Wednesday, June 12, 2013

MADIKTETA NDIYO VIPENZI VYA MAREKANI-2

WAZIRI Mkuu wa Ethiopia,Meles Zenawi, alikufa Ughaibuni mwaka jana,akaisababishia majonzi makubwa Marekani,kuliko Afrika!
Mwaka 2011 na 2012, Afrika iliondokewa na viongozi wake:Nigeria,Zambia,Malawi na hata Kanali Muammar al-Qaddafi,aliuliwa na Waasi waliojiita Baraza la Mpito,Libya waliosaidiwa na Marekani.
Kati ya Julai na Agosti,mwaka jana,Zenawi na Rais wa Ghana,John Atta-Mills waliaga Dunia.
Wamarekani wakaangua kilio kikubwa kwa Zenawi kuliko Atta Mills! Inasemwa Ghana inaongoza kwa upevu wa demokrasia Kusini mwa Jangwa la Sahara; na inasemwa,Ethiopia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kubinya demokrasia na uhuru wa watu kusema.
Vyombo vya habari Uhabeshi vimewekwa rumande,na sauti ya umma haisikiki; la sivyo waandishi wa habari watakabiliana na mkobo wa chuma na magari ya deraya ya kijeshi.
Wamarekani wakamwombolezea sana Zenawi;wakasema:
“Alileta maendeleo makubwa ya uchumi Ethiopia”, wakabwabwaja!Zenawi alikufa katika umri wa miaka 57,alitumiwa na Magharibi kama chambo cha kuondoa utawala wa adui yao,Kanali Mengistu Haile Mariam.
Huyu Meles, aliongoza Waasi wa Tirgrayan People’s Liberation Front ili kumpindua Mengistu mwaka 1991 akatimkia  “ZIM CONTRY” kwa Robert Gabriel Mgabe.
Magharibi wanamsifu sana Meles kwamba alifanya ndege ya uchumi kupaa kwa asilimia 10 kwa miaka mine mfululizo.
Hata hivyo, hizi ni takwimu za makaratasi,uhalisia wa mambo huko Addis Ababa, umasikini umeshamiri miongoni mwa raia wa kawaida,licha ya mabarabara na hospitali kujengwa katika kipindi cha Meles Zenawi.
Alitawala Ethiopia kwa mkono wa chuma;vyama vya siasa vilitiwa kabala,watu 200 walipojidai kuandamana na kuunga mkono Upinzani,wakafyekwa kwa risasi!
Chama chake,Ethiopia People’s Revolutionary Democratic Front(EPRDF)mwaka 2010 kilishinda viti vyote vya Bunge dogo,kasoro viwili. Kilipata viti 547.
Laiti CUF,NCCR ama CHADEMA wangekuwa Ethiopia zama za jamaa huyu, halafu wakajidai kuandamana na kumpinga,polisi ama jeshi wangefyatua risasi na kuua waandamanaji maelfu,Marekani ikiwa kimya!
Naam, Ethiopia ni miongoni mwa nchi zenye jeshi kubwa sana hapa Afrika;na hutumia asilimia kubwa sana ya Bajeti yake ya nchi katika shughuli za jeshimkuliko elimu,afya na huduma za jamii.
Ethiopia, Meles alishinda uchaguzi kwa asilimia 99 za kura zote,wapinzani wakiwa kimya mithili ya maji mtungini!
Sijui kwanini Marekani,Uingereza na Ufaransa hawakumkemea kwa ‘uhuni’ sampuli hiyo,badala yake wakawa wanambeba kwenye mbeleko na kumfanya ‘msemaji’ wa Afrika!
Ulinzi ulikuwa mkali kuwakata ngebe wapinzani wa serikali yake katili. Huyu na Isaias Afwewerk wa Eritrea(watu wao hutoroka nchi kila siku kukimbilia Ughaibuni),lakini alikuwa mboni ya jicho la Marekani.
Kama kuna nchi iliyogawanyika sana kwa misingi ya kikabila,kimajimbo,kikanda,kidini na kimikoa ndiyo hii Uhabeshi.
Hata hivyo,Masheikh,Maaskofu,Maimam,Manabii na Mitume kama hawa wa kwetu Tanzania,waliziba midomo zama za Meles,wasije wakachukuliwa ndani ya ‘Buti’za gari za Usalama na kupotezwa.
Umewahi kusikia zama za Amin kwamba kulikuwa na The State Research Bureau? Kwamba waliwahi kuwapoteza maaskofu ambao siku hizi wana midomo mipana hapa kwetu, kuikosoa serikali na kuhamasisha migomo na maandamano?
