Monday, June 17, 2013

namlilia mandela

NAANDAA makala haya ikiwa ni mwezi mmoja kamili,kabla ya Mwanahalisi wa Afrika,Nelson Mandela kuadhimisha miaka 95 kamili tangu azaliwe.
Mandela, sasa huugua-ugua na kulazwa Hospitalini kwa maradhi ya mapafu.
Binafsi,nimepoteza matumaini ya mtu huyu nimpendaye sana kuishi,japo afikishe miaka 100 kamili ifikapo Julai 18,mwaka 2018.
Nelson Rolihlahla ‘Madiba’ Mandela, alizaliwa Julai 18 mwaka 1918 katika kijiji cha Mvezo,katika Jimbo la Eastern Cape,Afrika ya Kusini.
Alikuwa mwanaharakati mashuhuri saka katika kupinga ubaguzi wa rangi wa Chama cha African National Congress(ANC)kinachoongoza sasa Afrika ya Kusini.
Miaka 27 ya uhai wake aliitumia akiwa jela,kufuatia harakati zake za kuwapinga Makaburu wa Afrika Kusini na siasa zao za Kibaguzi zilizoungwa mkono na Mataifa makubwa ya Magharibi.
Muda mwingi akiwa jela, akawa anaponda kokoto mchana wa hari akiwa hana viatu,hususan huko Kisiwa cha Robben,ambacho sasa ni kituo cha utalii.
Watu huenda kuona chumba alicholala shujaa huyu wa karne hapa Afrika na dunia nzima.
Namba yake ya jela, ‘46664’ itakaa kama ALAMA ya harakati za Ukombozi Kusini mwa Afrika, na katika harakati za uhuru hapa Barani.
Mtu huyu, ambaye sasa anaugua na matumaini ya kuishi muda mrefu yanatindika,aliachiwa huru na Makaburu Feburuali 11 mwaka 1990, na akawasamehe waliomsweka jela kwa jumla ya miaka 27.
Ni mzaliwa wa ukoo wa Thembu,katika kijiji cha Mvezo,wilaya ya Umtata,mji mkuu wa Transkei.Anatokana na ukoo wa Chifu Ngubenguka(alifariki 1832).
Babaye, Gadla Henry Mphakanyiswa(1880-1928) aliwahi kuwa chifu wa Mvezo,akapokonywa uchifu na wakoloni wa Kiingereza.
Mzee huyo alikuwa na wake wanne,akazaa watoto 13,Mandela alikuwa mtoto wa mke wa tatu,NESEKENI FANNY,Binfi wa Nkedama wa Mpemvu,wa kabila la XHOSA.
Jina la Rolihlahla maana yake ni ‘Kuvuta Tawi la Mti’ lenye kumaanisha ni mtu mwenye fujo!
Akiwa na umri wa miaka saba alikwenda shule, mwalimu wake aliposhindwa kutamka jina la Rolihlahla, akampa jina Nelson kwa heshima ya Mkoloni Mwingereza,Horatio Nelson.
Baba yake alifariki Mandela akiwa na miaka tisa tu; ikabidi sasa alelewe na rafiki wa baba yake.Mandela alisoma shule ya misheni ya Wesleyan.
Akaingia jandoni akiwa na umri wa miaka 16,kabla ya kwenda kusoma Clarke bury Insitute,alikotunukiwa cheti.
Aliwahi kucheza ndondi na riadha.Hapa namkumbuka mwanamasumbwi Nguli,Mweusi wa Marekani aliyetukanwa udongo wa mfinyanzi kufuatia kuwa Mweusi,Mohammed Ali.(Clay).
Mandela, alisoma Shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Port Hare, alipokutana na Mpigania uhuru mwenzake,Oliver Tambo.
Tambo, alikuja kuwa kiongozi wa ANC kabla ya kufariki dunia.Mandela aliwahi kuwa karani katika kampuni sheria mjini Johannesburg; alisaidiwa kupata kazi na Walter Sisulu.
Baadaye, alisoma sheria Witwatersand, ambako alikutana na wanaharakati wengine.Mandela na Oliver Tanbo waliendesha kampuni ya uwakili ili kuwasaidia Weusi waliokuwa wakikumbana na madhila ya kunyanyaswa na Makaburu.
Desemba 5, mwaka 1956 Mandela na wenzake walitiwa mbaroni na wenzake 150 na kushitakiwa kwa makosa ya uhaini-walishinda kesi hatimaye wakaachwa huru.
Johannesburg,ndiko aliswekwa rumande baadaye,baada ya kutafutwa sana na Shirika la Ujasusi la Marekani,Central Intelligence Agency(CIA).
Nataka msomaji,hasa vijana wa siku hizi kujua kwamba Marekani na washirika wake,waliwasaidia Makaburu na wakoloni wengine kuwahujumu Weusi wasije kujitawala siku moja katika nchi zao wenyewe.
Naam,leo hung’ata na kupuliza,na wajinga wote wanaona Mataifa haya ndiyo ‘Masihi’ na mabingwa wa demokrasia na Haki za Binadamu,kumbe ujinga mtupu!
Marekani na Shirika lake la CIA ambao hupigiwa goti siku hizi,wakishirikiana na Makabuu wa Afrika ya Kusini na tawala za Kiimla(Authoritarian) wakamshitaki Mandela kwamba alichochea mgomo wa wafanyakazi na kutoroka nchini kinyume cha sheria.
Yawezekana,ni wakati huu Mandela na wanaharakati wenzake walikuwa Mazimbu,Morogoro katika Makambi ya wapigania uhuru-Tanzania.
Oktoba 25 mwaka 1962 Mandela alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.Akiwa jela, huku nyuma polisi wa Makaburu waliwasweka rumande wanaharakati wengine wa ANC, akina Walter Sisulu,Govan Mbeki na wenzao.
Juni 12 mwaka 1964 wakahukumiwa kifungo cha maisha jela.Kati kesi hiyo MANDELA pia aliunganishwa,wakapelekwa Kisiwa cha Robben mahali ambao Mandela akakaa miaka 18.
Kazi yao ilikuwa kugonga miamba na kuipasua ili kupata kokoto za kujengea jela imara sana za Makaburu ili wafungwa(WEUSI)wasitoroke.
Machi,1982 Mandela alihamishiwa Polls moor, akiwa na wenzake wa ANC akina Walter Sisulu.
Feburuari,1985 P.W.Botha, alimpa Mandela ‘Offer’ ya kuachiwa huru kwa masharti kwamba aachane na harakati za uhuru wa Mtu Mweusi.
Mandela alikataa ‘offer’ hiyo akatoa taarifa kupitia binti yake,Zindzi akisema:
“Uhuru gani ninaopewa wakati taasisi ya watu inabaki imepigwa marufuku? Hata hivyo,mfungwa hawezi kuingia mikataba!” Mandela aligoma kuachwa huru-uhuru bandia.
Wewe kijana wa sasa ulishaona wapi msimamo mkali wa Mwanahalisi wa Afrika mithili ya MANDELA?
Makaburu WALIFANYA MKUTANO NA Mandela mfungwa mwaka 1985 Novemba, katika hospitali ya Volks,Capetown alipokuwa akitibiwa saratani-alikutana na waziri wa Makaburu,Kobic Coetsee.
Mwaka 1989,PW Botha aliugua kiharusi,nafasi yake ikachukuliwa na Frederic Willem de Klerk,rais wa Kwanza Kaburu Barani Afrika, wenzake walikuwa Mawaziri wakuu, akatangaza kuwa Mandela angekuwa huru mwaka 1990.
Waafrika tukafurahi,mtu huyu kipenzi cha watu kuwa huru.Alipewa nishani ya Amani ya Nobel,yeye na De Clerk mwaka 1993.
Baadaye Makaburu walimuua Chris Hani,Aprili 1993.Mandela alikuwa rais Afrika ya Kusini akiwa na miaka 77 mwaka 1994, akaja kustaafu mwaka 1999.
Aliapishwa kuwa Rais wa kwanza Mweusi wa Afrka ya Kusini Mei 10, mwaka 1994,de Clerk akawa Makamu wa Kwanza wa rais na Thabo Mbeki akawa Makamu wa Pili katika serikali ya Umoja wa kitaifa kama ya Zanzibar hivi.
Itaendelea
www.congesmrambatoday.blogspot.com
0713 324 074

No comments:

Post a Comment