SERIKALI ya Misri, iko katika vita vya maneno na
Ethiopia,kufuatia Ethiopia kujenga Bwawa la kufua umeme kwenye Mto Nile.
Mto Nile, huanzia Ziwa Victoria,katika maporomoko ya
Owen,Jinja nchini Uganda,mahali ambapo pia Uganda hufua umeme unaouzwa hata
mkoani Kagera hapa Tanzania.
Kuna mito kama Kagera unaoanzia Burundi na kutiririka hata
Rwanda,kabla ya kufika Kagera na kuingia Ziwa Nyanza linaloitwa Victoria, ambako
hutiririka chini kwa chini hadi Owen Dam,Jinja unapoanzia Mto Nile.
Kuna Mto Nzoia huko Kenya;Mito miwili:Kagera na Nzoia
huchangia takriban nusu ya maji ya ziwa hili la kwanza kwa ukubwa Afrika.Ni
ziwa la Pili kuwa na maji baridi duniani,nyuma ya Ziwa Superior huko Marekani.
Ipo mito mingine mingi kama Ruvubu na Nyabarongo ambayo pia
huingia ziwa Victoria na kuchangia Mto Nile kufurika na kutiririka kutoka
Afrika Mashariki.
Mito mingine ni
Suguti,Mori,Sio,Yala,Nyando,Sondu,Miriu,Mara,Simiyu n.k ambayo humwaga maji
yake ziwa hili wakati wa msimu wa masika,na hufanya Nile kutiririka kwenda
Bahari ya Mediterranean.
Bonde la Mto Nile linajumuisha nchi za
Rwanda,Burundi,Uganda,Tanzania,Kenya,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC),Eritrea,Ethiopia,Sudan
na Misri yenyewe.
Hata hivyo, serikali ya Misri ikitambua kwamba Mto Nile
ndiyo chanzo kikuu cha Uhai wa Taifa; na kwamba Nile ni hatma ya maisha na kifo
kwa watu wao,walikimbilia kuingia mkataba na serikali ya kikoloni ya Uingereza
mwaka 1929;mkataba ambao ulipiga marufuku nchi nyingine hizo kutumia maji ya
Ziwa Victoria na Mto wenyewe kumwagilia mashamba ama kufua umeme.
Mkataba huo ulisainiwa tena mwaka 1957 kati ya Misri na
Uingereza ili kuzuia nchi za Bonde hilo la Mto Nile kumwagilia mashamba yao na
kufua umeme kwa ajili ya maendeleo ya watu.
Misri, imewahi kutishia kupigana vita vikali na Kenya,endapo
ingechukua maji ya Ziwa Victoria ama matawi ya Nile(Blue Nile na White Nile kwa
miradi ya maendeleo; kwamba kungesababisha maji yasitiririke kutoka huko Owen falls,
Jinja.
Mto Nile hutiririka kwa zaidi ya kilomita 6,900 kutoka Afrika Mashariki hadi Misri na kuingia
Bahari ya Mediterranean.
Kitendo cha Tanzania kwa mfano kuchukua maji ya Ziwa
Victoria na kuyapeleka Kahama,Shinyanga eti ingeomba ruhusa ama kibali kutoka
Misri!
Hapa ndipo shida ilipoanzia.Ethiopia imeamua kujenga Bwawa
la kufua umeme katika Mto Nile ili kujiepusha na tatizo la nishati iliyo muhimu
sana katika maendeleo ya watu hivi leo.
Ingeweza hata kumwagilia mashamba,ili kuepukana na janga la
njaa inayoikumba dunia ya Ulimwengu wa tatu.Kwa Misri, eti Ethiopia imekiuka
mikataba ya kale ya Misri na utawala wa Malkia wa Uingereza.
Hivyo, Misri imetangaza vita na Ethiopia, na kama mgogoro
huo hautamalizwa kidiplomasia, basi vita vya maji ya ziwa hili vitakuwa
vimeanza.Ethiopia inatuhumiwa na Misri kukiuka mikataba hiyo ya 1929 na
1957;mikataba inayozuia nchi zetu kutumia maji haya kwa namna yoyote mbali na
kunywa,kuoga na kuoshea mifugo tu.
Misri na Sudan,hupata maji ya Nile baada ya maji haya kuwa yamesafiri kutoka
kwetu kutokana na mvua zinazonyesha huku za masika katika miezi ya Aprili na
Mei na maji hayo hutiririka hadi Misri
na kufika Agosti na Septemba.
Mvua zinaponyesha Tanzania,Kenya,Uganda,Burundi na Congo
maji huingia ziwa hili kwa mito mingi,halafu huanza kusafiri hadi Misri. Hawa
Wamisri hufikiri kwamba tukitumia maji haya ya ziwa huku au ya Mto Nile Sudan
na Ethiopia,basi kina cha maji yam to kitapungua kwa takriban mita(cubic
meters) bilioni 50.
“Maeneo mengine Misri,watu wamefariki kwa njaa na wengine
hulazimika kula mbwa ili wasife njaa kufuatia ukame”, alisema Waziri wa Maji ya
Umwagiliaji wa Misri, Dk. Mahmoud Abu-Zeid.
Wanataka kina cha maji kiwe kikubwa kabisa hadi juu ya kingo
kama cubic metres bilioni 150 hivi, ili wawe na amani na mataifa ya Afrika ya
Mashariki.
Hivyo,kupungua kina cha maji huko Nile ni kitisho cha maisha
ya watu milioni 85 huko Misri,ambako Nile huabudiwa kama moja ya miungu tangu
zama za Nabii Musa(BC 1500).
Binti Farao wakati akienda kuabudu mto huo asubuhi ndipo
alipokiona kitoto Musa ndani ya chombo kilichotengenezwa kwa majani ya Mto
Nile.Wakati Misri inawakataza watu wa Bonde hilo kutotumia maji haya,yenyewe
inafanya midadi mikubwa ya umwagiliaji na vyanzo vya umeme.
Kuna Mradi wa Bwawa la Aswan-Aswan High Dam,ili kutengeneza
Ziwa Nasser.Misri ni jangwa,na mvua hazinyeshi jangwani.maji yake yametoka hapa
Kwetu Afrika Mashariki.
Misri huendesha mradi mkubwa wa mashamba ya umwagiliaji
katika Bonde la Toshka,ambao ni takriban ekari 600,000.Mradi huo uko katika
jangwa la Kusini,umejengwa mfereji wenye urefu wa kilomita 310 ambao utabeba
maji yenye ujazo wa cubic metres bilioni 5.5 kutoka ziwa bandia la Nasser.
Hali hii huonesha kuweko kwa miradi mikubwa sana ya kilimo
cha umwagiliaji huko Misri na miradi hiyo hutumia jumla ya cubic metre bilioni
25 za maji ambayo chanzo chake ni ziwa
Victoria.
Watu wengi Misri huishi kandoni mwa mto huu na wamekuwa
wakimwagilia mashamba tangu zama za Nabii Musa nakabla ya hapo kama miaka 3000
BC.
Hata hivyo, mataifa ya Afrika Mashariki yamegomea ‘ujanja’
huo wa Misri na wakoloni wakisema Kenya,Uganda,Tanzania n.k walipata uhuru
miaka ya 1960,hawakuwepo wakati Misri ikiingia mikataba ya kitapeli na
Uingereza-hatukushirikishwa- iweje kufungwa na mikataba ya 1929 na 57?
Ziwa Victoria liliitwa hivyo na Mwingereza wa kwanza
kuliona,John Hanning Speke,ambaye aliliita Victoria kwa heshima ya Malkia
Victoria wa Uingereza.
Zama za Ukoloni,Uingereza ilijitia kumiliki ziwa hilo hivyo
ikawauzia Misri ‘Mbuzi kwenye gunia. Ili wakamwagilie mashamba yao kwa maji ya
ziwa hili,wakati sisi tunapokufa na kuzimia kwa kiu na njaa huko Afrika
Mashariki.
Je, mikataba ya takriban karne moja iliyopita,itatuzua nchi
zetu kutumia maji ya Ziwa Nyanza ili kumwagilia mashamba na kupata nguvu za
umeme?
Uganda,hutumia maji haya kupata umeme huko Owen falls
Dam,Jinja.Rais Yoweri Kaguta Museveni amesema, “Hatutaki Misri wafe njaa,lakini
lazima sisi tukae na kuzungumza suala hili,kwani hata sisi tunahitaji chakula”.
Sasa Misri hutaka kutumia vita kutuogopesha sisi kutumia
maji hayo kwa miradi ya maendeleo ama nishati-hydroelectric projects.
Umoja wan chi za Bonde la Mto Nile-Nile Basin
Initiative(NBI)Makao makuu ya sekretariati yao yako Jinja Uganda,kandoni mwa
ziwa kubwa lenya ukubwa wa kilomita za eneo 68,000.Tanzania humiliki asilimia
51,Kenya asilimia 6 na Uganda humiliki asilimia 43 ya ziwa hili.
Maji ya ziwa hili ambayo hufika hata Misri na kuingia
Mediterranean,baada ya kukusanywa na mito ya Afrika Mashariki katika eneo la
kilomita za mraba 193,000 Rwanda,Uganda,Kenya,Tanzania na Congo.
Takriban watu milioni 35 wanaishi kandoni mwa ziwa hili
katika nchi hizi zetu,na ziwa ni chanzo cha samaki takriban tani 500,000 kwa mwaka.
Sasa,vita viko mlangoni kati ya Misri na nchi za Afrika
Mashariki,vita vya kugombea maji ya Ziwa hili.
“Ole wan chi ya uvumi na mabwawa,iliyoko mbali kupita mito
ya Kushi(Ethiopia),taifa ambalo Mito inakata nchi yao(Tanzania) ambayo bendera
imeinuliwa Mlima Kilimanjaro”, Isaya 18:1,3.
Congesmrambatoday.blogspot.com
0713 324 074/0786 324 074
No comments:
Post a Comment