israeli kwa njia za kigaidi kwa kutumia vikundi kama Balack Septemba, kilichowateka nyara Wanamichezo wa Israeli wakati wa    michezo ya Olimpiki,mjini Munich,mwaka 1972.
Naam, Osama naye alikimbilia mafichoni Sudan kama Carlos The Jackal
.Akaanza Operesheni za kigaidi dhidi ya maslahi ya Marekani,kama mwaka 1993 aliposhambulia jirani na jengo la WTC, mjini New York na kuua watu 18.
Nataka kusema kwamba, Osama alisaidiwa na Marekani dhidi ya Urusi,mafunzo ya kijeshi. Akaja kuwageuka kama Saddam Hussein alivyowageuka wakati ule akishirikiana nao kupigana vita dhidi ya Iran, zama za Ayatollah Khomeini.
 Unakumbuka, Ayatollah Khomeini, alitoka Paris Ufaransa,uhamishoni, akampindua Shah kibaraka wa Marekani huko Iran, zama za uporaji wa mafuta. Tumeeleza jambo hili katika makala zetu zilizotangulia.
Osama, alinyang’anywa Hati ya kusafiria ya Sudan na Saudi Arabia mwaka 1994,akatimkia Afghanistan alikoanza kushirikiana na Taliban waliouteka mji wa Kabul,Septemba mwaka 1996.
 Osama, aliwapa pesa Taliban kwa sababu kiongozi wa Taliban,Mullah Muhammad Omar alikuwa swahiba wake.
Wakaanzisha mafunzo kwa wanamgambo,wakapigana dhidi ya India huko Kashmir.
Agosti mwaka 1998 Bin Laden akatangaza ‘Jihad’ dhidi ya Marekani huko Peninsula ya Arabia,tumesema huko Marekani ilikwenda kutafuta mafuta inayosaka sana.Kila kwenye mafuta mengi,kuna majeshi ya Marekani karibu.
Marekani wakaanza kumsaka Osama huko Afaghanistan,wakapindua serikali ya Wataliban na Mullah Muhammad Omar akakimbia kujificha mvua ya madege ya NATO na washirika wao.
‘Fatwa’ dhidi ya Marekani ilitolewa na akina Osama Feburuari 23 mwaka 1998. Mashambulizi dhidi ya Balozi za Marekani mjini Dar es salaam na Nairobi yakafanywa Agosti 7 mwaka 1998 yakasababisha zaidi ya watu 200 kufa.
Aidha,yamefanywa mashambulizi mengi dhidi ya maslahi ya Marekani duniani,na vikundi vya kigaidi vya al-Qaeda na al Shabab,hasa shambulizi la Septemba 11 mwaka 2001 lililoua watu zaidi ya 5,000 huko New York na Washington na Pennsylvania
 Hata mwaka jana waliuawa watu mjini Kampala wakati wakitazama Kombe la dunia kwenye televisheni.
Nataka kusema kwamba,Osama na Saddam Hussein walikuwa ‘washirika’ wa Marekani,maslahi yakafika ukingoni,wakageuka maadui wakubwa.
 Osama aliwasaidia Marekani kupambana na majeshi ya Urusi mjini Kabul mwaka 1979,wakati Saddam alipewa jukumu la kupambana na Iran zama za Marehemu Ayatollah Khomeini,mfuasi wa itikadi kali na Ukomunisti.
Sasa, Osama na Saddam, washirika wa zamani wa Marekani waliogeuka adui, wamekufa katika mkono wa Marekani.
 Je, ugaidi umekwisha?
 Barack Obama kawatangazia Marekani kwamba vita vimefika ukingoni, mabaki ya ugaidi na ukomunisti yatamudu kupingana na Marekani?
 Akina Saif al-Arabu wamekufa mjini Tripoli, Gaddafi anawindwa, siku na saa yoyote anawafuata akina Saif,kama Saddam alivyowafuata Qussay na Udday!
 Ni shangilizi Marekani. Huenda sasa joto la Obama kupingwa kwamba siyo raia wa Marekani litapoa na huenda akapewa mhula wa pili wa utawala hapo Novemba mwaka kesho,2012.
Rais Obama, anapingwa na wabaguzi wa rangi wa Republican kwamba hakuzaliwa na Hussein Obama na mama yake Ann Dunham Stanley huko Hawaii. Kwamba, eti alizaliwa Kenya na siyo  Mmarekani!
Sasa,kifo cha Osama Mei Pili mwaka huu wa 2011,usiku wa kuamkia Jumatatu huko Pakistan kitamwokoa Obama asizame 2012?
 Osama atamwokoa Obama? Ni mwisho wa vita vya ugaidi na mwanzo wa Marekani kuwakamata watu wanaoipinga na mipango yake ya uporaji wa rasilimali za dunia na hata za sayari nyingine kama Mars na Mwezi?
Ni mwanzo wa Marekani kulazimisha watu wa Dunia nzima kutumia euro yenye sura ya Papa? Ama, ni mwanzo wa amani ya kudumu duniani,kwa kuwa magaidi kama Osama hawapo tena?
Ni vita vikali vilivyodumu kwa muongo mmoja na kuwajeruhi na kuwaua watu wengi duniani kote-vita vya maslahi ya Marekani dhidi ya maslahi ya waarabu,mabaki ya ukomunisti.
 Hata Bush alishatangaza kwamba Osama alikwishauawa na Majeshi ya Marekani huko Tora Bora, sasa ni Osama gani aliyeuliwa Pakistan?
    0786/0754-324 074


No comments:

Post a Comment