Meles, alikuwa mbabe, na wapinzani wake walikuwa wakikabiliana na mauti ya bunduki kama ile ya Yoweri Kaguta Museveni(Seven Battalion), inayoitwa ‘Lwitabagomyi” ama kiboko ya wanaojidai kugomea amri ya mamlaka!!
Meles, alitoka kikundi cha Tigray, akawakata kauli makundi makubwa ya nchi hiyo, Oromo na Amhara.
Alitumika vilivyo kutuliza ghasiaUpembe wa Afrika(The horn of Africa).Majeshi yake yaliingia Somalia mwaka 2006, ili kuwakata ngbe Waislam wenye msimamo mkali,al-Shabaab.
 Ni Meles huyu aliyetumika kuhakikisha Sudan ya Kusini inajitenga na Khartoum  ya Omar Hassan al-Bashir ambaye anatakiwa na Mahakama ya mjini Hague kwa makosa ya mauaji,husuan Darfur.
Mahakama hii ambayo Umoja wa Afrika umeishutumu kwa kuitazama Afrika kama ‘target’ huku ikiwaacha wauaji wengine wa Ulaya na MAREKANI,wahalifu wa kivita huko Irak,Libya n.k
Wenye mahakama hii iliyoundwa na Wakoloni,waliposikia kwamba Afrika imeanza kuipinga,wakaona wamwondoe Louis Moreno-Ocampo wa Buenos Aires,wakamweka Fantou Bensouda wa Gambia,ili kuwafanya Waafrika mbumbumbu waone Waafrika wanajaliwa!
The Hague,ni mahakama ya kikoloni na yenye malengo ya kibaguzi na makengeza, ‘double standards’ ndiyo maana Kenya wameamua akina Uhuru Kenyatta,Rutto na Arap Sam washitakiwe mjini Nairobi, ama imependekezwa hata Tanzania!
Kwani Afrika hakuna mahakama hadi Ulaya? Acheni ujinga!
Wazungu wanasema,wakati Afrika ina ombwe(vacuum) la viongozi wenye mvuto, “Charismatic leadership”,Meles alikuwa kiongozi mwenye mvuto mkubwa,akachaguliwa kuwa ‘Msemaji’ wa Afrika kila jambo!
Alialikwa mikutano takriban yote ya G 8,G 20 na akatoa kauli katika mikutano hiyo ambayo madikteta wengine wa Afrika,akina Mugabe,Gaddafi,Obiang Nguema Mbasongo na wenzao hawakusogea.
Alitazamwa mshirika  mkuu wa Dola za Magharibi katika medani ya amani duniani. Hata madege yasiyo na rubani ya Wamarekani-Drones- yalitumia Uwanja wa ndege wowote Ethiopia,kufanya Operesheni zao.
Sijui unaelewa msomaji? Yaani,kama mtu angejidai kukiuka matakwa ya maslahi ya Marekani huko Upembe wa Afrika na Kusini,yangetumwa madege hayo, akamwagiwa mvua ya risasi na kusambaratishwa kutokea Ethiopia.
Haya madege yaliipeleleza Afrika ili kujua kama kuna wanaharakati wanaoitwa Magaidi.
Magharibi walimpenda Meles kiasi kwamba hawakuona makosa,aliwapa kila walichotaka,akaitwa KIONGOZI WA KIZAZI KIPYA wa Afrika na Bill Clinton mwaka 1998.
Walimwombea adumu uongozini hata miaka 100!! SIJUI unaelewa nini kuhusu Marekani kumwombea mtu kudumu miaka 100 katika zama hizi za demokrasia?
Sasa utaona ni kwanini Marekani inaomboleza baada ya mauti kumpokonya Meles Zenawi katika umri mdogo wa miaka 57.Mwaka 2012 alipotembelea Washington akazungumza angeachia madaraka 2015, akafikiria kufundisha katika shule yake ya Uongozi.
Wapinzani walimwita katili katika masikio kiziwi ya Marekani na washirika wake wanaotetea demokrasia duniani kwa mauaji ya akina Saddam na Gaddafi huku wakifunga watu jela Abu-Ghraib na Guantanamo Bay,wakivamia nchi kama Syria na kusambaratisha utu na amani.
Wazungu walisema,Meles aliimarisha miundo minu na kuwapa maisha bora masikini wa Uhabesbi!
Ethiopia ina watu milioni 90;nchi ya pili kuwa na watu wengi Kusini mwa jangwa la Sahara.
Mwezi mmoja baada ya Meles kuaga dunia Rais Atta-Mills wa Ghana akaaga dunia.
Hata hivyo wazungu walimlilia Meles kuliko kiongozi wan chi ya Demokrasia kama Ghana,John Atta Mills
Itaendelea
congesdaima@yahoo.com
0786 324 074/0754 324 074
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment