Friday, June 28, 2013

MANDELA,MFUNGWA MAARUFU DUNIANI ANAPOAGANA NA OBAMA KATIKA KITANDA CHA MAUTI





RAIS BARACK Hussein Onyango Obama, anawasili katika miji ya Dakar,Johannesburg,Pretoria na Dar es salaam, Mandela akiwa anashindana na kifo katika kitanda cha Mauti, MediClinic.
Afrika iko chini ya ulinzi wa makachero wa Marekani,Obama anapotua katika ardhi ya Afrika,wakati huu Mandela anapolala usingizi usiojulikana mustakabali wake huko Mediclinic.
Ujio wa Obama,Afrika naam,Afrika Kusini, Senegal na Tanzania kitovu cha harakati za Ukombozi wa Mtu Mweusi, wakati huu wa mashaka ya kuishi au kufariki kwa Mandela, unatupa kurejea historia.
Mzungu wa kwanza kufika Rasi ya Tumaini Jema(Cape of Good Hope),Afrika ya Kusini, Bartholomew Diaz,mwaka 1485 ilikuwa ni katika safari za kwenda India
Muongo mmoja na ushee hivi baadaye,(1497-98) alikuja Vasco Da Gama;hawa Wareno wakizunguka dunia ili kujua ilivyoumbwa-huu ulikuwa mwanzo wa Utandawazi.
Ni wakati huo, Amerigo Vespucci wa Italia alipofika Pwani ya Amerika Kusini mwaka 1497-99,Zama hizo(1492-1502) ndipo Christopher Columbus wa Italia alipofika hasa Marekani na kunakoitwa, West Indies.
Huu ndio wakati wageni kutoka Ulaya walipoanza safari za kwenda Afrika ya Kusini ambako walisimika tawala zao za kidhalimu kwa zaidi ya karne nne, hadi Mandela alipozaliwa Julai 18 mwaka 1918.
Nataka kueleza namna Wazungu walivyofika Afrika na kuanzisha tawala za kidhalimu,kasha wakachukua ndugu zetu kuwa watumwa Marekani, ambako pia walitawala kabla ya Marekani kupata uhuru Juni 4,mwaka 1776.
Mandela, ameishi kwa taabu na wapigania uhuru wenzake wakijificha-ficha wasiuliwe ama kukumbana na kifungo cha maisha jela.
Rais wa kwanza Mzungu katika Bara la Afrika, FW De Clerk ,alizaliwa Machi 18,mwaka 1936 mjini Johannesburg,wakati tayari Mandela akiwa katika madhila ya ukoloni,Afrika ya Kusini.Huyu De Clerk, ndiye aliyekuja kumwacha huru Mandela Feburuari 11,mwaka 1990.
Mandela ameachwa na mkewe kufuatia harakati za kujificha-ficha asikamatwe,hakufika nyumbani muda mrefu, na laifukuzwa Chuo Kikuu cha Port Hare kwa kosa la kujihusisha na migomo huko Transkei.
Alijisomea nyumbani akatunukiwa shahada ya kwanza,BA.Alitiwa mbaroni 1952,1956,1962 na 1964 akafungwa kifungo cha maisha gerezani.
Wakati Mandela anafungwa huko Afrika Kusini,Mtu Mweusi(Negros) hakuwa na ruhusa kuoa Mzungu katika majimbo 19 ya Marekani,na Afrika Kusini ilikuwa Mzungu akikukuta ndani ya basi umeketi,unampisha kiti!
Naam, ni wakati huu kulikuwa na Mitaa na mahoteli Mweusi huwezi kukanyaga,inaandikwa mlangoni, ‘For Whites Only’!
Marekani na Afrika ya Kusini zilifikiwa na wapelelezi(explorers) wakati mmoja,zikajikuta makoloni ya wageni,wakati Marekani inapata Uhuru mwaka 1776 kutoka Uingereza Afrika Kusini ilibaki chini ya makucha ya Waingereza, na baadaye Makaburu wabaguzi wa rangi.
Rais Barack Hussein Onyango Obama, anatua Afrika Kusini wakati Mandela roho yake inapokuwa ikishindana na malaika wa kifo huko MediClinic; akiwa anapumulia mashine.
Obama, amezaliwa Agosti 4, mwaka 1961 wakati harakati za Uhuru zikiwa zimepamba moto duniani.
Ubaguzi wa rangi ukiwa umepamba moto hata Marekani kwenyewe, ni wakati huu huu mamaye Obama,Ann alipokuja kutengana na Hussein Onyango Obama,akaolewa Indonesia akaishi Jakarta.
Nataka kusema kwamba, huyu mamaye Obama, alipata msuko-suko kuolewa na ‘Mjaluo’ wa Kenya-Afrika, akaondolewa chuoni alipopata ujauzito wa Obama, mama huyo akiwa na umri wa miaka 18!Alionja madhila ya ubaguzi wanaoshuhudia akina Eto'o siku hizi!
Hizi ndizo zama akina Martin Luther King Jr, walipowindwa mithili ya nguruwe pori, walipinga ubaguzi wa rangi kabla ya kuuliwa na Pentagon mwaka 1968.
Obama,huyu aliyeko Dar es salaam sasa, alizaliwa Honolulu huko Hawaii na mama Ann Dunham,mzaliwa wa Wichita, Kansas.
Kwa mara ya mwisho Obama alikutana na Mandela mwaka 2005 alipokuwa angali Seneta; na safari hii alitarajia kukutana na Mandela akiwa Rais wa Taifa baguzi la rangi…
Bahati mbaya,Mandela yu kimya kitanda cha mauti; kauli haitokei kumwambia Obama, “The change has Come to America! The change must come  to Africa!!”
Hussein Onyango Obama, aliachana na Ann, Barack akiwa na miaka miwili,sababu ni mbinyo na ubaguzi wa rangi,wakati huo akina Martin Luther King Jr,Malcom X na wenzao sheria ziliwapiga marufuku kumuoa Mzungu.
Naam, Obama na bintize,Malia na Sasha, ni Weusi wenye damu halisi ya Afrika,wakati huu wanapokuwa nyumbani Afrika.
Obama, kasoma Indonesia,kasha Honolulu kabla ya kusoma vyuo vikuu vya Columbia na Harvard,chini ya usaidizi wa mamaye na nyanyaye, Madelyn Dunham.
Huyu nyanya alikufa wakati Obama akifanya kampeni mwaka 2008.Ilikuwa Novemba 3,mwaka 2008.
Mkewe Obama, Michelle, ni binti wa Fraser na Mariam Robinson,mabaki ya watumwa ndugu zetu waliopelekwa Marekani kulima miwa katika mashamba ya Mzungu.
Hawa ndugu zetu-Obama na Michele-wametua Dakar,Johannesburg,Pretoria na Dar ili kukumbuka nyumbani.
Obama alikusudia kuzulu kisiwa cha Robben alikofungwa Mandela kwa miaka 18, alizaliwa Julai 18 mwaka 1918, akafungwa Robben kwa miaka 18, na De Clerk aliyemwachia huru alizaliwa Machi 18,mwaka 1936.
Mandela, amefungwa jumla ya miaka 27;zamani kisiwa cha Robben kilitengwa kwa sababu ilikuwa ni koloni la wakoma-Leper colony.
Kwa takriban miaka 30,utawala wa Makaburu uliwafunga maelfu ya Waafrika Weusi waliopinga ubaguzi wa rangi mahali hapa.
Mwaka 1987(miaka mitano baada ya Mandela kuhamishwa kutoka kisiwani hapo kwenda Bara) eneo hilo liligeuzwa Kivutio kikuu cha utalii.
Mandela alifungwa Robben miaka 18; eneo ambalo Obama huenda amefika,ili kukagua mateso ya Mtu Mweusi-Mandela na wenzake- ndiyo akina Walter Sisulu, Goven Mbeki, na viongozi wengine wa African National Congress(ANC) na Robert Sobukwe wa Pan Africanist Congress.
Wafungwa hawa,Mandela,Mbeki,Sisulu na wenzao waliponda kokoto bila viatu mchana wa hari-vumbi liliishia kifuani Mandela akaugua kifua.Asskari walinzi wa gereza waliwakojolea puani,wakati mwingine walilazimishwa kuoga maji ya baridi.
Jela ya Robben ilikuwa na vitanda 600;mahali ambapo hata baada ya mauti kumkumba ‘TATA’Mandela,itabaki kumbukumbu ya mateso ya mtu Mweusi wakati wa madhila ya ukoloni na ubaguzi wa rangi.
Waziri wa Sheria wa Makaburu, Cobie Coetsee, akahamuru akaina Mandela wahamishwe,wawachie ndege makazi.Kumbuka lilikuwa eneo la kutupwa wakoma,hakuna aliyeishi maeneo haya.
Siku hizi,kunajengwa mahoteli ya fahari na ni kituo cha utalii-a world class attraction! Obama,Michelle,Malian na Sasha, wanafurahi kukanyaga alipofungwa ‘Tata’Mandela.
Lilikuwa eneo la kuzika wakoma,katika selo nambari 30 B katika chumba kidogo cha mita 2 kwa 2 ndipo alipolala mtu huyu mwenye urefu wa mita 2.
Alijifunika shuka la kijivu na blanketila sufu rangi ya kahawia, taulo la samawati.
Gazeti la TIME la Julai 1991,LILIMKARIRI Brigedia Erika Van Zyl, Ofisa Uhusiano wa gereza hilo akiwakaribisha watalii mahali hapo na kusema mahali hapo ni ‘A world class attraction!
Zama za utawala wa Makaburu,hapa palikuwa The Worst Part of Imprisonment!
Hata hivyo, Mwandishi, Scot Mac Leod, aliandika katika gazeti hilo la TIME,Julai 22 mwaka 1991,mwaka mmoja baada ya Mandela kuachiwa huru na de Clerk,kwamba Brigedia Erika van Zyl,aliwakaribisha mahali hapo Robben, alikofungwa Mandela.
Bila shaka,hata kaburi la Mandela litageuka ‘Tourist Site’ maarufu hapa Afrika na dunia nzima.
Hakika,Mandela ameishi duniani bila raha na amani,sasa akifariki atazikwa katika kisiwa cha amani ya milele.
Kwa Obama, kitabu cha ‘Dream from my Father’ kilichoandikwa na  wakati babaye anarejea Kenya, ni kumbukumbu tosha Obama kutomsahau Mandela,Nyerere,Samora Machel,Kwame Nkrumah na wenzao, zama za harakati za Mtu Mweusi, akina Martin Luther King Jr, naam akina Malcolm X.
Obama, amekuwa rais wa taifa beberu lililounga mkono ubaguzi wa rangi akiwa na umri wa miaka 47, na sasa anapokuwa Dar atambue msingi wa Urais wake ni Mandela,Nyerere,Kwame Nkrumah,Patrice Emery Lumumba,Martin  Luther King Jr, mama Coletha King na wenzao mashujaa wa kupinga ubeberu na ubaguzi wa rangi.
“The change has come to America; and it must come to Africa too!
Buriani tata MANDELA,Mfungwa maarufu kuliko wote duniani aliyegeuka Shujaa kuliko wote duniani.
congesdaima@yahoo.com
0786 324 074/0713 324  074
 
 
 
 
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment