Friday, July 12, 2013

DAR HATARINI KUVAMIWA

                  KUFUATIA ZIARA ZA OBAMA NA JI XINPING
Dar Es Salaam kuvamiwa!!

‘Zanzibar,’ ni neno la Kiarabu, “Zinj el-Bahir” maana yake,Nchi ya Weusi-The land of the Blacks!!
Wafanyabiasra wa Kiarabu waliuita hivyo mji huo katika karne ya 8 au ya 9 hivi AD, hadi Wareno walipofika katika eneo hili katika karne ya 15.
Wareno,wao waliita Pwani yote ya Bahari ya Hindi katika eneo hili, “Zanguebar”;Wagiriki waliita eneo hilo lote la Pwani ya Afrika ya Mashariki,AZANIA.
Dar es salaam,ulikuwa vijiji vidogo vidogo vya wavuvi katika karne ya 19.Mwaka 1860,Sultani Seyyid Majid wa Zanzibar akaazimu kuiendeleza Dar es salaam,ili iwe Bandari muhimu ya Bara,kwa ajili ya wafanyabiashara kupata kituo cha kususha na kupandisha shehena za biashara zao kutoka na kuingia Bara.
Sultani Seyyid Majid,aliliita eneo hili ‘Dar es salaam’ maana yake mahali pa salama na amani(Haven of peace).
Alipokufa Seyyid Majid, Dar ikaangukia mikononi mwa watu wasiofahamika.Mji huu ulikuja kushindwa ama kuzidiwa na Bagamoyo,ilikokuwa bandari nyingine muhimu sana kwa majahazi,upande wa Kaskazini.
Wasafiri wengi wa kutoka sehemu mbalimbali waliifanya Dar es salaam kituo chao;hata Wamishenari waliufanya mji huu kituo chao kwa ajili ya safari zao kati ya Pwani na Bara.
Utawala wa kikoloni wa Kijerumani,uligeuza mji huu kuwa Bandari ya salama zaidi kuliko Bagamoyo.
Mwaka 1891,Makao Makuu ya Utawala wa kikoloni yakahamishwa kutoka Bagamoyo hadi Dar es salaam; na kuanzia hapa mji huu ulikuwa Makao Makuu ya serikali hadi mwaka 1973 yalipohamishiwa Dodoma.
Siku hizi Dar es salaam ni jiji lenye wakazi zaidi ya milioni tatu.Ni bandari ya pili kwa ukubwa hapa Afrika Mashariki,nyumba ya Mombasa nchini Kenya.
Ni kituo kikubwa cha biashara ya kimataifa katika Ukanda wa Mashariki na Kati mwa Afrika.Ni eneo muhimu lenye kuvutia watu wengi kutoka Asia hadi Marekani,Australia,Ulaya n.k
Jiji hili limevutia tangu Wachina,Wahindi,Wazungu wa Ulaya na Marekani na wageni wengine kutoka kila mahali duniani.
Mwaka 2008,Wachina walilichagua jiji la Dar es salaam miongoni mwa miji mikuu ya dunia ambako mwenge wa Olimpiki ulifanya mbio zake.
Safari ya mwenge wa Olimpiki(The Olympic Journey of Harmony) ilikuwa kilomita 137,000 ikifuata njia yenye manufaa makubwa kwa Wachina.Uliwashwa mjini Athens,Ugiriki kama ilivyo ada, ukaenda Beijing,Uchina.
KUTOKA Beijing,mwenge huo wa Olimpiki ulikwenda Almaty,ukasafiri hadi London na Paris(Ulaya);kisha ulikwenda San Francisco, Marekani ambapo ni mahali panapokisiwa kuwa na jamii nyingi za Wachina huko Marekani.
Mwenge huo ulipita Buenos Aires,Argentina ukatua Dar es salaam kwa dege moja la Kichina rangi ya njano.
Gazeti la TIME la Mei 14,mwaka 2007 liliandika kwamba Wachina walichagua kukimbiza mwenge huo Dar mwaka 2008 kwa sababu Tanzania inaiuzia China dhahabu nyingi,na madini mengine na vito vya thamani tangu miaka ya 70.
Tanzania iliiunga mkono China kurejeshwa Umoja wa Mataifa(UN) mwaka 1971.Tangu zama za Mwenyekiti Mao Tse Tung,makampuni ya Kichina huongoza kupewa zabuni nyingi hususan katika sekta za Ujenzi na miradi ya maendeleo kwa ujumla.
Mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar wamepewa zabuni Wachina;ambao pia hufanya shughuli zingine za Kimachinga Dar,Arusha,Mwanza n.k
Mwenge wa Olimpiki kutoka Beijing ulipotua Dar ukaenda Muscut,Oman Wachina wanakopata mafuta kwa wingi,ulikwenda Islamabad,Kazakhstan,Australia,Pyongyang na Taipei.Ulifikishwa katika kilele cha Mlima mrefu duniani, Everest.
Hata kabla ya Rais Barack Obama kutua Dar es salaam Julai Mosi mwaka huu, tayari Rais wa China Ji XINPING alishatua Dar es salaam ili kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia Dar es salaam.
Uhusiano ulioanza tangu miaka ya 1960,kwa sababu DAR ES SALAA, ni Bandari ya Amani(The Haven of Peace),Madola makubwa ya Magharibi yanapigana vikumbo kuja kujipatia fursa tele za  kibiashara na uchumi.
Kwa sababu hiyo,inahisiwa Zanzibar ikijitenga kutoka katika Muungano(baadhi yao wanapinga Katiba inayopendekeza serikali ya Zanzibar isiyo Dola kamili);iko siku watadai Dar es salaam kwamba ni sehemu ya himaya yao tangu zama za Sultan Seyyid Majid!!
Na wazungu wa Ulaya na Marekani,Wachina na wageni wengine ambao sasa wanaifahamu Dar es salaam,baada ya ujio wa Bush,Obama,Ji Xinping na wengine watakaokuja baadaye Jiji hili la Dar es salaam ‘litavamiwa’!
Huenda wenyeji wakatupwa mbali na mji ili kupisha upanuzi mkubwa wa viwanda,mabarabara na miradi mikubwa ya kimataifa.
 
 
 
 
 
 
 
 



No comments:

Post a Comment