Na Conges Mramba
Jumatano, Agosti 7 mwaka huu
tulikumbuka mashambulizi ya magaidi yaliyofanywa katika Balozi za Marekani,
Dar es salaam na Nairobi ; mwaka 1998
.Na juzi tu,tukakumbuka matukio ya Septemba 11,mwaka
2001.Leo tunaomboleza,West Gate Nairobi.Watu takriban sabini wamekufa,wengi
wamejeruhiwa vibaya!
Zaidi ya watu
240 walikufa mwaka 1998; hawa hawakuwa wa Kenya pekee bali pia wa
Tanzania . Hawakuwa wa kabila moja au wa dini fulani, waliokuwa
wakisali msikiti mmoja ama kanisa fulani.
Magaidi ni hatari kwa raia wote wa
dunia.
Tunawaombolezea
waathirika wa tukio hilo la Agosti 7 mwaka huo wa 1998, ambalo msingi mkubwa
ni uadui kati ya Marekani na Waarabu walioamua kuisaka Marekani popote
duniani, ili kulipa kisasi.
Naam,kuisaka
Marekani katika ardhi yetu, kusababisha hasara ya maisha na mali za watu
wetu, ni vitu tunavyovipinga leo na kesho hata kama mbingu zishuke; ama jua
litue mchana saa saba!
Hata mgogoro wa Somali ni matokeo
ya Vita Baridi kati ya Urusi na Marekani na washirika wao,sisi tunapokwenda
kupambana na al-shabaab ama al-Qaeda,maana yake twapambana na mabaki ya
minyukano ya Mashariki na Magharibi.
Si lengo la ukurasa huu kusema kwamba magaidi ni Waarabu peke yao, ama watu
wa imani fulani. Nitajadili malengo ya ugaidi na chimbuko lake. Nitajadili
imani inavyoupa msukumo na nguvu ugaidi duniani.
Kuna vikundi tele vya kigaidi duniani. Usishangae, hakuna gaidi anayejiita
gaidi.
Wote
wanajiita, wanaharakati(activists) wa ‘Haki’ za ubinadamu wao. Ugaidi unakula
maisha ya watu na mali vinapopotea au kuharibiwa.
Kila
mmoja ana tafsiri yake ya ugaidi. Sitajali kusikia Rais George W. Bush wa
Marekani naye ni gaidi kama Osama bin Laden.
Hata hivyo,
najua, magaidi kama wale waliolipua Balozi la Marekani Dar es salaam na
Nairobi, Agosti 7 miaka 10 iliyopita, wote ni wauaji; wanastahili adhabu
kali.
Walioua watu
Nairobi nao wanastahili adhabu kali.
A-Qaeda ni kundi la harakati za kigaidi, bila kujali wanaharakati wake
wanatokana na itikadi gani. Japan, kuna kundi moja linaitwa, “Ukweli Mkuu”
kwa Kijapani, Aum shinrikyo-hawa nao hata wakifanya mauaji, watasema wameua
ili kuueneza huo Ukweli(The supreme Truth). Mauaji hayaenezi haki yoyote.
Uhispania, kuna kundi linaitwa, ETA(Freedom for The Bosque
Homeland), nalo linadai uhuru. Lebanon , kuna kundi maarufu sana kama ,
Hezbollah(Chama cha Bwana Mungu), wakati Ireland Kaskazini kuna kundi
liitwalo, Irish Republican Army(IRA).
Nchini Israeli,
kitovu cha uadui wa mgogoro wa Mashariki ya Kati, kuna kundi liitwalo, Kach
and Kahane Chai, Uturuki kuna PKK(Kurdistan Peoples Party), Sri Lanka kuna,
Liberation Tigers of Tamil Eelam(LTTE); wakati nchini Iran kuna Mujahedin-E-Khalq.
Ugiriki kuna kundi
linaitwa, November 17 Revolution.
Juzi tulisikia kundi la FARC(Revolutionary
Armed Forces of Columbia) likifanya utekaji nyara; lakini ni ‘Jeshi la
Kimapinduzi’.Jeshi la kimapinduzi hupindua raia?
Hakuna anayemaizi
kuwa matendo yake ni kinyume cha sheria za nchi, za kimataifa, ama ubinadamu.
Wengine wanajisingizia, wametumwa na Mungu ili kuwaua binadamu wenzao,
waabudu sanamu ama wapagani.
Wapo, Shining Path kule
Peru . Columbia pia kuna National
Liberation Army(ELN),
na Ufilipino kuna New People’s Army.
Tumjadili
kidogo tu, gaidi la kale, Ilych Ramirez Sanchez, ambaye kwa utani anaitwa,
Carlos The Jackal-mzaliwa wa mjini Caracas , Venezuela . Venezuela , ni nchi
aliyoongoza Hugo Chavez, ambaye alimtukana rais Bush, wakati anahutubia
Mkutano wa Umoja wa Mataija, jijini New York , akapewa saa chache awe
ameondoka nchini humo.
Chavez alishakufa akabaki Nicolas
Maduro.
Carlos, gaidi
anayetumikia kifungo cha maisha Ufaransa, ikifika Oktoba 12 mwaka
huu, atakuwa anaadhimisha miaka 59 ya kuzaliwa kwake.
Sasa, huyu jamaa
katika mafaili ya uhalifu na Jinai duniani, kuna mambo yake mengi, ambayo
yametokana na chuki za siku nyingi kati ya nchi za Amerika ya
Kusini(zilifuata siasa za Carl- Marx) na Marekani. Carlos, ambaye baba yake alikuwa
mjamaa, alimpeleka Chuo Kikuu cha Patrice Lumbumba, mjini Moscow , kusoma.
Huko alikutana na
Wapalestina, akaiva katika siasa za mrengo tofauti na ubeberu wa Kimarekani.
Hata jina
‘Ilych’ aliitwa na babaye ili kuwaenzi ‘makomredi’ wa Urusi ya Ujamaa,
akina Lenin.
Sasa Carlos anaipinga
Marekani hata huko jela, alishasema alimuunga mkono Osama bin Laden, kwa
asilimia 100; na kwamba anawataka watu wasiache kujitoa mhanga ili kufa na
Wamarekani, popote walipo!
Nitajadili kauli hii
baadaye kidogo. Hata hivyo, huyu jamaa aliyetiwa mbaroni na mashushushu wa
Ufaransa akiwa mjini Khartoum, Sudan alishakaa Urusi tangu 1968, amekaa
Ujerumani mwaka 79, amekaa Syria 91-93, na Ufaransa. Vituko vyake unaweza
kuvipata katika sinema za akina James Bond.
Hapa, nitajadili ugaidi, si
Carlos.
Naam, ugaidi wa Agosti 7 mwaka 1998, ulileta hadithi
nyingi. Lakini, tuseme kwamba wale magaidi walishambulia Balozi za Marekani
Dar es salaam na Nairobi , karibia muda uleule mmoja, kwa sababu nchi hizi
hazikuwa zimejiandaa.
Wengine wanasema hata
Kampala ingeshambuliwa. Kilichoiponya ati ujio wa Rais Bill Clinton wakati
ule mjini Kampala , ulivifanya vikosi vya usalama vya Uganda kuwa ‘more
alert’ kuliko Dar na Nairobi ! Hayo tuyaache.
Kampala
ilishambuliwa na al-Shabaab mwaka 2010 wakati wa Kombe la Dunia Afrika
Kusini.
Shambulizi lingine la magaidi Afrika Mashariki lilifika Novemba 28 mwaka
2002.
Magaidi waliua watu 16 mjini Mombasa, katika
hoteli ya Paradise iliyoko Kikambala. Ni kilomita 25 kutoka mjini Mombasa.
Hii hoteli ni ya Waisraeli; sasa unaweza kukisia hata wewe, kwamba ilishambuliwa
na adui zao Wapalestina. Wapalestina walikuja Afrika Mashariki kuwawinda adui
zao Waisraeli, katika ardhi ya Kenya. Hawakuua Waisraeli tu, waliua na
Wakenya, na raia wa mataifa mengine.
Sasa tuseme, vita vya kudai uhuru vinavyoendeshwa na Wapalestina dhidi ya
Mayahudi, vina leseni ya kuua na kuumiza binadamu wengine wasio na hatia?
Halafu, hao magaidi wa Kipalestina walifanya jaribio la kuilipua ndege ya
Arkia Airlines ya Israeli, iliyokuwa ikiruka kutoka uwanja wa ndege wa Moi,
mjini Mombasa. Bahati tu, lile kombora, bila shaka la Kirusi, liliikosa- kosa
ndege ile iliyokuwa na abiria 271 hivi.
Fikiria, kama kombora lile lingeipata ndege ile,wangekufa Waisraeli pekee?
Hata raia wa mataifa mengine, wasiojua uadui
waa Israeli na Wapalestina wangeungua katika miali ya moto wa mlipuko. Sasa
ugaidi unasura ya ukombozi au uokozi na uhuru wa wapi?
Narejea mada yangu ya madhara ya ugaidi Afrika Mashariki. Matukio yote ya
ugaidi yalisababisha watu mamia kufa, inakisiwa kulitokea hasara ya dola
mabilioni. Ili kuponya majeraha ya ugaidi, zimetumika dola matrilioni, ambazo
pengine zingetumiwa kuleta maendeleo-ugaidi ni adui wa maendeleo ya watu.
