Monday, July 22, 2013

marekani na uasi Afrika

MISRI, hamkani si shwari tena!
Ni mapinduzi juu ya mapinduzi.Watu wajinga sana watasema sababu za vurugu Misri hutokana na siasa mbaya za Bara la Afrika.
Huu ni umajununi kuifananisha Misri na siasa za Uganda,Zimbabwe,Kenya,Sudan ama Somali.Tunapaswa kuitazama Misri.
Ina watu takriban milioni 90 wanaosongamana(watu 181 katika maili moja ya mraba);Mabedui na Waberiberi ambao ni asilimia 99 ya Wamisri wote;wanaozungumza Kiarabu,baadhi yao Kiingereza na Kifaransa.
Misri, ni taifa la mchanganyiko wa watu wengi,ambalo baada ya kupinduliwa Mohammed Mursi,sasa yupo Adly Mansour.
Wengi wao,(asilimia 94) ni Waislam wa Madhehebu ya Sunni,Wakristo wa Madhehebu ya Coptic ni asilimia sita tu.Sasa angalia kwamba Washia na Sunni hugombana, halafu Wakristo wa Misri hawajawahi kukubaliana,hususan chaguzi za kura zinapokuja.
Hawa Sunni na Washia wamehasimiana tangu Irak,Iran hadi Misri haiko salama. Hosni Mubarak aliyezaliwa Mei 4,mwaka 1928 akaingia Ikulu ya mjini Cairo Oktoba 14, mwaka 1981,tayari alishapinduliwa kwa maandamano ya medani ya Tahrir,na yuko nyuma ya nondo za gereza.Alikuwa mshirika wa madola makubwa ya Magharibi.
Hili ni taifa la kijeshi tangu zama za Farao mwaka  kwa takriban miaka 5000 sasa.Ina wanajeshi 448,500.Hata Nabii Musa(1500 BC) alifundishwa kuwa kiongozi wa jeshi la Misri,ambalo aghalabu ndilo lenye mamlaka makubwa katika nchi.
Bila jeshi Misri hakuna Misri,taifa kubwa kando ya Mto Nile unaotiririka kutoka Afrika Mashariki na kuweka uhai Misri.Nchi ya uchumi wa pamba,mpunga,maharage na matunda yanayostawishwa kwa umwagiliaji wa maji ya Mto Nile.
Misri ni nchi ya uchumi wa mafuta,nchi yenye akiba ya mafuta,mapipa takriban bilioni tatu.Haimo kwenye Umoja wa Nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi Duniani( Organization of Petroleum Exporting Countries),ambazo ni Algeria,Libya,Nigeria(hapa Afrika),Indonesia,Iran,Irak,Kuwait,Qatar,Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu(UAE) na nchi ya Nicolas Maduro, Venezuela.
Tazama hali ya kisiasa na kiusalama ya nchi hizi zenye mafuta mengi;linganisha uchumi wake na hali za watu,kasha angalia kama wanaelewana na nchi za Magharibi-nyingi ni shida tupu,vita vya wenyewe kwa wenyewe na uadui mkubwa na Marekani na Ulaya.
Nikusaidie msomaji.Makampuni makubwa ya mafuta duniani, Major Oil Companies,ni mali ya Wamarekani,Waingereza,Wafaransa,China na sasa Warusi na wabia wao wa biashara na washirika wa kijeshi.
Mafuta ni siasa, ‘Oil Politics’ na mafuta ni vita vya kiuchumi na kijeshi mahali popote yanapopatikana na kuonekana yanatosha kutumika katika nchi zenye viwanda vikubwa.
Hizi kampuni za mafuta za mataifa makubwa-SUPERMAJORS-hufuatiliwa kwa karibu mno na Ikulu kama Kremlin, White House, Number 10 Downing Street, n.k
Marekani hutumia mafuta mara 20 zaidi ya wastani wa matumizi ya dunia nzima.Mafuta ni sawa na damu katika mishipa ya mwili wa mwanadamu.Mafuta ni oxygen;ni uhai wa  n chi.Marekani wana mafuta yao.
Lakini,ni watumiaji wa mafuta kuliko Afrika nzima;wanaongoza duniani kutafuta na kuagiza mafuta na nishati nyingine hata kwenye sayari ya Mars ama mwezini!
Safari za anga lengo lake ni kusaka nishati huko.Marekani huagiza mafuta ambayo ni zaidi sana ya nusu ya kiasi kinachoagizwa na kutumiwa na dunia nzima kila siku.Ukiwanyima mafuta wanakutoa roho.Ni rafiki hata wa Shetani,mradi kakubali kuwapa mafuta,gesi,Uranium ama nishati nyingine muhimu kwa ajili ya mitambo yao.
Nataka kukwambia kwamba,mafuta yanapotindika hapa duniani,nchi inayogunduliwa ina akiba ya mafuta mengi inageuka eneo lenye hatari kubwa zaidi kijiolojia na kisiasa.
Hapa ndipo penye uchafuzi mkubwa wa mazingira,penye machafuko,vita vya wenyewe kwa wenyewe na kila aina ya majanga ya kijamii,kisiasa,kiuchumi na kiafya.Nchi zenye rasilimali nyingi wakati mwingine watu hugeukia mambo mengine na kusahau elimu ama dini,katika maeneo hayo haiwezekani kulinda amani kwa kirungu,bali silaha za kivita.
Ili kudhibiti amani katika nchi ya utajiri wa rasilimali nyingi ni kuwa na jeshi imara sana;na kwenye vita aslani hakuna haki za binadamu wala demokrasia.Ni unyama unyama,rushwa,ubabe mwenye nguvu ndiye hustawi-survival of the fittest.
Angalia Congo(DRC) akina Jenerali Kagame na washirika wao wamekuwa   wakijiingiza huko na kuiba rasilimali za madini(nitajadili hili baadaye),angalia Sudan ya Kusini,Chad,Libya,Irak ndiyo sasa Misri.
Tanzania bado hatujaanza kufaidika na gesi.lakini mpaka sasa huwezi kulinda amani Mtwara kwa virungu vya polisi;ni jeshi imara lenye silaha!
Na bado, gesi ikianza kuleta pesa,eneo hilo lazima kulindwa na jeshi imara sana;na huko hadithi za demokrasia zitakoma maana makampuni lazima kujilinda dhidi ya majasusi,magaidi ama tuseme piracy kama hao wa Somali.
Nigeria,Royal/Dutch Shell walitumia jeshi la Je. Sani Abacha kulinda eneo zima la Niger Delta,la sivyo eneo zima halitatawalika. Hii ndiyo laana ya rasilimali- the resources curse.
Hali hiyo haitokani na ‘siasa mbaya za Afrika’ kama wengine walivyokaririshwa bila kufikiri, ni rasilimali kuvutia majambazi,wahalifu,wachochezi,walafi wa kila namna duniani.Raia wan chi husika wanapaswa kuufahamu jambo hilo na kujiandaa kuishi maisha kando na vurugu.
Nataka watu waelewe kwamba kwenye rasilimali ama gesi,mafuta na madini yanakuja makampuni ya kigeni makubwa na tabia zao,mkizubaa wao haja yao ni ku- maximize profit, kwa  hiyo, hiyo win win situation inatoweka.
Matokeo yake kunakuwa na uchochezi toka nje,vita,wenye tamaa wanapokosa wanaona ujanja ni kutumia silaha ama nguvu za kisiasa,uasi na ushirika na majambazi wan je wenye silaha za kivita,ndiyo hali kama ya Sierra Leone inazuka.
Mnaletewa silaha ili muuane,mnawapa dhahabu,almasi ama mafuta na gesi.Turejee Misri ambako taifa ni la tangu mwaka 4000 BC.Tangu zama za Hawa na Adamu,tangu zama za Nuhu akawazaa watoto wake na Misri(Mizra) ni mjukuu wa Nuhu.
Tangu zama hizo,Misri ni chi ya jeshi kubwa ili kulinda maslahi,Mapiramidi,mafuta,Mto Nile n.k
Nchi inakaliwa na watu wengi wa kutokaaa tangu Syria,Uturuki,Israeli,Irak,Iran na hata Warumi,Wazungu n.k
Uingereza imeitawala Misri tangu 1882;ingawa ilikuwa chini ya Dola ya Kiislam ya Ottoman(Uturuki) hadi mwaka 1914.
Dola ya Ottoman iligeuza mataifa mengi ya Kaskazini mwa Afrika kuwa Waislam,zamani walikuwa Wakristo.Jamhuri ya Misri ilitangazwa Juni 18 mwaka 1953.Luteni Kanali Gamal Abdel Nasser alikuwa Waziri Mkuu mwaka 1954; akaja kuwa rais mwaka 1956 kwa kuchaguliwa.
Nasser,alikufa mwaka 1970,Anwar al Sadat aliyekuwa Makamu wa Rais akawa RAIS.Oktoba 6, mwaka 1981 Anwar Sadat alilimwa risasi na na KOMANDOO mmoja wakati akikagua gwaride la kijeshi mjini Cairo,watu wengine saba waliuawa,28 walijeruhiwa.
Watu wanne walikamatwa wakanyongwa baadaye-nchi ya mapinduzi,nchi ya jeshi tangu Farao.
Msomaji akumbuke kwamba, aliyemtabiri rais Obama,Martin Luther King Jr, aliuliwa huko Memphis, Aprili 4,mwaka 1968, akina Robert F Kennedy wameuliwa kwa risasi huko Marekani,siyo Misri.
NJAMA!Naam, tunazungumza njama za mapinduzi na mauaji duniani ili kulinda na kutafuta maslahi ya wenye nguvu duniani-unapaswa kujua yupo atawalaye dunia na marais kama Kikwete ni marais wan chi ndogo-ziko kubwa.
Nitasimulia siku nyingine Marekani inavyopanga kuondoa demokrasia na haki za watu kama uhuru wa dini(Ufunuo 13:11-18) halafu watu wataona nchi nyingine zina nafasi gani ya kukubali ama kukataa?
Obama kaja Tanzania ili kuwafanya wajinga wagutuke kwamba,kumbe Marekani hutawala kila mahali duniani? Kumbe rais wao hutawala Ulimwengu mzima kasoro mbingunni?
Hosni Mubarak, aliingia mamlakani MISRI baada ya Anwar al-Sadat,Mubarak naye alishapinduliwa yuko jela na alikuwa akipelekwa mahakamani akiwa kwenye machela.Mohammed Mursi naye kaingia kichwa-kichwa,sasa yuko kizuizini,sasa wapo akina   Adly.
Hii  ni nchi ya ‘tensions’ ambazo huwezi kuziondoa kwa siasa bali jeshi,ndiyo maana watu zaidi ya 50 wamefagiliwa kwa risasi za kijeshi na Marekani haijasema kitu bali kuongeza misaada kwa Misri.Sasa wapinzani wakahoji,kwa nini kununua silaha za kulinda raia halafu silaha hizo zikapindua demokrasia na kuua raia mbele ya macho ya Marekani?
Kwa nini badala ya kuondoa msaada kwa serikali,Obama anasema ataendelea ku ‘supply’ msaada wa kijeshi? Labda hii nayo ni demokrasia? Wenye midomo mipana mbona hamlisemi hilo?
Sadat alipigwa risasi Oktoba 6 mwaka huo 1981 kufuatia hiyo mivutano iliyoenea nchi nzima.Misri ni nchi ya maadui wengi,mikataba ya amani kama ya Camp David Marekani zama za Jimmy Carter,ndiyo inayofanya Misri isipigane na Israeli n.k
Vita vimekuwa vikipamba moto tangu Gaza, Sinai ,Milima ya Goran n.k
Hii ni nchi ya Mfereji wa Suez;nchi iliyowahi kuwa mshirika mkubwa wa Urusi(Ukomunisti) sasa utaona kwa nini itazamwe sana na Magharibi.Mfereji wa Suez wenye urefu wa maili 103 unaunganisha Bahari ya Mediterranean na Red Sea ndiyo bahari ya Sham waliyovuka Waisraeli bila boti,baada ya utumwa wa miaka 400.
Mfereji wa SUEZ unaiunganisha Ulaya na Bahari ya Hindi;na ulijengwa  na Wafaransa mwaka 1859-1869 tazama ramani uone umuhimu wake.Mwaka 1875 Waingereza wakajipenyeza na kuanza kuumiliki,ukawa unalindwa na vikosi vya Kiingereza.
Mameli ya Ulaya na Marekani hupita hapo yakiwa na shehena ya mabilioni ya Dola,kutoka Mashariki mwa dunia.Vikosi hivyo vya Uingereza viliondolewa katika mfereji huo Juni 13, mwaka 1956,na ilipofika Julai 26 mwaka huo serikali ya Misri ikautaifisha.
Kutaifisha Mfereji wa SUEZ uliojengwa ama kuchimbwa na wafaransa kwa miaka 10,kuna maana gani kwako? Fikiri. Tunazungumza umuhimu wa mfereji huu na mafuta ya Misri, tazama kuunganisha bahari za Sham,Mediterranean na Hindi kupitia hapo SUEZ.
Mpaka hapa umeona umuhimu wa Misri kisiasa,kijografia na kiuchumi.Unaona mataifa makubwa wakija Misri ili kuweka mambo sawa huko Mashariki ya Kati-hata Obama alikanyaga Cairo mara tu baada ya kuapishwa.
Sasa tunaona nguvu za Misri kisiasa zinashikiliwa na jeshi, wapo vijana wanaoota ndoto za  kufanikiwa siku moja na mapinduzi kutoka Nasser aliyekuwa mshirika wa akina Nyerere,Kwame Nkrumah(Nkrumah wa Ghana alioa kwa Nasser yupo mtoto  anaitwa Gamal Nkrumah)akaja Sadat na Osni Mubarak waliolelewa katika mbeleko za Magharibi.
Demokrasia ya kura imepinduliwa miguu juu kichwa chini huko Misri mbele ya Wamarekani, Muslim Brotherhood wanapaswa kutambua wamepinduliwa na nani? Labda walitaka Misri iwe kwa maslahi ya WAMISRI-KOSA KUBWA!
Dola hii ya Farao inakwenda mikononi mwa Magharibi kama ilivyo Irak na mataifa mengine ya Mashariki kwa kutumia minyukano ya medani ya TAHRIR na jeshi. Mapinduzi ya kijeshi na maandamano ya vijana wamachinga,ni mkono msaidizi wa Marekani na washirika wao, amini usiamini.
Akina Mohammed El-Baradei, waliokuwa juzi wakuu wa International Atomic Agency ni washirika wakubwa wa Magharibi,sasa watakabidhiwa nchi hii,Waislam wenye msimamo mkali walie tu!
Nchi nyingine kama Korea Kaskazini,Iran n.k zikae mkao wa kunyolewa kavu-kavu
Itaendelea toleo lijalo
0713 324 074
 
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment