Thursday, August 18, 2011

viongozi gani hawa wa AU?



UKICHUNGUZA kwa makini siasa za Afrika,unaweza kucheka sana , halafu mbavu zikauma,ukapatwa kwikwi na hatimaye kulazwa chumba cha wagonjwa mahututi(ICU)!
Gazeti la East African la Desemba 27 mwaka 2010 hadi Januari Pili mwaka huu 2011  ukurasa wa mbele, lilibeba kichwa cha habari kisemacho,
“THE LEAGUE OF AFRICAN EXTRAORDINARY DICTATORS”.
  Chini ya maneno hayo kulikuwa na picha za viongozi watano wa Bara la Afrika:Rais wa Sudan ya Kaskazini sasa, Omar Hassan al-Bashir,Rais wa zamani wa Cote d’ Ivoire, Laurent Koudou Gbagbo, Rais wa Zimbabwe, “R.G” Mugabe,Rais wa Guinea ya Ikweta,Teodoro Obiang Nguema Mbasongo,na Waziriri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi.
   Gaddafi, hakuwepo ‘Front Page’.ipokuwa, kulikuwa na vituko vyao ndani ya gazeti hilo vilivyopewa kichwa cha habari, “African President’s Index”
   Akina Mfalme Mswati III wenye jumla ya vimwana warembo 13 kama wake zao wa ndoa, Jacob Zuma Mushorozi, mwenye wake watatu, wote walikuwemo kwenye orodha.
   Kuliwekwa  nafasi na alama(rank) zao walizopewa kulingana na kazi walizofanya kila mmoja.
 RaisJakaya Kikwete alishika nambari 10 katika orodha, akiwa na asilimia 60.39 ambazo zilimpa B-
 Alitanguliwa na Sir Anerood Jugnaut wa Mauritius,Pedro Pires wa Cape Verde ,Ian Khama, John Atta-Mills,Hifikepunye Lucas Pohamba ,Jacob Zuma Mushorozi,James Michel wa Sychelles,Amadou Toure na Ernest Bali Koroma wa Sierra Leone.
  Mwenyekiti wa sasa wa AU, Teodoro Obiang Nguema Mbasongo wa Guinea ya Ikweta, alishika nambari 50 kati ya nchi 52 za Au zilizoorodheshwa. Kuna nchi 53 huru za AU, na Sudan ya Kusini baada ya uhuru juzi, sasa inakuwa nchi ya 54.
  Rais huyu, ambaye ndiye kiongozi wa sasa wa AU alipata asilimia 20.81 ambazo ni mbaya zaidi, na aliwatangulia Omar al Bashir na Isaias Afweki wa Eritrea aliyepata asilimia 12.14.
  Ndugu msomaji, utamaizi kuwa, utawala mbovu wa huyu Afweki wa Eritrea ,umewafanya wachezaji wa timu ya Red Sea, kuingia mitini mjini Dar es salaam(mji wa amani) wakichelea kurejea makwao baada ya mashindano ya Kombe la Kagame kumalizika na Dar es salaam Young Africans,kutwa ubingwa. Hongera sana Yanga!! Hata Fikra Pevu ni Yanga damu!!!
 Hawa wachezaji, sasa wanaomba hifadhi ya ukimbizi.
 Teodoro Obiang Nguema, ndiye Mwenyekiti wa sasa wa AU, ambaye nchi yake ya Guinea ya Ikweta ilianza zamu yake ya uenyekiti AU Januari 31 mwaka huu wa 2011 na labda atamaliza muda wake Januari mwakani.
  Ni Mwenyekiti wa tisa tangu Umoja huu AU Mwaka 2002; wengine waliomtangulia ni kama ifuatavyo:
  Thabo Mvuyelwa Mbeki(Julai 9mwaka 2002-Julai 10, 2003),Joaquim Chissano(Julai 10, 2003-6Julai 2004),Olusegun Mathew Obasanjo(6 Julai 2004- 24 Januari 2006),Denis Sassou Nguesso( 24 Januari 2006-24 Januari 2007) na John Agyekum Kufour(30 Januari 2007-2FEB 2008).
   Wengine, ni Jakaya Kikwete(31 Januari, 2008-2Feb, 2009),Muammar al-Gaddafi(2Feb 2009- 31 Januari 2010), Bingu wa Mutharika(31 Januari 2010-31 Januari 2011) na Teodoro Obiang Nguema Mbasongo alianza kuongoza 31 Januari 2011 hadi Jauari mwakani.
 Rais Teodoro Obiang Nguema, wa Guinea ya Ikweta alishawahi kujitangaza kwamba yeye ni ‘mungu’ wan chi hiyo!
  Radio ya Taifa hilo dogo Magharibi mwa Afrika alitangaza mwaka 2003 kwamba, ni kama Mungu wa mbinguni,kwa sababu yu na nguvu zote(Omnipotent) juu ya wanadamu na vitu vyote huko Guinea ya Ikweta! Sijui hata huku Tanzania ?
   Katika kipindi cha redio kijulikanacho kama ‘Bidzenduan’ maana yake, “Kuzika Moto”ilitangazwa kwamba rais huyo eti alikuwa akifungamana karibu na Mungu mwenyezi.
  “Yu kama Mungu wa Mbinguni,ambaye ana nguvu zote juu ya wanadamu na vitu vyote!” redio hiyo ya taifa ilisema, na watu wanaoamini maneno hayo walisema wakakaririwa na Shirika la Utangazaji l a Uingereza(BBC).
 Kwa muda mrefu,nchi hiyo haikuwa na vyombo vya habari huru, kama utitiri wa magazeti ulioko hapa kwetu.Watu walilazimika kusikiliza redio hiyo ya taifa tu iliyomtangaza rais huyo kuwa ni mungu,ili wapate habari.
  Rais Nguema(69) alishinda uchaguzi kwa takriban asilimia 100 mwaka 2002 ambao ulimweka madarakani hadi 2009 kulingana na katiba. Ingekuwa huku kwetu wangeandamana dhidi ya mungu-mtu huyu, ambaye amejipatia madaraka tena na tena!
  Anatawala zaidi ya vipindi vitatu. Alizaliwa Juni 5 mwaka 1942, akaingia madarakani Oktoba 1979 baada ya kumpindua mjomba wake kwa mapinduzi ya kijeshi, Agosti mwaka 1979.
  Marehemu Marcius,ama Masie Biyogo eti alikuwa ‘Rais wa Maisha’ wan chi hiyo tangu mwaka 1972! Idi Amin naye alikuwa Rais wa Maisha. Naam, Jean-Bedel Bokassa, Mobutu, orodha ni ndefu.
 Kufuatia redio ya taifa kumtangaza rais huyu kuwa ni mungu wa taifa(labda na dunia nzima!) ikatangazwa kwamba alikuwa na mamlaka ya kuua mtu yeyote pasipokuwajibishwa wala kukabiliwa na hukumu hata ya ahera!
  Kwa sababu,alionana na Yehovah,na kuonana na Yehovah kwake eti ni kitu cha kudumu, ndivyo ilivyotangazwa na msaidizi wa rais kupitia hiyo redio ya taifa.
  Jamhuri ya Kidemokrasi(Demokrasi au Uimla) ya Guienea ya Ikweta ina eneola maili za mraba 10,800 na mwaka 2003 kulikuwa na watu 500,000, sawa na watu walioishi mjini Mwanza wakati huo.
Wanazungumza lugha ya Fang. Kila juma msaidizi wa rais anatangaza sera anuwai za ‘mungu’ Nguema,yakiwemo madai kuwa anakaribiana sana na Mungu Yehovah,ili kuwatiisha raia wan chi hiyo.
  Ni nchi ya tatu kwa kuzalisha sana mafuta hapa Afrika.Ilinusurika kupinduliwa na mamluki toka Afrika ya Kusini, waliotumwa na motto wa Waziri Mkuu wa zamani Uingereza, Margaret Thatcher, anayeitwa Sir Mark Thatcher.Walitiwa mbaroni Zimbabwe .
 Rais huyu alishapiga marufuku vyama vya siasa,katika nchi iliyopata uhuru Oktoba 12 mwaka 1968.
 Utawala wa Dikteta Masie Nguema Biyogo(mjomba wake) ni moja ya tawala za kikatili sana hapa Afrika,zilizofanya nchi kufilisika.
 Nchi hii,mwaka 2000 ilikuwa na akiba ya mafuta, mapipa yasiyosafishwa milioni 12 hivi. Ilikuwa na ng’ombe 4,800,kuku 245,000,mbuzi 81,000,nguruwe 5,300 kondoo 36,000 na huuza mbao nje ya nchi.
 Wananchi wake ni wavuvi na wakulima wa mpunga,viazi,kahawa,kakao na kahawa.Asilimia 68 ya pato hutokana na mauzo ya mafuta nje,lakini pato la jumla kwa mwaka ni Dola 2,000.
 Nataka kusema kwamba,katika nchi ya ‘mungu’huyu watu ni duni sana,kati ya watu 1,000 wenye televisheni ni  100 tu, wenye redio ni 500 tu wastani wa kuishi ni miaka 52 hadi 57 tu.
Ati, nchi inayoongozwa na ‘mungu’ watu wake hufa wangali vijana namna hii,na wanaishi kwa kiwango cha umasikini wa pato la chini ya dola moja kwa siku.
 Mbasongo, anafanana sana na viongozi wengi hapa Afrika wanaojifananisha na Mungu, hadi wanahujumu demokrasia  na haki za raia.
 Hata hivyo, hii siyo sababu Afrika kuanza kutawaliwa kwa mabavu na Marekani, Ufaransa na majeshi ya NATO. Afrika itaamua mambo yake yenyewe, na aslani siyo wakoloni.
 Msomaji wangu mwenye simu nambari 0712 964 193 alinitaka niongelee udhaifu wa utawala wa viongozi wetu,nilishaandika sana , na sasa nimempa kionjo, asiache kusoma gazeti hili kamambe kwa uchambuzi wa masuala ya dunia nzima.
  Tunaitazama dunia nzima,na kamwe hatuwashambulii watu,hasa wanasiasa wa hapa peke yao .
 Tunatazama mambo mengi na wanaosoma Tazama Tanzania kila Jumanne ni mashuhuda wetu.
 Ni kwa sababu hii tunasema, huyu ndiye Mwenyekiti wa sasa wa AU ambayo Wazungu wanasema ni klabu cha Madikteta!
    0786 324 074
  

 

No comments:

Post a Comment