Nimesema magaidi wapo Wazungu kama IRA, na wa mataifa mengine kama akina
Carlos The Jackal; lakini ni magaidi. Magaidi hawana rangi, dini ama taifa
moja.
Ugaidi ni mauaji ya kinyama yanayoendana na matakwa ya ulipaji kisasi.
Pengine, magaidi kama Black Banners wa Iraki, wakati ule wa vita, waliwateka
jamaa watatu wa Kenya, ili kutafuta fedha kutoka kwa makampuni waliyofanyia
kazi.
Sasa nijadili jambo ambalo watu hupenda kunitolea matusi. Watoa lugha
chafu, hawana weledi juu ya lolote. Silaha yao ni matusi na vitisho.
Wanadhani, ukweli ni ule unaolingana na wanavyopenda, ama wanyofikiria wao.
Hata hivyo, ugaidi ni unyama, hata Mungu mahali popote hajawahi kusema watu
walipizane visasi. Sera za ‘Jino kwa Jino’ ama ‘TIT FOR TAT’ ni za Ibilisi.
Mungu anawataka watu kutong’oana meno, ili kulipa baya kwa baya?
ungu
anawataka watu wawe vibogoyo au chongo?
Juzi,
Papa Benedict XVI ameungama kwamba Kanisa Katoliki nalo lilishafanya ugaidi.
Ugaidi hauna rangi, kanisa, msikiti wala watu wa kabila moja.
Nilipata kutukanwa na hawa jamaa kwa kupinga kauli ya Carlos, kuwataka watu
kufuga midevu mingi kama shamba la miwa la Kilombero, halafu eti
wasiache kujilipua ili kuwakomesha Wamarekani, popote watakapowaona!
Sasa kama
Carlos kawaambia, kwa nini wasiende kujilipua New York au Washington ? Kwa
nini Mombasa , Nairobi au Dar? Huku Wamarekani hawapo!
Mkijilipua huku mnatuumiza sisi, wao hawapo.
Kama wapo ni mmoja tu au wawili-wafuateni Wamarekani kwenye uwanja wa
mapambano! Wenye uwezo walikwenda kulipua New York na Washington, Septemba 11
mwaka 2001; hadi leo historia inaelekea kuwasahau.
Sipendi kuamini kuwa,
mtu mwenye uwezo wa kufikiri anaweza kuwa’Shahidi’ mwaminifu wa imani
yake(uwe Ukristo,upagani ama Uislamu)kwa kujilipua, ili afe yeye na kumuua
adui!
Huku ni kushika dini
kupita kiasi(fanaticism), kunakogeuza dini kuwa vifo na mauti, kwamba ni ushahidi(martyr).
Hii si Jihad halali kuua hata watoto wasio na hatia, kwa sababu tu walikaa
meza moja na adui.Kwa nini kuua adui mmoja kati ya ndugu mamia?
Najua vita kati
ya Waisraeli na Waarabu wa Mashariki ya Kati, inaitwa ‘Vita kati ya wema na
uovu’. Sasa kama
pande mbili zinaua hata wasiohusika, mwema nani na mwovu ana alama gani?
George Bush na Tony Blair, wakati wanaishambulia Irak, walisema ni vita dhidi
ya watu wasiostaarabika. Wakati magaidi waliposhambulia London, wakasema ni
vita dhidi ya ustaarabu.Sasa tujiulize pia, kuua watu wasiohusika hata huko
Irak ni ustaarabu? Ni kwa sababu hii, safu hii inasisitiza kuwa mauaji ni
jinai, na kila muuaji ni Ibilisi mwenye mikia saba.
Hakuna kitabu kitakatifu kinachotuma watu kuwaua wenzao wasioamini ama
waabudu sanamu. Ndiyo maana hapa Tanzania si lazima kwa mujibu wa Katiba mtu
kuwa dini fulani.Hata wapagani na waabudu sanamu ni watu; wasiuawe kwa
kutokuwa na dini kwao.
Nasema hivi kwa sababu
rafiki yangu aliniambia, Allah kasema kuua hawa walao nguruwe ni kupata
thawabu hata akhera!(to be elevated to a higher plane of existence, where
life is an eternal bliss).
Ni kwa sababu hii,
msomi na mhadhiri, Imam mashuhuri anasema kila siku, kwamba Kuran
inakataza kabisa kuua au kujitoa mhanga-na kwamba wanaofanya hivyo, hawafanyi
kwa jina la Uislam; bali wanasaliti mafundisho ya Mtume Muhammad.
“Hatutaruhusu
imani yetu adhim kutekwa nyara na wahalifu”, alisema.
Maneno kama haya kayasema Kiongozi
wa Upinzani Bungeni juzi, Hamad Rashid Mohamed, alipokuwa akitoa hutuba fupi
wakati wa kuaga mwili wa Chacha Zakayo Wangwe, “Rasta” wa Tarime. Buriani
Chacha Wangwe.
Hamad Rashid,
alisema alikwaruzana na Marehemu Chacha Wangwe, lakini wakasameheana, kwa
sababu, Kuran inasema, ‘kusamehe ni lazima’ ili upate thawabu.
Biblia inasema kusamehe ‘saba x
sabini’ maana yake siku zote za maisha. Saba ni alama ya ukamilifu wa
utimilifu; hivyo tusichoke kusamehe.
Sasa
hata hapa mtanitukana na kutishia kunipiga kwa kuhimiza amani? Mungu gani
kawaambia kumpiga mwenye mawazo tofauti nanyi? Dini yenu ni ya amani,
kwa nini Jino kwa Jino?
Nilishasema katika makala mbili zilizotangulia, kwamba kuna upendeleo na
‘double standards’. Alichofanya Bush au Blair, akikifanya Mugabe au
Mpalestina, ataitwa gaidi, wao “Patriots”.
Hili
ni tatizo ambalo haliondolewi kwa watu kujilipua, lawama hizi haziondoki kwa
kujifunga mabomu. Hatupambani na ‘metropolitan power’ kwa kulipua Dar,
Mombasa na Nairobi.Tunatakiwa kuilipua Washington kisayansi, maana yake
kumlipua Bush pekee bila raia wasio na hatia.
Ukijifunga bomu utamlipua Blair au Bush? La hasha.
Utawalipua ndugu zako wa Dar, Mombasa ama Nairobi. Tutafute njia mwafaka ya
kuondoa ‘double standards’ duniani. Tusijiite,
“Liberators” ama ‘in the service of’ Allah’ kumbe wauaji wa ndugu zetu
wenyewe.
Tusidhani tunakomboa,
kumbe tunajiua! Kujiua ni dhambi kubwa na kosa katika sheria za binadamu na
Allah. Mashahidi
waaminifu wa imani, hawatoki msikiti fulani tu, hata sinagogi au kanisa.
Je,
hamjaona watu wakienda uwanja wa ndege na biblia pasipo nauli,hati za
kusafiria wala visa wakadhani Mungu atawapeleka Ulaya kuhubiri? Huku nako
kujifunga mabomu! Magaidi hawana dini moja.
Nimalize, kwa kusema
Kuzimu kumepanua kinywa chake. Kuna visasi vingi tangu matukio ya Septemba 11 mwaka
2001. Lakini, tuangalie faida yake nini? Nani kasema ukifa kwa kujilipua kwa
bomu na kuangamiza Mzungu mmoja na Waafrika wenzako 200 ni thawabu? Imani
zisitugawe;sisi ni wamoja hapa Tanzania ama Afrika.
Tutafakari msugoano uliopo kati ya Magharibi na Mashariki. Leo, siasa za
akina Hugo Chavez, zinashindwa. Akina Carlos The Jackal wanaonekana majambazi
tu, hata kama walifanya kazi bega kwa bega na makomredi kama Fidel Castro,
katika kuzuia ubeberu.
Hatuwezi kuupinga ubeberu kwa kuangamizana Paradise Mombasa, au katika
usafiri wa ndege kama ile ya Arkia Airline, ama wa treli London.
Hata
katika balozi za Wazungu, kama Dar, Kampala na Nairobi, ukijilipua hukosi
kuua Mzungu mmoja na Waafrika wenzako 300. Kuna thawabu gani hapo?
Tufanyeje sasa? Tufikiri kwa makini; tuepuke kutukana watu, kupandisha mizuka
ili kuhuisha roho ya kisasi. Tutaushinda uadui kwa akili na imani, si
imani bila busara. Busara hutoka kwa Mungu.Kwa mungu kuna haki na thawabu.
Mungu ni wa utaratibu, si wa machafuko.Palipo na machafuko, hapana Mungu. Na
sheria ni msumeno.
. Ukweli si ule unaomfrahisha mtu; ukweli ni mchungu lakini mtamu. Ukweli ni
ubinadamu. Tuimarishe ubinadamu-humanity.
Ndivyo
tunavyoikumbuka Septemba 11 mwaka 2001,tunawapa pole Nairobi kwa kipigo cha
al-SHABAAB,
www.congesmrambatoday.blogspot.com
0754 324 074,0786 324 074 |
Wednesday, September 25, 2013
AL SHABAAB NAIROBI PIGO KWETU TANZANIA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment